Dodoma. Kuna kila dalili kwamba mabadiliko
mengi yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba yakigusa miundo ya
taasisi nyeti za umma yatawekwa kando na huenda Bunge Maalumu likatoa
Katiba isiyokuwa na mabadiliko makubwa kama ilivyotarajiwa.
Gazeti hili limebaini kuwa kamati nyingi za Bunge
hilo zimebadili mapendekezo mengi hasa yanayowagusa viongozi na taasisi
nyeti kama Bunge, tofauti na ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji
Joseph Warioba.
Miongoni mwa mambo ambayo yamependekezwa
kurejeshwa kama yalivyokuwa ni muundo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambalo kwa mujibu taarifa kutoka kwenye kamati mbalimbali, ni
kuendelea na muundo wa sasa unaowajumuisha wabunge kutoka Zanzibar.
Katika maelezo yake, Jaji Warioba alisema moja ya
kero za muungano katika eneo la Bunge ni malalamiko kwamba wabunge
kutoka Zanzibar wamekuwa wakishiriki katika Bunge la Muungano na
kushiriki kujadili mambo yanayohusu Tanzania Bara.
Kupitia mfumo wa Serikali tatu, Rasimu ilikuwa na
mapendekezo ya kuwapo kwa Bunge la Muungano lenye wabunge 75, lakini
mapendekezo hayo pia yamefutwa katika kamati karibu zote na kurejesha
mfumo wa sasa pamoja na uwapo wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid
Mohamed alisema jana kuwa suala la muundo wa Bunge lilisababisha mvutano
mkubwa katika kamati yake na baadhi ya wajumbe walikuwa wakihoji
uwakilishi mkubwa wa wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Muungano hata
kwa mambo ya Tanzania Bara.
Hata hivyo, alitetea hali hiyo akisema uwapo wa
wabunge kutoka Zanzibar ni moja ya masharti yaliyowekwa na Katiba. “Hata
Katiba ya sasa imeweka sharti la idadi ya wabunge wa Zanzibar, hilo
nalo ni sharti la Katiba huwezi kuliondoa, kama unataka kuliondoa
unapotunga Katiba maana yake ni lazima uvunje muungano.”
Alisema mwaka 1964 mambo yote ya Tanganyika
yaliingizwa kwenye Serikali ya Muungano... “Kwa hiyo ni lazima ukafumue
Muungano, useme haya ni ya Tanganyika na haya ni ya Muungano,” alisema.
Hamad alisema katika hadidu ya rejea, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilikatazwa kugusa mambo ya Muungano. “Hivi wabunge
70 wanaokuja kutoka Zanzibar wakazungumzia mambo ya Bara, hivi kuna
dhambi gani, sioni kosa kabisa.” Mwenyekiti huyo alisema kamati yake
imebaini kwamba Rasimu ya Warioba ina upungufu mwingi kwani hata baadhi
ya kero zilizotajwa zilishafanyiwa kazi na Serikali.
Hoja ya ushiriki wa Wazanzibari katika masuala ya
Tanzania Bara iliripotiwa kuibuka katika Kamati Namba Moja ambako mmoja
wa wajumbe, Ally Keissy alinikuliwa akihoji sababu za wajumbe wa
Zanzibar kushiriki mambo ambayo wao siyo sehemu yake.
Mbali na muundo wa Bunge, kamati nyingi pia zimefuta mapendekezo
kadhaa yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ni pamoja na wabunge
kutokuwa mawaziri, ukomo wa ubunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano
mitano, wabunge kuwajibishwa na wananchi, kupunguzwa kwa madaraka na
kinga ya rais.
Katika Kamati Namba Tano, Hamad alisema suala la
wananchi kumuondoa mbunge lilikataliwa. “Hivi ni kigezo gani ambacho
kinaonyesha mbunge hakuweza kuwaletea wananchi maendeleo. Nini utatumia
cha kupima ufanisi wa huyu mbunge?”
Alisema kuliweka jambo hilo katika Katiba ni
kuleta matatizo na kwamba wameliacha suala hilo mikononi mwa vyama vya
siasa kuangalia kama mbunge anafanya kazi ya ilani zao au la.
Mgawanyiko mpya
Habari zaidi zinasema kuwekwa kando kwa
mapendekezo mengi yaliyolenga kurekebisha mifumo ya uongozi na utawala,
kumesababisha mgawanyiko hasa miongoni mwa wajumbe watetezi wa muungano
wa serikali mbili, ambao awali, waliahidiwa kwamba muundo huo usingekuwa
na sura yake ya sasa, bali ungeboreshwa.
Mmoja wa wabunge wa CCM alisema jana kwamba:
“Tutawapa wapinzani sifa maana umma utaamini kwamba bila wao hakuna
kinachoweza kubadilika, sasa kama tunarejesha kila kitu ambacho kiko
kwenye Katiba tuliyonayo kuna maana gani ya kuwa na mchakato?”
Mmoja wa wenyeviti wa kamati za Bunge Maalumu naye
alisema kinachoendelea ndani ya kamati nyingi ni kufuta mapendekezo ya
Rasimu na kuleta mapendekezo mapya ambayo ni sawa na yaliyomo kwenye
Katiba ya sasa.
“Ndani ya chama (CCM) tuliamua kupinga mapendekezo
ya serikali tatu baada ya kuahidiwa kwamba tutakuja na muundo wa
serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hata hizo hatuzioni. Kwa hiyo
wananchi wataamini kwamba kilichosemwa na Ukawa (Umoja wa Katiba ya
Wananchi), ni cha kweli,” alisema mwenyekiti huyo.
Utata wa akidi
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis
Michael aliamua kuahirisha kikao jana saa tano asubuhi kutokana na kile
alichokiita kuwa ni kuwapa muda wajumbe waende kusoma zaidi sura ya tisa
ambayo inahusu muundo wa Bunge.
Hata hivyo, habari ambazo zilikuwa zimelifikia
gazeti hili mapema zinasema kuahirishwa kwa kikao hicho kulitokana na
akidi kutotimia, taarifa ambazo Dk Michael alizikanusha kwa kuonyesha
idadi ya wajumbe ambao walikuwa wamesaini karatasi ya mahudhurio.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo alikiri kwamba hadi
ilipotimu saa 4:00 asubuhi jana kamati yake ilikuwa ikikabiliwa na
upungufu wa wajumbe wanne, hivyo waliwapigia simu na kubaini kwamba
walikuwa katika shughuli nyingine ikiwamo kumpokea Rais Jakaya Kikwete.
“Baadhi ya wajumbe ni mawaziri kwa hiyo baada ya
kukamilisha majukumu yao walifika na saa tano hivi akidi ilikuwa
imetimia,” alisema Dk Michael.