Thursday 16 July 2015

Mtoto wa bwana shamba awa kinara kitaifa

Dar es Salaam. Wakati Ramadhani Gembe (pichani) anafanya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita miezi miwili iliyopita, hakuwahi kufikiri angeshika namba moja kwa ufaulu kitaifa licha ya jitihada zake za kujituma.
Lakini siku zote Mungu hamtupi mja wake. Kama jina lake linavyosadifu mwezi mtukufu unaomalizika siku mbili zijazo, Ramadhani ambaye amehitimu Shule ya Wavulana ya Feza jijini Dar es Salaam, ameibuka mwanafunzi bora nchini kati ya waliofanya mtihani huo wa kujiandaa kwa masomo ya elimu ya juu.
“Nilitegemea ningefaulu lakini siyo kwa kiwango hicho… hii ni ‘surprise’ (shtukizo),” alisema Gembe alipohojiwa na Mwananchi baada ya matokeo ya kidato cha sita kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa.
“Nawashukuru wazazi, walimu, ndugu na wanafunzi wenzangu kwa kunipa ushirikiano. Nilikuwa nafanya sana ibada hivyo haya matokeo ni juhudi binafsi na majibu ya Mungu,” alisema Ramadhani aliyesoma mchepuo wa fizikia, kemia na baiolojia (PCB).
Historia ya Ramadhani darasani si haba kwani mwaka 2008 alikuwa ni mwanafunzi pekee aliyejiunga na shule ya vipaji maalumu ya Ilboru, Arusha akitokea shule ya Msingi Mombo na alipata daraja la kwanza akiwa na pointi 11 katika matokeo ya kidato cha nne.
“Siku zote kilichonifanya niongeze juhudi katika masomo yangu ni malengo ya baadaye... mimi nataka kuwa daktari wa binadamu hivyo sikutaka kulegalega kusoma. Pia, wazazi wangu pamoja na hali ngumu walijitahidi kunisaidia kimawazo, kirasilimali na kimaadili…naomba na wazazi wengine wawafanyie hivyo watoto wao,” alisema.
Baba azungumza
Nurdin Gembe, ambaye ni mzazi wa Ramadhani, alisema familia imepokea kwa furaha matokeo hayo na kwamba alikuwa akiyategemea kuwa mazuri kutokana historia ya kijana wake katika madarasa ya nyuma.
“Huyu mtoto namlea kawaida japo zamani alikuwa mtundu sana… ilibidi nimpe mafundisho mengi sana ya kidini bila kupoteza ratiba ya kusoma shuleni. Nashukuru kuwa alizingatia na amefika hapo alipofika,” alieleza Gembe ambaye ni bwana shamba kitaaluma.
Mwanafunzi wa tisa
Kwa upande wake Yonazi Senkondo, aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa, alisema matokeo hayo ni majibu ya maombi kwa Mungu na juhudi zake kusoma na ushirika na wanafunzi wenzie.
“Siku zote nilikuwa naombea niingie 10 bora, najua leo Mungu amejibu maombi yangu. Nilikuwa nafanya mijadala na wanafunzi wenzangu hasa huyo aliyeshika namba moja. Sishangai yeye kuwa katika ngazi hiyo.
“Siku zote naamini maombi na nidhamu ndiyo msingi wa yote kwa sababu unaweza kukesha unasoma, lakini matokeo yakaja tofauti,” alisema Yonazi aliyekuwa akisoma fizikia, kemia na bailojia (PCB) katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Feza, jijini Dar es Salaam.
Mama yake, Jeanette Senkondo alisema matokeo ya kuingia 10 bora ni kama shtukizo kwa kuwa alikuwa anajua mwanaye ana uwezo wa kufaulu ila siyo kwa kiwango hicho na kwamba ni mafanikio ya sala, juhudi na mipango, ushirikiano, nidhamu na malezi bora ya mwanafunzi.
“Tangu chekechea alikuwa na juhudi za masomo na siku zote akipanga kitu lazima akitimizie… pia huwa anasali na kufunga hata mimi wakati wa majuma mawili ya mtihani nilifunga kumuombea. Bila shaka Mungu amejibu maombi,” alisema Senkondo ambaye ni mhadhili wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki.
Mkuu wa Feza alonga
Makamu Mkuu wa Shule ya Wavulana ya Feza, Ali Nungo alisema kitendo cha kuingiza wanafunzi 10 bora ni changamoto wanayotakiwa kuliendeleza siku zote kwani hawajawahi kufanya kwa kiasi hicho.
“Vijana hawajatuangusha, tulitegema watafanya vizuri ila siyo kiwango hicho. Sisi kama walimu na uongozi wa shule tumefanya tuwezalo kuwawezesha kwa kuwafundisha na kuwapa ushirikiano lakini lazima wazazi watambue kumleta mtoto tu Feza si kwamba anakuwa bora, lazima kuwe na ushirikiano mzuri baina ya pande zote,” alisema.

No comments: