Wabunge waliofukuzwa na Naibu Spika, Job Ndugai juzi ni pamoja na Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa
Ilemela, Highness Kiwia, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema.
Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe amesema kuwa watakata rufaa katika Kamati ya Kanuni ya Bunge dhidi
ya mwongozo wa Spika uliobariki adhabu ya kuwatimua kwa siku tano
wabunge sita wa Chadema kwa kudharau mamlaka ya Spika.
Akitoa mwongozo wake jana, Spika Anne Makinda alibariki wabunge hao kutimuliwa akisema kuwa Kanuni za Bunge zilikiukwa.
Wabunge waliofukuzwa na Naibu Spika, Job Ndugai
juzi ni pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah
Wenje na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Juzi Mbowe aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia
Kanuni ya 68 (7), akimtaka Spika aeleze naibu wake (Ndugai) alitumia
kanuni gani ya Bunge, kuwasimamisha siku tano wabunge sita wa Chadema
wasihudhurie vikao vya Bunge vinavyoendelea.
Mwongozo wa Makinda
Akitoa mwongozo huo jana,
Spika Anne Makinda alisema kuwa kitendo kilichotokea hakiwezi kupuuzwa
na wala kuvumiliwa na Bunge, pamoja na wananchi kwa kuwa ni utovu wa
nidhamu ya Bunge na wananchi kwa jumla.
Alisema: “Kanuni ya 2(2) na 5(1), inampa mamlaka Spika ya kuleta amani bungeni.
Kanuni ya 2(2) inaeleza: “Iwapo jambo au shughuli
yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi, Spika ataamua utaratibu
wa kufuata katika jambo au shughuli hiyo, kwa kuzingatia Katiba, Sheria
nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika
wa Bunge na mila na desturi za uendeshaji bora wa shughuli za Bunge na
uamuzi huo utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa
baadaye wa uendeshaji wa shughuli za Bunge.”
Kanuni ya 5(1) inaeleza: “Katika kutekeleza
majukumu yake yaliyotajwa katika Ibara ya 84 ya Katiba, Spika ataongozwa
na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazikutoa mwongozo, basi Spika
atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni
nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila
na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na
utaratibu wa bunge la Tanzania.”
Makinda alisema kwa kutumia kanuni hizo mbili
anakubaliana na uamuzi uliotolewa na Ndugai na kwamba suala hilo
litaingizwa kwenye kitabu cha uamuzi wa Spika.
“Natumia Kanuni ya 2(2) na 5(1) kusema kuwa uamuzi
uliofanywa na Ndugai ni halali na itaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi
ya Spika,” alisema Spika Makinda.
Kauli ya Mbowe
Mbowe jana
alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi wa Spika ulijielekeza katika jambo
lisilo na kanuni inayolisimamia, tofauti na lile la kudharau mamlaka ya
kiti cha Spika, lililotolewa maelekezo na Kanuni ya 74 (1).
Kanuni hiyo inasema: “Spika anaweza kutaja jina la
mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo
kwenye Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge; ikiwa kwa maneno au
vitendo mbunge huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya Spika; au Mbunge
huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya
Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.”
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema alisema kuwa majibu ya
Spika ni ya bahati mbaya kwa sababu yameonyesha mwendelezo wa kupuuza
Kanuni za Bunge.
Akieleza kiini cha tatizo, Mbowe alisema kuwa ni
kuyumba kwa kiti, upendeleo wa wazi, kupanga mikakati na CCM na kumpuuza
Mnadhimu wa Chadema. Alisema nidhamu bungeni haitapatikana kwa
kuwatimua wabunge na kwamba wapo tayari kwa hilo, hata kama wataisha
wote, hadi pale Kiti cha Spika kitakapoacha upendeleo.
“Tutaliheshimu Bunge kama taasisi huru, lakini si
lilivyo sasa kama taasisi ya CCM,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa:
“..Nje ya Bunge wote tunaheshimiana, lakini mambo yanakuwa tofauti
bungeni kwa sababu ya Kiti cha Spika kutotenda haki.”
Alifafanua kuwa katika tukio zima, mbali na
kupuuza kanuni, adhabu yenyewe ilitolewa nje ya utaratibu, ikiwa ni
pamoja na kuruhusu askari wasiokuwa na sare kuingia bungeni.
“Bungeni pale kukiwa na siwa ni mahali patakatifu,
lakini Naibu Spika ‘alipaniki’ akaruhusu watu wakatoka kusikojulikana
bila sare na huo ni ukiukwaji wa taratibu,” alisema na kuongeza:
“Pale hata Makamu wa Rais ili aruhusiwe kuingia,
lazima kanuni itenguliwe, watumishi wa Bunge na askari wanaoruhusiwa
ndani, lazima wawe na sare maalumu, lakini mara hii Kiti cha Spika
kimeruhusu watu wasiohusika kuingia.”
Alisema kwamba, Ndugai aliyaacha kando mambo ya
msingi, akabakia kusema Tundu Lissu amesimama mara nyingi na kusahau
kuwa mbunge huyo ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, hivyo anaweza
kusimama mara nyingi kadri ya mahitaji.
Alifafanua kuwa siku ya kufukuzwa kwa wabunge hao,
Lissu alikuwa akitaka kuweka sawa kauli isiyokuwa sahihi ya Mwigulu
Nchemba kuwa Dk Slaa hakufanya mkutano wa hadhara Singida wakati wa
Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, badala yake alifanya mkutano wa ndani ya
viongozi wa dini.
Katika hatua nyingine, Frederick Katulanda,
anaripoti kutoka Mwanza kuwa, wabunge watano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge
watafanya ziara katika mikoa mitano kwa ajili ya kuwaeleza wapigakura wa
majimbo yao hali ya Bunge na upendeleo wa Spika wa Bunge , wanaoamini
umesababisha wao kutimuliwa.
Akielezea ziara yao katika majimbo yao Mbunge wa
Nyamagana, Ezekiah Wenje alisema kuwa wamefikia uamuzi huo ili kuwaeleza
wananchi uonevu ndani ya Bunge na jinsi Spika na naibu wake
wanavyoshindwa kusimamia kanuni kwa sababu ya kuwalinda CCM na Serikali.
Wenje alisema kwamba ratiba yao itaanzia katika
Mkoa wa Mwanza, ambapo watafanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa
Sahara na kwamba wabunge wote watano watakuwapo kueleza yaliyowakuta
bungeni.