Siku chache zilizopita nilitembelea Kitongoji cha Magomeni,
mjini Bagamoyo, katika kitongoji hicho nilipiga picha vipande vya nguzo
ambayo ni mabaki ya lango la mji huo.
Dereva wa bodaboda aliyenipeleka hapo nilimuuliza
kama anaelewa chochote kuhusu kuta hizo mbili, lakini cha ajabu alisema
hajui licha ya kuishi Bagamoyo miaka mingi.
Baada ya hapo nilikutana na dada ambaye anasema
amezaliwa na kuishi eneo la Magomeni, lakini hajui maana ya kuta hizo.
Nilimwambia kijana kwamba enzi hizo, Bagamoyo ilipokuwa chini ya
Wakoloni wa Kiarabu, eneo hilo palikuwa na lango likionyesha mtu
anaingia mjini na kwa wenye nchi.
Misafara ya watumwa, wamisionari na wavumbuzi,
wafanyabiashara, walipita katika lango hilo. Kuta nyingine zilizokuwa
upande mwingine wa barabara, zimepotea. Kuta nilizopiga picha ziko
kwenye uwanja wa mtu. Zinaweza kupotea kwa kuharibiwa wakati wowote.
Pia kulikuwa na nguzo nyingine pale ‘top life bar’
lakini sasa imebaki moja, nyingine imepotea. Nilielezwa na wahifadhi
kwamba eneo linalozunguka Caravan Serai, katika soko, na kule kituo cha
mabasi kipya lilitumika kujenga kambi za watumwa. Lakini hakuna
anayefahamu hilo.
Katika Idara ya Mambo ya Kale, inayoshughulikia
masuala ya historia, hakuna maelezo yanayoonyesha eneo hilo kulikuwa na
lango hilo. Hakuna kumbukumbu yoyote.
Nimekwenda Bagamoyo mara kadhaa, kila
unapotembelea moja ya kivutio cha historia utapata habari tofauti, aidha
itatofautiana na ya zamani, au itapotoshwa kidogo. Inafika mahali
unashindwa kuelewa ukweli ni upi.
Baada ya kusoma kitabu cha Henry Morton Stanley
anaeleza walipoanza safari walipumzika kwenye shamba la mama mmoja,
Gonera wa Kihindi, nje ya Bagamoyo. Lakini safari hii niliambiwa Gonera
alikuwa ni askari mlinzi aliyejengewa nguzo pale eneo la Mji Mkongwe na
von Wisman mwaka 1898.
Inaonekana Bagamoyo ina maeneo mengi ya kihistoria ambayo hayajawekwa katika historia kuu. Na hili ni kosa la idara husika.