Friday 10 April 2015

Bakora sita za Ukawa kwa CCM

Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.
Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.
Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.
Mgawanyiko na makundi
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake, tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu baada ya uteuzi.
Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.
Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika uchaguzi wa Oktoba.
Mchakato wa Katiba
Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM, ambazo hadi leo bado zinatia shaka.
Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ufisadi 
Haitoshi, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imekuwa kwenye kipindi kigumu cha matukio ya ufisadi yaliyosababishwa na ama watendaji au makada wake. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na sakata la Richmond ambavyo kwa vyovyote mwaka huu, litaibuka kwa kuwa linahusishwa na baadhi ya wagombea, sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo bado ni bichi, Epa ambayo baadhi ya watuhumiwa walisamehewa baada ya kurejesha fedha ambazo hazikuelezwa bayana zilikopelekwa na matukio yasiyokoma yanayoibuliwa katika ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Nguvu ya upinzani
Matokeo ya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 nayo yanaonekana kujenga hofu kwa CCM kwa kuwa yameibua picha mpya kuwa vyama vya upinzani vinakubalika hadi vijijini ambako chama hicho kimekuwa kinazoa kura bila upinzani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa CCM umepungua kutoka zaidi ya asilimia 91 za uchaguzi wa 2009 hadi asilimia 70 katika mitaa na vijiji mwaka jana, jambo ambalo lisipoangaliwa linaweza kukiathiri chama hicho.
Ahadi zisizokamilika
Mambo mengine mwiba kwa CCM kama chama tawala ni baadhi ya ahadi za 2010 ambazo hazijakamilika, zikiwamo za ilani ya uchaguzi na nyingine alizotoa Rais Jakaya Kikwete binafsi kadri alivyokuwa anaona mahitaji ya wananchi katika kampeni zake.
Baadhi ya ahadi hizo ni meli katika baadhi ya maziwa, barabara, vivuko, madaraja, hospitali na huduma nyingine mbalimbali.
Mahakama ya Kadhi
Pengine suala ambalo limeacha kovu kubwa katika uso wa CCM ni suala la Mahakama ya Kadhi. Suala hili liliingizwa katika ilani yake ya 2005 kuwa ikishinda itatafuta suluhisho ambalo hadi leo limeshindikana, badala yake likaweka ufa mkubwa katika utengamano wa Taifa.
Katika siku za karibuni, Waislamu walishuhudiwa wakidai ahadi hiyo iingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini Serikali ikaomba isiwemo, ikisema itatungiwa sheria ambayo hata hivyo inapingwa na viongozi wa Kikristo wanaodai Serikali haina dini hivyo isijihusishe nayo. Muswada huo tayari umewasilishwa na kuondolewa bungeni mara mbili.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumza vikwazo hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliungana na gazeti hili, akisema kashfa serikalini kwa vyovyote utakuwa ni mtaji mkubwa kwa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema suala la Katiba ni kesi inayojitegemea kwa Watanzania wengi wasiokubaliana na uamuzi wa Serikali kulazimisha muundo wa Serikali mbili ikiwa ni tofauti na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Kuna athari za escrow ambazo zimeanza kuonekana tangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hakuna aliyetegemea matokeo yale kwa upinzani, kwa hivyo hali siyo nzuri mpaka baadhi ya maeneo ya vijijini,” alisema na kuongeza:
“Hali ni mbaya katika tathmini inayoonekana kwa sasa na kama asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana chama hicho kisingekuwa na dalili za kurudi Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Kinana ameiombea CCM msamaha na kwa kiwango fulani ameibeba.”
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema vikwazo hivyo, haviwezi kuwa kipimo pekee cha kuikwamisha CCM kutokana na uzoefu uliopo.
“Kuna makundi matatu ninayoyajua, kuna Watanzania ambao huwezi kuwabadili kitu kwa CCM, wataichagua tu bila kujali changamoto hizo. Pili, kuna kundi la vijana ambao hufanya uamuzi dakika za mwisho, hawajulikani, kuna kundi la vijana la mabadiliko na kundi la kina mama wanaoangalia upepo wa utulivu, hawa hupiga kura kwenye utulivu wa chama,” alisema Dk Mallya.
Alisema Serikali bado inayo nafasi kubwa ya kutafuta maridhiano na taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kwenye jamii ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.
Dk Mallya alisema masuala ya Mahakama ya Kadhi na Mchakato wa Katiba yanaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kwa wananchi kupigia kura vyama vya upinzani.
“Serikali inaweza kurejesha imani ya Watanzania hata kwa muda uliobakia endapo itakubali kujadiliana, kukubaliana na taasisi, mashirika, viongozi wa dini na wadau,” alisema Dk Mallya.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema suala la Katiba limewakatisha tamaa Watanzania wengi waliokuwa wameweka maoni yao na kuondolewa.
Profesa Penina alisema mchakato wa Katiba ulikuwa na matarajio mazuri kwa Watanzania lakini jinsi ulivyochakachuliwa, umewafanya wengi kugawanyika.
“Sasa siwezi kujua kama hatua hiyo inaweza kuwa ni hasira ya kuiadhibu CCM, hilo sijui, ila kwa kweli imewakatisha tamaa sana, labda tusubiri tuone,” alisema Profesa Mlama.
Kauli ya CCM 
Kupitia ziara zake za ujenzi wa chama, Kinana amekuwa akisema asilimia 90 ya ahadi za 2010 zimeshatekelezwa.
Siku chache zilizopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alilieleza gazeti hili kwamba, hata kama Ukawa wangeunganisha vyama vyote vya upinzani, bado CCM itakuwa na mtaji mkubwa wa kushinda Uchaguzi Mkuu.
Kauli ya Nape inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyesema CCM haiteteleki kutokana na muungano wa Ukawa kwa kuwa ina mtaji wa wapigakura wengi.
“CCM tunajivunia kwa sababu Watanzania bado wana matumaini nasi, lakini hata kwa umoja wetu kama chama, tumefika vijijini tofauti na chama chochote, hao wapinzani wanakomea mjini tu,” alisema Simba.
Hata hivyo, mwenyekiti mstaafu wa UWT, Anna Abdallah alitoa maoni yake kwa tahadhari akisema kigezo pekee na muhimu kuliko vyote kitakachoifanya CCM kurejea madarakani ni uteuzi wa mgombea anayekubalika kwa wananchi, kwa kuwa huo ndiyo mtaji mkubwa kuliko vyote.
Alisema CCM imewahi kufanya makosa katika uteuzi wa majimbo kadhaa na kuchukuliwa upinzani.
“Kuchagua anayekubalika ni kigezo kikubwa kuliko vyote, kuhusu habari nyingine ya tuhuma au vigezo sita, sioni kama zina mashiko sana. Waswahili wanasema, “ukimpenda Mmakonde basi penda na ndonya yake”, alisema akimaanisha ukikipenda chama, penda na makandokando yake.

Mambo sita yaliyomshinda Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi lukuki kwa makundi mbalimbali ya jamii katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kupitia kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, lakini anaondoka madarakani mwaka huu akiwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi  na zaidi ameacha manung’uniko na mgawanyiko.
Mwaka 2005, alipoingia madarakani aliahidi kuondoa uhasama wa kisiasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kuwapatia wanahabari Sheria ya Habari, kupambana na ufisadi; na mwaka 2010 aliahidi kuwapa Waislamu Mahakama ya Kadhi na wananchi Katiba Mpya.
Mambo hayo sita yamekuwa mfupa mgumu kwa Rais Kikwete na anaondoka akiacha uhasama mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar, wakulima na wafugaji wakihasimiana, ufisadi ukiotesha mizizi, vyombo vya habari kufungiwa, nchi ikipasuka kuhusu Katiba Mpya na Mahakama ya Kadhi.
Sheria ya Habari
Rais Kikwete alijigamba kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari na Serikali yake ilianza kuandaa muswada mwaka 2007 lakini haukufikishwa bungeni. Machi 30, 2012 Kikwete alipokuwa mgeni rasmi katika utoaji Tuzo za Umahiri katika Uandishi (EJAT), aliahidi mambo mengi mazuri likiwamo la kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari katika Bunge la Oktoba.
Kuthibitisha kwamba Rais Kikwete hamaanishi anachokisema, Julai 30, 2012 yaani miezi minne tangu awape matumaini wanahabari, Serikali yake kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ililifungia gazeti la MwanaHalisi, kwa muda usiojulikana. Halafu Septemba 27, 2013 gazeti  la Mtanzania lilifungiwa kwa muda wa siku 90 na Mwananchi kwa siku 14. Magazeti mengine yaliyowahi kufungiwa siku 90 ni Kulikoni (Januari 8, 2010) na MwanaHalisi (Oktoba 13, 2008).
Desemba 8, 2011 mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima, Samson Mwigamba; mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Absalom Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd iliyochapisha gazeti hilo walifikishwa kortini wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi.
Septemba 2, 2012 aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alipigwa na kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi alipokuwa akiripoti mkutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Januari 23, 2015 Serikali yake imeamua kupiga marufuku usambazwaji wa gazeti la The EastAfrican nchini.
Katiba Mpya
Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 haikuwa na ahadi ya Katiba Mpya, lakini Novemba 8,      2010 siku alipozindua Bunge la 10, Kikwete alizungumzia umuhimu wa kuipa uhai Katiba iliyopo na Februari 2011 katika sherehe za CCM alisema atawapa Watanzania Katiba Mpya.
Kwa kuwa wazo hilo halikutokana na CCM, Kikwete alipata shida kulinadi ndani ya vyombo vya chama na Serikali na hata walipokubali, wasaidizi wake walidai ni marekebisho yeye akisema kuhuisha. Serikali ikatengeneza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,  akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba ambayo ilifanya kazi ya kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Katiba. Mwaka 2014 akaunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo liliandika Katiba Inayopendekezwa.
Ukosoaji mkubwa aliofanya Rais Kikwete alipozindua BMK, uliwagawa wabunge katika makundi mawili ya kudumu; wanachama wa CCM upande mmoja na wapinzani upande wa pili. Pia, Tume ya Warioba ilipingana na BMK lililoongozwa na Samuel Sitta.
Aprili 16, wapinzani chini ya umoja wao Ukawa walisusia BMK, likawa pigo la kwanza. Pigo la pili na la mwisho ni Januari 23, 2015 Ukawa walipotangaza kususia Kura ya Maoni iliyopangwa Aprili 30. Kutokana na misuguano hiyo, na kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa imepewa fedha za kutosha zikiwamo za kununulia mashine za BVR kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, Aprili 2, 2015 Kura ya Maoni ikafutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mahakama ya Kadhi
Mwaka 2010, katika mazingira tata CCM iliingiza ahadi ya Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Lakini Serikali haikufanya juhudi kubwa kutengeneza mazingira ya kukubalika kwa mahakama hiyo; kwanza, kwa Waislamu wenyewe; pili, kwa Wakristo.
Kosa namba moja. Agosti 30, 2011 alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idi katika msikiti wa Gadaffi, Dodoma, Rais Kikwete aliwaambia Waislamu kwamba amezungumza na maaskofu na wamemwambia kuwa hawana shida na Mahakama ya Kadhi isipokuwa wanataka iundwe na kuhudumiwa na Waislamu wenyewe. Waislamu walilalamika mambo yao kujadiliwa kwanza na Wakristo ndipo waelezwe wao.
Kosa namba mbili. Serikali imekuwa ikikutana na uwakilishi mpana wa maaskofu kutoka madhehebu yote kupata maoni yao lakini imekuwa ikikutana na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambalo halikubaliwi na Waislamu wote.
Kosa namba tatu. Dalili zote zikionyesha hakuna uwezekano wa kukubalika kwa Mahakama ya Kadhi, Serikali ilitoa ahadi nzito ndani ya BMK na Waislamu waliporidhia, hazikuwepo juhudi za kuandaa semina za kuelimisha wadau kuhusu muundo na uendeshwaji wake hali iliyosababisha hata baadhi ya Waislamu kuikataa kwamba siyo kati ya nguzo tano za Uislamu. Vilevile, lilikuwepo shinikizo kutoka kwa maaskofu na hasa ulivyoligawa Taifa mapande mawili.
Mgogoro Zanzibar
Moja ya ahadi nzito iliyofurahiwa na Watanzania ni ile ya kumaliza uhasama wa kisiasa Zanzibar kati ya wanachama wa CCM wengi wao wakiwa Unguja na wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ngome yao ikiwa Pemba. Ahadi hiyo iliianza kutekelezwa baada ya kuanzishwa mazungumzo baina ya viongozi wa CCM na CUF na hatimaye kufikia maridhiano na Katiba ikafanyiwa marekebisho kuruhusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongozwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pamoja na mafanikio hayo, uhasama wa kisiasa umerejea; CCM wakionekana kuwa vinara wa siasa za uhasama; wanawavizia na kuwapiga wafuasi wa CUF. Katika mikutano yao huhubiri ubaguzi kwa kuzingatia asili ya watu kwamba Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu wanatajwa kuwa ni vibaraka wenye lengo la kurudisha utawala Kisultani. Wanadai kwamba vibaraka hao wanataka kurudisha utawala wa Sultani aliyepinduliwa mwaka 1964,  Jamshid bin Abdullah Al Said, kizazi cha masultani kutoka Oman kilichotawala Zanzibar kuanzia mwaka 1832 hadi mwaka 1964.
Huu ni unafiki, ukweli ni kwamba Jamshid aliyetawala Zanzibar kuanzia Julai Mosi, 1963, baada ya kupinduliwa Januri 12, 1964 alikimbilia Uingereza. Salmin Amour, Rais wa awamu ya tano wa SMZ alitangaza kumpa uhuru Sultani huyo anayeishi Portsmouth, kurejea Zanzibar kama raia mwingine. Hajarudi.
Wakulima, wafugaji
Jambo jingine kubwa aliloahidi kushughulikia katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la Tisa Desemba 31, 2005 ni kulinda mazingira kwa kuhakikisha wakulima wanaachana na kilimo cha kuhamahama na wafugaji aliodai wanatembea umbali mrefu kusaka malisho wakiwa wamekonda na mifugo imekonda, kuwapa mbinu za ufugaji ili sekta ya ufugaji iwe ya kisasa.
Baada ya kuunda Serikali alitembelea Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, aliwaagiza watendaji: kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa; kudhibiti uhamishaji holela wa mifugo; kuimarisha huduma za ugani; kufufua ranchi zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa; na kutoka katika uchungaji wa kuhamahama na kwenda katika ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.
Vilevile, aliwaagiza kutafuta masoko ya nje ya kuuza mifugo na mazao yake; na kufikisha madawa na huduma za mifugo kwa wafugaji. Lakini miongoni mwa picha zilizojaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia mwaka 2006 ni za maiti ya wakulima na wafugaji katika maeneo tofauti nchini.
Baadhi zikionyesha watu waliokatwa koo, waliopasuliwa vichwa na waliopigwa mishale na mikuki; nyingine zikionyesha nyumba au maboma yalivyochomwa moto, mifugo kuuawa. Hasira na uhasama vimetanda kila mahali.
Katika kipindi cha uongozi wake, imeshuhudiwa migogoro mingi ya ardhi kati ya masikini na matajiri, wakulima wazawa na wawekezaji na mbaya zaidi kati ya wakulima na wafugaji ambao wamechinjana Mbarali, Kilosa, Kiteto na kwingineko. Rais Kikwete anaondoka huku hali ikiwa mbaya kuliko alivyoikuta.
Vita ya ufisadi
Ahadi nyingine ya Rais Kikwete kwa Watanzania aliyoitoa katika hotuba yake ya Desemba 31, 2005 ni kuanzishwa kwa mapambano dhidi ya rushwa kubwa kubwa kwa vitendo na siyo lazima ushahidi uwepo kwa asilimia 100.
Alisema: “hata ukihisiwa umekula rushwa tutahakikisha tunachunguza na kushughulikia…” Lakini licha ya Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutaja waliokula rushwa kupitia ununuzi wa rada ya kuongozea ndege, Serikali ilikataa kuwashughulikia.
Mafisadi wengine ambao hawakushughulikiwa na Serikali yake ni walionufaika kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), walitoengeneza dili kupitia kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans, walioiuzia vifaa hospitali ya Muhimbili kwa bei mbaya, waliochangisha fedha za kula tu baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini (2012) na sasa waliotengeneza mazingira ya kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Serikali imewanasa walimu na mahakimu na kuwafungulia mashtaka kwa madai ya kuchukua rushwa ndogondogo.