Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amewasilisha ripoti tano za ukaguzi
wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi
ya Sh600 bilioni katika maeneo mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo
hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali Kuu,
Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa
maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi hewa wa
umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za Tanzania
waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na matumizi
yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha Maafa,
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC),
Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi
watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano wa pamoja
na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za Kitengo cha
Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya kufanya
shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema ililidanganya
Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi
wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika
katika mambo mengine kabisa, yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo
ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa
na makandarasi Sh800 bilioni.
Misamaha ya kodi
Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini kasoro
katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na kusababisha ukiukaji
wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33 bilioni
yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold Mine na
Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili msamaha na
kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
Alisema pia misamaha ya kodi kwa malengo tofauti
na yaliyokusudiwa, ilitolewa na kusababisha upotevu wa Sh392.7 milioni
katika Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa
imesamehewa kodi Sh465.2 ili kuingiza magari 28.
Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kati ya hizo kukusanya Sh72.5 milioni.
Pia, alisema misamaha ya Sh53.4 milioni ilitolewa kwa Kampuni ya
Kilemakyaro Mountain Lodge Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi na
upanuzi hoteli katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, lakini
kampuni iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha na mengine matano
‘kuchepushwa’.
“Hata hivyo, ukaguzi ulithibitisha ununuzi wa gari
moja tu ya Hyundai Santa. Magari mengine matano aina ya BMW na Toyota
Land Cruiser Prado hayakufahamika yalipo,” alisema. CAG aliishauri
Serikali izibe mianya ya upotevu wa kodi kupitia misamaha ya kodi
aliyobaini katika ukaguzi wa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha
usimamizi na ufuatiliaji wa misamaha ya kodi iliyotolewa.
Mashine za EFD
Alisema katika ukaguzi wa malipo na matumizi ya
mashine za kielektroniki (EFD), ofisi yake ilibaini kuwa kampuni binafsi
hazitumii mashine hizo za kutolea stakabadhi.
Alisema hali hiyo imesababisha malipo ya Sh4.4
bilioni kutokuwa na stakabadhi za kielektroniki kwa taasisi za Serikali
Kuu na Sh4.6 bilioni kwa sampuli 22 ya mamlaka za serikali za mitaa.
“Katika suala hili, TRA ilitoza faini Sh440.8
milioni kwa wafanyabiashara ambao walishindwa kutumia mashine za EFD
ambapo jumla ya Sh72 milioni zililipwa sawa na asilimia 16 na hivyo
kufanya bakaa ya Sh369 milioni ambayo haikulipwa,” alisema.
Alisema pia ukaguzi ulibaini upungufu katika
usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile, malipo yasiyokuwa
na nyaraka. Upungufu mwingine ni hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa
kwa ukaguzi, fedha zilizotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na
manufaa na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Alishauri taasisi za Serikali zisiendelee kanunua
vifaa na huduma kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFD kutoa
stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
“Hii iende sambamba na kuhakikisha kuwa maofisa
masuuli wanaimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani ikiwa pamoja na
kuimarisha ukaguzi kabla ya malipo,” alisema.
Mishahara hewa
Alisema fedha zilizolipwa kwa watumishi hewa wa
Serikali Kuu ni Sh141.4 milioni, “Hali hii inaendelea licha ya kuwa
Serikali imewekeza kwenye mfumo wa Lawson kama njia mojawapo ya
kudhibiti hali hiyo,” alisema. Hata hivyo, alisema suala hilo linazidi
kupungua ikilinganishwa na mwaka jana. Lakini alisema Sh1.01 bilioni
katika halmashauri 36 zililipwa kama mishahara kwa watumishi waliotoroka
kazini, waliofariki, waliostaafu na kufukuzwa kazi.
Alisema kutokana na watumishi hewa, Sh845 milioni
za halmashauri zililipwa kama makato ya taasisi mbalimbali kama vile
mifuko ya pensheni, taasisi za fedha, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) na TRA kwa ajili ya wafanyakazi hao hewa.
Katika balozi
CAG pia ameeleza jinsi Serikali ilivyolipa Sh543.7
milioni kutokana na kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania
waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na
changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani.
Watumishi hao ni wa balozi za Tanzania Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani).
Ripoti hiyo inaonyesha tarehe ambazo watumishi hao
walistaafu, lakini Serikali iliendelea kuwalipa huku wakiwa katika
maeneo yao ya kazi, zikijumuisha kodi za majengo huku baadhi ya
watumishi hao wakifanya kazi licha ya kuwa mikataba yao kumalizika.
Ufisadi Tanesco
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo kwa ununuzi wa
Sh3.2 bilioni uliofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bila
kuzingatia kiasi kilichotengwa kwenye bajeti ya Sh400 milioni.
“Katika zabuni nyingine, Tanesco iliingia mkataba
wa Sh340 milioni ambayo ni zaidi ya bajeti iliyotengwa ya Sh154 milioni.
Ukaguzi haukuweza kupata ushahidi wa kuwapo kwa marejeo ya bajeti kwa
kiasi kilichotumika nje ya makisio,” alisema
Vyama vya siasa
Kuhusu ukaguzi wa vyama vya siasa, CAG alisema
hadi kufikia Juni, 2013 vyama 21 wakati vinakaguliwa, ni 12 tu ndivyo
vilivyowasilisha taarifa za hesabu.Alisema kati ya vyama 12, tisa
havikuwasilisha taarifa za hesabu ambavyo ni UPDP, Tadea, UDP,
Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa vyama
sita vya siasa vilipata hati ya shaka ambavyo ni CCM, Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi, TLP na Chauma na vya vingine vilipata hati mbaya ambavyo
ni NRD, UMD, ADC, APPT, NLD na SAU.
Alishauri Msajili wa Vyama vya Siasa akishirikiana
na Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu
(NBAA), waandae mwongozo wa aina ya muundo wa taarifa za fedha
utakaotumiwa na vyama vyote vya siasa.
Bajeti
Kuhusu bajeti, alisema tathmini waliyofanya kuhusu utekelezaji
wa miradi ya maendeleo, programu na shughuli nyingine za maendeleo
katika baadhi ya halmashauri, imeonyesha kuwa hadi kufikia Juni 30,
mwaka jana, halmashauri hizo zilikuwa na bakaa ya jumla ya Sh29.2
bilioni sawa na asilimia 28 ya jumla fedha zilizotolewa.
Alisema kubakia kwa kiasi kikubwa cha fedha bila
kutumika katika utekelezaji wa miradi kunatokana na ucheleweshaji wa
kutuma fedha katika halmashauri.
Deni la Serikali
Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, deni la
mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia Sh1,699 milioni na Sh975.1
milioni zilipaswa kuwa zimereshwa, lakini hadi wakati wa kuandika
ripoti hiyo zilikuwa bado hazijalipwa.
Alishauri mifuko na Serikali kuzingatia na kufuata
mwongozo wa uwekezaji wa fedha za mifuko ambao pamoja na mambo mengine,
unatoa ukomo wa aina za mali ambazo mifuko inaweza kuwekeza.