Sunday 25 January 2015

Ukawa waivuruga Serikali, hawatashiriki kura ya maoni

Dar es Salaam. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimeeleza kuwa kuna matatizo mengi kwenye mchakato wa Kura ya Maoni na kutangaza rasmi kutoshiriki, vikidai vitahamasisha wananchi kuwaunga mkono.
Tamko hilo limekuja siku chache baada ya mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kueleza kuwa uwezekano wa Kura ya Maoni kupigwa Aprili 30 ni mdogo na kwamba juhudi za kutaka azma hiyo itimie zinaweza kusababisha sheria kupindishwa.
Kauli yake iliungwa mkono na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye alisema uwezekano wa kupiga Kura ya Maoni siku hiyo ni mdogo na kwamba Serikali inahitaji kuwa makini ili kuhakikisha inapigwa Aprili 30.
Jana, vyama hivyo viliongeza uzito kwenye hoja hiyo ya kutaka mchakato huo usimamishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu vilipotoa tamko la pamoja la kususia mchakato huo, vikieleza kuwa muda uliosalia kukamilisha mchakato wa Kura ya Maoni ni mfupi, ikilinganishwa na maandalizi hafifu yanayofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ambayo imetangaza uandikishaji katika Daftari la Wapigakura utaanza Februari 16.
Wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, Freeman Mbowe wa Chadema, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzina na Emmanuel Makaidi wa NLD, walitangaza msimamo huo jana baada ya kumalizika kwa kikao chao kwenye ofisi za makao makuu ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba ambaye alitoa tamko la Ukawa kujiondoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba Aprili mwaka jana, alisema wamefikia uamuzi wa kutoshiriki katika Kura ya Maoni kwa sababu mchakato mzima haukuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Vyama vya siasa, ikiwemo CCM vilikubaliana mwaka jana kwamba Kura za Maoni ifanyike mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu, tulisaini wote na Rais Jakaya Kikwete alikubali,” alisema Lipumba.
Alisema jambo la kushangaza, Rais Kikwete aliwageuka na kutangaza kwamba Aprili 30, mwaka huu kuwa siku ya kupiga kura ya maoni.
“Tukashangaa Rais anatupiga chenga kwenye jambo kubwa kama hili ambalo tulishakubaliana naye kuwa lifanyike baada ya uchaguzi,” alisema.
Alisema pamoja na kutangaza siku ya kupiga kura, bado uandikishaji katika Daftari la Wapigakura haujaanza kwa sababu wanasubiri vifaa.
“Hadi sasa vifaa vya Biometric Voter Registration (BVR) vilivyopo ni seti 250 wakati vinavyohitajika ni seti 7,500, Tume inasubiri hadi sasa, zoezi hili litafanyika?” alihoji Lipumba.
Hata hivyo, juzi uongozi wa Nec ulisema Kura ya Maoni itafanyika kama ilivyopangwa licha ya vifaa hivyo kuchelewa kufika.
Ulisema muda uliobaki utatosha kwa asasi za kiraia kutoa elimu na vyama vya siasa kufanya kampeni.
Lipumba alisema historia ya mchakato huo imekuwa haishirikisha maoni ya watu na matatizo yanayojitokeza katika maandalizi ya Kura ya Maoni, wameamua kujitoa na hawatashiriki kutengeneza Katiba ambayo ni batili.
Naye Mbowe aliwaomba Watanzania wote kujitoa kwenye mchakato wa kura za maoni kwa sababu unalazimishwa na unafanyika bila ya kuwa na uhakika.
“Tumeamua kwamba hatuwezi kukengeuka na kushiriki kupigia kura kwenye mchakato ambao ni haramu. Tumeona tuwaachie CCM wenyewe wamalizie mchakato wao haramu,” alisema Mbowe.
Akifafanua zaidi Mbowe alisema Sheria ya Kura ya Maoni inataka Jaji wa Tanzania na Jaji wa Zanzibar kutengeneza kanuni ambazo wasioridhika kwenye kura ya maoni wanaweza kushtaki.
“Lakini hadi leo majaji hao hawajakaa kutengeneza kanuni hizo jambo ambalo tunaona mchakato huu hauna masilahi ya wananchi bali ya watu,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema mchakato mzima wa Katiba sasa `umeporwa’ na Ikulu kwa sababu hata kutangaza siku ya kupiga Kura ya Maoni kulitakiwa kufanywe na mwenyekiti wa Nec, lakini cha kushangaza Rais ndiye aliyetangaza.
Naye Mbatia alisema Katiba haitakuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Hatuwezi kushiriki kwenye Kura ya Maoni kwa sababu muda uliobaki hauruhusu, tunawaachia wenyewe CCM waendelee kuchakachua, sisi tunaona tusijihusishe kuleta Katiba haramu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa NLD, Makaidi alisema amegundua mbinu za kuanza kuwasafirisha wananchi wa Bara kwenda kuishi Zanzibar kwa lengo la kupiga kura za ndiyo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Maoni ya wadau
Baadhi ya wasomi walioongea na gazeti hili jana, walikuwa na mawazo tofauti kuhusu tamko hilo.
Profesa Aidan Msafiri wa Chuo Kikuu cha Mtwara, alisema Serikali ni lazima izungumze na Ukawa ili kueleza kuhusu mchakato huo.
“Tunajenga nyumba moja kwa nini tugombanie fito, Serikali ni lazima iangalie hoja za Ukawa kama ni za msingi na ichukue hatua.”
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema Ukawa wameshaandaa ajenda yao ya kutokea katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema Ukawa hawana hoja na hawana huruma na mamilioni ya fedha zilizotumika katika mchakato wa Katiba mpya.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wameshasema kwamba muda uliobaki unatosha kufanya kampeni na kutoa elimu lakini wao wanajitoa,” alisema Bashiru.
Alisema siasa za Tanzania hivi sasa zimekuwa za vituko na matukio kwa sababu walitakiwa kusubiri ili kuona Nec wameshindwa kutekeleza zoezi hilo ndipo waamue kususia.

Vita vya Profesa Muhongo

Sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow linaweza kuwa limefanya jina la Profesa Sospeter Muhongo kuzungumzwa sana na kuonekana amekuwa kwenye wakati mgumu tangu lilipoibuka, lakini ukweli ni kwamba lilikuwa hitimisho tu la matukio mengi tangu msomi huyo aanze kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.
Muhongo, ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge Mei 3, 2012 kabla ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri, amekuwa kwenye kiti moto wakati wote tangu ashike uwaziri kutokana na kashfa ambazo hazikomi kwenye sekta ya madini na nishati, na tabia yake ya kushambulia wanaotoa hoja kwa maneno ya dhihaka na kujisifu, ambayo mara nyingi yalikera watoa hoja.
Mikataba 26
Waziri Muhongo alianza kazi kwa kuliagiza Shirika la Mafuta (TPDC) kupitia upya mikataba 26 ya utafutaji gesi, hatua ambayo iliungwa mkono na wengi huku wakitaka ripoti ya kazi hiyo iwe bayana ili Watanzania wajue uozo uliopo, hata hivyo, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi huo, Profesa Muhongo hakuweka bayana matokeo ya ripoti hiyo, badala yake akasema ripoti hiyo itatumika wakati wa kuingia mikataba mipya tofauti na alivyoeleza mwanzo kuwa angefuta mikataba mibovu.
Akajikuta anaingia kwenye mzozo na wadau, hasa wabunge, na miaka miwili baadaye, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ikaiagiza menejimenti ya TPDC kupeleka mikataba hiyo kwenye kamati, lakini menejimenti ikagoma, kitendo kilichosababisha viongozi wa shirika hilo wakamatwe.
Kampuni ya Puma Energy
Hatua iliyozua tafrani zaidi ni ile ya wizara yake kuipa kampuni ya Puma Energy zabuni ya ugavi wa mafuta mazito kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa, hasa bungeni ambako watunga sheria walidai kuwa zabuni hiyo ilitolewa bila ya kufuata Sheria ya Manunuzi. Wabunge walidai kuwa Puma Energy haikuwemo kati ya kampuni zilizoomba, na kutuhumu kuwa kulikuwa na rushwa.
Wabunge walitaka Profesa Muhongo na katibu wake, Eliackim Maswi wawajibishwe, hoja iliyosababisha mgawanyiko mkubwa bungeni kiasi cha CCM kuitisha kikao cha wabunge wake kupanga mikakati ya kumuokoa waziri huyo.
Katika sakata hilo, Profesa Muhongo aliingia kwenye mgogoro na mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye alichangia hoja. Katika majibu yake, Profesa Muhongo alisema kuwa alikuwa akidhani mbunge huyo kuwa ni msomi, na akalazimika kufuatilia elimu yake. Alipotaka kueleza matokeo ya kidato cha nne ya Ole Sendeka, Spika Anne Makinda alimzuia na kumtaka aendelee na hoja iliyokuwa mbele yake.
Wafanyabiashara wazawa
Tabia ya Profesa Muhongo kujibu hoja kwa kushambulia walioitoa iliamsha mjadala mkubwa baada ya wafanyabiashara wakubwa kulalamika kuwa wizara hiyo haitoi kipaumbele kwa wazawa katika utoaji wa leseni za utafutaji gesi na mafuta. Katika kujibu hoja hiyo, mtaalamu huyo wa jiolojia, aliwaita wafanyabiashara hao kuwa ni madalali na hawana uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Alieleza kuwa kazi hiyo inahitaji mtaji mkubwa. Alisema maombi tu ya kazi hiyo yanagharimu Dola 700,000, wakati takwimu za kazi hiyo zinagharimu Dola 3 milioni, utafutaji Dola 15,000 hadi 20,000 kwa mita moja ya mraba, kuchoronga kwenye kina kirefu kuna gharimu Dola 1 milioni kwa siku, wakati kumaliza tundu moja ni Dola 1 na yanahitajika matundu 12.
Pia alisema kuchimba kwa ajili ya kupitisha mabomba kwenda nchi kavu kunagharimu dola 200. Profesa alisema hayo bungeni huku akitamba kwamba yeye ni msomi na wabunge wanaojaribu kujenga hoja hizo ni mawakala ambao “wana-retire imprest” kwa kuzungumza bungeni, akimaanisha kuwa wanaonyesha kwa waliowalipa fedha kuwa wametekeleza kazi waliyotumwa.
Kufuta leseni za vitalu
Pia alizua kizaazaa kingine aliposema kuwa atapitia leseni zote za vitalu vya madini na kufuta vile ambazo hazifanyi kazi kama sheria inavyotaka. Alisema kuna leseni 597, lakini wanaolipa kodi ni wanaomiliki vitalu 10 tu na baadaye akatangaza kuwa alishafuta leseni za vitalu zaidi ya 150 na alikuwa anakusudia kufuta nyingine 78.
Mkakati wake uliwagusa wafanyabiashara wengi wazawa na mara kadhaa walipokutana walitoa kauli ya kulaani misimamo ya mbunge huyo wa kuteuliwa.
Wakati kashfa ya escrow ilipoanza, Profesa Muhongo alitumia tena mbinu yake ya kushambulia watoa hoja kwa kueleza kuwa maneno hayo yote yanatokana na uamuzi wake wa kufuta mkataba wa Tanesco na kampuni ya uwakili ya Mkono, akisema ililipwa Sh62 bilioni na hivyo kuwa moja ya taasisi zinazotafuna fedha za shirika hilo la umma.
Katika kashfa ya escrow, Profesa Muhongo anatuhumiwa kwa kushindwa kushughulikia vizuri sakata hilo la uchotwaji fedha kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa kwa pamoja na Tanesco na IPTL baada ya pande hizo mbili kuingia kwenye mgogoro na kufungua kesi mahakamani.
Akitoa utetezi wa Serikali bungeni, Profesa Muhongo alitumia staili yake ya kuwananga waliokuwa wakituhumu huku akijisifu kuwa ni msomi. Alieleza kuwa fedha hizo, Sh306 bilioni, hazikuwa mali ya umma bali za IPTL, lakini hoja zake zikapingwa vikali na wabunge ambao walionyesha nyaraka mbalimbali kuthibitisha kuwa msomi huyo hakusema ukweli.

Viongozi kujiuzulu pekee haitoshi

Jana Profesa Sosperter Muhongo alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini, akieleza kuwa anataka nchi isonge mbele kwa kuwa suala la kumtaka Rais amwondoe kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, limesababisha mambo mengi kukwama.
Profesa Muhongo amekuwa waziri wa pili kuondoka baada ya Profesa Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kuingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa IPTL, fedha ambazo zinahusishwa na sakata la escrow.
Mbali na mawaziri hao, tayari Jaji Fredrick Werema amejiuzulu kazi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa ushauri wake kuhusu fedha za escrow haukueleweka na kusababisha tafrani.
Pia, katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa sakata hilo, wakati watumishi watano wa Tanesco, Benki Kuu (BoT) na Mamlaka ya Mapato (TRA) wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kupokea rushwa inayohusu sakata hilo. Kashfa hii ni moja ya matukio mengi makubwa yaliyosababisha Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Baadhi ya matukio hayo ni kashfa ya Richmond, CAG na Operesheni Tokomeza ambazo zilisababisha Rais kupangua baraza lake.
Ni jambo la kupongeza kwamba angalau hatua zimechukuliwa kwa kiwango fulani katika kushughulikia tatizo hilo lililohusu uchotwaji wa takriban Sh306 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa BoT.
Kitu cha ajabu ni hii tabia inayoendelea kujengeka ya kuibuka kwa kashfa, mawaziri kujiuzulu, kuundwa kwa baraza jipya na baadaye mambo kuendelea kama kawaida kusubiri kashfa nyingine kuibuka bila ya hatu za dhati kuchukuliwa kudhibiti matukio kama hayo.
Jambo la ajabu ni kwamba kila kashfa inapoibuka, hutumika nguvu nyingi kuizua au kutetea viongozi wa Serikali hadi mambo yanapoonekana kuwa yamekuwa makubwa ndipo hatua zichukuliwe.
Tumeona katika kashfa ya escrow zilitumika nguvu nyingi kutetea wahusika hadi maji yalipozidi unga ndipo hatua zilipochukuliwa na kushughulikia wahusika. Kitu kibaya ni kwamba hadi wakati hatua zinaanza kuchukuliwa, tayari Serikali inakuwa imeshafuka na wananchi wameshaumia.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri sasa yamekuwa ya kawaida kwa kuwa kila yanapofanyika hazichukuliwi hatua thabiti kuzuia kashfa zisitokee. Suala la fedha kuchotwa kwa fedha zinazokuwa BoT sasa linaonekana kuwa la kawaida kwa kuwa kashfa ya Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje lilipotokea, hakukuchukuliwa hatua madhubuti kuziba mianya kama hiyo kwenye taasisi hiyo nyeti ya fedha.
Tunadhani ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuweka misingi imara ya uongozi itakayowabana viongozi wetu kujiingiza kwenye kashfa kama hizo. Misingi hiyo pia ihusishe hatua kali ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa viongozi ambao wataingia kwenye kashfa hizo kwa makusudi au uzembe ili kuzuia wengine kufanya mambo ya aibu na yanayoumiza wananchi.
Pia, siyo ufahari kuwawajibisha viongozi wakati ufisadi umeshafanyika kama ilivyokuwa kwenye sakata la EPA na sasa escrow kwa kuwa fedha za walipa kodi zinakuwa zimeshachotwa. Ufisadi unatakiwa uzuiwe mapema kuliepusha Taifa kupoteza mabilioni ya fedha na wanaowajibishwa wachukuliwe hatua kwa kujaribu kula njama za ufisadi na siyo kuadhibiwa kwa kufanya ufisadi.
Kadri Serikali inavyoonekana kuweka mikakati ya kuwakingia kifua watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ndivyo vitendo hivyo vinavyozidi. Serikali inatakiwa ionyeshe kuchukia ufisadi kwanza.Na ikichukia ufisadi, basi kujiuzulu wa kuwavua madaraka wahusika kutakuwa ni moja ya hatua za kuwashughulikia wahusika wote nah ii itasaidia kupunguza vitendo hivyo.

Monday 12 January 2015

Baada ya miaka 20, maridhiano yasakwa Loliondo

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Wilaya ya Ngorongoro ilikuwa na jumla ya wakazi 174,278 ikiwa na eneo la kilomita za mraba 14,036. Asilimia 52 ya ardhi yake ni hifadhi ya wanyamapori.
Wilaya hii yenye tarafa tatu za Loliondo, Ngorongoro na Sale, wakazi wake wanatumia asilimia 48 ya ardhi iliyobaki kwa shughuli za ufugaji. Ni sehemu ndogo ya ardhi hasa Sale ambayo wakazi wake wanatumia ardhi kwa shughuli za kilimo.
Kwa sababu ya kuongezeka kwa watu na mifugo, mahitaji ya eneo la malisho na kilimo nayo yanakua siku hadi siku.
Leo tutazungumzia mgogoro mmoja baina ya kata saba na kampuni ya ya Ortello Business Cooperation (OBC,) licha ya eneo hilo kuwa na kampuni zaidi ya tano zenye maslahi tofauti.
Kampuni hii ya OBC ndiyo imekuwa ikiendesha uwindaji wa kitalii katika eneo la pori Tengefu Loliondo. Mwaka huu, mgogoro ulikuwa mkubwa zaidi hasa baada ya Serikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kulipunguza eneo la pori tengefu la Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 .
Katika uamuzi huo, Serikali ilisema eneo la kilomita za mraba 2,500 litabaki kwa wakazi wa Loliondo na Sale na eneo la kilomita za mraba 1,500 litabaki chini ya Serikali kwa ajili ya uhifadhi ili kulinda mazalia na mapito ya wanyamapori.
Eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 zinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa Mashariki na pia linapakana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Eneo hilo linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo wa ikolojia wa Serengeti ambao unaruhusu wanyama kuhama kutoka ndani ya hifadhi na kuingia katika eneo hili kwa malisho na mazalia hasa nyakati za masika.
Tangazo hilo la Serikali, liliibua malalamiko ya wananchi wa Loliondo wakiungwa mkono na mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje ya wilaya. Wapingaji wa tangazo hilo, walisema Serikali imekiuka Sheria ya Ardhi ya mwaka 2009 na pia Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009.
Malalamiko hayo yalisababisha Serikali kuingilia kati baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenda Loliondo Aprili mwaka jana na kutengua uamuzi wa awali kuligawa eneo hilo.
Pia, Chama cha Mapinduzi (CCM), mapema mwaka jana, kiliunda tume ya kuchunguza mgogoro huo. Tume hiyyo iliongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba.
Tume hiyo ilipokutana na wananchi na viongozi wa eneo hilo, ilikumbana na tishio kubwa la wanachama wa CCM kukihama chama hicho baada ya kukabidhiwa rundo la kadi za chama.
Maridhiano
Baada ya kuendelea mgogoro kwa huu bila ya mwafaka, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu alizindua vikao vya maridhiano.
Akitumia kauli mbiu yake, ‘Ngorongoro bila migogoro inawezekana’, anatangaza kuunga mkono, uamuzi wa kata tatu, za Oloipili, Losoito Maalon na Olorieri Magaidulu kuamua kuanza kushirikiana na wawekezaji wa wilaya hiyo, kwa manufaa ya wananchi.
Nyalandu anasema haiwezekani miaka zaidi ya 20 Loliondo, iendelee kusifika kwa migogoro ambayo imekuwa ikisababishwa na watu wachache kwa masilahi yao.
“Ni lazima sasa mkubali kukaa viongozi wa kata zote saba ambazo zinapakana na mwekezaji OBC na wengine na kujadiliana mambo ya msingi kwa masilahi ya pande zote,” anasema.
Anasema ni muhimu mwekezaji akazingatia taratibu na sheria katika eneo lake kwani Serikali haitamvumilia mwekezaji ambaye hana uhusiano mwema na jamii, lakini pia ni lazima wananchi wajue kwamba wanapaswa kufuata sheria na taratibu katika makazi yao.
Nyalandu, anatoa wito kwa wakazi wa tarafa hiyo, kuendelea kuishi bila hofu, kwani Serikali haina mpango wa kuwaondoa kama ilivyotangazwa na vyombo vya habari vya kimataifa na kutoa ardhi yao kwa mwekezaji yoyote.
“Hakuna mpango wa kuwaondoa leo wala kesho na kutoa ardhi hii kwa mwekezaji kutoka Falme za Kiarabu, tunawataka muishi bila hofu na hakuna ambaye anaondolewa na kuchomewa makazi hapa Loliondo, kikubwa tunataka migogoro imalizike,” anasema .
Madiwani waliotangaza kujitenga na mgogoro
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Raphael Long’oi anasema wamechoshwa na migogoro isiyokwisha ambayo inachangiwa na watu wachache kwa masilahi yao.
Long’oi ambaye ni Diwani wa Losoito Maalon, anasema kata yake na zile za Oloipili na Olorieni wamekubaliana kuachana na migogoro na wawekezaji kwa manufaa ya wananchi.
Hata hivyo, anaiomba Serikali iliwalinde kutokana na vitisho kutoka kwa kundi ambalo halitaki maridhiano ambalo sasa linabadilisha maridhiano yao na kutangaza wao kama viongozi wanauza ardhi kwa wawekezaji.
Diwani wa Kata ya Oloipili, William Alais anasema kwake hakuna mgogoro na wawekezaji na taarifa nyingi ni za uchochezi zinazowanufaisha watu wachache.
Alais anasema wamefikia maridhiano na wawekezaji na wameanza kunufaika na miradi ya maendeleo.
“Wanaochechea ni watu wachache, kwa manufaa yao sasa sisi tumekubaliana kusema hatutaki migogoro tunataka maendeleo”anasema
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Elias Ngolisa anasema wanachohitaji wananchi wa Ngorongoro ni kuishi maisha yao kama zamani bila kuhamishwa.
“Kama wananchi hawa wakiachwa katika ardhi yao, sidhani kama kutakuwa na mgogoro Loliondo, sisi tunataka maendeleo,” anasema.
Ngolisa ambaye ni Diwani wa Malambo, kata ambayo haijafikia maridhiano na mwekezaji OBC, anasema atashiriki kikao cha maridhiano ambacho kinashirikisha pia viongozi wa kata nyingine ambazo bado hazijafikia maridhiano za Arash, Soitsambu na Ololosokwani.
Mtandao wa mashirika watoa msimamo
Kwa miaka kadhaa, Serikali imekuwa ikiyatupia lawama mashirika yasiyo ya kiserikali Ngorongoro na kuyataja yamekuwa chanzo cha vurugu kutokana na kutoa taarifa za uchochezi, ikiwamo upotoshwaji juu ya taarifa kuwa wananchi 40,000 wa Loliondo wanatakiwa kuondolewa kumpisha mwekezaji.
Mratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali Wilaya ya Ngorongoro (Ngonet), Samweli Nang’irwa anakanusha madai hayo.
Anasema mashirika yao yakiwa wadau wa maendeleo, hayapingani na mwekezaji yoyote, bali wanataka wawekezaji wafanye majukumu yao na wananchi waendelee na maisha yao.
Nang’irwa ambaye hivi karibuni, alikamatwa na kuhojiwa kwa saa zaidi ya tatu kuhusiana na mgogoro huo, anasema mashirika yao, yanajihusisha na masuala ya maendeleo ya jamii na utetezi, hivyo kama wananchi wakifikia maridhiano na wawekezaji wao hawana matatizo.
OBC wataka maridhiano 
Kampuni ya OBC inaungana na Serikali na madiwani wa kata tatu kutaka maridhiano ili kila upande uendelee na shughuli zake kwa manufaa ya pande zote .
Mkurugenzi Mtendaji wa OBC, Isack Mollel anasema tangu kampuni hiyo iliposaini mkataba huo, imekuwa ikiwinda kitalii chini ya usimamizi wa Serikali kama zilivyo kampuni nyingine.
Mollel anasema, eneo la pori tengefu lina historia ndefu kwani awali, lilikuwa chini ya shirika la umma la uwindaji wa kitalii la Tawico ambalo sasa tayari limebinafsishwa.
“OBC tangu tumefika Loliondo licha ya uwindaji, tumefanya mengi. Hakuna kampuni ya uwindaji nchini ambayo imefanya vitu vingi kama sisi. Tumejenga sekondari, tumetoa misaada mingi katika sekta ya afya, maji na elimu na uhifadhi,’’ anaeleza.

Miaka 51 Mapinduzi ya Zanzibar

Zanzibar ya Karume
Chini ya uongozi wa Karume, Zanzibar inatajwa kama nchi iliyokuwa ikipiga hatua nzuri hasa katika maendeleo ya uchumi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Kwa mfano, ‘tarikhi’ ya Zanzibar inaonyesha wananchi walikuwa wakipata huduma za maji safi na salama, afya, chanjo na matibabu, kujengewa makazi bora na ya kisasa.
Chini ya Serikali ya awamu kwanza kulikuwa na kasi ya ujenzi wa viwanda, karakana, mashirika ya Serikali. Usafirishaji wa mazao kama pilipili, mbata na karafuu nao ulikuwa juu na kuiwezesha Zanzibar kupata fedha za kigeni hatua iliyosaidia kuimarisha uchumi.
Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa msingi wa Mapinduzi ulikuwa ni kuwatoa wananchi katika kadhia ya unyonge, uonevu, ukandamizaji wa haki na fursa. Pia kuwapatia huduma bora za jamii baada ya kuondoa utawala wa Kisultan uliohamia kutoka Oman.
Baada ya Mapinduzi, ujenzi wa viwanda vya sigara, mvinyo, nguo, sukari, soda, viatu, maziwa, magodoro na vitu vya nyumbani, kulitanua wigo wa ajira kwa wananchi, huku kukiwa na kasi kubwa ya uzalishaji mazao shambani kutokana na Serikali kupeleka pembejeo na mbolea kwa wakulima.
Hali ilivyo sasa
Kati ya mambo yaliyowasukuma Waafrika wa Zanzibar na kulazimika kukiunga mkono Chama cha Afro Shirazi Party ( ASP) ilikuwa ni tatizo la ardhi. Walowezi na mabebari wengi ndiyo waliokuwa wakimiliki na kuhodhi ardhi yenye rutuba.
Awamu ya kwanza iligawa ardhi kwa wananchi, lakini hali ilivyo sasa ni sawa na ile iliyokuwa kabla ya Mapinduzi mwaka 2964.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega uchumi Zanzibar (ZIPA), Nassor Salum anasema hivi sasa Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la uwekezaji wa miradi hasa katika sekta ya utalii, kutokana na maeneo mengi ya fukwe hasa katika ukanda wa Mashariki kuchukuliwa na baadhi ya vigogo na watendaji serikalini.
“Maeneo makubwa ya ardhi yamehodhiwa, kuzungushwa kuta bila ya kuendelezwa kwa maelezo kuwa yamekuwa yakiwekwa ili kusubiri matajiri wa nje na ndani na kuuzwa kwa bei ya juu,’’ anasema.
Elimu
Wakoloni walitoa elimu kwa misingi ya rangi, Waafrika waliwekwa kando. Miaka 51 ya mapinduzi wananchi hawaridhiki na hali ilivyo kwenye sekta hiyo.
Ukweli ni kuwa elimu Zanzibar inaendeshwa kimatabaka. Wananchi walio wengi wanasomesha watoto wao katika shule za Serikali zinazokabiliwa na changamoto nyingi za kitaaluma. Watoto wa viongozi, matajiri wengi wanasoma shule binafsi zenye mazingira bora ya utoaji taaluma.
Makazi
Kabla ya mapinduzi, nyumba nyingi za wananchi wenye asili ya Kiafrika, zilikuwa zikisikitisha. Zilijengwa kwa miti, udongo na kuezekwa kwa makuti au vipande vya madebe.
Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu zilizowahamasisha wananchi kukiunga mkono Chama cha ASP, kilichofanikiwa kuuondosha utawala wa Kisultan uliokuwa ukilindwa na Waingereza.
Hata hivyo, mara baada ya Mapinduzi, Serikali ya awamu ya kwanza, ilitimiza ahadi ya kuwapatia wananchi makazi bora kwa kuwajengea makazi bora. Mpango huo uliendelezwa na awamu zilizofuatia ingawa haukuwa na tija kubwa kwa wananchi wanyonge, kutokana na nyumba nyingi za gharama nafuu zilizojengwa kuhodhiwa na vigogo badala ya wananchi makabwela.
Kilimo
Wananchi wanyonge kabla ya Mapinduzi walipata dhiki katika ufanyaji wa kazi za kilimo kutokana na ardhi kubwa kuhodhiwa na walowezi na matajiri.
Wengi walilazimika kukodi ardhi kwa ajili ya kilimo na sehemu ya mazao waliopata walitakiwa kuwapa waliowakodisha ardhi.
Yalikuwa ni madhila na mashaka makubwa yaliowakumba Waafrika. Mara baada ya Mapinduzi, Serikali iliwapa ekari tatu kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.
Hata hivyo, leo kilimo kimedorora licha ya kuwa sehemu kubwa ya visiwa vya Unguja na Pemba kuna ardhi ya kutosha yenye rutuba. Kilimo hicho kwa sasa kinachangia asilimia 31 ya pato la Zanzibar.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, Serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya bajeti ya mishahara badala ya bajeti ya miradi ya maendeleo.
Taarifa zinaonyesha bajeti ya mwaka inayokwenda katika mishahara ni zaidi ya Sh12 bilioni, ilhali bajeti inayotengwa kwa maendeleo ni Sh1.5 bilioni. Kinachosikitisha ni kuwa wahisani ndio wanaoonekana kuwa na uchungu na kilimo kwa kutenga bajeti ya Sh8 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Afya
Mchango wa Serikali katika kutoa huduma za afya baada ya miaka 51 ya Mapinduzi, hauridhishi hali inayosababisha Wizara ya Afya kuonekana ni tegemezi kwa wahisani.
Kwa sababu ya udogo wa bajeti ya sekta ya afya, huduma nyingi zimezorota, huku idadi ya wagonjwa wanaolazimika kutibiwa nje ikiongezeka kila mwaka. Fedha nyingi zinatumika nje kwa ajili ya kuwatibia wagonjwa wa moyo na saratani, kwa kuwa nchi haina wataalamu bingwa wa magonjwa hayo na vifaa vya kisasa.
Tunatekelezaje malengo ya Mapinduzi?
Ili Serikali ionekane ikitekeleza malengo ya Mapinduzi, haina budi kusimamia dhana ya usawa, haki na uwajibikaji.
Kero tete za wananchi kama vile kushamiri kwa rushwa, kuuzwa kwa ardhi, elimu duni, huduma mbaya za afya, zinaweza kufikia kikomo ikiwa Serikali itaamua kuzifungia kibwebwe.
Kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na hata Taifa, hatuna budi kuwekeza katika elimu, kilimo, ufugaji, uvuvi na ujenzi wa viwanda.

Friday 2 January 2015

Mwaka wa uchaguzi,Kikwete atoa salamu za mwisho za mwaka

Dar es Salaam. Mwaka wa uchaguzi umeingia. Usiku wa kuamkia leo, Watanzania wameupokea mwaka mpya 2015 huku tafakari kubwa ikiwa ni matukio makubwa yatakayotokea mwaka huu, ukiwamo Uchaguzi Mkuu na kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Mbali na uchaguzi wa rais wa awamu ya tano, wananchi wataamua ama kuipitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa, mambo ambayo wasomi, wanasiasa na wanaharakati wameonya kuwa yanatakiwa kuendeshwa na kusimamiwa kwa weledi na umakini mkubwa.
Vilevile, kutokana na matukio hayo kugharimu fedha nyingi, wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa mwaka huu utakuwa mgumu na itakaowalazimu Watanzania kufunga mikanda zaidi.
Pia, macho na masikio ya wananchi yako kwa vyama vya upinzani ambavyo vimeungana na kuzaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuona kama vitasimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi za ubunge na udiwani kama vilivyokubaliana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Maandalizi ya uchaguzi huo yanaanza mwezi huu kwa wapigakura kuandikishwa upya katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, ambalo tangu mwaka 2009 halijawahi kuboreshwa na hivyo kusababisha wengi kushindwa kupiga kura katika uchaguzi wowote uliofanyika baada ya 2010.
Pengine jambo ambalo linasubiriwa kwa hamu na wananchi ukiacha Uchaguzi Mkuu na Katiba Mpya ambayo kampeni zake zitaanza Aprili 30, ni mchakato wa ndani ya vyama vya siasa wa kupata wagombea urais, hasa kutokana na mvutano ulioanza kujitokeza ndani ya CCM na mvutano unaotarajiwa ndani ya Ukawa.
Matukio
Tukio litakaloanza mwaka huu ni lile la Januari 30 la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao utakamilika Aprili 28 ukifanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kulingana na uandikishaji wa majaribio uliofanyika katika majimbo matatu ya Kawe, Kilombero na Katavi, shughuli yenyewe inatarajiwa kuvuta hisia na hamasa za Watanzania wengi hasa kutokana na muda, matatizo ya kukwama kwa mashine za kielektroniki (BVR) na wingi wa watu waliojitokeza.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ametangaza tarehe ya upigaji Kura ya Maoni kuwa ni Aprili 30.
Februari mwaka huu, CCM imeahidi kutoa msimamo wake kuhusu wanachama wake walioanza kufanya kampeni mapema kujihusisha na vitendo vilivyokiuka maadili ndani ya chama na jamii. Huenda chama hicho kikawaengua baadhi yao kwa kuongeza muda wa onyo hivyo kujikuta wakishindwa kuwania nafasi hiyo, iwapo watabainika kuendelea kukiuka maadili ya chama, licha ya awali kuonywa na kupewa adhabu ya kutojihusisha na masuala hayo mpaka baada ya miezi 12.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; mawaziri Bernard Membe (Mambo ya Nje), Stephen Wasira (Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Mei utakuwa na tukio la aina yake pale Ukawa na CCM pamoja na vyama vingine vitakapokuwa vikiteua wagombea urais, ikiwa ni baada ya wengi waliojitokeza kuchujwa katika vikao vya ndani vya vyama hivyo.
Juni mwaka huu, Rais Kikwete atalivunja Bunge baada ya kumalizika kwa Mkutano la Bajeti utakaoanza Aprili mwaka huu, ukiwa tayari umepitisha bajeti ya Serikali ambayo sehemu yake itatumiwa na Serikali mpya ya awamu ya tano. Pamoja na kwamba siyo utaratibu wa kikanuni, lakini kwa utamaduni wa Bunge la Tanzania, Rais Kikwete anaweza kutoa hotuba ya kulivunja Bunge.
Miezi inayotarajiwa kuwa na changamoto kubwa ni kuanzia Julai hadi Oktoba ambayo itakuwa ya kampeni za uchaguzi ambao wagombea urais, ubunge na udiwani watakuwa wakinadi sera zao.
Mwishoni mwa Oktoba, ndipo utakapofanyika Uchaguzi Mkuu na Tanzania kupata rais mpya ambaye mpaka sasa ni vigumu kutabiri atakuwa nani na atatoka chama gani. Hali hiyo inatokana na CCM hadi sasa kuwa na makada zaidi ya 14 wanaotajwa kuutaka urais wakiwamo wanne ambao tayari wametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo. Kwa upinzani, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vinavyounda Ukawa ndiyo wanaopewa nafasi za kugombea nafasi hiyo. Hao ni Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willbrod Slaa, James Mbatia na Freeman Mbowe huku vyama vyenyewe vikisema vinaweza hata kumpata mtu nje ya muungano huo.
Uchambuzi wa kisomi
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam (Tudarco), Lois- Singa Metili alisema mwaka 2015 ni kipindi cha mpito ambacho endapo mambo yote yaliyopangwa yatakwenda sawa, miaka inayofuata itakuwa mizuri kwa Watanzania.
“Hatujui kura za hapana au za ndiyo kwenye Kura za Maoni ya Katiba zitakuwa ngapi, hatujui kama NEC itapewa meno ya kutosha ya kusimamia uchaguzi ili tupate rais kwa njia ya haki.”
Alisisitiza kuwa iwapo haki itatumika katika kupitisha mambo hayo, nchi itajenga msingi imara kwa maendeleo ya watu wake kwa miaka mingi ijayo.
Alisema kwa kuwa Tanzania mwaka 2014 ilitajwa vibaya kwenye vyombo vya habari vya Magharibi, ikihusishwa na kashfa za rushwa, inabidi taasisi zote nchini kurekebisha kasoro hiyo.
Kuhusu siasa, Metili alisema CCM itakuwa na kibarua cha kumpata mgombea mwenye sifa atakayekubalika kwa wananchi. Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kutokana na mwaka 2015 kukabiliwa na mambo mazito ya kitaifa yanayohitaji fedha nyingi, Serikali itakuwa katika wakati mgumu kifedha.
Dk Ngowi aliutaja mwaka huu kuwa ni wa kipekee kwa kuwa licha ya kuhitaji fedha nyingi, utaongezewa maumivu na hatua ya wahisani kukataa kutoa msaada kwa sababu ya kashfa ya escrow iliyotokea mwishoni mwa 2014.
Alieleza kuwa ingawa maisha ya wananchi yanaweza yasibadilike sana, lakini Serikali itahitaji kujipanga upya katika kukusanya fedha.
Uchambuzi wa Dk Ngowi unaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila aliyesema mwaka huu uchumi wa nchi utaporomoka kwa sababu ipo katika mahitaji makubwa ya fedha za uchaguzi, uandikishaji Vitambulisho vya Taifa na vya kupigia kura sambamba na upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya.
“Uchumi unakua lakini maendeleo ya uchumi hayaonekani kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na uchumi kukuzwa na sekta za madini, utalii, mawasiliano ambazo hazibebi watu wengi kama ilivyo katika kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema licha ya mwaka huu kuwa na mambo mengi muhimu, Serikali haionekani kuchukua hatua za dharura.
Dk Kijo- Bisimba alisema ili taratibu ziende kama zilivyopangwa, ilitakiwa hadi sasa nakala za Katiba Inayopendekezwa ziwe zimeshasambazwa kwa wananchi, lakini hilo linaonekana kusuasua.
“Maboresho ya Daftari la Wapigakura yalitakiwa yawe tayari, lakini mamlaka hazijajipanga kama ulivyoona kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Watanzania wanaingia mwaka mpya wakiwa wamechanganyikiwa, hawajui nani anasema ukweli kuhusu fedha za escrow kama zilikuwa ni za umma au la... “Bunge lilisema fedha zile ni za umma, lakini huyu mwingine naye kasema siyo fedha za umma.”Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (Duce), Dk Aneth Komba alisema; “Ninachokiona mwaka huu utakuwa mfupi sana kutokana na mambo kuwa mengi.”
JK atoa salamu za mwisho za mwaka akiwa Rais
Rais Jakaya Kikwete jana alitoa salamu zake za Mwaka Mpya kwa mara ya mwisho katika utawala wake huku akisema mwakani atakuwa akifuatilia salamu kama hizo kupitia televisheni na redio akiwa kijijini kwake Msoga mkoani Pwani.
Katika hotuba hiyo yenye maneno 5,988 iliyojaa mapitio ya mambo mbalimbali ya mwaka 2014, Rais Kikwete alisema wakati Rais wa awamu ya tano akitoa zake za kwanza za mwaka mpya, yeye atakuwa raia wa kawaida na itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa.
Sanjari na hayo, Rais aliwaagiza viongozi wa Serikali wanaowawekea vikwazo wafanyabiashara wanaouza mazao nchi za nje kuacha vitendo hivyo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kutimiza azma yao.
Alisema uzalishaji mazao mwaka huu umeongezeka hadi tani milioni 16.2 ukilinganisha na tani milioni 14.38 za mwaka 2013 na kwamba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) si mnunuzi wa mazao yote hayo, hivyo mengine yatanunuliwa na wafanyabishara wanaotakiwa kushawishiwa kuyanunua kwa wingi.
“Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo,” alisema Rais Kikwete. Aliwataka Watanzania kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwani kushindwa kufanya hivyo kutawanyima fursa ya kupiga kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa pamoja na Uchaguzi Mkuu.

Zitto: Nitamuunga mkono Mbowe

Mtwara. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amesema atamuunga mkono Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe pale atakapowasilisha hoja yake bungeni kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh1 trilioni katika mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Zitto aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa mkoani hapa uliandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF) kuwashukuru wakazi wa mkoa huo kwa kuwachagua viongozi wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Najua bado mnalia kuhusu bomba la kupeleka gesi Dar es Salaam, machozi yenu yatafutika kwani tayari habari za ufisadi mkubwa katika ujenzi wa bomba hili zimeanza kuchomoza.
“Kiongozi wa Upinzani Bungeni (Mbowe) ametamka mara kadhaa kuwa atatoa hoja kuhusu ufisadi katika ujenzi wa bomba la gesi. Pale atakapohitaji msaada wetu tutamsaidia, tunaamini gharama za mradi huu zimezidishwa mara mbili na inawezekana kabisa kuwa zaidi ya Dola ya Marekani 600 milioni (zaidi ya Sh1 trilioni) zimegawanywa kwa watu kama rushwa kuanzia China mpaka hapa Tanzania. Machozi yenu wana Mtwara yatafutwa kwa uwezo wa Mola,” alisema Zitto.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Mtwara umechukua sura mpya kitaifa baada ya kugunduliwa kwa gesi na wao (wananchi) wameonyesha kwamba wakiamua wanaweza kupigania masilahi ya Taifa.
“Mmesimama kidete kuhakikisha utajiri huu hauporwi na haturudii makosa yaliyofanyika Kanda ya Ziwa pale tuliporuhusu madini kuporwa na mabeberu wa kimagharibi,” alisema.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwahutubia wakazi hao, aliwataka viongozi wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa kuongoza kwa misingi ya chama ya haki sawa kwa wote.
“Profesa Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter) hana uwezo wa kuendelea kuwapo madarakani na hapaswi kufumbiwa macho, wote waliohusika na sakata hili lazima wachukuliwe hatua,” alisema.
Kuhusu uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura alisema, “watakapokuja kuwaandikisha jitokezeni hiyo ndiyo njia pekee ya kutafuta ukombozi wa pili wa Taifa hili lakini msipofanya hivyo hatutawaondoa hawa CCM.”
Mapokezi yalivyokuwa
Pilika pilika za mapokezi ya viongozi hao zilianza tangu asubuhi na ilipofika saa 5.20 zaidi ya magari 40 yaliyopambwa kwa bendera za CUF, pikipiki 300 na bajaji 30 zilikusanyika katika daraja la Mikindani kuwapokea viongozi hao.
Wakiwa wamevalia sare za chama chao, wafuasi hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali ukiwamo wa “Tunataka fedha zetu za escrow zirudi... mtumbwi wa Chenge umetoboka.’
ACT wapata kipigo
Wanachama wa chama kipya cha ACT-Tanzania waliosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara wakitumia basi dogo aina ya Coaster walikumbana na kipigo kutoka kwa wafuasi wa CUF waliowazuia wakidai kuwa hawakualikwa.
Mmoja wa wanachama wa ACT ambaye pia ni Mwenyeji wa Mkoa Kigoma anayeishi Dar es Salaam, Monalisa Ndala alisema; “Tuliambiwa huu mkutano siyo wa kwetu na ACT hawahusiki, ndipo walianza kutupiga wakitutaka kuvua sare kama tunataka kuendelea na msafara.”

Vita ya urais yashika kasi mtandaoni

Dar es Salaam. Wakati safari ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ikipamba moto, kumeibuka makundi ya watu yaliyofungia akaunti katika mitandao ya kijamii yakiwaunga mkono baadhi ya wanasiasa waliotangaza au wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea urais ya kuwashambulia washindani wao.
Kila kundi limejipatia wafuasi wengi ambao wanaonyesha kumkubali mwanasiasa husika wanayedhani anafaa kuwa rais wa Tanzania endapo atapitishwa na chama chake na kupigiwa kura na wananchi.
Hata hivyo, wasomi na wachambuzi wanaonya kuwa pamoja na njia hii kuwa ya haraka kuwafikia wapigakura walio wengi ambao ni vijana na wanawake, inatakiwa kutumika kwa uangalifu la sivyo inaweza kusababisha machafuko.
Makundi yenyewe
Makundi hayo, mengi yakipatikana katika mitandao ya Facebook, Twitter na WhatsApp yanafanya kazi ya kuwanadi wanasiasa na kubainisha shughuli mbalimbali wanazozifanya kila siku wawapo katika ziara zao za binafsi, za kiserikali au kichama katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi ya kurasa za makundi hayo zenye wafuasi wengi ni pamoja na ule wa ‘Team Lowassa’, kundi linalomuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambao hadi jana ulikuwa na wafuasi 46,124 ambao wanaweza kupata habari mbalimbali zinazomhusu kiongozi huyo.
Hata hivyo, mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu, hivi karibuni alikaririwa na gazeti hili akiikana moja ya akaunti za Twitter iliyokuwa imechapisha taarifa zilizomkariri akizungumzia suala la ufisadi wa escrow.
Akizungumzia kurasa hizo, Msaidizi wa Lowassa, Abubakar Liongo alisema akaunti hizo zinatengenezwa na marafiki na kusisitiza kwamba kiongozi huyo hahusiki nazo kwa namna yoyote.
“Hawa ni marafiki tu, huwezi kuwazuia kufanya wanachotaka kufanya, sisi tumeshatoa taarifa kuwa hizi hatuhusiki nazo,” alisema Liongo.
Kundi jingine linajitambulisha kama ‘Team Hamis Kigwangalla’ linalomuunga mkono Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla na mpaka kufikia jana lilikuwa na wafuasi 9,893. Hili ni kundi la pili kuwa na wafuasi wengi katika mtandao wa Facebook baada ya lile la Team Lowassa.
Ukurasa mwingine umeanzishwa na watu wanaomuunga mkono Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba. Ukurasa huu umepewa jina ‘January Makamba – The next President’ na hadi jana ulikuwa na wafuasi 7,075.
Wanasiasa wengine wanaohusishwa na mitandao hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye mbali na akaunti yake kwenye WhatsApp, ukurasa wa marafiki zake kwenye Facebook wenye jina la ‘Bernard Membe Fans Page’ umefikisha wafuasi 5,120.
Kundi la wafuasi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa linafuatia. Kundi hilo lililoanzisha mtandao uliopewa jina ‘Dr Slaa Team Winner – 2013/2015’ hadi jana lilikuwa na wafuasi 4,337.
Vilevile, lipo kundi jingine linalomuunga mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na ambalo ukurasa wake uitwao ‘Wasira wa Watanzania (WWW)’ lina wafuasi 3,524.
Pia upo ukurasa wa “Marafiki wa Samwel Sitta’ katika Facebook wenye mashabiki 2,238 wanaomuunga mkono Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Katika mtandao wa Twitter, wanasiasa hao na wengine hawako nyuma, karibu kila mmoja ana akaunti binafsi huku wafuasi wao wakipata nafasi ya kusoma yale wanayoyaandika wakati wowote.
Miongoni mwa wanasiasa wenye wafuasi wengi ni Zitto Kabwe ambaye watu 208,294 wanafuatilia hoja zake na wakati mwingine kujibizana.
Anayefuata ni Makamba mwenye wafuasi 151,822, Bernard Membe (45,889) na Dk Slaa (40,830). Lazaro Nyalandu aliyetangaza wiki iliyopita kuingia katika mbio za kusaka urais, akaunti yake ya Twitter inafuatiliwa na watu 36,726.
Wengine katika mkondo huo ni Dk Khamis Kigwangalla (26,322), William Ngeleja (11,110), Anna Tibaijuka (8,053), Freeman Mbowe (4,162), Asha-rose Migiro (4,736), Edward Lowassa (2,123), Stephen Wasira (750) na Dk Emmanuel Nchimbi (515).
Ni dhahiri kuwa wanasiasa vijana ndiyo wanaotumia zaidi mitandao ya kijamii na kuwa na wafuasi wengi ambao wengi wao pia ni vijana.
Maoni ya wachambuzi
Baadhi ya wasomi nchini wameelezea kuwa si jambo baya kutumia mitandao ya kijamii kujinadi kwa wananchi. Hata hivyo, wameonyesha wasiwasi kwa jinsi inavyotumika na kuwa inaweza kusababisha machafuko.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kadri muda unavyokwenda, ndivyo jamii inavyobadilika na mabadiliko haya yanahusisha pia matumizi ya mitandao ya kijamii.
Salim alisema vijana na wanawake ambao ndiyo idadi kubwa ya wapiga kura, sasa wanatumia mitandao ya kijamii. Alisisitiza kuwa hii ndiyo sababu pekee iliyowasukuma wanasiasa kuanza kutumia mitandao ya kijamii.
“Mitandao hii inawasaidia wanasiasa kujitangaza kwa wananchi, pia haina gharama kwao. Tulizoea kuona wanasiasa wakipita mitaani kutoa zawadi na kujinadi kwa wananchi kipindi cha uchaguzi, sasa ni rahisi,” alisema.
Hata hivyo, Salim alionya kuwa mitandao ya kijamii isipodhibitiwa kikamilifu, inaweza kusababisha machafuko ya kisiasa kama ilivyotokea katika nchi za Tunisia na Libya na kusababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yanaendelea mpaka sasa.
“Tuliona pia wakati wa sakata la escrow, watu walianza kuunda baraza la mawaziri mtandaoni kabla hata Rais hajasema chochote. Sasa hii ni hatari, wakati mwingine inaweza kujenga chuki,” alisema.
Alisema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni, Ukawa hawakutumia nguvu kubwa kwa sababu walishajenga ngome kwenye mitandao ya kijamii.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema sasa hivi mitandao ya kijamii ni sehemu ya maisha ya Watanzania. Hivyo, inakuwa rahisi kwa wanasiasa kuwafikia wengi ndani ya muda mfupi kwa njia hiyo.
Alisema uzuri wa mitandao ya kijamii ni kuwa wanasiasa wanapata nafasi ya kujitangaza na wananchi pia wanapata kuwafahamu na kuwapima kama wanaweza kuongoza Taifa hili.
Aliuangana na Salim akisema kuwa Tanzania haina udhibiti mzuri wa mitandao ya kijamii, jambo linaloweza kusababisha chuki na mifarakano miongoni mwa wanajamii.
“Si kila linaloanzishwa ni jema asilimia 100, wengine wanatumia mitandao ya kijamii kuwachafua wengine, hasa mahasimu wao kisiasa,” alisema Mbunda na kuitaka Serikali kuwa na udhibiti wa mitandao hiyo hasa wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu.