Habari za michezo

Kesi ya ngono ya Benzema, Ribery kuanza kusikilizwa

PARIS, UFARANSA
KESI ya ngono inayowakabili mastaa wawili wa timu ya taifa ya Ufaransa, Franck Ribery wa Bayern Munich na Karim Benzema wa Real Madrid inatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa jijini Paris.
Nyota hao wanakabiliwa na kesi ya kufanya ngono na mrembo, Zahia Dehar ambaye wakati wakifanya naye ngono zembe hiyo alikuwa na chini ya umri wa miaka 18 kitu ambacho ni kinyume na sheria za Ufaransa.
Wote wawili, Ribery, 30,  na Benzema, 26, wamedai kwamba hawakuwa na habari kwamba wakati wanafanya ngono na msichana huyo alikuwa na umri chini ya miaka 18. Kutokana na kosa hilo, kuna uwezekano mkubwa wakafungwa jela miaka mitatu na faini ya Euro 45,000 juu.
Hakuna yoyote kati yao ambaye anatazamiwa kuhudhuria kesi hiyo, hii ni kwa mujibu wa Mwanasheria wa Ribery. Hata Zahia pia hatazamiwi kuwepo mahakamani hapo na badala yake atawakilishwa na Mwanasheria wake.
Wakati mwanasheria wa Ribery, Carlo Alberto Brusa akijigamba kwamba wana uwezo mkubwa wa kushinda kesi hiyo, Mwanasheria wa Zahia, Daniel Vaconsin amedai kwamba mteja wake hadai lolote katika kesi hiyo zaidi ya heshima yake.
Wakati ngono hiyo ikifanyika kati ya Zahia na Benzema, mrembo huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu, na wakati mrembo huyo alipofanya ngono na Ribery, mrembo huyo alikuwa na umri wa miaka 17.
Umri ambao binti anaruhusiwa kufanya ngono kwa hiyari nchini Ufaransa ni miaka 15, lakini kwa kuifanya ngono hiyo kwa malipo ni kinyume kabisa ya sheria kama akina Ribery walivyofanya.
Kesi hiyo itasikilizwa baada ya Mahakama Kuu ya Ufaransa kutoa shauri kuwa kesi yoyote ya Malaya aliye chini ya umri wa miaka 18 ni uvunjaji mkubwa wa sheria za nchi.
Shemeji wa Ribery pia anahusika katika kesi hiyo kwa kosa ya kusaidia kufanyika kwa ngono hiyo, na watu wengine watano wanahusika katika hukumu ambayo wanaweza kufungwa kwa miaka 10 kutokana na mashtaka yaliyopo.
Ribery amekiri kufanya ngono na Zahia baada ya Mrembo huyo kupaa na ndege mpaka jijini Munich mwaka 2009 akifanywa kama zawadi kwa Ribery kwa kutimiza miaka 26, lakini Ribery anajitetea kwa kudai kwamba hakujua kuwa Zahia alikuwa na umri chini ya miaka 18 wakati huo.
Mapema wiki hii, vyombo vya habari vya Ulaya vilikuwa na habari za ndani jinsi Zahia, ambaye ni mzaliwa wa Algeria alivyokuwa anafanya biashara ya ngono kwa malipo ya Pauni 1,740 kwa siku huku akijishughulisha zaidi na wachezaji wenye majina makubwa nchini Ufaransa.
Katika mahojiano yake na gazeti moja la Paris, Zahia anaelezea jinsi alivyotumiwa tiketi na kupaa mpaka Munich April mwaka huo kwa ajili ya kumpa ngono Ribery aliyekuwa anatimiza miaka 26.
“Nilikuwa kwa ndege nikiwa na mmoja wa rafiki zangu ambaye nadhani Ribery alimtuma kwangu. Alichukua chumba katika hoteli moja ya kifahari. Tulifanya ngono na alinilipwa. Eti mimi nilikuwa zawadi ya sikukuu ya kuzaliwa kwake.” Alisema Zahia.
Hata hivyo, kwa kutazama picha zake kupitia magazeti, Zahia alionekana kuwa mkubwa kuliko miaka yake. Lakini bado kuna swali lenye utata kuhusu nani alimkatia tiketi yake ya ndege kwenda Munich ukizingatia kwamba alipaswa kutoa taarifa zake muhimu ikiwemo tarahe yake ya kuzaliwa.
Benzema ambaye anashutumiwa kufanya ngono na mrembo huyo katika hoteli maarufu ya Paris, amekanusha kabisa kama aliwahi kupanda kitandani na mrembo huyo.
Zahia anasisitiza kwamba hakumwambia yoyote kati ya Ribery na Benzema kuhusu umri wake, ingawa pia anakiri kuwa na Benzema naye alilipia huduma yake ya ngono. Hata hivyo Benzema ameendelea kusisitiza kwamba mwanasheria wake kwamba hakufanya jambo lolote baya na mrembo huyo.
Nyota mwingine ambaye ameingia katika kashfa hiyo ya ngono ni staa wa zamani wa Lyon na timu ya taifa ya Ufaransa, Sidney Govou, ambaye hata hivyo amenusurika kwa sababu imethibitika kuwa alifanya ngono na Zahia wakati mrembo huyo akiwa na umri wa miaka 18.
Kwa mujibu wa ripoti za polisi, umalaya wa Zahia ni tatizo kubwa la umalaya wa kisasa linaloendelea katika jiji la Paris. Kutokana na polisi kuzuia tatizo hilo, huku matumizi ya mitandao ya kijamii yakiongezeka, umalaya wa Zahia ni aina mpya ya mtandao wa ngono ambao ni ngumu kuzuilika.
Wengi kati ya wanaofanya biashara hiyo mpya jijini wanafunzi na wanasoka mahiri wamekuwa walengwa wakubwa kutokana na kipato kizuri wanachoingiza katika soka huku pia umaarufu wao ukileta mvuto.
Kutokana na kashfa hiyo, umaarufu wa Zahia ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 21 umeongezeka kwa kiasi kikubwa na ameingia mkataba katika kampuni ya Lagerfeld huku akiwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki kutokana na ngono yake zembe kwa Ribery na Benzema.
 Hata hivyo, kesi hiyo ilimkera vilivyo Waziri wa michezo wa Ufaransa, Rama yade ambaye alikaririwa akidai kwamba wachezaji hao walikuwa hawastahili kuvaa tena jezi ya timu ya taifa ya Ufaransa.
“Jezi ya timu ya taifa ya Ufaransa imebarikiwa. Haipaswi kuvaliwa na mtu ambaye anachunguzwa na vyombo vya dola,”  alisema Yade.
Hata hivyo, kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps amedai kwamba suala hilo lipo katika mikono ya sheria na haliwezi kuwaathiri wachezaji hao au timu ya taifa ya Ufaransa.
Bahati nzuri kwa Ribery ni kwamba walau ametetewa vizuri na mkewe wake, Wahiba Ribery ambaye kwa sasa amesimama upande wake. Wawili hao wana watoto watatu ambao ni Hizya aliyezaliwa mwaka 2005, Shaninez aliyezaliwa Januari 2008 na Seif aliyezaliwa Septemba 2011. Ribery amesilimua na jina analotumia ni Bilal Yusuf Mohammed.
Haijaeleweka mambo yatakwenda vipi kwa Benzema ambaye yupo katika uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na mrembo, Sarah Williams lakini haitazamiwi kama penzi lao linaweza kuwa imara kama ilivyozoeleka.
Wawili hao wamekuwa katika penzi zito tangu wakati nyota huyo akikipiga katika klabu ya Lyon ya Ufaransa.


Wachovu Manchester United kujiuliza kwa Sunderland leo
 London, England. Manchester United wanatakiwa kusahau mwendo wao mbovu katika mbio za ubingwa wa ligi, lakini kocha David Moyes anatakiwa kuhakikisha wanamaliza msimu wakiwa hata na kombe moja la ndani.
Jumapili United walipokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Chelsea na kuifanya nafasi yao kuwa finyu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na kufungwa na Swansea City katika Kombe la FA ni wazi taji pekee lililobaki kwa United msimu huu England ni Kombe la Ligi.
Leo watacheza na Sunderland katika mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa kwanza kufungwa 2-1 kwenye Uwanja wa Light, na mshindi wa mechi hiyo atafuzu kwa fainali ambayo itakuwa dhidi ya Manchester City mwezi Machi.
Kipigo cha Chelsea ni mwendelezo wa matokeo mbaya wa Man United ambayo kwa sasa ipo nafasi ya saba katika ligi wakiwa nyuma kwa pointi 14, pia wameachwa kwa pointi sita katika kuifikia nafasi ya nne ambayo itawawezesha kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Japokuwa mashabiki wa United bado wanaendelea kuumunga mkono Moyes katika kila matokeo mabaya ya timu hiyo, Mscoti huyo aliyechukua mikoba ya Alex Ferguson msimu huu, alisema uchezaji wao mzuri nyumbani ni kutokana na kuhofia kuzomewa.
“Tutahakikisha tunafanya kila tuwezalo tunapata matokeo mazuri,” aliimbia (www.manutd.com) baada ya kufungwa na Chelsea ikiwa ni mechi ya saba kufungwa kati ya 22 za ligi walizocheza.
United imekuwa kwenye wakati mgumu tangu kuumia kwa washambuliaji wake Robin van Persie na Wayne Rooney, pamoja na chipukizi mwenye miaka 18, Adnan Januzaj wachezaji wengine wameshindwa kuziba pengo hilo.
Sunderland ilipata ushindi katika mchezo wa kwanza kwa bao la mkwaju wa penalti wa Fabio Borini  na kushinda 2-1, pia vijana hao wa Gus Poyet waliamka kutoka kufungwa mbili  na kusawazisha 2-2 dhidi Southampton Jumamosi iliyopita.
Kiungo Craig Gardner alisema sare hiyo imewasaidia katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wa leo.
“Kila mechi ni muhimu kwetu kwa sasa, tupo katika nusu fainali, lengo letu ni kusonga mbele, japokuwa tunategemea kupata upinzani mkubwa Old Trafford,” aliimbia tuvuti ya Sunderland (www.safc.com).


Ligi kuu England
Mabingwa watetezi Manchester United wataanza kutetea taji lao ugenini kwa kuifuata Swansea City ikiwa ni mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu chini ya kocha mpya David Moyes huku Manuel Pellegrini ataiongoza Manchester  City wakiwa nyumbani dhidi ya Newcastle United hapo Agosti 17.
Ratiba hiyo ya Ligi Kuu ya England iliyotangazwa jana  pia itashudia Hull City iliyopanda daraja wakimkaribisha Jose Mourinho kwa mara ya nyingine Chelsea. Roberto Martinez, mni moja wa makocha watatu bora waliofanya uhamisho wao msimu uliopita ataiongoza Everton kuivaa Norwich City siku hiuyo.
Huku timu iliyopanda daraja ya Cardiff City watakuiwa wageni wa West Ham United na Crystal Palace wataijaribu Tottenham Hotspur.
Msimu huu inatarajiwa kuwa na ushindani tofauti kwa sababu timu tatu zilizoshika nafasi tatu za juu msimu  uliopita hivi sasa zipo chini ya makocha wapya ambao wanatarajiwa kuleta staili mpya ya uchezaji katika klabu zao.
Timu hizo tatu zilizoshika nafasi tatu za juu msimu uliopita katika Ligi Kuu ya England ni Manchester United, Manchester City na Chelsea, ambazpo zinatarajiwa kupata ushindani kutoka kwa klabu kama Tottenham na Arsenal.
Baada ya kocha Alex Ferguson kustaafu kuifundisha Manchester United, kocha mpya wa klabu hiyo David Moyes ataanza kibarua cha msimu mpya wa Ligi Kuu England wa 2013/14 kwa mechi ya ugenini dhidi ya Swansea.
Mechi tano za kwanza za Moyes akiwa anainoa Manchester United ni Agosti 17 dhidi ya Swansea (ugenini), Agosti 24 dhidi ya Chelsea (nyumbani), Agosti  31 dhidi ya Liverpool (ugenini), Septemba 14 dhidi ya Crystal Palace (nyumbani) na Septemba 21 dhidi ya Manchester City (ugenini).
Katika ratiba ya ligi hiyo iliyotangazwa jana inaonyesha kuwa Ligi Kuu ya England itaanza Agosti 17, ambapo kocha Jose Mourinho aliyerejea Chelsea ataanza kwa mechi ya nyumbani dhidi ya Hull City.
Naye kocha mpya wa Manchester City, Manuel Pellegrini atakabiliana na Newcastle kwenye Uwanja wa Etihad. Timu zilizopandishwa daraja, Cardiff  itasafiri kuifuata West Ham wakati Crystal Palace itaikaribisha Tottenham.
Kocha mpya wa Everton, Roberto Martinez ataiongoza timu yake kwenda kucheza na Norwich katika wikiendi ya ufunguzi wakati Liverpool itakuwa mwenyeji wa Stoke City.  
Arsenal imepangwa kuanzia nyumbani dhidi ya Aston Villa, wakati Sunderland itaikaribisha Fulham na Southampton itaifuata West Brom. Msimu huo utamalizika Mei 11 mwakani kwa Manchester  United kuifuata Southampton, Chelsea itakuwa wageni  wa Cardiff, Arsenal itakaribishwa na Norwich wakati Manchester City itakuwa mwenyeji wa West Ham.
Mechi za washindani wa jadi ni kama ifuatavyo: Arsenal vs Tottenham: Agosti 31 Tottenham vs Arsenal: Machi 15 Manchester City vs Manchester United: Sept 21 Everton vs Liverpool: Novemba 23 Sunderland vs Newcastle: Oktoba 26 Cardiff vs Swansea: Novemba 2.


Emma Okwi kuuzwa Ulaya

Dar es Salaam. Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia inatarajia kumpiga bei mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi kabla hata haijamaliza malipo ya deni la kumnunua mchezaji huyo raia wa Uganda kutoka Simba ya Dar es Salaam.
Okwi, aliyenunuliwa na Simba kutoka Sports Club Villa ya Uganda mwaka 2010 kwa ada ya uhamisho ya Dola 40,000, anatarajiwa kuuzwa klabu ya FK Partizan ya nchini Serbia.
FK Partizan inayocheza Ligi Kuu, maarufu kama SuperLiga inashika nafasi ya pili kwa ukubwa na mafanikio ya jumla, kiuchumi na uwanjani Serbia tangu ilipoanzishwa mwaka 1945.
Taarifa za klabu ya Etoile du Sahel kumuuza Okwi aliyecheza kwa mafanikio Msimbazi, zilithibitishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope.
“Ni kweli, Okwi anaweza kuuzwa Ulaya na sisi hatuna namna ya kumzuia hata kama bado Etoile du Sahel haijatulipa pesa za kumnunua kutoka kwetu,” alisema Hanspope.
Pope alisema kama hatua ya kuuzwa mchezaji huo itatimia, basi itakuwa neema kwao kwani makubaliano yanaonyesha, kama ikitokea klabu hiyo ya Tunisia ikamuuza Okwi, basi Simba itapata asilimia 25 ya mauzo.
Hanspope pia alisema kuwa, kama Okwi atauzwa basi maana yake klabu hiyo ya Tunisia italipa pesa mara moja wanazodaiwa za kumnunua mchezaji huyo mwaka jana, ambazo Sh450 milioni.
“Makubaliano yetu ya kuuzwa Okwi ni kwamba, klabu hiyo ya Tunisia itatulipa pesa kwa awamu, lakini kama itatokea na wao wakamuuza basi pesa zetu tutalipwa mara moja,” alifafanua Hanspope.
Okwi alionyesha kiwango kizuri kilichowavutia kocha wa klabu hiyo ya Serbia, Vuk Rasovic na Mkurugenzi wake Albert Nagy wakati akiichezea Uganda dhidi ya Angola katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka.
Taarifa zilizopatikana kwenye tovuti, zimeeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yameshaanza na yanasimamiwa kwa karibu na Kocha wa Timu ya Taifa ya Uganda, Sredojevich ‘Micho’ Milutin.
Mbali na Simba pia timu yake ya Sports Club Villa ya Uganda itanufaika na mgawo huo wa mauzo ya Okwi kutokana na kukuza kipaji chake toka akiwa mchezaji chipukizi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alipoulizwa alisema hana pingamizi lolote la kuuzwa kwa mshambuliaji huyo zaidi ya kupaswa kulipwa fedha zao kihahali kwa mujibu wa kanuni.
 Klabu hiyo iliwauza nyota wake wawili, Mbwana Samatta na Patrick Ochan kwenda klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa thamani ya dola 150,000 kila mmoja sawa na Sh240 milioni.

TFF kuivunja Taifa Stars

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema litaivunja Timu ya Taifa (Taifa Stars) mpaka Novemba mwaka 2014 iwapo itaondolewa na Uganda katika machi ya marudiano kusaka tiketi ya kucheza michuano ya CHAN mwakani.
Mwanza. Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Saad Kawemba amesema iwapo Timu ya Taifa (Taifa Stars) itafungwa katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes), timu hiyo itavunjwa mpaka Novemba 2014.
Stars inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN). Katika mchezo wa kwanza Stars ililala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa.
Akizungumza katika hafla ya mlo wa jioni iliyoandaliwa na Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) juzi, Kawemba alisema hakutakuwa na sababu ya kuwa na timu ambayo haishiriki mashindano makubwa ya kimataifa, hivyo amewataka wachezaji kuhakikisha wanashinda mchezo wa marudiano.
“Sababu ya kuja kuweka kambi Mwanza ni kuhakikisha tunashinda mchezo wetu wa marudiano dhidi ya Uganda. Mwaka jana timu ilipoweka kambi hapa Mwanza, ilikwenda Kampala na kushinda mechi tatu kwenye michuano ya Chalenji iliyofanyika Uganda,” alisema Kawemba.
“Tupo Mwanza kwa sababu tunakwenda kucheza Kampala Julai 27, mwaka jana wakati wa Chalenji tuliweka kambi hapa na tulipotoka tulifika Kampala na kushinda mechi tatu mfululizo, sasa kama tupo Mwanza tena ni kwa nini tusiende kushinda mechi hii.”
Kawemba alisema ni jukumu la wachezaji kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kupata fursa ya kushiriki mashindano makubwa Afrika mwakani.
“Naamini timu yetu nzuri na inaweza kushinda mechi ya marudiano. Wachezaji hampaswi kuvunjika moyo na mashabiki kwa kufungwa mchezo wa kwanza. Mashabiki siku zote wanataka ushindi na siyo kufungwa,” alisema zaidi.
“Mashabiki ni watu wa kulaumu sana, wanataka timu ifanye vizuri na matokeo yanapokuwa kinyume chake wanakasirika,” alisema Kawemba na kuongeza:
“Wametusema viongozi kwamba tumeisahau timu na kuweka mkazo zaidi kwenye uchaguzi wa TFF. Hakuna ukweli kwenye jambo hili, TFF imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye mashindano.”
Kwa upande wake Meneja wa Kanda wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Malaki Sitaki alisema wadhamini hujisikia raha timu inapofanya vizuri kwenye mashindano.
“Imani yetu ni kuwa tunayo timu bora, nzuri na mategemeo yetu ni kushinda hata kwao. Kama walitufunga nyumbani, kwa nini na sisi tusiwafunge kwao?” alihoji Sitaki.

No comments: