Historia yake
Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama
kipya cha siasa, ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23, 1959 katika
hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao
Manispaa ya Singida Mjini. (Januari mwaka huu alitimiza miaka 56).
Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa
Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo
na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa, akiwamo Anna.
Mgwira alianza safari ya kielimu katika Shule ya
Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea na sekondari kwenye
Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha
masomo ya juu ya sekondari (kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary
kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea na masomo ya chuo kikuu mwaka 1982
baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Thiolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na
kuhitimu Shahada ya Thiolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea shahada ya Sheria.
Kati ya mwaka 1987 – 1998, aliendelea na shughuli
za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu
mkubwa.
Safari ya elimu ya Mghwira ilikamilikia Chuo Kikuu
cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM)
mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia
aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu
katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya
kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala
ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Mghwira ana historia ya kupenda siasa, masuala ya
jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko
yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Alianza siasa tangu wakati wa Tanu akiwa
mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi
kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika Tanu lakini
baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika
masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na siasa
hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi
mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake ngazi ya wilaya na katibu
wa baraza la wanawake mkoa.
Machi mwaka huu alijiunga rasmi na ACT – Wazalendo na katika
Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Kwanza wa ACT.
Aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na
walibahatika kupata watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mumewe hivi sasa ni marehemu.
Mbio za ubunge
Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara
ya kwanza Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo
cha Solomon Sumari.
Alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema
akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo, chama hicho kilimpitisha Joshua
Nassari (Josh) na Mghwira alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono
hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Mbio za urais
Mghwira hajatangaza kuwa atagombea urais. Ila,
tafiti kadhaa na maoni ya Watanzania zinaonyesha kuwa yeye ni miongoni
mwa viongozi wa kisiasa ambao wamejipambanua hivi karibuni na kuonyesha
uwezo mkubwa katika uwanja wa kisiasa na hivyo anapewa nafasi kubwa kuwa
anaweza kupewa majukumu makubwa na anaweza kuyahimili.
Nguvu yake
Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni
umahiri katika elimu. Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini
ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa
nyingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake. Kwa nchi kama
Tanzania ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu,
Mghwira anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.
Kwa sababu Mghwira ni mwanamke imara na
anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni
baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali
na kutafuta mchango wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, kijamii na
kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika
jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume.
Lakini nguvu ya tatu ya Mghwira ni uthubutu.
Ameniambia kuwa hata alipoingia katika ndoa bado alithubutu kujiendeleza
kielimu bila kuchoka. Alipambana na changamoto za ndoa na shule.
Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye
alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu
vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi
kubwa.
Mghwira ni mtu wa kuhoji kila jambo, si mwanamama “Ndiyo Mzee”.
Wakati natafuta maoni ya watu waliowahi kufanya naye kazi katika Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu, mtendaji mmoja aliniambia kuwa ukimpa
Mghwira kazi ya harakati iliyo kwenye maandishi, hataondoka kwako hadi
umpe taarifa za kina za kila jambo na atakuhoji hadi utachoka.
Hata mtaalamu mshauri wa chama hicho Profesa
Kitila Mkumbo ameniambia kuwa wakati wanafanya marekebisho ya katiba ya
chama cha ACT walikabidhi kazi hiyo kwa jopo maalumu la wataalamu
akiwemo Mghwira.
Profesa Kitila ananiambia kuwa kwa kiasi kikubwa
katika timu hiyo, Mghwira ndiye aliyehoji na kutoa mapendekezo ya
masuala mengi kuliko hata wataalamu wengine wa sheria ambao walikuwa
wanaume.
Nilipojaribu kumfikia Mghwira kwa ajili ya kupata
taarifa zake za kina na maisha binafsi, nilijikuta nashushiwa maswali
matano mfululizo kiasi kwamba nilirudi kujipanga na kumtafuta tena. Huyu
ni mwanasiasa wa kisasa ambaye anahoji kila jambo lililoko mbele yake,
sifa hii wanaikosa wakuu wengi wa nchi.
Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha
wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa,
Mghwira ni mwanamama wa kawaida sana. Watu wa karibu naye wanamtaja
hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda
kuandika makala za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea
na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada.
Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji
uongozi mkubwa wa nchi.
Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa nilioubaini na hata kujulishwa na
watu wa karibu naye ni kuwa yeye ni mwanasiasa mpole sana. Nimeambiwa
kuwa ni mpole kupita kiasi na mara nyingi huwa anakuwa msikilizaji mzuri
kabla hajaanza kuhoji mambo mfululizo. Moja ya sifa muhimu za Rais
ajaye ni uwezo wa kuwa mpole na mkali kutegemeana na mazingira.
Kiwango cha upole cha mwanamama huyu kinazidi
kiwango cha ukali alionao na naliona kama ni jambo linalopaswa kufanyiwa
kazi kwa sababu Taifa letu lilipofikishwa, mara kadhaa nimesisitiza
kuwa tunahitaji kiongozi anayeweza kumudu hali zote mbili.
Lakini udhaifu wa pili mkubwa wa Mghwira ni
kutojijenga kisiasa ndani ya nchi. Katika siasa, bado namuona kama
mchanga, hajakomaa na kuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kujipa jina kubwa
kwa jamii.
Mchango wake katika jamii ni mkubwa kwa sababu
amewahi kusimamia masuala mengi ya kijamii na kisheria yanayoonekana,
lakini ninachokisema hapa ni kuwa, chama chochote kile kina jukumu la
kusimamisha kiongozi ambaye anajulikana katika tasnia za siasa.
Kutojijenga na kuwa juu tokea alipokuwa Chadema nakuchukulia kama
udhaifu ambao anahitaji kuufanyia kazi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama ACT - Wazalendo kitampitisha mwanamama huyu
kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,
sababu ya kwanza ya kufanya hivyo inaweza kuwa ni ile dhana ya kumpa
mwanamke nafasi.
Chama anachotoka ndicho peke yake kimeweza kumpa mwanamke nafasi
ya juu ya uongozi, nadhani pia bado chama hicho kinaweza kumpa jukumu
kubwa zaidi ya hilo kwa sababu tayari kimeshajijengea misingi ya
kuwajenga kina mama.
Lakini ikiwa Mghwira atapitishwa, uzoefu wake
kimataifa na katika masuala ya haki za binadamu na kushughulika na
masuala ya kijamii kunaweza kuwa moja ya sababu.
Mwanamama huyu amefanya kazi mbalimbali za
kitaaluma na kijamii hapa Tanzania, Sweden, Marekani, Uingereza na nchi
nyingine za Afrika. Amekuwa mwalimu wa vyuo vikuu hapa Tanzania na
msimamizi wa miradi mbalimbali ya kitaifa ya mashirika ya ndani na nje
ya nchi. Uwezo na uelewa wake vinampa fursa ya juu ya kuteuliwa kugombea
urais na kuonyesha kuwa kina mama wanaweza ikiwa wanapewa fursa sawa na
wanaume.
Nini kinaweza kumwangusha?
Dhana ileile ya kijinsia inayombeba, pia ndiyo
inayoweza kumuangusha. Ikiwa ACT kitadhani kuwa vyama vingine washindani
vitasimamisha wagombea wanaume imara ambao wanaungwa mkono na mfumo
dume uliotawala nchi hii, chama hicho kinaweza kumuweka nje Mgwira na
kutafuta mwanachama mwingine “mwanamume” ambaye atakuwa na fursa ya
kupambana na wanaume wengine kutoka vyama vingine na kuangaliwa na jamii
“ambayo kwa kiasi kikubwa bado inatawaliwa na wanaume”.
Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha ni
ugeni wake katika masuala ya kisiasa. Kama nilivyoeleza, Mghwira hana
uzoefu wa uongozi wa juu wa kisiasa katika vyama, nadhani nafasi
aliyonayo ndani ya ACT - Wazalendo ndiyo inayompa uzoefu wa kwanza wa
siasa za kitaifa.
Lakini uzoefu wa jumla unaonyesha kuwa vyama
mbalimbali hapa Tanzania huteua wagombea urais wake miongoni mwa
wanachama wazoefu au wale waliowahi kushika madaraka muhimu katika chama
kwa muda mrefu. ACT ikipiga hesabu hizi inaweza kabisa kumuweka nje
mwanamama huyu.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Ikiwa hatapewa fursa ya kugombea urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake, anaweza kuwa na mipango
mitatu mezani:
Mpango wa kwanza ni kugombea ubunge katika jimbo
mojawapo Tanzania. Bahati nzuri nimejulishwa kuwa moja ya majimbo
anayojipanga kugombea ni pale Singida. Ikiwa ndivyo basi, mpango huu
unaweza kumfaa kwa maana ya kuzidi kujifunza na kupata uzoefu wa siasa
za Tanzania kwa upana.
Lakini mpango wa pili ni kuendelea kufundisha
vijana katika vyuo vikuu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri
kwa wanafunzi na wa kisheria katika jamii. Katika masuala haya ana
uzoefu mkubwa nayo na itakuwa tu ni kiasi cha kuendelea pale alipoishia.
Nadhani mpango wa tatu ni kuendelea kuongoza chama
cha ACT - Wazalendo. Nimeambiwa kuwa uongozi (Uenyekiti wake) unapaswa
kuisha Februari, 2020. Ikiwa ndivyo nadhani ana fursa njema ya kuendelea
kufanya uongozi.
Mgwira ni mwanasiasa na kiongozi wa chama kipya
ambacho kimeanzishwa na wanachama wengi waliotoka Chadema. Safari yake
kisiasa na hata ugombeaji wa nafasi nyingine kubwa za nchi kwa namna
moja au nyingine, lazima utaathiriwa na ustawi au uzorotaji wa Chadema.
Ikiwa Chadema kitazidi kukubalika kwa Wwatanzania
na kuwa chama kinachoimarika zaidi kuishinda ACT, ndiyo kusema kuwa yeye
na wenzake watakuwa na wakati mgumu kujipambanua kisiasa na hivi ndivyo
siasa za Afrika hutizamwa.
Pamoja na sintofahamu hizo, namuona Mgwira kama
mmoja wanasiasa watulivu na wenye maono mapana katika Taifa hili. Kwa
maneno yake yeye mwenyewe amenieleza kuwa “Natamani siku moja nchi hii
iongozwe kwa misingi ya udugu na kusaidiana, kwa misingi ya malezi ya
maadili bora kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Mimi nimekulia kwenye
familia kubwa sana lakini wazazi wetu walitulea sote kama ndugu na
tuliishi kwa furaha kubwa, nina ndoto kuwa Tanzania ijayo ipite katika
njia hiyo.”
Ninachoweza kusema kwa sasa ni kumwombea mama huyu
nguli wa upinzani na kumtakia safari njema katika nia zake za kisiasa
ikiwamo hii ambayo ametajwa kwamba ana sifa za kuongoza Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na
Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana
Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu
(Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi
(M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia
+255787536759.
No comments:
Post a Comment