Katika maisha ya kawaida, binadamu ana msimamo wake na hata uamuzi asiopenda ubadilike.
Katika medani ya siasa nchini msimamo wa Chama Cha
Mapinduzi ( CCM) kuhusu Muungano na muundo unafahamika. Ni muundo wa
kutaka Serikali mbili ambao chama hicho unakipigania kwa udi na uvumba.
Hata hivyo, msimamo huo ni kinyume na mapendekezo
au matakwa ya wengi kama ilivyoainishwa kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba
ilikusanya maoni ya wananchi na ilipendekeza muundo wa Muungano wa
Serikali tatu.
Hivi karibuni akifungua Bunge Maalumu la Katiba,
Rais Jakaya Kikwete akaunga mkono msimamo wa chama chake, jambo
lililoibua mjadala unaoendelea hadi sasa.
Hoja ya Serikali mbili
Kwanini CCM wanataka Serikali mbili na siyo tatu
au moja kama ilivyo maoni ya wananchi walio wengi kwa mujibu wa maelezo
ya Tume ya Warioba? Makala haya yanachambua hoja hiyo.
Profesa Bakar Mohammed ni Mhadhiri Mwandamizi na
Mkuu wa Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
anayesema msimamo wa CCM wa kudai Serikali mbili unatokana na hofu ya
uhafidhina wa kuogopa mabadiliko.
Anasema viongozi wengi wa CCM wanasumbuliwa na
hofu na woga wa mabadiliko na kwamba wanakuwa wagumu kuyakubali
yanapotaka kutokea.
“Kama mtu unaangalia madaraka zaidi, lazima
kunakuwa na woga, na hii ni hulka ya binadamu kuwa na woga wa kuacha
kile ulichokizoea… Lakini ukiangalia masilahi ya nchi na kuacha yale
yanayokusukuma kusingekuwa na wasiwasi huu unaoonekana sasa,” anasema.
Anasema CCM inachofanya ni kuhakikisha haking’oki
madarakani, huku viongozi wake wakiamini kuwa wana sifa za kuongoza na
siyo wengineo.
Profesa Bakari anailinganisha hofu ya sasa ya CCM
na ile waliyokuwa nayo viongozi wa chama hicho miaka ya 1990 zilipoanza
vuguvugu za mabadiliko ya siasa za vyama vingi. Anasema CCM kiliendesha
propaganda kuwa mfumo wa vyama vingi haukuwa na tija na ungeleta vita.
Hofu hiyo anasema ndiyo inayokifanya chama hicho kikongwe kuhofia kung’olewa madarakani.
“Woga huo bado upo, wanaogopa pengine mfumo ukiwa
wa Serikali tatu uwezekano wa wao kubaki madarakani utakuwa mdogo,”
anafafanua.
Anaongeza kusema kuwa hofu ya CCM siyo kwa ajili ya masilahi ya nchi, badala yake inaonekana chama kinaangalia masilahi yake.
Ingekuwa vyema anasema kwa CCM kueleza madhara yanayoweza kulikumba taifa ikiwa muundo wa Serikali tatu utapita.
“Wanatoa hoja kuwa mfumo wa Serikali tatu unaweza
kusambaratisha nchi, lakini hakuna uhakika kama mfumo huu uliopo nchi
hauwezi kusambaratika,” anasema.
Hofu ya kuyumba na kuanguka
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk. Benson Bana
anasema siri ya CCM kung’ang’ania Serikali mbili inatokana na hofu ya
kuyumba na kuanguka.
Anasema CCM kimekuwa madarakani na mfumo huo kwa
miaka 50 na kwamba hofu yao ni kuwa ukiondoa Serikali mbili kinaweza
kuyumba na kuachia madaraka.
Anasema misingi ya wanasiasa ni madaraka, na kwamba ukishayapata, huwezi kuyaachia kirahisi.
“Misingi ya wanasiasa ni madaraka… Kuyalinda,
kuyahifadhi na kuyatumia madaraka yale kwa namna yoyote…Huwezi kuyaachia
madaraka kirahisi. Utafanya ujanja, utatumia mbinu chafu ili tu
kuhakikisha unabaki madarakani, na hiki ndicho wanachofanya CCM,”
anasema.
Dk. Bana anasema CCM kingeeleweka na kingekuwa na mwonekano mzuri zaidi endapo wangepigania kuwapo kwa Serikali moja.
“Wangekuwa wanataka muungano imara, endelevu na
uliokomaa wangeelekeza katika Serikali moja…Lakini hawataki kwa sababu
wanajua moja inaweza ikawanyima uongozi,” anasema.
Dk. Bana anasema ni vyema wananchi wakaelimishwa huu muungano
una faida gani na wanafunzi shuleni katika elimu ya uraia waelezwe faida
zake.
“Ingekuwa wazi tungejua nani anafaidika na nini,
mikopo misaada, nani anachangia nini…Je zile sababu za waasisi za
kuungana bado zipo sasa miaka 50 ya Muungano, ule woga kuwa Zanzibar
itamezwa bado upo leo?” Anahoji.
Anaongeza kuwa ni vyema kwa watawala kutazama
mazingira ya sasa ya siasa zetu kwa kile anachoeleza kuwa hata Katiba
ikipita ikakubali kuwapo wa Serikali mbili, bado wananchi watahoji
mantiki ya muundo huo.
Msomi mwingine wa siasa, Dk. Alexander Makuliko
anasema hofu ya CCM ni kuwa ndio iliyouasisi Muungano wa Serikali mbili,
hivyo isingependa hali hiyo ibadilike.
Anaendelea kusema kuwa CCM imezoea mfumo huu na
kuwa ikiukosa itaathirika, kwakuwa ni sera yake na imekuwa ikiitekeleza,
lakini msimamo wa wananchi ndiyo kitu cha msingi kuzingatiwa. Hoja
zijengwe na zisikilizwe, ubabe hautakiwi, busara inahitajika zaidi.
Anasema pamoja na suala la Serikali mbili kuwa
ni pimajoto ya uhai wa CCM, hata hivyo hoja zinazotolewa katika
kutetea msimamo wao ni nzuri tu na zinazoeleweka vyema.
“Sioni kama wanang’ang’ania, lakini ukweli ni kuwa
kila chama kina sera yake, na CCM kimeweka sera yake katika suala la
Muungano wao wanasema ni Serikali mbili, na siyo tatu…kwamba tatu
zitaongeza gharama na mengineyo, ni sababu za msingi kabisa,” anasema.
Anaongeza kuwa hoja zinazotolewa na chama tawala
ni kubwa na siyo za kupuuzwa, lakini vilevile kero zinazotajwa kuhusu
mfumo wa Muungano uliopo nazo zipo na zinaweza kutatuliwa katika mfumo
uliopo.
“Unajua hivi vyama kila kimoja kinataka kuvutia
kwake, hata bila rasimu ya Warioba…Ninashauri walete hoja, kisha watu
wazipime hizo hoja, kwanini serikali mbili, na wale wa tatu tayari
wameleta hoja na ushahidi, watu waachwe wapime,” anasema na kuongeza:
‘’Jambo la msingi kuzingatiwa ni kuwa mawazo ya
wananchi wengi yataonekana wakati wa kura za maoni. Angalizo ni
kuhakikisha kuwa kura hiyo isije ikachakachuliwa.’’