Friday 18 October 2013

Wasomi watoa tahadhari majadiliano ya JK, wapinzani

Dar es Salaam. Wasomi wameonyesha wasiwasi wao juu ya mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya siasa vya upinzani vyenye wabunge, kuhusu tofauti zilizojitokeza katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Wasomi hao licha ya kuunga mkono mazungumzo, wamesema wanasiasa wana kawaida ya kuwa na agenda za siri jambo ambalo baadaye huzusha tena mzozo, huku wakirejea kwamba si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kufanya mkutano wa aina hiyo.
Kauli hizo zimetokana na Rais Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa; CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, TLP na UDP kukubaliana kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Azavery Lwaitama alisema uamuzi wa Rais Kikwete ni mzuri lakini unaweza ukawa umechezwa kwa karata ya kisiasa.
Alifafanua, “Inaweza kuwa karata ya kisiasa kwa sababu bado Bunge lina wabunge wengi wa CCM, pia marekebisho yatasimamiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, (Mathias Chikawe) sijui kutakuwa na jipya gani.”
Lwaitama alisema ili mambo yaende sawa, Rais Kikwete anatakiwa kuhakikisha kuwa marekebisho hayo yatakayofanywa nje ya Bunge, hayabadilishwi tena bungeni. “Ahakikishe kuwa wabunge wanapitisha tu yale ambayo yamerekebishwa nje ya Bunge.”
Naye Profesa Gaudence Mpangala wa UDSM alisema: “Tutajua kama hili jambo limetulia ama la, kama Bunge likipitisha mapendekezo mapya, kama ikiwa hivyo mambo yatakwenda vizuri.”
Hata hivyo, Profesa Mpangala alionyesha wasiwasi wake kama wabunge wataamua kuyapinga mabadiliko hayo, huku akishauri itumike njia ambayo itawafanya wabunge kukubaliana na kile kilichojadiliwa nje ya Bunge.
Alisema Katiba nzuri ni lazima itokane na mwafaka wa pamoja na kwamba nia ya Rais Kikwete inapaswa kuendelezwa hadi bungeni.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally alisema: “Siku zote mtu asiyejua anapokwenda hawezi kupotea njia, mchakato wa Katiba Mpya una mgongano wa mtazamo kuna maswali mengi kuhusu mchakato huu kuwa wa kisiasa na kisheria.
Alisema kuwa mchakato huo sasa haujulikani unaendeshwa kwa masilahi ya nani, kwa sababu kila malalamiko mengi yanayotolewa yamebebwa na vyama vya siasa.
“Tupo njiapanda, binafsi sina imani kubwa na mchakato huu, vyama vimeweka masilahi yao zaidi mbele,” alisema Bashiru.
Aliyekuwa Mbunge wa Monduli na Mkuu wa wilaya, Lepilal Ole Moloimet alisema mtindo wa Rais Kikwete wa kuzungumza na wapinzani ni mzuri kwa sababu unasaidia kuweka mazingira ya utulivu na maelewano nchini.
Alisema utaratibu huo ni mzuri katika kuondoa manung’uniko, hasa kwa wale ambao hawaridhiki na hali halisi ya mambo yanavyokwenda nchini.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema atakuwa kwenye mazingira mazuri ya kuchambua mpango wa Rais Kikwete kukutana na vyama vya upinzani, pindi mchakato ukikamilika.
“Bado ni mapema sana. Mazungumzo bado hayajamalizika. Tusubiri yamalizike ndipo nitakapokuwa na nafasi nzuri ya kuyazungumzia,” alisema Nape.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Ntatiro alisema kwamba wanatarajia kutoa taarifa kuhusu mazungumzo hayo na Rais Kikwete.
Alisema mpaka sasa chama hicho bado hakina uhakika kama kweli kilichoandikwa kwenye vyombo vya habari jana ndicho kilichoafikiwa kwenye mazungumzo hayo.
Kwa upande wake Chadema kupitia kwa Ofisa wake wa Habari, Tumaini Makene nao walisema watatoa taarifa yao baadaye.
Makubaliano ya mkutano
Taarifa ya Ikulu juzi, ilisema Rais Kikwete na viongozi hao walikubaliana vyama vyote vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha sheria hiyo, viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili itafutwe namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Wenyeviti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Chadema, Freeman Mbowe, NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Katika hoja zao, wapinzani wanataka kuangaliwa upya kwa idadi ya wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba, utaratibu wa
kupitisha Katiba Mpya kwenye Bunge Maalumu wakisisitiza kwamba kuwapo haki sawa kwa kila upande wa Muungano
Hoja nyingine ni ukomo wa Tume ya Mabaraza ya Katiba ambapo viongozi hao walipendekeza kwa rais kuwa tume iendelee kuwapo hadi Katiba Mpya itakapopatikana badala ya kuvunjwa mapema kabla ya Katiba Mpya.
Hoja nyingine kuingizwa kwa mambo ambayo hayakujadiliwa wala kupitishwa na Bunge kwenye muswada huo, wakitoa mfano wa
kifungu kipya kinachompa Katibu wa Bunge na yule wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mamlaka ya kusimamia mchakato wa kumchagua mwenyekiti wa muda wa Bunge.
Walisema pendekezo hilo ni jipya na kwamba halikuwepo kwenye muswada uliotolewa maoni na wadau.

No comments: