Sunday 30 June 2013

Wengi wamtakia Mandela afya njema

Mamia ya watu wanaendelea kukusanyika nje ya hospitali alikolazwa Nelson Mandela mjini Pretoria Afrika Kusini. Inaarifiwa Mandela bado yuko hali mahututi.Wamekuwa wakimuimbia nyimbo na kumuombea nje ya hospitali. Wengine wamekusanyika katika iliyokuwa makaazi ya Mandela mtaani Soweto.
Watu wana wasiwasi kuhusu hali y mandela lakini pia wanataka kuonyesha wanavyojivunia kiongozi wao ambaye wanamuona kama baba wa taifa lao.
Mandela , rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini, anaugua maradhi ya Mapafu.
Mamia ya wananchi walikesha kwa maombi maombi nje ya makaazi ya zamani ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Nelson mtaani Soweto.
Rais Jacob Zuma amesema kuwa afya ya shujaa huyo aliyepigana dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini humo inaendelea kuimarika.
Mandela aliye na umri wa miaka 94 amekuwa hospitalini akiuguwa ugonjwa wa maambukizi ya mapafu.
Awali mwanawe wa kike, Makaziwe alisema afya ya babake inaendelea kuwa njema.
Aidha Makaziwe amevikashifu vyombo vya habari kwa kukita kambi nje ya hospitali alikolazwa shujaa huyo akisema wanahabari wanapaswa kumheshimu babaake.
Rais Jacob Zuma alisema Alhamisi kuwa hali ya Mandela iliimarika lakini bado yuko hali mahututi.
"leo angalau yuko sawa kidogo kuliko nilivyomwacha jana usiku,'' alisema Rais Zuma baada ya kuongea na madakatari wanaomtibu Mandela.
Bwana Zuma alifutilia mbali safari yake ya Msumbiji ili kumtembelea Mandela hospitalini.
Wakati huohuo mwanawe Mandela Makaziwe alisema Mzee 'bado yupo' na kuwa anaweza kuhisi mtu akimgusa.

Akiondoka Rais Obama, karibu Malkia Elizabeth

Watu hao wanaondolewa maeneo yao huku ikielezwa kuwa zoezi hilo ni endelevu, viongozi wa Manispaa za jiji hilo nao wamekuwa wakitoa elimu juu ya usafi kwa wafanyabiashara wa hoteli pia.
  Acha hilo, katikati ya wiki hii nyakati za jioni lilikatiza gari katikati ya jiji hilo likipuliza dawa ya kuua mbu na kuwafanya watu waliokuwa wamesimama kando ya barabara wakisubiri usafiri kukohoa hovyo, kupiga chafya na kutafuta sehemu ya kujificha kukwepa adha hiyo.
  Hayo yote yanafanyika ili Rais Barack Obama wa Marekani atakapowasili nchini na msafara wake alione Jiji la Dar es Salaam likiwa safi na kila njia inafanywa kuhakikisha jiji hilo linakluwa safi. Duh, usafi kwa ajili ya ujio wa wageni tu? Aibu gani hii.   Natambua wazi kwamba ugeni mkubwa wa viongozi wa zaidi ya nchi 14 umekuja nchini kwa mkutano wa Majadaliano ya Kiuchumi, pamoja na ziara ya Rais Obama wa Marekani ni heshima kubwa kwa taifa letu.    Pia, natambua kwamba ugeni huu utakuwa na manufaa kwa wafanyabiashara wetu wa hoteli, migahawa, huduma za usafiri na hata wafanyabiashara ndogondogo kwani watapata fursa ya kuingiza kipato.
  Sina tatizo na ujio wa viongozi hao, lakini kinachonishangaza ni kuanza kwa  operesheni ya usafi uliyoshindikana miaka nenda rudi kwa sababu tu ya ujio wa viongozi hao, huku watendaji wakidai ni zoezi endelevu.   Nchi yetu inawajali wageni kuliko wenyeji, ipo tayari kuhakikisha wageni hawang’atwi na mbu, hawasumbuliwi na wafanyabiashara na ombamba waliotapakaa maeneo ya mjini wala kusikia harufu chafu ya takataka zilizotelekezwa katika maroli, aibu gani hii!
  Kila kukicha tumekuwa tukishuhudia takataka zikitapakaa maeneo mbalimbali ya jiji na karibu kila kona kuna chupa za maji yaliyotumika, mifuko ya plastiki na taka nyinginezo.
  Kama hiyo haitoshi, kuna matela yaliyojaa takataka, yametelekezwa katika sehemu mbalimbali za masoko au maeneo ya makazi ya watu.    Mifereji ya kupitisha majitaka, mingi imeziba, jambo ambalo husababisha maji yanayotokana na mvua kusambaza uchafu, unaobebwa kwenye maeneo ya makazi au barabarani.
  Taka hizi husambaa na kuziba njia za waenda kwa miguu, hivyo kuwapa watumiaji hao wa barabara ugumu wakati wanapotembea.
  Katika mitaa mbalimbali kuna madimbwi yaliyosahauliwa na mamlaka husika, madimbwi ambayo yanawasitiri mbu na kuwa mahala pao kuzaliana na kueneza magonjwa ikiwamo Malaria.
  Kwa miaka nenda rudi Jiji la Dar es Salaam, ambalo ndilo kioo cha taifa letu, limekuwa likiongoza kwa kuupalilia ugonjwa wa kipindupindu, ambao chanzo chake kikuu ni uchafu. Karibu kila mwaka uongozi wa Hospitali za Jiji hilo hupokea wagonjwa wa Kipindupindu.
  Operesheni hii ya usafi inayofanyika sasa ilitakiwa kuanza miaka mingi iliyopita, siyo tu katika usafi wa mazingira bali ingekwenda hadi katika kusimamia miundombinu na ujenzi holela wa makazi usiozingatia mipango miji kwani ujenzi huo husababisha uchafu kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya maji taka.
  Takataka kila mahali, harufu za vinyesi, maji taka, magari mabovu, biashara kila kona hadi makaburini. Mitaro imefurika , chupa za mikojo na mifuko ya plastiki imezagaa hadi barabarani mingine ikiwa na kinyesi, hiyo ndiyo Dar es Salaam.
  Lakini hivi sasa, ujio wa wageni hawa umewaamsha wahusika, wanafanya usafi kila kona kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda sawa na siyo ajabu kuona kila kitu kimelala baada ya viongozi hao kuondoka.
  Usafi katika Jiji la Dar es Salaam unahitaji utafiti wa kina na njia za kitaalamu zaidi katika kuhakikisha masuala ya usafi na mazingira yanafanikiwa.
Nasema hivi kwa sababu mipango na miundo mbinu ya miji huo ni ya zamani tangu enzi ya mkoloni ambapo idadi ya wakazi likuwa ndogo ukilinganishwa na sasa. Natambua kuwa jukumu la usafi ni la watu wote, ila kwa upande wa Serikali inatakiwa kuja na mikakati mipya na endelevu itakayolitoa jiji hili katika hali ya uchafu kwa kutumia fedha zitokanazo na ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali na  siyo kusubiri ujio wa viongozi.
Wafanyabiashara kupanga bidhaa, barabarani na mbele ya majengo ya Ofizi za Serikali, kushamiri kwa gereji bubu mitaani, kumbi za burudani zinazopiga muziki usiku kucha, ni moja ya kero zilizowashinda watendaji wa mamlaka husika.
Mamlaka husika zimeshindwa hata kudhibiti mfumuko wa vilabu vya pombe, kiasi kwamba hata shule za msingi na sekondari za jijini Dar es Salaam zimezungukwa na Baa na nyumba za kulala wageni.
Karibu Rais Obama kwani ujio wako umewakumbusha wahusika kulifanyia usafi Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni baada ya muda mrefu kupita tangu wafanye hivyo, pengine watakumbuka tena kufanya usafi siku atakayokuja Malkia Elizabeth wa Uingereza.
 

 

 

SPORTS: FAINALI CONFEDERATIONS CUP BRAZIL VS SPAIN LEO USIKU

Mtanange wa kombe la mabara(Confederation cup) unaoendelea huko nchini Brazil leo utafikia tamati ambapo ni fainali kati ya Brazil na Spain . Kwa Brazil hii ni furaha kwao kuingia fainali kwani wana historia nzuri ya fainali kwenye mtanange huo na mara tano za mwisho kuingia fainali hawajapoteza mchezo. Kwa Spain hii ni changamoto kubwa hasa baada ya kupita kwa mikwaju ya penati na hali ya Brazil kutumia faida ya kuwa nyumbani . Hata hivyo kocha wa Brazil (Scolari) amesema amejiandaa vyema na mchezo huo, atawatumia wachezaji wake wazuri kupambana na Spain na dakika 90 zitaamua mshindi kati yao. Timu hizo mbili mara ya mwisho kucheza ni miaka 14 iliyopita ambapo walitoa suluhu ya 0 - 0.
Mtanange huo utapigwa usiku wa leo (Saa Sita Kamili Usiku- Saa za Afrika Mashariki)
Wakati vigogo hao wawili wakipambana kwenye fainali hiyo, Uruguay na Italy watakuwa wanashindania mshindi wa tatu.

Vijana msikubali kununuliwa-Sumaye

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amewatahadharisha vijana kuwa wanaelekea kwenye uchaguzi mkuu wasikubali kupewa rushwa ya kanga, fulana na fedha na mtu yeyote anayetaka kuingia madarakani.
Akizungumza jana alipokuwa kwenye bonanza la michezo la kikundi cha Ukwamani Jogging kilichopo Kawe, alisema vijana wawe makini katika kuchagua mtu mwenye uwezo wa kuongoza ambaye atajali masilahi ya wananchi wake siyo kwa masilahi yake binafsi.
“Najiuliza kama ninajiamini nataka kugombea Kawe au Arusha au Sumbawanga kama ninafaa na wananchi wananiamini mimi ninafaa na wananchi wananihitaji kwa nini niwachochee kwa kanga au fedha ukiona hivyo huyo hawafai kuwaongoza,” alisema na kuongeza:
“Ukiona mtu anatoa kitu ili achaguliwe hafai kuwa kiongozi kwani uongozi ni mzigo,” alisema Sumaye.
Aliwashangaa watu wazima wanaochukua fedha na kuweka mfukoni kisha wanapita mitaani huku wakisema fulani anafaa kwa kuwa anatoa rushwa na fulani hafai kwa kuwa hatoi kitu chochote.
Sumaye alisema anayetoa fedha ili apewe kura huyo hafai kuwa kiongozi kwa sababu atakuwa anawatumikia watu wake waliompa fedha sio mwananchi ambaye alijitolea kumchagua kiongozi hiyo kwa kumpigia kula halali ili aweze kusaidia kumtatulia kero mbalimbali zinazomkabili.
Alisema kama kuna watu wanaumizwa kwa kuambiwa wanapokea au kutoa rushwa huku akiwa anaendelea na kufanya hivyo aache ili asiendelee kuumizwa na hilo.
Sumaye alisema nchi haiwezi kuwa na maendeleo kama viongozi wataendelea kudidimiza nchi kwa rushwa,ufisadi na kuingiza dawa za kulevya nchini.
Alisema viongozi wanaoleta dawa za kulevya kama ni nzuri wangezitumia lakini hawazitumii matokeo yake wanaoathirika ni vijana ambao wanategemewa kulijenga taifa hili.
“Hatuwezi kudidimiza jamii kwa kuwaletea dawa za kulevya ili watoto wa wenzao waharibikiwe kwa nini wasiwape au kutumia hao viongozi ili waathirike wao wenyewe?” alisema Sumaye.

Wamachinga: Ujio wa Rais Obama umetuletea njaa

Dar es Salaam. Wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katikati ya jiji na kuondolewa kutokana na ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama, wamelalamika kuwa sasa wanakabiliwa na maisha magumu.
Obama anatarajia kuwasili nchini kesho katika ziara ya kikazi ya siku mbili huku akiambatana na ujumbe wa watu wapatao 700.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili, wafanyabishara hao walisema kuondolewa huko kumewafanya kukosa kipato walichokuwa wakikipata hivyo kusababisha ugumu wa maisha.
Frank Mkama alilalamika: “Hapa Serikali isiseme kuwa wanafanya usafi wa jiji kwa kuwaondoa wafanyabiashara hii si kweli! Mbona hawakufanya zamani, hapa ni Obama ndiyo amesababisha sisi tukaondolewa.”
“Hivi sasa maisha yangu yamekuwa magumu. Kipato ambacho nilikuwa nakipata hapa na kula na familia yangu sasa sikipati.”
Naye, Elizabeth Makata alilalamika Serikali ilipaswa kuwaandaa wananchi kwa kuwaeleza ujio huo wa Obama watanufaika vipi na si kuwafanya waathirike kwa kuvunjiwa maeneo yao.
Alielezea wasiwasi kuwa huenda baada ya ziara hiyo wakashindwa kuendelea na biashara kwa kuwa watakuwa wamekula mitaji.
Kwa upande wake, Ramadhan Issa alisema ziara hiyo ya Rais Obama imeathri maisha yake kutokana na kuvunjiwa kibanda alichokuwa akifanyia biashara hivyo hajui hatima ya maisha yake.
Kadhalika Mwananchi Jumapili iliwashuhudia askari polisi wakionekana kuongezeka katikati ya jiji wakipita huko na kule kuhakikisha hali ya usalama inaimarika.
Pia hali ya usafi imeendelea kuimarika kutokana na ujio kutokana na juhudi zinazoendelea kufanywa kwa lengo la kusafisha mazingira.
Licha kwamba wafanyabiashara hao wameondolewa hivi karibuni baadhi yao wameanza kurejea kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Picha kamili ujio wa Obama

Dar es Salaam. Wakati magari 150 ya msafara wa ziara ya Rais Barack Obama yamewasili nchini, majina ya mawaziri wa Tanzania yatakayoruhusiwa kumpokea kiongozi huyo kuchujwa na makachero wa FBI.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Moses Malaki aliliambia gazeti hili jana kuwa matayarisho ya ujio wa Rais huyo ni kabambe na hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
Pia alisema shughuli za kumpokea Rais Obama, anayetarajiwa kutua Jumatatu saa 8:40 mchana, zitaanza asubuhi kwa maofisa wa Marekani kushika majukumu yote katika uwanja huo, ikiwemo kuongoza ndege, ukaguzi wa abiria na mizigo, kwa maana wafanyakazi wa uwanja huo kuwa likizo kwa siku mbili.
“Wamesema kuwa wao watasimamia kila kitu kuanzia wageni watakaoingia na kutoka na wataamua nani aingie na kutoka,” alisema Malaki.
Aliongeza kuwa japokuwa Mamlaka ya Anga Tanzania (TAA) inaendelea kufanya kazi zake kama kawaida, lakini Jumatatu, Wamarekani watasimamia kila kitu hadi ukaguzi wa wageni.
“Siku hiyo mwongoza ndege wa TAA, atafanya shughuli kidogo, mambo mengine yatafanywa na wao,” alisema.
Idadi ya maofisa wa Tanzania
Imebainika kuwa hata idadi ya maofisa wa Tanzania wakiwemo viongozi watakaompokea pia itapangwa na Wamarekani wenyewe.
“Wenyewe wana orodha yao na wanajua nani atakuwepo au hatakiwi kuwepo katika kundi la wageni watakaompokea Rais Obama,” alisema na kuongeza:
“Nilimuuliza Ofisa Usalama wa Marekani iwapo nitaweza kumwona Rais Obama, akaniambia: Utamwona ukibahatika kuwepo kwenye orodha.”
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe naye alikiri kuwa mawaziri wanaotakiwa kuwepo katika msafara wa kumpokea Rais Obama ni wachache watakaochaguliwa tu na Wamarekani, baada ya kuyapitia na kuyachunguza majina hayo kwanza kabla ya kuyakubali.
“Hii sijawahi kuiona, hata sisi wenyewe tunateuliwa na wakishayapitia wataamua, nani aende au asiende,” alisema Chikawe.

Miti yatiliwa shaka
Malaki anaendelea kueleza kuwa maofisa usalama kutoka Marekani wamekuwa wakifanyia ukaguzi kila eneo la uwanja huo, kwa kiwango cha hali ya juu na kinachoshangaza.
Ilibainika kuwa maofisa hao wameagiza hata miti mirefu na yenye matawi mengi ikatwe ili kuondoa nafasi ya adui kufanya mashambulizi.
“Hawa jamaa hawataki kufanya makosa, kitu chochote wanachokitilia shaka wanakiondoa na kukisimamia ipasavyo,” alisema.
Malaki alisema licha ya maofisa hao kuambiwa kuwa miti hiyo mikubwa ipo katika ofisi za Jeshi la Polisi wa uwanja wa ndege, walikataa kata kata na kuagiza ifyekwe.
Mafuta ya ndege
Katika kuhakikisha kuwa hakuna chochote cha hatari kinachoweza kuipata ndege ya Rais Obama, maofisa hao wamenunua mapipa kumi ya mafuta ya ndege na kuyahifadhi katika eneo nyeti la uwanja huo.
“Wamenunua mafuta na kuyahifadhi wao wenyewe na kuyafanyia vipimo vya hali ya juu,” alisema.
Huduma za zimamoto hazihitajiki
Wakati huduma ya zimamoto ikiwa inahitajika zaidi wakati ndege inapotua au kupaa, maofisa wa usalama wa Marekani wamekataa kutumia zimamoto wa Tanzania.
“Katika maandalizi hayo, tulitaka kuandaa gari la zimamoto ambalo kwa kawaida linatakiwa liwepo ndege inapotua, lakini walisema halina haja siku hiyo,” alisema Malaki.
Aliongeza kuwa maofisa hao hawaamini mtu yeyote ikiwamo wafanyakazi wa Jeshi la Zimamoto katika kumpokea Rais Obama, hasa wakati atakapokuwa anatua.

Wakati huohuo, gari lililobeba maofisa usalama wa Marekani likiongozwa na pikipiki ya askari wa usalama barabarani ambalo lilionekana likizunguka katika barabara kuu za jiji katika kile kilichobainika ni kuhakiki usalama wa barabara hizo.
Shughuli za usafi ndani ya uwanja huo zimeendelea kufanyika, ambapo Malaki amekiri kupewa agizo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick kufanya usafi katika viwanja vyote vya ndege.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wakati huu wa ujio wa Obama, ulinzi ni mkali na wa kutisha kwa wahalifu na wa kufurahisha kwa raia wema.
“Ofisi haikaliki, hapa nilipo nipo doria nahakikisha kila kitu kinakwenda sawa, hatutaki kufanya makosa,” alisema Kamanda Kova.
Alisema mtandao mkubwa wa askari umeshawekwa tayari barabarani kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama ilivyopangwa hadi siku ya tukio lenyewe.
Mfanyakazi wa uwanja huo, William Masuka, alisema hali katika uwanja huo imebadilika na uwanja umefurika maofisa usalama wa Marekani ambao wanakagua kila eneo.
“Hawa watu wamefurika hapa, sijawahi kuona kabisa. Wapo kila mahali na wapo makini,” alisema William.
Masuka alisema ulinzi wa eneo hilo hauwezi kufananishwa na ziara yeyote ya marais wakubwa waliowahi kufika hapa.
Magari 150 yatua Dar
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa ndege hizo zilitua jana saa 5:00 usiku, zikiwa na uwezo wa kubeba magari zaidi ya 50 kila moja. “Hii ni historia, wamekuja marais wengi hapa, lakini ukaguzi, ulinzi na matayarisho mengine kama haya hayajawahi kutokea,” alisema Malaki.
Alisema hivi sasa mazoezi ya kumpokea Rais huyo uwanjani hapo yanafanyika ambapo bendi rasmi ya askari wa Tanzania itakayotumbuiza siku hiyo, maofisa wa Marekani na viongozi wa TAA, wanafanya mazoezi na kuelekezana jinsi watakavyompokea Rais Obama.
“Mazoezi haya yatatoa picha rasmi ya jinsi Rais huyo atakavyotua, wapi bendi ikae, wapi maofisa wasimame, wapokeaji na msafara wake mzima.

Kwa ufupi, maandalizi haya ni kabambe,” alisema Malaki.
Mazoezi ya kumpokea yafanyika
Pamoja na hayo, mazoezi hayo yatajumuisha maelekezo kamili ya jinsi watu wanavyotakiwa kujipanga siku ambayo Rais Obama atawasili, Jumatatu.
Kwa mfano, wataelezwa ndege ya Rais Obama itakaposimama, ndege maalumu ya waandishi wa habari, maofisa wake wengine wakati magari ya msafara huo yakisubiri.
Mizinga 21 kupigwa
Pia, mizinga 21 itapigwa kama ilivyo ada ya mapokezi ya marais na viongozi wengine wa kimataifa, wanaokuja kwa shughuli za kiserikali.
Hata hivyo, Malaki alisema wafanyakazi wa TAA wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na maofisa wa usalama kutoka Marekani.

CHADEMA NGANGARI,MBINU ZA CCM ZA GONGA MWAMBA

 KUIMARIKA kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kunazidi kuwachanganya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotumia mbinu mbalimbali kukidhoofisha.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa licha ya viongozi wa CCM kuvitumia vyombo vya dola kuzima kasi ya CHADEMA, bado mambo yanaonekana kukiendea mrama chama tawala.
Hali ya mambo inaonesha kuwa CHADEMA inainyima usingizi CCM na serikali yake, ndiyo maana hivi sasa wameamua kukipaka matope kwa kutumia mbinu mbalimbali kuwafungulia kesi za ugaidi makada wao.
Uchambuzi wa kina wa matukio ya kisiasa ya hivi karibuni uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kwa sasa CCM inakabiliwa na wakati mgumu kisiasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya chama hicho.
Kuna viashiria vya wazi kuwa enzi za CCM kutawala siasa za Tanzania zinaelekea ukingoni kadiri CHADEMA inavyoimarika.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imeamua kulitumia Bunge na vyombo vya dola, ikiwamo polisi kufanikisha azima yao ya kuidhoofisha CHADEMA.
Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa na viongozi wa CHADEMA na wananchi kuwa linatumiwa kuanzisha vurugu zinazosababisha mikutano ya CHADEMA kuvurugika au kutokea vurugu.
Vurugu hizo zinaelezwa ni mipango maalumu ya kukipaka matope chama hicho kikuu cha upinzani nchini mbele ya umma ili wasikichague kwenye chaguzi zitakazofanyika mwakani na mwaka 2015.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wameanza kupata hofu juu ya mwenendo wa Jeshi la Polisi katika mikutano ya CHADEMA ambayo mara nyingi risasi na mabomu ya machozi hutumika.
Agosti 27, mwaka jana polisi walizuia na kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakielekea kwenye mkutano uliopigwa marufuku.
Katika purukushani hiyo kijana mmoja aliyekuwa akiuza magazeti mjini Morogoro aliuawa kwa risasi ingawa polisi walidai alipigwa na kitu kizito nyuma ya kichwa chake.
Septemba 2, jana mkoani Iringa, polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA na mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alilipuliwa na bomu. 
Viongozi na wanachama wa CHADEMA walikusanyika katika ufunguzi wa tawi la chama chao katika Kijiji cha Nyororo, mkoani Iringa.
Kumekuwapo juhudi za makusudi za polisi na CCM kujaribu kuihusisha CHADEMA katika matukio yote mawili ya mauaji kwa lengo la kukichafua lakini bado upepo unaonekana kuvuma vibaya kwa watawala na vyombo vya dola.
Tanzania Daima, Jumapili, limedokezwa kuwa mkakati wa pili unaotumiwa na CCM dhidi ya CHADEMA ni kuwabambikiza kesi za ugaidi viongozi wake ili chama hicho kionekane hakifai mbele ya Watanzania. 
Machi, mwaka jana, Mkururgenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, alionekana kwenye mitandao ya kijamii akipanga kile kilichodaiwa na polisi na CCM kuwa mpango wa kumteka na kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications, Denis Msacky.
Baadaye Lwakatare akashtakiwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi na kesi hiyo ikaanza kutumiwa kisiasa na makada wa CCM ili kuidhoofisha CHADEMA.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, alikiri kufahamu watu walioiandaa video hiyo na kuiweka kwenye mitandao.
Kama ilivyokuwa kwa mipango mingine, mpango huu nao haukufua dafu baada ya Mahakama Kuu kumfutia Lwakatare mashtaka yote yaliyohusu ugaidi.
Kufutwa kwa mashtaka hayo kulikuwa pigo kubwa kwa CCM na polisi.
Harakati hizo zinaonekana kuzidi kushika kasi ambapo Juni 24 mwaka huu, makada wa CHADEMA wamefunguliwa mashtaka mengine ya ugaidi mkoani Tabora.
Makada hao wanatuhumiwa kumteka na kumdhuru kwa tindikali kada wa CCM wilayani Igunga mwaka 2011.
Washitakiwa hao ni pamoja na Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian wa Bukoba, Oscar Kaijage wa Shinyanga, Seif Magesa Kabuta wa Mwanza na Rajab Daniel Kihawa wa Dodoma.
Watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi kwa madai ya kumteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Juni 15, mwaka huu kulitokea mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani mkoani Arusha, ambapo watu wanne waliuawa na zaidi ya 70 kujeruhiwa.
Mara baada ya mlipuko huo viongozi wa CCM wamekuwa wakiihusisha CHADEMA na tukio hilo huku CHADEMA wakidai polisi na serikali ya CCM ndio wahusika wakuu.
Tukio hilo lilianza kuchukua mwelekeo wa kisiasa huku CCM wakionekana kutaka CHADEMA idhibitiwe katika mikutano yake ambayo imekuwa ikisababisha vifo na majeruhi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema wanao ushahidi unaomuonesha aliyerusha bomu alikuwa ni askari na alilindwa na wenzake wakati akitoka uwanjani hapo.
Katika mwendelezo wa kuibana CHADEMA kwa kuwafungulia makada wake kesi zisizo na msingi, juzi polisi walimshtaki mahakamani Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kwa tuhuma za kumtukana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Polisi walidai kuwa Mbilinyi maarufu kama Sugu alisambaza katika mtandao wa kijamii wa facebook ujumbe wa kumtusi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya kauli yake kwamba: “Wanaokaidi amri ya polisi wapigwe tu,” kuwa ni upumbavu.
Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Dodoma ilitupilia mbali shtaka kutokana na hati ya mashtaka kukosa maelezo ya kutosheleza kuonesha kosa lililotendwa na Sugu, hivyo hati hiyo kukosa nguvu za kisheria.
Aidha, katika kuthibitisha kuwa viongozi wa CCM wamechanganywa na nguvu na ushawishi wa CHADEMA, uongozi wa Bunge nao umezidisha harakati zake za muda mrefu za kuwabana wabunge wa chama hicho kwa kuwazuia kuvaa suti za kombati ndani ya Bunge.
Kuzuiwa kwa mavazi hayo ambayo sasa yanatafsiriwa kuwa mavazi ya chama hicho, kunaelezwa ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge.
Licha ya mbinu zote hizo, CHADEMA hivi sasa inaonekana kuimarika zaidi kwani katika uchaguzi wa udiwani uliofanyika hivi karibuni ilifanikiwa kuipoka CCM kata tatu.
Matokeo hayo yanatoa ishara kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utaofanyika mwakani na ule mkuu utakaofanyika mwaka 2015, hali itakuwa ngumu zaidi kwa CCM.
Wadadisi wa masuala ya siasa wameweka wazi kuwa CCM imo katika hali ngumu kisiasa na haitashangaza kuiona ikishindwa vibaya katika uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwaka 2015.
Kama CCM itashindwa katika uchaguzi mkuu ujao, basi itakuwa imefuata njia iliyopitwa na vyama vingine vikongwe katika Bara la Afrika, vilivyopigania uhuru wa nchi zao na ambavyo vimeondolewa madarakani na wanamageuzi kuanzia miaka ya 1990.
Vyama vikongwe Afrika vilivyowahi kuangushwa na wanamageuzi ni pamoja na chama kilichopigania uhuru wa Zambia cha UNIP chini ya Dk. Kenneth Kaunda, Chama cha Malawi Congress (MCP), kilichoongozwa na hayati Dk. Kamuzu Banda na Chama cha KANU kilicholeta uhuru wa Kenya, chini ya hayati Jomo Kenyata, ambacho kilitimuliwa madarakani mwaka 2002.