Dar es Salaam. Serikali inakusanya nguvu
kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, inang’ata
wagombea wote watakaojihusisha na rushwa katika harakati zao za kusaka
uongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watendaji kutoka
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) wamesema, utekelezaji wa sheria hiyo ulikuwa na
changamoto nyingi katika uchaguzi uliopita mwaka 2010.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty
Nyahoza alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ofisi yake
ilikumbana na changamoto nyingi zilizofanya ishindwe kuisimamia sheria
hiyo ipasavyo.
“Mwaka 2010 changamoto zilikuwa nyingi lakini
tumejifunza. Uchaguzi wa mwaka huu tumeshajipanga, tunajua jinsi gani ya
kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, tunajua tunahitaji ushirikiano wa
karibu wa wadau ili kuweza kufanikisha jambo hilo,” alisema Nyahoza.
Nyahoza alitaja wadau ambao ofisi hiyo inatarajia
kushirikiana nao katika kuisimamia sheria hiyo kuwa ni pamoja na vyama
vyote vya siasa, asasi za kijamii, waandishi wa habari na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ushirikiano huu unaanza kuimarishwa kabla ya
uchaguzi. tumebaini kwamba wadau hawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya
namna wanavyoweza kushiriki kufanikisha utekelezaji wa sheria hii, pia
kutakuwa na simu maalumu za kuripoti matukio yatakayokuwa kinyume,”
alisema.
Kauli ya Takukuru
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah
alikiri kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha nguvu hizo, licha ya
kukabiliwa na changamoto ya rasilimaliwatu.
“Ni kweli hata sisi tumeona kuna umuhimu wa
kushirikiana katika kufanikisha jambo hili, ingawa kuna changamoto ya
rasilimali watu, tunaamini kazi zitafanyika kwa namna ambayo
itadhihirisha dhana ya kuwapo kwa Takukuru,” alisema Dk Hoseah.
Dk Hoseah pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa
wananchi kuepuka kuuza haki zao za kuchagua viongozi bora kwa
kudanganywa na zawadi za kanga, fulana, kofia na fedha.
Sheria ikoje?
Ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari 2010. Sheria
hiyo imeweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato, matumizi na
gharama za kampeni na uchaguzi wa vyama vya siasa na wagombea.
Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Jakaya Kikwete Machi 17, 2010 ili iweze kutumika katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kwa lengo la kukuza demokrasia ya mfumo
wa vyama vingi nchini.
Madhumuni ya kuwekwa Sheria hii ya Gharama za
Uchaguzi ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi
katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na
kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa
mgombea na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hii imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu
ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo ni jina,
tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hii katika Tanzania Bara na
Zanzibar na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.
Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa
Vyama vya Siasa, ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za
uchaguzi kwa vyama vya siasa na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.
Sehemu ya tatu inahusu masharti kuhusu fedha
zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi,
uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama ambazo vyama vya siasa
vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti kwa Vyama vya Siasa na
wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango
au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha
kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama
kwa vyama na taasisi za kiserikali wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na
chaguzi za kisiasa.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu masharti
yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na
uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu gharama kwa vitendo
vinavyozuiwa au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sehemu ya sita ya sheria hii inapendekeza makosa
ya ujumla pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya
Sheria hii.
Sehemu ya saba inaweka masharti kuhusu haki ya
mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari,
wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia haki hiyo.
Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa
kutumia vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya
Siasa, wagombea wao na wapiga kampeni wanafikia wapigakura bila ubaguzi
wala kupewa vitisho.
Sehemu ya nane ya sheria inafanya marekebisho
katika Sheria ya vyama vya siasa ili kuoanisha masharti ya sheria
hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza kifungu cha 13A katika Sheria
ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili
wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa
kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii
wakati wa kampeni za uchaguzi.