Tuesday 1 September 2015

Ujinga, umasikini na maradhi vitakuwa historia kwenye serikali yangu-Lowassa

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wakiwapungia wananchi wa mjini Ngombe walipokuwa wakiwasili katika Uwanja wa National Housing mjini humo ulipofanyika mkutano wa kampeni za mgombea huyo jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Ruvuma. Mgombea urais wa Chadema kwa mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa  amesema akiwa rais wa Awamu ya Tano atafuta maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini waliodumu tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Lembuka katika Kijiji cha Madaba mkoani Ruvuma, Lowassa aliyekuwa akitumia staili ya kuwauliza wananchi matatizo yanayowakibili na kisha kuwajibu atakavyoyatatua, alisema tangu nchi ipate uhuru maisha ya Watanzania ni duni  na kuahidi kuwaondoa katika umasikini.
Wakati Lowassa akisema hayo, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye aliwataka wananchi kuipa Chadema na Ukawa miaka mitano tu ili iweze kuwaletea maedeleo na kama wakishindwa, warudi tena CCM.
“Jambo kubwa ni kupiga kura na kuzilinda na ikiwezekana akina mama mpike chakula kabisa nyumbani ili waume zenu wakifika nyumbani wajipakulie wenyewe. Tusipoitoa CCM madarakani hatutaweza kuwatoa tena na lazima wang’oke safari hii. Hata wana-CCM wenzangu nawashauri waondoke huko na kujiunga na sisi. Ondokeni huko nyumba inawaka moto,” alisema Lowassa.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na watu wachache ikilinganishwa na mikutano mingine ya kampeni ya mgombea huyo wananchi hao walieleza kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa maji na  umeme, migogoro ya ardhi, ada na michango iliyokithiri katika shule pamoja na ushuru katika mazao.
“Tutamaliza tatizo la umeme ndani ya mwaka mmoja, tutamaliza suala la kuporwa ardhi,” alisema Lowassa huku akiwahoji wananchi wa kijiji hicho kwanini wakubali kuporwa ardhi.
Wananchi hao walisema katika vituo vya afya wagonjwa wanaruhusiwa kurudi majumbani kutokana na vituo hivyo kukosa maji sambamba na kutozwa ushuru wa mazao usiokuwa na kichwa wala miguu.
Akizungumza katika mkutaano huo, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema maendeleo ya Tanzania hayafanani na rasilimali zilizopo nchini, akiwataka wananchi kuyakubali mabadiliko ili kuepuka matatizo mengine.
“Nilikuwa waziri mkuu kwa miaka 10 lakini nchi haikuwa na vita. Mkichagua upinzani kutakuwa na amani kama kawaida,” alisema Sumaye huku akitolea mfano yaliyotokea Masasi ambapo wananchi walichoma moto vituo vya polisi na Halmashauri baada ya bodaboda kugongana na gari la polisi, “Hali hiyo inatokana na wananchi kuchoka kuona viongozi waliowachagua wananeema na wao wanaendelea kuwa masikini.”

Dk. Slaa aibuka, atangaza kuachana na siasa za vyama

Dk Wilbroad Slaa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Serena jijini Dar es Salaam leo; Slaa amebainisha kuachana na siasa za vyama.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Dk. Wilbroad Slaa amesema leo kuwa amejiondoa kwenye siasa na hatajiunga na chama kingine chochote cha siasa ila ataendelea kuwatumikia Watanzania kwa namna yoyote.
Dk Slaa amesema alichukua uamuzi huo tangu Julai mwaka huu baada ya kutofautiana na chama chake juu ya masharti ya kumpokea mgombea wa urais kupitia Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
Dk. Slaa akizungumza jijini Dar es Salaam leo, amekiri kushiriki vikao kujadili ujio wa waziri mkuu huyo wa zamani lakini alishangazwa na viongozi waandamizi wa chama chake kuharakisha kumpokeea pasipo kutimiza masharti aliyopendekeza.
“Sina tabia ya kuyumbishwa….sina chuki na mtu yoyote lakini sipendi siasa za udanganyifu na propaganda,” amesema Dk. Slaa na kusema ameachana na siasa tangu 28 Julai, 2015 baada ya kuona misingi ya chama alichoshiriki kukijenga imepotoshwa.
Sharti la kwanza ambalo Dk. Slaa alitaka lizingatiwe ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya serikali ya CCM kujisafisha kwenye tuhuma ya kashfa ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa kama Waziri Mkuu.
Aidha, Slaa alitaka ajue Lowassa ataongeza thamani gani ndani ya Chadema, ikiwa ni pamoja na viongozi watakaojiunga toka chama tawala.
Baada ya Lowassa kutokidhi vigezo tajwa, huku akiwataja viongozi waliojiunga Chadema wakitokea CCM wakiwa ni “mizigo” ndani ya chama tawala, amejiweka kando na Chadema.
DK Slaa ametumia takribani saa mbili kueleza msimamo wake na matatizo anayoyaona kwa Lowassa na waziri mkuu mstaafu ambaye naye amejiunga na upinzani, Frederick Sumaye kuwa hawafai na si watu safi.