Monday 29 July 2013

Utafiti:Sera ya uwekezaji madini hainufaishi jamii

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Uhasibu Arusha na Mchumi, Balozi Morwa alitoa mapendekezo hayo juzi, wakati akiwasilisha utafiti kuhusu wajibu wa kampuni kwa jamii(CSR),uliofanyika katika machimbo ya Tanzanite Mirerani, wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Arusha. Serikali imeshauriwa kubadili sera ya uwekezaji nchini kwa kulazimisha kisheria kampuni za wawekezaji hasa wa Sekta ya Madini, kutekeleza miradi ya jamii inayozunguka maeneo yao ya uchimbaji badala ya suala hilo kuwa ni la hiari.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Uhasibu Arusha na Mchumi, Balozi Morwa alitoa mapendekezo hayo juzi, wakati akiwasilisha utafiti kuhusu wajibu wa kampuni kwa jamii(CSR),uliofanyika katika machimbo ya Tanzanite Mirerani, wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Morwa akiwasilisha utafiti huo ,ambao uliratibiwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali ya Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Finnish NGO Platform, alisema wamebaini kuwa jamii zinazozunguka migodi ya Tanzanite hazinufaiki ipasavyo.
Morwa alisema utafiti huo, ulihoji watu 350 na nyaraka kukusanywa,wamebaini,wajibu wa kampuni ya wawekezaji kwa jamii ukiwa wa kisheria kama Ghana, utawanufaisha na ikishindika ifutwe na kampuni hizo zilipe kodi kubwa kama nchi nyingine.

Tume ya Uchaguzi itasababisha vurugu

Uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne za Jimbo la Arusha Mjini ulifanyika juzi, ambapo Chadema kiliibuka mshindi katika kata zote nne za Themi, Kimandolu, Elerai na Kaloleni.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya madiwani wake kutimuliwa uanachama na chama hicho kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama chao kuhusu kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha.
Kinyume na matarajio ya wengi, uchaguzi huo ulikuwa na idadi ndogo sana ya wapigakura kulinganisha na chaguzi zilizopita, kwani kati ya wapigakura zaidi ya 60,000 waliojiandikisha ni 11,042 tu waliojitokeza kupiga kura.
Kwa mfano, Kata ya Elerai inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wapigakura 23,885 lakini waliojitokeza kupiga kura juzi ni 3,824 tu.
Takwimu hizo zinaibua maswali magumu, hasa kuhusu hali inayoendelea kujitokeza ya kudidimia kwa demokrasia nchini.
Takwimu hizo zinatoa tahadhari ya kishindo kwamba huko tuendako sio salama na kwamba nchi yetu inakabiliwa na maangamizi makubwa iwapo Serikali haitaweka mazingira ya kuwawezesha wananchi kushiriki katika chaguzi mbalimbali pasipo kuhofia maisha yao.
Kutojitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kupiga kura katika uchaguzi wa Arusha juzi kumehusishwa na hofu iliyotokana na bomu lililorushwa katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani za Chadema mwezi uliopita ambapo watu wanne walikufa na wengine 60 kujeruhiwa, hivyo kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi katika kata hizo hadi juzi.
Lakini pia utendaji mbovu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Tec), katika chaguzi mbalimbali, ukiwamo wa juzi jijini Arusha pia umedhihirisha kwamba huko tuendako hapatakuwa salama iwapo tume hiyo haitafanyiwa mabadiliko makubwa.
Tunalazimika kusema hapa kwamba yafaa tutumie fursa tuliyonayo hivi sasa ya kuandika Katiba mpya kuhakikisha kwamba Katiba hiyo inatuzawadia Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyo huru na yenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu.
Uchaguzi wa juzi jijini Arusha umedhihirisha ulegelege na udhaifu mkubwa uliopo katika Tume hiyo. Pamoja na kuwa na uzoefu wa kutosha katika kusimamia chaguzi mbalimbali, Tume hiyo haionyeshi kubadilika wala kuwa na dira na mwelekeo wa kuiwezesha kwenda na wakati kuhakikisha chaguzi zinafanyika kwa mujibu wa sheria.
Kama tulivyoshuhudia katika uchaguzi wa Arusha juzi, kasoro ambazo zingeweza kuzuilika zimeendelea kujitokeza na nyingi zimekuwa zikijirudia kutokana na watendaji wa taasisi hiyo nyeti kufanya kazi kwa mazoea tu.
Pamoja na wananchi kuwa na shahada halali za kupigia kura na majina yao kubandikwa katika mbao za matangazo, baadhi yao walizuiwa kupiga kura kutokana na Daftari la Wapigakura kutokuwa na majina, maelezo na picha zao.
Baadhi ya majina ya wapigakura yalitokea zaidi ya mara moja wakiwa na namba tofauti, huku wataalamu wa mifumo ya kompyuta wakisuasua kurekebisha matatizo yaliyojitokeza.
Matatizo hayo, ikiwa ni pamoja na Tume kushindwa kuhakiki Daftari la Wapigakura mara kwa mara ni viashiria vya vurugu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwani wananchi hawatakubali kuondoka vituoni pasipo kupiga kura kwa uzembe tu wa Tume hiyo.
Hii pengine inadhihirisha kwamba haitaweza hata kutumia teknolojia ya kisasa kuhesabu kura mwaka 2015. Matokeo yake ni vurugu zitakazotokana na kasoro hizo.

Bajeti finyu kikwazo cha kupata haki mahakamani-Jaji mkuu Tz



Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman, amesema ni vigumu mahakama kama taasisi ikaweza kutoa haki kwa wakati kama haitaweza kujitosheleza kimapato.
Aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizindua kitabu kilichoandikwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta kiitwacho ‘Uhuru wa Mahakama’ na kuchapishwa na Kampuni ya Mkuki na Nyota.
“Uhuru wa kitaasisi ambao haujakamilika ni ule wa kifedha na kimiundombinu, bila huu kukamilika ni vigumu kila mwananchi kuweza kupata haki kwa wakati,” alisema Jaji Chande.
Alisema licha ya kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuongeza bajeti ya mahakama, bado lengo halijafikiwa na kuwa ni vyema muhimili huo ukatengewa fedha za kutosheleza kuendesha shughuli zake.
Jaji Chande alisema kuwa, katika bajeti ya mwaka 2013/14 muhimili huo umetengewa Sh160 bilioni ingawa mahitaji yake halisi ni Sh300 bilioni.
Alisema pia kuwa,kitabu hicho kitawasaidia viongozi wengi ambao wamekuwa wakidhani kuwa mahakama ni chombo cha Serikali. “Wakisoma kitabu hiki wataelewa na wataachana na dhana hii,” alisema Jaji Chande.
Akizungumzia maudhui yaliyopo kwenye kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kiswahili, Jaji Chande alisema kuwa kimelenga kumsaidia mwananchi wa kawaida kuijua mahakama na pia watawala, vyama vya siasa na wanasheria watapata mwongozo makini.
Kwa upande wake Jaji Samatta alisema kuwa, mwanzoni kabisa wazo lake lilikuwa ni kuandika juu ya kesi ambazo zimewahi kutikisa nchini kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar.
Alisema, alikuja kuachana na wazo hilo baada ya kuona hapati baadhi ya vielelezo ambavyo vingemwezesha kuandika kitabu hicho.

Saturday 20 July 2013

TENDWA HAMA CHOHOTE KITAKACHO ANZISHA KAMBI YA MAFUNZO YA KIJESHI TUNAKIFUTA

OFISI ya Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini imevitaka vyama vya siasa kutii agizo la kutoanzisha kambi za mafunzo ya kulinda amani maarufu kwa jina la mgambo , huku ikisisitiza kwamba itachukua hatua za kisheria kwa chama chochote kitakachoiuka , ikiwemo kukifuta.

Aidha ofisi hiyo imesema kuwa Katiba ya nchi imempa jukumu kila mwananchi kulinda amani na usalama wa nchi, pia kujilinda yeye mwenyewe na mali zake kwa kutoa taarifa katika vyombo vya dola pale anaposikia au kuona mtu anataka kufanya au anafanya uhalifu au amemdhuru mtu.

Kauli hiyo imetolewa  jijini Dares Salaam na ofisi hiyo katika taarifa yake iliyoitoa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Rajab Juma kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa kufutia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza hivi karibuni kinakusudia kuanzisha kambi za mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.

Alisema suala hilo lilitangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kuandikwa katika vyombo vya habari kabla ya chama hicho, kuwasiliana na taasisi husika ikiwemo ofisi hiyo ili kupata ushauri kuwa

Mbunge wa Bumbuli akataa kupokea mradi wa maji

lipangwa kujenga tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 135,000, lakini mkandarasi aliamua kujenga tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita 90,000 ili kuuunganisha na tanki la zamani lenye uwezo huohuo lakini mkandarasi hakuunganisha matanki hayo jambo ambalo ni kosa’’ alisema..

Tanga. Katika hatua inayoashiria kuchoshwa na utekelezaji usioridhisha wa miradi, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, wilayani Lushoto, January Makamba amekataa kuupokea mradi wa maji uliojengwa katika Halmashauri Mpya ya Bumbuli kutokana na kile alichokieleza kuwa umejengwa chini ya kiwango.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bumbuli, Makamba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia alisema kuwa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh400 milioni haukutekelezwa ipasavyo pamoja na kutengewa fedha nyingi na wahisani ambao ni Benki ya Dunia.
Mradi huo umepangiwa kuwanufaisha, wanakijiji katika vijiji vinne vya Bumbuli Mission, Bumbuli Kaya, Mboki na Kwamanolo na ulikuwa uanze kutoa huduma ya maji kuanzia Kijiji cha Kwamanolo.
“Ilipangwa kujenga tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 135,000, lakini mkandarasi aliamua kujenga tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita 90,000 ili kuuunganisha na tanki la zamani lenye uwezo huohuo lakini mkandarasi hakuunganisha matanki hayo jambo ambalo ni kosa’’ alisema..
Alisema fedha zilizotumika na thamani halisi ya mradi ni tofauti na kwamba ni vigumu kwake kuamini kwamba mradi huo utatekelezwa kama ulivyokusudiwa awali.
Alisema ni afadhali asipokee kwanza mradi huo ili taratibu zingine za kuchunguza zifanyike kama ni kweli mradi huo utasambaza maji ya kutosha.

Masaibu haya ndiyo huwatokea wanawake ndani ya vyumba vya leba

Mwanahamisi Majube amelala katika kitanda cha hospitali moja ya umma (jina linahifadhiwa) ikiwa ni  saa chache  baada ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua.
Analia na kuugulia kwa uchungu, akilalamikia maumivu makali ya tumbo.
Kwa sababu hiyo, anamwita daktari akimweleza kuwa anahisi kuna kitu tumboni mwake na kinamuumiza mno,  lakini daktari anamjibu kuwa maumivu hayo yatatulia.
“Nisaidieni nitakufa kabla ya kumwona mtoto wangu, naumwa daktari, nakufa jamani,” anasema Mwanahamisi.
 Anapoendelea kuita, wakunga ndani ya wodi hiyo wanaibuka na kumjibu: “Acha kudeka, ulifikiri kuzaa ni kama kucheza kamari. Nyamaza, unawapigia kelele wenzako.”
Anaendelea kuita kwa zaidi ya saa lakini bila msaada wowote na baada ya kulia kwa muda mrefu, anatupa miguu huku na kule…ananyamaza, kisha anatulia. Kumbe… Mwanahamisi amekata roho!
 Mwanahamisi ni miongoni mwa wanawake wengi nchini ambao hukumbana na vifo vya kuepukika wakati wa kujifungua au muda mfupi baadaye.
Vifo hivyo, vingi vinasababishwa na uzembe wa madaktari, huduma dhaifu, ukosefu wa vifaa na sababu nyingine zinazozuilika wakati wa kujifungua.
 Pamoja na uchungu wa kujifungua anaoupata mwanamke, ukosefu wa vifaa tiba, maumivu mengine huyapata toka kwa baadhi ya  wahudumu wa afya.
 Hali hiyo imesababisha baadhi ya wanawake, hasa wale wanaojiweza kukimbilia katika hospitali binafsi ambapo wanapata huduma bora zaidi.
Hata hivyo, ni wanawake wachache nchini wenye uwezo huo na zaidi ya asilimia 80 wanategemea hospitali za Serikali ambazo  baadhi, ndizo zenye changamoto.
Katika mdahalo wa afya ya uzazi uliondaliwa na Dk Tausi Kida na Riziki Pansiano, wadau walikiri kuwa kuna matatizo mengi yaliyowakumba wanawake wakati wa kujifungua, kubwa likiwa rushwa na matusi.
Kwa mfano, wadau walieleza kuwa watoa huduma wengi, yaani wauguziwamelalamikiwa kuwa wanadai hongo ili waweze kutoa huduma kwa wagonjwa.
 Hii ni sababu mojawapo muhimu inayowafanya kinamama wasijifungue chini ya uangalizi wa wataalamu wa tiba kwenye vituo vyetu vya afya na hivyo kuwa kwenye hatari zaidi ya kupata matatizo wakati wanapojifungulia nyumbani.
“Niliwahi kushuhudia mama mjamzito kuachwa mapokezi mpaka kafariki bila hata kuhudumiwa. Ndugu wa dada huyu waliambiwa kuwa bila ya elfu 75 mgonjwa wenu hapati huduma kwa daktari. 
Kinamama hawa wakiendelea kuchangishana mmoja hadi mwingine wakifuata fedha hadi huko Morogoro, mwishowe baada ya saa karibu nane baada ya pesa kutopatikana mwenzetu akafariki.”
Wachangiaji pia walihusisha matatizo ya vifo na matusi na maneno ya kukatisha tamaa wanayoyatoa manesi kwa wajawazito.
 “Mama akiomba msaada utasikia mfuate huyo aliyekupatia mimba”. Alisema mchangiaji mmoja.
Maneno mengine yanayowatoka wauguzi ni kama vile usitusumbue hatupo kwa ajili yako hapa, mara unataka nijigawe ili nimhudumie huyu na wewe.
“Nimepata kumsikia nesi akisema kuwa huyu mwanamke asije akatulaza macho, anasema Dk. Salatiel Moyo, mchangiaji katika mjadala huo.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa vifo vya uzazi Tanzania  ni 578 kati ya vifo 100,000 ambayo ni sawa na asilimia 18 ya vifo vyote vya wanawake wa kati ya miaka 15 hadi 49.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaeleza kuwa, asilimia 46 tu ya wanawake ndiyo husaidiwa na mtaalamu wa afya wakati wa kujifungua.
Faraja Mujuni, alimpoteza mtoto wake na kujikuta akiondolewa kizazi baada ya kupata uchungu pingamizi kwa muda mrefu.
“Kila nilipomwambia mkunga kuwa mtoto anatoka alikataa, kila nililomweleza alikuwa akiniangalia na kunifyonza, mwishowe, mtoto alifariki na mimi kuondolewa kizazi, kwani kilipasuka,” anasema Faraja.
Mwanamke mwingine, Anastazia Simwanza, mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam anasema alipofikishwa katika wodi ya wazazi, alikuta vitanda vimejaa, hivyo akaambiwa alale chini.
“Ilikuwa saa tisa usiku. Wakati huo uchungu ulikuwa ukiniuma kwa kasi, nikamwita nesi, lakini akaniambia bado kabisa mtoto hajashuka,”anasema Simwanza.
Simwanza anaeleza kuwa, baada  ya dakika kadhaa, chupa ilipasuka na mtoto akaanz saa kutoka, jambo lililosababisha ajifungue mwenyewe, bila msaada wa muuguzi na mtoto aliangukia chini sakafuni.
“Mwanangu alipata matatizo kwa sababu aliangukia sakafuni ndiyo maana hajatembea mpaka sasa wakati ana miaka sita,” anasema.
Paschal Msechu anaeleza jinsi yeye na mkewe mjamzito walivyotukanwana na wauguzi wakati mke wake alipokuwa akiugulia maumivu ya uchungu wa kujifungua.
“Kila nikijaribu kuwaeleza waliniambia niwaache wao wanajua kazi yao, walianza kumtukana mke wangu kwa sababu alikuwa hawezi kutembea, wakamrushia maneno mazito,” anasema Msechu.
 Si huyo tu, Yohana  Mwanga, anaeleza jinsi mke wake mpenzi alivyopoteza maisha kwa sababu  tu ya kukosa vifaa.
“Hatukuwa tumebeba vifaa vyote, wakati muuguzi ananiambia hayo, mke wangu alikuwa katika hali mbaya mno. Wakati natafuta hela za kununua, mke wangu alifariki kwa kukosa huduma.” Anasema Mwanga
 Mwanga, kwa masikitiko anasema: “Nimempoteza mke wangu kwa kukosa fedha tu, wala si kingine.”
Idadi kubwa ya vifo vya uzazi katika baadhi ya maeneo duniani inaonyesha ni kutokana na kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa huduma za afya, na inaonyesha pengo kati ya matajiri na maskini.
Karibu wote, vifo vya uzazi (asilimia 99 hutokea katika nchi zinazoendelea.
 Mhadhiri wa Chuo cha Wakunga katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya  Tiba Muhimbili, Dk Sebalda Leshabari, anasema wakunga wenye tabia zinazolalamikiwa na wanawake wanafanya makosa kwani hawakufundishwa hivyo vyuoni mwao.
Hakuna mkunga anayefundishwa kuwa jeuri au kutukana, sisi tunawafundisha mawasiliano mazuri na mama mjamzito na ujuzi mwingine,’ anasema Dk Leshabari.
Anasema hata Chama cha Wakunga Tanzania (TMA) wakati wa makongamano hutoa elimu na kuwakumbusha wakunga kuhusu huduma nzuri kwa wajawazito.
“Hizo  shutuma  tunazisikia zote na tunawapa mifano wanafunzi wetu wasirudie  tabia hizo,” anasema
 Dk Leshabari pia anatoa angalizo zaidi na kusema mpaka sasa ni asilimia 61 tu ya wanawake Tanzania wanaojifungulia hospitali, je, wengine wanajifungulia wapi?  

Janjaweed wadaiwa kuhusika mauaji ya askari wa Tanzania

. Wakati miili ya wanajeshi saba wa Tanzania waliouawa nchini Sudan ikiwasili leo, taarifa zinadai kundi la Janjaweed ambalo linaungwa mkono na Serikali, linahusika katika mauaji hayo.
Wanajeshi hao wa Tanzania ambao ni sehemu ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), waliuawa Julai 13 eneo la Kusini mwa Darfur.
Askari wengine 17 walijeruhiwa katika shambulio hilo na wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali maalumu.
Taarifa za UN, zilieleza juzi kwamba ingawa kundi hilo halijatambuliwa rasmi, mashuhuda wamekuwa wakieleza mauaji hayo yamefanywa na kundi linaloungwa mkono na Serikali ya Sudan.
Kiongozi wa moja ya makundi ya wapiganaji la Sudan Liberation Movement (SLM), Minni Minnawi, ndiye aliyeibuka awali na kuwatuhumu mgambo wanaoungwa mkono na Serikali na kutaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa.
Katika mahojiano yake na gazeti la Sudan Tribune alipokuwa akihudhuria mkutano wa majadiliano kuhusu namna ya kupata amani ya kudumu nchini Sudan uliofanyika mjini Geneva, Uswisi, Minnawi alikanusha tuhuma kwamba kundi lake linahusika na shambulio hilo.
Kiongozi huyo alikuwa akijibu tuhuma za Serikali ya Sudan kwamba, kundi lake ndilo lililohusika na shambulio hilo.
“Tuna uhakika shambulio lililofanywa dhidi ya walinzi wa amani wa Unamid liliandaliwa na kutekelezwa na Janjaweed, tuko tayari kutoa ushirikiano kwa chombo maalumu cha kimataifa kitakachoundwa kufanya uchunguzi kuhusu tukio hili,” alisema.
Alisema wanamgambo wa Janjaweed hivi sasa wanakabiliwa na ukata wa hali ya juu na ukosefu wa vifaa, kwa sababu Serikali haina tena uwezo wa kuwafadhili hivyo wameamua kufanya matukio ya uporaji kukidhi mahitaji yao.
Wanajeshi saba waliuawa kwenye shambulio lililotokea Julai 13 huko Khor Abeche, Nyala nchini Sudan wakati walinda amani.
Wakati huohuo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema miili ya wanajeshi hao itawasili leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, (Terminal one) saa 9:00 alasiri.
“Baada ya kuwasili miili hiyo itapelekwa Hospitali ya Kuu ya Jeshi, Lugalo. Baada ya maandalizi, miili hiyo itaagwa rasmi kwa heshima zote Jumatatu kuanzia saa 3:00 asubuhi viwanja vya Wizara ya Ulinzi, Upanga, Dar es Salaam,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Martin Nesirky, alisema walinda amani hao waliwekewa mtego wakiwa katika majukumu yao ya msingi ya kulinda amani. Alisema UN imeanza kufanya uchunguzi wake binafsi na kuitaka Serikali ya Sudan kuwasaka wahusika ili wawajibishwe.