Bush kuwasili nchini Tanzania
Idadi ya watu waliofariki dunia baada ya
mlipuko wa bomu katika mkutano wa Chadema imeongezeka baada ya mtoto
Fahad Jamal (7) ambaye hali yake ilikuwa mbaya na kulazwa chumba cha
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Selian,
kuaga dunia juzi saa saba mchana hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa
Hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga mtoto huyo alifariki dunia wakati timu
ya madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya
Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam wakijitahidi kila hali kuokoa maisha
yake.
Kifo hicho kinaongeza idadi ya marehemu
na kuwa wanne baada ya vifo vya Amiri Ally (7), Judith Moshi (25) ambaye
ni Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) Kata ya Sokon One
jijini hapa na Ramadhan Juma (15).
Dk Kisanga alisema hospitali hiyo juzi
ilipokea majeruhi wengine 17 wa mabomu ya kutoa machozi katika eneo la
Soweto wakati polisi wakitawanya wafuasi wa Chadema.
Alisema majeruhi 14 wamelazwa huku
watatu wakitibiwa na kuruhusiwa ambapo pia Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari aliyekuwa amelazwa hapo kutokana na kuumia shingoni
aliruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.
Mganga Mkuu alaani Naye Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Mkoa wa Mount Meru, Dk Frida Mokiti, amelaani vitendo vya
uvunjifu wa amani na vitisho vya wafuasi wa Chadema, ambavyo
vilisababisha kuvunjwa kwa mlango wa gari la wagonjwa na kuvunja lango
kuu la kuingilia hospitalini hapo.
Alisema katika tukio hilo la bomu,
wafuasi hao wa Chadema, walitishia madaktari na wauguzi wa zamu na
kutaka kuchoma moto majengo ya hospitali hiyo, wakishinikiza kutibiwa
haraka kwa majeruhi wa bomu.
Aliongeza kuwa hospitali haikupata
taarifa mapema ya mlipuko huo na hivyo kuchelewa kupeleka gari la
wagonjwa kwenye eneo la tukio ili kutoa msaada na kilichotokea ni
wafuasi wa chama hicho wakiwa na majeruhi walifika hospitalini na kuanza
vitisho na kufanya fujo zikiwamo kutishia kuchoma moto magari na
majengo ya hospitali hiyo.
Alisema hospitali hiyo haibagui wagonjwa
wala haitoi huduma kwa itikadi au imani ya mgonjwa bali kazi yake ni
kuhudumia watu wote bila ubaguzi.
Dk Mokiti, aliishukuru Wizara ya
Maliasili na Utaliii kwa misaada ya vifaa vyenye thamani ya Sh milioni
120 kwa hospitali zote tatu za Mount Meru, Selian na St Elizabeth.
Alisema pia wamepokea madaktari bingwa
kutoka Hospitali ya Moi Kenya, ambao wameongeza nguvu ya kuhudumia
majeruhi wa mlipuko huo. Wakati huo huo, kitendo cha wanasiasa
kunyoosheana vidole kuhusu tukio hilo la bomu kimeshutumiwa kuwa
kinaweza kuathiri upatikanaji wa wahusika sahihi.
Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na
gazeti hili, walisema shutuma na mvurugano miongoni mwa wanasiasa,
vitasababisha Serikali kujikita katika kutatua mifarakano hiyo badala ya
kutafuta mbaya wa Watanzania.
Utalii Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa
kuhusu sekta ya utalii kuathirika na milipuko ya mabomu Arusha au safari
za watalii kusimama, alisema hali ya usalama Tanzania hususan Arusha ni
nzuri na kuomba watalii kuendelea kuja nchini kuona vivutio vya utalii.
Alisema Tanzania kuna amani na ndiyo
maana hata Rais wa Marekani, Barack Obama anatarajia kuja nchini na
kuongeza kuwa kutokana na amani iliyopo milango ya utalii imezidi
kufunguka, kwani hivi sasa watalii kutoka Japan, China, Uturuki na
sehemu mbalimbali duniani wanakuja kuangalia vivutio hivyo.
Aliongeza kuwa amani ni muhimu kwa
Tanzania hususan Arusha ambalo ndio mlango wa sekta ya utalii na
kuwasihi viongozi wa vyama vya kisiasa kuhakikisha wanalinda amani
nchini kwani endapo itapotea waathirika wengi wakiwamo wadau wa sekta ya
utalii, hoteli, wauzaji mboga na wengine wataathirika kimapato na
uchumi kudorora.
Katika hatua nyingine, wananchi wa
Arusha na viunga vyake, wanaendelea na shughuli zao za kila siku huku
wengine mapema jana asubuhi walifika eneo la Soweto kuangalia vitu
walivyokuwa wameangusha juzi.
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia
baadhi wakiwapa watoto wa mitaani Sh 500 hadi Sh 1,000 ili kuwasaidia
kuangalia kama simu, pochi na vitambulisho vyao kama vipo; wengine
walivipata lakini wengine hawakuambulia kitu.
Imeandikwa na Veronica Mheta, Gloria Tesha, Shadrack Sagati na Prisca Libaga
No comments:
Post a Comment