Hatupaswi kufurahia kushughulika na matokeo bali uhodari wetu wa kuzuia mabalaa.
Kama ambavyo Watanzania wengi wiki hii na siku
chache zinazokuja mijadala yao imegubikwa na sakata la Akaunti ya Escrow
na tuhuma za ukwapuaji wa mabilioni ya pesa za Watanzania na mimi
nitumie fursa hii kujadiliana nanyi kuhusu nafasi ya Katiba katika
kuzuia ubadhirifu wa mali ya umma.
Kwa namna ninavyoona mambo yanakwenda Watanzania
tusipokuwa makini tutakuwa watu wa matukio, watu wanaoendeshwa kwa
matukio, kama tukikubali hali hiyo itakuwa jambo baya sana kwa taifa
letu. Matukio kama haya huwa ni matokeo ya chanzo fulani, matukio haya
huwa ni chanzo cha udhaifu wa mifumo yetu ya udhibiti pahala fulani. Kwa
sababu haiwezekani jambo likishatokea ndio tuulizane ilikuwa kuwa vipi,
nafuatilia mjadala wa Bunge ninaona kila anayezungumza ama anasema mtu
au taasisi fulani alipaswa kujua.
Haya mambo hayakufanyika kwa kutumia mbinu za
kijasusi, mbinu ambazo hutumia intelijensia ya hali ya juu kiasi kwamba
hata kama ulikuwa mlinzi anayelinda lango lakini mtu akapita katika
lango hilo pasina kuonekana. Jambo linaloendelea kujadiliwa bungeni wala
halikutokea kwa kificho au kutumia intelijensia ya hali ya juu kufanya
wanaotuhumiwa kutenda wasijulikane kwa namna yoyote, la hasha.
Hii inanipeleka katika hoja nyingine kwamba,
unapoona katika nchi yenye utawala wa sheria, mchana kweupe mambo
makubwa na ya kutisha hasa yale yenye nasaba na ubadhirifu wa mali ya
umma yanafanyika mchana kweupe basi hatupaswi kusubiri kuona mawingu
kujua mvua itanyesha.
Ninayaandika haya kwa maana ya kujifunza, hata
kama tungepata Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wazuri
kiasi gani, kama mifumo ya utawala wa nchi haijashonwa vema na kwa
umadhubuti kikatiba kazi yao njema ingeishia katika jitihada zao za
kibinadamu na kukosa usaidizi wa mifumo na taasisi za kikatiba. Binadamu
kwa asili amekuwa kiumbe ambaye bila kujitungia kanuni huwa ni msumbufu
kabisa, hata kama binadamu ni mwema kiasi gani, iwapo ataishi katika
mazingira yasiyo na kanuni basi wema wake utakuwa hatarini kughiribika.
Katika ulimwengu wa leo utaratibu wa kuenenda
katika jamii na Taifa lolote lile ni Katiba na sisi tumeamua kuandika
Katiba Mpya na Bora. Ni Katiba Mpya na Bora ndiyo pekee inaweza kuwa
silaha ya mwisho kuliangamiza joka ambalo limekuwa likitaga mayai kama
vile Epa, Majengo ya Benki Kuu, Richmond na haya ni mayai ambayo
tumeyaokota kweupe, bado hatuna hakika ya mayai ambayo joka ameyataga
kwenye mashimo, vichakani na mayai ambayo joka huenda akayataga hivi
karibuni tena. Sumu ya joka ni Katiba Mpya ambayo inatuwezesha wananchi
kutumia mamlaka yetu kuiwajibisha Serikali, Bunge na Mahakama. Nchi
ambazo zilipuuza kushughulika na joka kikatiba zimeishia kuwa mataifa
yaliyoshindwa “failed states”. Tusikubali kufika huko.
Matukio ya escrow na Katiba
Nitumie pia fursa hii kutoa rai yangu kwa
Watanzania kwamba, kuwa na Katiba Bora na inayotungwa na wananchi ndiyo
mwarobaini wa kuziba mianya ya ubadhirifu katika Taifa letu. Kuwa na
Katiba Bora ndiyo itakuwa salama yetu katika kuona wale tuliowapa
dhamana wanawajibika haraka iwezekanavyo pindi tuhuma za ubadhirifu
zinapotokea katika maeneo na mamlaka yao.
Sikiliza na usome pia, kwa namna ambavyo mjadala
wa sakata hili umejipambanua katika Bunge letu la Jamhuri je, unadhani,
viongozi wetu hawa watadiriki kwenda kutunga masharti makali na magumu
ya kuwawajibisha viongozi wanafanya ubadhirifu wa mali ya umma, ilhali
wao wenyewe ni viongozi wa umma wakati huo?
Nikuoneshe kidogo Rasimu ya Warioba ilisema hivi
katika suala la Maadili na Miiko ya Viongozi na Watumishi wa Umma, akiwa
katika kazi za ofisi au kazi binafsi au wakati amejumuika na watu
wengine, atahakikisha kwamba mwenendo wake: hauruhusu kutokea mgongano
wa masilahi kati ya masilahi binafsi na maslahi ya utumishi wa umma;
hauhatarishi masilahi ya umma kwa ajili ya masilahi binafsi; au
haushushi hadhi ya ofisi anayofanyia kazi. (2) Kwa madhumuni ya ibara
ndogo ya (1), mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha
Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kusimamia utekelezaji wa
masharti yanayohusu kanuni za uongozi wa umma. (3) Wadhifa wa “Kiongozi
wa umma” kama ulivyotumika katika Sehemu hii utajumuisha viongozi wa
kuchaguliwa (hii inamaanisha Rais, makamu wa rais, wabunge, madiwani
n.k) na kuteuliwa (Mfano, mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na
manaibu wao, wakurugenzi wa idara za Serikali n.k) kama
watakavyoainishwa kwenye sheria za nchi.
Ibara hii pamoja na mambo mengine imefutiliwa mbali na Katiba
Inayopendekezwa na zaidi ya yote masharti yake mahususi yakielekezwa
kutungiwa sheria na Bunge. Hebu nikuulize tena, juzi ijumaa Bunge
ilibidi liahirishwe baada ya wabunge kushindwa kutengeneza sentensi ya
pendekezo la hatua za kuchukuliwa kwa wale ambayo wanatuhumiwa katika
sakata la escrow, unadhani wabunge hawa watakaa na kutunga masharti
mahususi na makali yatakayowabana na kuwawajibisha wao dhidi ya
ubadhirifu ambao huenda baadhi yako wakaja kuufanya hapo baadaye? Jambo
la kuhuzunisha zaidi hata ile Ibara ndogo ya 2 inayosema Tume ya Maadili
ya Uongozi na Uwajibikaji kusimamia utekelezaji wa masharti yanayohusu
kanuni za uongozi wa umma hakuna tena.
Yaani tunarudi kule kule ambako Secretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma isiyo na meno ambayo wananchi waliipigia
kelele sana kwamba kuna tuhuma nyingi kuliko masuala yanayoshughulikiwa
na sekretarieti hiyo na hasa hasa wananchi wakaweka msisitizo kwa wale
watuhumiwa wakubwa wakubwa.
Matukio ya escrow na maadili
Masharti mahususi yafuatayo kuanzia 203(2)(b)(e)
hadi (o) yamefutwa kutoka katika Rasimu ya Warioba na hayamo katika
Katiba Inayopendekezwa.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya jumla ya ibara
ndogo ya (1), majukumu mahususi ya Tume yatakuwa ni: (b) kufanya upekuzi
kwa kushirikiana na taasisi nyingine; (e) kutoa ushauri juu ya masuala
ya ubadhirifu wa fedha kwa mamlaka husika; (f) kufanya upekuzi kwa
kiongozi wa umma anayepewa dhamana kabla ya kuingia madarakani; (g)
kutoa elimu kwa umma kuhusu maadili na miiko ya viongoziwa umma; (h)
kufanya uchunguzi kwa uamuzi yake yenyewe, au baada yakupokea malalamiko
kutoka kwa mtu yeyote, kutokana nakutenda au kutokutenda kwa kiongozi
wa umma au mtumishi (i) yeyote wa umma, au wakala wa Serikali, ikiwa
kitendo kilichotendwa au kutokutendwa ni kinyume cha maadili ya umma;
(j) kumwelekeza, baada ya kupata malalamiko au itakapoona inafaa,
kiongozi wa umma au mtumishi wa umma, taasisi auwakala wa serikali au
chombo chochote cha umma kufanya jambo lolote linalotakiwa na sheria,
kuacha, kuzuia au kusahihisha utendaji mbaya au usiyo sahihi wa majukumu
yake;
(k) kutoa ushauri kuhusu kuchukuliwa hatua
kiongozi wa umma au mtumishi wa umma; (l) kumwelekeza kiongozi wa umma
au mtumishi wa umma, kwa mujibu wa sheria za nchi, kutoa nyaraka
zinazohusiana na matumizi ya ofisi, matumizi ya fedha au mali za umma,
au kutoa taarifa ya matumizi mabaya kwa Tume, kwa hatua stahiki; (m)
kuomba msaada au taarifa muhimu kutoka kwa mamlaka yoyote ya Serikali au
binafsi katika kutekeleza wajibu wake,na kukagua kumbukumbu muhimu na
nyaraka husika; (n) kwa kuzingatia sheria, kutangaza kwa umma, mambo
yote yanayohusiana na uchunguzi uliofanywa na Tume, iwapo mazingira
yanaruhusu; (o) kuchunguza jambo au mazingira yoyote yanayokiuka au
kusababisha ukiukaji wa maadili.
Ninapofuatilia sakata hili sishangai sana kwanini
masharti haya mahususi yameondolewa na badala yake Katiba
Inayopendekezwa ikasema katika ibara yake ya 231(3) kwamba “Bunge
litatunga sheria kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Ibara hii”.
Mtu yeyote mwenye mapenzi mema na nchi yetu na
anayependa kuona tunasifika kwa vivutio vya kitalii na siyo ufisadi kwa
hakika atahakikisha Katiba Inayopendekezwa inaboreshwa na kurudisha
masharti haya muhimu. Aidha, ikumbukwe kwamba ili Katiba Inayopendekezwa
iboreshwe Sheria ya Kura ya Maoni inasema katika kifungu chake cha 35,
kwamba Katiba Inayopendekezwa ikipata kura za “hapana” itakuwa ni fursa
ya kuiboresha kabla haijapelekwa katika duru ya pili ya Kura ya Maoni.