Friday 31 October 2014

Mkapa atoa ya moyoni rais 2015

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, amezungumzia mbio za kuwania urais wa 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitaja sifa za mtu anayepaswa kuteuliwa kuwa mgombea wake, ikiwamo ya kukubalika na kuuzika kwa jamii.

Amesema kukubalika na kuuzika kwa mtu katika siasa kunatokana na utendaji, haiba, wasifu na ushawishi wa mtu huyo ndani ya chama na serikalini na kwamba, umri siyo kigezo cha kuangaliwa ingawa siyo dhambi vijana wakajitokeza kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Mkapa, ambaye anasifika kwa kuwa kiongozi jasiri na asiyemung’unya maneno, alisema hayo wakati akihojiwa na televisheni ya Citizen ya nchini Kenya, kwa njia ya simu.

Alikuwa akihojiwa juu ya kifo cha Rais wa Zambia, hayati Michael Satta, aliyefariki dunia, jijini London, nchini Uingereza Jumanne wiki hii.

Katika mahojiano hayo, Mkapa pia aliulizwa na mwandishi kuhusu Tanzania kutazamiwa kufanya uchaguzi mkuu mwakani huku mambo mengi yakisikika, hasa kwa wanaojitokeza kupitia CCM kutaka kuwania urais katika uchaguzi huo hadi wengine kufikia kuadhibiwa na chama.

Kabla ya kujibu, Mkapa alianza kwa kucheka na kisha akasema anachelea kupata jibu sahihi kuhusiana na swali aliloulizwa na mwandishi.


“…Ila niseme CCM ni chama kikongwe na kina hazina kubwa ya kutosha. Na Katiba ya chama chetu inaelezea kuhusu dhumuni la chama chetu, kubwa ikiwa ni kuhakikisha tunakamata dola, kuanzia serikali za mitaa mpaka serikali kuu. Sasa swali ni kwamba, dola inakamatwaje?” alihoji Mkapa.

Aliongeza: “Chama kama chama lazima muwe na mtu anayeuzika na kukubalika katika jamii kwa utendaji wake, haiba yake, wasifu wake (ndani ya chama na serikali).

“Lakini vile vile, ushawishi wake...Haya mambo ya umri na kadhalika, sisi hatukutazama wakati huo. Ila siyo dhambi vijana wakijitokeza. Maana yake hata wakati wangu, Rais wa sasa Mheshimiwa Kikwete na kina Lowassa walijitokeza. Na leo unaona Kikwete ndiye Rais.”


Alisema wakati wa utawala wake, viongozi wenzake wengi walihisi na kuamini kuwa hakuwa akimuunga mkono Rais Kikwete.

“Lakini mwandishi, nataka nikuhakikishie, hata kama mimi Ben Mkapa siko na Kikwete, mwisho wa siku wanachama ndiyo watakaosema wewe humtaki ila sisi tuachie huyo huyo...,” alisema Mkapa. 

Aliongeza: “Na hayo yalijitokeza mwaka 2005. Watu walimtaka Mheshimiwa Kikwete. Sasa mimi kuwa mwenyekiti wa chama hakunipi Mandate (mamlaka) ya kushindana na walio wengi. Na mliona (Kikwete) alishinda kwa asilimia kubwa kweli kweli”.

“Hivyo CCM ina taratibu zake na wanajua nani anafaa. Maana yake siasa hizi, tuhuma zingine za kipuuzi kweli kweli. Sasa mkiendekeza tuhuma, mwishowe mnakuta mnabaki bila chama. Na kwenye siasa mkianza kutuhumiana, hakuna wa kusimama...”

Alisema yeye binafsi, anaamini chama kitapata mtu safi, mwenye nguvu ya kukisaidia chama na serikali na kuendeleza yatakayoachwa na Rais Kikwete.

Mkapa alisema hakuna chama duniani kinachoona fulani atakivusha halafu kimwache na kusema kufanya hivyo, maana yake ni kukiua chama.

“Hivyo, hata sisi vyombo vyetu vya ndani vilikuwa vinatueleza kabisa kwamba, fulani yuko vizuri sana. Ila labda kuna aka katatizo. Sasa ako katatizo tunakafanyia kazi kwa maslahi ya chama na kwa maslahi ya huyo ajaye,” alisema Mkapa na kuongeza kuwa ana amini ndivyo ilivyo mpaka sasa.

Alisema tafiti zimefanyika na kwamba, anaamini wamesikika watu wakisema wanamtaka nani.

“Na wakati wangu mimi mgombea alikuwa ameshatungiwa nyimbo na watu mbalimbali wenye mapenzi naye. Hivyo, labda hata sasa yaweza kuwa hivyo...Waswahili walisema nyota njema huonekana asubuhi,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Nimalizie kama nilivyosema, ukongwe wa CCM na viongozi wake, naamini watapata mtu bora na mwenye nia njema na Taifa hili...”

Akijibu kuhusu wana CCM waliotajwa kwamba, anaamini yupo mmoja au wawili, ambao ameona wanaweza ama kufuata nyayo zake au za Mwinyi au za Mwalimu Nyerere au za Rais Kikwete, kwanza alianza kwa kucheka.

Baada ya kicheko, Mkapa alisema Tanzania kuna Kamati ya Maadili na kwamba, yeye na wenzake hivi sasa kikatiba ni wazee washauri, hivyo akasema vikao vya chama ndivyo vitakavyowaongoza na baada ya hapo, nao wanaenda na mtu huyo huyo.

Makada wa CCM waliowahi kutuhumiwa kuanza kampeni za kuwania urais mwaka 2015 kabla ya kuzuiwa na chama kupitia Kamati yake Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kujihusisha na suala hilo kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa, ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Wengine ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira.

Yumo pia aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pia hivi karibuni alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akitangaza nia yake ya kuwania urais 2015. Mwingine aliyekwisha kutangaza nia ya kuwania urais mwakani ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla.

KUHUSU USHIRIKIANO WA VYAMA VYA UPINZANI (UKAWA)

Akijibu swali kuhusu ushirikiano uliosainiwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD wa kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi, kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa hadi urais kama ilivyokuwa kwa Kenya, Mkapa alisema bado hajajua
sera za vyama hivyo na namna makubaliano yao yalivyo.

Alisema pia bado hajaelewa kama inawezekana kuufananisha ushirikiano wa vyama hivyo na muungano wa Coard na Jubilee uliokuwapo nchini Kenya.

“Otherwise I'd like to wish them all the best (vinginevyo ningependa kuwatakia kila kheri),” alisema Mkapa na kumfanya mwandishi aangue kicheko.

KIFO CHA RAIS SATTA

Akimzungumzia hayati Rais Satta, Mkapa alisema hakuitwa “King Cobra” kimakosa, bali alistahili kutokana na uwezo aliokuwa nao ama wa kimaamuzi au wa kimsimamo.

“Nina hakika sana kwamba Wazambia na sisi kama Mataifa ya Afrika tutamkumbuka daima ndugu Satta. Satta daima alikuwa kwa ajili ya watu wake na Bara letu kwa jumla. Alisema na kusimamia kile alichokiamini kuwa ni cha kweli na chenye mafanikio, Satta ataendelea kuwa kiongozi mzuri daima,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Hivyo, maumivu yanayotukabili kwa kumpoteza Mzee Nyerere, Mzee Nkrumah, Mzee Mandela, Mzee Kenyatta ni sawa na yale yanayotukabili leo tunapomjadili Mheshimiwa Satta (Inatosha kusema kwamba tumempoteza shujaa mwingine katika Bara letu) Naitakia roho yake mapumziko ...”

Akijibu swali namna anavyoziona siasa za Afrika akiwa Rais mstaafu, Mkapa alisema ni kawaida na hana jambo kubwa la kusema japo kuna mengi yanatokea, ambayo mengine ni ya hovyo.

“Mathalan, Waafrika wazee wetu, walipigania sana ukombozi wetu. Ila nadhani wengi bado kuna watu wana matatizo na wanahitaji kukombolewa kifikra,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Maana yake kuna wenzetu wanatumika pasipo kujua na kusababishia nchi zao kuingia katika matatizo, kama vita na wengi wao wameanza kujuta”.
“Hivyo, ni lazma ifikie mahali watu waweze kujitambua na kujua ni yepi malengo mema kwa Bara letu ni yepi tunashinikizwa...” aliongeza kusema Mkapa.

Lowassa amuombea radhi Sitta kwa Kanisa

Wakati Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (MBK) ikitarajia kuingia katika hatua ya kura ya maoni mwakani, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameibuka na kuliomba radhi Kanisa Katoliki kufuatia mgongano iliyojitokeza kati ya kanisa hilo na baadhi ya viongozi serikali na wa Bunge hilo.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliomba msamaha huo wakati akitoa salamu zake katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge, mkoani Morogoro.

Alisema Kanisa Katoliki lina mchango mkubwa katika kudumisha amani na mshikamano nchini, hivyo mambo yaliyojitokeza yanapaswa kusamehewa.

“Najua hivi karibuni tumewaudhi, lakini mimi naomba mtusamehe bure tu, kama vile mzazi anavyomsamehe mtoto wake anapokosea,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa Kanisa Katoliki ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

Ingawa Lowassa hakueleza kwa undani tofauti zilizojitokeza kati ya Kanisa hilo na baadhi ya viongozi wa serikali, lakini  wakati BMK likiendelea, taasisi za dini zilisambaza waraka uliosainiwa na viongozi wake ukilikosoa Bunge hilo kwa mambo mbalimbali ikiwamo kuendelea kujadili rasimu bila maridhiano kutokana na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia.

Kadhalika, viongozi wa madhahebu hayo ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT) na Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), walilikosoa BMK kwa kupuuza maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Waraka huo ulisababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kujiweka katika wakati mgumu kwa kuzua mgogoro dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo, baada ya kuita waraka huo kuwa ni wa kipuuzi na wa hovyo hovyo.

Sitta ambaye alitoa kauli hiyo Oktoba Mosi mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa waraka wa maaskofu una lugha ya Ukawa, ingawa maaskofu kwa upande wao waliueleza kuwa ni waraka wa kinabii, kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.

Sitta alitoa kauli ya kuuponda waraka huo bungeni alipokuwa akielezea mwenendo wa upigaji kura za kupitisha ibara na sura za rasimu ya katiba iliyopendekezwa kabla ya upigaji wa kura na wakati wa kutangaza matokeo, akisema watu wa Mungu kama maaskofu hawawezi kutoa waraka kama huo na kudai kuwa amekuwa akituhumiwa kwenye mitandao kwamba anadharau maaskofu.

“Nimalizie na viongozi wangu wa kiroho…mababa zangu maaskofu, natuhumiwa sana kwenye mablog kwamba nadharau maaskofu. Wakiwa na matendo kama hayo hao baadhi ya maaskofu itabidi tuendelee kuwadharau,” alisema na kuongeza:

“Ninao waraka huu ambao umelazimishwa kutumwa katika makanisa. Sioni utukufu wa Ukristo katika waraka huo. Huu waraka unamwamuru Rais airudishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba.”

 Kuna Ukristo hapa?” alihoji na kuendelea: “Waraka huu unamlazimisha Rais asitishe mchakato wa Bunge Maalum…tangu lini watu wa kiroho wanatoa maagizo ya kisiasa? Hii sio haki hata kidogo…kuna Ukristo hapa? Waraka una lugha za wale Ukawa tuliowazoea.”

“Hivi kweli maaskofu wa Kikristo wanaweza kusema kwamba Wizara ya Katiba na Sheria irudishe tovuti ya Tume ya Jaji Warioba na kuirejeshea nyaraka zake zote ili wananchi wasome na kujifunza?” alihoji Sitta.

“Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauriwa na chama tawala, hivyo basi Bunge la Katiba lijadili na kuboresha tu rasimu ya katiba na si kubadilisha,” alisema Sitta.

“Waraka huu kwa shinikizo la maaskofu umesambazwa kwenye makanisa na kusomwa. Mimi nasema kama Mkristo, tukianza kuruhusu nchi yetu kutoa nyaraka hizi za kisiasa zisomwe makanisani kwa kudai huo ni msimamo wa maaskofu, basi nchi hii tutaipeleka kubaya.

“Na mini kama mtu mzima lazima nionye kuhusu tabia hii, ukizingatia nchi hii haina dini, hawa baadhi ya maaskofu ambao walikusanywa Dar es Salaam na makundi yale yale yanayohusishwa na Ukawa, kama wao ni wanachama wa siri wa vyama vya siasa vinavyochukia CCM wajitokeze waziwazi,” alisema Sitta.

Sitta aliendelea kunukuu waraka huo kwamba kuna askofu mmoja ameapa kwamba atawaelimisha waumini wake ili siku za usoni wawashughulikie viongozi kama mimi (Sitta). Nasema aendelee, lakini Mungu anaona yote yaliyo moyoni mwetu.”

Baada ya Sitta kutoa kauli hiyo, Askofu wa Jimbo la Katoliki la Bunda, Mhashamu Renatus Nkwande, alisema matamshi ya Sitta yanaonyesha anavyohangaika kualalisha kilicho haramu.

Alisema kitendo cha Sitta kuendesha BMK kwa kukejeli wajumbe wenzake walioondoka bungeni (Ukawa) na wajumbe walioandaa rasimu ya pili kwenye Tume ya Katiba Mpya chini ya Jaji Joseph Warioba, ni jambo la aibu ambalo halivumiliki, na ndiyo maana walitoa waraka wa kutokubaliana nacho.

“Kwa kweli Sitta ametutukana, ametafuta ubaya kwa viongozi wa dini, kwa kuwa tumesema ukweli ? Sisi tulikuwa tunatimiza wajibu wetu kwa Wakristo …tulizungumza kutokana na hitaji la wakati, na ulikuwa waraka wa unabii,” alisema.

Viongozi wengine wa kanisa Katoliki waliojibu kauli za Sitta ni Makamu Mwenyekiti wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, ambaye alinukuliwa akisema kuwa Sitta amelewa madaraka.

JK: Watendaji wakuu wananikwamisha

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amewatuhumu baadhi ya watendaji wa serikali yake kuwa ni kikwazo katika kufanikisha masuala mbalimbali ya maendeleo kutokana na urasimu usiokuwa wa lazima katika kutoa huduma kwa wananchi.
Akifungua kongamano la miaka 10 ya Tume ya Utumishi wa Umma Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alikemea na kulaumu tabia ya baadhi ya watendaji hao wa Serikali ambao wamekuwa wakikwamisha kwa makusudi kasi ya viongozi wa kisiasa ya kuleta maendeleo.
“Katika utendaji wa baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali limekuwa ni tatizo na wamekuwa wakikwamisha sana kasi ya utekelezaji wa haraka wa malengo ya kisiasa,” alisema.
“Mara nyingine, viongozi wa kisiasa wamekuwa mbele kimtazamo kuliko watumishi wa umma, hili limekuwa tatizo sana katika utekelezaji wa malengo kwa haraka,” alisema Kikwete.
Alisema kumekuwa na malalamiko kwa makatibu wakuu wa wizara kutoka kwa wawekezaji ambao huwachelewesha kwa makusudi kwa visingizio vya kufuata utaratibu.
Alisema katika kufuatilia, amekuwa akilazimika kuingilia utendaji wa baadhi ya wizara ili kuhakikisha mambo yanakwenda na mara nyingine urasimu huo umekuwa ukifanywa kwa makusudi ili kuwachosha wawekezaji na ‘kuwatoa upepo’ kwa manufaa binafsi.
“Haya ni malalamiko makubwa sana na yanatoa picha mbaya kwa nchi yetu…watendaji wa namna hii ni lazima wabadilike, ninahitaji kuona mabadiliko makubwa kwa kupitia Tume ya Utumishi ambayo inatakiwa kukaa na hawa watumishi na kuwapa mafunzo ya kiutendaji yanayoendana na mahitaji ya sasa,” alisema.
Abeza zawadi ya uprofesa
Akizungumzia utaratibu wa upandishwaji vyeo, Rais Kikwete alisema ni muhimu weledi ukazingatiwa na utaratibu uliowekwa ukaheshimiwa, kwamba lazima wafanyakazi wapandishwe vyeo na madaraja ndani ya kipindi kilichowekwa, ambacho ni miaka mitatu.
Alisema kumekuwa na malalamiko kwa wafanyakazi wengi wa Serikali kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na hata wanapopandishwa vyeo mabadiliko ya mishahara kuendana na vyeo na madaraja mapya hayafanyiki kwa wakati.
Alieleza kwamba utaratibu unaotumika katika vyuo vikuu wa namna ya kuwapata wahadhiri wasaidizi, wahadhiri, maprofesa ni wa wazi na ni mfano wa kuigwa kutokana na namna unavyofanyika, kwa kutoa mafunzo kisha kuyathibitisha na kumpandisha mhusika daraja.
“Vyuo vikuu wana ngazi wanazotakiwa kuzipitia na mafunzo maalumu hadi mtu anakuwa profesa. Siyo honorary professor (uprofesa wa heshima) niliopewa mimi nilipokwenda China…walinishtukiza. Nilifika pale wakanipiga na uprofesa, nikasema haya sasa makubwa! (kicheko),” alisema.
Alisema matatizo ya upandishwaji vyeo yasipotatuliwa kwa wakati ni tatizo kubwa kwa Serikali hasa unapokutana na vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu kama Chama cha Walimu na wanapofikia hatua ya kusema wanagoma, unalazimika kuwaangukia.
Alisema suala la mtumishi kupandishwa cheo ni haki yake ya msingi kazini hivyo hatarajii kusikia matatizo ya malalamiko ya watumishi kutopanda vyeo kwa wakati.

Ukawa na dhana ya nguvu ya mnyonge au ‘zamu yetu kula’

Dar es Salaam. Kwa jumla, kuungana ni jambo jema kwani muungano huongeza nguvu. Muungano ni silaha ya mnyonge dhidi ya mwenye nguvu.
Ni kwa sababu hii, tumekuwa tukipigania umoja wa Afrika ili kujenga nguvu ya pamoja dhidi ya mabeberu wa mataifa ya Magharibi tukiamini kwamba bila nguvu moja mataifa ya Afrika hayataweza kuukabili ubeberu wa mataifa haya.
Tunao msemo maarufu usemao nguvu ya mnyonge ni umoja na hivi ndivyo waasisi wa mataifa ya Afrika walivyofanya katika kumfukuza mkoloni.
Bila kujali tofauti zao za kikabila na vinginevyo, wananchi wa Afrika waliunganisha nguvu na hatimaye pamoja na silaha zao duni, wakafanikiwa kumfukuza mkoloni katika ardhi ya Afrika.
Katika uwanja wa siasa, vyama vya siasa huungana kwa sababu mbalimbali lakini sababu tatu ni za msingi zaidi. Mosi, huungana pale ambako hakuna chama kinaibuka na ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi ulio na ushindani mkali.
Katika mazingira haya, inakuwa hakuna chama kinachoweza kuunda serikali imara peke yake bila kushirikisha kingine kwa sababu hakitaweza kupitisha sera au sheria yoyote bungeni.
Hivi ndivyo vyama vya Conservatives na Liberal Democrats vilivyoungana huko Uingereza baada ya vyama vikuu nchini humo vya Labour na Conservatives kushindwa kupata ushindi ambao ungekiwezesha chama kimojawapo kuunda serikali na kupitisha sera bungeni bila msukosuko mkubwa.
Hivi ni vyama ambavyo vina itikadi na msimamo tofauti kabisa kifalsafa na ilibidi viongozi wake wakae saa nyingi kukubaliana programu ya kutekeleza kabla hawajakubaliana kugawana nafasi za uongozi.
Kiongozi wa Liberal Democrats, Nick Cleggy alimshinikiza David Cameroon akubaliane na masharti ya kulegeza misimamo mikali ya chama chake kuhusu sera ya uhamiaji na hifadhi ya jamii kabla hajakubali kuingia naye ubia kuunda serikali.
Cameron amekiri mara kadhaa kwamba alilazimika kulegeza msimamo kuhusu sera mama za Conservatives ili kufanikisha kuwashawishi Liberal Democrats kuunda nao serikali vinginevyo Nick Cleggy angeunda serikali na Gordon Brown wa chama cha Labour.
Ni katika mazingira ya chama kimoja kushindwa kupata ushindi wa wazi ambayo yalivilazimisha vyama hasimu vya CUF na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar.
Pamoja na kwamba SUK iliundwa kama njia sahihi ya kuepusha shari na vita visiwani, msingi wa serikali hiyo ni ukweli kwamba hakuna chama chochote kati ya hivi viwili chenye uwezo wa kuunda serikali imara kwa sababu ushindi wa chama chochote huwa ni mwembamba. Hata hivyo, hatujui ni kwa kiwango gani vyama vya CUF na CCM huko Zanzibar vilikubaliana kutekeleza programu ya pamoja inayotokana na sera za vyama hivyo viwili.
Sababu ya pili ya vyama kuungana ni kuunganisha nguvu katika jitihada za kumwondoa adui anayefanana.
Kwa mfano, huko Zanzibar kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964, vyama kadhaa viliungana katika jitihada za kuuondoa utawala wa Sultani uliokuwa unaendeshwa kibaguzi. Kwa hiyo, adui hapa alikuwa Sultani na ubaguzi wake wa rangi.
Sababu ya tatu ni pale vyama vinapounganisha nguvu ili kushinda uchaguzi kwa kutambua kwamba vikiingia kwenye uchaguzi kimoja, kimoja havitaweza kushinda kutokana na nguvu kubwa aliyonayo mshindani wao.
Hata hivyo, kushinda uchaguzi hakuwezi kutokana na kuunganisha nguvu ya kiuongozi pekee. Ni lazima kuunganisha pia nguvu ya kiitikadi, kifalsafa na kisera ili kuweza kujipambanua kwa wananchi.
Muungano wa kisera ni muhimu ili kuweza kutabirika tabia za wagombea watakapokuwa madarakani. Aidha, ni programu ya kisera inayoweza kuongoza kuchagua mgombea anayefaa zaidi kushika usukani wa utekelezaji wake baadaye.
Muungano wa vyama vinavyounda Ukawa umepokewa kwa shangwe kubwa. Furaha hii inatokana na msingi nilioueleza hapo awali kwamba wanyonge wakiungana hupata nguvu ya ajabu hata ya kuweza kuangusha milima.
Kwa hiyo, watu ambao wamekuwa wakisubiri utawala wa CCM kuanguka wanaamini kwamba kwa muungano huu angalau vyama vya upinzani vitafuta unyonge.
Nami naungana na Watanzania wengine kuwapongeza viongozi wa vyama ya Chadema, CUF, NCCR na NLD kwa ujasiri na uthubutu waliouchukua katika kujaribu kushirikiana katika chaguzi mbalimbali zijazo.
Lakini tunapowapongeza Ukawa, ni vizuri kutambua kwamba kuunganisha nguvu kama walivyofanya ni hatua moja tu inayopaswa kuanzisha hatua nyingi huko mbele. Hatua muhimu inayofuata sasa ni kujipambanua kwa wananchi kiitikadi, kifalsafa na kisera.
Kwa bahati viongozi wa sasa wa vyama vilivyoungana siyo watu wanaoamini katika mambo ya itikadi na falsafa.
Hawa ni viongozi ambao huitwa ‘wayakinifu’ (pragamatists). Myakinifu ni kiongozi anayeamini katika kinachowezekana leo na haongozwi na falsafa bayana ya kisiasa.
Kwa hiyo kiongozi yakinifu atambeba yeyote anayeona anafaa na huwezi kumuweka katika mrengo wowote kiitikadi. Kimsingi, hii ndiyo aina ya viongozi tulionao sasa tangu Mwalimu Julius Nyerere alipoondoka.
Ndiyo maana tumekuwa Taifa ambalo si la kijamaa, wala kiliberali wala kibepari. Tupotupo tu maadamu siku zinakwenda.
Pamoja na uyakinifu wao, bado naamini kwamba Ukawa watahitaji programu ya pamoja ya kisera. Hii ni hatua muhimu ili kutoa nafasi kwa wananchi kupima aina ya serikali watakayounda kama watashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Bila msimamo yakinifu wa kisera, ni rahisi kutofautiana kwa sababu ya kukosa msingi wa kugawana madaraka. Bila sera yakinifu, utakapofika wakati wa kugawana nafasi za kugombea na hatimaye katika kuunda Serikali watalazimika kuzingatia sifa za kuchagulika na umaarufu badala ya sifa za kiuwezo.
Nakumbuka mwaka 2005 palipokuwa na jitihada za kuunda ushirikiano kama huu wa sasa, nilipewa jukumu la kufanya utafiti kujua nani alikuwa anakubalika zaidi katika Jimbo la Ubungo kati ya mgombea wa Chadema (John Mnyika) na mgombea wa CUF (marehemu mama Minja).
Niliandaa hojaji na nikaligawa katika kata zote za Jimbo la Ubungo kwa kutumia sampuli iliyopatikana kwa njia ya bahati nasibu. Matokeo yalionyesha kwamba Mnyika alikuwa anakubalika kwa mbali dhidi ya wagombea wengine wa upinzani.
Hata hivyo, katika kikao cha kujadili matokeo hayo, wawakilishi wa CUF waliyakataa na kunituhumu kwamba nilikuwa napendelea chama changu na huo ndiyo ukawa mwanzo wa ushirikiano kusuasua na hatimaye kusambaratika kabisa kabla ya kampeni kuanza.
Yote hii ni kwa sababu tuliwekeza zaidi kwenye kugawana wagombea lakini hatukuwekeza kabisa katika ushirikiano wa kisera.
Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba, muungano wowote endelevu wa vyama vya siasa Tanzania, lazima uwe wa kuunganisha nguvu za wanyonge dhidi ya mabavu ya chama dola cha CCM.
Muungano wa namna hii lazima uwaunganishe kisera Watanzania na ndiyo unaopaswa kuwa msingi wa kugawana vyeo.

Lipumba: Kwanza CCM ing’oke, ruzuku baadaye

Dar es Salaam. Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akisema suala la ruzuku na viti maalumu ni changamoto kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hicho si kipaumbele.
“Tunachokitaka ni kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha tunaing’oa CCM madarakani kwanza, masuala mengine kuhusu ruzuku tutaweka utaratibu maalumu baadaye,” alisema.
Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililokutana Jumatatu na Jumanne iliyopita.
“Wenzetu Kenya waliweza kuungana na kuhakikisha wanaking’oa chama tawala madarakani, lakini sasa kwa hapa mkiungana na kuwa chama kimoja ni lazima msajili chama chenu, sasa tunachokitaka ni kushirikiana tu kwanza,’’ alisema.
Alisema suala la ruzuku na uteuzi wa viti maalumu siyo lengo kuu la Ukawa inayoundwa na vyama vinne; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD kwa kuwa linajadilika. Alisema jambo la msingi hivi sasa ni ushirikiano wa amani.
Alisema kinachotakiwa kwa viongozi wa Ukawa ni kuaminiana kwanza ili kulinda muungano huo ambao alisema umeshaanza kukitikisa chama tawala, CCM.
Maazimio ya Baraza Kuu
Alisema Baraza hilo lilisisitiza umuhimu wa kuaminiana miongoni mwa vyama washirika katika ngazi zote ili kudumisha umoja huo na kufikia lengo la kuitoa CCM madarakani.
“Baraza limetaka uwepo utaratibu mzuri na wa wazi utakaoonyesha mambo ya msingi ambayo vyama vinavyounda Ukawa vimekubaliana. Utaratibu huu uwafikie viongozi wa ngazi zote za chama ili kuhakikisha jukwaa la Ukawa linatumika kwa lengo na dhamira iliyopo ndani ya hati ya makubaliano ambayo ni kuing’oa CCM madarakani,” alisema.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa Profesa Lipumba alisema Baraza limetaka sheria irekebishwe ili uchaguzi wa diwani ufanyike pamoja na wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji kwa wakati mmoja, kwa vile diwani ndiye kiongozi mkuu wa kuchaguliwa wa kata.
Baraza hilo pia limetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iratibu na kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na utengenezwe utaratibu ambao utaifanya Tume hiyo kuwa huru kuwezesha chaguzi zote zijazo kufanyika kwa uhuru na haki.
“Taarifa za Tume zilieleza kuwa itaandikisha wapigakura mpaka kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji, kwa hiyo uchaguzi wa Serikali za Mitaa usubiri mpaka daftari la kudumu la wapigakura likamilike na ndilo litumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema.
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu la CUF, limesikitishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha kupitishwa na kutangazwa kwa katiba hiyo na Bunge la Katiba lililoongozwa na Samuel Sitta akisema halikuzingatia sheria na taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
“Ni ukweli usiofichika kwamba mchakato mzima wa kupitisha katiba haukuwa na mwafaka wa kisiasa, kanuni za uendeshaji wa bunge hilo zilikiukwa na Katiba yote inayopendekezwa haikupigiwa kura ya mwisho,” alisema
Profesa Lipumba alisema, katika vikao vya ushauriano na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Rais Jakaya Kikwete alikubaliana na viongozi hao kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya, hususan kura ya maoni uahirishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
“Mwanasheria wa Serikali alitangaza kura ya maoni Machi 30, Rais akiwa China alisema Aprili, yaani tayari tarehe imeshatangazwa kabla hata ya daftari la wapigakura kukamilishwa,” alisema.
Alisema baraza hilo pia limesikitishwa na utaratibu unaofanywa na NEC juu ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapigakura akisema hadi sasa hatua za uandikishaji hazipo wazi na wadau wengi hawana taarifa za kutosha juu ya nini kinaendelea.
Alisema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012, zinaonyesha kuwa kuna vijana zaidi ya milioni 4.6 ambao watafikisha umri wa kuwa wapigakura kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 lakini bado hawajapewa fursa ya kuandikishwa huku wananchi wengi wakiwa wameshapoteza vitambulisho vya kupigia kura.
Alisema Juni, 19 mwaka huu, Nec, ilitangaza kufuta matumizi ya vitambulisho vya kupigia kura vya sasa na badala yake itatumia teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), ikiwa ni maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alinukuliwa akisema katika Kura ya Maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu, mpigakura atatumia kitambulisho kipya baada ya kuandikishwa upya katika mfumo huo na si vinginevyo.
Pia alisema Baraza Kuu linalaani vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na sheria vinavyoendelea kufanywa na Serikali kwa kulitumia Jeshi la Polisi.
Alitoa mfano wa masheikh waliokamatwa Zanzibar na kuhamishiwa Dar es Salaam na kufunguliwa kesi akisema walijitokeza mbele ya Mahakama na kusema waziwazi kwamba wamefanyiwa mateso na vitendo vya kinyama lakini hakuna hatua zilizochukuliwa ikiwamo kupelekwa hospitali.
Kadhalika, alisema baraza hilo limepokea kwa mshangao taarifa za utoaji wa uraia unaofanywa na Serikali kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi. Alisema uamuzi wa kuwapa uraia wakimbizi katika majimbo yanayoongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani ni mbinu ya kudhoofisha upinzani kwa kuwa wakimbizi wanaopewa uraia wanahamasishwa kuwa wachague chama tawala.
Kuhusu ardhi alisema: “Pamoja na Tanzania kuwa na ardhi ya kutosha kwa raia wake, ugawaji wa mapande makubwa ya ardhi kwa wawekezaji yataleta mtafaruku wa uvunjifu wa amani na kuwafanya raia wazawa kuwa maskini wa kudumu,’’ alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu maradhi hatari ya ebola, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu limeitaka Serikali kuwa makini ili usiingie nchini akisema limesikitishwa na taarifa ya kwamba mpaka sasa nchi haina vifaa vya kuthibitisha kuwapo kwa vimelea vya ebola.

Monday 27 October 2014

KNCU wamlaumu mrajisi wa vyama

Moshi. Chama Kikuu cha Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), kimemjia juu mrajisi wa vyama hivyo nchini kwa kile ilichodai kukwamisha ustawi na maendeleo yake.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa KNCU, Maynard Swai wakati akisoma hotuba yake katika mkutano mkuu maalumu ulioitishwa kwa shinikizo la mrajisi huyo, Dk Audax Rutabanzibwa.
Licha ya kupokea lawama hizo, Dk Rutabanzibwa aliyekuwa mwenyekiti katika mkutano huo hakuweza kujibu malalamiko yaliyoelekezwa kwake na mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo aliwaachia wajumbe wa mkutano huo kufanya uamuzi kwa njia ya kura kama bodi ya uongozi iendelee au ing’oke ambapo kura 83 zilikataa na 68 zikitaka ing’oke.
Swai alisema ofisi ya mrajisi huyo imekuwa kikwazo cha maendeleo kwa KNCU .
“Mfano, shamba la Garagagua lilitakiwa kuuzwa Mei 2014, wajumbe mlisharidhia lakini kutokana na ukiritimba wa ofisi ya mrajisi imekwama,” alisema Swai. Swai aliitaja mipango mingine kuwa ni ujenzi wa hosteli ya kisasa na hoteli kwenye eneo la makao makuu ya KNCU.
“Sina nia ya kuifundisha au kuikumbusha ofisi ya Mrajisi wajibu wake kiutendaji lakini ina wajibu wa kushauri na kusimamia ushirika ili uendelee kushamiri nchini kwa manufaa ya wanachama,”alisema.
Lakini Swai alisema hata tume mbalimbali za uchunguzi zilizotumwa KNCU katika kipindi kifupi cha miaka miwili na Mrajisi, hazijawahi kutoa mrejesho wa matokeo ya uchunguzi huo.
“Kifungu 57(1) cha sheria namba 6 ya Ushirika ya mwaka 2013 imeweka bayana kuwa ikiwa kuna uchunguzi au ukaguzi umefanywa dhidi ya chama cha Ushirika, Mrajisi atapaswa kutoa matokeo ya uchunguzi huo,”alisema Swai.
KNCU kimeshangazwa pia na hatua ya Mrajisi kutoamini ukaguzi uliofanywa na COASCO ambacho ni chombo cha Serikali kuhusu kiasi cha hasara ambayo KNCU ilipata wakati wa mdororo wa uchumi duniani mwaka 2008.
Katika hesabu hizo, KNCU ilionyesha kupata hasara ya zaidi ya Sh765 milioni wakati uhakiki uliofanywa na hazina ulionyesha KNCU kilipata hasara ya Sh250 milioni.
“Mrajisi aliagiza kufuatiliwa kwa tofauti hii huku akionesha kutokuwa na imani na hesabu zilizokaguliwa na COASCO jambo ambalo linashangaza kama Serikali haiwezi kuamini kazi iliyofanywa na chombo chake,” alisisitiza Swai.
Swai alisema tofauti hiyo ilifanyiwa kazi na KNCU na taarifa kurejeshwa kwa Mrajisi lakini hawajaona mawasiliano yoyote yanayoonyesha ufuatiliaji wa suala hilo hiyo inadhihirisha namna Mrajisi alivyoshindwa kuitetea KNCU.
Mwenyekiti huyo alipigilia msumari zaidi pale alipodai hata mkutano huo mkuu maalumu ulioitishwa na Mrajisi ni batili na unakiuka kifungu namba 55(9) cha sheria ya Ushirika.
“Sheria iko wazi kuwa hesabu zikishawasilishwa na kujadiliwa na kisha kupitishwa na mkutano mkuu, uamuzi wao (wajumbe) kuhusiana na hesabu hizo unakuwa wa mwisho,”alisema Swai.
Swai alisema ilikuwa ni batili kisheria, kwa Mrajisi kushinikiza kuitishwa kwa mkutano huo ili kujibu hoja za ukaguzi ambazo alidai hazikupatiwa majibu ya kutosha na KNCU wakati wenye mali walisharidhika na majibu hayo.

Kiwanda cha matrekta kujengwa Tanzania

Warsal, Poland. Kampuni ya Ursus ya Poland imesema ina mkakati wa kujenga kiwanda cha kutengeneza matrekta Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Suma JKT.
Rais wa Bodi ya Ursus, Karol Zarajczyk alisema hayo jijini Warsaw jana wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokutana na wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza Tanzania.
Zarajczyk alisema wanataka kujenga kiwanda hicho kwa kuwa wametambua Tanzania ina fursa ya kufungua milango ya kibiashara kwa nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.
Alisema lengo jingine la kampuni hiyo inayotengeneza matrekta ni kutoa mafunzo kwa wakulima ya jinsi ya kutunza matrekta hayo, ili waone umuhimu wake katika sekta ya kilimo.
“Barani Afrika tulianza kupeleka matrekta Ethiopia, Ghana na Guinea. Sasa hivi tumeamua kwenda Tanzania na Zambia.
“Nia yetu siyo kujenga tu kiwanda, bali pia kutoa huduma kwa wakulima juu ya uendeshaji na utunzaji wa matrekta hayo,” alisema.
Alisema wako tayari kutoa mafunzo kwa vijana wa Tanzania waliopo vyuoni ili waweze kuunganisha matrekta hayo, kuyafanyia ukarabati na kutengeneza vipuri vyake wakati kunapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
“Tunapenda kujenga kiwanda mahali ambapo itakuwa rahisi kupata vijana wa kuajiriwa ili iwe rahisi kuwafundisha teknolojia tunayoitumia kutengeneza matrekta,” alisema.
Kwa upande wake, Pinda alisema atawasilisha maelezo hayo kwa waziri anayehusika na sekta hiyo ili mawasiliano rasmi ya kujenga kiwanda hicho yafanyike.

Chadema kujipima serikali za mitaa

Bukombe. Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) limesema uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu, utatoa picha halisi ya uwezo wao wa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Pia, Chadema imewaomba wananchi wote waliofikisha umri wa kupiga kura kujitokeza kujiandikisha katika daftari la makazi na daftari la kudumu la wapigakura wakati uandikishaji utakapoanza.
Halima Mdee, ambaye ni mwenyekiti wa Bawacha na mbunge wa Kawe, alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kilimahewa wilayani Bukombe mkoani hapa.
Mdee alisema chama hicho kimejiandaa kuchukua dola mwakani, lakini hilo litafanikiwa ikiwa uchaguzi wa serikali za mitaa utatoa dira kamili ya ukombozi wa pili wa taifa.
“Watanzania, uchaguzi huu wa Desemba 14 ndiyo utatoa dira kamili… utakuwa ni uchaguzi muhimu kuliko hata huo wa mwakani wa madiwani, wabunge na urais kwani unapotaka kujenga nyumba madhubuti lazima uanzie msingi imara na ndiyo maana tunasema uchaguzi huu ni muhimu,” alisema.
“Wanawake wenzangu, acheni kuhongwa chumvi na kanga na CCM. Kama wameshindwa kuwaletea maendeleo kwa miaka 52 ya uhuru, ni maendeleo gani tena wanayotaka kuyaleta?” alihoji Mdee huku wananchi wakimjibu, “hakuna, hakuna… wameshindwa”.
Naye katibu mkuu wa baraza hilo, Grace Tendega alisema ifikapo Novemba 23, mwaka huu wananchi wajitokeze kujiandikisha katika daftari la makazi ili kuwawezesha kushiriki ipasavyo katika uchaguzi huo wa vijiji, vitongoji na mitaa.
“Tunawaomba wananchi ambao mmefikisha miaka 18 kujitokeza kwa wingi ili kuanza kuifuta CCM kuanzia ngazi ya chini kwa kuanzia huko ili mwakani wakati wa uchaguzi ujao, tuwe tumewaonyesha mlango wa kuondokea,” alisema Tendega.
Uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika Desemba 14, wakati Uchaguzi Mkuu utakuwa Oktoba mwakani.
kupigiwa kelele na CCM lakini hazina nguvu kutokana na kutodaiwa mahakamani kama hazitatolewa.
“Leo hii eti wanasema kuna haki za watoto, wazee, afya, wasanii lakini wanashindwa kusema kwamba haki hizo Ibala ya 20 (1)(2) zimefungwa kudaiwa makahakani…ikataeni pindi itakapokuja kupigiwa kura ya maoni kwani haina kitu na badala yake maoni yenu yametupwa kando,” alisema Mwaifunga

Upinzani waandika historia mpya

Dar es Salaam. Vyama vya upinzani vimeandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya vyama vinne vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutiliana saini makubaliano saba ya ushirikiano, kubwa ikiwa kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia sasa.
Tukio hilo lilifanywa na viongozi wakuu wa NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD jana katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi wa dini na taasisi mbalimbali.
Akisoma makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alianza kwa kueleza historia ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilitengenezwa kwa muundo wa chama kimoja cha siasa (CCM)... “ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi.
Mwaka 2011 tulianza mchakato wa kuandika Katiba Mpya, ilipatikana Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi lakini maoni hayo yameondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.”
Alisema kitendo cha kuachwa kwa maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, kimesababisha athari katika matukio muhimu ya kidemokrasia.
Akitaja makubaliano hayo, saba aliyosema yana lengo la kuzaa Tanzania Mpya, Dk Slaa alisema, “Jambo la kwanza ni kuhusisha sera za vyama vyetu na kuchukua yale yote yanayofanana ili tumwe na kauli zinazolingana na kufanana kwa Watanzania.”
Alisema jambo la pili ni kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye ngazi zote za uchaguzi kuanzia Serikali za Mitaa, madiwani, wabunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Tatu, alisema utaratibu wa namna gani vyama vinavyounda Ukawa vitashirikiana katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015, utatolewa na vyama hivyo katika wakati muafaka na kusambazwa kwa viongozi wa vyama hivyo wa ngazi zote ili waweze kuutumia kama mwongozo na kufanyia kazi.
Nne, kushirikiana katika mchakato wa kuelimisha umma kuifahamu na kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa ambayo haijazingatia maoni ya wananchi badala yake imezingatia masilahi ya kikundi kimoja cha watu ambacho ni CCM.
Tano, kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za kitaifa na zenye masilahi kwa Watanzania.
Sita, kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya masilahi kama ilivyo sasa na kama inavyojidhihirisha katika Katiba Inayopendekezwa.
Saba, “kuhimiza na kusimamia ushirikiano wa pamoja baina yetu na asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania yenye nia ya dhati ya kulinda na kuenzi Muungano wetu bila kunyenyekea masilahi binafsi ya kikundi, kabila au itikadi.”
Dk Slaa alisema kwa uamuzi huo wa Ukawa ni wazi kuwa Watanzania watawaunga mkono huku akiwataka wajiandae kuwa na Tanzania Mpya.
Maalim Seif
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alisema msimamo wa Ukawa ni msimamo wa Watanganyika na Wazanzibari, huku akiwataka wananchi kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa na kuifananisha na takataka.
“Wamepiga kura kupitisha Katiba peke yao, wakaikubali peke yao, wakaitangaza peke yao. Eti wameikabidhi Katiba kwa Rais (Jakaya) Kikwete na Rais wa Zanzibar, sijui hawa viongozi wameikubali vipi hii Katiba, hakuna kitu pale,” alisema huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Maalim Seif alisema theluthi mbili kutoka Zanzibar haikupatikana na Bunge hilo lilitumia ujanja wa kuongeza idadi ya wajumbe wawili kutoka Zanzibar, ambao hawakutakiwa kupiga kura kupitia upande huo wa Muungano.
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Ukawa ina msingi wa uadilifu, uwazi na uwajibikaji na ndiyo kiboko ya kupambana na CCM. Kama mnataka rasilimali za nchi yenu kataeni Katiba Inayopendekezwa. Adui wa nchi hii ni mafisadi ndani ya CCM, lazima tuwe na mtandao wa mabadiliko nchi nzima. Vijana tufanye mazoezi ya viungo kwa ajili ya kupambana na mafisadi hawa.”
Aliwataka wananchi kuhakikisha kuwa wanajisajili katika daftari la Serikali za Mitaa ili kuwachagua viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa... “Naanza kuona mwanga wa kuiondoa CCM madarakani. Tujenge ushirikiano kwa ajili ya nchi yetu.”
Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Yaliyotokea leo siyo mapenzi ya Lipumba, Mbowe, Mbatia, Makaidi wala Nyambabe, bali ni mapenzi ya Mungu. Kama kuna mmoja wetu aliyepo hapa anayeshuhudia tukio hili huku amenuna … dhoruba limtokee.”
Huku akishangiliwa na umati wa wafuasi wa Ukawa, Mbowe alisema ni mategemeo yake kuwa viongozi wote waliotia saini makubaliano hayo, walizungumza kutoka rohoni kwamba wanaungana na wana nia moja.
Aliwataka viongozi wa chama chake katika ngazi zote, kuhakikisha wanakubaliana na mapendekezo yanayotolewa na Ukawa na kwamba yeyote anayeona hataweza aondoke mapema.
“Katika chama chetu hakuna masilahi ya maana kuliko nchi yetu. Ni marufuku kiongozi wa Chadema kupuuza muungano wa Ukawa na kama yupo mwenye masilahi binafsi aanze safari mara moja,” alisema Mbowe.
Aliwaagiza viongozi wa taasisi zote za Chadema, Bawacha, Bavicha na Baraza la Wazee, kuhakikisha wanafanya kampeni za kuipinga Katiba Inayopendekezwa nchi nzima kuanzia Novemba Mosi. Aidha, aliwaomba viongozi wa Ukawa kuhamasisha viongozi wao kuipinga Katiba Inayopendekezwa.
Mbatia
Mbatia alisema Taifa limeandika historia mpya na kuwaomba viongozi wenzake ndani ya Ukawa kuaminiana ili Watanzania nao wawaamini kwa kuwa wanataka kuweka mbele masilahi ya taifa.
Kuhusu Katiba, Mbatia alisema ni maarifa, mwongozo na inayounda dola hivyo asiwepo wa kuifanyia mchezo. Alitaka Katiba Inayopendekezwa ikataliwe na wananchi kwa kuwa haisadifu sifa hizo.
“Ukawa wana utulivu wa ndani wa kuwatumikia Watanzania wote… tuache kuangalia masilahi binafsi. Wakishinda Chadema… mimi nikubali, akishinda CUF lazima nikubali, hata wakishinda NLD nao nitakubali lakini na NCCR tukishinda nao waone tumeshinda kusiwepo na kinyongo kwa kuwa wote tunapigania mama Tanzania,” alisema.
Makaidi
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema umoja wa wananchi ndiyo utakaowapa nguvu viongozi wa Ukawa na kuongeza kuwa anaipenda Tanzania na anataka Zanzibar iwe na mamlaka kamili.
“Mungu siyo Athuman wala siyo wa John… Mungu alijua kupitia misukosuko hii ya Katiba, Ukawa tutaunganishwa. Bahati hii inaweza isitokee tena, wakati wa ukombozi ni sasa na utakapofika wakati wa kupigia kura ya maoni tuseme hapana, hapana, hapana na moto… moto mpaka CCM iungue,” alisema Dk Makaidi huku akishangiliwa kwa nguvu.

Saturday 25 October 2014

Chadema walaani Meghji kuipigia kura Zanzibar

Sengerema. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitendo kilichofanywa na uongozi wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba cha kumfanya Mjumbe wa Bunge hilo, Zakia Meghji kupiga kura kama Mzanzibar badala ya ‘Mtanzania Bara’ ni ‘uhuni’ unaotakiwa kuchukuliwa hatua na wananchi.
Hayo yalisemwa juzi na viongozi wa Mabaraza ya Wanawake na Vijana ya Chadema (Bawacha) na (Bavicha) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi, Segerema mkoani Mwanza.
Kauli hiyo wameitoa ikiwa ni saa 48 baada ya gazeti hili kubainisha utata wa kura ya Meghji wakati wa kuipitisha Katiba inayopendekezwa kupiga kama mjumbe kutoka Zanzibar badala ya Tanzania bara kama alivyotakiwa.
Akihutubia mamia ya wananchi, Mwenyekiti mstaafu wa Bavicha, John Heche alisema, “Kilichofanywa na Sitta (Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta) cha kumbadilisha dakika za mwisho Meghji kuhalalisha Katiba yao ni uhuni ambao Watanzania wanatakiwa kuwawajibisha kupitia kura ya maoni.”
Aliongeza: “Hivi kweli inawezekanaje mtu katika vikao vyote awe anahesabika kama mjumbe kutoka Tanzania Bara halafu dakika za majeruhi baada ya kuona wanachokifanya hakitapata theluthi mbili, hususani Zanzibar wampeleke huko….”?
Huku akishangiliwa na umati huo, Heche alisema wajumbe wa CCM wameondoa tunu za taifa za uwazi na uadilifu baada ya kuona zimewabana.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bawacha, Hawa Mwaifunga alisema wanawake wakiacha kutumika na CCM. hususani nyakati za chaguzi zinapokaribia wataifanya nchi hii iliyokosa maendeleo kwa miaka 52 baada ya uhuru kusonga mbele.
“Wanawake wenzangu nawaombeni mjitokeze kugombea nafasi mbalimbali lakini pia kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na makazi ili muweze kushiriki kikamilifu katika chaguzi hizo,” alisema Mwaifunga
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega alisema,”Nawasihi wanawake wenzangu na vijana wenye sifa kwenda kujiandikisha ili kuweza kuwa na sifa ya kuchagua na kuchaguliwa...wanawake msiache kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani tunaweza.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Kunti Yusuph alisema nchi hii imefika hapa kutokana na kuwakumbatia viongozi wasiotimiza wajibu wetu.
“Watanzania leo kupata huduma bora ni anasa, kuapata huduma za afya, elimu na maji navyo ni anasa hivyo tuchukue hatua kupitia uchaguzi wa serikaki za mitaa kubadili uongozi,” alisema Yusuph

Pinda atangaza rasmi kuwania urais

Dar es Salaam. Siyo tetesi tena. Sasa ni rasmi kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akitajwa kuwania urais amethibitisha wazi kuwa atagombea kiti hicho katika uchaguzi mkuu mwakani.
Alitoa uthibitisho huo juzi akiwa London, Uingereza ambako yuko katika shughuli za kikazi. Hatua hiyo inaondoa uvumi ambao umekuwapo kwa takriban miezi mitatu sasa kwamba naye tayari ameingia katika kinyang’anyiro hicho.
Pinda aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu akisisitiza kuwa hajatangaza rasmi lakini akasema kuwa ameanza harakati hizo ‘kimyakimya’. Alikuwa akijibu moja ya maswali aliyoulizwa katika Kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Alitamka rasmi kuwania nafasi hiyo baada ya kuulizwa kuwa anafikiri ni kiongozi gani anayefaa kurithi mikoba itakayoachwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Mikoba ya Rais Kikwete inaweza kuchukuliwa na yeyote atakayeonekana mwisho wa safari kwa utaratibu wa chama na ndani ya Serikali .... kama anafaa. Waliojitokeza sasa ni wengi na mimi ninadhani ni vizuri,” alisema Pinda.
Alipoulizwa kama yupo miongoni mwa wengi alisema, “… umesikia kama nimo … basi tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu aliyejitokeza ni katika jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana?”
“……..fanyeni hivyo kwa mwingine na mwingine, mwisho wa yote zile kura zitakazopatikana kwenye mkutano mkuu kama ni kutokana na chama kile kinachotawala na hatimaye Watanzania watakaojitokeza kupiga kura Oktoba kutokana na wagombea watakaojitokeza kutoka kwenye vyama mbalimbali huyo ndiye tutakayempata kama rais. Hivyo natangaza nia hiyo kimyakimya.”
Kiongozi huyo atakuwa wa pili kutangaza nia hiyo kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Alitangaza nia hiyo Julai 2, 2014, alipokuwa Uingereza katika mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa kwenye kipindi hicho hicho cha Dira ya Dunia.
Urais CCM
Kuingia kwa Pinda katika mbio za urais kupitia CCM tayari kumebadili mwelekeo wa kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini kutokana kuzigawa baadhi ya kambi za wagombea ambao walikuwa wakitajwa kwa muda mrefu kabla yake.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla.
Nguvu ya Pinda
Baadhi ya wapiga debe wa Pinda wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka za Mitaa Tanzania (Alat), ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, wamekuwa wakiweka kambi zao Dodoma kila kunapokuwa na vikao rasmi vya CCM ili kuwashawishi wajumbe wa vikao vya juu vya chama hicho wamuunge mkono.
Wakati wa vikao vya CC na NEC vya CCM vilivyomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini humo kuendelea na jitihada za kusaka wafuasi.
Harakati hizo zinaweza kuwa ndiyo maana ya kauli ya Pinda pale aliposema kwamba tayari ametangaza ‘kimyakimya’ nia yake ya kugombea nafasi hiyo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana anaunga mkono msimamo wa Pinda na wengine waliojitangaza katika chama chake huku akivilaumu vyama vya upinzani kwa wagombea wao kukaa kimya badala ya kujitokeza ili wananchi wawapime kama wa CCM wanavyofanya.
Kuhusu Pinda, Dk Bana alisema: “Ni mzoefu amekaa Ikulu muda mrefu na kwa wadhifa wake, si vibaya kujitangaza kwani anayejitangaza wananchi wanapata muda wa kumpima na chama pia kinampima tofauti na wale ambao hawajitangazi ambao ni hatari sana kwa kuwa wanapita chinichini kutoa rushwa.”
Kuhusu upinzani, alisema: “Sijui upinzani wana matatizo gani, ningefurahi kuona (Halima) Mdee, (John) Mnyika au (Willbrod) Dk Slaa wanajitokeza ili wananchi wawapime kwani Dk Slaa wa 2010 siyo Dk Slaa wa sasa. Wakijitokeza italeta uhai kwenye hizi harakati na wananchi watakuwa na nafasi nzuri ya kuwapima,” alisema na kuongeza: “Upinzani wanapokaa kimya wanatunyima fursa wananchi kuwapima.”
Manung’uniko
Tangu kuanza kwa tetesi kwamba Pinda ameingia katika kinyang’anyiro cha urais, kumekuwa na malalamiko ya chinichini dhidi yake kwamba amekuwa akicheza rafu kama ambazo ziliwafanya na makada wenzake wenye nia sawa na yake kufungiwa na Kamati Kuu ya CCM.
Itakumbukwa kwamba makada sita wa chama hicho ambao ni Sumaye, Lowassa, Membe, Makamba, Wasira na Ngeleja wanatumikia adhabu na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa.
Baadhi ya wagombea na makada wa CCM wamekuwa wakidai kuwa Pinda naye anacheza rafu hivyo kutaka ashughulikiwe, lakini wengine wamekwenda mbali zaidi na kuhoji ushiriki wake katika Kikao cha Kamati Kuu ambacho kilitoa adhabu hiyo ilhali akijua kwamba naye atakuja kugombea.
Makamba, Kigwangalla
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kikwangalla wamesema wanamkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika mpambano wa kuwania safari ya kwenda Ikulu kupitia CCM.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Makamba na Kigwangalla walionekana kutostushwa na uamuzi wa Pinda kuingia rasmi katika mbio hizo huku wakisema siyo tishio kwao.
Makamba kwa upande wake alisema hakuna cha ajabu kwa Pinda kuwania nafasi hiyo kwani 1995 alijitokeza Cleopa Msuya ambaye alikuwa pia waziri mkuu kupambana na mawaziri wengine kama Jakaya Kikwete na Edward Lowassa lakini alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye alipitishwa.
Alisema pia mwaka 2005 alijitokeza Waziri Mkuu, Frederick Sumaye dhidi ya mawaziri wengine wadogo, lakini walimshinda.
“Mara zote hizo wagombea wengine walifanikiwa dhidi ya mawaziri wakuu. Nafasi za madaraka ya kiserikali hazina nafasi katika uteuzi wa wagombea ndani ya CCM,” alisema Makamba.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli alisema anamkaribisha ili wapimane ubavu lakini akasema ni muhimu kuanzia sasa hadi Mei mwakani, harakati hizo zisiathiri kazi za Serikali hasa ikizingatiwa kuwa Pinda ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali.
Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayosimamia Ofisi ya Waziri Mkuu alisema haogopi mgombea hata mmoja, hata akiwa na cheo kikubwa au kidogo kwake si tishio.
“Waziri Mkuu anakaribishwa kwenye mbio hizi na asifikiri zitakuwa rahisi kwani watu tumejipanga na tuna mikakati ya kushinda,” alisema Kigwangalla.
Hata hivyo, Dk Kikwangalla alisema kuingia kwa Pinda kunaweza kuharibu mchakato mzima kwenye chama kwa kuwa ni mmoja wa watu wanaotoa uamuzi hasa ikizingatiwa kuwa kwa nafasi yake, anaingia kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
“Waziri Mkuu yuko kwenye nafasi ya kutuchuja, hivyo ni kama kusema refa ameamua kucheza kitu ambacho ni tatizo. Kitendo cha kutaka uongozi katika nafasi kama yake kitaondoa usawa,” alisema Dk Kikwangalla.

Kura ya Maoni mkorogano

Dar es Salaam. Kitendo cha Serikali kutoa kauli tatu tofauti ndani ya wiki moja kuhusu tarehe ya Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa, kimeelezwa na watu wa kada mbalimbali nchini kuwa ni matokeo ya viongozi wa Serikali kukosa uongozi wa pamoja.
Wakizungumza na Mwananchi Jumamosi, wasomi, wanaharakati, viongozi wa dini na wanasiasa wamesema kauli hizo zinawachanganya Watanzania, kwamba mpaka sasa hakuna anayejua tarahe rasmi ya kufanyika Kura ya Maoni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alilieleza gazeti hili kuwa  kura hiyo ingefanyika Machi 30 mwakani na kwamba upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30, kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi Katiba Inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi yanayoipinga.
Siku moja baadaye, Rais Kikwete alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China alisema endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa, Watanzania wataipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa Aprili mwakani.
Kauli ya Jaji Werema pia ilipingwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva na kufafanua kuwa kura ya maoni haiwezi kufanyika Machi 30 mwakani kwa sababu kazi ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura haitakuwa imekamilika.
Utata umezidi kuongezeka baada ya jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, Jaji Lubuva kusema kuwa Daftari la Kudumu la Wapigakura litakamilika Aprili 18 mwakani, huku taratibu zikieleza kwamba kura ya maoni itafanyika baada ya elimu kutolewa kwa wananchi na hutolewa kati ya miezi mitatu hadi sita.
Awali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kukaririwa akisema kuwa Kura ya Maoni ifanyike kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, huku Rais Kikwete akikubaliana na viongozi wa vyama vya siasa kuwa kura ya maoni itafanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms alisema, “Hayo ni matokeo ya kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja. Sina hakika kama AG ndiye alipaswa kutaja tarehe ya kura ya maoni, yeye ni mshauri tu.”
Alisema kitendo cha kauli ya AG kutofautiana na iliyotolewa na rais ambaye amemteua ni ishara mbaya katika utendaji kazi wa Serikali.
“Wakati mwingine kauli kama hizi zinaweza kuwavunja moyo walioteuliwa. Nakumbuka Waziri Mkuu Pinda aliwahi kutoa kauli ya kupinga maelezo ya Waziri wa Ujenzi, Magufuli (John). Tafsiri ya kilichotokea ni kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja,” alisema.
Naye Katibu Mkuu  wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Leonard Mtaita alisema kazi iliyobaki ni kuwahamasisha wananchi wakati wa kupiga kura ya maoni utakapofika  kwa maelezo kuwa kila mtu atapiga kura kutokana na anachokiamini.
Dk Mtaita alisisitiza pia kuboreshwa kwa Daftari la Wapigakura, akisema kuwa hilo ndilo litakuwa jambo la msingi ili kuwafanya Watanzania wote wenye sifa waweze kupiga kura, huku akiiomba Serikali kuhakikisha inasambaza nakala za kutosha za Katiba Inayopendekezwa.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima alisema, Serikali kupuuza mawazo na malalamiko ya watu ni ishara mbaya, kufafanua kwamba Katiba Inayopendekezwa ina uhalali wa kisheria lakini inakosa uhalali wa kisiasa na ili kuokoa mvutano, maridhiano ni jambo la msingi.
“Wananchi wanaulalamikia mchakato wa Katiba, pamoja na mvutano unaoendelea, haya malalamiko ya wananchi si ya kufurahia hata kidogo. Jambo hili linatakiwa kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Aliongeza, “Rais ndiye anayetakiwa kutueleza msimamo wake ni nini juu ya suala hili. Je, na yeye atafuata masilahi ya CCM au atazungumza kama Rais. Kama maridhiano yatakosekana na Katiba hiyo ikapitishwa, haitadumu muda mrefu kwa sababu watawala wengine watakaokabidhiwa kijiti wataibadili Katiba hiyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii, Fordia, Bubelwa Kaiza alisema tofauti za kauli za viongozi zinaonyesha kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya uliendeshwa katika taratibu zisizo sahihi, ndio maana hakuna kauli moja kuhusu siku ya kupiga kura ya maoni.
“Hayo ni majibu kwamba ndani ya serikali kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu suala zima la Katiba Mpya. Hakuna msemaji sahihi, kila mtu anazungumza lake. Ndio maana hata katika Bunge Maalumu kila mtu alifanya lake, sheria zilibadilishwa bila kufuatwa kwa utaratibu,” alisema.
Alifafanua kuwa ni ngumu kwa kila jambo linalohusu Katiba kwenda vizuri kwa sasa kwa sababu mchakato uliharibika baada ya kuanza vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema elimu ya uraia inatakiwa kutolewa miezi mitatu hadi sita kabla ya kufanyika Kura ya Maoni, si siku 30 alizozitaja Jaji Werema.
“Huwezi kutoa elimu ya uraia kwa siku 30, mfano Zimbabwe walitumia miezi sita kutoa elimu ya uraia. Mchakato huu umeingiliwa na wajanja, si riziki tena, ni kama mtu aliyejifungua mtoto aliyekufa,” alisema.
Kibamba alisema Nec ilieleza kuwa kufikia Mei ndiyo itakuwa imemaliza kazi ya kuboresha Daftari la Wapigakura, kwamba kitendo cha Jaji Werema kueleza kuwa Kura ya Maoni itafanyika Machi mwakani, ni ishara ya ‘ukambale’.
“Waziri Mkuu (Pinda) alisema Katiba ipatikane kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, Rais Kikwete akakubaliana na TCD kuwa ni 2016, jana (juzi) Jaji Werema anatueleza kuwa ni Machi mwakani, tumsikilize nani?”
Alisema tarehe ya kura ya maoni kwa mujibu wa sheria inatakiwa kutangazwa na Rais si Mwanasheria Mkuu wa Serikali.  Kibamba alisisitiza kuwa Serikali bora ni ile inayojiendesha kwa uwajibikaji wa pamoja.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema, “Tamko la Serikali kwa jambo kama hilo huwa ni moja na si kila kiongozi kutoa tamko lake. Ndiyo maana tarehe ya  Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, si mtu mwingine.”

Alisema huenda mkanganyiko ulioibuka juu ya tarehe rasmi ya kura ya maoni unatokana na nchi kutowahi kuendesha zoezi la upigaji wa kura hiyo.
“Sheria inaeleza wazi kuwa rais atatangaza tarehe rasmi siku 84 baada ya kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa. Ili muda usogezwe mbele ni lazima sheria ibadilishwe, nadhani hilo linaweza kufanyika katika kikao kijacho cha Bunge,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi  alisema  mchakato wa Katiba ni suala la kisheria na kisiasa, hivyo kama Rais alikutana na wanasiasa na kukubaliana, ingekuwa jambo jema kama makubaliano hayo yangezingatiwa.
 “Kama ni suala la sheria, sheria husika inabadilishwa lakini kama ni suala la makubaliano ya wanasiasa, pia lilitakiwa kuzingatiwa. Kwa sasa kuna mvutano mkali, sijui nini kitatokea,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa alisema jambo hilo linatokana na viongozi wa Serikali kugawanyika huku akitolea mfano kauli ya Rais Kikwete kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ungefanyika Februari mwakani, lakini baadaye Waziri Pinda akatangaza kuwa utafanyika Desemba 14 mwaka huu.
“Nchi inayokuwa na viongozi ambao kila mmoja anatoa kauli yake haiwezi kuwa na mshikamano. Wao hawana umoja halafu wanataka Watanzania kuwa na umoja, hilo litawezekana kweli?” alihoji Dk Slaa.
Aliongeza, “Hata kura ya maoni ikifanyika leo haina maana tena kwa sababu Katiba Inayopendekezwa imeondolewa mambo ya msingi yaliyotokana na maoni ya wananchi. Wanasema Katiba hii ni bora barani Afrika, sijui nani kawadanganya. Dk Slaa alisisitiza kuwa ili hali iwe shwari ni lazima kura ya maoni ifanyike wakati ambao Nec itakuwa imeliboresha Daftari la Wapigakura. “Watambue kuwa safari ya kudai Katiba Mpya ndiyo inaanza sasa kwa sababu Katiba Inayopendekezwa ni mali ya CCM, si Watanzania.”
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema, “Kama tunaamini kuwa Katiba Inayopendekezwa siyo nzuri, umefikia wakati wa kuwaachia wananchi wapige kura. Kama ni nzuri wataipitisha na kama hawaikubali wataikataa.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Tangu mwanzo niliupinga mchakato wa Katiba na matokeo yake imezaliwa Katiba Inayopendekezwa isiyokuwa na maoni muhimu ya Watanzania. Sikubaliani na mchakato wa kura ya maoni.”
Profesa Mpangala alisema mchakato wa kupata Katiba Mpya unatakiwa kurudiwa mwaka 2016 kwa maelezo kuwa Katiba itakayopatikana haitakuwa na ridhaa kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe alisema, “Hayo ni matokeo ya nchi kuwa na sheria mbovu. Katiba yetu pamoja na sheria za nchi hii hazieleweki. Rais amepewa madaraka makubwa kiasi kwamba wengine wakitoa kauli hata kama wanaweza kufanya hivyo, kauli zao zinaonekana si kitu mbele ya kauli ya Rais.”

Saturday 4 October 2014

Wanajeshi, polisi watwangana risasi

Tarime. Watu 12 wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi ya kurushiana risasi baina ya askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi 128 KJ cha Nyandoto na Polisi wa Kituo cha Stendi wilayani Tarime mkoani Mara.
Hatua hiyo imekuja wakati wanajeshi hao walipokuwa wakijaribu kumchukua askari mwenzao aliyekamatwa na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuendesha pikipiki bila kuwa na kofia ngumu.
Mashambulizi hayo ya kurushiana risasi na kutwangana ngumi na mateke yalitokea juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Stendi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Bernard Makonyo alisema amepokea majeruhi 10, kati ya hao wawili ni askari wa JWTZ, polisi saba na raia mmoja. Alisema majeruhi tisa wameruhusiwa na mwingine kupelekwa Hospitali ya Shirati kwa matibabu zaidi.
Dk Makonyo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Aloyce Filbert (24) aliyepigwa risasi mguu wa kulia, Deodatus Dominic (26) aliyejeruhiwa puani na wote ni askari wa JWTZ.
Wengine ni askari polisi saba ambao ni Makoye Katula (26), Sylvester Michael (31), Salum Omary (44), Abdallah Halifa (24), Joel Msabila (25), Ally Juma (27) na Deogratius Tryphon (32) na raia Hamza Jumanne (33) aliyepigwa risasi mguu wa kushoto ambaye alipelekwa Hospitali ya Shitari, Rorya kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Ndalama Salumu anadaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa katika vurumai hizo huku mwananchi mwingine, David Kisaro (20) akijeruhiwa kwa bomu jichoni. Alitibiwa katika Zahanati ya Tarime.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Benedict Mambosasa alisema mwanajeshi aliyekamatwa alifanya makosa kwani baada ya kukamatwa na kuombwa kwenda kituo cha polisi, alikaidi.
Mambosasa alisema mwanajeshi huyo licha ya kukiuka taratibu, aliwatolea lugha za matusi polisi jambo lililowalazimu kumkamata kwa nguvu, ndipo wanajeshi wenzake walipoingilia kati na kusababisha kutokea kwa majibishano ya risasi za moto. Hata hivyo, alisema hakuna aliyejeruhiwa.
Alisema wanajeshi watatu ambao hawakutajwa majina, wamekamatwa na polisi kwa kuvunja utaratibu wa usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amelaani kitendo hicho cha kurushiana risasi za moto hewani akisema ni cha utovu wa nidhamu na maadili ya kazi ya jeshi na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema wananchi Tarime wameshangazwa kwa kitendo kilichofanywa na walinda usalama hao, wakisema si cha kinidhamu huku wakisema kilikwamisha shughuli zao kwa muda kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
 Mkazi wa Tarime, Joseph Samson amesema kitendo hicho kimewashangaza sana wananchi.

KATIBA: Mtifuano wahamia uraiani

Dar es Salaam. Baada ya Bunge la Katiba juzi kufanikiwa kupata theluthi mbili ya wajumbe wa pande zote mbili za Muungano na kupitisha Katiba inayopendekezwa, sasa msuguano kuhusu Katiba unaonekana kuhamia uraiani.
Msuguano kuhusu Katiba hiyo unatarajiwa kuendelea mitaani, ndani ya vyama vya siasa na kwenye majukwaa kutokana na tofauti ya mitizamo iliyoibuka kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopitishwa.
Ingawa matokeo ya kura za ushindi yalipokewa kwa furaha na wajumbe waliokuwapo bungeni kwa kucheza na kurusha vijembe kwa wapinzani, huenda kibarua kitakuwa kigumu kwa CCM itakapolazimika kupambana na wananchi, wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa dini ‘waliojeruhiwa’ na mwenendo wa Bunge.
Bunge hilo liliendeshwa kwa upinzani mkali kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu waliokuwa wakitaka lisimamishwe kwa madai kuwa limechakachua maoni yao kama yalivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
CCM na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar
CCM iliingia doa baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kuzua kizaazaa bungeni Jumatano wiki iliyopita kwa kupiga kura ya hapana katika ibara 22 kwenye Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
Mwanasheria huyo ambaye awali alijiondoa kwenye Kamati ya Uandishi kwa kutoridhishwa na mambo yalivyokuwa yanakwenda, alizomewa na baadhi ya wajumbe na kulazimika kutolewa ukumbini akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Bunge.
Akizungumza na gazeti hili, Othman alisema kuwa alichofanya kilikuwa ni utashi wake kwa kuwa Serikali ilitamka kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kuwa haikuwa na msimamo.
 “Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa maana ya upande, maana yake ni ipi pengine unisadie… nilipiga kura kwa kuzingatia utashi wangu na maoni yangu,” alinukuliwa Othman.
Ingawa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta alimtetea Othmani kwa kusema wajumbe hawakupiga kura kwa kutumia vyeo vyao, kwa namna wajumbe walivyoonyesha jazba imeonyesha kuwa CCM itapaswa kusafishwa taswira iliyochafuka.
Sitta na viongozi wa dini
Kwa upande mwingine, Sitta amejikuta akiingia kwenye ‘vita’ na viongozi wa dini, baada ya kuwataka waumini wa madhehebu mbalimbali kuupuza nyaraka zilizotolewa na viongozi hao kwa kuwa hazina utukufu wowote wa Mwenyezi Mungu.
Sitta alisema baadhi ya viongozi wa dini wanalenga kuliingiza taifa kwenye machafuko na kwamba yeye hatakuwa tayari kuvumilia hali hiyo.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
Huku akiwa na waraka huo mkononi, Sitta alisema kuwa lugha iliyotumika haina staha na haikupaswa kutumiwa na watu wanaohubiri dini duniani.
Akizungumzia kauli ya Sitta, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema kauli ya Sitta inaonyesha kuwa amechoshwa na mwenendo wa Bunge la Katiba.
 “Sikutarajia kiongozi kama huyo kutoa kauli mbaya kama hiyo kwa Taifa zima. Sikutegemea mheshimiwa kama huyo kusema maneno kama hayo… Huenda ana stress (msongo wa mawazo). Hata ikiwa hivyo, hakupaswa kutoa kauli nzito kama hiyo. Anatakiwa kufahamu kuwa waraka huo umetoka kwa Wakristo wote hapa nchini,” alisema Askofu Kilaini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana alisema kitendo cha Sitta na wenzake kushindwa hata kuelewa waraka wa viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”, ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.
Hata hivyo, jana Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Father Raymond Saba, amesema bado wanaendelea kutafakari kauli ya Sitta na kwamba kwa sasa hawajatoa taarifa yoyote.
Akizungumzia kauli ya Sitta, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kauli ya kiongozi huyo imeongeza mpasuko wa dini nchini hasa kuhusu mahakama ya kadhi.
“Viongozi wa dini wameipokea kauli ya Serikali kwa kuwa tu alisema ni kiongozi wa Serikali, lakini itatokea shida kama ahadi yao haitatekelezwa,” alisema Salim.
Sitta na Jaji Warioba
Sitta amejikuta kwenye vita ya maneno na Jaji Warioba huku kila mmoja akisisitiza kuwa anafanya kazi aliyotumwa na wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hivi karibuni, Jaji Warioba alisema ataingia mitaani kuitetea Rasimu ya Katiba iliyokuwa imebeba maoni ya wananchi.
Alisema kuwa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu.
Hata hivyo, akizungumza jana na gazeti hili alisema kuwa Katiba hiyo imeacha maswali mengi kuliko majibu hasa kwa upande wa Zanzibar.
Sitta alalamikia kutukanwa
Sitta atakuwa na kibarua kingine cha kujisafisha mbele ya wananchi ambao alikaririwa akisema kuwa wamekuwa wakimtumia meseji za matusi za ya 50 kila siku.
Kwa nyakati tofauti wananchi wasiojulikana wamekuwa wakiandika meseji za matusi kwenye mitandano na simu kwa kile wanachosema kuwa Sitta amelazimisha maoni ya CCM yatawale Bunge.
Wananchi wasubiri waelezo zaidi
Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu mwenendo wa Bunge hilo, waliwalaumu wajumbe wa Bunge waliokuwa wakisema walipiga kuwa kwa niaba ya wananchi kwenye majimbo yao.
Walihoji ni lini wajumbe hao ambao ni wabunge wao walikwenda kuwauliza iwapo wanataka kupiga kura ya hapana au ndiyo dhidi ya Katiba iliyopendekezwa?
‘Mimi nimesikia tu mbunge wetu (anamtaja) amesema wananchi wake wamechagua kura ya ndiyo. Ni nani alimtuma kwenda kuwa tunataka Katiba hiyo wakati maoni yetu tulitoa tofauti, “ Yohana Change mkazi wa Vwawa, Mbozi.
Mwanaidi Suleiman alisema haelewi nini kilichotokea bungeni, kwa kuwa matarajio aliyokuwa nayo kuhusu Katiba yameyeyuka baada ya kusikia mambo mengi yamekataliwa.
“Nafuu kama wangeondoa mambo mengine, lakini siyo serikali tatu na uraia wa nchi mbili. Mimi hayo niliyaona makubwa sana, kama hayapo sasa Katiba itahusu nini?” alihoji Mwanaidi.
Chadema na wanachama wake.

Hali ya hewa ndani ya Chadema ilichafuka baada ya Sitta kusema kuwa kuna wajumbe wawili wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka Zanzibar walikubali kupiga kura kinyume na msimamo wa vyama vyao.
Sitta alisema kuwa kati ya wajumbe hao, mmoja alikubali kupiga kura na kusema yuko tayari hata kufukuzwa na chama chake.
“Sasa wale wanaotumia mbinu za ovyoovyo ili mchakato huu usikamilike wanapoteza muda, maana ukizuia maji huku, yanaelekea kwenye mkondo mwingine,” alisema Sitta.
Taarifa hizo zilionekana kuwalenga wabunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha na Mwanamrisho Abama ambao kwa nyakati tofauti walithibitishwa kutafutwa ili apige kura.
“Kweli nimesumbuliwa sana na watu ambao siwezi kuwataja na wananitaka nipige kura na wengine walifika mpaka nyumbani lakini mimi siwezi kushiriki maana nikifanya hivyo dhamiri yangu itanishtaki,” alisema Msabaha.
Naye Abama alisema kuwa alikuwa amepewa ilani na viongozi wake kwamba anatafutwa ili akapige kura, hivyo aliamua kukaa ndani kukwepa mtego huo.
Kauli hizo mbili tofauti zinauachia Ukawa maswali magumu yanayohitaji majibu ili kubaini iwapo kuna usaliti wowote umefanyika au la.
Wabunge wengine ambao wanaweza kukukumbana na matatizo ndani ya chama hicho ni Mbunge John Shibuda (Maswa Mashariki), Said Arfi (Mpanda Mjini) ambao walikiuka uamuzi wa Ukawa kutoshiriki Bunge hilo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alisema kuwa suala la wasaliti wa chama linatarajiwa kuzungumzwa kwenye vikao vya ndani.
“Siwezi kulitolea uamuzi suala hilo, baada ya kumaliza uchanguzi sasa litazungumzwa ndani ya vikao vya chama na kutolewa uamuzi,” alisema Dk Slaa.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kuwa Sitta alipaswa kuwataja wajumbe kutoka Ukawa waliokubali kupiga kura, lakini hakufanya hivyo.
“Juzi amechukua kura zao na hawataji ni kina nani wala walipiga kura kwa njia gani. Hata akijiongezea hizo kula mbili feki bado BMK upande wa Zanzibar wanabakiwa na kura 145 tu na siyo 146,” alisema Mtatilo.
Wanananchi waikataa rasimu
Naye Joseph Lyimo kutoka Manyara, amesema kuwa baadhi ya wakazi wa mkoani humo, wamesema Bunge la Katiba limepitisha rasimu ya Katiba bila maridhiano kwa baadhi ya wajumbe hivyo kusababisha hofu ya kupatikana kwa katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi.
Wakizungumza jana na mwandishi wa habari hizi, wananchi hao walidai kuwa rasimu hiyo iliyopitishwa bungeni juzi haikukidhi maoni yaliyotolewa kwenye tume ya Warioba kwani ibara 28 zimefutwa na kuwapo ibara mpya 42.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Abdalah Mtengeti alisema kwenye Tume ya Warioba wananchi walipendekeza mbunge awe na ukomo wa madarakani kwa miaka 15, lakini sasa wabunge hao wameridhia asiwe na mwisho wa utawala.
“Wananchi hawawezi tena kumwajibisha  mbunge waliyemchagua wao wenyewe kama walivyopendekeza awali pia hakuna ukomo wa mbunge tena hivyo atatawala hadi mwenyewe aseme sigombei tena,” alisema Mtengeti.
Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Manyara, Frank Oleleshwa alisema rasimu hiyo ya wabunge haikujali maoni ya wananchi kwani walipendekeza kufutwa kwa vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya lakini, wabunge wameridhia.
“Pia wananchi walipendekeza kuwepo na Serikali tatu ikiwamo kurudisha Tanganyika ili kuwapo na usawa wa nchi, lakini wabunge wamegoma hilo na kuridhia Rais wa Zanzibar awe makamu wa pili wa Rais,” alisema Oleleshwa.
CCM, CUF Zanzibar
 Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai walipozungumza na  gazeti hili kwa nyakati tofauti visiwani humo, Mazrui alisema kwamba mambo yaliyopitishwa na Bunge la Katiba katika rasimu hiyo yanagongana na Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ikiwamo suala la mamlaka ya ugawaji mikoa aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Alisema Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano utekelezaji wake utakuwa mgumu kwa baadhi ya mambo Zanzibar mpaka Katiba ya Zanzibar ifanyiwe tena marekebisho na kabla ya kufanyika hivyo lazima kuitishwe kura ya maoni kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kwamba kama viongozi wote watafanya kazi kwa kuzingatia sheria na katiba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK) haitoyumba kwa sababu hakuna mshindi wala mshindwa baada ya rasimu ya katiba kupitishwa.
“Matokeo ya kura ya rasimu ya katiba, ni ushindi wa wazanzibari wote na watanzania kwa ujumla, na hakuna mshindi wala mshindwa” alisema Vuai ambaye pia alikuwa mjumbe wa bunge maalum la katiba.

Warioba: Katiba bado ina maswali mengi

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Katiba inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba hiyo bado ina maswali mengi kuliko majibu, hasa katika muungano na mgombea binafsi.
Amesema licha ya Zanzibar kuridhia mambo kadhaa kuwekwa katika orodha ya mambo ya muungano, hali inaweza kuwa tofauti ukifikia wakati wa Zanzibar kubadili Katiba yao ili kuwezesha utekelezaji wa mabadiliko hayo.
Juzi Bunge hilo lilipitisha Katiba inayopendekezwa kwa tofauti ya kura mbili na kuhitimisha kwa sasa mchakato wa kuandika Katiba hadi mwaka 2016 ambapo litafanyika zoezi la upigaji wa kura ya maoni.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana, Jaji  Warioba alisema, “Wasiwasi wangu ni juu ya muungano kwa sababu katika masharti ya mpito ni lazima Zanzibar ifanye marekebisho ya Katiba yake. Rasimu inayopendekezwa inasema Tanzania itakuwa nchi moja pamoja na madaraka ya rais kugawa nchi. Kwa maana hiyo lazima Katiba ya Zanzibar ibadilike.”
Alisema katika mambo ya muungano, Katiba inayopendekezwa imeliweka suala la kodi ambalo halikuwamo katika rasimu iliyotolewa na Tume ya Katiba, kusisitiza kuwa kitendo hicho hakitajibu swali la ‘Tanganyika kuvaa koti la Muungano’.
“Wameongeza kodi ya mapato, ushuru wa forodha  na bidhaa katika mambo ya muungano. Maana yake ni kwamba kodi yote inayokusanywa, ikiwamo ya kutoka Zanzibar itaingizwa kwenye mfuko wa muungano,”alisema.
Aliongeza, “Wakati huo huo Zanzibar imepewa uwezo wa kusimamia mambo yake yenyewe na ili iweze kulitekeleza hilo ni lazima iwe na vyanzo vyake vya mapato. Sasa watasimamiaje wakati mapato yote yanaingia kwenye mfuko wa muungano.”
Alisema ili suala hilo liweze kutekelezwa ni lazima Zanzibar ibadili Katiba yake na kusisitiza kuwa utakapofika wakati wa kubadili Katiba ya Zanzibar, jambo hilo linaweza kukwama.
“Sioni kama Wazanzibar watakubali suala hili. Kama mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yatakwama, ni wazi kuwa Katiba inayopendekezwa haitatekelezeka. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yanategemea maridhiano ya Wazanzibari wenyewe na kumbuka kuwa CUF na CCM wanavutana sana,” alisema Jaji Warioba.
Akifafanua hilo, alisema mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar lazima yapate theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kusisitiza kuwa kwa mvutano wa vyama hivyo viwili visiwani Zanzibar, itakuwa kazi ngumu kupitisha jambo hilo.
“Katiba ya Zanzibar isipobadilishwa kero za muungano zinazozungumzwa zitaendelea. Kazi iliyopo sasa ni kufikiria maridhiano kuhusu muungano, lazima tuhakikishe Zanzibar imekubali kubadili katiba yake na kuridhia mapato yake kuingizwa katika mfuko wa muungano,” alisema.
Aliongeza, “Kama ambavyo Tanzania Bara waliitegemea Zanzibar kupitisha Katiba inayopendekezwa, ni lazima pia ihakikishe kuwa Zanzibar inakubali kubadili Katiba yake.”
Kuhusu mgombea huru Jaji Warioba alisema, “Katiba inayopendekezwa imeweka masharti ya mgombea ubunge na kutaja sifa za ziada za mgombea huru ambazo ukizitazama kwa undani utabaini kuwa wanamkataa mgombea huru kistaarabu.”
Alisema sifa hizo za ziada walitakiwa kuwekewa na wagombea wengine, si mgombea huru pekee.
“Mfano ni kutoruhusu mtu kutoka katika chama cha siasa kisha  kugombea kama mgombea huru,” alisema.
Jaji Warioba aliyataja baadhi ya mambo ya msingi yalikuwamo katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingizwa tena katika Katiba inayopendekezwa kuwa ni malengo muhimu ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimazingira.

Ukawa sasa waja na tuhuma nzito kuhusu kura

Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeibua shutuma dhidi ya uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kwamba unawarubuni kwa fedha baadhi ya wajumbe wa umoja huo ili kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.
Kamati ya Ufundi ya Ukawa, ilisema jana kuwa wajumbe wanaorubuniwa wapige kura ya ‘ndiyo’ kwa ahadi ya kupewa zaidi ya Sh500 milioni ni wa CUF na wengine wanne wa Chadema wanaotoka Zanzibar.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Khamis Hamad alikanusha madai hayo, akisema hajasikia kitu kama hicho na ndiyo kwanza alikuwa anasikia hilo kutoka kwa mwandishi wa habari hizi... “Hakuna kitu kama hicho, hilo jambo ndiyo nalisikia kutoka kwako.”
Kutokana na madai hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukawa, John Mnyika alisema kamati hiyo ilianza kikao cha siku mbili kuanzia jana kujadili hali hiyo na kutoa mapendekezo kwa uongozi wa juu wa umoja huo.
Licha ya Mnyika kukataa kutaja majina ya wajumbe waliorubuniwa, wajumbe wa Chadema wanaotokea Zanzibar ni Zeudi Abdallah ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Maryam Msabaha, Mwanamrisho Abama na Raya Ibrahim. “Tumewataka wajumbe wetu wote kukusanya ushahidi na kuuwasilisha kwa viongozi wa Ukawa,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara.
Aliongeza, “Chadema ina wajumbe wanne, watatu ni wabunge wa kawaida na mmoja wa kuteuliwa na Rais (Kundi la 201). Tumepata taarifa kutoka kwa wajumbe hao kwamba wanapigiwa simu na uongozi wa Bunge ukiwataka wasaini karatasi za kupigia kura ili uongozi wa Bunge uchakachue kura.
“Tumeanza kikao kujadili suala hili ila tumeamua kwanza tuueleze umma kupitia vyombo vya habari juu ya ‘uharamia’ unaofanywa na Bunge la Katiba linaloongozwa na Sitta (Samuel) na Makamu wake Samia (Suluhu Hassan).”
Ukiukaji kanuni
Akinukuu Kifungu cha 36 (3) cha Kanuni za Bunge la Katiba, Mnyika alisema si sahihi Sitta kutaka wajumbe waliopiga kura ya ‘hapana’ kuitwa katika Kamati ya Mashauriano na uamuzi huo ni kinyume na kanuni...
“Ni kama kuwatisha tu wajumbe.”
Kanuni hiyo inasema; “Endapo baada ya ibara ya Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa upya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye Kamati ya Mashauriano ili kupata mwafaka.”
Sitta awataje
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Joran Bashange alimtaka Sitta kutaja majina ya wajumbe wa CUF na Chadema waliopiga kura... “Tunamtaka awataje kwa majina maana ujanja wake na wenzake tumeshaujua na tuna ushahidi wote.”
Bashange alisema mpaka sasa hakuna mjumbe wa Bunge hilo ambaye ni mjumbe wa Ukawa aliyepiga kura kupitisha Katiba inayopendekezwa.
“Ndiyo maana walibadili kanuni ili kuruhusu wajumbe kupiga kura kwa faksi na baruapepe ili kufanya ‘uharamia’ wa kuiba kura,” alisema.