Tuesday 20 May 2014

Wabunge wataka JK aunde tume ya elimu

Dodoma/Dar. Baadhi ya wabunge jana walichachamaa wakisema elimu nchini ipo mahututi na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kudumu ya elimu itakayochunguza mfumo wa elimu nchini.
Wabunge hao walikuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2014/2015 iliyowasilishwa na waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa Jumamosi usiku.
Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer alipendekeza safari zote za wabunge na mawaziri nje ya nchi zifutwe na fedha zake zipelekwe kuboresha shule za kata.
Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alizungumzia uduni wa vitabu na mitihani ya wanafunzi wa shule za msingi akisema inakosewa kutungwa.
“Nina mtihani wa majaribio wa darasa la saba ambao haufanyiki. Niliwahi kumpa profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye alitumia saa mbili na nusu bila kupata jibu lolote la kuandika. Mtihani wenyewe haufanyiki,” alisema Mbatia na kutoa ofa ya Sh10 milioni kwa profesa mwingine yeyote bungeni ambaye ataweza kufanya mtihani huo na kupata alama 100.
“Haya ni madudu ya kutisha. Mwaka jana nilivyotoa maoni yangu hapa na waziri akasema maoni yetu yamechukuliwa, alisema rasimu ya mwisho sera ya elimu imepelekwa Baraza la Mawaziri Machi 2013, lakini hadi sasa bado haijakamilika,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni dalili ya Bunge kutoheshimiwa.
Pia alizungumzia ripoti za kamati zilizoundwa kuchunguza elimu lakini hazikufanyiwa kazi na badala yake zikawekwa kwenye makabati.
“Tumwombe Rais aunde Tume ya Kudumu ya Elimu kwa sababu kwa hali inavyokwenda ni mbaya sana na napendekeza tume hii ishughulike na kudhibiti mambo yote yanayofanya kutetereka kwa ubora elimu nchini.
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alisema elimu ya Tanzania iko mahututi na kuwaomba wabunge kuacha siasa katika elimu.
“Bajeti itapita lakini tunaua kizazi kijacho. Mheshimiwa mwenyekiti nenda darasa la kwanza mpaka la saba anayoyasema Mbatia yapo hata kama hatuyapendi lazima tuseme ukweli,” alisema.
Alisema ukienda katika vyuo vikuu ni majanga. “Kama unajiangalia wewe na familia yako, basi tunaliua Taifa. Nimefanya utafiti kwenye nchi 35, Tanzania ni nchi ya mwisho kwa ufaulu,” alisema na kuongeza kuwa nchi zote zilizoendelea kiuchumi, kiwango cha ufaulu ni juu ya asilimia 60.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina alisema hakuna Wizara ya Elimu baada ya elimu ya sekondari na msingi kuondolewa
“Mbele ya Waziri Mkuu niseme kuwa sasa hatuna Wizara ya Elimu… na sasa wanaondoa elimu ya watu wazima, shule zote za mazoezi zimeondolewa.”
Mbunge wa viti maalumu (CUF), Magdalena Sakaya alisema anashangazwa na wizara kushusha madaraja ya ufaulu ambayo awali, kuanzia alama 34 ilikuwa ni daraja O lakini leo ni ufaulu.
“Kiukweli waziri aliyeko katika wizara hii ameshindwa kusaidia elimu nchini. Tangu ameshika wadhifa huo anazidi kubebwa. Kwa nini tunambeba mtu ambaye ameshindwa kusaidia elimu nchini?” alihoji.
Safari za nje
Laizer alitaka safari za mawaziri na wabunge nje ya nchi zifutwe na fedha hizo ziboreshe shule za kata ambako ndiko watoto wa maskini wanakosoma.
Alisema anashindwa kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo wakati watoto wake wote katika jimbo lake wanafeli kutokana na shule za kata kutokuwa na walimu wa kutosha.
Akifanya majumuisho, Waziri Kawambwa alikiri deni la Sh61 bilioni la madai ya walimu, lakini akasema serikali imekuwa ikilipa.
Alisema kuanzia Agosti mwaka jana hadi Machi, jumla ya Sh16 bilioni zimelipwa na kwamba si kweli kwamba deni hilo limebakia kuwa Sh61 bilioni.

Sunday 11 May 2014

Mbowe atangaza mawaziri kivuli

Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ametangaza Baraza lake la mawaziri kivuli 28 na naibu mawaziri 12, na kufanya baraza lote kuwa na mawaziri 40.
Katika baraza hilo la mawaziri linalojumuisha wabunge wanaotokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), mawaziri 25 wanatoka Chadema, 11 wanatoka CUF na NCCR-Mageuzi ni wanne.
Mawaziri kivuli walioachwa katika baraza hilo ni Sylvester Kasulumbay (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Highness Kiwia (Viwanda na Biashara) na Rose Kamili (Kilimo, Chakula na Ushirika).
Wengine walioachwa na Mbowe akasisitiza kuachwa kwao siyo kwa sababu hawawezi kazi bali ni kutaka kuwa na baraza la mawaziri dogo ni Sabrina Sunga (Naibu Waziri Maji).
Katika Baraza hilo, nafasi ya mnadhimu mkuu wa upinzani Bungeni iliyokuwa ikishikiliwa na Tundu Lissu (Chadema) sasa itashikiliwa na Mbunge wa Tumbe, Rashid Abdalah kutoka chama cha CUF.
Akitangaza baraza hilo Bungeni mjini Dodoma jana, Mbowe alisema Wizara ya Katiba na Sheria imeongezewa majukumu ya Muungano na waziri wake atakuwa ni Lissu na naibu wake ni Abdalah.
Pia amemteua Mbunge wa kuteuliwa na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa taifa wa NCCR-Mageuzi,  James Mbatia ambaye anakuwa Waziri wa Fedha wakati Naibu wake atakuwa Christina Lissu kutoka Chadema.
Mawaziri Ofisi ya Rais ni Profesa Kulikoyela Kahigi (Utawala Bora-Chadema), Vicent Nyerere (Utumishi-Chadema) na Esther Matiko (Mahusiano na Uratibu-Chadema).
Ofisi ya makamu wa Rais itakuwa na mawaziri wawili ambao ni mchungaji Israel Natse kutoka Chadema atakayeshughulika na Mazingira na Naibu wake atakuwa ni Assah Othman Hamad (CUF).
Mnadhimu wa Upinzani Bungeni ndiye atakayeshikilia pia nafasi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mazingira.
Mawaziri katika ofisi ya Waziri mkuu ni Pauline Gekul (Uwekezaji na Uwezeshaji-Chadema), Rajabu Mohamed Mbaruku (Sera, Uratibu na Bunge-CUF) na David Silinde (Tamisemi-Chadema).
Wizara ya Chakula, Kilimo na Ushirika itashikiliwa na Meshack Opulukwa (Chadema), Wizara ya Nishati na Madini atakuwa John Mnyika Chadema na Naibu wake “atakuwa Raya Ibrahim (Chadema).

Kulingana na orodha hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itashikiliwa na Ezekiah Wenje (Chadema) na Naibu wake ni Rashid Abdalah  kutoka  CUF.
Mawaziri wengine na wizara zao kwenye mabano ni Felix Mkosamali (Ujenzi-NCCR-Mageuzi), Magdalena Sakaya (Maji-Cuf), na Moses Machali (Uchukuzi- NCCR- Mageuzi).
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaongozwa na Godbless Lema wa Chadema na Naibu wake ni Khatibu Said Haji wa CUF wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ni Halima Mdee wa Chadema.
Kwa mujibu wa orodha hiyo, Mbowe amemteua Rose Kamili Sukum kutoka Chadema kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi wakati Naibu wake atakuwa ni Mkiwa Adam Kiwanga wa CUF.
Wizara ya Maliasili na Utalii itashikiliwa na mchungaji Peter Msigwa (Chadema), Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeenda kwa Joseph Selasini (Chadema) na naibu ni Rukia Ahmed Kassim (CUF).
Mbowe pia amemteua Masoud Abdalah Salim wa CUF kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na Wizara ya Elimu itashikiliwa na Susan Lyimo  na Naibu wake ni Joshua Nasari wote toka Chadema.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeenda kwa Dk Gervas Mbassa na Naibu wake ni Conchesta Rwamlaza wote wa Chadema. David Kafulila (NCCR) ameteuliwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Katika baraza hilo la mawaziri, Injinia Habib Mnyaa wa CUF ameteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wakati Lucy Owenya kutoka Chadema akiteuliwa kuwa naibu wake.
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imeenda kwa Baruan Salum Khalfan wa CUF na Naibu wake ni Subreena Sungura wa Chadema. Cecilia Paresso wa Chadema anakuwa Waziri wa Kazi na Ajira.
Wizara ya Habari, Vijana na Michezo imeendelea kushikiliwa na Joseph Mbilinyi wa Chadema.
Akizungumza na wanahabari, Mbowe alisema wakati katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya CCM, wanaume ni 36 na wanawake 15, wao upinzani wanaume ni 26 na wanawake ni 14.
Hali kadhalika Mbowe alisema wakati Baraza zima la mawaziri la Serikali ya CCM likiwa na mawaziri kamili 28 na manaibu 22, wao Baraza lao Kivuli lina mawaziri kamili 28 na naibu mawaziri 12.
Alisema nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Ubungeni iliyokuwa ikishikiliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe itantangazwa baadaye

Lugola: Serikali ya CCM inaendeshwa kisanii

Dodoma. Mbunge machachari wa Mwibara, Alphaxard Kangi Lugola, amedai kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii.
Lugola ambaye katika Bunge lililopita aliwaongoza wabunge wenzake kuichachafya Serikali hadi mawaziri wanne kujiuzulu nyadhifa zao, jana aligeuka tena mwiba kwa Serikali ya CCM.
Akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Lugola alisema anashangaa Waziri mwenye dhamana, Christopher Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blabla.
Pia alimgeukia naibu wa wizara hiyo, Godfrey Zambi na kumwambia kuwa amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma bungeni akipaza sauti, lakini baada ya kupata madaraka amewageuka na kushirikiana na waziri.
Akichangia kwa hisia kali, Lugola alihoji inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki ofisini kama Waziri.
“Waziri huyuhuyu ndiye anayezindua mbegu aina ya Chutoni ambayo haioti, bado ni Waziri. Waziri huyu huyu analipa ruzuku mbegu ya pamba isiyoota bado ni Waziri,” alisema Lugola.
Lugola alihoji kama Mchina aliyekuwa akijenga daraja la Kilombero alijiua kwa sababu tu ya kuhofia kupigwa risasi atakaporudi kwao, hata Waziri Chizza alipaswa awe ameiacha kazi hiyo.
“Simshauri waziri ajiue, lakini kwa vitendo vyote hivi waziri huyu angekuwa ameacha wizara hii na kupumzika na kufanya kazi nyingine mbadala,” alisema Lugola huku akipigiwa makofi.
Lugola alikumbushia Chizza alikuwa ni miongoni mwa mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo na kusema mambo yanayofanywa na wizara hiyo yatakigharimu Chama Cha Mapinduzi.
Mbunge huyo alibainisha kuwa, katika hotuba yake mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha mfuko wa kinga ya pamba ili kuwasaidia wakulima.
Hata hivyo, alisema katika hotuba ya Waziri Mkuu juzi, hakuna sehemu aliyozungumzia mfuko huo wala Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika hotuba yake ya mwaka huu, naye hajazungumzia mfuko huo.
“Hivi nchi hii tunaiendesha kwa usanii mpaka lini? Usanii juu ya usanii… Hatuwezi kuwadanganya wananchi kwa kiwango hiki. Itakuwaje mimi mbunge niunge mkono bajeti ya namna hii?” alihoji.

Alimgeukia Zambi na kumweleza kuwa aliwahi kumtahadharisha kuwa atakapokuja na bajeti yake ahakikishe anampa majibu ya asilimia 20 ya malipo waliyoahidiwa wakulima waliotumia mbegu ya chutoni.
“Uniambie asilimia 20 ya malipo ya wakulima ambayo waliahidiwa kwamba wakitumia chutoni walipwe kama sehemu ya malipo yao, lakini hili halimo kwenye bajeti,” alisema na kuongeza:
“Hakuna lolote humu ni blabla tu… Mheshimiwa Zambi wewe ulikuwa ‘backbencher’ (kiti cha nyuma) kama mimi ulikuwa unapiga muziki kama kasuku juu ya wizara hii, leo unashirikiana na waziri wako unakuja na vitu ambavyo havina majibu, maana yake nini?”
Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema wakati Zambi akiwa mbunge, alikuwa msitari wa mbele kupinga matumizi ya mbolea ya minjingu na kumtaka aeleze kama bado ana msimamo huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), aliwashukia wakuu wa mikoa ya Simiyu na Geita kuwa ni chanzo cha tatizo kwa wakulima wa pamba.
Mbali na hilo, amemtaka Balozi wa Uingereza nchini ajitokeze kueleza misaada inayotolewa na nchi yake inavyotumiwa kwenye sekta ya pamba kwani imekuwa ni sehemu ya ubabaishaji kwa kuendeshwa semina zisizo na maana.
Shibuda alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia maoni kwenye hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2014/15.
Aliwatuhumu wakuu hao kuwa walimpeleka Waziri Mkuu katika kampuni ya Kiotoni wakamdanganya kuwa mbegu hizo ni nzuri, lakini kumbe hazikuwa zimefanyiwa utafiti wa kina na kuwasababishia hasara kubwa wakulima.
Shibuda alisema mbegu za kiotoni zina udhalimu mkubwa na hazina tija yoyote kwa wakulima lakini kila siku wakuu wa mikoa na wilaya wanazipigia debe licha ya kuwa wanatambua kwamba wakulima wanaumizwa.
Magdalena Sakaya aliifananisha Serikali kuwa ni sawa na sikio la kufa kwa kuwa kila wakati imeshindwa kuwa na majibu ya ukombozi kwa wakulima wa Tanzania ambao ndio wapigakura wao.
Mbunge wa Kasulu, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) aliwapongeza wabunge wa CCM wanaoonyesha ujasiri wa kuisema Serikali yao kuwa inaendesha mambo kisanii na hivyo kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo.
“Serikali imekuwa ikidanganya katika kutatua matatizo ya wananchi ndiyo maana tunaona ni Serikali ya maigizo… Ukisoma hotuba ya bajeti hapa haijibu matatizo ya wananchi,” alisema.
Wakati wabunge hao wakiiponda bajeti hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Serikali, kueleza ni lini na vipi wakulima walioathirika na mbegu feki watafidiwa.
Msemaji wa Kambi hiyo wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili, alisema tayari wakulima wameshapata hasara na bado wako wanaoendelea kuathirika na tatizo la mbegu kutoota.

Friday 9 May 2014

Kafulila awalipua mawaziri akaunti ya Escrow

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila jana aliibua tuhuma nzito bungeni akiwahusisha mawaziri wawili na Sh200 bilioni zilichotwa katika Akaunti ya Escrow, iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika tuhuma hizo, alimuunganisha pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wa Serikali, wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Kafulila alitoa tuhuma hizo bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/15.
Mbunge huyo alisema fedha zilizoibwa katika Akaunti ya Escrow ni nyingi kuliko zile zilizoibwa katika kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT mwaka 2005.
“Pamoja na hilo, Watanzania wamekuwa wakisikia kwenye vyombo vya habari kwamba Tanesco wakati ilipokuwa na mgogoro na IPTL walifika mahali wakafungua akaunti ya Escrow,” alisema.
Mbunge huyo alisema akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2004 na hadi jana, akaunti ile ilishafikia Dola za Marekani 122 milioni,” alisema Kafulila.
Alisema fedha hizo ziliwekwa kwa lengo maalumu kutokana na mgogoro uliokuwapo kati ya IPTL na Tanesco ili ziweze kusaidia malipo baada ya mgogoro kuisha katika Baraza la Usuluhishi wa Kibiashara la ISCID.
Alitaka jambo hilo liingie kwenye rekodi kwa kuwa linahusu BoT na vigogo akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu wake na pia Waziri wa Fedha.
Alisema wakati Tanesco ikidaiwa madeni zaidi ya Sh400 bilioni, viongozi hao wameidhinisha kugawanywa kwa fedha hizo kihuni jambo alilosema halivumiliki hata kidogo.
Kafulila alisema fedha hizo zilichotwa na Kampuni ya PAP aliyosema ya “Singasinga na ya kitapeli” ambayo iliidhinishiwa kuchota fedha hizo kinyume na utaratibu.
Alisema fedha hizo hazikupaswa kuchukuliwa kwa kuwa kulifanyika udanganyifu mkubwa kwamba PAP ilikuwa imenunua IPTL wakati jambo hilo si la kweli.
Alisema IPTL ilikuwa na makubaliano ya kufanya kazi kwa kampuni mbili ambazo ni VIP Engineering ya Tanzania iliyokuwa na hisa asilimia 30 na Mecmer ambayo ilikuwa na asilimia 70 ya hisa.
Hata hivyo, alidai kuwa anao ushahidi kuwa PAP ilikuwa imenunua hisa za VIP na hakukuwa na vielelezo vya kununua Mecmer kwa kuwa kampuni hiyo tayari ilishapoteza uhalali wake kwa kuwa ilikuwa chini ya muflisi nchini Malaysia.
Aliliambia Bunge kuwa wakati wa uchukuaji wa fedha hizo kutoka BoT, ilipaswa kulipiwa kodi lakini zilichukuliwa kinyemela bila hata ya kulipiwa kodi.
Alisema TRA iliiandikia Hazina na nakala kwa BoT kwamba wakati wa kulipa fedha hizo lazima kodi ikatwe, lakini cha ajabu hilo halikufanyika licha ya kukumbushwa.
“Kwa mfano, tulimwita Gavana katika kikao chetu cha Kamati ya Uchumi pale Bagamoyo na alikiri kuwa alibanwa na viongozi wa juu kiasi cha kushindwa kufurukuta, kwa hali kama hiyo Naibu Spika unategemea nini?” alihoji.
Kafulila alisema, Gavana katika kikao hicho alikiri kuwa, kulikuwa na presha (shinikizo) ambazo asingeweza kuzizuia na kuwa alikuwa amejitahidi kwa kiasi kikubwa hadi kufikia alipofika.
Alisema ISCID lilitoa hukumu ndogo Februari, mwaka huu kuwa Tanesco na IPTL wakae pamoja na kupitia hesabu zao namna watakavyogawanya fedha hizo na walipewa siku 60 ambazo mwisho wake ulikuwa jana.
Aliituhumu Tanesco kuwa katika makubaliano hayo ilikataa kukaa meza moja na kufanya hesabu za namna ya kulipana jambo alilosema linaonyesha ilidhamiria kufanya hivyo.
“Kwa sababu wanajua kuwa fedha ile ilishaliwa na wajanja wachache, Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili kwa vyovyote halikubaliki na halivumiliki kwa sababu Dola122 milioni ni zaidi ya Sh200 bilioni ambazo ni nyingi kuliko za EPA, lazima litoke na mtu.”
Alisema hayuko tayari kuona fedha hizo zikitafunwa bila ya utaratibu na akashangazwa kuona Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akishindwa kuchukua hatua.
Akoleza moto jioni
Katika kikao cha jioni, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alimwita tena Kafulila kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa mchana, ambayo iliombewa mwongozo na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kwamba Gavana alishinikizwa kutoa fedha hizo.
Wakati wa mwongozo huo, Kafulila hakuwapo na ndiyo sababu ya Mwenyekiti kumpa nafasi ya kufuta kauli yake kuwa Gavana alishinikizwa. Hata hivyo, Kafulila alikazia akisema alishinikizwa kutoa fedha hizo.
“Gavana aliwahi kuniambia, mnanionea bure. Kulikuwa na presha kubwa sana kuhusu fedha hizi… ukweli ni kwamba IPTL inabadilishwa tu rangi na watendaji ni walewale.”
Baada ya Kafulila kuzungumza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na kusema: “Tuhuma dhidi ya Gavana wa Benki Kuu zinatolewa kwa kuwa hawezi kuingia bungeni kujitetea.
“Lakini Gavana tulimuuliza na akakanusha kuwa aliwahi kuyatamka hayo maneno na kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni atakuja kufafanua jambo hili kesho (leo) katika hotuba yake,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisimama kuomba mwongozo akisema: “Kamati ya Bunge iundwe ili tuchunguze fedha hizi za Escrow zimekwenda wapi? Kafulila ana ushahidi wa kutosha, kwa nini hamtaki athibitishe?
“Vikao vyote vya kamati vinawekewa kwenye kumbukumbu rasmi (hansard) ili kujua kama Gavana alitoa maneno hayo ama hakutoa, iundwe kamati ijulikane mbivu na mbichi na wezi wa fedha za Escrow tunao humu ndani ya Bunge.”