Tuesday 20 May 2014

Wabunge wataka JK aunde tume ya elimu

Dodoma/Dar. Baadhi ya wabunge jana walichachamaa wakisema elimu nchini ipo mahututi na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kudumu ya elimu itakayochunguza mfumo wa elimu nchini.
Wabunge hao walikuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2014/2015 iliyowasilishwa na waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa Jumamosi usiku.
Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer alipendekeza safari zote za wabunge na mawaziri nje ya nchi zifutwe na fedha zake zipelekwe kuboresha shule za kata.
Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alizungumzia uduni wa vitabu na mitihani ya wanafunzi wa shule za msingi akisema inakosewa kutungwa.
“Nina mtihani wa majaribio wa darasa la saba ambao haufanyiki. Niliwahi kumpa profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye alitumia saa mbili na nusu bila kupata jibu lolote la kuandika. Mtihani wenyewe haufanyiki,” alisema Mbatia na kutoa ofa ya Sh10 milioni kwa profesa mwingine yeyote bungeni ambaye ataweza kufanya mtihani huo na kupata alama 100.
“Haya ni madudu ya kutisha. Mwaka jana nilivyotoa maoni yangu hapa na waziri akasema maoni yetu yamechukuliwa, alisema rasimu ya mwisho sera ya elimu imepelekwa Baraza la Mawaziri Machi 2013, lakini hadi sasa bado haijakamilika,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni dalili ya Bunge kutoheshimiwa.
Pia alizungumzia ripoti za kamati zilizoundwa kuchunguza elimu lakini hazikufanyiwa kazi na badala yake zikawekwa kwenye makabati.
“Tumwombe Rais aunde Tume ya Kudumu ya Elimu kwa sababu kwa hali inavyokwenda ni mbaya sana na napendekeza tume hii ishughulike na kudhibiti mambo yote yanayofanya kutetereka kwa ubora elimu nchini.
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alisema elimu ya Tanzania iko mahututi na kuwaomba wabunge kuacha siasa katika elimu.
“Bajeti itapita lakini tunaua kizazi kijacho. Mheshimiwa mwenyekiti nenda darasa la kwanza mpaka la saba anayoyasema Mbatia yapo hata kama hatuyapendi lazima tuseme ukweli,” alisema.
Alisema ukienda katika vyuo vikuu ni majanga. “Kama unajiangalia wewe na familia yako, basi tunaliua Taifa. Nimefanya utafiti kwenye nchi 35, Tanzania ni nchi ya mwisho kwa ufaulu,” alisema na kuongeza kuwa nchi zote zilizoendelea kiuchumi, kiwango cha ufaulu ni juu ya asilimia 60.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina alisema hakuna Wizara ya Elimu baada ya elimu ya sekondari na msingi kuondolewa
“Mbele ya Waziri Mkuu niseme kuwa sasa hatuna Wizara ya Elimu… na sasa wanaondoa elimu ya watu wazima, shule zote za mazoezi zimeondolewa.”
Mbunge wa viti maalumu (CUF), Magdalena Sakaya alisema anashangazwa na wizara kushusha madaraja ya ufaulu ambayo awali, kuanzia alama 34 ilikuwa ni daraja O lakini leo ni ufaulu.
“Kiukweli waziri aliyeko katika wizara hii ameshindwa kusaidia elimu nchini. Tangu ameshika wadhifa huo anazidi kubebwa. Kwa nini tunambeba mtu ambaye ameshindwa kusaidia elimu nchini?” alihoji.
Safari za nje
Laizer alitaka safari za mawaziri na wabunge nje ya nchi zifutwe na fedha hizo ziboreshe shule za kata ambako ndiko watoto wa maskini wanakosoma.
Alisema anashindwa kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo wakati watoto wake wote katika jimbo lake wanafeli kutokana na shule za kata kutokuwa na walimu wa kutosha.
Akifanya majumuisho, Waziri Kawambwa alikiri deni la Sh61 bilioni la madai ya walimu, lakini akasema serikali imekuwa ikilipa.
Alisema kuanzia Agosti mwaka jana hadi Machi, jumla ya Sh16 bilioni zimelipwa na kwamba si kweli kwamba deni hilo limebakia kuwa Sh61 bilioni.

No comments: