Zitto akiwa wilayani Igunga hivi karibuni,
alijitoa mhanga na kutangaza viwango alivyodai kuwa ni mishahara ya
rais na waziri mkuu kwa mwezi, huku akihoji iweje viwango viwe siri na
visikatwe kodi.
Baadhi ya watu wamepinga hatua hiyo wakisema
mshahara wa mtu ni siri yake. Waliopinga ni pamoja na Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai na Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
utumishi wa Umma, Celina Kombani akisema kuwa kufanya hivyo ni kinyume
cha sheria.
Sawa, inaweza kuwapo sheria inayozuia jambo hilo, lakini kwanini itungwe sheria ya namna hiyo?
Kwa upande wangu naunga mkono mishahara hiyo kuwa
wazi. Nakubali kwamba mshahara wa mtu ni siri yake, lakini kwa viongozi
wa umma kama rais na waziri mkuu, mishahara yao haipaswi kuwa siri,
ndiyo maana nchi nyingi duniani zikiwemo Marekani, Ufaransa, Kenya na
Afrika Kusini, mishahara ya viongozi kama huwekwa wazi.
Ifahamike kuwa rais ni kiongozi anayechaguliwa na
wananchi, wao ndiyo wanaompa ajira ya kuwatumikia. Iweje mwajiri asijue
anacholipwa mtumishi wake?
Kwenye nchi zilizoendelea kidemokrasia kama vile
Marekani na nchi za Ulaya, masilahi na utendaji wa rais na waziri mkuu
na viongozi wengine ni ya kikatiba.
Wananchi wanajua wazi kabisa, rais wanayemchagua
watamlipa kiasi gani, Katiba inamwelekeza rais ateue mawaziri wangapi na
watendaji wa Serikali kwa idadi maalumu.
Cha ajabu huku kwetu, rais anaamua kufanya
atakavyo – anaweza hata kuteua mawaziri idadi anayoitaka na asiulizwe,
mambo yanafanywa kwa siri ndiyo maana hata mikataba ya madini na
uwekezaji mwingine ni siri.
Siri hizi za nini kama sisi wananchi ndiyo tumeichagua Serikali yetu wenyewe?
Hoja nyingine ni kuhusu mshahara wa rais kutokatwa
kodi. Rais ni mtumishi wa umma namba moja na mlezi wa watumishi hata wa
sekta binafsi.
Kwa muda mrefu wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia
kiwango cha asilimia 15 cha kodi wanayokatwa katika mishahara ndiyo
ikashushwa hadi asilimia 14, hata hivyo bado ni mzigo.
Lakini rais atauonaje mzigo huo ikiwa yeye hakatwi kodi? Rais
kwa mujibu wa Zitto analipwa wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila
kukatwa kodi, ana marupurupu ya safari za ndani na nje ya nchi na posho
nyinginezo.
Kwa maana nyingine rais anaweza asiuguse kabisa
mshahara wake kwa posho hizo, lakini bado akistaafu analipwa pensheni na
atatunzwa na Serikali maisha yake yote.
Tuna viongozi wa Serikali wangapi wanaolipwa hivi,
tuna marais wastaafu na mawaziri wakuu wangapi wanaofaidi kiinua mgongo
cha Serikali huku idadi kubwa ya Watanzania ikiteseka katika lindi la
umasikini na mlolongo wa kodi?
No comments:
Post a Comment