Mikoani

Idadi ya watu waliofariki Tanzania yaongezeka

Idadi ya watu waliofariki dunia baada ya mlipuko wa bomu katika mkutano wa Chadema imeongezeka baada ya mtoto Fahad Jamal (7) ambaye hali yake ilikuwa mbaya na kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Selian, kuaga  dunia juzi saa saba mchana hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga mtoto huyo alifariki dunia wakati timu ya madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam wakijitahidi kila hali kuokoa maisha yake.
Kifo hicho kinaongeza idadi ya marehemu na kuwa wanne baada ya vifo vya Amiri Ally (7), Judith Moshi (25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) Kata ya Sokon One jijini hapa na Ramadhan Juma (15).
Dk Kisanga alisema hospitali hiyo juzi ilipokea majeruhi wengine 17 wa mabomu ya kutoa machozi katika eneo la Soweto wakati polisi wakitawanya wafuasi wa Chadema.
Alisema majeruhi 14 wamelazwa huku watatu wakitibiwa na kuruhusiwa ambapo pia Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyekuwa amelazwa hapo kutokana na kuumia shingoni aliruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.
Mganga Mkuu alaani Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mount Meru, Dk Frida Mokiti, amelaani vitendo vya uvunjifu wa amani na vitisho vya wafuasi wa Chadema, ambavyo vilisababisha kuvunjwa kwa mlango wa gari la wagonjwa na kuvunja lango kuu la kuingilia hospitalini hapo.
Alisema katika tukio hilo la bomu, wafuasi hao wa Chadema, walitishia madaktari na wauguzi wa zamu na kutaka kuchoma moto majengo ya hospitali hiyo, wakishinikiza kutibiwa haraka kwa majeruhi wa bomu.
Aliongeza kuwa hospitali haikupata taarifa mapema ya mlipuko huo na hivyo kuchelewa kupeleka gari la wagonjwa kwenye eneo la tukio ili kutoa msaada na kilichotokea ni wafuasi wa chama hicho wakiwa na majeruhi walifika hospitalini na kuanza vitisho na kufanya fujo zikiwamo kutishia kuchoma moto magari na majengo ya hospitali hiyo.
Alisema hospitali hiyo haibagui wagonjwa wala haitoi huduma kwa itikadi au imani ya mgonjwa bali kazi yake ni kuhudumia watu wote bila ubaguzi.
Dk Mokiti, aliishukuru Wizara ya Maliasili na Utaliii kwa misaada ya vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 120 kwa hospitali zote tatu za Mount Meru, Selian na St Elizabeth.
Alisema pia wamepokea madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Moi Kenya, ambao wameongeza nguvu ya kuhudumia majeruhi wa mlipuko huo. Wakati huo huo, kitendo cha wanasiasa kunyoosheana vidole kuhusu tukio hilo la bomu kimeshutumiwa kuwa kinaweza kuathiri upatikanaji wa wahusika sahihi.
Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, walisema shutuma na mvurugano miongoni mwa wanasiasa, vitasababisha Serikali kujikita katika kutatua mifarakano hiyo badala ya kutafuta mbaya wa Watanzania.
Utalii Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa kuhusu sekta ya utalii kuathirika na milipuko ya mabomu Arusha au safari za watalii kusimama, alisema hali ya usalama Tanzania hususan Arusha ni nzuri na kuomba watalii kuendelea kuja nchini kuona vivutio vya utalii.
Alisema Tanzania kuna amani na ndiyo maana hata Rais wa Marekani, Barack Obama anatarajia kuja nchini na kuongeza kuwa kutokana na amani iliyopo milango ya utalii imezidi kufunguka, kwani hivi sasa watalii kutoka Japan, China, Uturuki na sehemu mbalimbali duniani wanakuja kuangalia vivutio hivyo.
Aliongeza kuwa amani ni muhimu kwa Tanzania hususan Arusha ambalo ndio mlango wa sekta ya utalii na kuwasihi viongozi wa vyama vya kisiasa kuhakikisha wanalinda amani nchini kwani endapo itapotea waathirika wengi wakiwamo wadau wa sekta ya utalii, hoteli, wauzaji mboga na wengine wataathirika kimapato na uchumi kudorora.
Katika hatua nyingine, wananchi wa Arusha na viunga vyake, wanaendelea na shughuli zao za kila siku huku wengine mapema jana asubuhi walifika eneo la Soweto kuangalia vitu walivyokuwa wameangusha juzi.
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia baadhi wakiwapa watoto wa mitaani Sh 500 hadi Sh 1,000 ili kuwasaidia kuangalia kama simu, pochi na vitambulisho vyao kama vipo; wengine walivipata lakini wengine hawakuambulia kitu.
Imeandikwa na Veronica Mheta, Gloria Tesha, Shadrack Sagati na Prisca Libaga


 Mizengo Pinda, Nasema wapigwe tu!!!!!



Dodoma/Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma jana, Pinda alisema watu wanapokaidi wanajitakia matatizo na vyombo vya dola.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.”
Pinda alisema Serikali imedhamiria kurejesha amani nchini ikiwamo mkoani Mtwara na kuwataka Watanzania waiache Serikali ifanye kazi hiyo. Alisema Serikali ina orodha ya watu wanaosemekana kuwa ni vyanzo vya vurugu na matatizo yaliyotokea Mtwara na kushangaa wale wanaopinga kukamatwa kwao.
“Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, jeuri, watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda. Nami nasema vyombo vya dola vijipange imara vihakikishe vinadhibiti hali hii,” alisema.
Hata hivyo, jibu hilo lilipata upinzani wakati Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji alipomwuliza Waziri Mkuu: “Hapo awali umetoa kauli nzito ya kuliambia taifa hili kwamba wale raia wote, ambao watakaokuwa wakaidi wapigwe tu na watapigwa tu; naomba ninukuu Katika Ibara ya 13 na Kifungu cha 6B cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
“Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kuteswa kama mtu mwenye kosa, mpaka itakapothibitika anayo hatia kwa kutenda kosa hilo.
“Pia ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema ni marufuku kwa mtu yoyote, kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazoweza kumdhalilisha. Kwa kauli yako uliyoitoa huoni kwamba umevunja Katiba?” Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni lazima kutofautisha kati ya mtu aliyekwishakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria... “Mimi ninayemzungumza hapa ni mtu yule ambaye ameamua kufanya vitendo hajakamatwa na ndiyo maana nilikwambia usiandamane... hapa mahali hutakiwi kwenda wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mko wengi, ndiyo maana nikasema, hawa watu tutashughulika nao hivyohivyo.”
Mbunge huyo hakuridhishwa na majibu hayo na kumtaka Waziri Mkuu kuyafuta.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia katika na kumweleza mbunge huyo kuwa kila mtu alikuwa amemwelewa Waziri Mkuu na hakukuwa na haja ya kuendelea na hoja hiyo.
 
Kabla ya swali lake la nyongeza, Mangungu aliuliza: “Ukisikiliza nyimbo nyingi za taifa katika Afrika zinasema hekima, umoja na amani ndiyo ngao zetu. Je, hali ambayo imejitokeza katika nchi yetu na matatizo yaliyojitokeza Arusha na maeneo mengine kama Mtwara. Nini tamko la Serikali?
Waziri Mkuu alijibu: “Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mangungu ni jambo linalotugusa sisi wote. Suala la amani, ulinzi, utulivu ndiyo hasa tunu ya kila nchi ingependa kuwa nayo. Ni kweli hivi karibuni kumejitokeza vurugu za hapa na pale kwa hiyo angependa tuwaeleze Watanzania kama Serikali tunafikiria tufanye nini.
Alisema ipo haja ya jukumu hilo kuachwa kwa viongozi wa kisiasa bila ya kujali itikadi zao... “Yako mambo ambayo lazima tukubali kwamba ni jukumu letu sisi wote na kila mmoja lazima azungumze lugha moja.
Ninyi wote ni mashahidi. Chadema waliposhinda hapa, wao walikuja waziwazi, wakasema tutahakikisha nchi hii haitawaliki. Sasa, inawezekana pengine ndiyo mwendelezo wa utekelezaji wa kauli hizo.
“La pili ni upande wa Serikali, lazima tuhakikishe kwamba wale wote ambao kwa kweli wanajaribu kuvunja amani kwa namna yoyote ile, kazi kubwa tuliyonayo ni kubanana, kupambana kwelikweli kwa njia zozote zile zinazoonekana zinastahili.
“Sasa mimi ninaomba sana Watanzania, maana kila juhudi zinapoonekana zinaelekea huko, unapata watu wengine wanajitokeza, unajua...unajua. Acheni Serikali itimize wajibu wake kwa sababu jambo hili ni la msingi, lazima tulilinde kwa nguvu zetu zote.
“Rai yangu kwa Watanzania kila mmoja ajue kwamba siku tukiingia katika vurugu, hakuna mshindi. Wote tutaumia, sasa wote tuhakikishe hili jambo tunalisimamia vizuri.”
Chadema waja juu
Akizungumzia kauli hiyo, Mkurugenzi Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema: “Kauli ya Pinda inakiuka Katiba ya nchi na imethibitisha kwamba matumizi mabaya ya vyombo vya dola na kusababisha mauaji ya raia yana baraka za Serikali.”
Alisema kauli ya Pinda kama ilivyokuwa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi zinatoa mwelekeo kwamba mauaji ya Arusha yana baraka za Serikali.
Wanasheria wakerwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Waziri Mkuu hakustahili kutoa kauli kama hiyo.

Alisema Pinda hapaswi kuwa na jazba, bali anatakiwa kuwa na busara na kuzungumza kwa kuzingatia sheria za nchi badala ya kutoa matamshi ambayo siyo mwafaka kwa nchi inayoongozwa kwa kufuata sheria na taratibu.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema kauli hiyo ya Waziri Mkuu, mbali ya kwenda kinyume cha Katiba na sheria ya nchi, inaweza kuhatarisha amani.
Stola alisema matumizi ya nguvu kupita kiasi kudhibiti hali yoyote korofi hayaruhusiwi.


Bongo Star Search kusajili zaidi 50,000

Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel, imezindua msimu mpya wa shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search, mwaka huu ikiwa imejipanga kuwapa vijana wengi zaidi fursa ya kuonyesha na kuendeleza vipaji vyao.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benchmark Production, Rita Paulsen msimu huu wa saba toka shindano hilo lianzishwe mwaka 2006, kuna vitu vingi vipya ikiwamo ongezeko la jaji mmoja ambaye ni mdau wa muziki kutoka mkoa husika.
Naye Afisa Biashara mkuu wa Zantel, Sajid Khan alisema uzinduzi huo ni furaha kwa kampuni hiyo kwani unaashiria ufunguzi wa milango ya kuwasaidia vijana wengi wa Kitanzania kutimiza ndoto zao.
“Mwaka jana pekee Epiq BSS ilifanikiwa kusaili vijana zaidi ya elfu hamsini, jambo ambalo linaloonyesha kuna uhitaji wa kuwekeza zaidi katika kuwaendeleza vijana’ alisema Khan.
Katika kuwapa fursa vijana ambao hawatafikiwa na majaji, Zantel kwa kushirikiana na Push Mobile watafungua laini za kurekodi kwa simu.

 



No comments: