Ni jana tu nimemaliza uchambuzi wa watu wanaotajwa au
waliojitokeza kugombea urais au wale ambao hawajajitangaza na hawana nia
lakini jamii ndani na nje ya vyama vyao inawataja kama watu wenye sifa,
uwezo na hata vigezo vya kuiongoza nchi yetu, kutoka vyama vya
upinzani.
Lengo la uchambuzi huu ni kuwafanya Watanzania
waanze kuwafahamu viongozi wao wajao na hata aina ya sifa wanazoweza
kuwa nazo. Inawezekana kabisa kuwa wagombea waliochambuliwa asitokee
mmoja wao kugombea au la, lakini hapa ninachoangalia ni kwamba tayari
wananchi watakuwa “wamesogezwa karibu na ajenda ya uchaguzi” na hata
akiletwa mgombea kutoka wapi, walau wananchi watakuwa wanajua wafanye
uamuzi wa namna gani.
Leo nahitimisha hoja ya wagombea wa upinzani kwa
kutoa sifa 10 za mgombea urais bora kutoka upinzani ambaye anaweza
kupigiwa kura nyingi na Watanzania na hatimaye kuwa rais mpya wa
Tanzania:
1. Mwenye umaarufu/umashuhuri na anayekubalika
Sifa hii ni muhimu, unapokuwa nje ya dola na nje
ya chama tawala siyo rahisi kukishinda chama kinachoongoza Serikali.
Umaarufu, umashuhuri na kukubalika ni mambo ya lazima. Ukitizama
historia ya dunia na hata Afrika, vyama vikongwe vilipoondolewa
madarakani waliofanya hivyo walikuwa wapinzani mashuhuri. Umuhimu wa
sifa hii ni kuwa walau mtu maarufu na mashuhuri au anayekubalika, tayari
amewekeza “mbegu” kwenye mioyo ya wananchi, wanaweza kumwamini ili
waondoe hatima ya nchi mikononi mwa chama kilichowaongoza kwa miaka 50
na kuiweka mikononi mwa watu wapya. Wananchi wasipomwamini kiongozi wa
upinzani anayekuja kwa sababu wanamkubali, ndipo huzuka ile kasumba ya
“tupige kura kwenye zimwi likujualo”.
Hatari ya sifa hii
Umaarufu, umashuhuri na kukubalika vitaweza
kufanya kazi kwa upinzani ikiwa mgombea husika hatatumia mwanya wa
kukubalika kwake kujenga kiburi na hatimaye kuwasaliti wananchi. Ndiyo
kusema kuwa vyama vya upinzani vitapaswa kuchagua mtu bora ambaye
atatimiza matakwa ya wananchi “hata kama ni maarufu kuliko jua”.
2. Atakayebeba ajenda bora na kuifafanua vizuri
Kubeba ajenda bora na kuwa na uwezo wa kuifafanua
kwa lugha rahisi ni jambo la muhimu kwa mtarajiwa kutoka upinzani. Moja
kati ya makosa makubwa ya vyama vya upinzani katika bara la Afrika ni
kutaka kubeba ajenda nyingi na kumrundikia mgombea urais, nakubali kuwa
Afrika ina matatizo katika kila sekta ya maisha ya mwanadamu, lakini
lazima iwe na vipaumbele vinavyowaumiza wananchi. Mgombea bora wa urais
kutoka upinzani atapaswa kuwa na ajenda bora kuliko ile ya CCM na
atapaswa kuwa na uwezo wa kuifafanua akaeleweka na mipango ya
utekelezaji wake ikawa siyo ya “kusadikika”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale inapotokea kuwa mgombea bora wa urais
kutoka upinzani anazunguka nchi na ajenda iliyo bora kabisa lakini
utekelezaji wake ukifanana au kushabihiana moja kwa moja na ule wa
mgombea wa CCM. Wananchi wakiona upinzani unahubiri mipango na mbinu
zilezile za CCM wataamua pia kuchagua “shetani wanayemjua” ili kujiweka
kwenye mazingira ya usalama zaidi. Hivyo, ajenda ya mgombea bora wa
upinzani na utekelezaji wake vinapaswa kuwa “vya kipekee”.
3. Mwenye uzoefu na rekodi ya uchapakazi
Uzoefu wa uongozi na uchapakazi unaofahamika ni jambo la msingi
kwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani. Vyama vya upinzani haviwezi
kushinda uchaguzi na mgombea bora vitakayekuwa naye ikiwa mtu huyo si
mzoefu na mchapakazi anayefahamika, mtu mwenye kujali wengine katika
kazi lakini ambaye wananchi wataamini kuwa huyu atasimama pamoja na sisi
usiku na mchana kuleta mabadiliko ya nchi.
Katika siasa, wananchi hupaswa kwanza kuamini na
kisha hufanya uamuzi. Ikiwa mgombea bora wa urais wa upinzani hatakuwa
na rekodi za uzoefu wa utumishi (katika taasisi za dini, serikali, vyama
vya siasa na nyinginezo) si rahisi kumuuza kwa wananchi. Pia, ni lazima
awe ni mtu ambaye rekodi zake zinatajwa kuwahi kuleta mabadiliko
makubwa mahali alipofanya kazi.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii hupaswa kuelezewa na kufahamika kwa
wananchi kutoka kwa timu za kampeni za wagombea, wakati mwingine wapambe
wa wagombea huchukua muda mwingi kutaja elimu ya mgombea wakidhani
wananchi wanachagua elimu, kumbe elimu ni jambo moja tu kati ya sifa 100
za kiongozi. Ikiwa sifa hii muhimu haielezwi kwa uwazi kwa wananchi na
hasa kwa kutaja rekodi bora za mgombea wa upinzani, wananchi wanaweza
kumpa kisogo.
4. Mwenye uadilifu usio na shaka
Mgombea bora wa upinzani katika uchaguzi, anapaswa
kuwa na uadilifu uliotukuka, usio na madoa wala shaka. Hapa nina maana
kuwa, awe ni mtu ambaye uadilifu wake unatambulika kwa wananchi na kwa
Taifa zima. Awe na rekodi za uadilifu kumshinda mgombea wa CCM, nina
maana kuwa, wananchi wakimpima huyu wa upinzani na yule wa CCM – haraka
haraka wasimame na kusema, “…naam! Huyu wa upinzani ni mwadilifu zaidi”.
Marais wengi walioingia madarakani hasa hapa Afrika na hata Ulaya na
Marekani kwa kuviondoa vyama vilivyokuwa madarakani, walipimwa kwa sifa
hii.
Hatari ya sifa hii
Kigezo hiki hupata shida kubwa katika nchi ambazo
uelewa wa wananchi vijijini na hata mjini si mkubwa. Wagombea waadilifu
nao huweza kuchafuliwa ndani ya siku moja tu. Katika nchi ambayo si
ajabu mgombea akawa hata na uwezo wa “kuhonga” chombo cha habari ili
kimchafue mwenzake, sifa za mgombea bora zinaweza kuingizwa katika tope.
Vyama vya upinzani vitapaswa kuwa na mfumo sahihi wa kuhakikisha
uadilifu wa mgombea wake unazungumzwa kama ulivyo na haubadilishwi na
propaganda za CCM.
5. Mwenye uwezo wa kusimamia, kuinua uchumi
Moja ya matatizo ambayo hayana dawa hapa Tanzania
ni usimamizi wa uchumi. Nchi yetu inayumba kila mara na tunashindwa
kutekeleza mipango yetu kwa sababu ya uchumi dhaifu, unaobadilika kila
dakika na ambao hauna dira. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani
atapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuinua uchumi wa nchi. Awe ni mtu
ambaye akisimama na kuweka ajenda ya uchumi mezani, Watanzania wote
wanamwelewa, kwamba “naam, huyu ana uwezo wa kusimamia uchumi na kuondoa
umaskini wa nchi”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale mgombea wa upinzani atazunguka na mipango
kabambe ya uchumi lakini yenye shaka kubwa kwenye utekelezaji au kuondoa
umaskini, lakini pia ni pale mipango hiyo haitakuwa ya muda mfupi.
Katika nchi maskini, wananchi wanahitaji matokeo haraka, vyama vya
upinzani vitakuwa na jukumu la kuwa na mipango ya mfano ya muda mfupi
ili kuwahakikishia wananchi kuwa ile ya muda mrefu pia itaweza
kutekelezeka kwa wakati.
6. Kuongoza mapambano dhidi ya rushwa
Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa katika
ukuaji wa uchumi wa Afrika. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani
atapaswa kuwa mtu wa kipekee ambaye moja ya sifa zake kuu ni mapambano
dhidi ya rushwa, ndogo na kubwa. Awe ni Mtanzania ambaye si tu kwamba
anapiga vita rushwa, bali anawachukia wala rushwa kama “kifo” na ni mtu
ambaye yuko mbali kabisa na wala “rushwa”. Ndani ya CCM kwenyewe nadhani
watatafuta mgombea wa namna hii ili kulinda hadhi yao, vyama vya
upinzani vitakuwa na jukumu la kutafuta mpinga rushwa mahiri kuliko yule
wa CCM, kwamba ukiwaweka pamoja hawa wawili – wananchi wenyewe waseme
“…naam huyu wa upinzani anaweza mapambano haya zaidi kuliko huyu wa CCM”
Hatari ya sifa hii
Ikiwa upinzani utakuwa na mtu mashuhuri katika
mapambano ya rushwa lakini ukawa hauna mipango ya kuhuisha haraka mifumo
inayoleta mianya ya rushwa ndani ya nchi. Ndiyo kusema kuwa moja ya
mipango ya upinzani inapaswa kuwa ni pamoja na kuweka wazi mifumo mipya
ya usimamizi wa mapambano dhidi ya rushwa na hata kueleza watu
watakaokuwa na sifa za kufanya kazi na mifumo hiyo.
7. Asiyependa kulipiza visasi na atakayefuata sheria
Jambo hili si dogo katika siasa. Rais ajaye kutoka
upinzani anapaswa kuwa na sifa hii. Kwamba afahamike na kujulikana kwa
kutokuwa na tabia ya kulipiza visasi lakini ambaye atazingatia matakwa
ya sheria katika utendaji na awe na rekodi hizo. Unajua, kuna mambo ya
kisheria ambayo ni lazima rais yeyote yule akiingia lazima ayafuate,
mfano, wizi wa pesa za umma, hata kama umefanywa mwaka 1960 na ushahidi
upo, lazima watuhumiwa wachukuliwe hatua leo, “jinai haifi wala
kupotea”. Lakini kuna masuala mengine mengi tu ya kawaida ambayo
yalikuwa yanatendwa na uongozi uliopita kwa sababu “za kipuuzi” na
zisizo na maana, hayana haja ya kuwa kichwani kwa rais anayekuja.
Hatari ya sifa hii
Wananchi wengi huhofia masuala ya usalama iwapo
vyama vipya vitaingia madarakani, hasa Afrika na moja ya masuala ambayo
hupoteza usalama ni “kulipiza visasi”. Ndiyo maana vyama vya upinzani
vinawajibika kuwa na mgombea ambaye hatalipiza visasi kwa makosa ya
nyuma ya kiutendaji, ila atafanya hivyo kwa yale yaliyokosewa kwa
makusudi na kwa kutofuata sheria.
8. Uwezo wa kubadilisha mfumo wa nchi
Tangu tumepata uhuru, nchi yetu imekuwa inasifika
kwa kuwa na mifumo mibovu na isiyo na tija katika kila sekta. Hili ni
janga kubwa. Rais bora ajaye kutoka upinzani ana kazi kubwa ya
kubadilisha mfumo wa sasa wa nchi katika kila eneo ili mifumo ifanye
kazi kwa mbio na kwa tija kubwa zaidi. Leo kuna watu walishtakiwa miaka
ya 1990 na bado wako gerezani bila kuhukumiwa, kuna Kiwanda cha Sukari
Kilombero na huko bei ya sukari ni kubwa kuliko Dar es Salaam. Haya ni
matatizo makubwa ya kimfumo. Wananchi watahitaji kuwa na kiongozi ambaye
atakuja kubadilisha kabisa mifumo ya utendaji kazi katika nchi. Kwa
bahati nzuri, upinzani unaweza kuwa na hoja kama hii kwani vyama hivyo
havikuwahi kuongoza Serikali na vimekuwa “waathirika” wa mfumo uliopo.
Hatari ya sifa hii
Ubadilishaji wa mifumo ukifanywa haraka na kwa
pupa, utaingilia na kuvunja hata mifumo ambayo ilikuwa imeanza kukua na
kukomaa kwa upande chanya. Ni jukumu la mgombea bora wa upinzani na timu
zake kutambua mifumo yote ya utendaji katika sekta za jamii na
kubainisha tangu wakati wa kampeni, ipi itavunjwa na ipi itarekebishwa
ili kutoleta hofu yoyote kwa wapiga kura.
9. Msimamo unaoeleweka juu ya Katiba
Suala la katiba mpya ni ajenda muhimu katika
uchaguzi wa mwaka huu. Mgombea bora wa upinzani atapaswa, yeye mwenyewe
kuwa na busara za kutosha na msimamo thabiti juu ya masuala ya kikatiba
na hasa mchakato wa Katiba Mpya. Naona kuna Watanzania wengi watapiga
kura katika uchaguzi wa mwaka huu kwa chama au mgombea ambaye atakuwa na
misimamo ya wananchi katika suala la katiba. Hadi sasa hatuelewi kama
katiba itapitishwa au la na hatuelewi kama wananchi wanaikubali au
wanaikataa. Nani atatuvusha na kwa utaratibu gani? Majibu atakuwa nayo
mgombea bora wa urais kutoka upinzani.
Hatari za sifa hii
Msimamo wowote ule wa mgombea urais wa upinzani
katika jambo hili unaweza kuwa na athari chanya au hasi kulingana na
namna wananchi wanavyolitazama suala la katiba. Kama mgombea huyu
atakuwa na msimamo katika kuikataa Katiba Inayopendekezwa na kwamba
ataanzisha mchakato mpya na ikiwa hayo ndiyo matakwa ya wananchi walio
wengi, jambo hili peke yake litamuongezea kura za kutosha. La ikiwa
kinyume chake, litakuwa na athari ya kiwango hichohicho bila kujali kama
athari yenyewe ni chanya au hasi.
10. Uzoefu wa masuala ya kimataifa
Moja ya kazi kubwa za mkuu wa nchi ni
kuliwakilisha Taifa katika masuala ya kimataifa. Rais bora kutoka
upinzani hakwepi kuwa na rekodi imara ya masuala ya kimataifa, si kuishi
Ulaya na Marekani, lakini kuwe na ushahidi wa kutosha kuwa amewahi
kushiriki katika baadhi ya shughuli muhimu za kimataifa na kwamba huenda
hata kimataifa yeye ni mtu bora. Nadhani CCM inaweza kuwa na mgombea
mwenye sifa hii pia, ni jukumu la upinzani pia kuwa na mtu ambaye
amejipanga vyema kimataifa na mambo aliyoyasimamia kimataifa pia
yanajulikana, si lazima yawe ya kiserikali, yanaweza kuwa ya kijamii, ya
kitaasisi au ya kitaaluma.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii inaweza kufanywa moja ya propaganda za
kuisaidia CCM, kwamba ndicho chama pekee chenye watu waliofanya kazi za
kimataifa na wataifanya Tanzania ikubalike kimataifa. Vyama vya upinzani
vitakuwa na jukumu la kupambana na propaganda hii kwa kuwa na mgombea
ambaye tayari wananchi wanatambua kuwa ana uzoefu wa kimataifa usio na
shaka ili kusiwe na tabu ya kuanza kumwelezea muda mrefu kwa wapigakura
juu ya eneo hili.
HITIMISHO
Andiko hili peke yake haliwezi kujadili sifa zote
muhimu za kiongozi bora kutoka vyama vya upinzani anayeweza kulivusha
Taifa. Nimechokoza mjadala wa masuala muhimu tu. Tukumbuke kuwa, kazi ya
kuongoza Serikali si nyepesi, inataka kujipanga kila idara na
kuwathibitishia wapigakura kuwa mnaweza bila shaka. Tabia ya wapigakura
huwa ni kutafuta namna gani watawaamini watu wanaowapa madaraka. Bahati
nzuri vyama vya upinzani katika Taifa letu vimekwishafanya kazi ya
kupigiwa mfano inayothibitisha, uzalendo, uadilifu, uzoefu uwajibikaji
na utendaji kazi bora.
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya
Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa
Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A)
katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na
Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana
kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.