Tuesday 28 January 2014

Kufungiwa umeme 27,000 alisema Waziri Muhongo



BEI ya kuunganisha umeme katika vijiji ambavyo bomba la gesi linapita kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, imeshushwa zaidi na kuwa Sh 27,000. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametangaza kuanzia mwaka huu wanavijiji ambako bomba la gesi linapita wataunganishiwa umeme kwa bei hiyo.
Profesa Muhongo alitangaza bei hiyo wakati wa uzinduzi wa upelekaji umeme katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, ambao ulifanywa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nanyumbu ni miongoni mwa wilaya tano za Mkoa wa Mtwara, lakini ndiyo pekee ambayo makao yake makuu yalikuwa hayajaunganishwa na umeme.
Profesa Muhongo alisema Wizara yake imefikia uamuzi huo baada ya agizo la Waziri Mkuu ambaye aliitaka iangalie namna wanakijiji hao watakavyofaidika na bomba hilo ambalo linapita katika makazi yao.
“Sasa napenda kutangaza, kwamba baada ya agizo hili la Waziri Mkuu, nimekaa na wataalamu wangu na tumeafikiana kuwa wanavijiji hawa ambako bomba la gesi linapita, waunganishiwe umeme kwa Sh 27,000 tu, duniani kote hakuna Serikali inayojali watu wake kama tulivyofanya sisi,” alisema Profesa Muhongo.
Juzi Pinda aliiagiza wizara hiyo kuhakikisha vijiji hivyo vinaunganishiwa umeme kwa bei rahisi, ili wananchi waone kuwa ni sehemu ya jamii inayofaidika na bomba hilo ambalo linatarajiwa kuwa ‘mwarobaini’ wa kumaliza tatizo la umeme nchini.
Pia Waziri Mkuu aliagiza Wizara hiyo kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), iangalie namna gani itahamasisha wanavijiji hao kwa kuwapa huduma zitakazowasaidia kuinua kipato chao; lakini pia kwa kujengea vijiji hivyo, huduma za jamii kama zahanati na shule.
Katika hotuba yake, pia Muhongo alisema Serikali inaendelea na juhudi za kupeleka umeme vijijini, ili angalau ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya Watanzania wawe wamepewa huduma ya nishati hiyo. Kwa sasa ni asilimia 23 tu ya Watanzania ndio wanapata huduma hiyo.
Muhongo alisema ili kufikia lengo hilo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeagizwa mwaka huu liwafungie umeme wateja wapya wapatao 250,000 kutoka wateja 99,000 ambao wamefungiwa mwaka huu.
Pia alihadharisha wananchi wanaokwamisha miradi ya umeme vijijini kwa kudai fidia kuwa watasababisha lengo hilo lisifikiwe.
“Hivi kuna mtu hapa anadai fidia kutokana na mpango huu wa kuweka umeme hapa?” Alihoji Muhongo na kuongeza;
“Nashukuru kama hakuna mtu wa namna hiyo. “Kama mtajitokeza kudai fidia tutalazimika kusimamisha mradi huu ili tutafute fedha za kulipa fidia kwanza na fedha za umeme tutazipeleka sehemu nyingine,” alisema Muhongo.
Akitoa taarifa ya mradi huo wa umeme wilayani Nanyumbu, Meneja wa Kanda wa Tanesco, Mahenge Mgaya alisema kazi za kufikisha umeme makao makuu ya Wilaya ya Nanyumbu na vijiji vya jirani, zinahusisha ujenzi wa kilometa 139 za njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 kutoka Masasi hadi Mtambaswala.
Alisema gharama za mradi huo ni Sh bilioni 5.9 ikiwa ni pamoja na za ujenzi wa kilometa 50 za njia ya umeme wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma 34 na kuunganisha wateja wapatao 780.
Pinda aliyezindua mradi huo alisema Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata huduma ya umeme hasa vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wednesday 22 January 2014

Chadema kutikisa nchi; Helikopta kurushwa nchi nzima

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo, kinarusha helkopta tatu kwa siku 14 mfululizo, katika  kutekeleza kampeni iliyopewa jina la Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini.
Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita; matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia usafiri wa magari.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha chama hicho na kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Tumejigawa katika makundi sita na makundi matatu kati ya hayo yatatumia helikopta kila moja, makundi mengine yatawafikia wananchi kwa misafara ya ardhini,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza kuongeza wiki nyingine moja.”
Alisema chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi wengi kadri itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wake wa ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata 27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni hata kidogo, huu ni mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika Jimbo la Kalenga ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza kufanyika uchaguzi katika jimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.
Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia mahakamani ili kunusuru uanachama wake.
Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na zuio la mahakama, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa uanachama, likiwa ni hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa zao pamoja na Zitto.
Daftari la wapigakura
Mbowe alisema msimamo wa chama chake ni kutaka daftari la kudumu la wapigakura lifanyiwe marekebisho kabla ya kupigwa kwa kura za maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Mpya.
“Tutagomea upigaji wa kura na tutawahamasisha wananchi kugomea kupiga kura. Serikali ya CCM isijidanganye kwa kuweka mikakati ya kukwamisha zoezi hili,” alisema Mbowe.
Alisema kama Serikali inataka amani iendelee kuwepo isifanye mzaha katika mchakato wa Katiba Mpya kwa maelezo kuwa Katiba siyo mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi.
“Katiba siyo ya  Chadema, CUF wala NCCR-Mageuzi. Sheria inaeleza wazi kwamba daftari la wapigakura ni lazima lifanyiwe marekebisho mara mbili baada ya Uchaguzi Mkuu na kabla ya kuanza Uchaguzi Mkuu mwingine lakini hilo halijafanyika mpaka sasa licha ya Uchaguzi Mkuu  kufanyika miaka minne iliyopita,” alisema Mbowe.
Alisema wapo Watanzania waliohama maeneo yao ya awali, waliopoteza vitambulisho, waliofikisha umri wa kupiga kura na kusisitiza kuwa kuwaacha watu hao nje ya mfumo wa kupiga kura ni kuwanyima haki yao ya Kikatiba.
“Kwa mujibu wa utafiti tulioufanya tumebaini kuwa wapo watu zaidi ya milioni 5 wanaohitaji kuingizwa katika daftari la wapigakura,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kama Katiba haitapita kwa sababu ya kutokuboreshwa kwa daftari la wapigakura hatutarudi katika Katiba ya sasa hiyo ni ndoto.”

Ushabiki unavyowatesa vijana katika siasa

Dar es Salaam. Mwamko wa vijana katika siasa ulianza kujitokeza katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka 1995. Chama Cha Mapinduzi (CCM) mbali na mwamko wa vijana ulioibuka ndani yake, pia kilianza kupata upinzani mkali na kutupiwa lawama na kila aina ya kejeli kwa madai ya viongozi wake kukosa sifa za kuongoza nchi.
Mwamko huo kwa vijana umeendelea kukua kwa kasi mpaka sasa kupitia uhamasishaji wa makundi mbalimbali ya wanaharakati, wasomi na huo ukawa ni mwanzo wa baadhi ya vyama vya siasa kuona umuhimu wao, hivyo kila chama kuwavuta upande ke kwa maslahi yake.
Idadi kubwa kati ya vijana hao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali na walioko vyuo vikuu ambao ni rahisi kupokea agenda za vyama husika na kuziendeleza, hivyo kutimiza malengo ya vyama husika.
Pamoja na hao, wapo vijana wenye elimu ya wastani, na wengine walioikosa kabisa, ambao ni rahisi kufanya lolote bila kujali matokeo yake, kwa kuwa wao ni ‘bendera fuata upepo’.
Kwa hali ya siasa ilivyo nchini, baadhi ya vijana wameanza kujikuta njiapanda, wakishindwa kuchagua ni chama gani, mwanasiasa yupi au kundi lipi linaweza kuwa tumaini jipya kwao.
Hatua hiyo inatokana na udhaifu unaoendelea kuonekana ndani ya vyama vya siasa, hususani vile vyenye ushindani mkubwa katika kipindi fulani – kama ilivyokuwa kwa NCCR na CCM mwaka 1995; CCM vs CUF mwaka 2000; na CCM vs Chadema mwaka 2010 na sasa tunapoelekea 2015.
Sote ni mashuhuda wa mivutano iliyopo, vurugu na tuhuma mbalimbali za mara kwa mara zisizokuwa na majibu.
Vuguvu hilo la vijana limeanza kuingia hata ndani ya vyama vyewenye, mfano ni katika uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka juzi, na hivi karibuni katika sakata la Chadema dhidi ya Zitto Kabwe.
Katika matukio hayo, tumeshuhudia jinsi vijana walivyoamua kupigana wao kwa wao, kila upande ukitaka kutimiza malengo yake.
Kutokana na mazingira hayo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaeleza mitazamo mbalimbali inayosababisha vijana kuathiriwa na mapenzi ya vyama, au watu binafsi ndani ya vyama hivyo mpaka kufikia hatua ya kukosa uvumilivu, wakiamini kuwa chama hicho au watu hao ndio suluhisho la matatizo yao.
Vijana wanapotoka?
Tofauti na fikra za vijana hao, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam (UDSM), Bashiru Ali anasema mpaka sasa haamini kama kuna chama chochote cha siasa duniani kilichowahi kuwa na historia ya kuleta mabadiliko ya kuikomboa jamii kuondokana na changamoto zinazoikabili.
Bashiru anasema kila chama kimekuwa na ajenda ya kuhakikisha kinashika dola pasipo kuangalia au kupigania mabadiliko katika huduma za kijamii.
“Vyama huwa na ajenda ambazo vinaona zitafaa kuwatengenezea mazingira ya kufanikisha itikadi zao. Mfano kodi za nyumba zimekuwa zikiongezeka kila wakati na hatujasikia chama hata kimoja kimesimama kulisemea, ni changamoto inayowagusa wananchi na maisha yao, kwani wanasiasa hawaoni?”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kiraia inayofuatilia mwenendo wa Bunge nchini (CPW), Marcossy Albanie anasema hatua ya vijana kupigana inatokana na hali tofauti na matumaini waliyokuwa nayo ndani ya chama.
“Wamewekeza kwa muda mrefu wakiamini ndiyo sehemu ya kuleta mapinduzi mapya  ya kiutawala, sasa inapotokea mivutano kama tukio la Chadema, matokea yake wanakosa uvumilivu,” anasema na kuongeza;
Kina nani hawajitambui?
Katibu wa Hamasa na Chpikizi katika Umoja wa Vijana wa VCCM, Paul Makonda anasema bila kuangalia itikadi za vyama vya siasa, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mpaka sasa asilimia 75 ya vijana hawajatambua itikadi za kisiasa.
Anasema mbaya zaidi miongoni wasiojitambua ni wasomi wengi waliohitimu elimu za vyuo vikuu.
“Hawajui siasa, hawajui itikadi ni nini na hawajui hata wanachokitaka kupitia vyama vya siasa, ila picha iliyopo kwa sasa wamekuwa wakifuata ushabiki tu wa kisiasa na kuangalia mwanasiasa gani, kundi au chama gani kinachozungumzia hisia zao,” anasema Makonda.
Kiongozi huyo aongeza kuwa kundi jingine la vijana sawa na asilimia 25 ni lenye ujasiri lakini linaishi kwa hofu na woga, linakosa nguvu ya kuhoji udhaifu uliopo katika mfumo wa vyama kutokana na nguvu za wanasiasa wachache wanaotaka kulinda maslahi yao.
Anasema kutokana na mazingira hayo, mwasiasa amekuwa akitumia fimbo hiyo kama udhaifu wa kuendelea kumtumia kijana katika jambo lolote analohitaji kupenyeza maslahi yake kwa wakati fulani.
Makonda anasema mbaya zaidi mpaka sasa taifa halina mfumo wa kuwaandaa vijana katika uelewa wa itikadi za kisiasa ndani ya vyama.
“Kutokana na hali hiyo ukijumlisha na uvivu wa kufikiri hoja na maazimio ya wanasiasa, matokeo yake vijana wanapigana ovyo wao kwa wao au kuwa watumwa wa wanasiasa,” anasema Makonda.
Nini Kifanyike?
Bashiru anasema hatua ya kwanza katika kuwakomboa vijana hapa nchini ni pomoja na kuwasaidia waweze kufikiri na kuchambua kwa makini kila hoja inayotolewa na mwanasiasa yeyote.
Anasema uwezo wa vijana ujengeke mpaka kufikia hatua ya kutengeneza msimamo na ajenda zao kama vijana.
“Tunataka tuone vyama vya siasa ndiyo vinafuata ajenda za vijana, siyo vijana wanafuata ajenda za wanasiasa, matokeo yake wanajikuta kwenye mpasuko wa makundi,” anasema.
Bashiru anasema uelewa mdogo wa vijana katika kuchambua itikadi za kisiasa hapa nchini utaendelea kuwa changamoto mpaka pale vijana wanakapokuwa tayari kufanya mabadiliko.
“Vijana watengeneze vyama vyao kwa ajili ya kupigania maslahi yao, waunde vyama ambavyo vitakuwa na ajenda ambazo zitakuwa na ushawishi wa kutumiwa hata na hao wanasiasa, kama ambavyo tuliwahi kuwa na vyama vya wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara,” anasema Bashiru.

Chuki zaanza ndani ya CCM, Sinyanga, Monduli, Mgeja, Lowasa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja ameonya baadhi ya viongozi wa chama hicho kuwajengea chuki wanachama kadhaa na viongozi kwa madai wako karibu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Hatua ya Mgeja imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ kumkana na kumshutumu, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai kuwa anawalazimisha kuwa nyuma ya Lowassa wakati sivyo ilivyo.
Hata hivyo, Msindai alikanusha madai hayo kuwa hakuwahi kuwazungumzia wenyeviti wa CCM wa mikoa kuwa nyuma ya Lowassa zaidi ya kusema kuwa wanamuunga mkono katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mgeja alimtetea Msindai kuhusu suala la wenyeviti wa CCM kuwa nyuma ya Lowassa katika urais. Alisema: “Nataka kutoa angalizo kwa viongozi ndani ya chama, Tanzania kwa ujumla, kumejitokeza tabia ya baadhi ya watu kuchukiana eti tu kwa sababu wako nyuma ya Lowassa,” alisema na kuongeza:
“Kumeanza watu kuchukiana, kuhukumiana kwa sababu uko karibu na Lowassa au kuwa na imani naye katika utendaji kazi wake, kumpenda na kumkubali mtu ni utashi wa mtu binafsi...tusihukumiane wala kuchaguliana marafiki,” alisema Mgeja.
Mgeja alisema: “Hakuna dhambi ya kumpenda au kumwamini Lowassa, lakini watu wanachukia, watu wananung’unika, wananuna haya yote ni majungu, woga, wivu na kutokujiamini. Inawezekana wanaofanya hivyo, wanatumwa na walio nyuma yao.
“Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, tusianze kusakana uchawi, muda ukifika, kila mtu atabebwa kwa sifa zake na atajibeba kwa umahiri wake.”
Mgeja alisema, kazi kubwa inayotakiwa kufanyika kwa wabunge, mawaziri na viongozi wa kada mbalimbali ni kukaa chini na kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha wanapata maji safi, dawa hospitalini na elimu kuliko kutumia muda mwingi kuangalia nani anampenda Lowassa.
“Kuna changamoto nyingi zinazowakabili wananchi na kila siku wanatuangalia viongozi, suala la vijana ni tatizo kubwa huduma za msingi kuliko kukaa na kuangalia Lowassa anafanya nini na yuko na nani, haileti tija hata kidogo,” alisema.
Mgeja aliwataka wanaCCM kutulia na kutafakari mambo ya maendeleo kwa kuwa hakuna mtu aliyejitangaza urais akiwamo Lowassa zaidi ya kuanzisha safari ya matumaini ambayo ndani yake kuna mafanikio katika elimu, huduma za afya, ajira kwa vijana na mambo mengi,” alisema.
Hivi karibuni, Msindai alikaririwa akisema: “Mimi ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa wenyeviti wote wanamwunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu 2015... kikubwa tulichozungumza ni kumuunga mkono katika safari yake ya mafanikio katika kuendeleza elimu, maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na uwezo wake katika kusimamia mipango yake ya maendeleo na zaidi katika kupigania elimu pana kwa Watanzania.

Ana umri wa miaka 12, aolewa kwa ng’ombe 15

Kiteto. Wamasai ni miongoni wa jamii chache duniani, ambazo zimefanikiwa hadi sasa kudumisha mila zake. Katika mila za jamii hii, zipo ambazo zinapaswa kuendelezwa na nyingine zinapaswa kupigwa marufuku.
Miongoni mwa mila ambazo zinapaswa kuendelezwa ni pamoja na kuendelea kutambua na kuheshimu viongozi wa mila ‘Laigwanaji’ kuheshimu viongozi wa rika na Serikali, kuishi kwa umoja na kudumisha tamaduni.
Mila ambazo zimepitwa na wakati katika jamii hii ni pamoja na kurithi wajane, ukeketaji watoto na kuoa watoto wadogo.
Katika makala hii, leo nitazungumzia mila ya kuoa watoto wadogo kama nilivyobaini katika vijiji kadhaa wanapoishi Wamasai, wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Nikiwa katika uchunguzi wa mapigano baina ya wafugaji wa Kimasai na wakulima katika vijiji saba vinavyozunguka eneo la Hifadhi ya Emborey Murtangosi nakutana na mtoto wa miaka 12 aliyeolewa.
Nilipata bahati ya kufika katika familia ya mtoto huyu, katika Kitongoji cha Ndiligishi kaya ya Engusero Sidani baada ya kuwa ni moja ya familia ambazo zimeathirika na mapigano baada ya kuchomewa makazi na kuibiwa vyakula.
Wakati nahojiana na wanafamilia napata fursa ya kuonana na mtoto huyo aliyegeuzwa kuwa mke, nashawishika kumuhoji baada ya kuona akiwa amejitenga na watoto wenzake huku akiwa na mawazo.
Mtoto huyo ambaye jina lake tumelihifadhi kutokana na sababu za kimaadili, hajui kiswahili  vizuri, hivyo nalazimika kumuomba mtoto mwenzake, Stela Paulo aje anisaidie kuongea naye.
Ananieleza kuwa yeye ni mke wa Lembau Leseri  na ameolewa  mke wa pili na ana miaka miwili ya ndoa.
Akiwa  anaonekana kutokuwa na raha ya maisha, mtoto huyo anasema wazazi wake, ndio walimpeleka kwa mwanaume baada ya kupewa mahali.
Anasema hajui kusoma wala kuandika kwani hakufanikiwa kupelekwa shule na wazazi wake.
Ninapomdadisi kama angependa kusoma, anasema angepata fursa hiyo angefurahi lakini sasa haiwezekani tena kwani ni mke mtu.
Kwa umri wake na umbile bado ni mdogo lakini, anaeleza huku akiwa kichwa chini na kwa aibu kuwa majukumu yote muhimu kwa mume wake aliyepewa na wazazi anafanya.
Hata hivyo, mtoto huyu anaonekana afya yake kudhoofika kutokana na maradhi ya ngozi na huenda na majukumu ya kifamilia.
Mume wa mtoto azungumza.
Mume wa mtoto huyo, Lembau Leseri hivi sasa ni mgonjwa na takriban wiki mbili, alikuwa amelazwa hospitali ya kiteto kutokana na kutokewa na majipu mwilini.
Ananieleza kuwa, mtoto huyo ni mke wake wa pili, ambaye alimuoa kutoka kijiji jirani cha Taiko.
Anasema mke wake wa kwanza, Kawie Lembau sasa ana watoto saba.
Lembau haoni kama amefanya makosa kuoa mtoto mdogo, kwani ananieleza kuwa alimuoa kwa ng’ombe 15.
Hata hivyo, anaeleza maisha yake ya ndoa na mtoto huyo, hayakuwa ya taabu kwa mwaka mmoja uliopita lakini sasa ana matatizo kutokana na kukabiliwa na maradhi.
“Sijui naumwa nini kwani nimelazwa hospitali na wamenipa dawa nirudi nyumbani,” anasema.
Anasema licha ya maradhi yanayomkabili,  maisha yamekuwa ya magumu, mapigano ya ardhi yameifanya familia yake kukosa chakula kwani zaidi ya magunia 50 ya mahindi yaliibwa.
Anasema pia vijana wa kiume wa familia yao, wamekimbia kwa sababu  polisi wanaendesha msako kuwakamata waliohusika na mauwaji ya wakulima tisa kutokana na mapigano ya ardhi.
“Hali ni ngumu, mimi naumwa siwezi kutembelea umbali mrefu kutafuta chakula, vijana wa hapa wamekimbia wanaogopa polisi,”anasema Lembau
Hali ya njaa katika familia hiyo yenye maboma matatu, inathibitishwa na jinsi nilivyoikuta akina mama wazee na watoto wadogo walikuwa wakichemsha mchicha majira ya saa saba lakini hadi naondoka takriban saa tisa walikuwa hawajala chakula kingine.
Mke mkubwa
Mke mwingine wa Lembau ambaye anaonekana ni mtu mzima ni mkimya na nilipotaka anieleze kuhusiana na mke mwenza wake  anashindwa kusema kitu na anaingia ndani ya boma lao.
Lakini natambua kwa mila za kimasai ni nadra sana mwanamke kuwa na ujasiri kupingana na mwanaume kutokana na misingi ya mila na desturi zao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wazungumza.
Shilinde Ngalula ni Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anapatwa na mshangao anapoelezwa mtoto huyo ni mke wa mtu hasa kutokana na umri wake mdogo.
Hata hivyo, baada ya kuzungumza naye anaeleza kusikitishwa na maisha ya ndoa ya mtoto huyu.
“Hili ni tatizo kubwa katika jamii hizi kwani mtoto huyu alipaswa kuwa shule lakini kaolewa na mtu mzima ambaye sasa ni mgonjwa,”anasema Shillinde.
Shilinde na maafisa wengine wa LHRC ambao wanafanya uchunguzi wa mapigano baina ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, anaahidi kutafuta muda muafaka kufuatilia maisha ya mtoto huyo.
“Jamii hizi za pembezoni zinakabiliwa na matatizo mengi ambayo mengine yanatokana na kutokuwa na mazingira bora ya kupata elimu na huduma nyingine muhimu”
Shillinde hata hivyo, anaongeza kuwa umefika wakati, Serikali na wadau wengine kufika maeneo ya vijiji katika jamii kama za kimasai ili kusaidia kutatua matatizo yao ikiwepo ya umasikini,elimu na mila zilizopitwa na wakati.
Je, maisha ya ndoa ya mtoto huyu yataendelea vipi kwa sasa kwani licha ya kuwa na umri mdogo bado ana mzigo mkubwa wa kumuuguza mume wake na je, nani atamuokoa na ndoa ya utotoni na kumrejesha shule kwa watoto wenzake?
Hili ni swali zito lisilo na jibu kwa sasa hata hivyo huenda LHRC wakalivalia njuga suala hilo na haki kupatikana kama ambavyo tayari wameahidi.

Kikwete afunga mjadala wa gesi

Dar es Salaam: Rais Jakaya Kikwete amefunga mjadala wa wafanyabiashara wazawa wanaotaka kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa sekta ya gesi akisema Shirika la Maendeleo la Petroli(TPDC) linajitosheleza kuwasaidia Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo.
Katika kipindi cha miaka miwili, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameshikilia kuwa hakuna Watanzania wenye uwezo wa utafutaji, uchimbaji na uzalishaji, jambo ambalo linapingwa vikali na wafanyabiashara wazawa.
Akizungumza jana wakati wa Kongamano la Viongozi wa Dini kuhusu rasilimali ya gesi, mafuta na madini kwa ajili ya amani na maendeleo ya taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema hakuna kampuni nchini yenye dhamana ya kupata mikopo kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kampuni za kigeni zenye mitaji mikubwa zinafanikiwa kupata mikopo kwa kuwa zina dhamana inayowasaidia kupata mikopo kwenye mabenki,” alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kama kuna kampuni za Watanzania zinatakiwa kushirikiana na wawekezaji watapaswa kufuata taratibu zilizowekwa.
Rais Kikwete alisema uwekezaji kwenye sekta ya mafuta ni kama mchezo wa kamari kwani mtu anaweza kuwekeza fedha nyingi katika utafutaji wa gesi na asipate kitu.
“Ni kampuni gani Tanzania ambayo itakuwa tayari kucheza kamari?” alihoji Rais Kikwete.
Alisema ndio maana Serikali imeona ni vizuri iandae mpango wa kuiwezesha TPDC kuingia kwenye shughuli za gesi badala ya kuwa kutoa leseni tu.
“Tunataka siku moja TPDC iwe na uwezo wa kuwauzia hisa Watanzania iwe kama kampuni kubwa za Statoil(Norway) na Petro Plus(Brazil) zinazoendeshwa na Serikali zao,” alisema.
Rais Kikwete alisema baada ya kuliwezesha shirika hilo, Watanzania watanufaika kwa kiwango kikubwa tofauti na kutoa kipaumbele kwa kampuni binafsi za Watanzania.
Washiriki watoa maoni tofauti
Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima alipinga kongamano hilo kufanyika sasa kwani alieleza lilipaswa kufanyika miaka mitano iliyopita na sio sasa wakati ambapo shughuli za uchimbaji wa gesi zinakaribia kuanza.
Akizungumza wakati wa akisoma salamu za viongozi wa Dini ya Kikristo katika kongamano hilo, Dk Kitima alisema kongamano kama hilo haliwezi kubadili chochote na kinachofanyika ni kwa wawekezaji kujifagilia njia wakati wanaelekea katika kuanza kutekeleza miradi waliyowekeza.
“Hapa ninachoweza kusema ni kuwa wafadhili hao wametoa fedha, wamefadhili kongamano hili ili wakianza shughuli zao wasisumbuliwe,” alisema na kuongeza kuwa kinachofanyika sasa hakitoi taswira nzuri kwani jamii imelishwa sumu kuwa haiwezi kufanya lolote bila kuombaomba.
Akionekana kujibu hoja hiyo, Askofu Stephen Munga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), aliomba kuweka sawa dhana hiyo kwa kusema kuwa sio sahihi kuwa mkutano huo umefadhiliwa na matajiri wa gesi na mafuta.
“Kongamano tumeandaa wenyewe baada ya baadhi ya maaskofu wa KKKT kufika ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo kuzungumza nae kuhusiana na uharibifu wa mazingira na akataka pia tuzungumzie suala la gesi, ndio tukaona kuna haja ya kufanya kitu kama hiki ambacho kinafanyika sasa,” alisema.
Naye Sheikh Aboubakary Zuberi alisema ni vizuri watu ambao wanaishi katika maeneo ambako rasilimali zinapatikana ni vizuri wakanufaika nazo badala ya kuwa kama ilivyo sasa jambo ambalo haliwezi kuleta matokeo mazuri siku za mbeleni.
Alisema nchini kuna mgawanyiko mkubwa wa mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.

Tuesday 21 January 2014

Mbatia ashinda tena NCCR, mizengwe yatawala mkutano

Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa nane wa Chama cha NCCR-Mageuzi, umemchagua tena James Mbatia kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo huku mizengwe ikitawala katika uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo ulioanza juzi, idadi kubwa ya wajumbe walikuwa na mkakati wa kumng’oa Katibu Mkuu, Samwel Ruhuza aliyekuwa akitetea nafasi yake, Mosena Nyambabe na Rehema Sam waliokuwa wakiitaka nafasi hiyo.
Wajumbe walikuwa na mpango huo kwa kuwa Nyambabe yuko vizuri kiutendaji ikilinganisha Ruhuza. Jana kwa nyakati tofauti, wajumbe walionekana katika makundi kujadili hali hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mbatia.
Ukiacha hali hiyo, Mbatia alipata upinzani mkali akichuana kwa mbali na aliyekuwa Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Katavi, Charles Makofila, ambaye ni mlemavu wa viungo.
Tangu kuanza kwa mkutano huo katika Ukumbi wa Diomond Jubileee, hapakuwa na dalili za upinzani wa nafasi hiyo ya uenyekiti na baadhi wa wajumbe wa mkutano walisikika wakisema, “Makofila bwana sijui amekosa cha kufanya, ila ndo hivyo wacha amsindikize mwenzake.”
Zoezi la upigaji kura lilianza saa 10 jioni hadi saa moja usiku chini ya Msimamizi wa Uchaguzi huo, Moses Machalli.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 228 kati ya 289.
Machalli akitangaza matokeo hayo alisema, Mbatia ameshinda kwa kura 201 na Makofila ameambulia kura 26 na kura moja imeharibika.
“Ndugu Mbatia atakiongoza chama hiki kuanza hii leo (jana) hadi Januari 2019 hivyo tumuunge mkono na uchaguzi usiwe chanzo cha migogoro, tumemaliza salama na sasa tunaangalia mbele,” alisema Machalli.
Mbatia akitoa shukrani zake alisema, “Nawashukuru sana kwa kutumia demokrasia yenu kunichagua, nawaahidi kuwatumikia kwa moyo wangu wote, uchaguzi umekwisha sasa tujenge chama chetu.”
Mwenyekiti huyo mpya, aliwataka wabunge wa chama hicho kuacha kubweteka katika majimbo yao na sasa wazunguke nchi nzima kukijenga chama.
“Machali, Kafulila kumbukeni kulipa fadhila za chama, zungukeni nchi nzima acheni kujisahau bila NCCR tusingekuwa katika Bunge tukufu, sasa kazi kwenu kwani tunaweza kama tutaamua,” alisema Mbatia.
Akiongea baada ya kutangazwa matokeo, Makofila alisema uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na uwazi ila wajumbe wa mkutano huo waliomnyima kura wamepoteza kura zao.
“Niliwaahidi ningeongeza posho za mkutano kutoka elfu 30 hadi elfu 60 sasa kwa kuwa hawakunichagua wamepoteza kura zao,” alisema Makofila.
Makofila alisema kushindwa kwake hakutamfanya ajitoe ndani ya NCCR ila atatumia kipindi hiki kuongeza elimu ambayo hadi kufika uchaguzi mwingine mapema mwaka 2019 atakuwa amejiimarisha zaidi.
Katika uchaguzi huo ambao haukuwa na ushindani katika nafasi nyingi kutokana na baadhi ya nafasi kujitokeza wagombea wanaokidhi nafasi husika hivyo kuwachagua kwa kura za ndiyo au hapana.
Mfano ni nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara na Visiwani hapakuwa na washindani hivyo wajumbe walipiga kura za ndiyo na hapana.

Ndoa ya Obama, Michelle shakani

Marekani. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyanzo vya ndani vya Ikulu ya Marekani, wenza hao wamekuwa katika migogoro na Obama alilazimika kusherehekea sherehe za mwaka mpya mjini Hawaii akiwa na binti zake wawili, Sasha na Malia bila kuwepo Michelle.
Jarida la National Enquirer lilieleza kwamba katika moja ya matukio, Obama aliwahi kukutwa akiwa na mwanamke mwingine katika ‘mazingira ya kutatanisha’ wakati mkewe akiwa safarini.
Kutokana na ripoti iliyotolewa na Bombshel , Michelle na Obama wamekuwa wakilala vyumba tofauti ndani ya Ikulu. Michelle pia anajiandaa kuhama katika jumba lao pale Chicago ambalo wameishi wakati wa uchumba wao miaka 21 iliyopita na kwa msisitizo watajadili juu ya talaka.
Taarifa ilidai tatizo limeanza miaka minane iliyopita pale Obama alipodhamiria kujijenga kisasa. Ni mtoto wao Sasha ambaye aliumwa ugonjwa unaosababishwa na woga wa maisha unaoitwa Spinal Meningitis ndiyo uliowafanya waendelee kuwa pamoja.
Kitabu cha Anderson kinaelezea tatizo lilivyoanza baada ya Barack Obama kuamua kuingia kwenye siasa, ambapo Michelle alisikika akimwambia mumewe; “Wewe unajifikiria mwenyewe tu.”
Naye Barack Obama amesikika akisema: “Sikuwahi kufikiri kamwe kwamba ningelea familia mwenyewe siku moja.” Anderson anadai kuwa Obama amechoshwa na malalamishi ya mkewe.
“Nampenda sana Michelle lakini ananiumiza na ubishi wake wa kila mara,” alisikika akisema Obama na kuongeza kuwa; “Anaonekana ni mwingi wa machungu na hasira siku zote.”
Akizungumza na televisheni ya CBS ya Marekani, Anderson alidai kuwa ilikuwa nusura Michelle atembee nje ya ndoa kwa sababu ya upweke.
Kwa miaka mitano wamekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wao wa kupata watoto kabla Malia hajazaliwa. Walishajadili sana suala la kuasilia watoto (adoption) na marafiki zake wa karibu lakini kwa bahati nzuri Malia alizaliwa mwaka 1998 na kuondoa wazo hilo.
Jina kamili la Obama ni Barack “Barry” Hussein Obama, Jr, alizaliwa Agosti 4, 1961 Honolulu, Hawaii, alikulia huko huko Hawaii na Indonesia, baba yake mzazi ana asili ya Kenya. Jina kamili la mkewe ni Michelle LaVaughn Robinson, alizaliwa Januari 17, 1964 Chicago, Illinois.
Kukutana kwako
Barack na Michelle walikutana mwaka 1989 katika mazingira ya kikazi, walifunga ndoa Oktoba 18, 1992, katika Kanisa la Umoja wa Kristu la Trinity lililopo Chicago, Illinois.
Lakini vyanzo vingine vya taarifa zinadai kuwa ndoa haiko imara, hasa baada ya tukio la Obama kupiga picha za pamoja bila aibu na Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning-Schmidt (46) wakati wa mazishi ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Afrka Kusini, Neslon Madiba Mandela.
Obama akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, alikuwa akicheka na kumnong’oneza kitu waziri huyo mara kwa mara kwa muda wote, huku Michelle akiwa pembeni yake amenuna. Mara nyingi alikuwa akimshika shika mabega.
“Lakini kwa sasa Michelle anajiona kanyanyasika na kuaibishwa mbele ya dunia kwani picha hizo zilirushwa duniani kote kupitia televisheni, magazeti na mitandao mbalimbali. Alisikika akimtapikia Obama huku akisema “Nimechoshwa.”
Pia tatizo limekuzwa na safari ya kikazi ya Obama hivi karibuni kule Thailand ambayo ilimkutanisha na Waziri Mkuu mrembo kuliko pengine wote duniani , Yingluck Shinawatra.
Tarifa zaidi zilieleza kwamba usalama wa taifa nchini humo unafahamu kuhusu suala hilo, lakini umekuwa ukilichukulia kama suala binafsi na Michelle alionekana kukasirishwa kupita kiasi alipopata taarifa hizo.
“Baada ya tukio hilo Michelle aliamua kuwasiliana na mwanasheria wake akitaka kujua namna ya kuomba talaka na alimwambia Obama kwamba anahitaji kuishi mbali naye,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa makubaliano waliyofikia, ilielezwa kwamba Michelle ataendelea kuishi mjini Washington DC hadi binti yao mdogo, Sasha (12) atakapomaliza elimu yake ya sekondari. Binti yao mkubwa, Malia (15) tayari ameshaingia sekondari.
“Michelle (50) kwa sasa ataendelea kuishi kwenye Ikulu ya Washington hadi Obama atakapomaliza muda wake wa urais ili tu aweze kuonekana kama yupo, lakini aliweka wazi kabisa kwamba wataishi maisha tofauti,” ilieleza ripoti hiyo ikimkariri mmoja wa vyanzo kutoka Ikulu hiyo. Ripoti hiyo ilikariri chanzo hicho kikieleza; “Michelle kwa sasa anaishi katika vyumba vya watumishi kwenye nyumba yao ya familia na anajiandaa kuchukua vifaa vyake na kuvipeleka kwenye nyumba yao binafsi ya Chicago”.
Taarifa nyingine ilieleza kwamba tayari mambo baina ya wanandoa hao yameshakuwa magumu kiasi kwamba wamekuwa wakiishi kwenye vyumba tofauti katika Ikulu ya Marekani.
Mgogoro wao
Barack na Michelle wamekuwa katika mgogoro kwa miaka kadhaa na wanalazimika kuwepo pamoja kwa sababu tu ya watoto wao na kulinda hadhi yake kisiasa. Lakini kwa sasa Michelle amekuwa mkali kweli kweli. Anaona kama amepuuzwa na kudhalilishwa mbele ya dunia nzima na amekuwa akipiga kelele akisema, “Nimevumilia vya kutosha”, taarifa zaidi zilieleza.
Kwa sasa Michelle anaonekana kupigania kukamilisha namna ya kupata talaka, lakini baadhi ya taarifa zinaeleza kwamba anafanya makusudi kuuchelewesha ili aweze kuukamilisha baada tu ya Obama kumalizia muda wake wa urais ambapo ataweza kupata Dola za Marekani 30 milioni kupitia mpango wa vitabu na zaidi ya dola 65 milioni kwa kuonekana hadharani.
“Kwa sasa Barack anaonekana kama amemwaibisha Michelle mbele ya dunia na kwa hili ni wazi kwamba atalilipa kwa gharama kubwa,” kilieleza chanzo kutoka Ikulu ya Marekani.
“Ni jambio lililo wazi kwa sasa kwamba Michelle ameshamwambia Obama kwamba anahitaji kuishi mbali naye, japokuwa kwa sasa imekuwa ni suala gumu kwa kuwa anahitaji aendelee kuonekana wakiwa pamoja kwa sababu muhimu, lakini wanapokuwa nyumbani wanaishi maisha tofauti ya kutengana,” kilieleza chanzo hicho.
Iwapo taarifa hizo ni sahihi, hii inamaanisha kwamba Michelle ameudhika kupindukia na hii si mara ya kwanza jambo hilo kutokea miongoni mwao.
Tangu Obama alipochaguliwa kuwa rais, vitabu viwili vimemtaja vikidai kwamba wenza hao walikaribia kutengana katika kipindi cha miaka yao ya mwanzo ya ndoa na hata Michelle alifikia hatua ya kutaka kuomba talaka akidai kwamba anaona maisha yake ya kisiasa yanawanyima furaha na kuwa pamoja nyumbani.
Mwaka 2009 mwandishi wa siku nyingi wa Washington, Richard Wolffe alisema kwamba ndoa hiyo ilikuwa sawa na iliyovunjika miaka tisa kabla kutokana na harakati za kisiasa za Obama zilizokuwa zikimsababisha asiwe karibu na familia kwa muda mrefu.
“Kulikuwa na mawasiliano kidogo sana na familia yake na hata mapenzi yalipungua. Michelle alikasirishwa sana na hali hiyo akilaumu kwamba mumewe anaonekana kuwa mbinafsi; ilimpa wakati mgumu sana,” aliandika Wollfe.
Wakati huo Michelle alilazimika kutulia kwa kuwa tayari alishakuwa mama, mbinti zao awili, Malia na Sasha kwa sasa wana miaka 15 na 12. Mumewe ambaye walikutana kwa mara ya kwanza walipokuwa wakifanya kazi kwenye shirika moja la sheria mjini Chicago mwaka 1989, alikuwa ndiyo kwanza amechaguliwa kuwa Seneta wa Illinois na alikuwa akijipanga pia kuwania nafasi kwenye baraza la Congress.
Mke wa Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, Carla Bruni alipoulizwa katika moja ya vitabu kuhusu uzoefu wake wa maisha ndani ya Ikulu alijibu, ‘Acha kabisa! Usiulize ni kama jehanamu. Sikuwahi kuyafurahia’ ambapo Michelle alisema hakuwahi kuzungumza maneno ya aina hiyo.
Mwaka 2012 mmoja wa waandishi wa masuala ya siasa, Edward Klein alieleza kwamba Obama alionekana mwenye mawazo kupita kiasi, wakati ndoa yake ilipokuwa kwenye matatizo mwaka 2000 kiasi kwamba rafiki zake walihofu kwamba anaweza kujiua.
Alieleza kwamba Michelle alikuwa mwenye hasira kwa kuwa alimkataza Obama kuwania nafasi kwenye Congress, ushauri ambao hakuufuata na hata hivyo alishindwa kwenye uchaguzi.
“Baada ya kushindwa alirejea kwa Michelle kwa ajili ya kupata pumziko. Lakini Michelle hakuwa tayari kuonyesha huruma yoyote,” aliandika Klein aliyedai kwamba marafiki wa Michelle walimweleza kuwa tayari ameshafungua kesi akidai talaka.

Serikali yawabeba waliofeli kidato cha pili

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili.
Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa, imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (Tamongsco).
Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”
Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30 watatimuliwa.
“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa nyumbani.”
Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa uamuzi kuhusu matokeo hayo.
Kauli ya wizara
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, “Suala la wizara kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia.”
Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila shule ina taarifa hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”
Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”
“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa tathmini ‘Continuous assessment’ kwa mwanafunzi, hutumika pia katika mtihani wa kidato cha nne.”
Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. “Baada ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Msimamo wa Tamongsco
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema, “Inaonekana Serikali haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).”
“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na masomo katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne.”
Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.
“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa vijana wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.
Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao; “Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and vocational education).”
Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya ufundi stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).
“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji wake.”
“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.
Kidato cha pili 2012
Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu walikuwa wanafunzi 245.9,32.

JK atema wengine watano, wapya ni 10

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo yamewatupa nje mawaziri watano, kuwaingiza 10 wapya, kuwapandisha manaibu wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wengine wanane kutoka wizara zao kwenda nyingine.
Miongoni mwa walioachwa katika mabadiliko yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa ambaye nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge.
Wengine walioachwa na wizara zao kwenye mabano ni Manaibu Waziri, Goodlucky Ole Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Gregory Teu (Viwanda na Biashara), Benedict Ole Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
Mawaziri hao wanaungana na waliokuwa mawaziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais kutokana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Balozi Sefue alisema kuachwa kwa mawaziri hao ni moja ya hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete kuimarisha utendaji serikalini. Pia alisema mabadiliko hayo yametokana na kuwapo kwa nafasi baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
“Rais amefanya mabadiliko kwa mujibu wa Ibara ya 55 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka ya kutekeleza wajibu huo,” alisema Balozi Sefue.
Sura mpya
Sura 10 mpya zilizoingia katika Baraza hilo ni pamoja na Dk Asha Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani ambaye anakuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Naibu wake, Kaika Saning’o ole Telele ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro.
Wengine wapya ni wale walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri na wizara zao kwenye mabano, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (Fedha), Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
Pia wapo Mbunge wa Serengeti, Dk Steven Kwebwe (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi (Kilimo, Chakula na Ushirika), Mbunge wa Mufindi Kusini, Mahmoud Ngimwa (Maliasili na Utalii) na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Waliopandishwa, kuhamishwa
Mbali na Dk Mahenge, Rais Kikwete pia amewapandisha manaibu waziri wengine watatu kuwa mawaziri kamili pasipo kuwahamisha wizara walizokuwa. Hao ni Saada Nkuya Salum anayekuwa Waziri wa Fedha, Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii).
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete amewahamisha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuchukua nafasi ya Dk Nchimbi, wakati aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi amerejeshwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kuchukua nafasi ya Nahodha. Dk Mwinyi aliwahi kuongoza wizara hiyo.
Wengine waliohamishwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuchukua nafasi ya Charles Kitwanga aliyehamishiwa Wizara ya Nishati na Madini kuendelea na wadhifa huo. Kitwanga anachukua nafasi ya George Simbachawene ambaye amehamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima amehamishiwa Wizara ya Fedha kuchukua nafasi ya Janeth Mbene ambaye amehamishiwa, Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua nafasi ya Teu. Amos Makalla amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwenda Wizara ya Maji.
Sefue alisema mawaziri na manaibu waziri wapya wataapishwa leo saa 10 jioni Ikulu.

Hili ndilo Baraza la Mawaziri tunalolitaka

Baada ya kizaazaa cha wiki iliyopita ambapo mawaziri wanne walipoteza kazi zao kutokana na kuwajibishwa kwa vitendo vya ukatili na mauaji vilivyotokea wakati watendaji katika wizara zao walipokuwa wakiendesha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ nchi nzima, kinachosubiriwa na wananchi hivi sasa ni Rais Jakaya Kikwete kuunda Baraza jipya la Mawaziri.
Kutokana na udhaifu mkubwa katika utendaji ambao kwa muda mrefu umeonyeshwa na mawaziri wengi katika Baraza la Mawaziri, hatudhani kama kuna mwananchi hata mmoja  anayemtarajia Rais Kikwete kujaza tu nafasi za mawaziri aliowafukuza wiki iliyopita.
Nderemo na vifijo vilivyotokana na furaha ya wananchi katika kila kona ya nchi baada ya mawaziri hao kuondolewa katika nyadhifa zao ni ishara tosha kwamba hawamtarajii Rais Kikwete kuishia hapo, isipokuwa kuwaondoa mawaziri wengine wengi ambao tayari wamethibitika na hata kutajwa na chama chao cha CCM kuwa ni ‘mawaziri mizigo’.
Hii bila shaka ni fursa nzuri kwa Rais Kikwete kusoma alama za nyakati, kwamba wananchi wamefika kikomo cha uvumilivu na sasa wamechoka na uzembe unaotokana na mawaziri dhaifu walio katika Baraza lake la Mawaziri. Hao ni  mawaziri ambao karibu muda wote wamekuwa nyuma ya matukio na kuishia kuwa watazamaji, huku shughuli za Serikali zikienda ndivyo sivyo kutokana na kutochukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, ubadhirifu wa fedha za umma na ufisadi uliokithiri.
Kutokana na mawaziri wengi kutokuwa na dhamira wala uwezo wa kuthubutu na kutenda, programu za Serikali kama ‘Kilimo Kwanza’ na ‘Matokeo Makubwa Sasa’ zimebakia kuwa vichekesho vya karne, pamoja na kuanzishwa kwa mbwembwe na fedha nyingi za walipakodi.
Ni bahati mbaya kwamba Rais Kikwete amebaki na muda mfupi mno kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi Oktoba 2015. Kwa kifupi, amebakiwa na miezi 22. Kutokana na kuwapo programu nyingi ambazo hazijatekelezwa, anahitaji sasa kujipanga upya na kupata Baraza jipya la Mawaziri lenye watendaji waadilifu na wachapakazi. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakielekeza lawama nyingi kwake kwamba uteuzi wake wa mawaziri kwa kiasi kikubwa umekuwa siyo wa umakini kwa maelezo kuwa, hauzingatii vigezo vya ufanisi na utumishi wa umma uliotukuka. Kwamba wengi wamekuwa ni mawaziri wa kufunga tai na kupeperusha bendera kwenye ‘mashangingi’ yao.
Tunakubaliana na wanaosema kwamba mawaziri wachapakazi katika Baraza lake wanahesabika katika kiganja cha mkono na kwamba Baraza hilo ni kubwa mno kupita kiasi. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni mawaziri wasiozidi saba  wanaoweza kusimama leo na kuonyesha kitu walichokifanya na kukisimamia mpaka mwisho. Rais Kikwete atafanya vyema iwapo ataweka mfumo wa kupima utendaji wa mawaziri wake na kuwawajibisha wale wasiofikia viwango, badala ya kusubiri shinikizo la Bunge kama tulivyoshuhudia mwishoni mwa wiki.
Tunamshauri Rais Kikwete sasa aepuke kigezo cha ukanda na ukabila katika kuteua Baraza la Mawaziri. Hoja yetu ni kwamba siyo lazima kila kanda au mkoa kuwakilishwa na idadi sawa ya mawaziri hata kama baadhi yao hawana uwezo hata kidogo. Tunasema vigezo vikubwa katika uteuzi huo viwe ni uzalendo, uadilifu na utendaji, hata kama vigezo hivyo vitalazimu kuteuliwa mawaziri wawili kutoka katika kitongoji, kijiji au kata moja.

Wakosoa uteuzi wa manaibu wizara ya fedha

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa uchumi, wamekosoa uteuzi wa Manaibu Waziri wa Wizara ya Fedha, wakisema uteuzi huo haujalenga mikakati ya kuleta maboresho ya kuondoa changamoto zilizopo katika wizara hiyo.
Manaibu walioteuliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete ni pamoja na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira nchini (TAESA), Eliezer Mwasele alisema viongozi hao wamewekwa kwa lengo la kutimiza malengo ya kisiasa.
“Ni mwaka mmoja tu umebakia tuingie kwenye uchaguzi mkuu na ukiangalia Mwigulu ni mtu wa kusimamia sera na mipango ya chama, nadhani hiyo ni ‘strategic Plan’ (mkakati maalumu) ili kujipanga kisiasa,” alisema Mwasele.
Mwasele amepongeza uteuzi wa Waziri mpya wa Fedha, Saada Mkuya akisema: “Sina shaka naye, ila hao manaibu hakuna lolote katika suala la uwajibikaji, hawana uwezo wa kiutendaji ila ni siasa tu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni binafsi (CEO’s Roundtable), Ali Mufuruki alisema viongozi hao wanatakiwa kuwa makini na changamoto kubwa zinazohitaji kupatiwa majibu kwa sasa.
Mufuruki alitaja changamoto kubwa mbili ambazo ni juhudi za ukusanyaji wa kodi pamoja na mvutano wa suala la mafuta na gesi kwa Watanzania.
Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Mufuruki alisema mpaka sasa wafanyabiashara wengi bado hawajawa tayari kukubaliana na matumizi ya mashine za EFD.
“Binafsi sioni tatizo kwenye matumizi ya mashine kwa sababu ili kukuza uchumi ni lazima kila mtu alipe kodi, lakini cha kushangaza suala hilo mpaka limekuwa likipingwa na viongozi wa CCM, ni makosa,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Humphrey Mushi kutoka kitengo cha Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitaja maeneo makubwa matatu ya kuzingatiwa na mawaziri hao ambayo ni kuhakikisha serikali inapunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, kuwekeza bajeti kubwa katika sekta nyeti za Kilimo na Reli.

Mabadiliko sasa kuhamia CCM, bungeni

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vitalazimika kufanya mabadiliko katika safu zake za uongozi kutokana na athari zilizosababishwa na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika Baraza la Mawaziri.
Juzi, Ikulu ilitangaza mabadiliko katika baraza hilo ambayo yaliwaweka kando mawaziri na manaibu waziri watano, huku sura kumi mpya zikiingia, mabadiliko ambayo yameacha nafasi mbili wazi katika sekretarieti ya CCM na nafasi nne katika uongozi wa Bunge.
Miongoni mwa walioteuliwa na kuapishwa jana ni waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya CCM; Dk Asha-Rose Migiro ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba ambaye  ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Nchemba ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, wakati Dk Migiro ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alisema jana kuwa viongozi wa sekretarieti ya CCM wanapoteuliwa kushika nafasi nyingine za Serikali, wanalazimika kuziacha nyadhifa zao katika chama.
Nape alisema kwa maana hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete atalazimika kuteua watu wa kuziba nafasi za Dk Migiro na Nchemba. “Huu ni utaratibu tuliojiwekea katika chama kwamba viongozi wa sekretarieti hawatafanya kazi mbili za chama na Serikali, kwa hiyo viongozi hawa pia wataziacha nafasi za chama,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema utaratibu huo hauwagusi wenyeviti wa chama hicho wa mikoa, ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ama manaibu waziri kwani uenyekiti si nafasi ya utendaji.
Katika uteuzi huo, Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani aliteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wakati Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Hawa wanaweza kuendelea na nyadhifa zao za uenyeviti katika chama, huku wakiwa na nyadhifa serikalini, hii haina athari kwa sababu siyo watendaji wakuu wa chama,” alisema Nape.
Bungeni
Bunge pia litalazimika kuchukua hatua za kuziba nafasi zilizoachwa wazi  na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge pia Kiongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, Jenister Mhagama ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Mahmoud Mgimwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na sasa ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Naibu Spika, Job Ndugai alisema nafasi zilizoachwa wazi na wabunge hao zitazibwa kwa kuchagua wenyeviti wengine kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
“Mapema sana kamati za kudumu za Bunge zitakutana kabla ya Bunge la Katiba, nafasi ambazo zimeachwa wazi na walioteuliwa kuwa mawaziri zitazibwa kwa sababu kamati husika watachagua wenyeviti wao,” alisema Ndugai. 
Kuhusu mawaziri walioachwa katika mabadiliko hayo, Ndugai alisema wao wanarejea kuwa wajumbe wa kamati.
“Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati, kwa hiyo tutawapanga kwenye kamati mbalimbali na hawazuiwi kuchaguliwa kuwa wenyeviti ikiwa watapangwa kwenye kamati ambazo wenyeviti wao wamechaguliwa kuwa mawaziri,” alisema Ndugai.
Mawaziri walioachwa kwenye uteuzi huo ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck  Ole-Medeye,  Dk Terezya Huvisa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mazingira) na Benedict Ole-Nangoro,  aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine ni Gregory Teu, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Philipo  Mulugo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Viongozi hao wanaungana na wenzao wanne ambao uwaziri wao ulitenguliwa na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana kutokana na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Bunge kuhusu utekelezaji wa operesheni tokomeza ujangili.
Hao ni pamoja na waliokuwa Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.

Saturday 18 January 2014

Siasa ina athari soko la muziki?

Katika ushabiki wa kisasa tunaweza kufikia hatua ya kuchapana makonde mpaka kupelekana mahakamani, lakini tunaposikia ‘Bit’ kabla ya mashairi, taratibu kila mtu utamwona anaanza kujiachia bila kujali amekutana na hasimu wake wa kisiasa.
Hatua hiyo inatokana na nguvu iliyopo ndani ya muziki hususan ule uliongia katika karne hii ya 21, kwa staili mpya za kubana pua(R&B) na kufoka foka(Hip Hop).
Hata hivyo wakati hali hiyo ikijitokeza, kumekuwa na mtazamo, dhana na hofu juu ya wasanii wanaojihusisha kwa karibu na shughuli za kisiasa kwamba wanaweza kupoteza nguvu katika soko lao kimuziki.
Baadhi ya mashabiki waliozungumza na Starehe, wanasema hatua hiyo inaweza kusababisha idadi kubwa ya vijana ambao ni mashabiki wa Bongo Fleva, huku wakiwa wamejikita zaidi katika ushabiki na mivutano ya kisiasa.
Kutokana na mtazamo huo kwa mashabiki, Starehe imefanikiwa pia kuzungumza na baadhi ya wasanii wahusika ambao wako kwenye siasa pamoja na mameneja ambao husimamia soko la muziki huo hapa nchini.
Akizungumza na Starehe siku chache baada ya mvutano wa mbunge wa Kigoma Kaskazin Zitto Kabwe na Chama chake, Sunday Mangu ambaye ni kiongozi wa kundi la wasanii kutoka Mkoa wa Kigoma (KAS), anasema ni hatari kwa msanii kujihusisha moja kwa moja katika mgogoro na ushabiki wa kisiasa.
“Msanii hutakiwi kuwa sehemu ya ushabiki ila hatukatazwi kutoa ‘sapoti’ za kisiasa. Kwa mfano Zitto tumekuwa naye bega kwa bega kwenye mgogoro huo kama kijana mwenzetu ambaye amekutana na changamoto katika nafasi yake ya kisiasa,” anasema na kuongeza;
“Endapo msanii atafanya hivyo anaweza kujitenga na kundi fulani kwenye jamii hatua ambayo siyo sahihi, msanii hana kundi wala hatakiwi kuwa kwenye itikadi zozote za ushabiki.
Hata hivyo kwa upande wake Profesa Jay anafafanua akisema kuwa msanii kutumiwa kwenye kampeni za kisiasa haimaanishi kuwa yeye ni sehemu ya chama kile.
Jay anasema kwa msanii ambaye anatumika tu kwenye kampeni za siasa haoni kama inaweza kuathiri kazi zake na kwamba anachoangalia ni maslahi ya kazi yake.
“Msanii anatumiwa kwa pesa huwezi kusikia msanii anafanya kampeni bila malipo, mimi sijawahi kufanya kampeni na siwezi kujua moja kwa moja zimewaathiri vipi lakini sijawahi kuona kama kuna msanii yeyote aliyetumika kisiasa na akaathirika kimuziki,” anasema Jay.
Hata hivyo Jay anaongeza kuwa msanii pia ni binadamu kama wengine ambao wana haki ya kuwa na hisia katika ushabiki wa mambo wanayoyapenda katika jamii.

Akitoa mfano, Jay anasema msanii kabla ya kuwa msanii inawezekana alikuwa ni shabiki wa Simba, hivyo hawezi kuacha ushabiki wake kwa sababu ya muziki, kutokana na hofu ya kuathiri soko lake kwa mashabiki wa Yanga.
“Msanii kuwa na Kadi ya CCM au Chadema siyo dhambi pia japokuwa inaweza kuwa mbaya zaidi pale atakapojiingiza zaidi kwenye ushabiki wa kisiasa, binafsi sioni kama kuna tatizo ila mashabiki wanapaswa kujua msanii anapofanya hivyo ni sehemu ya kazi yake,” anasema Jay.Mbali na Jay, Afande Sele anasisitiza kuwa athari zinaweza kujitokeza katika upande wa wadau wa muziki.
“Wadau wa muziki wanaweza kuwa wamegawanyika katika makundi ya kisiasa kwa hivyo msanii unaweza kuwa chama fulani wakati mdau ambaye anatakiwa ‘kukusapoti’ bila kujua kumbe ana hisia na chama kingine cha siasa. Kwa mazingira hayo msanii unaweza kukosa msaada kwake,” anasema Sele.
Sele anasema pamoja na hofu hiyo lakini hakuna shabiki yeyote ambaye anaweza kumsaliti msanii kutokana na itikadi za kisiasa.
Anaongeza kuwa shabiki ambaye anaweza kuwa na dhana ya kumsaliti msanii kwa sababu za kisiasa, atakuwa hajamtendea haki.
“Mimi hakuna ambaye hajui kwa sasa ni mwanachama wa Chadema, lakini bado ninapopanda jukwaani nashangiliwa na mashabiki wangu wote wakiwamo hata wa vyama vingine. Hapo siasa inakuwa pembeni kabisa,” anasema Sele na kuongeza;
Kinachofanya msanii aendelee kukubalika kwa mashabiki wa aina zote ni kutokana na aina ya mashairi na ubora wa kazi zake.
Anasema shabiki mwenye mapenzi ya dhati kwa msanii, hawezi kubadilishwa mtazamo na mapenzi yake kwa itikadi hizo za kisiasa na badala yake mapenzi yataongeza kutokana na mwendelezo wa harakati.
“Kama mashairi yangu yalikuwa ni kugusa ukweli halisi wa maisha na udhaifu wa viongozi, naamini kuingia kwenye siasa itakuwa ni ushawishi zaidi kwa watu wanaohitaji mabadiliko,” anasema Sele.
Mameneja wanasemaje?
Meneja maarufu wa kundi la Tip Top Connection, Diamond, Shaa na wasanii wengine kadhaa anayejulikana kwa jina la Babu Tale, kwanza anasema ifahamike wazi kuwa msanii hana dini wala chama chochote anachokitumikia kupitia muziki wake.
Tale anasema msanii ni kama mfanyakazi yeyote mwingine ambaye yuko tayari kufanya kazi kwa ajili ya kuangalia masilahi yake.
“Kesho unaweza kumwona amevaa tisheti za CCM, lakini baada ya siku kadhaa utamwona Chadema endapo watapanda dau zuri. Hilo ni jambo muhimu sana kwa mashabiki kuelewa kabla ya kuyumbishwa na dhana za kisiasa,” anasema Tale na kuongeza;
Katika uchaguzi wa mwaka 2010 alitumika kwenye kampeni za Rais Kikwete akiwa na wasanii wake mbalimbali anaowasimamia. “Tulikubaliana kufanya shoo zile kwa sababu za kimasilahi, inawezekana siku nyingine ukawaona wasanii hao hao wakapanda kwenye jukwaa za vyama vingine.
Kwa upande wake Meneja wa kundi la Wanaume family(TMK), Said Fela anaongeza akisema changamoto kubwa iliyopo ni mashabiki ambao hawaelewi nini ambacho msanii anazingatia katika kazi zake.
Anasema kinachojitokeza ni mtazamo usiosahihi kwa mashibiki na kutokuelewa kama msanii anaweza kufanya shoo yoyote kama sehemu ya kazi zake kimuziki.
“Mashabiki wetu siwezi kuwahukumu kwani hawana ubaguzi hata kidogo, hawawezi kubadilishwa mapenzi yao kwa msanii kwa sababu za kisiasa, hatujafikia hatua ya kuwa na siasa au mashabiki wa aina hiyo,” anasema Fela.
Akitoa mfano Fela anasema msanii wa Hip Hop, Joseph Mbilinyi ambaye kwa sasa ni mbunge wa Mbeya Mjini, bado hajaathiriwa na siasa katika soko lake la muziki.
“Kama wasanii kujihusisha na siasa ingekuwa na athari basi ‘Sugu’ leo hii asingeweza kufanya shoo ambayo inaweza kuchanganya mashabiki wa aina zote bila kujali itikadi za vyama vyao,” anasema Fela na kuongeza;
Kwa hivyo mimi nadhani huo ni mtazamo ambao siyo sahihi kabisa, muziki wetu bado haujawa na tatizo kama hilo na siamini kama linaweza kujitokeza katika siku za mbele.

Kagame: Tutamshughulikia yeyote anayeisaliti Rwanda

Kigali. Rais Paul Kagame wa Rwanda ameonya kwamba yeyote atakayewasaliti Wanyarwanda na Serikali yake anastahili kuchukuliwa hatua kali na kwamba amejitolea maisha yake kuijenga na kuhakikisha Rwanda inakuwa salama dhidi ya wote wasio na mapenzi mema.
Akizungumza katika ibada maalumu ya kuliombea taifa juzi, Kagame aliwataka Wanyarwanda wote kuungana katika kusimamia misingi sahihi na msimamo wao kama taifa, bila kujali tetesi zinazotoka katika mataifa ya nje kuhusu wale waliotangaza kuisaliti Serikali yake.
Japokuwa hakutaja moja kwa moja kuhusu tuhuma zinazoikabili Serikali yake kuhusiana na mauaji ya aliyewahi kuwa Mkuu wake wa Ujasusi aliyeuawa Januari mosi akiwa hotelini huko Afrika Kusini, Patrick Karegeya, alisema wale wote wanaoigeuka nchi yao na kuchagua kuua raia wasio na hatia kwa sababu zao binafsi wanastahili kushughulikiwa ipasavyo.
“Sitakuwa na huruma na watu ambao wanasahau namna Rwanda ilivyowatengeneza na kuwa hapo walipo na hatimaye wanaamua kuisaliti kwa kuua raia wa Rwanda wasio na hatia, wakiwemo kinamama na watoto,” aliongeza.
Alisema Rwanda haina sababu ya kuhusishwa au kuwajibishwa kwa ajili ya wale walioamua kuchukua njia zaidi na kufanya mambo yao kwa nia ya kuharibu yale yaliyofanyika kwa ajili ya kuliimarisha taifa la Rwanda.
Aliwataka viongozi wa Rwanda kutokusumbuliwa kwa yanayowakuta ‘maadui wa taifa’ kwa kuwa Mungu aliwapa nguvu ya kujenga na pia kukilinda kile walichokijenga, hivyo wale wanaosahau kwamba wana dhamana kwa Wanyarwanda na kuamua kutenda mambo mabaya dhidi ya taifa lao ni hakika kwamba wamesahau kuwa hawataweza kuwa juu ya watu wao.
“Mliponiapisha kuwa kiongozi wenu mliniagiza kwamba wakati wote niilinde nchi hii, kwa maana ya kusimama kwa ajili ya watu wake.
 Lakini kila mmoja miongoni mwenu ana wajibu, aidha kwa njia ya kuhubiri au kukanusha tuhuma zozote za uongo kuhusu Rwanda,” alisema Kagame kama alivyokaririwa na gazeti la New Times la Rwanda.
Alisema watu wa mataifa ya nje ambao wamekuwa wakiinyooshea kidole Kigali wamekuwa wakifanya hivyo mara 1000 zaidi kwa ajili ya kulinda nchi zao.
Hakusita kukumbusha kwamba wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitishia wazi hadharani kutaka kuipindua Serikali na wamekuwa wakishiriki katika mikakati ya ulipuaji wa mabomu yaliyosababisha mauaji ya raia kwenye Mji wa Kigali.
Tutapambana
Mtandao wa Chimreports.com uliripoti kwamba Kagame alionekana ‘mwenye hasira’ aliposema: “Kwa wale waliotengenezwa na kuwa juu na Rwanda kisha kutugeuka kama taifa tutapambana nao. Yeyote anayeidharau Rwanda atashughulikiwa ipasavyo popote alipo.”

Serikali ya Afrika Kusini
Msemaji wa Wiara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Clayson Monyela alisema hajapata taarifa zozote kuhusu kauli hizo za Kagame na hata hivyo hawezi kusungumzia suala hilo kwa kuwa liko nje ua uhusiano wa kidiplomasia baina ya Rwanda na nchi yake.
Hiyo ni kwa sababu Kagame hakutaja nchi yoyote katika hotuba yake hiyo ya jumapili na Afrika Kusini haiwezi kuchukua hatua ya kujihisi kwamba labda ndiyo inayohusika.
“Tukio lililotokea Johannesburg liko chini ya uchunguzi wa polisi na wote tunasubiri matokeo ya uchunguzi huo. Hatuna sababu ya kuanza kumhisi mkuu yeyote wa nchi, hatuendeshi diplomasia yetu kwa mtindo huo,” alisistiza.
Kejeli
Jumamosi iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Jenerali James Kabarebe alikaririwa na mtandao wa AFP akizungumzia yaliyomkuta Karegeya aliyeuawa huko Afrika Kusini akisema: Unapochagua kuishi kama mbwa, utakufa kama mbwa.”
Alikaririwa akisema, “Msipoteze muda wenu kwenye ripoti kwamba fulani aliuawa kwa kutumia kamba katika gorofa ya saba kwenye nchi fulani. Unapochagua kuwa mbwa, utakufa kama mbwa, na wafanya usafi watasafisha na kutupa kwenye pipa la taka ili usiwachafue.
“Kimsingi hayo ni mambo yanayowapata waliochagua kupitia njia hiyo. Hatuna la kufanya juu yao, na hatuwezi kulaumiwa kwa ajili ya yanayowakuta,” alisema.
Mauaji ya Karegeya
Mwili wa Patrick Karegeya aliyekuwa mshirika wa Rais Kagame kisha kutofautiana na kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini ulikutwa ukiwa kwenye chumba cha hoteli mjini Johannesburg huku kukiwa na kitambaa chenye damu na kamba kando yake.
Baada ya polisi kueleza kwamba Karegeya aliuawa kwa kunyongwa, wasaidizi wake waliituhumu Serikali ya Rwanda kwa kuhusika na mauaji hayo.
Karegeya alikuwa mkuu wa usalama wa taifa akihusika na usalama wa nje wa Serikali ya Rais Kagame. Mwaka 2004 alishushwa cheo kisha kukamatwa na kuswekwa jela kwa miezi 18 kwa madai ya kwenda kinyume na mkuu wake wa kazi. Alikimbia nchini Rwanda mwaka 2007.
Pamoja na wapinzani wa Kagame kumtuhumu moja kwa moja kuhusika na mauaji hayo, Serikali yake haikuwahi kukubali au kukanisha moja kwa moja, lakini kwa kauli yake alisema juzi kwamba ‘Hahitaji kuomba ruhusua kwa yeyote anaposimamia ulinzi wa taifa lake.”

Nzuri kuitamka, tamu kuisikiliza

Bado tunazungumzia habari za mwaka mpya mpaka labda tutakapoingia mwezi wa pili. Mwaka mpya, mambo mapya au siyo?
Mwaka mpya umeanza, kila mtu sasa anazungumzia mipango yake kwa mwaka huu, huku wengine wakiwa na viporo vya mwaka jana, hata hivyo siyo ishu kwa kuwa huu ni mwaka mwingine na una mambo yake.
Ni mipango mizuri kuitamka na mitamu kuisikiliza, lakini je, huu ni uhalisia au tunatekeleza wajibu wetu kwa kuwa ndiyo maongezi yaliyotawala vinywa vyetu mwezi huu.
“Ninataka kubadilika, mwaka huu pombe no, situmii pesa ovyo, lazima nijenge, nitapunguza uzito, naacha sigara n.k,” hii ni baadhi tu ya misemo inayotawala mwezi huu.
Ni mitamu kweli kweli kuitamka na hata usikilizapo huleta raha. Kwa mhusika huenda inampa picha nzuri mbeleni kwani ikifanikiwa itakuwa bao la kisigino.
Cha kujiuliza hapa hivi ni kweli lazima tusubiri Januari mosi kuanza kutafuta mabadiliko katika maisha yetu, yaani ninaweza kuwa mtu tofauti Desemba 31, halafu nikaamka Januari mosi na kuwa mwingine.
Usiku wa mwaka mpya unalala ukiwa njwii kwa ulevi wa pombe, lakini ukiwa na matarajio ya kuacha ulevi kesho yake.
Kama ulikuwa hufahamu basi huu ndiyo ukweli, ni asilimia nane tu ya watu wote duniani ndio hufanikiwa kwa kutegemea mwaka mpya kubadilika, wengine wakijitahidi sana ni wiki moja tu baada ya hapo wanarudia maisha yao ya zamani.
Ni kujidanganya kudhani kuwa ifikapo tarehe fulani, unaweza kuiondoa tabia iliyojizoesha kwa miaka mingi.
Kisaikolojia unapojipangia tarehe za kubadilika katika kitu fulani, unakuwa unajiwekea ugumu kwani inatakiwa pale unapogundua tatizo uanze kulifanyia kazi na si kulipangia tarehe.
Maneno matupu hayavunji mfupa. Kupanga nitafanya hivi siku fulani ni sawa na usemi huo kwani hayo ni maneno matupu.
Kwa wenye tabia hii ni rahisi kusahau ulijipangia nini mara itakapingia Februari, pengine utaanza kuikumbuka mipango yako pale watu watakapoanza kuzungumza habari za mwaka kwisha.
Ikishafika Oktoba au Novemba kauli za ‘mwaka umeisha huu’ huanza kutawala maongezi yetu, hapo ndipo unaweza kukumbuka ulichojipangia kwa mwaka huu, lakini kwa kuwa ni mtu wa mwaka mpya basi utaona isiwe shida nitaaanza tena mwakani.
Kama unatamani mabadiliko basi usisubiri mwaka mpya, unapogundua kitu ndani yako ambacho ungependa kibadilike basi kifanyie kazi mara moja.
Mabadiliko hayaji mara moja bali kwa hatua ndogondogo, chukua hatua pale unapoona unapaswa kuanza.
Kuna matatizo mengine unapoyachelewesha ndipo yanapokuwa makubwa zaidi, badala ya kutumia muda mfupi kuyatatua unaweza kujikuta unatumia nguvu na pesa nyingi.
Mwaka mpya uwe wa kusherehekea sikukuu na mfanikio ambayo kwa uchache umeyafanikisha. Usisubiri mwaka mpya kuanza kufanya kitu fulani.

Makundi ya Urais yaivuruga CCM

Dar es Salaam. Makundi ya Urais wa 2015 yanaendelea kuivuruga CCM baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Singida, Mgana Msindai kuibuka na kusema atamburuta mahakamani Mwenyekiti mwenzake wa Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ asipomwomba radhi kwa kumchafua kwa kumwita mpuuzi.
Hata hivyo, Kasheku amesema Msindai anaweza kwenda mahakamani huku akisisitiza kwamba hawezi kumwomba radhi kwa kuwa anaamini kwamba alichofanya ni kinyume cha taratibu za chama na vikao.
Juzi, Kasheku alimponda Msindai mbele ya waandishi wa habari kwa kitendo chake cha kusema kuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa yote ya Tanzania wanamuunga mkono, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika safari yake ya urais wa 2015 wakati wa sherehe ya mwaka mpya huko Monduli, Arusha.
Msindai alisema jana kuwa amemtaka Kasheku aitishe mkutano wa waandishi wa habari na kumwomba radhi. “Asipofanya hivyo ndani ya siku saba nitampeleka mahakamani,” alisema Msindai.
Msindai pia alikanusha kuwa aliwekwa kitimoto katika mkutano wa wenyeviti wa CCM wa mikoa uliofanyika Zanzibar.
Msindai aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa miaka 15, alikiri kuwa alialikwa pamoja na wenyeviti wenzake sita katika sherehe ya mwaka mpya iliyoandaliwa na Lowassa huko Monduli.
Katika sherehe hizo, Lowassa alitangaza kuwa ameanza safari ya matumaini, kauli ambayo wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliitafsiri kama tangazo la kuwania urais mwaka 2015.
Msindai alikanusha kutangaza kuwa wenyeviti wote wa CCM wa mikoa wanamuunga mkono Lowassa wakati wa sherehe hiyo... “Mimi ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa wenyeviti wote wanamuunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu 2015... kikubwa tulichozungumza ni kumuunga mkono katika safari yake ya mafanikio katika kuendeleza elimu, maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na uwezo wake katika kusimamia mipango yake ya maendeleo na zaidi katika kupigania elimu pana kwa Watanzania.
“Alipokuwa Wizara ya Maji alichangia maji kupatikana Dar es Salaam na mikoani na maendeleo mengi, uwajibikaji kwenye jimbo lake na aendelee hivyo...hayo ndiyo tuliyomsifia. Nilizungumza haya na sitabadilika,” alisema Msindai, ambaye alisema haogopi kufukuzwa.
“Mimi si mpya ndani ya CCM kama ‘Msukuma’. Nina miaka zaidi ya 40, ninaelewa taratibu zote za chama za udiwani, ubunge na urais. Kama ni kampeni ni baada ya chama kumpitisha mtu na sisi tutamuunga mkono... hata mimi ninaweza kuwania urais,” alisema.
Siombi radhi
Kwa upande wake Kasheku alisema hamwombi radhi Msindai, kwani si wenyeviti wote wa CCM wanaomuunga mkono Lowassa katika safari yake aliyoiita ya matumaini.
“Siombi radhi na hata sasa hivi anaweza kushtaki, tulipokutana Zanzibar alitueleza kuwa alitoa kauli ya kuumuunga mkono Lowassa kimakosa na kusema alikuwa akimaanisha yeye na wenzake aliokwenda nao Monduli ndiyo wanamuunga mkono Lowassa,” alisema Kasheku.
Kasheku alifafanunua kuwa Msindani alisema kuwa wanahabari walikosea kumnukuu baada ya kuandika katika vyombo vya habari kuwa alisema wenyeviti wote wanamuunga mkono Lowassa.
Alisema baada ya Msindai kukiri jambo hilo, wenyeviti waliokuwa Zanzibar waliandaa tamko la pamoja na kuagiza lisomwe na Msindai mbele ya wanahabri katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Dar es Salaam.
“Katika huo mkutano ilitakiwa niwepo mimi (Kasheku), Msindai na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, ila cha ajabu mwenzetu (Msindai) alitukimbia na tulipomtafuta akasema yupo Singida, hivyo sisi tuliamua kutoa tamko lile,” alisema Kasheku.
Alisema kauli aliyoitoa Msindai ni kinyume na maagizo ya wenyeviti wote wa CCM, huku akimtaka kabla ya kwenda mahakamani, ahakikishe kuwa amewasilisha malalamiko yake ndani ya chama ili Kamati ya Maadili ya chama ikae na kutoa uamuzi.
“Hatuna ugomvi na Lowassa, tuna ugomvi na yeye aliyetuweka nyuma yake na kusema wote tunamuunga mkono Lowassa, nani alimwambia maneno hayo na ilikuwa katika kikao gani?,” alihoji Kasheku na kuongeza:
“Kama kuna watu wapo nyuma ya Lowassa au mtu yeyote ni siri yao, iweje yeye atulazimishe sisi kuwa nyuma yake kwa mgongo wa Mbunge wa Monduli”.
Mgeja amtetea Msindai
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja ambaye pia alikuwa Monduli, alimtetea Msindai akisema hakuwahi kuzungumzia suala la urais katika mkutano huo wa Monduli zaidi ya kumsifu Lowassa kwa mafanikio aliyoleta kwenye jimbo lake na maeneo mengine alipokuwa Waziri Mkuu.
Alisema hakuna dhambi kwa kumpenda mtu yeyote, wote wanaotoa kauli za kukanusha ni dalili za woga, wivu, kutokujiamini na inawezekana wana watu nyuma yao.

Pinda kuitia hasara Serikali

Dar es Salaam: Uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu malori makubwa ya mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetajwa kuwa ni hatari na utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Hasara hiyo inatokana na uharibifu wa barabara za lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha uzito wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya 2001.
Ujenzi wa barabara ni wa gharama kubwa na hata ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za walipakodi kutokana na uharibifu unaofanywa.
Mathalani katika bajeti yake ya 2013/14, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imetenga kiasi cha Sh314.535 bilioni kwa ajili ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa.
Kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi ya robo ya bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga barabara mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya kilometa moja kugharimu Sh1 bilioni. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti nzima ya Wizara ya Ujenzi ni Sh1.226 trilioni.
Kauli ya Dk Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, ujasiri wa Dk Magufuli ulizimwa na amri ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetengua agizo la waziri huyo na kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kutumia barabara.
Wasemaji wa Serikali
Ofisa Habari wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo alisema suala hilo wameliachia Ofisi ya Waziri Mkuu. “Hilo suala liko Ofisi ya Waziri Mkuu, siwezi tena kulizungumzia,” alisema Ntemo kwa kifupi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florence Turuka alisema siyo sahihi kusema kwamba Waziri Mkuu amevunja sheria kwani ilikuwa ni lazima serikali ichukue hatua jumuishi kwa kuwashirikisha wadau husika.
“Siyo sahihi kusema kuwa tunataka kuvunja sheria, sisi tumepokea mapendekezo na tutayaangalia kabla ya kutoa ripoti. Wewe vuta subira tu,” alisema Dk Turuka.
Dk Turuka alisema kamati iliyoundwa na Serikali ikiwajumuisha wadau mbalimbali wa barabara ilikamilisha kazi yake Desemba mwaka jana na kwamba hivi sasa Serikali inatafakari mapendekezo yaliyotolewa.
“Kamati ilishamaliza kazi tangu Desemba mwaka jana… tulipokea mapendekezo kwa sababu ile ilikuwa kamati jumuishi, kulikuwa na watu wa Tatoa, Taboa na Wizara ya Ujenzi na wataalamu, na sasa tunayafanyia kazi,” alisema Dk Turuka.
Baadhi ya barabara ambazo zilikuwa katika hali nzuri hivi sasa zimeharibika vibaya chanzo kikiwa ni uzito wa magari ya mizigo. Miongoni mwa hizo ni Barabara Kuu ya Morogoro - Dodoma kati ya Kijiji cha Magubike na Mji wa Gairo pamoja na Barabara ya Dar es Salaam ya Morogoro eneo la kati ya Mlandizi na Chalinze.
Hali hii ndiyo iliyomsukuma Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kufuta waraka unaoruhusu magari ya mizigo kuzidisha uzito na badala yake kutaka sheria inayotaka malori yanayozidisha uzito uliopo ndani ya asilimia tano kupunguza mzigo, kupanga mzigo upya au kulipia uzito uliozidi mara nne ya tozo ya kawaida, ifuatwe.
Uamuzi wa Dk Magufuli ulipingwa na wamiliki wa magari makubwa ya mizigo na kuungwa mkono na wamiliki wa mabasi ya abiria, hivyo Waziri Mkuu Pinda aliingilia kati na kuamuru utaratibu wa awali uendelee, ilhali suala hilo likiwa linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Hata hivyo, Pinda alitangaza uamuzi wa kusitishwa kwa utekelezaji wa amri ya Dk Magufuli katika mkutano ambao hata hivyo waziri huyo wa sekta husika hakuhudhuria. Wakati huo kulikuwa na tishio la kusitishwa kwa usafirishaji nchi nzima kama amri hiyo isingetenguliwa.
Chanzo cha habari ndani ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kinasema: “Tatizo kuna viongozi wengi wenye malori na mabasi ndiyo wanaokwaza utekelezaji wa sheria hiyo.”
Kiliongeza: “Utakuta mtu ana magari hadi 300 na yote yanazidisha uzito kwenye barabara kwa kisingizio cha kusamehewa asilimia tano, unadhani barabara zetu zitaishia wapi? Ndiyo maana Dk Magufuli kwa uchungu aliamua kuweka msimamo”.
Takwimu za vipimo
Takwimu za upimaji wa magari ambazo ziko kwenye tovuti ya wakala huyo wa barabara nchini zinaonyesha kuwa licha ya kuwepo nafuu katika sheria bado magari mengi yamekuwa yakizidisha uzito.
Mathalan 2011/12 magari 684,600 yalipimwa na kati ya hayo, 167,310 sawa na asilimia 24.44 yalikutwa yakiwa yamezidisha mizigo, huku mengine 8,856 sawa na asilimia 1.30 yalipitisha kiwango cha asilimia tano.
Hata hivyo, inaelezwa katika taarifa hiyo kuwa, asilimia 98.67 ya magari yanayozidisha mizigo huwa katika kiwango cha uvumilivu wa asilimia tano, hali inayoonyesha kuwa ama wanahamisha mizigo au upangaji mbaya wa mzigo ule ule katika gari.
Kwa mwaka 2011/ 2012, Tanroads ilitoza fani ya Sh865,408,344.20 ambapo Sh859,508,181.40 zilikusanywa. Kwa mwaka 2013, magari 3,060,057 yalipimwa na kati ya hayo, 790,777 sawa na asilimia 25.84 yakiwa yamezidisha mizigo. Asilimia 1.62 yalikuwa ndani ya mstari wa asilimia tano na kwa jumla adhabu ya Sh5,490,255,235 ilikusanywa.
Wadau wa usafirishaji
Mkurugenzi wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Zacharia Hanspope alitetea mgomo wao huku akimtaka mwandishi amtafute msemaji wao kwa maelezo zaidi. Hata hivyo, alipotafutwa msemaji huyo, Elias Lukumay hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo akisema kuwa bado wako kwenye vikao na Serikali.
“Nisingependa kuzungumzia suala hilo kwa kuwa kwa sasa kuna vikao vinaendelea. Tutawajulisha tu,” alisema Lukumay.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema kwa sasa wanaendelea na vikao na Serikali, lakini bado msimamo wao ni kutokubali kupima mabasi kwenye mizani.
“Tunaye mwakilishi wetu kwenye vikao na Serikali. Unajua kuna kamati iliyoundwa na Wizara ya Ujenzi na nyingine iliundwa na Waziri Mkuu,” alisema Mwalongo na kuongeza:
“Tumekuwa tukipinga hatua hiyo kwa muda mrefu. Mwaka 2004 tulipeleka madai serikalini na 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani alitoa tamko la kutusitishia upimaji, lakini Wizara ya Ujenzi haitaki,” alisisitiza Mwalongo.
Sheria ilipindishwaje?
Ruhusa inayovunja sheria hiyo, ilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba 2006, hatua ambayo iliwaudhi wafadhili kutoka Norway.
Katika barua yake aliyomwandikia Mwenyekiti wa Tatoa) wakati huo, S.A Seif, Julai 19, 2006 kujibu maombi yao, Waziri Mramba aliagiza kuwa gari lisionekane kuwa limezidisha uzito hata kama unazidi kiwango cha asilimia tano iliyowekwa na sheria hiyo.
“Kwa hiyo nimeamua kwamba, ekseli haitahesabika kuwa imezidisha kama mzigo huo utakuwa umepita kiwango cha kisheria baada ya kutoa asilimia tano cha uvumilivu wa kusoma mzani na baada ya kushuka hadi kilo 100,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Mramba ambayo gazeti hili limeiona..
Hata hivyo, barua hiyo ilipelekwa tu kama nakala Tanroads jambo linalodaiwa kumkera mkurugenzi wake. “Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads wakati huo, Ado Abeid alitaka sheria hiyo irudishwe kama ilivyokuwa, lakini Waziri Mramba alikataa,” kinasema chanzo cha habari.
Hatua hiyo ya kupindisha sheria inaelezwa kuwakera wafadhili wa barabara kutoka Norway, Kampuni ya Asborn Norwegian Public Roads Administration iliyokuwa ikishauri kuhusu udhibiti wa uzito na hivyo kujitoa tangu mwaka 2006 kwa kutoridhishwa na hatua hiyo.
Sehemu ya barua hiyo ya Novemba 18, 2006, inasomeka: “Baadhi ya vipengele vilivyomo katika barua vinahusika na vinatakiwa kufuatwa kama hatua muhimu za kuimarisha utendaji wa mizani, kanuni na vitendea kazi.
“Hata hivyo, barua yako pia imezungumzia mambo ya kufanya kuhusu udhibiti wa mzigo katika ekseli ambapo baadhi ya vipengele vimeachwa. Hali hii itaathiri udhibiti kwa ujumla na kusababisha vurugu na uharibifu utakaoathiri utendaji.”
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya barua hiyo na kutokuwepo kwa dalili ya kurekebisha sheria hiyo, tangu wakati huo kampuni hiyo ilijitoa kusaidia miradi ya barabara nchini.
Hata hivyo, uamuzi wa Mramba uliopata utetezi wa Pinda alipokuwa akitengua amri ya Dk Magufuli akisema ilitokana na malalamiko ya wadau.
“Lengo lake ilikuwa ni kufidia matatizo ya upungufu wa mizani kutoweza kupima kwa usahihi uzito wa magari yanayopimwa katika vituo mbalimbali vya mizani nchini, lakini hivi sasa mizani yetu ni mizuri na ya kisasa,” alisema Pinda na kuongeza:
“Lakini ikumbukwe kuwa agizo hilo lilikuwa kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 toleo la 2002 na kanuni zake za 2001, ambayo inazuia malori kuzidisha uzito. Mramba aliamua vile ili kumaliza hali iliyokuwa imejitokeza wakati akiwa Wizara ya Miundombinu”.
Chanzo kinaendelea kufafanua kuwa, baada ya Mramba kuondoka katika wizara hiyo mwaka 2007, wizara hiyo pia iliongozwa na mawaziri, Andrew Chenge na Dk Shukuru Kawambwa ambao pia hawakuwahi kuifanyika kazi sheria hiyo.
Matakwa ya sheria
Sheria Na. 30 ya 1973 na kanuni Namba 30 ya 2001 iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali tangazo Namba 30 la Februari 9, 2001 ilianza kutumika Januari 24, 2001 inafafanua uzito wa magari unaotakiwa.
Kipengele cha saba cha sheria hiyo kinaeleza magari yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea na aina ya makosa ya uzidishaji uzito, ambapo kifungu cha 2, 3, 4 vinafafanua matumizi ya uzito uliozidi asilimia tano.
Vifungu vya sheria hiyo vinasomeka ifuatavyo:
2. Kwa sababu ya usambazaji wa mzigo kwenye gari, ekseli au fungu la ekseli litahesabika kuwa limezidi uzito kama mzigo utazidi ukomo wa uzito unaoruhusiwa kisheria baada ya kuongeza asilimia tano (5) ya uzito unaoruhusiwa, na kisha kuiweka hesabu ya mwisho isomeke kwa wastani wa kilo mia moja za karibu.
3. Kwa kila ekseli yaweza kusafirisha kama ziada ya uzito kiasi cha asilimia tano (5) ya uzito unaoruhusiwa. Hata hivyo, kama mzigo wenye uzito wa ziada hautapakuliwa, tozo kwa uzito huo wa ziada itakuwa mara nne zaidi ya tozo ya kawaida inayolipwa kwa uzito uliozidi.
Mzigo wote wenye uzito unaozidi asilimia tano (5) utapakuliwa na kupakiwa kwenye gari jingine isipokuwa tu kama kibali maalum kimetolewa.”
4. Kama gari limethibitishwa kwamba limebeba uzito zaidi ya ule unaoruhusiwa gari hilo halitaruhusiwa kuendelea na safari mpaka hapo mzigo uliozidi utakapohamishiwa kwenye gari lingine au kupangwa upya ili kila ekseli iwe na uzito unaotakiwa.
“Baada ya kushusha au kupagwa upya gari lazima lipimwe upya tena kuhakikisha kuwa mzigo uliobebwa upo kwenye viwango vinavyokubalika.”