“Tutakuwa
live (kusikika na kuonekana moja kwa moja kutoka Jangwani) katika redio
nne na televisheni nne. Hatuwezi kutaja ni redio gani, lakini wananchi
wawe makini na kuzingatia uwezekano wa wao kupata matangazo hayo kuanzia
saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:00 jioni,” Tumaini Makene.
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chadema na
Ukawa, Edward Lowassa, ambaye leo atazindua kampeni zake kwenye viwanja
vya Jangwani, jana aliamua kufunguka dhidi ya vitendo vya Jeshi la
Polisi kupiga wananchi, akisema havikubaliki kwa kuwa vifaa
vinavyotumika vinanunuliwa na kodi wanazokatwa.
Lowassa,
ambaye anagombea urais chini ya mwavuli wa vyama vinne-Chadema, NLD,
CUF na NCCR-Mageuzi, anazindua kampeni hizo baada ya kukabiliana na
vizingiti kadhaa vilivyowekwa na taasisi za Serikali kuanzia wakati
anatafuta wadhamini hadi sakata la kibali cha kutumia eneo hilo leo.
Akizungumza
jana wakati wa majumuisho ya ziara zake fupi za jijini Dar es Salaam
ambazo pia zilikatishwa na mazuio kutoka Jeshi la Polisi na Wizara ya
Afya, Lowassa alisema vitendo hivyo vinaweza kuifanya Serikali ishtakiwe
iwapo kutatokea vurugu. “Haiwezekani hela za walipakodi zitumike na
polisi kupiga mabomu ya machozi. Tutawapeleka The Hague (Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Kihalifu),” alisema Lowassa wakati akiongea na
makundi mbalimbali kwenye Hoteli ya Lamada jana.
Lowassa
pia alisema kuna watu wanazusha kuwa akiingia madarakani atawafukuza
Watanzania wenye asili ya Asia, jambo ambalo alisema si la kweli na
hawezi kufanya hivyo kwa kuwa yeye si rais wa zamani wa Uganda, Idi
Amini.
Katika makundi hayo, kulikuwa na wasanii zaidi
ya 60 wa muziki wa kizazi kipya na waigizaji filamu, wengi wao wakiwa ni
wale ambao hawajaonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu kuanza kwa
harakati za uchaguzi.
Mkutano wa leo unafanyika baada
ya Chadema kukataliwa na Serikali kutumia Uwanja wa Taifa, wenye uwezo
wa kuchukua watu 60,000, na baadaye Ofisi ya Manispaa ya Wilaya ya Ilala
kukatalia viwanja vya Jangwani kwa madai kuwa vilishakodiwa na CCM kwa
siku tatu mfululizo kwa ajili ya matamasha ya wasanii.
Hata
hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliingilia kati na chama hicho
kikuu cha upinzani kuruhusiwa kutumia viwanja hivyo maarufu kwa michezo
na mikutano mikubwa ya kidini na kisiasa.
Vyama vilivyo
katika Ukawa vimepania kufanya mkutano mkubwa jijini Dar es Salaam
kabla ya Lowassa kwenda Iringa kuanza rasmi kampeni za mikoani, na
mgombea mwenza, Juma Haji Duni kuelekea Lindi na Mtwara.
“Tumekamilisha
maandalizi kwa asilimia 90,” alisema Tumaini Makene, Mkuu wa Kitengo
cha Habari na Mawasiliano wa Chadema, wakati akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu mkutano huo wa leo wa uzinduzi.
“Tutakuwa
live (kusikika na kuonekana moja kwa moja kutoka Jangwani) katika redio
nne na televisheni nne. Hatuwezi kutaja ni redio gani, lakini wananchi
wawe makini na kuzingatia uwezekano wa wao kupata matangazo hayo kuanzia
saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:00 jioni,” alisema Makene.
Alisema
baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa uzinduzi, Lowassa ataanza
kampeni katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kuanzia Mkoa wa Iringa
ambako alikusanya wanachama wengi waliomdhamini wakati alipokuwa
akiwania urais kwa tiketi ya CCM kabla ya kuhamia Chadema.
Lowassa
anatarajiwa kutumia mkusanyiko wa leo kuanza kumwaga sera za chama
hicho na Ukawa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mikutano ya awali
kuepuka kukiuka sheria inayokataza kuanza kampeni mapema.
Katika
taarifa yake ya jana, Jeshi la Polisi lilisema limejiandaa vizuri
kuhakikisha kunakuwa na usalama kwenye viwanja hivyo na askari wake
watalizunguka eneo hilo.
“Watu wanaruhusiwa kuja katika
makundi madogo madogo kwa kutumia vyombo vya usafiri kama vile mabasi,
magari madogo, pikipiki, watembea kwa miguu au baiskeli na si
kusubiriana katika makundi makubwa yanayoashiria taswira ya maandamano,”
inasema taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova.
Mkutano wa leo utahudhuriwa pia na
Duni, ambaye amepitishwa kuwa mgombea mwenza wa Lowassa baada ya Chadema
kufikia makubaliano maalumu ya yeye kuhamia chama hicho akitokea CUF
chini ya mpango wa ushirikiano wa Ukawa wa kujiandaa kushika dola.
Wengine
wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa leo ni Seif Sharif Hamad,
anayegombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Twaha Taslima (Kaimu
Mwenyekiti wa CUF), Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), James Mbatia
(Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi), na Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD).
Mkutano wa leo umetanguliwa na matukio mengi ya kusigana baina ya
Chadema na vyombo vya Serikali. Awali Chadema iliomba kufanyia mkutano
huo kwenye Uwanja wa Taifa kutokana na idadi kubwa inayomfuata Lowassa
kila aendako, lakini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
ilimkatalia kwa madai kuwa imeona kwa sasa uwanja huo ubakie kwa
shughuli za kimichezo tu.
Baadaye Lowassa alifanya
ziara fupi jijini Dar es Salaam, akianza kwa kupanda basi la daladala
kutoka Gongo la Mboto hadi Chanika na siku iliyofuata alitembelea maeneo
ya Tandale kabla ya Jeshi la Polisi kupiga marufuku safari zake
likisema zinasababisha foleni zisizo na umuhimu kutokana na kuibuka kwa
misafara kila anakokwenda.
Mbunge huyo wa Monduli pia
alipanga kutembelea hospitali tatu za wilaya za Dar es Salaam, lakini
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikatangaza kuzuia ziara hizo, ikidai
zingesumbua wagonjwa, kitu ambacho Chadema imekipinga ikitoa mfano wa
mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu kutembelea hospitali mjini Moshi
bila ya kubughudhiwa na vyombo vya dola.
Wakati Chadema
na Ukawa wakijiandaa kwa mkutano wa leo, Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya
Ilala aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kisingeweza
kutumia viwanja vya Jangwani kwa kuwa vimeshachukuliwa na CCM. Hata
hivyo suala hilo lilimalizwa juzi. Kutokana na msigano huo, NEC
imewaagiza wakurugenzi wote wa wilaya, ambao pia ni wakurugenzi
wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha shughuli za kampeni zinapewa
kipaumbele wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Juzi
Chadema ilikwepa vikwazo hivyo vya Serikali baada ya kuandaa mkutano wa
ndani na wanawake wa makundi mbalimbali jijini Dar es Salaam uliofanyika
katika jengo la Millennium Towers ambao ulihudhuriwa na wanawake kutoka
katika kila kada. Katika mkutano huo, Mbowe aliwaomba wakazi wa Dar es
Salaam kujitokeza kwa wingi leo kwenye viwanja vya Jangwani kumsikiliza
mgombea wa urais wa Chadema (Ukawa).
“Tunaomba
Watanzania waje kwa mamilioni sio kwa maelfu,” alisema Mbowe kwenye
mkutano huo na kuwaahidi wanawake wote watakaofika Jangwani kuwa
wataandaliwa eneo maalumu ambalo litakuwa na ulinzi ili kuwawezesha
kufuatilia matukio bila usumbufu.
Mkutano huo
unafanyika katika eneo hilo ikiwa ni siku sita tangu mgombea wa CCM, Dk
John Magufuli kuzindua kampeni zake kwenye viwanja hivyo akiwa
ameambatana na Rais Jakaya Kikwete, marais wa zamani, Benjamin Mkapa na
Ali Hassan Mwinyi na makada wengine wa CCM.
19 wapata dhamana
Wakati
kampeni za Chadema zikianza leo, wafuasi 19 wa chama hicho waliokuwa
wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kufanya mkusanyiko na maandamano
wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Wafuasi
hao, ambao ni pamoja na wanafunzi na wafanyabiashara, walikaa Segerea
kwa siku tatu kutokana na kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana.