Wednesday 9 April 2014

Kamati kumi zaitesa CCM

Dodoma. Kura za awali katika Kamati 10 kati ya 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zinakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi,(CCM) kutekeleza azma yake inayotajwa kuwa ni kufumua Rasimu ya Katiba, ili kuondoa mapendekezo ya Muundo wa serikali tatu, baada ya wajumbe wa Zanzibar kukwamisha upatikanaji theluthi mbili.
Kwa mujibu wa taarifa za kamati, ambazo tangu juzi zimeanza kutolewa katika sura ya kwanza na sita zinazungumzia Muundo wa Muungano, wajumbe kutoka Zanzibar kwa sasa ndiyo kikwazo kikubwa kwa CCM.
Hata hivyo, uamuzi ya mwisho kuhusu Muundo wa Serikali, kati ya mbili au tatu, unatarajiwa kujulikana Alhamisi wiki ijayo, wakati kamati zote zitakapowasilisha taarifa zao na kupigwa tena kura kwa wajumbe Tanzania Bara peke yao na Zanzibar peke yao.
Iwapo wajumbe wa Zanzibar wakiitetea kwa theluthi mbili kama sasa, mapendekezo ya muundo wa serikali tatu ndiyo yatakayopelekwa kwa wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo, Stephen Wassira, Ummy Mwalimu, Anna Abdalah na Paul Kimili, walitaja moja ya vifungu ambavyo vimeshindwa kupata theluthi mbili kuwa ni ibara ya kwanza kifungu cha kwanza.
Akizungumza jana Wassira ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita alisema kwamba katika kamati yake ibara hiyo imeshindwa kupata theluthi mbili, ili kuweza kufanyiwa marekebisho.
“Lakini huu siyo mwisho kama nilivyosema awali, tukirudi bungeni tutapiga kura kwa wajumbe wote na ndiyo itakuwa na uamuzi wa mwisho kama muundo wa Muungano utakuwa na Serikali tatu ama mbili, ambao utapelekwa kwa wananchi,” alisema Wassira.
Jussa, Lissu- tumeibana CCM
Jussa alisema: “Kwa taarifa za matokeo tulizonazo katika Kamati Namba 1, 2, 3, 4, 6, 10, 11 na 12 mapendekezo ya kubadilisha Rasimu katika ibara hizo mbili yamekwama. Kama CCM wakichakachua sura ya kwanza na sita, maana yake ni kwamba hapa hakuna Katiba, hakuna kura ya maoni na hakuna mwafaka.”
Vifungu hivi pia kwa mujibu wa wenyeviti wa kamati nyingine, isipokuwa kamati ya Tano, ambayo inaongozwa na Hamad Rashid, havikupata kura theluthi mbili na hivyo kubaki kama vilivyo kwenye rasimu.
Naye Lissu alisema kwa sasa CCM ndiyo inaweza kuanza mkakati wa kuvuruga Bunge kwani tayari wamejua hawana theluthi mbili ya Zanzibar ili kubadili Rasimu kama wanavyotaka.

Msekwa: Sitta ana lake jambo

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, ‘mzungumzaji huyo ana lake jambo’.
Sitta akizungumza na gazeti hili juzi mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alifafanua kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi ‘us’ kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno ‘Msekwa’ kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.
Msekwa akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi, lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo.”
Aliongeza: “Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino upo?”
Maoni mengine
Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Taarifa kwa Wananchi Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda alisema yote hayo yanatokea ni kuvuruga hoja iliyopo mezani.
Alisema kitendo cha kupoteza muda kuzungumzia suala la kuchezewa kwa saini halitakiwi kwani kama maudhui yake hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe.
“Tusianze kupoteza muda kwa mambo ambayo hayapo cha msingi wananchi wenyewe waulizwe wanaupenda Muungano au la lakini tusianze kumtafuta mchawi kuwa saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe kuhusu Muungano,” alisema Mwakagenda.
Sakata lilivyoanza
Utata huo ulianza wiki hii baada ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.
Hali hiyo ilitokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.
Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo katika hati hiyo ni ya kwake.
Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.
Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kwa upande wake Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.

Matumaini Katiba Mpya arijojo

Ikulu imeeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014.
Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue alilieleza gazeti hili kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa, wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu kupatikana Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.
“Kweli matarajio ya awali yalikuwa hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine, ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya,” alieleza Balozi Sefue.
Katika hali isiyoeleweka Balozi Sefue alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa Serikali kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.
Alisema muda huo wa kupatikana Katiba Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini ambao aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa alisema walipendekeza kwamba badala ya kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15 Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu ujao kwa lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba Mpya.
“Lakini walitukebehi na kututukana sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za mchana,” alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali kuna watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba.
Alisema ana taarifa za Bunge Maalumu kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.
“Kwa akili ya kawaida tu isiyohitaji elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi siyo watoto wadogo,” alieleza Dk. Slaa.
Kauli ya LHRC
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema siyo tu Serikali imeshindwa kutimiza ahadi ya muda iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.
Dk. Bisimba alisema kwa hali ilivyo, hawana hakika ya kupata Katiba na ikipatikana haitakidhi matakwa ya wananchi, kwa kuwa wanataka Katiba ya watu siyo ya kundi moja la watu.
“Mambo ya nchi hii tunayafahamu, inaweza ikapatikana kwa nguvu lakini wajue wananchi wataikataa na hata ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza kuathiri ustawi wa taifa,” alieleza Dk. Bisimba.
Alisema hilo waliliona mapema, wakataka kila hatua ya mchakato ipewe muda wa kutosha kabla ya hatua nyingine, ili wananchi waelimishwe lakini hawakusikilizwa.
Alisema kuwa katika mazingira hayohayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi kubwa hadi kufanikisha maoni ya wananchi kupatikana na kutengeneza Rasimu ya kwanza na ya pili iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014, lakini kwa jinsi Bunge Maalumu linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo itaharibiwa.
“Wakichezea Rasimu wajue wanachezea maoni ya wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia kura ya maoni na hivyo kusababishia taifa hasara isiyomithilika,” alieleza Dk. Bisimba.
Dk. Bisimba alisema mchakato huo umegharimu taifa fedha nyingi, muda mwingi, nguvu, akili, afya na hata uhai wa watu, hautakiwi kufanyiwa mzaha.
Alipotafutwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala hilo jana hakupatikana, lakini Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo ni dhahiri haiwezekani kupata Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na ilivyodhaniwa awali.
Hata hivyo, Kairuki alisema hawezi kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
“Hata hivyo tunachotakiwa kuzungumzia ni ubora wa kazi inayofanyika ili kufikia lengo la kupata Katiba itakayoongoza nchi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Kairuki.

Thursday 3 April 2014

Waathirika wa milipuko ya Osama Dar wafurahia fidia

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafamilia wa waliopoteza ndugu kwenye shambulio la ugaidi katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998, wameelezea kufarijika kutokana na malipo ya fidia, licha ya kwamba hayawezi kurejesha uhai wa waliokufa.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, ndugu hao walisema, licha ya mahakama nchini Marekani kuwapa fidia lakini pengo la jamaa zao halitazibika.
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Marekani, ilitoa amri ya kuwalipa fidia ya dola za Marekani 957 milioni (Sh1.555 trilioni) waathirika 23 wa shambulio hilo.
Jaji Thomas Bates katika hukumu yake alisema kati ya fedha hizo, Dola za Marekani 420 milioni (Sh670 bilioni) watapewa ndugu wa marehemu watano na waathirika wanne wa Tanzania wakati kitita kilichobaki kitakwenda kwa waathirika ambao ni Wamarekani.
Jaji Bates alisema Serikali za Iran na Sudan zitawajibika kulipa fidia hizo kutokana na kuhusika na mashambulio hayo mabaya kuwahi kutokea Afrika Mashariki.
Mmoja wa jamaa waliopoteza maisha katika tukio hilo, Kulwa Ramadhan alisema anasubiri kuletewa taarifa zaidi kuhusu taratibu za kupata fidia hiyo.
“Huwezi kuwa umeridhika na fidia kwa kuwa tumepoteza ndugu zetu lakini pia hata hicho kilichopatikana hatukukitarajia kupata,” alisema Ramadhan.
Alisema kuna baadhi ya jamaa wa marehemu watano hawakuingizwa kwenye idadi ya watakaopata fidia kutokana na kuchelewa kujiandikisha katika kesi hiyo.
“Baada ya tukio uongozi wa Ubalozi wa Marekani ulituambia tutoe taarifa zetu zote za mawasiliano na kwamba tusibadilishe namba za simu kwa ajili ya kuwasiliana kinachojiri.
“Lakini kuna baadhi ya jamaa walibadilisha namba zao na kufanya mawasiliano kuwa magumu hivyo kushindwa kuingizwa katika idadi ya wadai katika kesi hiyo,” alisema.
Ramadhan aliyempoteza pacha wake, Dotto Ramadhani alisema baadhi ya jamaa walijitokeza baadaye baada ya hatua muhimu za kesi kufanyika kitendo ambacho kiliwazuia kushiriki katika kesi.
Waathirika wengine
Naye Judith Mwila aliyempoteza mume wake kwenye tukio hilo, alisema anashukuru Ubalozi wa Marekani pamoja na mawakili waliowasaidia kufanikisha kesi hiyo.
“Binafsi nimepata taarifa kamili jana (juzi) kutoka kwenye gazeti la Mwananchi na sikutarajia kama tungeshinda kesi hiyo na tukapewa fidia ya fedha kiasi hicho. Hata hivyo tunaendelea kusubiri taarifa za mawakili wetu kuhusu taratibu zinazofuata kupata fedha hizo,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo atapata sehemu ya fedha hizo atashauriana na watoto wake jambo la kufanya ikiwamo kufanya biashara kubwa. Mwila ana watoto watatu alioachiwa na marehemu mume wake.
Alisema kuwa tangu mchakato wa kesi ulipoanza mwanzoni mwa mwaka 2001, Ubalozi wa Marekani na mawakili wao, walimpeleka Marekani mara mbili.
“Kesi hii imedumu muda mrefu. Mara ya kwanza nilikwenda 2001 kutoa ushahidi na mara ya mwisho ni 2010 na tangu wakati huo tulikuwa tukipewa tu taarifa juu ya maendeleo ya kesi,” alisema Mwila.
Kwa upande wake, Grace Paulo ambaye alifiwa na mumewe Elisha Paulo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa sisi kushinda kesi hii na hivyo tunasubiri mawasiliano na wahusika kufahamu jinsi ya kupata fedha hizo.
“Tumekuwa tukiishi kwa shida sana, hivyo hizo fedha zitatusaidia kujikwamua na matatizo yanayonikabili na mwanangu,” alisema Paulo ambaye aliachiwa mtoto mmoja aitwaye Mary Paulo.
Kwa mujibu wa waathirika hao, Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la Marekani (Usaid) liliwapa msaada wa kuwasomesha watoto pamoja na makazi ili kupunguza makali ya maisha.
Hata hivyo, wengi wao wanaendelea kufanya biashara ndogondogo kutokana na misaada hiyo kuwekwa katika eneo maalumu la ada za watoto.
“Kwa sasa ninafanya biashara ya kuuza nguo za mitumba na nilishaondoka Dar es Salaam mara tu baada ya msiba mwaka 1998 kutokana na maisha ya mjini kuwa magumu.
“Baadaye Ubalozi kupitia taasisi za kiraia walinitafuta hadi wilayani Mpwapwa ndipo waliponijengea nyumba ninayoishi sasa,” aliongeza Paulo anayeishi mkoani Dodoma.
Jamaa hao pia walisema kuwa gharama halisi za kesi hiyo hawazifahamu kutokana na kesi nzima kusimamiwa na Serikali ya Marekani na mawakili wao.
Hata hivyo, uhakika wa kupata fedha hizo unabaki mikononi mwa wakili wa jamaa hao, Thomas Fortune Fay ambaye baada ya hukumu hiyo alisema anafuatilia jinsi ya kupata fedha kwa Serikali za Sudan na Iran.
Alisema ataangalia jinsi ya kutaifisha baadhi ya mali za nchi hizo ili kupata fedha za kuwalipa waathirika hao.

Jaji Warioba aishangaa Serikali



Dodoma. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema waliokuwa wajumbe wa tume hiyo hawajawahi kudai malipo ya pensheni ya Sh200 milioni kama inavyodaiwa.
“Wajumbe wa Tume hawajatoa madai ya kulipwa shilingi milioni mia mbili. Hakuna mjumbe yeyote aliyetoa dai kama hilo na Serikali inajua,” alisema
Jaji Warioba katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, aliyoitoa kupitia Nyalali, Warioba and Mahalu Law Advocates ali ongeza:
“Nimeona taarifa iliyotolewa na Serikali kuhusu Tume ya Mabadiliko, nimeshangazwa na maudhui na lugha iliyotumika,” alisema Warioba akirejea taarifa iliyotolewa na Ikulu juzi ikieleza jinsi tume hiyo ilivyohitimisha kazi zake.
Wiki hii Jaji Warioba alikaririwa akilalamika jinsi yeye na makamishna wake walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari kwa haraka bila kusubiri siku waliyopanga kufanya makabidhiano, lakini Ikulu ilimjibu kwamba shughuli za Tume hiyo zilikoma siku ambayo Tume ilivunjwa.
Katika taarifa yake ya jana, Jaji Warioba alisema aliwasilisha Rasimu ya Katiba Machi 18 mwaka huu na Tume ilivunjwa Machi 19 wakati wajumbe wakiwa bado mjini Dodoma.
“Pamoja na lugha ya kejeli inayotumiwa na Serikali kuniita mnafiki, busara ya kawaida ilitakiwa kutumika kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe nyumbani na kuandaa makabidhiano,” alisema.
Alisisitiza kuwa Serikali ilikuwa na wajibu wa kuwarejesha makwao wajumbe wa tume hiyo, hata kama muda wa kisheria wa kufanya kazi ulikuwa umepita.
“Niliwasilisha Rasimu Machi 18, 2014. Tume imevunjwa Machi 19, 2014 wakati wajumbe wako Dodoma. Pamoja na lugha ya kejeli iliyotumiwa na Serikali na kuniita mnafiki, busara ya kawaida ingeonyesha umuhimu wa Serikali kujipa muda wa kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe nyumbani,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Hata kama sheria ilitaja muda wa kuvunja Tume bado ilikuwa ni wajibu Serikali kufanya mipango ya safari ya wajumbe baada ya kumaliza kazi. Sheria haikuizuia Serikali kufanya hilo. Huo ni wajibu wa Serikali na utaratibu wa kawaida unaotumiwa na Serikali kwa tume zote inazoziunda. Inaonekana Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliwekewa utaratibu tofauti. Kulikoni?”.