Friday 31 May 2013

Mizengwe yaanza Wizara ya Nishati

BAADHI ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini wakishirikiana na wenzao ndani ya mashirika na taasisi tanzu za wizara hiyo, wamekuwa wakihujumu jitihada za sasa za kuirejesha wizara katika mstari, Raia Mwema limeambiwa.
Jitihada hizo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari serikalini, zimekuwa pia zikiwahusisha kwa karibu baadhi ya wenyeviti wa bodi za mashirika na taasisi hizo na watendaji wakuu wake ambao wanahisi ya kuwa, kwa mazingira mapya wizarani, ajira zao zinakaribia ukingoni kutokana na ama utendaji binafsi usiokidhi au kwa kushindwa kudhibiti uozo katika taasisi na mashirika yao.   
Habari zaidi zinasema sasa upo mtandao wa makundi hayo ulioungana kuendesha kampeni ya kuukataa uongozi wa wizara kwa madai kwamba umekuwa ukiendesha mambo kibabe japo wengi nje ya wizara hiyo wanauona uongozi huo kuwa uliodhamiria utendaji kazi kwa viwango vya juu, urejeshaji imani ya umma kwa vyombo vya utoaji huduma na udhibiti mali na mapato ambao ulikwishakukosekana, na ambao ndio uliokuwa ugonjwa mkubwa ndani ya wizara na katika mashirika na taasisi  zake.
Raia Mwema limedokezwa pia kwamba nje ya wizara, taasisi na mashirika yake, mtandao huo unaungwa mkono na baadhi ya wabunge, wengine wakiwa katika kamati zinazohusiana na wizara hiyo, na kwamba mipango inayosukwa ili kupeleka ujumbe kwa mamlaka husika kuwa uongozi wa wizara haufai, uondolewe, ni pamoja na kukwamisha bajeti ya wizara itakayowasilishwa bungeni kiasi cha wiki mbili kuanzia sasa.
Hoja nyingine zanazodaiwa kushadidiwa na mtandao huo kama sababu za ziada kutaka mabadiliko ya uongozi wizarani ni kuwa Waziri mpya, Profesa Sospeter Muhongo, si mwanasiasa, ubunge wake uliompa uwaziri umetokana na yeye kuteuliwa na hilo linawakera baadhi ya wabunge wa majimbo ambao wanaona si vyema wao kuachwa, mtu wa “kuja” akapewa nafasi hiyo kubwa tena katika wizara inayotajwa kuwa tajiri na yenye ulaji kama ya Nishati na Madini.
Ukiacha hilo, Raia Mwema limeambiwa pia ya kuwa  madai mengine ni suala ambalo chimbuko lake ni ukabila. Waziri Profesa Muhongo anatoka Mkoa wa Mara ambako ndiko anakotoka pia Katibu Mkuu, Eliachim Maswi, ingawa inafahamika kwamba wanatoka katika maeneo mawili tofauti ya mkoa huo. Kwa mujibu wa madai ya wana mtandao huo, Profesa Muhongo na Maswi kuwa wanatoka katika Mkoa mmoja na sasa wanafanya kazi ofisi moja ni tatizo.
Maswi mwenyewe alipoulizwa na Raia Mwema juu ya madai hayo, mwanzoni mwa wiki hii, alisema hana namna ya kuzuia watu wasizungumze wanayoyataka. Alisema yawepo au yasiwepo, yeye na timu wanayoijenga wizarani wameamua kufanya kazi ili kuleta tija katika maeneo waliyokabidhiwa kuyasimamia.
“ Rais Jakaya Kikwete aliyetuteua hakufanya hivyo ili tuje hapa tuchezecheze. Tumepewa majukumu ya kutekeleza. Hebu niambie, nyumbani kwako siku hizi umeme unakatika mara ngapi?
“Ukiona kuna mawazo kama hayo, ujue tunafanya kazi. Sisi hatutajali yanayosemwa, kipimo chetu ni kama umma unaridhika. Kama unaona baadhi ya kero zilizokuwapo, zilizokuwa ndani ya uwezo wetu, sasa zimepungua kwenye vitu kama umeme, na kama tumeanza kupata stahili yetu kwenye maeneo kama ya migodi ujue wizarani sasa kuna wachapakazi,” alisema Maswi.
Katibu Mkuu Maswi aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Kaimu Katibu Mkuu katikati ya Julai mwaka jana, kiasi cha mwaka mmoja uliopita, akichukua nafasi iliyokuwa imeachwa na David Jairo aliyekuwa ametuhumiwa na Bunge, pamoja na mambo mengine, kwa ubadhirifu.
Aidha, Profesa Muhongo, mmoja wa Watanzania wachache wataalamu wa jiolojia,  amejiunga serikalini mwanzoni mwa Mei, mwaka huu, baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete kwanza kama mbunge kupitia nafasi 10 za Rais kuteua wabunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ni Shirika la Umeme (TANESCO) ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Jenerali mstaafu na mkuu wa zamani wa Majeshi, Robert Mbona, Mtendaji wake Mkuu ni Mhandisi Godfrey Mhando.
Mengine ni EWURA ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Simon Sayore; huku Mtendaji Mkuu akiwa Haruna Masebu; Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Balozi Ami Mpungwe na Mtendaji Mkuu ni Dk.  Dk Lutengano Mwakahesya; Wakala wa Madini (TMAA)  ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Dk. Yamungu Kayandabila, Mtendaji Mkuu akiwa Mhandisi Paul Masanja.
Mengine ni  STAMICO ambalo Mwenyekiti wa Bodi ni Ramadhani Omari Hatibu, Mtendaji Mkuu akiwa Grey Mwakalukwa; GST lililo chini ya Uenyekiti wa Bodi wa Profesa Idrissa Kikula na Mendaji Mkuu akiwa Prof Abdul Mruma  na TPDC ambalo Mwenyekiti wake ni Michael Mwanda na Mtendaji Mkuu  ni Yona Kilagane.
Kwa karibu mwaka mmoja sasa huduma kama ya umeme imekuwa ikitengemaa baada ya nchi kuwa imeingia katika mgao miaka iliyopita hali iliyoilazimisha Serikali kuanza kutegemea umeme wa kuuziwa na mashirika binafsi ambayo yalichipuka kufuatia mgao huo, mengi yakivuna mapesa mengi katika biashara hiyo na moja kati hayo likizua kashfa ambayo ilimlazimisha aliyekuwa waziri mkuu wa miaka ya mwanzo ya awamu ya Rais Kikwete, Edward Lowassa, kujiuzulu katika kile kilichojulikana kama kashfa ya Richmond.
Ulaji mwingine ambao Katibu Mkuu kwa kushirikiana na viongozi wenzake wameudhibiti ni ule uliokuwa ukifanyika katika sekta ya madini nchini.
Ulaji huo ulikuwa ukizihusisha kampuni tatu za uchimbaji madini nchini ambazo sasa zimetakiwa kulipa malimbikizo ya kodi ambazo awali hazikuwa zikilipwa.
Kampuni hizo ni Tanzanite One inayoendesha uchimbaji wa madini ya vito aina ya tanzanite, Mererani mkoani Arusha, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) na Kampuni ya Resolute (Resolute Mining Tanzania Ltd).
Kampuni hizo zimetakiwa na uongozi wa sasa wa Wizara ya Nishati na Madini kulipa zaidi ya dola za Marekani milioni 5.2 (zaidi ya Sh bilioni nane). Bado haijulikani “uvumilivu” wa awali miongoni mwa waliokuwa viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini uliofanya kampuni hizo kutolipa kodi hiyo ulikuwa unatokana na nini hasa.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Raia Mwema inazo, kampuni hizo zinakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kulipa kodi hizo, shinikizo linaloambatana na dalili za kuwekewa vikwazo.
Kati ya vikwazo vinavyoambana na shinikizo la kuzitaka kampuni hizo kulipa fedha hizo ni pamoja na Kampuni ya Tanzanite One kuwa katika hatari ya kupewa leseni baada ya leseni yake ya sasa kwisha muda wake.
Lakini wakati Tanzanite One wakikabiliwa na shinikizo la namna hiyo, kampuni za uchimbaji dhahabu za GGML na Resolute zinaweza kunyimwa leseni za kusafirisha madini nje ya nchi.

Piga vita tumbaku: zuia matangazo,uhamasishaji na udhamini wake

Mei 31, kila mwaka, yaani leo… ni siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani. Shirika la Afya Duniani(WHO) na washirika wake wameitenga siku hii kuwa ni maalum kwa ajili ya kupiga vita matumizi ya sigara inayotengenezwa kwa tumbaku.
Katika siku hii elimu hutolewa kuhusu athari za kiafya zitokanazo na tumbaku na pia  kuwakilisha sera bora za namna ya kupunguza utumiaji wa tumbaku.
WHO linasema tumbaku inaua takribani watu milioni 6 kila mwaka na kati ya hao 600,000 sio wavutaji wa tumbaku. Mwaka huu ikiwa na kauli mbiu “fungia matangazo yanayotangaza, uhamasishaji na udhamini wa tumbaku.
Tumbaku ni hatari kwa afya na huleta madhara makubwa  katika maeneo mbalimbali ya mwili kama vile moyo,ini na  mapafu.
Uvutaji wa tumbaku unakuweka katika hatari ya kupata shambulizi la moyo, kiharusi,kikohozi sugu,mikwamo katika mirija ya kupitishia hewa,kuharibika tishu za mapafu, saratani hasa ya mapafu,koo na mdomo,pia madhara ya mishipa ya damu kuifanya kunyauka na kuwa myembamba hivyo kusababisha shinikizo la damu.
 Matumizi ya kilevi hiki ni hatari kwa mvutaji na yule aliye karibu na mvutaji. Madhara ya kiafya ni yaleyale, tofauti ni ndogo kuwa muathirika sana ni yule anaevuta. Kwa sababu hii, nchi mbalimbali duniani  zimepiga marafuku matumizi ya tumbaku katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu; kama vile ndani ya vyombo vya usafiri,maeneo ya starehe na mikutano.
Je unayafamu Madhara ya tumbaku?
Utumiaji tumbaku huleta madhara kwa mwanamke kama vile ugumba, kijifungua kabla ya wakati, mimba kutoka na kuharibika, mtoto kufia tumboni, kuzaliwa na uzito mdogo.
 Moyo na ubongo
Utumiaji wa tumbaku husababisha mishipa ya damu kusinyaa/kuwa myembamba na kukamaa kwa mishipa ya damu inayopeleka damu katika misuli ya moyo, kuchochea mapigo ya moyo kwenda mbio na kuongezeka kwa lehemu (cholesteral). Matokeo ya haya ni kuharibika tishu za moyo,shambulizi la moyo, shinikizo la damu, ugonjwa wa kiharusi,ugonjwa wa kusahau kwa wavutaji wa umri mkubwa, upungufu wa uwezo wa kiakili, kushindwa kutambua na kupoteza kumbukumbu.
Mapafu
Kuharibika kwa tishu za mapafu na mirija ya hewa,madhahara yake ni Kikohozi sugu, mikwamo katika njia ya hewa,kushindwa kupumua vizuri, kupata maambukizi ya mara kwa mara ya vimelea vinavyoshambulia mfumo wa upumuaji na Saratani ya mapafu.

Taarifa za kitafiti kuhusu utumiaji tumbaku
Wataalamu wa saratani wanaeleza katika tafiti mbalimbali kuwa asilimia 30% za saratani zote hutokana na utumiaji tumbaki peke yake.Huku saratani ya mapafu ikiongezeka idadi kwa kina mama na kua….hii ni kutokana na taarifa ya utafiti uliofanyika nchini Uingereza,hii inatokana na wanawake wanaotumia tumbaku.Inakadiriwa kuwa 17.2% ya wanaume watumia tumbaku wako katika hatari yakupata saratani ya mapafu huku wanawake wakiwa ni 11.6%.
Tumbaki inasababisha vifo vya mapema ambavyo vinazuilika kama watu wasingeitumia,tafiti zinaonyesha kuharibika na kutoka kwa mimba kwa watumiaji tumbaku,pia watoto huzaliwa na uzito mdogo na pia kuzaliwa kabla ya mda kufika(njiti),Napia kuna hatari kwa zaidi ya 1.4 mpaka 3 yakupata vifo vya ghafla kwa mtoto aliye tumboni.
Tatafiti iliyofanyika kwa watoto wa panya wataalam wamegundua tumbaku  hupunguza uwezo wa ubongo wa mtoto kutambua hali ya hewa kua ndogo hivyo mtoto hupata jeraha la ubongo wakati wakuzaliwa. Uhanithi umeonekana kwa asilimia 85%  kwa watumiaj wa tumbaku ukilinganisha na wasiotumia, tumbaku ni moja ya kisababishi cha upungufu wa nguvu za kiume.
Tafiti nyingine ambayo ilichapishwa katika bbc health news ilisema kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa saratani ya mapafu kwa upande wakina mama imeongezeka nakukaribia ya wanaume ukilinganisha na miaka ya nyuma hii imetokana na tabia mpya yakina mama kujiingiza katika utumiaji na uvutaji tumbaku
Tafiti nyingine ambayo ilifanyika nchini uingereza ilihusisha madaktari wakiume 34,486 nusu yao walikufa mapema kutoka na uvutaji sigara,wavutaji wako katika hatari ya kufa mapema kabla ya kufika umri wa miaka 60-70 mara 3 zaidi ukilinaganisha na wasiovuta.
Kwa nini tumbaki ni hatari kwa afya ya mwili?
 Tumbaku ina takribani kemikali 19 ambazo ni visababishi vya saratani,,na matokeo yake hujitokeza hata baadae maishani zaid ya maika 20
Tumbaku imebeba kemikali ambayo ni moja ya kisababishi cha saratani mwili, inaitwa pyrolitic,husababisha vitu vilivyomo ndani ya chembe hai kuvurugika, kitaalam genetic mutation. Mvurugiko huu ndio baadaye huleta saratani,pia tumbaku ina kemikali iitwayo nikotini ambayo husababisha uteja (addiction), husababisha mtu kuwa na utegemezi(dependency) wa kimwili na kiakili(saikologia) kwa tumbaku, hivyo mtu hushindwa kustahimili kutoikosa tumbaki na mtu huridhika pale anapoipata
Namna yakuacha na kijikinga na utumiaji tumbaku.
Zipo zaidi ya mbinu ishirini za namna yakuacha utumiaji tumbaku,kwanza unatakiwa kujichelewesha zaidi ya dakika kumi pale unapopata hamu yakuvuta tumbaku halafu fanya jambo lingine lolote ili kupoteza wazo la hamu ya uvutaji. Fanya hivi kwa mara nyingi zaidi. Jaribu kukwepa na kuvitambua vitu vinavyokushawishi kuvuta sigara kama vile kunywa pombe, kusikiliza mziki au kampani ya marifiki wanaovuta tumbaku.Mazoezi ya viungo vya mwili yanasaidia sana kupoteza wazo la kutamani tumbaku, kufanya mazoezi kwa dakika 30 kila siku inasaidia, pia unapokuwepo mahali km ofisini jaribu kunyoosha miguu, mikono, shingo mgongo, au hata kupiga ‘pushup’,pia kusali kufanya kazi ndogondogo km kufuma.

Utafiti; Big G inaongeza usikivu, kumbukumbu

Utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa utafunaji wa Big G zisizo na sukari unasaidia kuongeza usikivu na kumbukumbu, kunakosababishwa na urahisishaji wa mtiririko wa damu kuelekea kwenye ubongo.
Pengine mzazi wako, mwalimu amewahi kukukataza kutumia, kununua kitu hiki, lakini imebainika Big G inaongeza kumbukumbu usikivu makini na uchangamfu, kuimarisha afya ya kinywa.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa utafunaji wa Big G zisizo na sukari unasaidia kuongeza usikivu na kumbukumbu, kunakosababishwa na urahisishaji wa mtiririko wa damu kuelekea kwenye ubongo.
Utafiti huo uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Cardiff nchini Uingereza na kuchapishwa mwezi uliopita, ulihusisha kikundi cha watu  ambao walitafuna Big G na wengine wasiotafuna kwa kuwapa zoezi la kuweka kumbukumbu katika sauti kwa muda wa nusu saa.
Zoezi hilo lilikuwa ni la kusikiliza sauti ya orodha ya namba na kuzitaja kwa mfululizo.
Big G inatoa majibu sahihi
Waliotafuna Big G walitoa majibu sahihi tena kwa haraka zaidi tofauti na wenzao ambao hawakutafuna Big G.
Tafiti zilizotangulia zilionyesha kwamba utafunaji wa Big-G una faida nyingi mwilini na Dk Chris Miles aliongoza utafiti huo uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Cardiff.
 “ Kutafuna Big-G kunawafanya watu wawe katika tahadhari zaidi.
“Kuna ushahidi wa kutosha kuwa kitendo hicho kinasaidia kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa damu safi kwenda kwenye ubongo,” anasema daktari huyo.
Lakini kama utawaambia watu watafune bila kuwapo kwa Big G, hutapata matokeo yanayofanana. Hivyo inaonekana kuwa, unahitaji kuwa na Big G ili kurahisisha utafunaji wako.
Madereva wa magari makubwa ya mizigo watakuwa wamepata habari njema, kwani ikiwa kutafuna Big-G kunaongeza tahadhari ni wazi kuwa inaweza kuwasaidia kuwa makini zaidi wawapo barabarani hususani wakati wa usiku.
Hili halijajulikana bado, licha ya ukweli kuwa athari za utafunaji huo hutegemea na aina ya Big-G yenyewe.

Dk Miles anasema watu wengi hutafuna Big-G kwa lengo la kupata harufu nzuri kinywani na sio kwa madhumuni ya kuongeza usikivu ama tahadhari.
Utafiti uliofanywa na  mchambuzi wa masuala ya masoko anayefahamika kama Mintel, unaonyesha kwamba asilimia  92 ya watumiaji wa Big-G wanafanya hivyo wakiwa na lengo la kutengeneza harufu nzuri vinywani.
Wengu wanaofanya hivyo wanajiongezea hali ya tahadhari bila ya wao kufahamu.  Zipo faida nyingi za kiafya zinazotokana na utafunaji wa Big-G.
Mapitio mengine yaliyofanywa na watalaam kutoka katika Chuo Kikuu hicho cha Cardiff mwaka 2011, yalitoa ushahidi kuwa utafunaji wa Big-G unasaidia sana katika kupunguza msongo wa mawazo.
Utafiti wa Cardiff haukuangalia athari zinazosababishwa na utafunaji wa Big-G kiafya, lakini utafiti wa Mintel uliofanyika Disemba mwaka jana ulionyesha kuwa ni watu sita kati ya kumi wanaotafuna Big-G huamini kuwa zinaweza kuwasaidia kuboresha meno yao.
Ukweli ni kwamba watu hao wako sahihi, hiyo ni kwa mujibu wa Dk Nigel Carter, Mkuu Taasisi ya Dental Health Foundation ya nchini Uingereza.
Pamoja na mapitio yaliyobainishwa na Jarida la British Jounal la Uingereza mwaka 2011, kuna athari iliyojificha katika bidhaa zenye sukari inayokinzana na zile zisizo na sukari.
Kwa kawaida Big –G zenye sukari zinaongeza ‘asidi’ mdomoni inayoweza kuharibu meno kwa kuathiri mizizi yake.
“Hii ni hatari, nafikiri ulaji wa aina hizo za Big-G ni hatari sana kwa afya ya meno yao,” anasema Carter.
Kuna kiwango kidogo sana cha Big-G zisizo na sukari zenye ladha inayoweza kuzalisha ‘asidi’ mdomoni. Kama athari zipo ni kwa kiwango kidogo sana.
Kama ‘asidi’ hiyo itazalishwa kwa kiasi kidogo sana nadhani itakuwa ni rahisi kupotea tofauti na zile za kawaida zilizoongezewa sukari.
Athari kubwa ya kutafuna Big-G, ni kusaidia kuongeza mate mdomoni anasema Dk Carter.
Mate yanasaidia utaratibu wa kinga asilia unaojumuisha chumvi iliyomo ndani yake kwa kuongeza ama kupunguza madini kwenye meno ambayo yanasababishwa na vyakula vyenye asidi inayotokana na sukari.
Kadri jinsi chumvi inavyokuwa nyingi kwenye mate, ndivyo utaratibu huo unavyokuwa rahisi zaidi.
Big G inalinda meno
Dk Carter anabainisha kwamba  kwenye Big-G zenye sukari, sukari inachanganywa haraka na mate hayo na kuondoa na uharibifu wa meno.
 Pamoja na yote hayo  BDHF inasisitiza matumizi ya Big-G zisizo na sukari kwamba zina faida zaidi.
Utumiaji wa vyakula visivyo na sukari ni muhimu sana katika kulinda fizi.  Je, matumizi hayo yanahesabiwa kama kitendo chanya kwa afya ya fizi na kinywa kwa ujumla?
“Ni kweli kabisa”.  Hivyo ni vizuri kutosafisha meno baada ya kula na badala watu wanapaswa  kutafuna Big G kwa muda wa dakika 10 hadi 20. Hii itasaidia kuongeza mate mdomoni na pia kuboresha meno yako kwa kuyaondoa katika hatari ya kuoza, anahitimisha Daktari huyo.

Wenye divisheni ziro 30,000 wapeta





Dar es Salaam. Wanafunzi 30,063 waliopata daraja sifuri katika matokeo yaliyopita, wameula baada ya kupandishwa hadi daraja la nne kutokana na ukokotoaji upya wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) na kutangazwa jana.
Marekebisho hayo yalifanyika baada ya kufutwa kwa matokeo ya awali yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu.
Kufutwa kwa matokeo hayo, ilikuwa ni utekelezaji wa sehemu ya mapendekezo ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, baada ya wanafunzi 240,909 kupata daraja sifuri kwenye matokeo yaliyotangazwa mara ya kwanza.
Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema sasa watakaokuwa na sifuri ni 210,846 sawa na asilimia 56.92 wakati wavulana wakiwa ni 104,259 na wasichana 106,587.
Hiyo ina maana kuwa sasa ufaulu umepanda na kuwa asilimia 43.08 badala ya ule wa kwanza ambao ulikuwa asilimia 34.5.
Dk Kawambwa alisema kutokana na ukokotoaji mpya wa matokeo ya sasa, idadi ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo kwa daraja la kwanza mpaka la nne imeongezeka na kufikia wanafunzi 159,747 kutoka 126,847.
Wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 3,242 wavulana wakiwa ni 2,179 na wasichana 1,063 ikiwa ni asilimia 0.88 ya matokeo yote, daraja la pili ni 10,355 sawa na asilimia 2.8 wavulana wakiwa 7,267 na wasichana 3,088.
Waliopata daraja la tatu ni 21,752 sawa na asilimia 5.87 wavulana wakiwa 14,979 na wasichana 6,773, daraja la nne ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 .
Tofauti na matokeo yaliyofutwa, ambayo watahiniwa waliopata daraja la kwanza walikuwa ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1997.
Waliopata daraja la tatu walikuwa 15,426, wavulana 10,813 na wasichana 4,613, waliopata daraja la nne 103,327, wavulana 64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903, wavulana 120,664 na wasichana 120,239.
Dk Kawambwa alieleza watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 480,029 na waliofanya ni 458,139 sawa na asilimia 95.44.
Alisema kuwa watahiniwa wa shule waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 411,225 na waliofanya ni 397,138 sawa na asilimia 96.57 huku wa kujitegemea wakiwa ni 68,804 na waliofanya ni 61,001.
Agizo la serikali
Dk Kawambwa alisema kuwa matokeo hayo yamefanyiwa kazi kwa kutumia mfumo wa `Fixed Grade Ranges’(ukokotoaji matokeo usiobadilika) badala ya ule wa zamani wa `Flexible Grade Ranges’ (ukokotoaji matokeo unaoweza kubadilika).
Mei 3, mwaka huu, Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta matokeo hayo na kusema kuwa yatatayarishwa kwa mfumo wa zamani wa `Flexible Grade Ranges’.
Lukuvi alisema kuwa, mapendekezo hayo yalitolewa na Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza na matokeo hayo na mapendekezo hayo yaliridhiwa na Baraza la Mawaziri.
Dk Kawambwa jana alisema kuwa, mfumo wa Fixed Grade Ranges ndiyo uliotumika na kuwa kuanzia sasa mitihani yote itakuwa ikitumia mfumo huo.
Alisema kuwa pendekezo la Serikali lilishindikana kutumika kwani isingewezekana kuchanganya mifumo miwili kwa wakati mmoja.
“Ni kweli kuwa Serikali iliagiza matokeo haya yachakatwe kwa mfumo wa 2011 ambao ulikuwa ni `Flexible Grade Ranges’, kitaalamu siyo sahihi kutumia mifumo miwili kwa wakati mmoja, kwa kuwa haya matokeo ya 2012 yalitumia mfumo wa `Fixed Grade Ranges’, isingewezekana kuubadili.
“Kwa hiyo tulishauriana serikalini tukakubali kufanya `standardisation’ (ukokotoaji) kwa mfumo wa `Fixed Grade Ranges’ kwani kama tungetumia mfumo wa zamani wa `Flexible Grade Ranges’ lazima yangetokea matatizo,” alisema.
Shule bora na za mwisho
Katika shule kumi bora, Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Kifungilo iliyoko Tanga imetolewa katika kundi hilo kwenye matokeo mapya na nafasi yake kuchukuliwa na Shule ya Wasichana ya Feza ya Dar es Salaam.
Baada ya ukokotoaji mpya bado St.Francis Girls ya Mbeya imebeki kwenye nafasi ya kwanza ikifuatiwa Marian Boys ya Pwani, Feza Boys ya Dar es Salaam, Marian Girls ya Pwani, Canossa ya Dar es Salaam, Rosmini ya Tanga, Anwarite Girls ya Kilimanjaro, St. Mary’s Mazinde Juu ya Tanga na Jude Moshono ya Arusha.

Shule 10 za Mwisho
Shule za Ungulu Morogoro, Mkumba na Tongoni za Tanga na Ndame ya Unguja zimetoka katika kundi hilo la shule za mwisho
Shule za mwisho katika matokeo haya zimeongozwa na Mibuyuni ya Lindi, Namndimkongo ya Pwani, Chitekete ya Mtwara, Kikale ya Pwani, Zirai ya Tanga, Matanda ya Lindi, Kwamndolwa Tanga, Chuno ya Mtwara, Maendeleo ya Pwani na Maendeleo ya Dar es Salaam.

Monday 20 May 2013

JK: mnaotaka Urais anzeni kupitapita

*Awataka wafanye mchakato wao bila kuvuruga chama
*Awashushua wanaokacha majimbo na kuwanunia wenzao
*Wabunge wamtaka awang’oe mawaziri watatu ‘mizigo’

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amefungua milango kwa kuwataka baadhi ya watu ndani ya chama hicho wanaowania urais mwaka 2015 kuendelea na mchakato huo.

Rais Kikwete amewatahadharisha watu hao kuendesha kampeni zao kwa ustaarabu pasipo kuibua chuki wala kujenga makundi ambayo alisema ni hatari kwa kuwa yanaweza kukipasua chama. Rais Kikwete aliyasema hayo katika mkutano ndani wa wabunge wa chama hicho uliofanyika jana katika ukumbi wa CCM (white house) mkoani hapa.

Mkutano huo ambao ulianza saa 3.00 asubuhi ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya taifa ikiwamo utekelezaki wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho katika majimbo na ahadi mbalimbali za viongozi wa taifa.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya ukumbi huo kilieleza kuwa Rais Kikwete aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea urais kuwa na tahadhari na watu aliowaita vishoka wa siasa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Rais Kikwete alisema watu wa aina hiyo wana tabia ya kula huku na huku kwa kujiingiza katika kambi zaidi ya moja.

“Tuangalie makundi ya urais 2015 yasishambuliane kwa kuvunja chama, wenye nia hiyo ya kugombea waendelee na mikakati yao kujenga chuki kwa makundi mengine.

“Katika hatua hiyo, pia mkumbuke kuwa katika kambi hizo za urais zinatakiwa kujitizama wao na wafuasi wao maana wafuasi wengine hawaaminiki, ” alisema Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, miongoni mwa ajenda alizokuwa nazo Rais Kikwete ni pamoja na suala la urais na utendaji wa wabunge majimboni.

Rais Kikwete aliwataka wabunge wa chama hicho kubadili mwenendo wa kuyatelekeza majimbo yao na badala yake akawahimiza kujenga tabia ya kutembelea majimbo yao mara kwa mara.

“Hili JK amelisemea kwa ukali kwamba tabia ya baadhi ya wabunge kuhamia mijini na kutelekeza majimbo yao ni hatari kwani mwisho wa siku wananchi watawanyima kura na kuzipeleka upinzani.

“Pia alikemea tabia ya baadhi ya wabunge kununa na kuwachukia watu wengine wenye nia ya kugombea katika majimbo yao. Akasema mbunge asiyetimiza wajibu wake kwa wananchi wake na bungeni ni vigumu kubaki.

“Wanatakiwa kurudi majimboni kwao kusimamia ilani ya chama pamoja na ahadi zao walizoahidi na zile za viongozi wa chama na Serikali ikiwamo ahadi zake kama rais,” alisema.

Kuhusu suala la ukosoaji, Rais Kikwete alisema wabunge wa chama hicho wana wajibu wa kuikosoa Serikali yao lakini akaonya aina ya ukosoaji wenye lengo la kuibomoa Serikali.

“Mnatakiwa kuisimamia Serikali na kuikosoa bila kuibomoa, lakini kuna baadhi yenu mmekuwa mkiibomoa Serikali kwa jinsi mnavyochangia huko bungeni… hilo si jambo jema hata kidogo, waachieni wale wenzetu,”alisema Kikwete.

Chanzo hicho kilieleza kuwa wabunge wamekuwa hawaridhishwi na utendaji wa baadhi ya mawaziri ambao walisema ni mizigo na kutaka waondolewe katika nafasi zao.

Chanzo hicho kilitaja majina ya mawaziri hao wanaodaiwa kuwa ni mizigo kuwa ni Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. David David Mathayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenera Mkangara.

Baadhi ya wabunge walimtaka Rais Kikwete kudhibiti ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri mbalimbali nchini, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.

“Rais anatakiwa kukunjua makucha yake kuondokana na uozo huu katika halmashauri zetu. Haiwezekani waendelee kunyamaziwa, tunatakiwa kuimarisha chama kwa kuangalia namna Serikali inavyoweza kutimiza ahadi kwa wananchi,” kilisema.

Kiliendelea kusema. “Serikali iweze kusaidia katika kutimiza ahadi kwa kutelekeza ilani ya chama, viongozi wa vijiji, kata na vitongoji kuanza kulipwa mshahara maana wamejitolea kwa muda mrefu hivyo huwalazimu kupata ushawishi kutokana na njaa,” kilisema.

Imeelezwa kuwa katika kikao hicho kinachoendelea kitakuwa na ajenda nyingi ambazo zitaibuliwa na wabunge.

Hizo ni pamoja na maslahi ya wabunge, utendaji kwa baadi ya mawaziri na aina ya ukosoaji inayofanywa na baadhi ya wabunge wa chama hicho.

Baada ya mapumziko ya mchana, kikao hicho kiliendelea kwa wabunge kupata nafasi ya kujadili hoja mbalimbali kutokana na hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa asubuhi.

Rais Kikwete anakutana na wabunge hao wakati wenyewe wanaonekana kugawanyika kutokana na kuwapo kundi la wabunge wanaoitetea Serikali na wengine wanaoikosoa.

Miongoni mwa wabunge wanaoikosoa Serikali ya chama hicho waziwazi ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy.

Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa wabunge hao machachari walichanwa hadharani na baadhi ya wabunge wanaoiunga mkono Serikali hali inayoonyesha kuwa wabunge hao si wamoja.

Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisimama na kueleza kuwa anashangazwa na aina ya ukosoaji unaofanywa na wabunge hao na kusema. “Kama hawataki kufuata maelekezo ya chama wahame,” alisema.

Matajiri watumia nyaraka feki ujenzi wa maghorofa

WATU wanaodaiwa ni matajiri wakubwa, wameendelea kulisumbua Jiji la Dar es Salaam kwa kupuuza na kukiuka sheria zilizopo, huku wakiendesha shughuli za ujenzi wa maghorofa kwa kutumia uwezo wa fedha zao. Pia matajiri hao wamedaiwa kuwasilisha taarifa za uongo Halmashauri ya Jiji wakiomba kupewa kibali cha ujenzi wa nyumba ya kaiwada, lakini baada ya kupatiwa hujenga jengo la ghorofa kuanzia tano hadi kumi.
Hata hivyo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imegundua taarifa za uongo juu ya ujenzi wa majengo pacha makubwa ya biashara yanayojengwa eneo la Manispaa ya Kinondoni kitalu namba 288 barabara ya Toure Drive Msasani.

Kitendo hicho kiliwafanya wananchi wa eneo hilo kupatwa na hofu juu ya usalama wao na kuiomba Serikali kupitia idara zinazohusika kuchukua hatua.

Kutokana na hali hiyo Manispaa ya Kinondoni, imelazimika kuzuia ujenzi wa majengo hayo pacha tangu Aprili 19, mwaka huu wakati yakiwa hatua ya mwanzo kwa sababu ya kuwa na wasiwasi na mkataba.

Kwa mujibu wa barua ya zuio ya halmashauri ya Kinondoni yenye kumbukumbu KMC/MEK/V22/24 kwenda kwa mmiliki wa majengo hayo, aliyetajwa kwa jina la Silverstone Properties, ilimtaka kusimama ujenzi huo.

Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Godfrey Mgomi ilifafanua kwamba mkataba huo hauonyeshi idadi halisi ya ghorofa zinazojengwa kwa majengo hayo.

Ilifafanua kuwa, mkataba wake huo hauna taarifa muhimu zinazoendana na ujenzi wa maghorofa jijini Dar es Salaam, jambo ambalo linatia wasiwasi wa ubora wa majengo na usalama wa watu.

Halmashauri hiyo ilitoa onyo kwa mmiliki wa majengo hayo kwa kumtaka atii amri hiyo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

MTANZANIA ilifika ofisini kwa Mhandisi Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Gerald Urio kujua sababu ya ujenzi huo kuendelea licha ya kuwapo na zuio.

Mhandisi Urio alikiri halmashauri hiyo kuzuia jengo hilo, kutokana na sababu mbalimbali huku akishangaa ujenzi wa jengo hilo kuendelea na kufikia ghorofa mbili.

“Ni kweli tulisimamisha ujenzi wa majengo hayo na hadi sasa ninapozungumza na wewe sijapata taarifa zozote kama yameruhusiwa kuendelea kujengwa,” alisema.

Gari la polisi lakamatwa na bangi

GARI la polisi wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha pamoja na askari polisi, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kukutwa wakisafirisha magunia 18 ya bangi. Polisi hao wakiwa na gari hilo, walikamatwa juzi katika maeneo ya Kilema Pofu, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani hapa. Askari hao walikamatwa Mei 18 mwaka huu na katika kusafirisha bangi hiyo, walikuwa wakishirikiana na mfanyabiashara mmoja aliyejulikana kwa jina la Livingstone Urassa (35).
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema askari hao walikamatwa kutokana na mtego uliokuwa umewekwa na askari polisi mkoani Kilimanjaro, baada ya kupata taarifa kuwa kuna mfanyabiashara anasafirisha bangi kwa kutumia gari ambayo haisimamishwi njiani.

Kamanda Boaz alisema kwamba, baada ya kuwakamata askari hao, walikwenda hadi nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kukuta magunia mengine 16 yakiwa yamefichwa kwenye migomba.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz gari hilo la polisi lilikuwa likiendeshwa na mmoja wa askari hao, ambaye ni koplo Edward na Pc George na kwamba namba za gari hazijafahamika.

Hata hivyo, taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema gari hilo la polisi linashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro.

Juu ya mishahara minono na posho kila siku bado na maziko tena??

Ni zilizotangazwa kutengwa kupitia Hotuba ya  Waziri Mkuu.
Dodoma. Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imelaumiwa kwa kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya maziko ya viongozi huku Watanzania wengi wakilia na umaskini mkubwa.
Shutuma hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki bungeni kwa nyakati tofauti wabunge akiwamo wa  Viti Maalumu Lucy Owenya (Chadema) na Kangi Lugola (Mwibara-CCM) wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya bajeti katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Katika mchango wake Owenya alisema inatia aibu kuona kiasi kikubwa cha fedha kikitengwa kwa ajili ya maandalizi ya kuzika viongozi huku mambo muhimu na ambayo ni kipaumbele yakiachwa.
“Ni aibu na fedheha kubwa, hivi mmetenga kiasi hicho kwani mnajua nani atakufa na lini atakufa ndio maana mnajiandaa kumzika,” alihoji Owenya.
Mbunge huyo alikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa Serikali imeshindwa kufikiri na hasa namna ya kuwaondolea umasikini na tabu wanazopata wananchi wake lakini inawaza habari za watu wanaojiandaa kufa.
Vile vile katika mchango wake Lugola ambaye alisema asingeunga mkono hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alihoji sababu za kutengwa kwa fedha hizo bila kujua nani atakufa lini.
Mbali na hilo, Owenya pia aliilaumu Ofisi ya Waziri kwa kushindwa kutumia mbinu mbadala za kuzuia matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi zinazotumiwa na wakuu wa mikoa kwa ajili ya kwenda Dodoma kufuatilia hotuba ya Waziri Mkuu.
Alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwatimua wakuu wa mikoa ili warudi mikoani kwao ili kuokoa fedha za walipa kodi zinazoteketea katika misafara yao mjini Dodoma.

Vurugu kubwa Iringa, Mchungaji Msigwa mbaroni

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa saa saba mchana kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na kwamba watu wapatao 50 walikuwa wamekamatwa katika fujo hizo zilizochukua karibu saa tatu.
Iringa. Mji wa Iringa uligeuka kuwa uwanja wa vita kati ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wafanyabiashara jana asubuhi. Watu 50 walikamatwa kutokana na tukio hilo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Katika vurugu hizo, gari la zimamoto lilivunjwa kioo na gari lingine dogo liliharibiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa saa saba mchana kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na kwamba watu wapatao 50 walikuwa wamekamatwa katika fujo hizo zilizochukua karibu saa tatu.
“Mchungaji Msigwa amekamatwa kwa makosa ya uchochezi, kufanya maandamano bila kibali na kuhamasisha watu kufanya biashara kwenye eneo ambalo limekatazwa kisheria.
Tumemkamata na hatutamwachia hadi uchunguzi wa suala hili utakapokamilika. Pia na hao watu wengine,” alisema Kamanda Kamhanda.
Alisema waliamua kufanya doria katika eneo hilo baada ya kupata taarifa za kiitelijensia kuwa wafanyabiashara walikuwa na mpango wa kuwashambulia mgambo wa Iringa kama wangekwenda kuwazuia.
Vurugu hizo zilichangiwa na mvutano uliokuwa unafukuta kwa muda mrefu kati ya Uongozi wa Manispaa na Mbunge huyo kuhusu amri ya kuzuia watu kufanya biashara kwenye Barabara ya Mashine Tatu, Iringa.
Uongozi wa Manispaa ya Iringa ulitoa tangazo Aprili 28, mwaka huu ukipiga marufuku kufanya biashara katika eneo hilo jambo ambalo lilipingwa na Mchungaji Msigwa na wafanyabiashara hao.
Alfajiri
FFU walianza kuimarisha ulinzi katika Barabara ya Mashine Tatu tangu alfajiri jana na wafanyabiashara hao walipofika kwenye eneo hilo walikuta limezingirwa na polisi.
Kusambaa kwa taarifa hizo kulimfikia Mchungaji Msigwa ambaye alifika hapo saa mbili asubuhi na kuanza kuzungumza na wafanyabiashara hao.
Watu walipomwona ndipo wakamzunguka na kuanza kuimba nyimbo za kumsifu na kumshangilia: “Rais wetu... Rais wetu... Rais wetu.”
Maofisa wa Polisi walimfuata Mchungaji Msigwa na kumwomba aondoke lakini aligoma akidai ni mwakilishi halali wa wananchi kwa hiyo hawezi kuondoka.
Badala yake alipanda kwenye gari lake na kuanza kuzunguka eneo hilo huku akifuatwa na umati wa watu. Polisi nao walikuwa wakimfuatilia kwa magari yao.
Baada ya idadi ya watu kuongezeka kwa wingi barabarani na kuanza kufanya kitu kama maandamano wakiwa nyuma ya gari ya Msigwa, polisi waliwataka kutawanyika lakini waligoma huku wakizidi kuimba nyimbo za kumsifia mbunge huyo.
Mabomu ya machozi
Ilipotimu saa tatu na nusu asubuhi, polisi walianza kutumia magari ya kumwaga maji ya kuwasha na kutumia mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia ovyo, huku wengine wakikusanya mbao, matairi na mawe na kuwasha moto ili kuwazuia polisi wasiwafikie.
Moto huo ulisababisha nyumba moja kuwaka moto ndipo gari la zimamoto lilipokwenda kuzima lakini nalo likashambuliwa.
Msigwa kukamatwa
Mchungaji Msigwa alikamatwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kabla ya kukamatwa, aliwaambia waandishi kuwa polisi walikuwa wanawaonea wafanyabiashara hao na kwamba manispaa haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuwazuia wafanyabiashara hao.
Mei 15 na 16, mwaka huu Msigwa alifanya mikutano ya hadhara kwenye Viwanja vya Mwembetogwa na Magorofani na kuwataka wafanyabiashara kutokuogopa kufanya shughuli zao kwenye eneo la Mashine Tatu.    

Ndoa za jinsia moja mpango wa shetani-Askofu Nzigilwa


 Waandamanaji nchini wanaopinga ndoa za jinsia moja na na haki ya kurithi watoto nchini ufaransa

SKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa amesema kuwa mpango wa ndoa za jinsia moja ulioruhusiwa na baadhi ya matifa duniani si mpango wa Mungu, bali ni wa shetani. Askofu Nzigilwa alibainisha hayo hivi karibuni alipokuwa akitoa mahubiri kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Maurus Kurasini jimboni humo, kwenye hafla iliyokwenda sambamba na kufungisha Ndoa takatifu kwa Waamini wa Parokia hiyo.
Askofu Nzigilwa alisema katika dunia ya sasa kumeibuka ndoa ambazo ziko kinyume na mpango wa Mungu kwa Wanadamu na hivyo nafasi ya mwanamke kuchukuliwa na mwanaume na nafasi ya mwanaume kuchukuliwa na mwanamke. “Sakramenti ya ndoa ina tabia moja ya mke na mume yaani mwanaume mmoja na mwanamke mmoja maana zipo ndoa za siku hizi ambazo mwanaume anachukua nafasi ya mwanamke halafu anaolewa na mwanaume mwenzake halafu mwanamke anachukua nafasi ya mwanaume halafu anamuoa mwanamke mwenzake hii ni kinyume kabisa na mpango wa Mungu kwa wanamdamu”,alisema Askofu Nzigilwa. Alisema ndoa ya Kisakramenti ya Kanisa Katoliki ni ya mume na mke wa jinsia tofauti ambayo hudumu daima haitenganishwi na kitu chochote mara baada ya kufungwa kihalali.
Aidha Askofu huyo, aliwaambia wanandoa hao kuwa wanaingia katika mpango wa Mungu ambao aliuratibu tangu mwanzo wa uumbaji na kuwataka iwe ya mume mmoja na mke mmoja. Askofu Nzigilwa alisema katika kitabu cha mwanzo sura ya pili inaeleza kwamba hapo mwanzo Mungu aliumba vitu ili Adamu avitawale na hiyo ilikuwa ishara ya mamlaka ya Adamu ya kuvipa hata majina ndiyo maana kuna alivyoviita mimea, samaki na wanyama kitendo ambacho kinaendelea hadi leo kwa wazazi kuwapa majina Watoto wao. Alisema pamoja na Adamu kupewa vitu hivyo vyote hakuwa na furaha hadi pale Mwenyezi Mungu alipompa mwenza Eva ambapo alikuwa na furaha na kusema kuwa huyo ndiye mnyama katika nyama na kila kitu katika maisha yake ambapo aliwataka wanandoa hao kuacha kuwakimbia wenzao kwa ajili ya mali.
“Katika ulimwengu huu wa leo tumekuwa tukishuhudia watu wakiwakimbia waume au wake zao ili waweze kumiliki mali jamani nguvu na furaha zenu mnazipoteza kwa sababu ya mali hakuna mwanaume aliyepewa mali hapa duniani kuliko Adamu lakini bado alionekana hana furaha hadi pale Mungu alipompatia mke:
Hebu muulizeni kwanza Adamu kwa nini hakuwa na furaha hadi alipopewa mwenza yaani Eva sasa nyinyi akina baba mkianza kuwakimbia wake zenu mkidhani mtapata furaha shauri zenu”,alisema Askofu Nzigilwa. Askofu Nzigilwa alisema furaha katika familia inakamilishwa kwa mume na mke kukaa pamoja na kutawala ulimwengu kwa kuwa huo ni mpango wa Mungu alipomuumba Eva na kumwambia Adamu kuwa huyo ndiye mke wake kwa kuwa angetaka ndoa ya mme mmoja na wanawake wengi angempatia adamu wake wengi na si Eva peke yake. Aliwataka wanandoa hao kila mmoja kuwa msaada kwa mwenzake katika safari ya kuelekea mbinguni huku wakizifanya familia zao kuwa Kanisa dogo la nyumbani kwa kuwalea katika imani na kwa njia ya sala kwa kuwa kanisa ni mahala ambapo Mungu anaabudiwa na kuheshimiwa na neema za zake zinapatikana mahala hapo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Waziri mkuu aliyehudhuria hafla hiyo ambaye ni Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji Dk.Mary Nagu alisema uaminifu na uadilifu kwa watu unatokana na uwepo wa Makanisa ambapo Viongozi wa dini wamekuwa wakitoa mafundisho mbalimbali ya kumcha Mungu. Alisema mauaji ya Vikongwe yanatokana na kutokuwepo kwa madhehebu ya dini sehemu wanazoishi na hivyo kukosa mafundisho ya dini kitendo kinachosababisha watu kukosa uadilifu. Alisema vitendo vya ongezeko la matukio ya wizi, ukahaba, uzinzi, rushwa, ufisadi, dawa za kulevya, uchochezi, udanganyifu, ulevi, uasherati na ulevi ni baadhi ya viashiria vya watu kupungukiwa na uchaji wa Mungu. Dk. Nagu alisema ili kuondokana na rushwa Waamini hawana budi kwenda katika nyumba za ibada kumuomba Mungu na kupata mafundisho stahiki husani kanisani kwa sababu Mungu huangalia wanaofanya vitendo hivyo viovu na kuwa wawapo Ofisini hujiona kuwa wapo salama kwa kutokukamatwa hasa pale ushahidi unapokosekana.
Kanisa la Mtakatifu Maurus lilijengwa mwaka 1894 na Padri Maurus Hagman na kuwekwa wakfu Februari 20, mwaka 1898 na hivyo kuwa makao makuu ya Vikariat ambapo mwaka 1965 ilifanywa kuwa kigango na mwaka 1970 ilifanywa kuwa Parokia. Mwaka 1988 ilikabidhiwa kwa Shirika la Wasalvatoriani na hivyo kufanya kuwa na Jumuiya ndogondogo 27 kitendo kilichoongeza Waamini na kusababisha kanisa kuwa dogo baada ya kukosekana kwa hewa ya kutosha wakati wa ibada ya misa na hivyo waamini wengine kusali nje.

Tuesday 7 May 2013

Sh 876.3 Bil kumaliza msongomano Jiji la Dar


Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM).

Dodoma. Wizara ya Ujenzi inatekeleza miradi ya Sh. 876.336 bilioni katika Jiji la Dar es Salaam,yenye lengo la kutafutia ufumbuzi wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM).
Katika swali lake,mbunge huyo alitaka kujua mpango wa Serikali wa kulitafutia ufumbuzi tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam hasa katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Lwenge aliiitaja miradi hiyo kuwa ni Barabara ya Kimara- Kivukoni, Fire-Kariakoo na Magomeni hadi Morocco na ujenzi wa karakana na vituo vya mabasi yaendayo kwa haraka pamoja na kuhamisha nguzo za umeme.
“Barabara ya Mwenge-Tegeta, Barabara ya Kilwa Bendera Tatu-Mbagala Rangi Tatu, ujenzi wa daraja la Kigamboni, Flyover ya TAZARA, Barabara ya Gerezani, Barabara ya Mandela na Barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo hadi Msata,’ alisema Lwenge.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (RBT) kutoka Morocco kwenda Magomeni hadi Kivukoni na Kimara kutapunguza msongamano wa magari kati ya Oysterbay Polisi na Daraja la Salender.
Kuhusu mipango ya baadaye, alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kujenga barabara ya juu pande zote za daraja la Salender, kupanua barabara kwenye maingilio ya daraja, kujenga lingine pembeni mwa daraja au kujenga mbadala kutokea Kenyata Drive kuunganisha na Ocean Road.

 

Serikali yataja changamoto ugatuaji madaraka nchini


Imetaja sababu hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa jamii kwenye shughuli za jamii na maendeleo, mahudhurio hafifu ya wananchi katika vikao vya uamuzi, ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa mapato yake.



Dodoma. Serikali imekiri kukabiliwa na changamoto kubwa zinazoikabili katika kutekeleza sera ya ugatuaji madaraka kwa wananchi wake.
Imetaja sababu hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa jamii kwenye shughuli za jamii na maendeleo, mahudhurio hafifu ya wananchi katika vikao vya uamuzi, ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa mapato yake.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri alisema ngazi ya mitaa na vijiji kumekuwa na tatizo kubwa la utunzaji wa vitabu vya hesabu, uandaaji taarifa za mapato na matumizi na taarifa za utekelezaji majukumu ya mitaa na vijiji.
Alikuwa akijibu swali la mbunge Viti Maalumu, Anastazia Wambura (CCM) ambaye alihoji Serikali inawezaje kuwahakikishia wananchi kwamba wenyeviti wa mtaa na vijiji wanajua wajibu wao kulingana na nafasi walizonazo.
Pia, mbunge huyo alitaka kujua Serikali jinsi inavyofuatilia fedha za uwezeshwaji na kujengewa uwezo, ambazo hutengwa kwa ajili ya kuwapa mafunzo viongozi hao ambazo hazifiki kwa wakati unaotakiwa.
Naibu Waziri alisema wenyeviti wa vijiji na mitaa wana wajibu wa kusimamia ulinzi na usalama maeneo yao, kuwakilisha wananchi katika vikao vya Kamati za Maendeleo ya Kata, wilaya na kuitisha na kuongoza mikutano.
“Kutokana na changamoto hizi, ni wazi kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwajengea uwezo wenyeviti wa vijiji na mitaa na watendaji wao ili kuhakikisha wanajua majukumu yao ipasavyo,” alisisitiza Mwanri.
Mwanri alisema Serikali imekuwa ikipeleka asilimia 40 ya fedha za kujenga uwezo katika vijiji na mitaa, asilimia 50 ya fedha hizo hutumika kuwajengea uwezo viongozi hao.

Grace Kihwelu alilia zao la kahawa



Dodoma..Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kihwelu (Chadema) ameitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa kufufua kilimo cha kahawa katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Akiuliza swali bungeni jana,mbunge huyo alisema kwa miaka mingi zao hilo limekuwa tegemeo kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro,lakini kwa sasa kilimo hicho ni kama kimekufa.
“Je Serikali ina mpango gani madhubuti na mahsusi wa kufufua kilimo cha kahawa Kilimanjaro ambacho kwa miaka mingi kimekuwa tegemeo kwa wananchi wa Kilimanjaro na mhimili mkubwa kwa uchumi wa taifa?” Alihoji Kiwelu.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira alisema Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza tasnia ya kahawa kwa lengo la kuendeleza kilimo cha kahawa nchini kwa kuongeza tija na ubora wa kahawa kitaifa.
Aliyataja maeneo mahsusi ya mkakati huo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa kahawa safi kutoka wastani wa sasa wa tani 50,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 ifikapo mwaka 2022.
Nyingine ni kuongeza ubora wa kahawa ili kupata bei ya ziada katika masoko ya nje kutoka wastani wa asilimia 35 hadi kufikia wastani wa asilimia 70 ifikapo mwaka 2022,” alisema
Alisema maeneo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani ili wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha kahawa na kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora ya kahawa.
Wassira alisema pia serikali inaendelea kuongeza matumizi ya viwanda vya kati vya kutayarisha kahawa ili kuongeza ubora wa zao hilo hivyo wakulima kunufaika na bei nzuri.

Kauli ya Kardinali imeacha maswali mengi kuliko majibu.



Jana nimebahatika kuisikiliza vyema taarifa fupi (KUNTU) iliyotolewa na mlezi wetu mkuu wa kiroho KARDINALI) ya kuujulisha umma ni nini kilichotokea kupitia chombo chake cha habari TUMAINI. Tunashukuru kwa taarifa yake hiyo ambayo kwa jinsi ilivyotolewa, nina hakika ilifanyiwa kazi ya kina kabla ya kuletwa hadharani.
Kwanza kabisa nashawishika kwa ukurasa wa awali kukubaliana na taarifa yake hiyo kutokana na imani yangu kuu kwake, na inavyojulikana kwa wachache kuwa kada ya UPAPA na UKARDINALI ni kada ambazo wanaozifikia pia wamepitia mambo ya kiintelijensia!
Tunashawishika kuamini hivyo kutokana na jinsi kiongozi huyu wa kiroho ambavyo ameweza kutoa ripoti yake ya kiintrijensia ndani ya chini ya masaa 24! Amesema suala hili lisihusishwe kwa aina yoyote ile na dini au itikadi ya uislamu bali waliofanya kitendo hicho ni WAKRISTO tena wa KANISANI hapo! Na kwa msisitizo akasema kuwa anao uhakika wa kile anachokisema!
Sasa inamaana kwa uweza wa kimungu ambao mtumishi huyu anao na ule wa uintelijensia alionao ameweza kuwasaidia hata polisi wetu kumaliza kazi ya upelelezi katika muda mfupi sana! Sasa kuna haja gani ya kuleta tena CIA? Na kama amesisitiza kuwa taarifa yake aliyoitoa ndiyo ya mwisho, kuna haja gani ya kuwashikilia hao watu wengine, si yeye apelike hiyo ripoti yake polisi ili kazi iwe fupi na amani irejee mioyoni mwa watu na kukata vilimilimi vya watu wengine ambao wanataka kupata umaarufu kupitia SAGA hilo?!

Lakini tukija katika upande wa pili, Je, hatuoni kuwa mtumishi wetu huyu amewahi sana kutoa ripoti yake hiyo ambayo inaonekana kama hitimisho la SAGA lenyewe?!

Na, Je, kama itatokea ikaja kuapatikina ripoti nyingine tofauti na hii tuliyoaminishwa na mtumishi wa mungu, Je, tutamwamini nani?
Maswali yapo mengi sana kuliko yale ya papo kwa papo ya Waziri mkuu, lakini katika hili nafikiri TAFAKARI ya kina ilitakiwa ichukuliwe kabla ya taarifa hii kutolewa.