Saturday 29 December 2012

Serikali Mkoa wa Kagera yawapiga jeki Vijana

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, katika taarifa yake kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk.

SERIKALI mkoani Kagera, kupitia vyama vya kuweka na kukopa, imevikopesha vikundi vya vijana, zaidi ya Sh83 milioni ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi .

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, katika taarifa yake kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk.

Fenella Mukangara aliyetembelea mkoa huo, kuangalia namna fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kusaidia vijana kujikwamua kimaisha.

Kanali Mstaafu Massawe alisema mikopo hiyo ilitolewa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kwamba hatua hiyo inalenga katika kusimamia utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana. Alisema chini ya sera hiyo, Serikali imekuwa ikiratibu shughuli za mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na urejeshaji wa mikopo.

Thursday 27 December 2012

Yaliyojiri Afrika mwaka huu wa 2012

LEO katika ukurasa huu wa habari za Afrika tunakuletea matukio muhimu ambayo yalitawala katika vyombo mbalimbali vya habari ndani ya mwaka huu kuanzia mwezi Januari.
Ikiwa wewe ni mfuatiliaji wa habari za Afrika hakika utakuwa umesikia  mambo mengi yaliyotokea katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwa ni pamoja na mauaji katika nchi zilizoingia katika machafuko ya muda au muda mrefu.
Mengine yaliyotokea ni baadhi ya wanajeshi kuamua kuwaondoa kinguvu viongozi waliopo madarakani na kuzitawala nchi hizo kimabavu.
Afrika Kusini
Miongoni mwa matukio ambayo yalijiri katika nchi hizo tukianzia na Afrika ya Kusini, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alitangaza maombolezo nchini humo kutokana na mauaji ya wachimbaji madini 38 yaliyosababishwa na polisi wakati wakiandamana kudai kuongezewa mishahara, tukio ambalo lilihuzunisha watu wengi Afrika.
Pia Ellinah Wamukoya ameteuliwa kuwa askofu wa kwanza wa kike wa Kanisa la Anglikana barani Afrika.
Akiongea muda mfupi baada ya kuteuliwa Ellinah Wamukoya alisema kwamba uamuzi huo umeonesha heshima kubwa kwa kina mama.
Tukio lingine kubwa kwa Afrika ni kuhusu mwana mama Ellinah Wamukoya (61) sasa atakuwa  kama askofu mpya wa kanisa hilo katika ufalme wa Swaziland, moja wapo ya nchi zinazokisiwa kufuata siasa za kihafidhina.
Kutawazwa kwake kumejiri huku Kanisa la Anglikana, likitarajiwa kujadili ikiwa kina mama wataruhusiwa kuapishwa kuwa maaskofu wa kanisa hilo.
Askofu wa Jimbo la Captetown, nchini Afrika Kusini, amesema kuwa wamechukua uamuzi huo ili wawe mfano kwa wengine na pia kuwatakia, viongozi wa kanisa hilo, faraja na hekima ili kujadilia suala hilo kwa haraka.
Kwa mujibu wa ripoti aliyotuma kwa vyombo vya habari, askofu huyo wa Jimbo la Capetown, Revd. Thabo Makgoba, amesema wimbi kwa sasa linavuma na kuwa wameshuhudia tukio la kihistoria ambao ni sawa na mbingu kufunguka.
David Dinkebogile aliongoza sherehe hizo na kukariri kuwa nia yao kuwa ilikuwa kumwapisha askofu na wale siyo mtu mweusi, mwafrika na raia wa Swaziland.
Askofu Wamukoya ni meya wa zamani wa mji mkuu wa Swaziland Manzini.
Somalia
Mwaka huu Wabunge wa Somalia waliandika historia ya nchi hiyo, baada ya kufanya uchaguzi uliotawaliwa na amani na kumchagua Hassan Sheikh Mohamud kuwa Rais wa nchi hiyo.
Waliopiga kura hizo ni wabunge pekee ambapo kulikuwa na wagombea 12 wa kinyanganyiro hicho cha kuongoza taifa hilo ambalo linakabiliwa na machafuko ya amani.
Licha ya Mataifa mbalimbali kuipongeza Serikali ya Somalia, kwa kufanya uchaguzi wa amani baada ya kipindi kirefu, Kundi la Al-Shabaab limesema kwamba haliwezi kuitambua serikali hiyo.
Pia  Al-Shabaab wameanza kuuza nyama ya fisi katika mji wa Bandari Kusini mwa Somalia, kama njia ya kukusanya pesa kwa ajili ya kuendesha oparesheni zake za kijeshi.

Padri ashambuliwa kwa risasi Zanzibar



Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki Mpendae,Zanzaibar akipakizwa kwenye gari kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar tayari kwa kusafirishwa kwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,Dar es salaam kwa matibabu zaidi baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana Mjini Zanzibar juzi jioni. Picha Martin Kabemba. 
Na  Waandishi Wetu  (email the author)

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Mkenda ambaye ni Paroko wa Parokia ya Mpendae, alipigwa risasi begani na shingoni na afya yake si nzuri.

PADRI Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, Mjini Zanzibar amepigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake juzi saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.
Hili ni tukio la kwanza katika historia ya Zanzibar kwa kiongozi wa kanisa kushambuliwa wakati wa Krismasi, lakini ni tukio la pili kwa kiongozi wa dini kushambuliwa mwaka huu.
Hivi karibuni, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga alimwagiwa tindikali iliyomjeruhi vibaya usoni na kifuani na watu wasiojulikana. Shambulio hilo lilimlazimu kiongozi huyo kwenda kutibiwa India ambako ameambiwa anapaswa kuripoti hospitalini kila baada ya miezi sita.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Mkenda ambaye ni Paroko wa Parokia ya Mpendae, alipigwa risasi begani na shingoni na afya yake si nzuri.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed alisema jana kuwa majeraha hayo yamemsababishia kutokwa na damu nyingi.

Alisema baada ya shambulio hilo, Padri Mkenda alipelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar. Hata hivyo, padri huyo alisafirishwa kwa ndege jana hadi Dar es Salaam ambako amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kamanda Aziz alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, lakini akabainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa alipigwa risasi baada ya watu hao kumshuku kuwa alikuwa na fedha za sadaka.

“Father Mkenda kitaaluma ni mhasibu na amekuwa akishika makusanyo ya fedha pale kanisani. Sasa huenda wahalifu hao waliona amechukua fedha na ndipo walipomfuata na kumpiga. Lakini hata hivyo, huo bado ni uchunguzi wa awali tu,” alisema Kamanda Aziz na kuongeza:

“Waliofanya tukio hili wamelifanya kwa madhumuni gani, ni swali gumu kujua sasa. Inawezekana kuna mambo mengine zaidi ya watu hao kutafuta fedha. Uchunguzi ukimalizika tutajua cha kufanya.”

Kamanda Aziz alisema walipata taarifa za tukio hilo saa 2:00 usiku na polisi walikwenda katika eneo hilo la Francis Maria anakoishi Padri Mkenda.

“Tulipofika tukakuta maganda mawili ya risasi za bastola na upande wa kulia wa kioo cha gari yake (padri) kuna damu katika viti vyake,” alisema Kamanda Aziz.

Alisema baadaye padri huyo alipelekwa hospitalini kwa ajili matibabu ambako madaktari walifanikiwa kumtoa mabaki ya risasi mwilini kabla ya jana kupelekwa Muhimbili.

“Tumempokea padri huyo saa 4:20 asubuhi leo (jana). Tulianza kumchunguza afya yake, baadaye kumfanyia uchunguzi kisha kumchukua kipimo cha CT Scan ili kubaini ilipo risasi hiyo,” alisema, mkurugenzi wa zamu katika hospitali hiyo, Agnes Mtawa.