Monday 30 June 2014

Msekwa aeleza sababu ya wasomi kukimbilia siasa

Dar es Salaam. Kwa nini siasa imegeuka kimbilio la wengi, wakiwamo wasomi Tanzania?
Ni swali aliloulizwa Spika mstaafu, Pius Msekwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni.
Akijibu swali hilo, Msekwa alieleza kwa ufupi sababu za wasomi kuacha taaluma zao na kuwekeza nguvu na akili zao katika siasa akisema inalipa kwa haraka na kwa njia nyingi zikiwamo mishahara minono, posho na marupurupu kuliko zilivyo taaluma nyingine.
Msekwa ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akitokea kwenye Chama cha Tanu na baadaye kurejea kwenye siasa, alisema malipo manono yamewafanya wasomi wengi, wakiwamo maprofesa, madaktari na wengineo kuifanya kimbilio.
Alisema pia uhuru wa watu kuchagua kazi nyepesi za kufanya katika maisha yao umefanya waione siasa kama kimbilio rahisi kuliko kutoka jasho kwenye taaluma, zikiwamo za utafiti, tiba, upasuaji, ualimu na nyinginezo. “Siasa imegeuka kimbilio kwa kuwa ina posho na marupurupu mengi zaidi,” alisema Msekwa na kuongeza kuwa wanasiasa wanajipitishia posho ambazo haziwezi kutolewa kwingineko.
“Mpe mtu choice (chaguo), acha aende kokote hata katika siasa, lakini ni vyema taaluma pia ikaheshimika,” alisema na kuongeza kuwa jambo hilo lilianzia  kwenye awamu zilizopita ambako wasomi, ama walioteuliwa au kuchaguliwa waliamua kushiriki siasa na hivyo kuziacha taaluma zao. Msekwa alimtaja msomi mmoja, Profesa Mazengo ambaye aligombea ubunge baadaye akautelekeza baada ya kushindwa kutimiza dhamira yake.
“Kulikuwa na mtu anaitwa Profesa Mazengo, yeye alikimbilia kwenye siasa akilenga kupata uwaziri. Ubunge alishinda lakini alipokosa uwaziri akautelekeza ubunge wake, hata jimboni hakwenda, hakuwakilisha wananchi na wapigakura wake, hivyo hakurudi baada ya miaka mitano,” alisema.
Kwa siku za karibuni, siasa na hasa ubunge, unaonekana kuwa na masilahi na fursa zaidi kuliko nafasi nyingine katika jamii na ndiyo maana wasomi wamekimbilia huko kwa matarajio ya kupata fursa za kupitisha mambo yao. Baadhi yao (wasomi), ubunge siyo tija, wamejikita zaidi kwenye nafasi katika serikali, zikiwamo za mitaa ili kufanikisha biashara zao au kuwa karibu wananchi wa ngazi ya chini.
Kwa mfano, orodha ya wabunge kwenye Bunge la sasa, inaonyesha wasomi wengi wakiwamo maprofesa, madaktari wa falsafa, madaktari wa tiba au wahandisi.
Msekwa alipoulizwa anadhani ni kwa nini Serikali haiboreshi masilahi ya wasomi katika taaluma zao, alicheka kisha akasema uwezo wa nchi ni mdogo, haiwezi kuboresha masilahi ya watumishi wote lakini inaweza tu kwa wabunge.

Dk Salim afichua siri ya JK na Tume ya Warioba

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa bungeni kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu walikuwa wanampa taarifa kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua iliyofikia,” alisema Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake na anazingatia mambo mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21, mwaka huu Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka. Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Serikali. Alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa na Tume na kuegemea katika muundo wa serikali mbili na idadi ya watu walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa ni ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na ubunge kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni pendekezo la mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo huku akisema baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi ambayo hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali katika sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya chama chake ili aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba Mpya haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo limeingizwa siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza kuleta matatizo.
“Tuko katika hali ambayo si nzuri inayohitaji uongozi thabiti, viongozi wote watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho ndicho kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari masilahi ya Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili zinazoshindana kuhusu idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila misuguano.
“Mwezi huu wa Julai ni muhimu sana, ni mwezi pekee uliobaki wa kuwaweka pamoja wanaotofautiana. Kila jitihada zinatakiwa kufanyika ili kuhakikisha Bunge Maalumu linakutana tena Agosti na wapinzani waliosusa wanarejea ili kumaliza kazi hiyo kabla ya kutoa rasimu ya tatu kwa ajili ya kura za maoni,” alisema na kuonya kuwa kuendelea na katiba ya sasa kunaweza kuleta matatizo.
Neno ‘wasaliti wa Mwalimu Nyerere’ lamchefua
Aidha, Dk Salim ameeleza kusikitishwa na kukatishwa tamaa na kauli za baadhi ya wanasiasa dhidi yake na wajumbe wenzake wa Tume kwa kuwaita wasaliti na hasa kitendo cha kutilia shaka uzalendo wao.
“Inakatisha tamaa sana. Mimi nina umri wa miaka 72, kati yake zaidi ya miaka 30 nimeitumikia nchi yangu, haiingii akilini katika umri huu wa mwisho nianze kuisaliti nchi yangu, inasikitisha sana kusikia eti hawa wasaliti wa Mwalimu Nyerere,” alisema.
Dk Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), alisisitiza kuwa wajumbe hao wamekuwa wakishutumiwa na watu wenye malengo yao, akitolea mfano kuwa hata Dk Mwesiga Baregu aliwahi kushutumiwa na chama chake na kutakiwa ajitoe kwenye tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Itakumbukwa kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikishutumiwa na wanasiasa hasa kutoka CCM kutokana na mapendekezo yake ya mfumo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mbili zinazoungwa mkono na chama hicho.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe walio wengi wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka CCM waliamua kubadili baadhi ya vifungu vya rasimu.
“Ni bahati mbaya sana binadamu unapotukanwa, unatupiwa madongo, tunaonekana wapuuzi kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, inaumiza sana,” alisema.
Kama ambavyo Jaji Warioba amesema mara nyingi, Dk Salim aliitetea Rasimu ya Katiba, akisema kilichopendekezwa ndiyo picha halisi ya maoni ya Watanzania.
Alisema Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi yenye hoja nzito yakieleza hasa matatizo yao katika nyanja mbalimbali kama afya, elimu, ardhi na mengine, ingawa hoja kuhusu muundo wa Serikali ndizo zinaonekana kushikiwa bango na wanasiasa.
Alisema ushahidi wa watu waliohojiwa upo katika maandishi, sauti na picha za video na idadi yao inatosha kuwakilisha Watanzania wote.
“Wanasema hatukuhoji watu wengi, waliohojiwa ni representative sample (sampuli), huwezi kuhoji Watanzania wote milioni 45,” alisema Dk Salim.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa mchakato umetekwa nyara na wanasiasa lakini Katiba inastahili kuwa ya kitaifa ya Watanzania wote, wenye vyama na wasio na vyama vya siasa.
Alisema hata kwenye tume, walikuwapo wajumbe zaidi ya 12 ambao hawatokani na CCM, wakitoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na wote walikuwa na mawazo tofauti lakini waliamua kuyaweka kando na kutoa rasimu inayotoa taswira ya mawazo na masilahi ya wananchi.

Monday 23 June 2014

Wabunge saba watikisa Bunge

Dodoma. Wabunge saba wamelitikisa Bunge tangu mkutano wa Bunge la Bajeti ulipoanza kutokana na michango yao binafsi.
Mwandishi wetu ambaye amekuwa bungeni tangu Mkutano wa Bajeti ulipoanza ametoa tathmini yake kuhusu michango ya wabunge iliyosisimua katika mjadala na kuibuka na orodha ya wabunge hao saba. Hata hivyo, katika tathmini hiyo, majina ya wabunge ambao walichangia kwa niaba ya kamati au kutokana na nafasi zao za uwaziri au uwaziri kivuli hajayaingizwa katika orodha hiyo.
Tathmini hiyo imefanyika huku leo mjadala wa Bajeti ya Serikali ya 2014/15 ukihitimishwa tayari kwa kupigiwa kura na wabunge kesho, baada ya kukamilisha mfululizo wa mijadala ya bajeti za wizara zote za Serikali tangu Bunge hilo lilipoanza Mei 6, mwaka huu. Hoja zilizoibuliwa na wabunge hao kwa nyakati tofauti ziliitikisa Serikali na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiti cha Spika au aliyekuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) kusimama kutoa ufafanuzi.
Waliotikisa
Wabunge waliotikisa Serikali katika michango yao ni Ally Keissy (Nkasi Kaskazini - CCM), David Kafulila (Kigoma Kusini - NCCR-Mageuzi), Kangi Lugola (Mwibara - CCM), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni - CCM), Tundu Lissu (Singida Mashariki - Chadema), Abbas Mtemvu (Temeke –CCM) na Cecilia Paresso (Mbunge wa Viti Maalumu-Chadema) .
Kafulila
Siku mbili baada ya Bunge kuanza Mei 8 mwaka huu, wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kafulila aliibuka na sakata la kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 milioni (Sh200 bilioni) akidai ni ufisadi uliofanywa na vigogo sita wa Serikali.
Aliwataja kwa majina vigogo hao na kusisitiza kuwa wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco na Tanesco ilipeleka shauri hilo mahakamani kulalamikia gharama kubwa za uwekezaji wanazotozwa na IPTL, hivyo kuamuliwa fedha hizo ziwekwe humo hadi shauri litakapoamuliwa, lakini baadaye zilichotwa katika mazingira ya kutatanisha.
Lugola
Lugola aliibuka Mei 10, mwaka huu katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na kusema kuwa Serikali ya CCM ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii huku akishangaa waziri mwenye dhamana ya kilimo, Christopher Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blaablaa.
Pia alimgeukia Naibu Waziri, Godfrey Zambi na kumwambia amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma bungeni akipaza sauti, baada ya kupata madaraka amewageuka wenzake na kushirikiana na waziri.
Akizungumza kwa sauti ya ukali ambayo mara nyingi haitarajiwi kwa wabunge wa CCM, Lugola alihoji inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki kama waziri?
Keissy
Mei 27, mwaka huu ilikuwa zamu ya Keissy, mbunge machachari wa Nkasi Kaskazini pale alipozua sokomoko wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje. Kauli yake kuwa Zanzibar haichangii katika Muungano hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili wa Muungano na kwamba hata umeme hailipi nusura imponze.
Alisema Zanzibar ina asilimia 2.8 ya watu wote wa Tanzania na kwamba kwa idadi hiyo, wananchi wa jimbo moja wanaweza kukusanyika eneo moja kwa kuitwa na mlio wa filimbi tu, kauli iliyosababisha wabunge kutoka Zanzibar kutaka kumpiga ‘kavukavu’.
Abass Mtemvu
Juni 5, Mtemvu naye aliibua mpya baada ya kumlipua Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya kuwa anafahamu uuzaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) ambalo alidai limeuzwa kwa Sh280 milioni.
Mtemvu alisema kulifanyika ujanjaujanja kati ya Kampuni ya Simon Group na Meya wa Jiji Dar es Salaam, Didas Masaburi kukopa benki na taasisi nyingine kwa ajili ya kununua shirika hilo, kauli ambayo ilipingwa na Kapuya huku suala la Uda likiendelea kukamata mjadala hadi Mwendeshaji wa Uda kuitwa bungeni.
Faustin Ndungulile
Mei 29 mwaka huu, Dk Ndugulile alimweka katika wakati mgumu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara hiyo na kuwa Serikali haijashirikisha wadau katika mradi wa Kigamboni utakaogharimu Sh11.7 trilioni.
Sakata hilo liliingiliwa na Waziri Mkuu ambaye alisema kuwa tatizo la mradi huo ni elimu kutotolewa kwa umma na kuomba wabunge waiachie Serikali suala hilo.
Tundu Lissu
Juni 2, Lissu aliwalipua Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge kwamba wanatumia vibaya nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Lissu alisema Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida.
Mawaziri hao waliokolewa na Profesa Mwandosya akisema kuwa miradi hiyo katika wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati yeye akiwa Waziri wa Maji, hivyo hawakujipendelea.
Cecilia Paresso
Mbunge huyu aliichachafya Serikali na kuungwa mkono na wabunge 13 wanawake wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakitaka iongezewe fedha ili kukabiliana na vifo vya kinamama na watoto.
Paresso alisema wizara hiyo imetengewa Sh622 bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/14 ilipotengewa Sh753 bilioni.
Hoja hiyo iliwanyanyua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima kutoa ufafanuzi. Wote hao walishindwa kumshawishi Paresso na wenzake, hadi Serikali ilipoahidi kuongeza fedha za wizara hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa Sh87 bilioni kwa ajili ya kulipa deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Friday 20 June 2014

Kiasi kingine kikubwa cha gesi chagunduliwa nchini. Je wananchi wanafaidikaje na gesi hiyo?

Dar es Salaam. Kampuni ya Statoil ya Norway na mshirika wake ExxonMobil wamegundua kiasi kingine kikubwa cha gesi katika Bahari ya Hindi nchini Tanzania.
Kiwango hicho kinakadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni mbili mpaka tatu (sawa na lita trilioni 56.6 hadi trilioni 84.9).
Ugunduzi huu unafanya jumla ya ujazo wa gesi iliyogunduliwa na washirika hao kufikia takriban futi za ujazo trilioni 20 (lita trilioni 566.25) kwenye Kitalu Namba 2, ambako washirika hao wanafanya shughuli za utafiti na uchimbaji.
‘’Tangu mwaka 2012 tumekuwa tukipata mafanikio ya asilimia 100 nchini Tanzania na eneo hilo limekuwa kitovu cha utafiti ndani ya muda mfupi. Ni kwa haraka tulitoka kwenye kuchimba kisima kimoja hadi kuwa na mkakati wa kuchimba visima vingi,’’ alisema Makamu wa Rais wa Shughuli za Utafiti za Statoil Ukanda wa Magharibi, Nick Maden.
Ugunduzi huo mpya katika Kisima Piri-1 umefanyika katika eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa wakati ilipogunduliwa gesi katika Kisima cha Zafarani-1 mwaka 2012.
Ugunduzi katika kisima hicho unakuwa wa sita katika Kitalu Namba 2.
Uchimbaji wa gesi katika kisima hicho ulifanywa na meli ya Discoverer Americas, usawa wa mita 2,360 za kina cha maji. Meli hiyo sasa inachimba kisima kingine cha Binzari katika Kitalu namba 2.
“Eneo lingine la utafiti limeshaandaliwa na litajaribiwa ndani ya mwaka 2014 na 2015. Tunatarajia kuchimba visima zaidi na tunatumaini kuwa matokeo ya visima hivi yataongeza kiasi cha ujazo wa gesi kwa ajili ya miundombinu ya mradi mkubwa wa gesi hapo baadaye,’’ alisema Maden.
Statoil ambayo imekuwapo nchini tangu 2007, inatafiti na kuchimba gesi katika kitalu namba mbili kwa niaba ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ikiwa na hisa ya asilimia 65 katika kitalu hicho wakati ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Limited ina asilimia 35.

Lissu ailipua tena Serikali

Dar/Dodoma. Serikali imeumbuliwa bungeni ikidaiwa kuwasilisha taarifa za uongo kupitia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ugawaji wa madawati yaliyonunuliwa kwa ‘chenji ya rada’.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alitoa tuhuma hizo jana, wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema Serikali imewadanganya wabunge kwa kuwa hakuna kitu kilichofanyika.
Alisema katika majibu ya Serikali kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa kuwa imetangaza kununua madawati 93,740 na kuyagawa katika halmashauri mbalimbali nchini wakati siyo kweli.
Alisema kwa mtindo huo, Serikali imelidanganya Bunge pamoja na Watanzania kwa kuwa imetangaza madawati hewa ambayo hayapo.
“Wabunge kama kweli mnatimiza majukumu yenu na hampo hapa kwa masilahi yenu tu, hebu hojini halmashauri zetu zimepelekewa haya madawati 93,000 yanayozungumzwa humu au mnapiga makofi tu? Serikali inadanganya tunatakiwa tuihoji tuiwajibishe,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitoa mfano wa mgawo huo kwenye Halmashauri ya Ikungi, Singida kwamba ilitangazwa kupelekewa madawati 508 lakini amekwenda jimboni na hakukuta dawati hata moja.
Alisema uchunguzi wake umebaini kuwa hata katika wilaya mbalimbali ikiwamo ya Iringa, hakuna kitu kama hicho.
“Jana sikuwa hapa bungeni nilikwenda kwenye halmashauri yangu, hakuna dawati hata moja. Hata Halmashauri ya Iringa kwa Mchungaji Msigwa (Peter) hapa ananiambia hakuna dawati hata moja, mnatudanganya ili iweje?” Aliwashauri wabunge wengine kufanya utafiti katika maeneo yao iwapo kuna madawati ambayo yamepelekwa kutokana na fedha zilizorejeshwa na Serikali kama chenji ya rada.
Lissu alisema ni maneno matupu ambayo yamekuwa yakiwahadaa wabunge na kuwafanya wasahau wajibu wao wa kuisimamia Serikali na kujikuta ni washangiliaji wakati wote. Lissu alisema kinyume na taarifa hizo za Waziri Mkuu, Bunge jana lilikuwa limeelezwa na Naibu Waziri (hakumtaja) kuwa madawati hayo hayajagawanywa.
Katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa akijibu swali la nyongeza la Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe - CUF), kuhusu madawati hayo, alisema kwa kuwa madawati hayo bado yanagawanywa, watakaa na kuangalia utaratibu mzuri wa kuyafikisha Zanzibar.
Lissu pia alisema fedha ambazo zilitajwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo kuwa ni pato la Watanzania ni uongo kwa kuwa ni mali ya wamiliki wa migodi.
Alisema takwimu za waziri zimesababisha Watanzania kuamini kuwa wameingiza fedha nyingi ilihali kiasi kilichoingia hakifikii hata asilimia 10 ya pato la wawekezaji.
Awali, akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga Mpina alielezea hofu yake kuhusu maendeleo ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwamba inaweza kufa kutokana na Serikali kutokuilipa madeni yake.
“Mifuko ya hifadhi ya jamii itakufa kutokana na kuidai Serikali madeni mengi makubwa. Kuna haja ya kuangalia jinsi ambavyo tunaweza kuishauri Serikali kwa suala hili,” alisema Mpina.
Mbunge huyo alielezea kukerwa kwake na matumizi ya Dola ya Marekani badala ya Shilingi katika malipo mbalimbali, jambo ambalo linazidi kushusha thamani ya Shilingi.
“Watu wanakuja na Dola wanatumia na wanaondoka nazo bila hata kuzibadilisha, basi ni vyema kama tunaona fedha yetu haifai tuiondoe tutumie hizo Dola,” alisema Mpina.
Aliikosoa Serikali akisema haijawahi kufanya mdahalo wa kina kujadili jinsi matumizi ya Dola yanavyoiathiri Shilingi ya Tanzania.
Majaliwa
Hata hivyo, Majaliwa akizungumza na gazeti hili jana jioni alisema inawezekana Lissu hakumwelewa au amefanya makusudi kupotosha kile ambacho yeye alikizungumza ili kujipatia sifa kwa umma.
“Nilichokisema hakitofautiani na kile kilichomo kwenye jedwali la hotuba ya Waziri Mkuu, nimesema kwamba hadi sasa tunaendelea kugawa madawati ya plastiki katika halmashauri za wilaya 41 na hivi ninavyozungumza halmashauri ya mwisho inayopelekewa madawati leo (jana) ni Temeke,” alisema Majaliwa na kuongeza:
“Kwa upande wa madawati ya mbao, ambayo yeye (Lissu) ameyaita ya chuma, nayo yanaanza kusambazwa katika halmashauri zilizobaki 123, na kazi hiyo itaendelea na ifikapo Agosti 15 mwaka huu kila halmashauri itakuwa imepata mgawo wake.”
Alisema tayari Serikali imetangaza zabuni ya utengenezaji wa madawati awamu ya pili ambayo itafunguliwa Jumatatu ijayo na kwamba baada ya taratibu kukamilika utengenezaji huo utaanza na kukamilika katika muda wa miezi miwili.
Alisema katika awamu ya kwanza, kila halmashauri inatarajiwa kupata madawati 756, sawa na madawati 123, 984.
“Kama unakumbuka awali tulipanga madawati haya yapelekwe kwenye wilaya kama sita nadhani, lakini wabunge walishauri kwamba kila wilaya inufaike na ndicho tulichokifanya,” alisema.

Suala la mgombea binafsi halina mjadala tena

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imeandika historia katika nchi yetu, baada ya kutoa hukumu iliyohitimisha safari ndefu ya wananchi kutaka wagombea binafsi waruhusiwe katika chaguzi za serikali za mitaa, ubunge na urais. Tunasema mahakama hiyo imeandika historia kutokana na suala hilo kukataliwa na Serikali yapata zaidi ya miongo minne sasa, hata pale mahakama za juu nchini zilipotamka kwamba kuwapo kwa mgombea binafsi ni haki ya kila raia kikatiba.
Pengine wananchi wengi hawajui kwamba nchi yetu iliwahi kuwa na wagombea binafsi. Katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi wa mwaka 1960, chama tawala cha TANU kilipoteza kiti cha ubunge katika Jimbo la Mbulu, baada ya Herman Elias Sarwatt aliyegombea kiti hicho kama mgombea binafsi kushinda.
Ushindi huo na mwingine wa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani ulikishtua chama hicho tawala na ndipo kilipotumia wingi wa wabunge wake bungeni kubadilisha Katiba na kufuta vyama vya upinzani na wagombea binafsi, hivyo kuifanya Tanganyika nchi ya utawala wa chama kimoja.
Hivyo kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kuliibua suala la mgombea binafsi. Serikali iliendelea kumkataa mgombea binafsi, ikisema lazima kila mgombea awe mwanachama wa chama cha siasa. Ndipo mwaka 1993 Mchungaji Christopher Mtikila alipofungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kawha Lugakingira ambaye alikubaliana na hoja zake, kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.
Lakini katika hali ya kushangaza mwaka 1994, Serikali kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilihakikisha chombo hicho kinafanya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia wagombea binafsi. Ndipo mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba. Hatimaye, jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi, Amiri Manento lilikubali hoja za Mchungaji Mtikila na kuruhusu mgombea binafsi.
Iliwashangaza wengi mwaka 2010 kuona Serikali ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Majaji saba wa mahakama hiyo walisikiliza kesi hiyo chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani. Serikali ilidai katika rufaa yake kwamba hakuna mahakama yoyote nchini yenye uwezo kisheria kusikiliza kesi inayotaka mgombea binafsi na kwamba mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri. Katika hukumu iliyokosolewa na wengi, mahakama hiyo, pamoja na kukubaliana na hoja ya haki ya kila raia kuchagua au kuchaguliwa bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa, ilisema siyo jukumu la mahakama kujielekeza katika masuala ya kisiasa.
Ndipo Mchungaji Mtikila alikata rufaa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoko Arusha na Juni mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa mrufani na kuitaka Serikali ya Tanzania kutoa taarifa ndani ya miezi sita kuhusu namna inavyotekeleza hukumu hiyo.
Ni jambo jema sasa kwamba Serikali imesema imo katika mchakato wa kisheria utakaoruhusu mgombea binafsi. Sisi tumetiwa moyo na hali hiyo na tunaitaka Serikali itambue kwamba suala hilo halina mjadala tena.

Thursday 19 June 2014

Lowassa: Bomu la ajira kwa vijana kulipuka muda wowote

Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema vijana 10,500 waliojitokeza hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi katika Idara ya Uhamiaji, ni ishara kuwa bomu la ajira litalipuka muda wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya Bunge, Lowassa alisema Serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.
Wasomi hao wa fani mbalimbali walijitokeza katika uwanja huo Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi wakisubiri kufanyiwa usaili huo.
Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira na akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.
Mbunge huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia kwenye malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na suala la ajira kwa vijana.
Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana.
Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora watu katika maeneo mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania sasa tupo milioni 48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu na kazi hakuna, pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,” alisema Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake, huku akimtolea mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya pili kwa sababu ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria kuanzisha kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,” alisema.
Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi jioni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu. Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa na kusisitiza kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa vijana.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema: “Vijana 10,500 kufanya usaili wa nafasi 70 ni janga la taifa. Yupo kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliwahi kulizungumza hili lakini akapondwa kwamba anazungumza mambo kwa kuzua. Sasa huu ndiyo ukweli wenyewe.”

Bajeti ya elimu 2014/15: Serikali imesikiliza kilio cha wananchi?

Pamoja na changamoto za viwango duni vya ubora, ufaulu hafifu, uhaba wa miundombinu, mazingira yasiyoridhisha ya kujifunza na kufundishia; sekta ya elimu imeendelea kukumbwa na matatizo ya miongozo duni inayosababisha ikose mwelekeo.
Matatizo haya ni kama vile kuanzishwa kwa utaratibu wa kuweka kivuli (OMR) kwa shule za msingi, kupanga upya viwango vya alama za ufaulu elimu ya sekondari (angalia matokeo ya kidato cha nne 2012).
Mengine ni kufutwa kwa daraja sifuri na kuanzishwa kwa daraja la tano (dalili ya kuficha aibu ya ongezeko la daraja sifuri), kurejeshwa na kubatilishwa tena kwa sharti la ufaulu kidato cha pili na kuanza kutumika kwa viwango vipya vya ufaulu vilivyokataliwa na Bunge mwaka 2013.
Kimsingi matatizo haya sehemu tu ya matukio yanayotoa picha ya mkanganyiko uliopo katika mfumo unaoongoza elimu.
Taswira inayojitokeza hapa ni kuwa serikali inatumia nguvu nyingi kuipamba sura ya elimu kwa kurekebisha matokeo na kurahisisha ufaulu huku kwa ndani imeficha udhaifu mkubwa katika ufundishaji, ujifunzaji, usimamizi wa shule, uwajibikaji na ubovu wa elimu inayotolewa.
Hakuna haja ya kulumbana, kila Mtanzania anaguswa na hali ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini. Umefika wakati Serikali ichukue hadhari na kuachana na tabia ya kupuuza ushauri unaotolewa na wadau wa elimu wanaosisitiza mambo ya msingi ya kufanyia kazi ili kuboresha elimu.
Kwa mfano, kufaulisha wanafunzi ambao hawakufundishwa kikamilifu ni kutengeneza kansa nyingine ambayo italitafuna taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Huu si uzalendo.
Tukemee tabia ya serikali kufanya amuzi wa mzaha katika elimu na kuitaka isikilize vilio vya wananchi na kuwataka watendaji kutanguliza mbele maslahi ya taifa.
Tunaitaka serikali na wabunge kuzingatia mambo muhimu yafuatayo katika bajeti ya elimu ya mwaka 2014/15.
Masilahi ya walimu
Kwa mujibu wa Takwimu za Chama cha Walimu (CWT), hadi kufikia Desemba 2013 madai ya walimu ambayo hayakulipwa yalifikia Sh 61bilioni. Ombi la CWT kwa serikali kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 50 limekataliwa na walimu wameendelea kupuuzwa.
Wakati huohuo serikali inatumia asilimia 43 tu ya fedha za mishahara ya watumishi wa umma kuwalipa walimu ambao idadi yao ni asilimia 67 ya wafanyakazi wote wa umma. Lakini serikali ilitumia asilimia 57 ya fungu la mishahara ya umma kuwalipa wafanyakazi wa sekta nyingine ambao ni asilimia 33 tu ya watumishi wote wa umma.
Serikali kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, imeahidi kuwa italipa madai haya ya walimu katika mwaka wa fedha 2014/15.
Hata hivyo, tunakumbusha kuwa haya ni madai ya muda mrefu na ahadi kama hizi zimekuwa zikitolewa mara kwa mara pasina utekelezaji.
Serikali itambue msemo usemao; “Uzuri wa mfumo wa elimu unategemea ubora wa walimu wake”. Kwa mantiki hii haina budi kuwathamini walimu kama kweli inakusudia kuboresha elimu.
Walimu wamekata tamaa na tusipokuwa makini hali hii itaambukizwa kwa watoto wetu, familia zao na hatimaye sehemu kubwa ya jamii pia itakata tamaa.
Uwekezaji katika elimu
Katika makubaliano ya mpango wa Elimu Kwa Wote (EFA - 1990), ambayo Tanzania imeridhia, iliazimiwa kuwa uwekezaji katika elimu katika kila nchi mwanachama ufikie walau asilimia 20 ya bajeti nzima au asilimia sita ya pato la nchi husika.
Hata hivyo, hali imekuwa tofauti katika nchi yetu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita uwekezaji umekuwa ukishuka badala ya kuongezeka.
Kwa mfano, mwaka 2008/09 bajeti ya sekta ilifikia asilimia 20, lakini ikashuka mpaka asilimiua 18 mwaka 2010/11. Na baadaye mwaka 2013/14 ikashuka hadi asilimia 17.3.
Tunazidi kuikumbusha serikali katika kipindi hiki wanachoelekea kupanga na kupitisha bajeti, izingatie makubaliano haya ambayo kwa hiyari ilitia saini na kuridhia kuwa itajitahidi kupanga walau asilimia 20 ya bajeti yake kuu katika sekta ya elimu.
Upungufu wa ruzuku shuleni
Tanzania iliporidhia kutekeleza mipango ya maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari, lengo lilikuwa kuziwezesha shule za umma kuwa na uwezo wa kujiendesha na kusimamia utoaji wa elimu katika kiwango kinachostahili.
Utoaji wa ruzuku (Sh 10,000 kwa wanafunzi wa msingi na 25,000 kwa sekondari) ulikuwa sehemu ya maazimio ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
Jambo la ajabu ni kuwa, taarifa za utekelezaji wa mpango na azimio hili la utoaji ruzuku zinaonyesha kuwa kiasi ambacho kimekuwa kikifika shuleni ni pungufu ya kilichopangwa.
Mathalani, katika awamu ya kwanza ya mpango wa elimu ya msingi, wastani wa Sh 6,497 tu ndizo zilizofika shuleni badala ya Sh10,000, huku wastani wa Sh 5,500 tu ndio ukifika shuleni wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili.
Hali hii inaendelea hata katika utekelezaji wa awamu ya tatu. Wastani wa kiwango kilichofika shuleni mwaka 2012/13 ni Sh 3,580 badala ya Sh 10,000.
Hali hii inazikumba pia shule za sekondari ambazo nazo zinapokea wastani wa Sh 16,384 badala ya 25, 000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Ikumbukwe tu hapa kuwa viwango hivi ni wastani tu wa hali ya utoaji ruzuku shuleni, lakini katika hali halisi ziko shule nyingi ambazo hupata chini ya wastani wa 1,500 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Bajeti ya elimu ya awali
Kwa kutambua umuhimu wa elimu ya awali katika makuzi na maendeleo ya mtoto kitaaluma na kijamii, serikali imeazimia katika mipango yake mbalimbali kufanya uwekezaji stahili katika eneo hili.
Sera ya Elimu ya 1995, mtaalaa wa elimu ya awali wa 2007, Dira ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM), Mkukuta ni miongoni mwa mipango ambayo inaakisi azimio la serikali kukuza elimu ya awali.
Pamoja na maazimio haya serikali imeshindwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano haya. Mathalani uwiano kati ya wanafunzi wa awali na darasa umebaki kuwa 1:115 badala ya 1:25, uwiano kati ya mwanafunzi kwa mwalimu pia ni 1:124 badala ya 1:25. (BEST 2013).
Tutakumbuka kuwa elimu ya awali haikugusiwa kabisa katika mpango wa ruzuku katika awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM ). Na hata ilipogusiwa katika awamu ya pili, fedha kwa ajili ya ruzuku elimu ya awali hazikutoka kabisa.
Katika awamu ya tatu, elimu ya awali imejumuishwa katika bajeti ya ruzuku kwa shule za msingi. Hata hivyo, taarifa za utekelezaji mipango zinaonyesha fedha kwa ajili ya elimu ya awali hazijumuishwi katika fedha ya ruzuku inayokwenda shuleni.
Kuimarisha ukaguzi 
Hali ya ukaguzi bado ni mbaya, uwezo wa serikali kukagua shule hauridhishi. Takribani asilimia 19.1 tu ya shule zote za msingi ndizo zinazokaguliwa kwa mwaka na asilimia 21.4 kwa shule za sekondari.
Wizara husika ijitahidi kuongeza bajeti ya ukaguzi wa shule angalau idara iweze kukagua asilimia 50 ya shule zote za msingi na sekondari kwa mwaka.
Kama bajeti ya ukaguzi itaongezwa tuna imani shule zetu zitakaguliwa. Hivyo viwango vya ubora vitafahamika, upungufu utafanyiwa kazi ili hatimaye tuweze kuwa na elimu bora.
Wakati tukiitaka serikali kuongeza bajeti ya ukaguzi, tunasisitiza pia umuhimu wa kuwa na Wakala ya Ukaguzi wa Elimu kama zilivyo sekta nyingine. Hii ndio njia pekee na sahihi ya kuboresha ufanisi katika suala la ukaguzi.
Mazungumzo ya mchakato huu yamekuwepo kwa taribani miaka mitatu sasa lakini mafanikio yake hayaonekani. Itaendelea wiki ijayo

Tuliteleza mikataba ya madini, sasa tusonge mbele-2

Madini na maisha ya wananchi
Haiingii akilini kuona kampuni za kigeni zinazochimba madini Tanzania zinawekeza nchi za nje, huku wananchi wa Tanzania wakiendelea kuwa maskini.
Nafahamu kuwa mimi siyo mwandishi wa kwanza kuandika suala la madini Tanzania, lakini haimaanishi kwamba tufunge mdomo au tutupe kalamu zetu.
Madini ni miongoni mwa rasilimali zenye thamani kubwa, hivyo kama zitawekewa sheria na usimamizi mzuri, taifa linaweza kunufaika sana kimaendeleo.
Tanzania tunazalisha madini ya aina nyingi kama dhahabu, almasi, rubi, tanzanite, ulanga nk.
Katika uzalishaji huo, kuna baadhi ya migodi inamilikiwa na wachimbaji wadogo wazalendo na mingine inamilikiwa na wachimbaji wakubwa hususani kampuni za kigeni na mingine inamilikiwa kwa ubia baina ya wageni na wazawa au mengine ya wazawa.
Ulinzi wa madini yetu
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 27 ibara ndogo ya 1 inaeleza kuwa kila mwanachi ana jukumu la kulinda mali ya nchi ikiwa ni pamoja na madini. Hii ndiyo kusema kwamba kwa kuacha madini kuchimbwa kiholela, wananchi na Serikali yenyewe haijitendei haki. Madini ni mali ya yote inapaswa kuwanufaisha wote.
Madini katika pato la taifa
Hivi karibuni kuna michango mbalimbali inaendelea bungeni kuijadili bajeti, hatujaelezwa kwa kina mapato yanayotokana na madini, miaka yote tumeendelea kuwa tegemezi.
Wasomi wanaongezeka, ajira haziongezeki, deni la taifa nalo linazidi kupanda. Tuna rasilimali nyingi zikiwamo madini, lakini ni kama yametushinda kujinufaisha, sasa tunakimbilia sekta ya gesi. Rais wa Botswana, Festus Mogae tarehe 7, Juni, 2006 alisema: “Kwa watu wetu, kila almasi inayouzwa inawakilisha chakula mezani, mazingira mazuri ya kuishi, afya bora, maji safi, barabara kuunganisha jamii zetu na vingi zaidi.”
Kasoro za sheria za madini Tanzania
Sheria inayosimamia madini Tanzania ni Sheria ya Madini ya mwaka 2010 Na.14 pamoja na kanuni zake mbalimbali zinazohusu mazingira zilitolewa na gazeti la Serikali Na. 403 la tarehe 5/11/2010 inayohusu kanuni za mazingira.
Sheria hizo zinahitaji kupitiwa upya kwa sababu ya kasoro zake kadhaa zinazoonekana.
Moja ya kasoro hizo ni kwamba katika maombi ya kupewa leseni za uchimbaji madini kama watu wana sifa sawa za kupewa, wanaangalia nani wa kwanza kuomba, kama wameomba siku moja wataangalia mazingira husika.
Tunahitaji kufanya mabadiliko na sheria hiyo kutamka kuwa utaifa ndiyo kitu cha msingi cha kuangalia.
Tumeona wiki iliyopita mjini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alikuwa akizindua kampeni ya Uzalendo, mambo haya ya uzalendo yasambae katika sekta zote mpaka za madini.
Mbili, waziri ana mamlaka makubwa sana kwenye sheria hii ya madini, anasaini mikataba kwa niaba ya Watanzania; kifungu cha 15 cha sheria ya madini ya mwaka 2010 kinamruhusu waziri husika kuamua kugawa maeneo ya uchimbaji kwa zabuni au kawaida.
Madaraka ni makubwa sana ukizingatia na unyeti wa sekta. Kumpa mtu madaraka makubwa kiasi hicho ni kuweka mwanya wa rushwa. Tatu, kamishna wa madini kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha sheria no. 14 ya mwaka 2010 ya madini huteuliwa na Rais tu. Hii ni nafasi nyeti inatakiwa kuwa ya wazi na ya kiushindani, Watanzania waombe nafasi hiyo, mwenye uwezo mkubwa ndiyo apewe nafasi.
Kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kinakataza mtu yeyote zaidi ya mmiliki halali wa leseni ya madini, kumiliki, kusafirisha au kuuza madini, jambo kama hili pia linapaswa kuangaliwa, kwa sababu kwa namna moja ama nyingine kinazuia watu wengine kujiingiza kwenye biashara hii.
Kifungu cha 18 (3) kinakataza mtu yeyote kusafirisha nje ya nchi madini au sampuli za madini bila kuwa na leseni ya madini, kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi na uthibitisho wa malipo ya mrabaha. Sheria kama hii inapaswa kuangaliwa, kwani angeweza kuruhusiwa tu yeyote ili mradi awe anafuata taratibu nyingine za biashara.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 18 (4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, mtu yeyote atakayekiuka sheria kuhusiana na umiliki na biashara ya madini akipatikana na hatia atatozwa faini ya kiasi kisichozidi Sh10 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu, au adhabu zote mbili.
Kwa kampuni, adhabu iliyopo kwa mujibu wa sheria kwa kosa hilo ni kulipa faini isiyozidi Sh50 milioni. Wataalamu wa madini wanabainisha kuwa faini iliyowekwa na sheria na adhabu yake ni ndogo sana ukilinganisha na thamani ya madini.
Kifungu cha 6 (4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kinampa mamlaka kamishna wa madini kutaifisha madini yaliyopatikana kinyume cha sheria, pamoja na vifaa vilivyotumika kuzalisha madini hayo. Sheria ilipaswa kueleza zaidi juu ya uhifadhi na uuzaji wa madini hayo.
Tano, sheria ya madini kifungu cha 25 (1) inaeleza kuwa ripoti inayotolewa na wamiliki wa haki miliki za migodi ni siri, kwa nini ripoti iwe siri? Kwa nini isiwekwe wazi mfano kwenye tovuti ya wizara na kufanya kila mwananchi ajionee kinachoendelea kwenye rasilimali ya nchi yao. Mikataba ni siri, ripoti kutoka kwa wamiliki nayo ni siri. Waswahili wanasema “halali haina siri, haramu ndiyo ina siri.”
Hizi ni baadhi ya kasoro kwenye sheria ya madini. Haya mambo yawekwe wazi kila mmoja ajue kinachoendelea.
Maeneo ya migodi yatangazwe wazi, kila mtu agombanie kwa ushindani ulio sawa. Maeneo ya madini yaianishwe na yatangazwe, watu wagombanie kwa usawa, kipaumbele wapewe wazawa wenye sifa na uwezo, tusiwabeze Watanzania juu ya hili.
Kwa mfano kwa sasa tunataka kujikita kwenye kuchimba urani, lakini imefahamika kuwa madini hayo ya urani yana hatari kubwa kwa binadamu kutokana na kuwa na mionzi yenye madhara. Lazima tujifunze kutoka kwenye uchimbaji wa madini mengine kama dhahabu, almasi, Tanzanite na chokaa, ambao ulisababisha wananchi kupata magonjwa ya ngozi, saratani, uchafuzi wa maji na vifo vya mifugo na wanyama wengine wa porini na majini.
Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na 403 la tarehe 5/11/2010 kanuni ya 7 na 8 zinakataza uchafuzi wa mazingira, lakini kanuni ya tisa inasema ukifanya kosa la uchafuzi faini haitazidi milioni moja au kifungo kisichozidi miezi sita, najiuliza hiyo adhabu kweli inaonyesha nia ya dhati ya kulinda mazingira kweli?
Jibu jepesi, hapana, tutunze mazingira yetu, madini yana thamani sana lakini hata mazingira yetu yana thamani kubwa sana.
Kwa kifupi, baada ya mikataba hiyo kutomnufaisha mwananchi, Serikali haina budi kuangalia mapungufu hayo katika sheria na kuyafanyia kazi ili madini na rasilimali nyingine ziwe na usimamizi thabiti na wenye manufaa kwa kila Mtanzania.

Kesi tano za mabilioni Uswisi zachunguzwa

Dar es Salaam. Tanzania imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery – ICAR (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la mabilioni hayo ya Uswisi, Serikali iliunda kikosi kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kulifanyia kazi.
Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na kubaini kuanza kwa uchunguzi huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba zinatokana na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi hivi karibuni, Mtafiti wa Sheria wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema: “Tuna makubaliano na Serikali ya Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), tunachunguza kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji wa fedha, hivyo tuko katika ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano ya moja kwa moja kwa sababu bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa katika utoaji wa taarifa.”
Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.
“Ni kweli tumeombwa na Serikali ya Tanzania kusaidia kuchunguza baadhi ya kesi… zilikuwa zimeshachunguzwa lakini kutokana na uwezo wao mdogo tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema tunazo kesi tano hivi… ni kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu masuala ya fedha. Hatuwezi kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa na mkataba wetu na taasisi tunazofanya nazo kazi.”
Licha ya kutotaja majina, Zinkernagel alisema wanaochunguzwa katika kesi hizo wanahusishwa na kampuni hewa zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota fedha kisha kwenda kuzificha nje ya nchi.
“Kuna watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa wakipokea rushwa au wamekuwa wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni kivuli na ushirika mwingine wa kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda kwenye kampuni fulani kwa lengo la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na wafanyabiashara kuhamisha fedha haramu na mwisho hujisafisha,” alisema.
Jaji Werema
Jaji Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya uchunguzi huo lakini akakataa katakata kutaja watu wala kampuni zinazofanyiwa uchunguzi.
“Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa kesi kwa sababu kwanza tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pili, tunaweza kuwataja lakini baadaye ikabainika kuwa si kweli, bali ni tuhuma tu na wakaja kutushtaki na tatu, tutakapowataja watu hao tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi wetu.
“Katika kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu kwa utaratibu ili tusiharibu upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani tumekaa kimya hatufuatilii lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika mtaona na mtasikia.”
Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema watu au taasisi zilizoweka fedha nchini humo hawawezi kutajwa kwani ulinzi wa faragha za watu ni suala la kimataifa... “Sizungumzii tu akaunti za Tanzania, suala la kulinda faragha za watu ni la kimataifa. Ukiwa raia wa Uingereza, Ufaransa au Tanzania, huwezi kupata taarifa za maisha ya mtu binafsi. Kwa sababu wewe kama ni raia mwema, una haki ya kuwa na faragha yako.”
Taarifa za 2011 kutoka Uswisi zilionyesha kuwa kuna kiasi cha Sh327.9 bilioni zilizofichwa kwenye benki za nchi hiyo, lakini Ripoti mpya ya mwaka 2012 ya Benki za Uswisi inaonyesha kuwa fedha hizo zimepungua hadi Sh291.96 bilioni.
Akizungumzia kupungua kwa fedha hizo, Balozi Chave alisema: “Inawezekana ni kutokana na kelele za vyombo vya habari hasa Mwananchi, pengine wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye benki za nchi nyingine.”
Taarifa ya Global Financial Integrity ya 2013 inaonyesha kuwa utoroshaji haramu wa fedha kutoka Tanzania kati ya 2008 na 2011 umefikia jumla ya Dola za Marekani 2.935 bilioni (Sh4.2 trilioni) na inakadiriwa kuwa Watanzania wanamiliki utajiri wa Dola za Marekani 750 milioni (Sh1.23 trilioni) katika Visiwa vya Jersey.
Muda wa uchunguzi
Wakati Tanzania ikiwa imepeleka kesi hizo mbele ya taasisi hizo ndani ya mwaka mmoja, Zinkernagel alisema zinaweza kuchukua miaka mitano hadi 10 ili kufanikisha kurejesha fedha zilizofichwa.
“Tangu uchunguzi unaanza hadi fedha zirudishwe kwa nchi husika inaweza kuchukua hadi miaka 10. Sisi hatuna muda mrefu tangu tuanzishe taasisi hii, lakini tunafahamu baadhi ya kesi zimechukua hadi miaka 20. Hizi ni kesi za kimataifa, hivyo unaanza kufuatilia akaunti na mifumo ya taasisi nyingine… hiyo tu inaweza kuchukua hata miezi sita. Bado mtuhumiwa anaweza kukata rufaa. Ni kweli unataka mambo yaende haraka lakini pia huwezi kukiuka utawala wa sheria.”
Mbali na Tanzania, Zinkernagel alisema taasisi yake pia inashughulikia kesi za nchi nyingine 12 duniani na kwamba wamefanikiwa kukamata baadhi ya fedha na mali zilizoibwa katika baadhi ya nchi.
Alisema kazi hizo hufanywa bila malipo yoyote kwa kuwa taasisi hiyo hupata fedha kutoka serikali za Uswisi na Uingereza.
Changamoto
Akieleza changamoto zilizopo katika kupambana na uhalifu wa fedha haramu, Zinkernagel alisema ni ushirikiano hafifu kati ya nchi zinazoibiwa fedha na zile zinazoficha.
“Mamlaka za Uswisi zikigundua kuwapo kwa mali labda kama za Tanzania, wanaweza kuanzisha uchunguzi wao lakini ili kuhusisha uchunguzi na nchi husika watahitaji msaada kutoka nchi husika. Mamlaka ya Uswisi haiwezi kuendeleza kesi bila ushirikiano na mamlaka za Tanzania, kwa mfano. Hapo ndipo tunapokumbana na siasa nyingi pale tunaposhughulikia kesi kama hizo. Inakuwa vigumu kupata ushirikiano wa wanasiasa tunapouhitaji, hiyo ni changamoto kubwa.
“Changamoto nyingine, ni uwezo mdogo wa vyombo vya usalama vya Tanzania wa kushughulikia kesi za rushwa, matumizi mabaya ya fedha na madaraka. Ni kazi ngumu kufuatilia kesi kama hizo kwani unahitaji kuhusisha sekta mbalimbali. Changamoto hiyo ya utaalamu pia inaigusa Tanzania ndiyo maana haina uwezo wa kuchunguza kesi kama hizo.”
Kwa upande wa nchi zinazoficha fedha, Zinkernagel alisema kuna tatizo la kutoweka vikwazo kwa taasisi za fedha zinazotuhumiwa kuhifadhi fedha haramu.
Tanzania imetajwa kuwa nchi ya 13 kati 20 duniani kwa utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika mitandao mbalimbali ikiwamo Global Financial Integrity, Carl Smith, One Dola Bilioni na Taarifa ya Swiss,” zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na biashara haramu ya uhamishaji wa fedha na misamaha ya kodi na mikataba mibovu.

Monday 2 June 2014

Polisi wanolewa Uchaguzi Mkuu wa 2015

Dar es Salaam. Harakati za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 zimeanza. Polisi wameanza mafunzo yatakayowaongezea uwezo wa kusimamia uchaguzi huo.
Mafunzo hayo yanafadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia mradi wake wa Uwezeshaji wa Demokrasia (DEP).
Wakufunzi wanane kutoka Chuo cha Polisi cha Uingereza wanaendesha mafunzo kwa maofisa 88 wa polisi wa ngazi za juu na kati.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema yamekuja wakati mwafaka wakati jeshi hilo likijiandaa kwa shughuli hiyo muhimu ya kitaifa.
Mafunzo hayo yanayofanyika Dar es Salaam na Zanzibar yanalenga kuwajengea uwezo makamanda wa polisi wa kupanga, kumudu na kuratibu kwa ufanisi hatua za kipolisi za matukio yanayotishia utulivu wa amani katika jamii.
Alisema katika kila kozi ambayo itaendeshwa kwa wiki mbili, itatoa mafunzo kwa maofisa hao ya kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria na namna ya kudhibiti ghasia na baadaye kuwafundisha askari wote waliobaki. “Tunataka maofisa wetu wawe na ujuzi wa kutosha kusimamia wakati wa vurugu ili uchaguzi ujao uwe wa haki na amani. Wawe na uwezo mzuri wa kuwaelewesha wananchi juu ya kazi yao ili kuendeleza imani juu ya polisi nyakati kama hizo. Pia yatatusaidia kutambua namna gani tufanye kazi katika mazingira ya vurugu yenye watoto na wanawake.”
Alipoulizwa juu ya matumizi ya nguvu nyingi kwa raia, Sirro alisema wasingependa polisi kutumia nguvu hizo lakini mazingira husika hulazimisha hali hiyo kutokea.
“Ukiona tumetumia moshi… moshi… tumeona mazingira yameturuhusu kufanya hivyo. Askari polisi anapotumia moshi kukutawanya unasema nguvu kubwa… nashindwa kukuelewa. Kwa mfano, wewe una panga na mimi nina kirungu… unakuja kunipiga na panga hivi nikitumia kirungu kukupiga ili nikupeleke polisi kuna ubaya?
Mtaalamu wa masuala ya usimamizi wa uchaguzi wa UNDP nchini, William Hogan alisema taasisi yake inathamini uchaguzi mkuu, pia namna polisi wanavyotumika katika uchaguzi katika nchi za kidemokrasia. “Umakini wa polisi wakati wa usimamizi wa uchaguzi hususan katika kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria ni moja ya vitu muhimu ambavyo hupima iwapo uchaguzi husika ulikuwa wa haki na wazi hivyo polisi wanahitajika kuongezewa uwezo,” alisema Hogan.
Alisema mafunzo hayo ni mwendelezo tu wa mafunzo kwa polisi kwani yalishafanyika 2010 na yalikuwa na mafanikio.
Alisema wanataka uchaguzi mkuu ujao uwe bora ulimwenguni kwa kuanzia na kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Rais wa Malawi ana msimamo mkali Ziwa Nyasa

Dar es Salaam. Wingu jeusi limeanza kutanda kuhusu hatima ya mzozo wa Ziwa Nyasa kutokana na msimamo wa hivi karibuni wa kiongozi wa Democratic Progressive Party (DPP), Peter Mutharika ambaye sasa ni Rais mpya wa Malawi.
Hiyo inatokana na msimamo wa Mutharika ambaye ni Profesa wa Sheria wa kupinga kuendelea kujadiliana na Tanzania kuhusu nani mwenye haki ya kumiliki ziwa hilo alioutoa wakati alipowatembelea wananchi wa Chipoko, kando ya ziwa hilo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu ambao ulimwigiza madarakani.
Pamoja na kwamba mazingira ya msimamo huo yanaweza kutofautiana na hali halisi ya sasa, tofauti za kisiasa baina yake na mtangulizi wake, Joyce Banda zinaweza kuongeza msukumo mpya wa kutaka kutoendelea na mazungumzo ya mpaka wa ziwa hilo.
Akizungumza na wananchi hao, Profesa Mutharika aliwatoa wasiwasi na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa maelezo kuwa ziwa hilo lipo kwenye himaya ya Malawi na kwamba kuendelea kujadiliana na Tanzania ni kupoteza muda.
“Hakuna haja ya kuendelea kujadiliana, Ziwa Malawi ni mali ya Malawi na litaendelea kuwa la Malawi daima,” alisema Mutharika ambaye pia amewahi kufundisha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alimshutumu Banda na kudai alikuwa dhaifu kiasi cha kutoa fursa kwa Tanzania kutumia udhaifu huo kutaka kupora ziwa hilo.
“Ziwa hili letu ila Tanzania inatumia tu udhaifu wa Serikali iliyopo kwani wenyewe wanajua ndani ya mioyo yao kuwa hawana chochote katika ziwa hilo. Tutakaporejea serikalini mwakani haya mambo yote yasiyo na kichwa tutayamaliza. Nataka niwahakikishie kwamba tutapeleka meli zaidi kwenye ziwa hili ili kuinua shughuli zetu za kiuchumi na kutengeneza ajira kwa vijana wetu.”
Hata hivyo, wiki iliyopita Serikali ya Tanzania ilitoa msimamo wake kuhusu mzozo huo wa mpaka na kudaia kuwa itaendelea kujadiliana na Malawi.
Akizungumza bungeni wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara yake, Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema Tanzania ilikuwa ikifuatilia kwa karibu uchaguzi wa Malawi na kwamba iko tayari kufanya kazi na serikali yoyote itakayoingia madarakani.

Mwanamke ‘apewa’ daraja la upadri

Michigan, Marekani. Mtandao wa wanaharakati wanaopigania wanawake kupewa daraja la upadri, umemtangaza mwanachama wake, Lillian Lewis (75), kuwa padri Mkatoliki.
Uamuzi huo ambao unauweka mtandao huo katika hatari ya kutengwa na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki duniani (Vatican), umefanyika mwishoni mwa wiki baada ya mwanamke huyo kutangazwa kasisi wa kwanza nchini Marekani.
Alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kuhudhuria masomo ya tauhidi (theolojia) katika Chuo Kikuu cha Marquette miaka ya 1960.
Lewis alisema kashfa za karibuni kwenye kanisa hilo na kutengwa kwa baadhi ya watu ni moja ya mambo ambayo yamemchochea kufikiria kupanda kwenye mimbari na kuhubiri.
“Nimedhamiria kuonyesha njia kwa wengine kwamba wanawake tunayo nafasi kubwa ya kuongoza kanisa kama makasisi. Nina mabinti wanne. Hakuna hata mmoja ambaye anasali kwenye kanisa hilo (Katoliki),” Lewis aliliambia shirika la ABC News. “Wamekerwa na matukio ya siku za nyuma, kashfa ambazo zimeliandama kanisa … wanasema Ukatoliki umebakia kuwa wa kwangu, si wao.”
Sherehe za upadrisho wa Lewis zilizofanyika Jumamosi, zilihudhuriwa na wageni 200 kwenye eneo la nyumba yake. Miongoni mwao walikuwa ni viongozi wa dini isipokuwa wale wa Kanisa Katoliki. Lewis ni mwanachama wa mtandao wa Roman Catholic Womenpriests ambao ulianzishwa mwaka 2002 na umekuwa ukitaka ushirikishi, kumjua Kristo zaidi kwenye karne ya 21 … wenye mtazamo wa kumfuata Yesu kikamilifu kwa kuwahusisha wanawake kama mitume na watu sawa kama ilivyo katika Injili.
Maofisa wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Michigan ambao hawakuhudhuria sherehe hizo walieleza kuwa waumini wake walioshiriki sherehe hizo batili nao watashughulikiwa.
Askofu Paul Bradley wa Jimbo Katoliki Kalamazoo, alitoa tamko kali kupitia mtandao wa WWMT-TV in Kalamazoo, Mich., akieleza kuwa yeyote aliyeshiriki shughuli hiyo hatambuliwi na Kanisa Katoliki.
Mbali ya kuonywa na jimbo hilo, Lewis alisema shughuli hiyo ilikuwa yenye mafanikio na alitarajia kuwa ingepingwa na Kanisa Katoliki. Hata hivyo, alisema licha ya kupewa daraja hilo, hafahamu jukumu ambalo atapewa na kanisa.
Alisema majirani zake na mwanawe wa kiume na mchumba wake, walimuunga mkono baada ya kutambua nafasi ya mwanamke kama kasisi na kusema yuko tayari kuwafungisha ndoa wapenzi hao.
Hilo ni pigo jipya kwa Kanisa Katoliki ambalo kwa siku za karibuni lina kilio cha kutaka mapadri waruhusiwe kuoa huku Papa Francis akieleza msimamo wake kuwa angependa kuendelea kuwa na mapadri waseja.

Lissu arusha kombora lingine kwa mawaziri

Dodoma. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge, jana walituhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Ilielezwa bungeni jana kuwa Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji jana, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alihoji kile alichokiita upendeleo wa wazi katika ugawaji wa fedha za maji, unaoipa kipaumbele baadhi ya mikoa wanakotoka mawaziri.
Pia aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe anakotokea Dk Mahenge ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa imetengewa Sh1.9 bilioni na kusema: “Upendeleo wa aina hii haufai kwa sababu utaleta matatizo na siyo haki hata kidogo.”
“Profesa Maghembe atueleze sababu za kutenga bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa isiyokuwa na vyanzo vya maji, mito ya kudumu na mabwawa ya maana imepewa bajeti kidogo ikilinganishwa na ile yenye mifumo mizuri ya maji,” alisema Lissu.
Alisema licha ya Profesa Maghembe katika hotuba yake kutaja mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga kuwa inakabiliwa na upungufu wa maji, imetengewa kiasi kidogo cha fedha, huku mikoa inayopata mvua za kutosha na vyanzo vya uhakika vya maji ikitengewa mabilioni ya fedha.
“Dodoma imetengewa Sh7.2 bilioni, Singida Sh3.2 bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni na Simiyu Sh2.8 bilioni, wakati mikoa yenye vyanzo vya maji na mvua za kutosha imetengewa fedha nyingi; mfano ni Tanga Sh10.7 bilioni, Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya Sh9.2 bilioni na Mtwara Sh7.5 bilioni,” alisema.
Lissu alisema hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa mawaziri hao wanatumia mamlaka yao kujipendelea na kuhoji kama huo ndiyo utaratibu wa Serikali ya CCM... “Kama utaratibu wa mgawanyo wa fedha ndiyo huu sisi tunaotoka mikoa yenye ukame tutapataje maji?”
Jana Profesa Maghembe aliendelea kuwa katika wakati mgumu, baada ya kuandamwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye alimwita kuwa ni mzigo kutokana na kutokutolewa kwa fedha za miradi ya maji.
Mnyika alionyesha kushangazwa na wabunge wenzake kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, licha ya kuwa ndogo na fedha za miradi zimekuwa hazitolewi kama inavyotakiwa.
“Kwa kufanya hivi sidhani kama tunamsaidia Profesa Maghembe ambaye ni CCM. Fedha zilizotengwa mwaka jana kuisaidia wizara hii hazijatoka na za bajeti hii hazitatoka kwa kiwango cha kuwezesha utekelezaji. Namna bora ya kumsaidia ili viongozi wa CCM wasiendelee kumwita mzigo ni kuikataa bajeti hii ili Serikali irudi mezani na kujiuliza.”
Mnyika alisema kuwa hata ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa Serikali itaongeza Sh80 bilioni kwa wizara hiyo kabla ya Mei 31 mwaka huu nayo haijatekelezwa na kusisitiza kuwa wabunge wakiipitisha bajeti hiyo watakuwa wameuziwa mbuzi kwenye gunia.
Alisema kuwa hata miradi ya maji jijini Dar es Salaam ambayo Profesa Maghembe aliahidi kuwa itakamilika mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alisema Profesa Maghembe amechota mabilioni ya fedha na kuyapeleka katika miradi ya maji kwenye jimbo lake la uchaguzi wakati maeneo mengine ameyaacha licha ya kuwa yana kipaumbele na kwamba anatumia miradi ya Serikali kujinufaisha kisiasa.
“Ukitaka takwimu zote ninazo hapa, idadi ya watu kwako ni wachache kuliko hata kwangu lakini kwa vipindi viwili mfululizo umekuwa ukijitengea mabilioni ya fedha, wewe ni mzigo kabisa,” alisema Silinde.
Mwandosya amtetea
Wakati akijibu hoja za wabunge, Profesa Maghembe hakugusia tuhuma hizo na badala yake Profesa Mwandosya alimtetea akisema miradi hiyo katika wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati yeye (Mwandosya) akiwa Waziri wa Maji... “Si kweli kwamba Profesa Maghembe anapendelea jimbo lake kwa sababu hakuwa waziri wa wizara hiyo wakati mradi huo unaanzishwa. Wananchi wa Same, Mwanga, Korogwe na Simanjiro wana haki ya kupata maji kama wananchi wa sehemu nyingine yoyote. Mwacheni waziri atekeleze majukumu yake ili watu hawa wapate maji”.
Alisema mradi wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe ni muhimu sana kwa sababu utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 400,000 ambao hawapati maji kabisa.
Alisisitiza kuwa yuko tayari kubeba lawama juu ya mradi huo na si Profesa Maghembe, kwani waziri huyo anafanya kazi nzuri ya kutekeleza mradi huo ambao ulikuwapo hata kabla hajapelekwa katika wizara hiyo.