Saturday 13 December 2014

Necta yatangaza mfumo mpya

Dodoma. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limeanza mfumo mpya wa kupanga matokeo ya kidato cha nne mwaka huu na ya kidato cha sita mwakani, ambapo sasa madaraja yatapangwa kwa wastani wa pointi (GPA) badala ya jumla ya pointi.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Msonde katika mkutano wa wadau wa kampeni ya elimu kwa watoto wa kike walio katika mazingira magumu (Camfed).
Dk Msonde alikuwa akitoa mada kuhusu uwekaji alama za ufaulu unaotekelezwa na Necta.
Alisema mfumo huo siyo mpya kutumiwa na Necta kwa sababu umekuwa ukitumiwa katika kupanga matokeo ya wanafunzi wa vyuo vya walimu.
“Mfumo utakaotumika kupanga madaraja ya mitihani kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa mwaka huu na kidato cha sita mwakani na kuendelea utakuwa si ule wa kutumia jumla ya pointi badala yake utakuwa ni wastani wa pointi,” alisema na kuongeza:
“Utaratibu huu siyo kwamba ni mpya kwa baraza la mitihani, tumefanya hivyo kwa matokeo ya ualimu na hata tunapopanga shule bora tumekuwa tukitumia GPA... Hatubadilishi thamani ya madaraja.”
Alisema kuwa thamani ya madaraja itabaki kuwa ni ile ile bali sasa watakuwa na mfumo unaolingana na kupanga matokeo ya ualimu.
Dk Msonde alisema lengo la kutumia mfumo huo ni kuwezesha kuwa na mfumo unaofanana katika ngazi zote za elimu nchini.
“Lengo jingine ni kuwarahisishia wenzetu wa TCU na Necta na wadahili wengine wawe wanatumia mfumo unaofanana na wa kwetu wasianze tena kubadilisha vyeti,”alisema.
Alisema lengo lingine ni kuelimisha Watanzania kuhusu mfumo huo mpya wa upangaji wa matokeo.
ya mtihani ambapo kwa kutumia mfumo wa jumla ya pointi ilikuwa ni vigumu kuuelewa.
Dk. Msonde alisema kwa mfumo wa kutumia jumla ya pointi watanzania wengi walikuwa wanafikiri mtu akipata pointi nyingi ndio amefaulu zaidi ya wale waliopata pointi chache.Alisema tayari wametoa mafunzo ya uelewa juu ya mfumo huo kwa wadau mbalimbali wa elimu na kwamba wanautambua.

Karatasi za kupigia kura zanaswa D’Salaam

Dar es Salaam. Wakati Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukitarajiwa kufanyika kesho nchi nzima, wafuasi wa (Chadema) na Jeshi la Polisi, wamekamata karatasi zinazodaiwa za kupigia kura kwenye uchaguzi huo za Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, zikirudufiwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Jimbo la Ubungo, Justine Mollel, tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wakati mwanachama wa chama hicho alipokwenda katika duka la vifaa vya shule na ofisini saa 8 mchana kwa lengo la kurudufu karatasi za chama hicho lakini aliambiwa arudi saa 12 jioni.
Gazeti hili lilifanikiwa kuiona moja ya nakala hizo kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo ikiwa na nembo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ikiwa na nafasi ya kupigia kura kwa wagombea wa CCM na Chadema.
Habari zaidi zinaeleza kuwa tayari zaidi ya nakala milioni moja zilisharudufiwa, huku zikiwa zimewekwa alama ya ndiyo kwa mmoja wa wagombea wa vyama hivyo.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema: “Uchunguzi bado unaendelea kwani waliokuwa wanarudufu walijitambulisha kuwa ni wasimamizi wa uchaguzi, hivyo tunaendelea na uchunguzi na hakuna mtu tunayemshikilia.”
Aliongeza: “Nimemwagiza OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) kuwasiliana na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ili kujua hizo karatasi ni kweli zilitakiwa kutengenezwa hapo au la... Kama ni hapo mambo yaishie palepale na kama siyo halali basi hatua zichukuliwe kwa wahusika.”
Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Khalist Luanda alisema kurudufu karatasi za kupigia kura kunatakiwa kufanyika katika wilaya au mkoa lakini siyo nje ya mkoa.
“Ni kosa kuchapa fomu za wagombea kutoka wilaya moja kwenda nyingine walipaswa kurudufu katika eneo kunapofanyika uchaguzi au wilaya husika na mchakato unaopaswa kuwa wa siri sana na siyo kila sehemu kwani haitakuwa rahisi kusafirisha kwa usalama bila kutiliwa shaka.”
Aliongeza kuwa: “Nimesikia katika vyombo vya habari na nimetuma wataalamu wangu kwenda kufuatilia jambo hilo kwani ni makosa na mkurugenzi huyo inaonyesha alikuwa na malengo au masilahi binafsi na kama ni kweli anatakiwa kuwajibika.”
Awali akisimulia tukio hilo Mollel alisema: MwanaChadema alikwenda pale kurudufu karatasi zake kwani gharama yake ni Sh25 kwa karatasi moja na aliambiwa arudi jioni kwani walikuwa na kazi maalumu, hivyo wasingeweza kumrudufia karatasi zake.”
Aliongeza: “Alipokwenda tena saa 12 aliambiwa bado hawajamaliza kazi hiyo maalumu hapo alipata hofu na kuanza kuchunguza kazi iliyokuwa ikifanyika, ndipo alipoona karatasi za kupigia kura zikirudufiwa.”
Mollel alifafanua kuwa alipoona hivyo mfuasi huyo aliwaita wanachama wengine wa Chadema waliozingira duka hilo lililopo maeneo ya Mabibo kabla ya kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mabibo umbali wa takriban mita 100.
Alisema polisi wa Mabibo na baadaye wa Magomeni walipofika waliwachukua wahusika na kuwapeleka Kituo cha Polisi Magomeni kwa ajili ya kuandika maelezo.
Shuhuda ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema: “Niliingia dukani hapo nikakuta wanachapisha hizo karatasi, lakini sikujali sana kwani nilikuwa nina haraka zangu, lakini baadaye niliporudi nikakuta baadhi ya hizo nyaraka zikiwa mezani na ndipo nikagundua kuwa ni nyaraka za siri ambazo hazitakiwi kuonekana kwa muda huo.”
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika kwa vifaa vyote kufika katika maeneo yatakayotumika kwa uchaguzi huo.
Alisema jumla ya wenyeviti wa mitaa 559 na wajumbe 2,795 wanatarajiwa kuchaguliwa. Jumla ya vituo 1,674 vya kupigia kura vitatumika huku masanduku yakiwa 5,022 na karatasi za kupigia kura zikiwa 1.7 milioni.
“Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni, tunawaomba wananchi waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura lakini wazingatie taratibu na sheria za uchaguzi,” alisema Sadiki.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, “Kila chama kihakikishe hakivunji sheria kwani hatutakuwa na hiana na mtu yeyote, ukienda kinyume tutakuchukulia hatua kali bila kujali chama ulicho na wadhifa wako.”
Aliongeza: “Tunawaomba wanawake ambao mara nyingi wamekuwa waoga kwenda kupiga kura wakihofia usalama wao kujitokeza kwa wingi kwani tumejipanga vizuri kiulinzi kuhakikisha uchaguzi unaanza na kumalizika salama.”

Sunday 7 December 2014

Escrow kuing’oa CCM

Kigoma. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema licha ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwadharau Watanzania na kuamini kwamba hawana madhara kwa ustawi wake, kashfa ya uchotaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow itaking’oa chama hicho madarakani.
Kauli hiyo imetolewa wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kuchukua hatua kutokana na mapendekezo manane ya Bunge yaliyotolewa na Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi maalumu wa malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow, uliofanywa na Mdhibiri na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) iliyowasiliwa bungeni hivi karibuni.
Akizungumza alipowasili mjini Kigoma jana, Kafulila alisema kuwa licha ya wananchi kukerwa na tabia ya wizi na ufisadi wa mali ya umma, bado CCM imeendelea kuwadharau kwa vile wananchi hao kila mara wanaunga mkono chama hicho.
“Watanzania wamechoka kulinda wezi na mafisadi, ndiyo maana wakati wa mjadala wa IPTL bungeni nimepigiwa simu nyingi na wananchi waliodai wapo nyuma yangu. Inatia faraja, nami nasema kashfa ya escrow itaing’oa CCM madarakani,” alisema Kafulila.
Alisema nchi ipo njiapanda na hali ni mbaya kwa vile licha ya uchumi kuporwa na watu wachache, Serikali imeshindwa kuwachukulia hatua stahiki wahusika na kuwafikisha mahakamani.
“CCM imeshindwa kumng’oa fisadi mmoja na kumburuza mahakamani. Sasa itawezaje kushughulikia matatizo ya Watanzania ili kuwaondoa katika matatizo?” alihoji Kafulila bila kutaja jina.
Akizungumza na gazeti hili mbunge huyo aliwataka wananchi kuikataa CCM kama kweli wanapenda maendeleo ya dhati.
Alidai kwamba sakata la IPTL limemjenga kisiasa kiasi kwamba anajisikia faraja kupigania masilahi ya umma na kuokoa mabilioni ya pesa ili jamii inufaike na matunda ya nchi.
Wiki iliyopita, mjadala kuhusu uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow uliligawa Bunge katika makundi mawili lilipojadili Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu fedha hizo hoja ikiwa; ni nani mmiliki wa fedha zilizogawanywa kwa watu mbalimbali?
Makundi yaliyodhihirika katika mjadala huo ni kundi la upinzani na wajumbe wa PAC ambalo lilitaka viongozi wa Serikali waliolegalega na kusababisha upotevu wa Sh306 bilioni zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow wawajibishwe.
Kundi jingine lilikuwa halioni kiongozi wa kuwajibishwa kwa sababu fedha hizo hazikuwa za umma. Hili lilikuwa na wabunge wengi wa CCM, wengi wakihoji mapendekezo yaliyotolewa na PAC wakati hayamo katika mapendekezo ya CAG.
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani alisema katika mahojiano ya PAC na CAG hakuna sehemu yoyote ambayo CAG alithibitisha kuwa fedha zile zilikuwa za umma, bali limechomekwa kinyemela na PAC. Jambo hilo lilimfanya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kusimama na kutoa taarifa akisema kuwa katika mahojiano yao na CAG swali la kwanza lilikuwa ni kutaka kujua kama fedha za escrow zilikuwa za nani.

Alieleza kuwa walijibiwa kuwa zilikuwa na sura tatu, kwa maana ya fedha za umma kwa sura ya kodi na fedha za umma kwa sababu mgogoro wa gharama za uendeshaji ulikuwa bado haujaamuliwa.
Mjadala huo ulilifanya Bunge kuandika historia kwa kumaliza kikao saa 4:49 usiku ikiwa ni mara ya kwanza na Spika wa Bunge Anne Makinda alilazimika kuliahirisha hadi siku ya pili kufuatia mvutano kuhusu maazimio ya Kamati ya PAC.
Katika siku iliyofutata Bunge hilo lililazimika kuunda Kamati ya Maridhioano iliyojumuisha wabumge kutoka chama tawala na upinzani na kuja na maazimio ya pamoja kutokana na Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi maalumu wa malipo yaliyofanyika katika akaunti ya Escrow, uliofanywa na Mdhibiri na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).
Akisoma mapendekezo hayo bungeni, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema: “Kwa kuwa Taarifa Maalumu ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalumu wa Malipo yaliyofanyika Katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), umeonyesha Herbinder Singh Seth wa PAP, James Rugemalila wa Kampuni ya VIP, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), imeonyesha walihusika kwa namna moja au nyingine na kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta, kwenda kwa kampuni za Pan African Power Solutions (PAP) na VIP Engineering and Marketing VIP...”
“Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Takukuru, Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya mamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.”
Mjadala huo uliibuliwa bungeni na Kafulila, baada ya gazeti dada la Mwananchi (The Citizens kuliibua).
Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kutunza fedha za gharama za uwekezaji baada ya kuibuka mzozo wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni binafsi ya IPTL ambayo iliingia mkataba wa kufua umeme na kuliuzia nishati hiyo shirika hilo la umma

Friday 5 December 2014

Zitto: Nina sharti moja tu kurudi Chadema

Dar es Salaam. Harufu ya kuisha kwa mgogoro baina ya Zitto Kabwe na chama chake cha Chadema inanukia, lakini mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini anataka kuwapo na mazungumzo kubaini tatizo ili atakayebainika kuwa alifanya makosa awe tayari kuomba radhi hadharani.
Zitto alikiri bungeni kuwa amekuwa “akimiss” harakati zilizokuwa zikifanywa na vyama vya upinzani wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, harakati zilizozaa Umoja wa Katiba ya Wananchi na kufurahia kuhudhuria kwa mara ya kwanza vikao vya umoja huo.
Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alipata fursa ya kuingia vikao vya Ukawa wakati wapinzani walipoungana tena kupambana dhidi ya wizi wa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, sakata ambalo liliwekwa bayana na kamati yake baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kulifikisha bungeni, lakini hakudokeza lolote kuhusu Chadema.
Hata hivyo, mapema wiki hii, Zitto, ambaye Novemba mwaka jana alivuliwa nyadhifa zote kwenye chama hicho kwa tuhuma za kukihujumu, lakini akafanikiwa kulinda uanachama wake baada ya kufungua kesi mahakamani na kufanikiwa kupata amri ya kuzuia asijadiliwe.
Baada ya kuongoza PAC kuchunguza wa tuhuma za Escrow na kufanikiwa kulishawishi Bunge kufikia maazimio manane ya kuwashughulikia kisheria wahusika kwenye uchotwaji huo wa fedha, kumekuwapo na wito kutoka kwa baadhi ya wafuasi wa Chadema kutaka pande hizo mbili zimalizane.
“Kabla ya jambo lolote kufanyika, ili kukata kiu ya Watanzania wanaotaka kuona tunaondoa tofauti zetu, ni lazima kusema ukweli na kila upande kuwa tayari kuomba radhi hadharani pindi ikibainika ulifanya makosa,” alisema Zitto alipotakiwa kuzungumzia harakati hizo za kumrejesha Chadema.
“Ukweli wangu ndani ya Chadema ni nini? Lakini mimi ninaona sina kosa ndani ya Chadema. Ninachotaka mimi nielezwe ukweli bila chembe ya shaka makosa yangu mimi ni nini,” alisema na kuongeza:
“Nitakuwa tayari kuomba radhi hadharani kama ikibainika nilifanya makosa na kama ikibainika chama kilifanya makosa, nacho kiwe tayari kuomba radhi hadharani na ukweli uwe mbele katika maridhiano.
“Kama hakutakuwa na ukweli itakuwa vigumu kupata mwafaka. Mimi sina tatizo. Nirudie nilivyosema bungeni kuwa nina-miss sana (ninapenda sana kuwamo kwenye) harakati za mageuzi kipindi hiki za kuiondoa CCM madarakani.”
Katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kuvuliwa nyadhifa zote, Zitto alisema: “Natambua kuwa wapo ambao wangependa kutumia nafasi zao kudhoofisha mapambano ya siasa za demokrasia nchini mwetu. Napenda wanachama wa Chadema na wapenda demokrasia watambue kuwa, mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki.
“Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina; waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu; na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye binafsi aliguswa na mzozo huo, hakuwa tayari kuzungumzia kumaliza matatizo baina ya chama na Zitto.
No comment (sina maoni) kwa hilo. Siwezi kuzungumzia suala hili katika media (vyombo vya habari),” alisema Mbowe
Hoja ya kutaka Zitto arejeshwe Chadema imekuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii na kwa baadhi ya wanasiasa baada ya kuonekana kuwa karibu na viongozi wa chama chake wakati Kamati ya PAC ilipoibua ufisadi wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow wiki iliyopita.
Wakati akihitimisha mjadala wa sakata la Escrow, mbali na kueleza bayana kuwa alifurahia kuhudhuria vikao vya Ukawa kwa mara ya kwanza, Zitto alikwenda mbali na kumpongeza “kwa namna ya pekee” Mbowe kwa jinsi walivyoshirikiana katika sakata hilo.
Zitto alisema hilo lilikuwa ni jambo la kitaifa ndiyo maana wabunge wote wa upinzani bila kujali vyama vyao waliungana.
Alisema mara baada ya sakata hilo kumalizika watu mbalimbali wamekuwa wakizungumzia kufanyika kwa maridhiano ili awe sehemu ya Ukawa na kwamba haoni tatizo.
“Katika hili, kipekee namshukuru kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuniunga mkono katika sakata hili,” alisema Zitto.
Kuhusu taarifa za kujiunga kwake na chama kipya cha ACT-Tanzania alisema: “Hizo ni taarifa ambazo hazina ukweli wowote.”
Kuhusu kesi aliyofungua mahakamani dhidi ya Chadema, Zitto alisema:
“Nilifungua kesi kwa sababu ya kulinda uanachama wangu, lakini mazungumzo yakifanyika na kujua kosa langu ni nini, nitaifuta kesi hiyo na kuanza upya harakati.”
Zitto.
Kuhusu taarifa za kujiunga kwake na chama kipya cha ACT-Tanzania alisema, “Hizo ni taarifa ambazo hazina ukweli wowote.”
Kuhusu kesi aliyofungua mahakamani dhidi ya Chadema, Zitto alisema: “Nilifungua kesi kwa sababu ya kulinda uanachama wangu, lakini mazungumzo yakifanyika na kujua kosa langu ni nini, nitaifuta kesi hiyo na kuanza harakati.”

RIPOTI: Watanzania wapoteza matumaini

Dar es Salaam. Zaidi ya nusu ya Watanzania wamekata tamaa ya maisha, badala yake wanafikiri hali zao zitakuwa bora miaka kumi ijayo, kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Twaweza pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Kitaifa (SID).
Kutokana na kukata tama, wananchi wa maeneo mbalimbali wamepoteza hata hamu ya kutumia haki zao za msingi, kama kushiriki katika kuchagua viongozi wao wa ngazio mbalimbali, kwa mujibu wa utafiti huo.
Utafiti huo uliofanywa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara mwezi Agosti mwaka huu kwa kuhoji watu 1,408 unaonyesha kwamba Watanzania wanaamini kuwa maisha yao yatakuwa bora mwaka 2015.
Matokeo ya utafiti huo uliopewa jina la ‘Tanzania Ifikapo Mwaka 2025: Je, Watanzania Wana Matarajio Gani na Maisha Yao ya Baadaye?, yamebainisha kuwa kwa kuangalia nchi kwa jumla, wananchi wawili kati ya watatu wanaamini kuwa Tanzania itakuwa mahali pazuri pa kuishi baada ya miaka 10 ijayo.
“Wananchi wa makundi yote bila kujali hali zao za kiuchumi, wanaamini hivyo. Wananchi wenye kipato kikubwa, asilimia 64 na wananchi maskini asilimia 68 wana matumaini na siku zijazo. Watanzania wana matumaini na akiba tuliyonayo kwa ajili ya nchi,” inaeleza taarifa ya matokeo ya utafiti huo.
“Baadhi ya wananchi bado wana wasiwasi na karibu mwananchi mmoja kati ya watano anahofia maisha yake yatakuwa mabaya zaidi mwaka 2025 kuliko yalivyo leo, na wapo wengine wanaodhani nchi itakuwa mahali pabaya pa kuishi mwaka 2025.
“Kuna baadhi ya tofauti kati ya matajiri na maskini, mwananchi mmoja kati ya wanne katika kundi la matajiri na mmoja kati ya watano katika kundi la maskini hawana matumaini ya siku zijazo.”
Utafiti huo unaendelea kueleza kuwa, wananchi tisa kati ya 10 wanaamini kuwa viongozi (asilimia 54) au wananchi (asilimia 37) watakuwa na udhibiti zaidi wa maamuzi ya nchi yao, lakini linapokuja suala la maisha yao wenyewe, wananchi wanaamini jitihada zao wenyewe kuwa ndizo zitazobadilisha maisha yao.
Wananchi sita kati ya kumi, wanafikiri kuwa wao wenyewe ndio w enye ushawishi zaidi juu ya hatma yao ya baadaye wakati mwananchi mmoja kati ya watano anaamini kuwa Serikali itakuwa na ushawishi mkubwa juu ya ustawi wa maisha yao ya baadaye.
Hata hivyo, katika utafiti huo, hakuna hata mwananchi mmoja wa mjini aliyetaja Serikali kama ina ushawishi muhimu. Mbali na wao wenyewe, wahojiwa wa mijini walitaja familia zao na marafiki au wenzao kuwa wenye ushawishi kuhusu ya maisha yao ya baadaye.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, mkurugenzi wa SID, Aidan Eyakuze alisema: “Watanzania kwa kiasi kikubwa wana matumaini na maisha yao binafsi ya baadaye, hasa ikilinganishwa na wenzao kutoka nchi zenye maendeleo makubwa kiuchumi, Marekani na Ulaya.
“Matumaini haya na mtazamo chanya ni mtaji mkubwa. Vinaimarisha uwezo wa nchi kusonga mbele kwa kujiamini na pia inaweka mzigo kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya mafanikio kwa nchi yetu.”
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa Twaweza, Rakesh Rajani, alisema: “Katika kipindi cha mabadiliko muhimu ya kitaifa na ya kimataifa, wananchi wa matabaka yote kiuchumi, maeneo na jinsia zote, wana matumaini ya kile kilichopo siku za baadaye nchini Tanzania.
“Changamoto kwa Serikali, wasomi wa ndani pamoja na wananchi wenyewe, ni kuhakikisha kuwa matumaini haya yanaendelezwa kupitia utungaji sera na utekelezaji wenye ufanisi, kuhimiza maendeleo yenye usawa na kujenga mshikamano wa kijamii, ili matarajio ya wananchi ya maisha bora siku zijazo yafikiwe.”
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mtafiri Elvis Mushi wa Twaweza alisema mtazamo huo ni tofauti kabisa na ule wa nchi za Marekani na Ulaya ambapo karibu wananchi saba kati ya kumi ambao ni asilimia 65, wanafikiri kuwa watoto wao watakuwa na hali mbaya zaidi kifedha kuliko walivyo wao sasa.
Hata hivyo, Mtafiti kutoka SID, Edmund Matotay alisema utafiti walioufanya na kulinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki unaonyesha kwamba uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi nzuri zaidi kwa sasa kuliko nchi nyingine, huku sekta ya huduma ikishika kasi zaidi ya sekta za uzalishaji na kilimo.

Mbowe: Tutazuia uchaguzi wa Mitaa mahakamani ikiwa...

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kama hali ya kuwaengua wagombea wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa itaendelea kama ilivyo sasa, basi wataupinga uchaguzi huo mahakamani.
Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa operesheni mshikemshike mzizima uliofanyika Vijibweni Kigamboni.
“Tangu kampeni zianze kumekuwa na tabia ya kuengua wagombea wetu kiholela. Tumeshaweka angalizo mahakamani na kama hali ikiendelea hivyo tutaupinga uchaguzi mahakamani.”
Alisema baada ya kuibuka kwa tabia ya wagombea kuenguliwa aliwasiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimsihi alitizame kwa kina suala hilo kwa sababu wagombea walienguliwa kimakosa.
“Alisema atalifanyia kazi lakini naona bado hali hiyo inaendelea na alisema atazungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuhusu jambo hili.
Nilipowasiliana naye mara ya pili alisema kama tunataka ushindi uchaguzi uwe wa haki. Kuona hivyo tumekwenda kutoa angalizo mahakamani,” alisema.
Aliongeza, “Tukutane katika uchaguzi na tuone nani ni bingwa kati ya CCM na Ukawa baada ya kutumia njia za mkato kama wao wanavyofanya.
Hata sisi hatutaki ushindi wa dezo ila wakitumia dola kutuyumbisha kamwe hatutokubali maana polisi wamekuwa wakitumika kama mawakala wa uchaguzi. Hilo halitakubalika.”
Aliwataka wananchi kutokaa mbali na vituo vya kupigia kura mara baada ya kuwachagua viongozi wanaowataka huku akisisitiza, “Msikubali kura zikahesabiwe sehemu nyingine watazichakachua.
Hata katika sheria za Uchaguzi hakuna sehemu inayosema baada ya kupiga kura, mpigakura anatakiwa kukaa umbali wa mita 100 kutoka katika kituo cha kupiga kura. Tumeweka mawakala nchi nzima kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.”
Alisema hakuna dhambi mbaya kama wananchi kushindwa kuleta mapinduzi ndani ya nchi yao, hasa nchi kama Tanzania ambayo ina kila aina ya umasikini.

IPTL yazua Kizaazaa Mahakamani

Dar es Salaam. Kampuni za Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), zimewasilisha maombi ya kutaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akamatwe kwa kukiuka amri ya Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) kwa kufuta Hati za Malipo ya Kodi za Mauzo ya Hisa (Capital Gain Certificate).
Kampuni hizo mbili, ambazo ziko kwenye mgogoro wa umiliki, ndizo zinahusika kwenye sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya kuuza umeme unaofuliwa na IPTL, kwa Shirika la Umeme (Tanesco), wakati wa kusubiri uamuzi wa mahakama katika kesi ya kupinga tozo hilo.
PAP, ambayo inadai imenunua hisa zote za IPTL, ndiyo iliyolipwa fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kuamsha mjadala mkubwa bungeni ulioisha kwa Bunge kufikia uamuzi wa kuwawajibisha kisheria wote waliohusika, wakiwemo mawaziri.
Lakini uamuzi huo wa Bunge haukuwa tamati la sakata hilo baada ya kampuni hizo mbili kukata rufaa TRAB dhidi ya Kamishna wa TRA na Msajili wa Kampuni na Leseni (Brela) zikipinga kusudio la kufuta hati hizo.
Jana kampuni hizo mbili ziliwasilisha maombi ya hati ya kutaka Kamishna Mkuu wa TRA akamatwe, zikidai kuwa amepuuza amri hiyo iliyomzuia kutekeleza azma yake ya kufuta Hati za Malipo ya Kodi ya Mauzo ya Hisa.
Katika maombi hayo walalamikaji hao wanadai kuwa licha ya TRAB kutoa zuio hilo Novemba 26, 2014, Kamishna Mkuu wa TRA, ambaye ni mlalamikiwa wa kwanza, alitoa amri ya kuziondoa hati hizo siku iliyofuata, yaani Novemba 27, 2014, bila kujali amri hiyo.
Walalamikaji hao pia wanaiomba TRAB, baada ya kumkamata Kamishna Mkuu wa TRA, itoe amri afungwe kwa kudharau amri halali iliyotolewa na bodi na pia imwamuru akidhi matakwa ya amri ya TRAB ya Novemba 26.
Pia walalamikaji hao wanaiomba TRAB imwamuru mlalamikiwa huyo, kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo pamoja na amri nyingine ambazo itaona kuwa zinafaa.
Maombi hayo ya PAP na IPTL ya hati ya kumkamata na kuamuru Kamishna Mkuu wa TRA afungwe yamepangwa kusikilizwa leo na Katibu wa TRAB, Respicius Mwijage.
Hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo inaeleza kuwa mlalamikiwa, akiwa ni raia wa Tanzania, siyo tu kwamba alipaswa kuwa mtiifu kwa mamlaka ya bodi hiyo, bali pia alipaswa kutekeleza sheria za nchi ambazo bodi hiyo ni sehemu yake.
Hati hiyo ya kiapo ya mkurugenzi wa operesheni wa IPTL, Parthiban Chandrasakaran, inaeleza kuwa kwa kitendo hicho cha kutotii amri ya bodi hiyo, mlalamikiwa amepoteza sifa ya kuwa mtumishi wa umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia inaelea kuwa kama bodi hiyo isipotumia mamlaka yake kukubali maombi hayo ya kutoa amri inayoombwa, basi walalamikaji watapata hasara isiyoweza kufidiwa.
Inafafanua hasara hizo kuwa ni pamoja na kodi nyingine ambazo tayari PAP wamelipa TRA kwa ajili ya kuendesha biashara.
Pia hati hiyo ya kiapo inafafanua kuwa kuondolewa kwa hati hizo kutahatarisha biashara ya walalamikaji ambayo wamekuwa wakiiendesha tangu walipota hati hizo.
Inaendelea kueleza kuwa kwa kuwa walalamikaji wako katika hatari ya kuvunja mkataba na Shirika la Umeme (Tanesco), na wadau wengine, jambo hilo litasabaisha vita ya kimahakama na hivyo kulipa fidia zisizo za msingi.
Hati hizo namba 004965600 na 0049657 zilitolewa na TRA Desemba 23, 2013, kwa ajili ya uuzaji wa hisa baina ya kampuni ya Mechmar Corporation (Malaysia) Berhard iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa za IPTL na Piper Links Investment Limited na kati ya Piper Link na PAP.
Hata hivyo baadaye, Novemba 19, 2014 TRA ilitoa taarifa ya siku sita kwa Brela ikionyesha kusudio la kuziondoa hati hizo kwa madai kuwa mkataba wa madai ya mauzo ya hisa hizo ulikuwa ni mkataba wa makubaliano ya uongo.
Wakati Huohuo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kitendo cha kushindwa kuwachukulia hatua wanaotuhumiwa kuchota Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow hadi sasa, ni ishara ya kuwa na Serikali dhaifu.
Mbowe, ambaye ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema viongozi waliotuhumiwa kwenye kashfa hiyo walitakiwa wawekwe kando kabla ya hatua zaidi.
“Leo (jana) ni siku ya tano na Rais Kikwete ameshindwa kutoa uamuzi wowote. Hii inaonyesha jinsi tulivyo na Serikali dhaifu,” alisema Mbowe wakati akihutubia mkutano wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwenye Kata ya Vijibweni, Kigamboni.
“Hadi leo Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka bado yupo ofisini na anasaini nyaraka mbalimbali za viwanja. Inakuwaje hadi leo wezi bado wapo ofisini?”
, kwanini wanalindwa?” alihoji.
“Wanapewa muda wa kukaa ofisini kujipanga ili hata Rais Kikwete atakapochukua uamuzi, wawe wamejipanga na kuchukua kidogo kilichokuwepo.”
Mbowe alisema sakata la Escrow lilitikisa nchi na kwamba kitendo cha watuhumiwa kutochukuliwa hatua hadi leo tafsiri yake ni kwamba viongozi wa Serikali wanalindana.