Friday 22 November 2013

Shivji auponda mchakato Katiba Mpya

Asema umehodhiwa na wanasiasa na kutahadharisha usipoangaliwa unaweza kuzaa machafuko.
Dodoma.  Mwanazuoni na  Mwanasheria nguli, Profesa Issa Shivji  ameuponda mchakato wa Katiba Mpya kuwa umehodhiwa na wanasiasa na kutahadharisha kuwa usipoangaliwa vizuri unaweza kusababisha machafuko.
Aliyasema hayo jana mjini hapa alipokuwa akitoa mhadhara kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udom). Mhadhara huo uliandaliwa kama sehemu ya mafunzo kwa ajili ya wanafunzi wanaojiandaa kuhitimu masomo yao (Convocation ).
Profesa Shiviji ambaye alitumia saa 1.15 kutoa mhadhara wake juu ya mchakato wa Katiba, alisema Bunge la Katiba lipo juu ya Bunge la Kawaida.
Alisema katika historia ya Tanzania imewahi kuwa na mabunge mawili yaliyoandaliwa kupata Katiba, lakini yote hayakuwa na wabunge waliochaguliwa.
“Tukiangalia katika historia hatukuwahi kuwa na Bunge la Katiba ambalo lilichaguliwa na wananchi. Safari hii tulikuwa na nafasi ya kuwa na Bunge ambalo lilichaguliwa na wananchi lakini kwa bahati mbaya hakuna nafasi ya kufanya hivyo ,”alisema.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, wabunge wote 357 na Wawakilishi 81 watakuwa ni wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba huku mashirika yasiyo ya kiserikali yakipewa wawakilishi 20.
Wajumbe wengine ni vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu 42, wawakilishi wa taasisi za elimu ya Juu 20, watu wenye mahitaji maalumu (20), vyama vya wafanyakazi (20), wafugaji (10), wavuvi (10), wakulima (20) na makundi mengine yenye mahitaji muhimu ni wawakilishi (20).
Profesa  Shivji  alisema Bunge la Katiba litakuwa na jumla ya wabunge  639, ambapo 438 asilimia 69  ya wabunge wa Bunge hilo wanatokana na vyama vya siasa.
Alisema kati ya wabunge hao kutoka vyama vya siasa asilimia  52 ni Wana-CCM na asilimia 16  ni kutoka vyama vya upinzani.
“Katika wajumbe 42 watatokana na vyama vya kisiasa, kwa hivi itafanya jumla ya wabunge la Katiba ambao watatokana na vyama vya siasa kuwa ni asilimia 75;
“Kama hesabu zangu ni sahihi ama zinakaribia wabunge wanaotokana na CCM watakuwa ni  asilimia 63, wapinzani asilimia 27 na wasiokuwa na chama ni asilimia 10,”alisema.
Alisema kwa kuangalia idadi ya wajumbe wanaotokana na mashirika yasiyo ya kiserikali wana uwiano sawa na wawakilishi wa mashirika ya wavuja jasho yaani wakulima, wavuvi, wafugaji na wanazuoni.
Alihoji mashirika yasiyo ya kiserikali yanawawakilisha kina nani katika Bunge hilo na mashirika hayo bila ya aibu yamejigeuza kuwawakilisha wananchi wakati hiyo siyo sahihi kwa kuwa hawahusiki na wananchi moja kwa moja.
“NGO’s zina nafasi ya wawakishi sawa, lakini si wawakilishi wa wananchi hawakuchaguliwa na wananchi, wala hawawajibiki kwa wananchi hali halisi wanawajibika zaidi kwa wafadhili, katika sheria  hii NGOs ndio wamepewa kipaumbele kana kwamba ni sawa na wananchi,” alisema Shivji na kushangiliwa.
Kwa upande wa kura ya maoni, Profesa Shivji alikikosoa kipengele katika sheria ya kura ya maoni ambayo inatarajiwa kuletwa Bungeni katika mkutano wa 14 wa Bunge.
Alisema katika sheria hiyo inataka ili jambo likubaliwe ni lazima lipate kura za ndiyo asilimia 50 kwa kila upande muungano.
Alisema hilo litafanya watu wachache waamue kwa ajili ya walio wengi.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo asilimia 50 inayotakiwa ni ya kura halali na wala si inayotokana na idadi ya wapiga kura waliopo kisheria katika Bunge hilo.
Aidha, Profesa Shivji aliwataka wasomi wanapoona mambo yanaharibika kusema badala ya kusubiria mambo yaharibike ndipo waseme.
Alisema mchakato mrefu katika kupata Katiba ni muhimu sana na hautakiwi kuharakishwa.
“Jambo hili linatakiwa kuwa na muda wa kutosha badala ya kuweka ratiba ya miezi, miaka, unatoa mwanya kwa matapeli wa kisiasa kupenyeza na wanaweza kuleta vurugu kubwa sana,”alisema.
Alisema suala la kuwapa wataalamu kuandika Katiba bila ya kuwa na sheria ni kuwapa nafasi wanasiasa kuuvuruga.

Hofu yatanda Kamati Kuu Chadema

Dar es Salaam. Hali ya wasiwasi iligubika eneo  kinapofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichoanza Dar es Salaam jana.
Ulinzi mkali wa walinzi wa Chadema (Blue Guard), uliimarishwa katika ukumbi wa Ubungo Plaza kinapofanyika kikao hicho ambacho kinatarajiwa kumalizika leo, huku kukiwa na maagizo yaliyoashiria kuwapo kwa mambo mazito.
Maazimio ya kikao hicho yanasubiriwa kwa hamu na wafuatiliaji wa mambo ya siasa nchini kwani kinafanyika katika kipindi ambacho chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapita katika misukosuko na hasa ya malumbano baina ya makamanda wake wa juu.
Maelekezo ya ulinzi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili ukumbini hapo saa 5.20 asubuhi na baada ya kuingia, wapiga picha waliruhusiwa kuingia kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo kwa dakika moja tu.
Waandishi wa habari hawakutakiwa kuingia na badala yake walielezwa kuwa wangepewa taarifa baadaye.
Wakati wapiga picha wakiwa ndani, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo alitoka na kutoa maelekezo kwa walinzi wa Chadema akiwataka kuwa makini kutekeleza kazi yao watakapopewa amri ya kumwondoa mjumbe yeyote mkutanoni.
“Kama mkipewa amri ya kuondoa mtu ingieni na mtekeleze amri hiyo mara moja,” alisisitiza mjumbe huyo na kuingia ndani haraka. Walinzi hao zaidi ya 10, walipokea maelekezo hayo kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana na amri hiyo.
Kikao kufunguliwa
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa dakika nane baada ya Mbowe kuwasili, kilipangwa kujadili mambo matatu jana.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kingepitia taarifa za vikao viwili vya Kamati Kuu vilivyopita.
Suala jingine ambalo lilipangwa kujadiliwa jana ni ushiriki wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar na kupitia taarifa ya fedha.
Leo moto
Ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa leo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa Kampeni ya ‘Movement For Change’ (M4C) na hali ya siasa.
Ajenda hiyo inatazamiwa kugusa matukio ya hivi karibuni ndani ya chama hicho. Hayo ni pamoja na malumbano kati ya Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara na pia kuondolewa kikaoni kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku posho na pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa kuhujumu chama hicho.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuwa iliandaliwa na Idara ya Upelelezi ya Chadema, ilieleza kuwa Zitto alikuwa akipokea fedha kutoka kwa maofisa wa usalama na kuzisambaza kwa makada wengine wa chama hicho ili wafanye kazi ya kukihujumu. Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mnyika ilitoa taarifa kupinga vikali suala hilo.
CAG kukagua ruzuku

Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na CAG. Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo.
Suala jingine linalotazamiwa kujadiliwa katika kikao hicho ni kusimamishwa kwa Mwigamba na Baraza la Uongozi Kanda ya Kaskazini ambako kulizuka vurugu kiasi cha kunyang’anywa kompyuta mpakato (laptop) baada ya kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Suala lake linasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kama lile la kuvunjwa kwa uongozi wa Chadema wa Mara.
Pia kitendo cha Baraza la Kanda ya Ziwa Mashariki kumtimua Shibuda kwa madai kwamba halina imani naye nacho kina uwezekano mkubwa wa kujadiliwa.
Zitto na Mnyika wakosekana
Zitto na Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho,  John Mnyika walikuwa miongoni mwa wajumbe walioshindwa kuhudhuria jana.
Zitto yuko na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) huko Sudan Kusini na Mnyika pia yuko katika ziara ya kibunge Uturuki.
Kikao cha jana kilihudhuriwa na wajumbe 23 kati ya 32.

Wednesday 20 November 2013

Viongozi AU wamejidhalilisha kesi ya ICC

Baada ya wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), kutumia mabilioni ya fedha za walipakodi wa nchi zao kufanya kampeni ulimwengu mzima kwa lengo la kuwanusuru Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na makamu wake, William Ruto wasishtakiwe katika Mahakama ya Uhalifu (ICC), hatua ya Baraza la Usalama kulikataa Azimio hilo wiki iliyopita bila shaka itakuwa imeufedhehesha na kuufadhaisha Umoja huo mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Rais Kenyatta, Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang walifunguliwa mashtaka ICC kwa kuhusishwa na vurugu zilizotokea Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,500 walipoteza maisha, huku maelfu wakiachwa bila makazi. Katika hatua ya kushangaza, viongozi hao wa AU waliamua kuinunua kesi hiyo kwa kutishia kwamba wangezitoa nchi zao katika Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC iwapo mashtaka hayo yasingefutwa.
Baada ya mkakati huo kukwama walikuja na kitu kipya. Kwamba ICC imekuwa na sera za kibaguzi dhidi ya viongozi weusi barani Afrika na kusema ndiyo maana inawalenga viongozi hao pekee. Lengo lilikuwa kuwachochea raia wa nchi zao barani Afrika waione ICC kama chombo cha kikoloni na chenye ubaguzi dhidi yao na viongozi wao, hivyo wazishinikize serikali zao kujitoa uanachama wa Mahakama hiyo. Viongozi hao walitegemea raia wa nchi zao wafanye maandamano na kuilaani ICC na mataifa yote yanayoiunga mkono.
Kinyume chake, vyombo vya habari na asasi za kiraia barani humo viliwaelimisha na kuwahamasisha wananchi ili watambue njama za viongozi wa nchi zao zenye lengo la kuitenga ICC ili kuendeleza ubabe na utawala wa mabavu, ukandamizaji, uvunjaji wa haki za binadamu na mauaji ya raia wasio na hatia.
Hata hivyo, hata baada ya njama hizo kugundulika, viongozi hao kupitia AU walibadili mbinu na kuitaka ICC ihamishie kesi hiyo barani Afrika, hasa nchini Kenya au Tanzania kwa maelezo kwamba Afrika ina uwezo wa kujiamulia mambo yake yenyewe. Mbinu hiyo pia ilishindwa, kwani ICC iligundua kwamba Afrika haina mfumo wa kimahakama ulio imara wa kuwawajibisha viongozi wa nchi wanaokiuka haki za binadamu.
Pamoja na AU kuwachochea washtakiwa wasihudhurie kesi zao ICC, wao walisema watahudhuria, pengine kwa kutambua athari na madhara ya kutokufanya hivyo. Ruto tayari amehudhuria kesi yake na Rais Kenyatta atafanya hivyo Februari 2014. Hapo ndipo AU ilipolazimika kutupa karata ya mwisho kwa kuandaa Azimio na kuliwasilisha katika Baraza la Usalama la UN, ikitaka kesi za kina Kenyatta ziahirishwe kwa mwaka mmoja ili viongozi hao wakabiliane na tishio la usalama nchini Kenya kutokana na tukio la kigaidi lililotokea jijini Nairobi hivi karibuni.
Hata hivyo, mbinu hiyo pia imeshindwa, baada ya Baraza la Usalama kulikataa Azimio hilo wiki iliyopita. Ni aibu iliyoje kwa viongozi wa Afrika kuwakingia kifua watawala wenzao, pasipo kujali waathirika wa ghasia za mwaka 2007, ambao wamesubiri kwa muda mrefu kupata haki zao pasipo mafanikio. Sisi tunasema uamuzi wa Baraza la Usalama ni ushindi kwa wana wa Afrika, wakiwamo wananchi wa Kenya ambao theluthi mbili walisema kupitia kura ya maoni wiki iliyopita kwamba kesi dhidi ya Rais Kenyatta na wenzake ziendelee kusikilizwa ICC.

Wednesday 6 November 2013

Sumaye amvaa Lowassa hadharani

Dar es Salaam.Vita ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 imeingia katika sura mpya baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kumlalamikia mrithi wake katika wadhifa huo, Edward Lowassa akimtuhumu kumfanyia mbinu chafu.
Huku akinukuu habari iliyoandikwa na gazeti hili Septemba 16, 2013 yenye kichwa cha habari, ‘Lowassa afichua siri ya mradi wa maji Ziwa Victoria’, Sumaye alisema Lowassa amekuwa akimfanyia propaganda na mbinu chafu.
Katika habari hiyo, ambayo Lowassa alialikwa katika Harambee ya kuchangia Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT huko Kahama, Shinyanga hivi karibuni, alikaririwa akisema mawaziri watatu, tu ndiyo waliounga mkono wakati alipopendekeza kutekelezwa kwa mradi huo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri cha Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa chini ya Benjamin Mkapa.
Lowassa, ambaye katika kipindi hicho alikuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, aliwataja mawaziri waliounga mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Mohamed Seif Khatibu, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sumaye
Alisema hizo ni mbinu chafu zilizokuwa na lengo la kumpaka matope… “Najua mhusika ametumia sana mradi huu kisiasa na sisi wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli kuhusu mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa Waziri Mkuu na mradi umetekelezwa chini ya uangalizi wangu,” alisema na kuongeza:
“Kama Waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi mkubwa hivyo peke yake, akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma? Mbona hata bado kuna kuna sehemu za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya maji?” alihoji Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika Serikali ya Awamu ya Tatu.
Alipotafutwa kwa simu kuelezea madai hayo, Lowassa, ambaye yuko Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, alisema hawezi kubishana na Sumaye kwa kuwa anamheshimu kwani amewahi kuwa kiongozi mkubwa serikalini.
“No comment’ (sina la kusema), siwezi kubishana na Sumaye kwani amewahi kushika nyadhifa za juu katika nchi hii,” alisema Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Sumaye alimtuhumu Lowassa kwa kusema uongo na kuongeza kuwa amefanya kosa la jinai kutoa siri za Baraza la Mawaziri.
“Pamoja na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo mkavu, mhusika kama waziri mwandamizi wakati huo na sasa anawinda nafasi kubwa katika nchi, hakutegemewa kutoa siri za Baraza la Mawaziri, labda amediriki kufanya hivyo kwa sababu anajua anayosema siyo ya kweli, vinginevyo ni kosa la jinai na akishtakiwa anafungwa jela,” alisema.
Sumaye alisema hizo ni mbinu chafu zinazofanywa dhidi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015

“Ziko mbinu nzuri na za kistaarabu na ziko mbinu chafu kama za kupakana matope (character assassinations). Mtu wa kwanza anajisafishia njia yake kwa kufyeka miiba na kuondoa magogo njiani ili wakati ukiwadia, mbio zake zisikwazwe na vigingi vyovyote. Aina ya pili ya mbinu chafu ni pale mhusika anapotengeneza mbinu za kuwamaliza wengine wanaodhaniwa kuwa washindani wake,” alisema Sumaye.
Hata hivyo, alipoulizwa kama amejipanga kugombea urais mwaka 2015, Sumaye alisita kujibu kwa muda mrefu, lakini baadaye akajibu:
“Nasema hivi, kama ni kugombea nina haki zote, kama ni uwezo ninao, kama ni imani ya Watanzania kwa sehemu kubwa ninayo. Kilichobaki ni uamuzi tu wa mimi kutamka. Kwa hiyo sijatamka msije mkasema nagombea urais. Nasema tu na mimi katika Watanzania wanaofikiriwa na mimi nasikia nimo. Kwani ninyi hamnifikirii? Sasa itakapofika huko mbele, si tutaamua wakati huo?”
Kuhusu hujuma zinazofanywa katika shughuli za jamii kwa maslahi ya siasa, Sumaye alisema kuna watu wanaomfanyia hujuma na kuzuia mialiko yake.
Alitoa mfano wa mwaliko wa Oktoba 27 mwaka huu wa kupokea maandamano ya kikundi cha Joggers katika shughuli, ambayo ilikuwa ifanyike Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
“Dakika za mwisho nikapewa taarifa kuwa shughuli imeshindikana kwa sababu imeingiliwa na kikundi chenye kulinda masilahi yake au ya mtu wao. Shughuli hiyo baadaye ilifanyika na kupatikana ‘mgeni rasmi’ mwingine,” alisema.
Hata hivyo, katika hatua nyingine, Shirika la Faita Jogging Sports Clubs limekanusha kumwalika Sumaye kwenye shughuli yao ya Mnazi Mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa shirika hilo, Steven Kaema alisema shirika hilo halikufanya mawasiliano ya aina yoyote na Sumaye tofauti na anavyodai.
“Hatukuwa na mawasiliano yoyote na Sumaye, sisi tulituma barua ya mwaliko kwa Makamu wa Rais ambaye alitujibu kuwa hatakuwepo siku hiyo na tulituma barua nyingine kwa Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulugo ambaye naye alijibu kuwa atasafiri kwa hiyo ofisi yetu haina barua yoyote ya kumuomba Sumaye kuwa mgeni rasmi,” alisema Kaema.
“Mara ya pili ni mwaliko wa kuzindua Saccos ya Nshamba Muleba, Kagera, Oktoba 28,” aliendelea Sumaye… “Mwaliko huu sikuomba, bali viongozi wa chama walinipendekeza kwa sababu zao wenyewe. Wakati najiandaa kwenda, nikaambiwa shughuli zimeingiliwa na watu fulani kwa kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa Saccos.”
Alipotakiwa kuwataja watu hao anaodai kuwa wanamhujumu, Sumaye katika mialiko yake, alijibu:
“Siwataji, hata ninyi mnawajua. Nataka niwataaarifu hao wanaohangaika na mialiko yangu kwa taarifa yao ninayo mingi mpaka mingine nakosa muda wa kuhudhuria. Siitwi kwa sababu ya fedha maana wanajua sina fedha za aina hiyo maana sijaiibia nchi na watu wake,” alisema Sumaye
Alidai kuwa wanaomhujumu wanafanya hivyo ili kumzima asizungumzie rushwa, ufisadi na dawa za kulevya… “Fisadi huliibia taifa fedha nyingi kiasi cha wananchi kutaabika halafu huja kutoa kijisehemu cha fedha alizofisadi kwa njia ya rushwa kukandamiza maendeleo ya watu.”
Rushwa CCM
Sumaye alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kupambana na rushwa na kutahadharisha kuwa tatizo hilo linaweza kukiangusha chama hicho. Aliahidi kuwa na Rais bega kwa bega katika vita hiyo.
“Rais Kikwete amesema kuwa rushwa inaweza ikafanya chama hiki kikashindwa. Mimi naamini, kama CCM itapitisha majina kwa kuangalia rushwa bila kujali, chama kitaanguka, bahati nzuri Mwenyekiti ameliona hilo, siamini kama watapitisha watu ambao watakiangusha… waliopitishwa kama hawataenguliwa, sitaweza kukaa nao, hata kama sitahama.”

Vita ya Lema na Zitto yafika pabaya

Dar es Salaam. Vita vya maneno kati ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe imefika pabaya.
Vita hiyo ya maneno iliyoanzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita kwamba Zitto anafanya unafiki kukataa posho, jana iliingia katika hatua nyingine baada ya mwakilishi huyo wa Arusha kumshushia tuhuma Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema kuwa, suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususani mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Katika hoja yake, Lema alisema kuwa Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) anakataa posho ya Sh70,000 kwa kikao kimoja cha Bunge, lakini anapokea Sh700,000 mpaka Sh1,000,000 kwa kikao kimoja cha kamati yake na haswa vile vinavyoandaliwa na mifuko ya jamii.
Hata hivyo, zitto alikanusha shutuma hizo akimtaka Lema kutoa ushahidi kama kuna mjumbe yoyote wa kamati ya PAC anayepokea posho, huku akieleza kuwa hawezi kubishana na Mbunge huyo wa Arusha mjini kwani yeye Zitto ni kiongozi wake ndani ya Chadema.
“Naomba kutaja masilahi yangu katika hili, wabunge wa kawaida wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa Sh500,000 kwa kikao kwa siku . Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na nikalipwa hivyo pamoja na chai na chakula cha mchana.” alisema Lema.
Lema alisema posho hizo za wabunge ni tofauti na zile za Mwenyekiti wa PAC kwani yeye pamoja na posho ya Sh700,000 mpaka Sh1,000,000 hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege ya kumtoa alipo na kumrudisha na kukodiwa hoteli yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo kwa siku gharama yake ni Dola za Marekani 100 mpaka 600 kwa siku .
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi alikwisha piga marufuku kwa PAC kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
“Toka nimekuwa Mwenyekiti wa POAC (Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma) sio tu nilipiga marufuku posho bali pia niliwashitaki PCCB (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa) wabunge wanaochukua posho kutoka kwa taasisi za Serikali,” alisema Zitto.
Alieleza baada ya hatua hiyo, wabunge walihojiwa na PCCB kuhusu jambo hilo mpaka aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Samuel Sitta alipoingilia kati na kuwatetea wabunge hao.
“Hiyo ilikuwa mwaka 2009 kabla hata Lema hajawa mbunge, wajumbe wa kamati ya PAC wanalipwa posho za vikao kama wabunge wengine, lakini mimi sichukui posho hizo za vikao,” alisema na kuongeza:.
“Sio tu PAC hata kwenye Baraza la Madiwani na Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma na popote kule. Hata NGO (Mashirika yasiyo ya Kiserikali) zikinialika kwenye vikao vyao sichukui posho za vikao. Nafasi yoyote ninayoalikwa kama mbunge sichukui posho za vikao,” alisema Zitto

Alisema mtu yeyote mwenye ushahidi wa yeye kuchukua posho za vikao popote pale auweke hadharani na atawajibika.
“Sio kuandika uzushi au maneno ambayo mtu yeyote anaweza kuandika. Mimi siwezi kubishana na Lema maana ni kiongozi wake katika chama. Natumaini kadiri anavyokaa kwenye uwanja huu wa siasa atabadilika na kukomaa zaidi,” alisema Zitto.
Kwenye hoja yake, Lema alisema kuwa Chadema walikuwa wanakataa posho na kupendekeza mishahara ipandishwe na posho zisizo za lazima ziondolewe ili kuondoa mwanya wa ubadhirifu wa fedha za umma.
“Huu ndio uliokuwa msimamo wetu kulikuwa na msingi mkuu ambao ungekuwa na faida kubwa kwa nchi na watu wake,” alisema Lema.
Lema alisema kwamba kabla msimamo huu haujawekwa hadharani na kutafsiriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto tayari alishatoka katika vyombo vya habari na kujipambanua kuwa yeye hataki posho na wala hatachukua posho.
Lema alisema kuwa, anaamini kuwa umaskini siyo uzalendo. “Sipendi umaskini, nachukia umaskini, pia sipendi kuona mafanikio yangu yanabaki kwangu tu huku wengine wakiteseka, lakini siwezi pia kukumbatia umaskini kwa lengo lakuthibitisha uzalendo wangu.
Najua watu wa jimbo langu wanataka maji , umeme na huduma bora za afya na mambo mengi yenye sura hii, lakini sitang’oa bomba la maji nyumbani kwangu kwa sababu jirani yangu hana maji ila nimtasaidia kwa kadiri nitakavyoweza na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji,” alisema Lema .

Nini kimemsibu Pinda kwenye uwaziri mkuu?

 
Dar es Salaam. Mwaka 2007 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na nafasi yake, Mizengo Pinda aliyeshika nafasi yake alitarajiwa kuja na moto mkali zaidi.
Itakumbukwa kuwa Lowassa aliyeangushwa na kashfa ya mradi tata wa umeme wa Richmond, alishaanza kuonyesha machachari yake hasa katika suala la elimu ambapo alihamasisha ujenzi wa shule za sekondari za kata na miradi mingine.
Pinda aliingia akiwa amevaa ngozi ya kondoo, huku akijiita mtoto wa mkulima. Leo ni miaka sita imepita, tunamwona Pinda halisi alivyo. Kuna kila dalili kwamba amepwaya katika nafasi hiyo.
Tofauti na walivyokuwa mawaziri wakuu wengine, Pinda hajaonyesha ubunifu katika mambo na kuyasimamia. Badala yake amekuwa mtu wa kuonekana wakati wa matukio.
Kukitokea vurugu, wananchi wa Mtwara wameandamana, Waziri Mkuu Pinda anakwenda kutuliza, madaktari wamegoma, anakwenda kuzungumza nao, wenye malori na mabasi wamegoma, anakwenda kuwabembeleza.
Huu ni udhaifu, haiwezekani kiongozi ashughulikie matukio tu wakati anaweza kuboresha utendaji ili mambo yasiharibike.  Kutokana na udhaifu huo, hata mawaziri walio chini yake hawawajibiki ipasavyo. Ndiyo maana hivi karibuni, Wabunge wanaoendelea na kikao mjini Dodoma walimtaja kuwa mmoja kati ya mawaziri wanaopaswa kuwajibika kutokana na kushindwa kusimamia kazi zao.
Wabunge hao waliomba kujadili kwa dharura utekelezaji wa Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza, huku wengi wakiwataja wazi mawaziri kadhaa akiwemo yeye Pinda, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Pinda analalamikiwa kwa kauli yake aliyoitoa bungeni katika mkutano uliopita akivitaka vyombo vya usalama kuwapiga wananchi wanaokiuka sheria.
Kutokana na usimamizi hafifu na kauli zake, kumekuwa na mauaji ya wananchi wasio na hatia kwenye operesheni ya ujangili wa meno ya tembo, kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji isiyokwisha, hali ya elimu imekuwa mbaya na mengineyo. Inawezekana nafasi ya uwaziri mkuu inakosa nguvu kwa sababu, Katiba inampa nafasi rais kama mtendaji.
Baadhi ya nchi hasa za kifalme, Waziri Mkuu ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho, nyingine hazina cheo cha Waziri Mkuu, badala yake anakuwepo tu makamu wa rais.  Hiyo yote ni kuondoa migongano ya madaraka kwa sababu huwezi kuwa na rais mtendaji na waziri mkuu mtendaji kwa wakati mmoja, ni lazima mmoja atakuwa mtumwa wa mwenzake.
Hata hivyo, bado Pinda angeweza kutumia mamlaka aliyonayo kujijengea heshima kwa Taifa kiutendaji kama walivyofanya mawaziri wakuu wengine.