Monday 16 November 2015

Kipindupindu chaota mizizi Dar, Morogoro


Dar/Moro. Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kipindupindu uliolikumba jiji la Dar es Salaam imeongezeka na kufikia saba huku waliolazwa wakifikia 230 na Mkoa wa Morogoro ukiwa na wagonjwa 32 na mmoja kupoteza maisha.Akizungumza ofisini kwake jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema Wilaya ya Kinondoni inaongoza ikiwa na wagonjwa186 huku Ilala na Temeke zikiwa na wagonjwa 22 kila moja.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Nicolaus Chiduo alisema tangu Agosti 18, watu 42 wameugua ugonjwa huo, na kutibiwa na sasa wamebaki 18.
Dk Rashid alisema wizara yake imetengeneza kambi katika  manispaa zote tatu; Kinondoni ipo katika Zahanati ya  Mburahati, Ilala (Kituo cha Afya Buguruni) na Temeke (Hospitali ya Temeke).
Alisema kuwa wananchi wanaweza kuwasiliana na mganga Mkuu wa Mkoa kwa simu namba 0767300234, endapo wataona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ili ushauri utolewe jinsi ya kumsafirisha.
“Naomba sekta nyingine kama maji, elimu, mawasiliano, uchukuzi na ujenzi tushirikiane kutokomeza ugonjwa huu kwa kuwapatia wananchi elimu ya ugonjwa huu,” alisema Dk Rashid.
Ofisa Afya Wilaya ya Kinondoni, Mathias Kapizo alisema tayari wameanza kuchukua sampuli za maji kutoka kwenye maeneo yaliyoripotiwa kutoa wagonjwa wengi ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema wilaya hiyo ilipokea wagonjwa 25 waliokuwa na dalili za ugonjwa huo ila sampuli zilionyesha kuwa 22 hawakuwa na ugonjwa huo.
Alisema wagonjwa watatu wa familia moja ambao sampuli zao zilionyesha kuwa wana vimelea vya ugonjwa huo, hawakutokea katika wilaya hiyo, bali Manzese na mmoja alipoteza maisha.
Morogoro
Kuhusu athari za kipindupindu wilayani Morogoro, imeelezwa kuwa mgawo wa maji katika maeneo mengi ndicho chanzo kikuu cha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa.
Akizungumza kwenye kambi ya Sabasaba, Dk Chiduo alisema Idara ya Afya imelazimika kufungia maeneo yote ya baba na mama lishe hasa yale yenye mkusanyiko wa watu na kuzuia uuzaji wa vyakula ndani ya mabasi.
Maeneo yaliyopigwa marufuku kufanya biashara ya vyakula ni Soko Kuu la Morogoro, Soko la Mawenzi na maeneo yote ya stendi ikiwamo ya Msamvu.
Alitaja maeneo yaliyoathiriwa kuwa ni; Kilakala, Kihonda, Chamwino, Mkundi, Boma, Lukobe, Kiwanja cha Ndege, Sua, Kididimo, Nanenane, Kichangani, Mafiga, Mwembesongo, Polisi Line, Mzinga, Mzumbe, Sultani, Mafisa na Mazimbu. Aliwataka wananchi kuzingatia usafi katika maeneo yao na kuacha kukaa na kula katika maeneo ya mikusanyiko kama misiba.
Akizungumza marufuku ya kuuza chakula, mama lishe, Amina Salim alisema kinachowaumiza ni mikopo waliyochukua katika taasisi za fedha.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Samson Akida aliyesema: “Wengi wetu tumekopa ili tufanye biashara, sasa hapa tunajiuliza tutalipa na kurejesha nini?”