Dar es Salaam. Mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa
amesema mabadiliko katika Taifa hili ni jambo la lazima na linalohitaji
nguvu ya wanawake ili kulifanikisha kwa maendeleo ya Watanzania wote.
Lowassa
alisema hayo jana kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za wanawake,
ulioandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na kutumia
nafasi hiyo kuomba kura kwa wanawake na kuwataka wamtafutie kura kwa
watu wengine.
Alisema anaamini kuwa wanawake katika
umoja wao, ndiyo nguzo kubwa ya mabadiliko na wakiamua kufanya hivyo
hakuna wa kupinga. Alisema wanawake wanakabiliwa na shida mbalimbali
ambazo zinahitaji mabadiliko ya kimfumo.
“Nimekuwa
mbunge kwa zaidi ya miaka 30, nina uzoefu kwamba mwanamke akisema
anakupa kura anakupa kweli. Wanawake mtanipa kura zenu?” Lowassa
aliwauliza wanawake waliohudhuria kwenye mkutano huo nao kwa pamoja
walijibu “umepataaa”
Alisema anakusudia kuleta
maendeleo kwa kasi kubwa ambayo hakuna anayeweza kufikia akitaka ifike
mahali Watanzania waache woga wa kutafuta mabadiliko ya kweli.
Lowassa
aliwataka wanachama wengine wa CCM kujiunga na upinzani kwa madai
kwamba ndiko yalipo mabadiliko ya kweli. Aliendelea kunukuu kauli ya
Mwalimu Julius Nyerere aliyowahi kuisema mwaka 1995, kwamba: “Wananchi
wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
Aliongeza:
“Hawa wenzangu wa CCM waje Ukawa. Huku hakuna noma, waje tu wajiunge na
gurudumu la mabadiliko,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wanawake
waliohudhuria katika mkutano huo.
Awali, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alizindua salamu mpya itakayotumika katika
kampeni zake nchi nzima. Alisema salamu hiyo inaambatana na ishara ya
kuzungusha mikono kumaanisha mabadiliko.
“Lowassa
amekuwa chachu ya mabadiliko nchini na ametuunganisha wote licha ya
tofauti zetu, sasa napendekeza salamu mpya tutakayoitumia kwenye
kampeni, nikisema Lowassa, mnazungusha mikono yenu kumaanisha
mabadiliko,” Mbowe alielekeza na salamu hiyo ilianza kutumika papo hapo.
Alisema
katika utafiti wake, amebaini kuwa wanawake wengi wamekuwa hawafiki
kwenye mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa sababu ya kusukumwa,
kukanyagwa na kudhalilishwa kijinsia, hali aliyosema sasa itabadilishwa.
Alisema
kuanzia sasa watatenga maeneo maalumu ya kukaa wanawake kwenye mikutano
yao yote ya hadhara kuanzia siku ya uzinduzi wa kampeni zao kesho
katika Viwanja vya Jangwani.
“Kuja kwa Lowassa ni
mpango wa Mungu. Alitoka alikotoka na kuja kuwaunganisha wanawake,
wasichana, wanaume na vijana nchi nzima. Hatuna budi kumuunga mkono ili
atuletee mabadiliko tunayoyahitaji,” alisema Mbowe.
Regina Lowassa alonga
Mke
wa mgombea urais wa Ukawa, Regina Lowassa ambaye hotuba yake ilikuwa
ikikatishwa mara kwa mara na shangwe za wanawake, alitumia muda huo
kuwaombea kura wagombea urais wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mama
Lowassa alibainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake
nchini ikiwamo mfumo mbaya wa elimu ambao haumuandai mwanafunzi
kujitegemea na kukosekana kwa huduma bora za afya kwa wajawazito.
Alisema
Tanzania bado iko nyuma kiuchumi kwa sababu Serikali imeshindwa
kutengeneza mazingira wezeshi kwa wanawake ili wanufaike na rasilimali
zilizopo.
Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia
alisema wanawake ni wengi wana nguvu kubwa ya kuamua nani awe rais,
hivyo kuwataka kumpa kura mgombea wa Ukawa ili akalijenge Taifa.
Ilivyokuwa
Licha
ya ratiba ya mkutano huo kuonyesha ungeanza saa 8.00 mchana, wanawake
wengi walifika kuanza saa tano asubuhi na kutumia muda mwingi kuimba
nyimbo za kumsifu Lowassa nje ya Jengo la LAPF.
Baadhi
ya watu walisikika wakiimba; “Kama siyo Kikwete, Lowassa tungempata
wapi?” huku wengine wakisema “CCM siyo chama, kingekuwa chama Lowassa
asingehama.”
Ilipofika saa nane mchana, idadi ya watu
iliongezeka kiasi kwamba walinzi waliokuwa wakilinda lango la kuingilia
ukumbini walilazimika kutumia nguvu ya ziada kuwazuia waliokuwa wanataka
kuingia ndani.
Kutokana na idadi ya watu kuendelea
kuongezeka, ilimbidi mshereheshaji kuomba vijana wa ulinzi wa Red
Brigade kusaidia kuwazuia watu waliokuwa wanataka kuingia ndani wakati
ukumbi umeshajaa.
Walinzi walilazimika kufunga milango
na kutangaza kuwa Lowassa na viongozi alioambatana nao watazungumza na
watu walio nje ya ukumbi kwanza, ndipo waingie ndani ili wote wasikie
anataka kuwaambia nini.
Hata baada ya kuzungumza nao,
wafuasi hao wa Ukawa waliendelea kufuatilia mkutano huo kupitia
televisheni zilizofungwa nje ya ukumbi huo.
Waimbaji wa
nyimbo za injili, Bahati Bukuku na Jeni Miso, walikuwa kivutio kwa
wafuasi hao kutokana na nyimbo walizoiimba za kutaka mabadiliko huku
msanii wa filamu Jackline Wolper akimzawadia Lowassa keki ya siku ya
kuzaliwa. Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953.
Wanachama walonga
Mkazi
Kitunda, Magdalena William (41) alisema amefika eneo la kongamano
kuanzia saa 2.30 asubuhi ili asikose nafasi ya kuona kila kinachofanywa
na kuamuliwa kwa ajili yao.
Zakia Haule (37), mkazi wa
Magomeni, alisema hakuenda kwenye shughuli zake ili kuungana na wenzake
kuleta mabadiliko kwa pamoja. Akiwa mwenye furaha na kujiamini, alisema
amejipanga kuipigia kura Ukawa.
Mkazi wa Tabata, Siwatu
Mussa (42) aliyefika saa nane mchana na kushindwa kuingia ukumbini
alisema: “Nitakaa hadi nimuone anatoka, najipanga kwa ajili ya Jangwani
naona nitakuwa wa kwanza, siku hiyo sitaki kupitwa na kitu.”
Tofauti
na inavyokuwa watu wanapoingia mpirani, zinapobaki dakika nne au tano
kuanza kuondoka, jana hakuna aliyefanya hivyo hadi Lowassa alipomaliza
kuzungumza.
Imeandikwa na Peter Elias, Goodluck Eliona na Kalunde Jamal