Monday 20 May 2013

Matajiri watumia nyaraka feki ujenzi wa maghorofa

WATU wanaodaiwa ni matajiri wakubwa, wameendelea kulisumbua Jiji la Dar es Salaam kwa kupuuza na kukiuka sheria zilizopo, huku wakiendesha shughuli za ujenzi wa maghorofa kwa kutumia uwezo wa fedha zao. Pia matajiri hao wamedaiwa kuwasilisha taarifa za uongo Halmashauri ya Jiji wakiomba kupewa kibali cha ujenzi wa nyumba ya kaiwada, lakini baada ya kupatiwa hujenga jengo la ghorofa kuanzia tano hadi kumi.
Hata hivyo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imegundua taarifa za uongo juu ya ujenzi wa majengo pacha makubwa ya biashara yanayojengwa eneo la Manispaa ya Kinondoni kitalu namba 288 barabara ya Toure Drive Msasani.

Kitendo hicho kiliwafanya wananchi wa eneo hilo kupatwa na hofu juu ya usalama wao na kuiomba Serikali kupitia idara zinazohusika kuchukua hatua.

Kutokana na hali hiyo Manispaa ya Kinondoni, imelazimika kuzuia ujenzi wa majengo hayo pacha tangu Aprili 19, mwaka huu wakati yakiwa hatua ya mwanzo kwa sababu ya kuwa na wasiwasi na mkataba.

Kwa mujibu wa barua ya zuio ya halmashauri ya Kinondoni yenye kumbukumbu KMC/MEK/V22/24 kwenda kwa mmiliki wa majengo hayo, aliyetajwa kwa jina la Silverstone Properties, ilimtaka kusimama ujenzi huo.

Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Godfrey Mgomi ilifafanua kwamba mkataba huo hauonyeshi idadi halisi ya ghorofa zinazojengwa kwa majengo hayo.

Ilifafanua kuwa, mkataba wake huo hauna taarifa muhimu zinazoendana na ujenzi wa maghorofa jijini Dar es Salaam, jambo ambalo linatia wasiwasi wa ubora wa majengo na usalama wa watu.

Halmashauri hiyo ilitoa onyo kwa mmiliki wa majengo hayo kwa kumtaka atii amri hiyo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

MTANZANIA ilifika ofisini kwa Mhandisi Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Gerald Urio kujua sababu ya ujenzi huo kuendelea licha ya kuwapo na zuio.

Mhandisi Urio alikiri halmashauri hiyo kuzuia jengo hilo, kutokana na sababu mbalimbali huku akishangaa ujenzi wa jengo hilo kuendelea na kufikia ghorofa mbili.

“Ni kweli tulisimamisha ujenzi wa majengo hayo na hadi sasa ninapozungumza na wewe sijapata taarifa zozote kama yameruhusiwa kuendelea kujengwa,” alisema.

No comments: