Dar es Salaam/Dodoma. Bunge la Katiba
linaloendelea mjini Dodoma kwa sasa liko katika hatihati ya kuendelea
baada ya kufunguliwa kesi ya kuhoji madaraka yake.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam jana na Mwandishi wa Habari Saidi Kubenea, kupitia kwa wakili
wake Peter Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo iliyopewa usajili wa namba 28 ya
mwaka 2014, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya
Mamlaka ya Bunge la Katiba. Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama
itoe tafsiri hiyo, chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya
Marekebisho ya Katiba namba Namba 83 ya mwaka 2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka
ya Bunge hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo
akiiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili
kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda
yaliyopewa usajili wa namba 29 ya mwaka 2014, pamoja na maombi ya msingi
ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge yote yalifunguliwa mahakamani hapo jana
chini ya Hati ya Dharura.
Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba Mahakama hiyo
itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia
itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya
Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango
gani.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kubenea anadai kuwa
msingi wa kesi hiyo unatokana na uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wa Desemba Mosi, 2011, lililopitisha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba. Anasema sheria hiyo ilikuwa na lengo la kuratibu mchakato wa
kutungwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaendelea kusema kuwa kutokana na sheria hiyo,
Rais aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na mambo mengine
vilevile kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mapendekezo ya Katiba Mpya
na kwamba kwa msingi huo Tume hiyo iliandaa Rasimu ya Katiba.
Anadai kuwa baada ya Tume hiyo kuundwa iliendelea
kukusanya maoni ya wananchi yaliyotolewa katika mikutano ya hadhara na
katika miundo tofauti ikiwamo mabaraza ya Katiba yaliyoanzishwa kila
wilaya kwa lengo hilo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa
takwimu halisi za tume hiyo, jumla ya watu 333,537 walitoa maoni yao
katika nyanja tofauti, tofauti za mapendekezo ya Katiba, ambayo ndiyo
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyatumia kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Inaendelea kueleza hati hiyo kuwa baada ya Rais
kukabidhiwa rasimu ya mwisho Desemba 8, 2013, kwa mujibu wa vifungu
vingine vya sheria hiyo, aliunda Bunge la Katiba kwa lengo la kujadili
Rasimu ya Katiba na hatimaye kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hati hiyo baada ya Bunge
la Katiba kuundwa, mjadala uliibuka ndani na nje ya misingi ya
kisheria kuhusu mamlaka yake, kama Bunge linaweza kwenda kinyume na
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na tume hiyo.
Inaendelea hati hiyo kubainisha kuwa mjadala huu pia uliibuka ndani ya Bunge la Katiba lenyewe kuhusiana na mamlaka yake katika utekelezaji wa majukumu yake kama lina mipaka au la kwa mujibu wa vifungu hivyo 25 (1) na 25 (2) vya sheria hiyo.
Inaendelea hati hiyo kubainisha kuwa mjadala huu pia uliibuka ndani ya Bunge la Katiba lenyewe kuhusiana na mamlaka yake katika utekelezaji wa majukumu yake kama lina mipaka au la kwa mujibu wa vifungu hivyo 25 (1) na 25 (2) vya sheria hiyo.
Katika kusisitiza mjadala kuhusu mamlaka ya bunge
hilo, hati hiyo inatoa mfano wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
katika mkutano wake wa mwaka, ambacho kilisema kuwa vifungu hivyo
havilipi bunge hilo mamlaka ya kubadili rasimu hiyo.
Hati hiyo inaongeza kuwa wakati TLS wakitoa
msimamo huo, kuna wataalamu wengine wa sheria wanadai kuwa Bunge hilo
linaweza kubadilisha na kuongeza ibara kadri itakavyoona inafaa bila
kujali rasimu hiyo.
Kwa mujibu wa hati hiyo, mvutano huo ndani ya
Bunge hilo ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kutoka nje na kususia vikao, wakidai kuwa rasimu hiyo haiwezi
kubadilishwa. Msimamo huo wa wajumbe wa Ukawa, kwa mujibu wa hati hiyo
ni tofauti na wajumbe wengine waliobaki wanaodai kuwa Bunge hilo lina
mamlaka ya kubadili vifungu vya rasimu.
Kwa mujibu wa hati hiyo, utungaji wa Katiba ni
jambo la kitaifa ambalo si tu kwamba linabeba matumaini ya Watanzania
bali pia linabeba mustakabali na ustawi wa nchi.
Hivyo, hati hiyo inaeleza kuwa tafsiri sahihi ya
mamlaka ya Bunge la Katiba dhidi ya Rasimu ya Katiba ni jambo muhimu
sana katika kuongoza mchakato huo ili kuhakikisha kuwa unakwenda kwa
mujibu wa sheria zinazohusika.
Katika hati ya maombi, Kubenea anaomba mahakama
itoe amri ya kusimamisha kwa muda vikao vya Bunge la Katiba
vinavyoendelea Dodoma, kusubiri uamuzi wa Mahakama kuhusu mamlaka yake.
Katika hati ya kiapo chake aliyoiambatanisha na
kesi na maombi hayo, Kubenea anadai kuwa hata baada ya Wajumbe wa Ukawa
kutoka nje, wajumbe waliobaki wanaendelea kujadili rasimu hiyo.
Hati hiyo ya kiapo inaeleza kuwa kufunguliwa kwa
kesi hiyo sambamba na maombi hayo ya kusimamisha kwa muda Bunge la
Katiba si tu kunalenga kupata tafsiri ya Kimahakama kuhusu mamlaka ya
Bunge la Katiba.
Rafu Kamati za Bunge Maalumu
Wakati kesi hiyo ikifunguliwa, kumekuwa na taarifa
ndani ya kamati za Bunge zinazoendelea kuchambua rasimu hiyo
zinazoeleza kuchezwa rafu ili kuwezesha upatikanaji wa akidi kwa ajili
ya hatua ya kupiga kura kupitisha ibara za rasimu hiyo katika baadhi ya
kamati.
Hivi sasa kamati nyingi ziko katika hatua ya
kupiga kura ili kupitisha ibara za Rasimu ya Katiba, kazi ambayo
inahitaji theluthi mbili ya wajumbe kutoka pande za muungano kwa mujibu
wa kanuni za Bunge Maalumu.
Ili kutimiza matakwa hayo, gazeti hili limebaini kuwa rafu
zimeanza kuchezwa hasa katika kamati ambazo zimeshindwa kutimiza sharti
hilo. Moja ya rafu hizo ni ile ya mjumbe wa Kamati namba tano, Maida
Hamad Abdallah kuhamishiwa kinyemela katika Kamati namba 8, kutokana na
kile kilichoelezwa kuwa ni kuwezesha upatikanaji wa akidi katika kamati
aliyohamia.
Habari zinasema mjumbe huyo kutoka Zanzibar
alishiriki kupiga kura juzi mchana na wajumbe wa kamati hiyo walielezwa
kuwa amepelekwa ili kuziba nafasi ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
ambaye hawezi kushiriki vikao hivyo kutokana na kwamba ni mgonjwa.
Hata hivyo, suala hilo lilizua mvutano kiasi
baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji uhalali wa uhamisho huo ambao ni
kinyume cha kanuni za Bunge Maalumu, hasa ikizingatiwa kwamba alipigia
kura mambo ambayo hakushiriki kuyajadili na kuyafanyia uamuzi.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano, Hamad Rashid
Mohamed alithibitisha Abdallah kuhamia kamati namba nane inayoongozwa na
Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai kwa maelezo kwamba aliomba
mwenyewe.
“Ni jambo ambalo ameomba mwenyewe kuhamia huko na
ameruhusiwa maana hilo ni jambo la kawaida kama ambavyo wajumbe wengine
kama kina Mbowe (Freeman) waliwahi kuomba, siyo jambo geni,” alisema
Rashid.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis
Hamad alisema hakuwa na taarifa za uhamisho huo. Alipoulizwa kuhusu
iwapo Kanuni zinaruhusu alisema suala la kupanga ujumbe wa kamati liko
chini ya mamlaka ya mwenyekiti wa Bunge hilo.
“Kwa kweli sifahamu na wala sina taarifa hiyo,
hilo suala la kanuni pengine hebu zisome ili ufahamu zinasemaje kuhusu
mjumbe kuhama kutoka kwenye kamati moja kwenda kamati nyingine,” alisema
Hamad.
Wajumbe wa Bunge Maalumu waliokwisharipoti
wanakaribia 450, idadi ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya akidi
inayotakiwa, lakini hali ni tofauti kwenye kamati kutokana na sababu
mbalimbali, utoro ikiwa mojawapo.
Kutokana na mwenendo huo na wajumbe wengi
kutoingia kwenye vikao licha ya kuripoti, kuna wasiwasi iwapo akidi
itapatikana wakati wa kupitisha rasimu hiyo wakati Bunge Maalumu
litakapoanza kukutana kwa umoja Septemba 2 mwaka huu.
Matakwa ya kanuni
Kanuni ya 55 (1) ya Kanuni za Bunge Maalumu Toleo
la 2014 inasema: “Kamati zinaundwa na mwenyekiti kwa namna ambayo
itawezesha kila mjumbe kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati mojawapo.”
Fasili ya pili ya kanuni inasema wakati wa kufanya
uteuzi wa wajumbe hao, mwenyekiti atazingatia kwa kadri inavyowezekana
idadi ya wajumbe inalingana kwa kila kamati na uwiano kutoka pande zote
za muungano.
Kadhalika kanuni hiyo inasema katika uteuzi wake mwenyekiti
atazingatia idadi ya kila aina ya wajumbe ilivyo katika Bunge Maalumu,
jinsia, wajumbe wenye mahitaji maalumu na uwepo wa wajumbe wenye
utaalamu wa sheria.
Kanuni hiyo iko kimya kuhusu uhamishaji wa wajumbe
na fasili yake ya nne inasema: “Ujumbe katika kamati utadumu kwa
kipindi chote cha maisha ya Bunge Maalum.”
Waraka wa uchambuzi wa mgawanyo wa wajumbe katika
kamati unaonyesha kuwa Kamati namba tano alikotoka Maida ina wajumbe 52
na kati yao 34 wanatoka Tanzania Bara na 18 Zanzibar wakati kamati
alikohamia pia ina wajumbe 52; 35 kutoka Tanzania Bara na 17 kutoka
Zanzibar.
Kwa maana hiyo hata kama uhamisho wa Maida
ungekuwa na lengo la kuimarisha uwiano kwa maana ya pande za muungano,
ni dhahiri kwamba unaathiri kwa maana ya idadi wajumbe kutoka Zanzibar
katika kamati namba tano.
Gazeti hili lilimtafuta Ndugai kwa lengo la kupata
maelezo jinsi alivyompokea mjumbe huyo, lakini kutwa nzima ya jana simu
yake ilikuwa ikiita bila majibu. Kadhalika Maida naye alitafutwa lakini
simu yake ilikuwa imezimwa wakati wote. Maida hakuwamo kwenye kamati
yake ya awali namba nne ilipokutana jana mchana baada ya kuwa
wamepumzika asubuhi kupitia sura za nyongeza.
Kupitisha uamuzi
Kanuni hizo pia zinaelekeza kwamba wakati wa
kupitisha uamuzi lazima wajumbe wawe wamefikia theluthi mbili kwa pande
zote za muungano, jambo ambalo limekuwa gumu kutokana na mahudhurio
hafifu kwenye kamati husika.
No comments:
Post a Comment