Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameingia
rasmi katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
hatua ambayo imebadili mwelekeo wa kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kubwa
ya uongozi nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.
Gazeti hili limethibitisha kwamba Pinda tayari
ameamua kujitosa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ambayo tayari inawaniwa
na makada wa chama hicho wasiopungua 15 na baadhi yao wameishatangaza
nia zao kwa nyakati tofauti.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema uamuzi wa
Pinda kuwania urais mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwakani, umesababisha kiwewe miongoni mwa wagombea na
kunakifanya kinyang’anyiro hicho kuchukua sura mpya.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia gazeti
hili siku chache zilizopita mjini Dodoma kuwa: “Na sisi tumesikia
kwamba PM (Waziri Mkuu) amejitosa na kama ni kweli atawasumbua wagombea
wengi kutokana na rekodi yake hasa katika uadilifu.”
“Yeye (Pinda) ana faida tatu kubwa; kwanza hana
kundi katika chama, anaelewana na watu wote, pili nafasi yake ya uwaziri
mkuu inampa nafasi ya kufahamika kwa watu wengi na tatu rekodi yake ya
uadilifu, hana kashfa za ovyoovyo, labda kama ataharibu dakika hizi za
mwisho,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania uraia
kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake
katika nafasi hiyo, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk
Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe.
Wegine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na
Waziri wa Katiba, Asha-Rose Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na aliyewahi kuwa
Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Balozi Ali Karume.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho
alisema wingi wa wanaojitokeza kutaka kuwania urais ni njia ya kuunda
mtandao utakaomwezesha mtu fulani au mmoja kunyakua tiketi hiyo.
“Watu wanapiga kampeni katika harambee kwa njia ya
kutengeneza mitandao, kwani ukifika wakati wa chama kumpitisha mgombea,
asiposhinda ataibuka na kuwaeleza kuwa mnaoniunga mkono mimi muungeni
fulani,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Richard Mbunda alisema kujitokeza kwa idadi kubwa ya wanaowania nafasi
ya urais, kutatoa fursa ya wananchi kutambua udhaifu wa kila mmoja jambo
litakalowezesha kupatikana kwa mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya
chama hicho.
“Wakiwa wengi, kila mmoja atataka kuonyesha umahiri wake na sisi
ambao ni wananchi watawaliwa tutaweza kutambua upungufu wa kila mmoja,
jambo litakalosaidia kupatikana kwa mtu sahihi,” alisema Mbunda
Kambi ya Pinda
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku
kadhaa mjini Dodoma ambako vikao vya Bunge Maalumu vinaendelea umebaini
kuwa kambi ya Pinda inaongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka za Mitaa
Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas
Masaburi.
Inadhaniwa kuwa Dk Masaburi atatumia ushawishi
wake kwa viongozi wa mamlaka za miji na wilaya zinazoongozwa na
wenyeviti wa halmashauri na mameya wa miji, manispaa na majiji kumuunga
mkono mgombea huyo ambaye pia hivi sasa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa ziko chini ya ofisi yake.
Wiki hii kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na
Dk Masaburi lilikuwa mjini Dodoma likijaribu kutafuta kuungwa mkono na
makada viongozi wa CCM ambao walikuwa wakishiriki kikao cha Kamati Kuu
ya chama hicho pamoja na wale walioko katika Bunge Maalumu. Habari
zinasema mbali na Dodoma, tayari kambi hiyo imeshafanya vikao kadhaa
jijini Dar es Salaam na Visiwani Zanzibar lengo likiwa ni kutafuta
kuungwa mkono na makada wa CCM katika sehemu hizo. Hivi sasa nguvu za
Pinda zinaelekezwa katika mikoa mingine nchini kwa lengo hilohilo.
Kutokana na kasi ya kambi yake, wafuasi wa baadhi ya wagombea wameanza
kufuatilia mwenendo wao kwa lengo la kukusanya ushahidi wa kile
wanachokiita ‘rafu’ zinazochezwa ili kupata ushahidi unaoweza kutumika
dhidi ya mgombea huyo wakati mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM
utakapoanza mapema mwakani.
Itakumbukwa kwamba makada watano wa chama hicho
ambao ni Lowassa, Membe, Makamba, Wassira na Ngeleja wanatumikia adhabu
na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa
makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema
hivi sasa ni mapema mno kusema ni lini mchakato wa kupata wagombea wa
nafasi za uongozi ndani ya chama hicho utaanza na kwamba wakati mwafaka
ukiwadia wananchi watafahamishwa.
Uwezo, udhaifu wake
Hata hivyo wakosoaji wake wanasema Pinda akiwa
Waziri Mkuu hana cha kujivunia na kwamba amekuwa mzito kufanya uamuzi
mara kadhaa kiasi cha kusababisha baadhi ya mambo muhimu ya nchi kukwama
na kwamba kwa maana hiyo hastahili kuwa rais.
“Ni kitu gani ambacho nchi inakikumbuka kuhusu
huyu bwana ambacho alikifanya katika miaka yake ya uwaziri mkuu, kama
alikuwa kwenye nafasi kubwa kiasi hicho na hakuna alichofanya, atawezaje
kumudu madaraka ya mkuu wa nchi?” alihoji mmoja wa makada wakongwe wa
CCM.
Waziri mmoja wa sasa (jina tumelihifadhi), alisema
Pinda hana uwezo wa kuongoza nchi, kwani wao wakiwa mawaziri ameshindwa
kuwasaidia katika kero mbalimbali walizokuwa wakimfikishia kama
kiongozi wao.
“Muulize waziri yeyote kuhusu uwezo wa jamaa,
kila kukicha tunampelekea mambo tunayokutana nayo, lakini hakuna
kinachowezekana kwake, atakwambia subiri leo, subiri kesho na hatimaye
jambo linaishia hivyohivyo,” alisema.
Kwa upande mwingine, watetezi wake wanasema Pinda wanayemnadi ni
yule aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi) kiasi cha kuonekana anafaa kuwa
Waziri Mkuu.
Wanasema kushindwa kwake kufanya kazi ipasavyo ni
matokeo ya sababu zilizomfanya mtangulizi wake, Lowassa kung’oka katika
nafasi yake.
No comments:
Post a Comment