Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi
amefichua siri na kueleza kwamba wakati alipochaguliwa kuiongoza wizara
hiyo nchi ilikuwa imefilisika.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa ushirikiano na rais wa wakati huo, aliweza kuimarisha uchumi ndani ya siku 365 alizofanya kazi.
Profesa Mbilinyi aliyeshika wadhifa huo katika
Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin William Mkapa,
alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake
Upanga, Dar es Salaam, ambapo alieleza hali ya uchumi ilivyo sasa
ikilinganishwa na miaka 19 iliyopita.
Alisema wakati alipopewa jukumu la kuiongoza
wizara hiyo mwaka 1995 na Rais Benjamin Mkapa, alikuta uchumi
umetetereka kwa kiasi kikubwa, hata taifa kushindwa kukubalika na
taasisi za fedha za kimataifa na wafadhili waliosusa kutoa misaada wala
kuikopesha fedha.
“Mkapa aliniteua kuwa waziri wake wa fedha, lakini
wakati ananikabidhi ofisi hiyo, hali ya uchumi ilikuwa ni mbaya sana.
Nilikuta uchumi umetetereka, sababu hatukulipa madeni ya kimataifa,
wakasusa. Kimsingi nchi ilifilisika, lakini hatukuweza kusema mbele ya
wananchi,”alisema Profesa Mbilinyi na kuongeza:
“Nilikubali na kuanza kufanya kazi kama waziri
tukishirikaina naye (Mkapa), katika mambo mbalimbali ili kuweka uchumi
katika hali nzuri. Uhusiano baina ya Serikali na taasisi hizo za
kimataifa pia nchi wafadhili haukuwa mzuri, kwa hiyo tukajitahidi
kurudisha heshima yetu. Tulirudisha heshima na kukubali masharti
machache ya msingi ya Shirika la Fedha Duniani(IMF) na Benki ya Dunia,
ikiwamo suala la uanachama, uchumi ukaanza kufufuka.”
“Kwa kipindi hicho hatukuingia kwenye makubaliano
mengine ya mikopo hadi baadaye sana. Kwa hiyo ndiyo ilikuwa njia ya
kurudi kwa IMF na WB kwa kuzingatia hayo,”alifafanua Profesa Mbilinyi.
Baada ya muda kiasi alisema wakaanza tena kufanya
makubaliano ya baina ya nchi mbili na kuanza tena kupata misaada hasa
kutoka Korea Kaskazini, India, Japan na Urusi na baadaye uchumi ukaanza
kuonekana unaweza kufufuka ndipo Benki ya Dunia ikarejea na makubaliano
ya kawaida.
“Hata hivyo, sikukaa hapo muda mrefu. Nilifanya
kazi zote ndani ya mwaka mmoja nikamaliza. Hapo tulishainua uchumi hadi
ukakaa sawa, tulikuwa kwenye nafasi nzuri kiuchumi kama nchini nyingine
wanachama wa Benki ya Dunia,”alisema.
Kiongozi huyo mkongwe wa masuala ya uchumi
alisema, licha ya kuwa alifanya kazi kwa juhudi na bidii kwa ajili ya
masilahi ya taifa katika Wizara ya Fedha, baadhi wa watu hawakuona jema
katika hilo.
“Licha ya kuwa mambo yalienda vizuri, kipindi
hicho cha mwaka mmoja nilijenga uadui na watu wengi kwani niliwazibia
mianya ya ulaji. Hata hivyo, jambo hilo ndilo lililosababisha kuachia
nafasi hiyo na kumwambia Mkapa:“Naenda kuendelea na ubunge wangu,
mchague mwingine akusaidie katika masuala ya fedha,”alisema Mbilinyi na
kuongeza kuwa hilo ni moja kati ya mambo yaliyoweka historia katika
maisha yake ya kulitumikia taifa la Tanzania.
Profesa Mbilinyi ambaye pia amewahi kuwa mashauri
wa kiuchumi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema baada ya uamuzi
huo aliamua kujikita kwenye ubunge pekee.
“Wakati Mkapa aliponiteua kuwa waziri wake wa fedha nilikuwa
mbunge wa Peramiho, hivyo baada ya mwaka mmoja na kama mwezi mmoja hivi
nilipoamua kuachia wadhafa huo, nikawa mbunge kwa jimbo langu kwa miaka
kumi, kabla ya kuacha kujihusisha na masuala ya kisiasa. Huo ndiyo ukawa
mwisho na siasa zangu. Ilikuwa mwaka 2005,” alisema Profesa Mbilinyi.
Akilinganisha hali ya uchumi wakati alipokuwa
waziri na sasa, Profesa Mbilinyi ambaye sasa anafanya shughuli za
mshauri wa uchumi akiwa pia mkulima na mfugaji alisema kuwa kwa mtazamo
wake mwenendo wa uchumi ni mzuri.
“Sasa hivi nadhani una matatizo ya kawaida, lakini
tunaendelea vizuri. Kwa mwendo huu, nadhani tutafikia malengo ya kuwa
kati ya mataifa yenye uchumi wa kati duniani ifikapo mwaka 2025, kama
tukiendelea hivi ,” alisema Profesa Mbilinyi na kuongeza:
“Kwa gesi iliyogunduliwa, uwezekano wa kupatikana
mafuta na madini, inatia imani kwamba tunaweza kufika mbali. Rais
Kikwete awe wa mwisho kuiongoza Tanzania ikiwa katika hali ya umasikini.
Lakini pia nampongeza Rais Kikwete kwa kufikisha uchumi wa nchi ulipo
sasa.”
Kuteuliwa na Nyerere
Akizungumzia kuteuliwa kwake na Nyerere alisema:
“Alikuwa mwalimu wangu nilipokuwa nasoma Shule ya Sekondari Pugu. Wakati
anaondoka kwenda kuanza siasa mwaka 1955 alituacha pale. Nilimaliza
shule 1956 nikawa nafanya kazi ya kuuza mafuta Sheli BP, Pugu.
Lakini wakati huo nilikuwa namsaidia Mwalimu kufundisha makada wa TANU ambao ni vijana.
Niliwafundisha hesabu na Kiingereza wakati wa
usiku katika Mtaa wa Lumumba kwa sababu wakati ule watumishi wa Serikali
walikuwa hawaruhusiwi kuingia kwenye siasa” alisema Profesa Mbilinyi.
Aliongeza: “Alipokuwa rais akakumbuka kuwa
Mbilinyi yupo Chuo Kikuu na kwa vile nilikuwa nafundisha vijana wa TANU,
basi akaniita mimi pamoja na Justine Rweyemamu tumsaidie kumsomea
makaratasi yake ya uchumi.
Alikuwa anasema kuwa uchumi wake ni wa kisiasa,
hivyo tukawa wasaidizi wake wa masuala ya uchumi pamoja na vijana
wengine kama saba hivi.”
Alielezea kuwa alifanya kazi na Mwalimu Nyerere kwa maika minane na kwamba anamkumbuka kwa mambo mengi.
No comments:
Post a Comment