Friday 1 August 2014

JOTO 2015: Mrema asema yuko tayari kumkabili Mbatia

Moshi. Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP) amesema amejiandaa kuingia ‘vitani’ na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye ametangaza kuwania ubunge katika jimbo hilo, mwaka 2015.
“Siogopi mtu yeyote. Nimejiandaa vilivyo kwa mpambano huu. Najivunia rekodi yangu nzuri ya utendaji wala sitishiki na wananchi wangu nimewauliza wameniambia nisihofu,” alisema Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema, anaamini rekodi yake nzuri ya utendaji ndiyo itakayomuuza mwaka 2015 na kwamba, ni rekodi hiyo nzuri ndiyo iliyowafanya wananchi wa jimbo hilo wakamchagua mwaka 2010.
“Umesahau nilikuwa mbunge wa Moshi Vijijini wakati huo ikiwa ni pamoja na Vunjo? Rekodi yangu nilipokuwa naibu waziri mkuu inajieleza. Yeye (Mbatia) aje nimejiandaa kwa mpambano,” alisema.
Juzi, Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, alisema kwa sasa ameelemewa na maombi ya makundi mbalimbali ya jamii yakimtaka agombee ubunge katika jimbo hilo mwakani.
“Nimefuatwa mara kadhaa na viongozi wa dini wakiniomba nigombee tena 2015. Wapo wananchi wamenifuata hadi bungeni. Simu yangu imejaa meseji nyingi za kuniomba,” alisema Mbatia.
Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliwahi pia kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 hadi mwaka 2000.
“Hayo maombi ya wananchi siwezi kusema nawakatalia, mimi ni nani nikatae kuwatumikia Watanzania wenzangu? Niko tayari kuwatumikia ila wajue kwa sasa kuna mbunge,” alisema.
Mbatia aliongeza, “Natarajia kwenda Vunjo wakati wowote kuanzia leo ili nitoe jibu rasmi mbele ya Wanavunjo. Nashukuru kwa heshima hii waliyonipa. Naahidi sitawaangusha.”
Wiki iliyopita, baadhi ya wananchi waliodai kuwawakilisha wenzao kutoka kata zote za jimbo hilo, walitoa tamko lililosomwa na Mathew Temu wakimtaka Mbatia agombee ubunge kupitia vyama vya NCCR, Chadema na CUF vinavyounda Ukawa. Katika tamko hilo, wananchi hao walisema rekodi ya Mbatia alipokuwa mbunge haijawahi kuvunjwa.

No comments: