Friday 1 August 2014

Malecela: Wakati utafika wasomi watabaki kwenye taaluma zao

Katika toleo la jana Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela alizungumzia historia yake katika siasa na mchakato wa Katiba Mpya. Katika sehemu ya pili ya mahojiano na gazeti hili, anaeleza pamoja na mambo mengine, ubinafsishaji, ajira na ushiriki wa wasomi kwenye siasa.
Swali: Kuna taarifa kwamba uliwahi kuwekwa ndani kutokana na ushiriki wako katika harakati za ukombozi kupitia Tanu. Hili likoje?
Malecela: Sikuwekwa ndani kwasababu ya harakati za Tanu, hapana. Wakati narudi kutoka India baada ya kumaliza masomo yangu ya shahada ya kwanza, nilipita njia ya Mombasa, kutoka Mombasa nikaja Arusha. Arusha pale alikuwepo Nsilo Swai ambaye alikuwa mwalimu wangu Mazengo halafu India tukasoma wote, kwa hiyo alikuwa pale kama Katibu Mkuu wa Meru Cooperative Union. Nikaona nipite kwake nikae pale siku mbili, tatu hivi, kutoka Arusha nikaja Dodoma. Nilipofika tu nikaitwa kituo cha polisi. Nilipofika pale wakapekua mizigo yangu sasa wakanikuta na kitabu kimoja cha George Padimo ambacho kilikuwa kinaitwa Pan Africanism or Communism, wale wapekuzi kwa bahati mbaya hawakuwa Wazungu walikuwa ni weusi wenzangu.
Basi wakasema huyu mtu ana chembe-chembe za ukomunisti huyu ngoja tumweke ndani. Nililala mahabusu pale siku mbili aliyekuja kunitoa alikuwa ni Mzungu. Wakati huo wa Waingereza kila siku lazima mkuu wa polisi aende akaripoti kwa Mkuu wa Wilaya akieleza kwake ana watu wangapi mahabusu na makosa yao.
Sasa alipokwenda kuripoti kwamba kwenye mahabusu wana kijana ametoka India na wanafikiri kwamba ni mkomunisti, akawaambia kwamba mleteni. Mkuu wa Wilaya huyo alikuwa anaitwa Eyas, nikaenda ofisini kwake bahati yule Eyas alikuwa ni raia wa Ireland. Sasa nilipofika ofisini kwake akaagiza chai tukawa tunakunywa, akasema Waingereza hawa wabaya ndio maana sisi tunapigana nao we kijana angalia usifanye ovyoovyo.
Wakati huo ulikuwa mwaka 1959. Basi akanihubiria hapo, baada ya hapo akawaambia wale polisi ujinga huo, huyu hawezi kuwa mkomunisti, huyu ni Mgogo mwacheni arudi kwao. Na kweli yule Mkuu wa Wilaya alifurahi kuona kuwa mimi nimetoka kijijini huko akanipeleka mpaka nyumbani Mvumi kwa gari yake.
Swali: Hapa tulipo kuna tatizo kubwa la ajira na wengi wamelizungumzia, wewe unalizungumzia vipi?
Malecela: Kwanza nataka muelewe huku tulikotoka chama kilikuwa kinasema nini. Chama kilikuwa kinawakilisha siasa ya ujamaa na kujitegemea ndio maana katika miongozo mingi ya Tanu na baadaye Chama Cha Mapinduzi, ilikuwa kila siku inaomba watu wajiunge pamoja katika vikundi ili kuzalisha. Nitawapa ushahidi wakati nikiwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Mara tu tulipopata uhuru Nsilo Swali alikuwa ndio Waziri wa Mipango wakalizungumzia hilo la ajira ya vijana Dar es Salaam. Wakasema si tunayo mashamba ya sukari Kilombero, basi wakachukua vijana pale zaidi ya 3,000 wakakaa nao, nakumbuka walisindikizwa na treni la kwenda Kidatu kuwapeleka vijana waende wakafanye kazi na walipewa mishahara kama ya miezi miwili na vifaa vyote vya kwenda kukata miwa. Hiyo yote ilikuwa ni nguvu za kuwapa vijana ajira.
Wakaenda kule miezi mitatu baadaye hakuna hata mmoja aliyebaki. Niwape ushuhuda wa karibuni wakati Mama Kunambi (Bernadetha, DC wa Dar es Salaam) aliwahi kuja na wazo lilelile, mimi nikamwambia wazo hili huko nyuma tulijaribu, lakini baada ya miezi mitatu wote wakawa wamerudi hapa. Kwanza tukapita kwenye mashamba ya mkonge tukatafuta vibarua, sio ya wasomi hapana, ni ya vijana kufanya kazi kwa mikono. Mama Kunambi akahesabu vijana wake 3,000, hizi rekodi sijui kama Ilala wanazo, tukahangaika, tukawapeleka hawa vijana kwamba waende wakafanye kazi huko na wao wakakubali.
Tukawapa mishahara miezi miwili kabla hata hawajafika huko. Baada ya miezi mitatu minne wote wakawa wamesharudi Dar es Salaam. Sijui kwa nini tukianza kusema ajira mimi nahisi mara nyingine sisi Watanzania tunaanza kujiona Serikali yetu haifanyi chochote, ndio maana tunakuwa na matatizo haya tunasahau hili ni tatizo la ulimwengu mzima.
Ni kweli wenzetu walioendelea tatizo hili linakuwa tofauti, kwa mfano Uingereza utakuta vijana wasiokuwa na ajira ni wengi, lakini kule mara nyingine ni kwa sababu ya kuchagua kazi ambayo ni sawa na huku ambako watu wanafikiri kuwa bado wanaweza kupata kazi ya kufagia ofisini na siyo kwenda kukata mkonge.
Kwa hiyo hili tatizo la vijana tunalo, lakini sisi kama Tanzania tunachotakiwa kufanya ni vitu viwili ambavyo kweli tuvifanye kwa juhudi kubwa kabisa maana yake ndio urithi ambao baba wa taifa ametuachia wa kukabiliana na matatizo yetu. Kama tunaweza kuboresha maisha ya vijijini kweli huwezi kupata wamachinga Dar es Salaam. Jamani kwa sababu ninyi ni watu wa habari naomba muende mkachunguze Dar es Salaam, muone hawa watu wa Lushoto, Wasambaa nenda kahesabu hawa watu kama utamkuta Msambaa Dar, hakuna, kwanini?
Mimi nimekwenda Lushoto unakuta kijana ana eka yake ya nyanya, anailima vizuri kweli kweli na kiutaalamu. Ukiilima eka moja vizuri, inakupa zaidi ya tani mia moja za nyanya na kule wanalima mara tatu kwa mwaka.
Kwa hiyo kule Lushoto hupati vijana wa kuja kuwa wamachinga, hapana.
Swali: Viwanda vingi vilibinafsishwa haiwezi kuwa sababu ya tatizo la ajira?
Malecela: Mimi sisemi kuwa viwanda vingi vimebinafsishwa ndio tatizo la ajira, hapana. Ninachosema kuna wakati katika miaka ya 1970 Tanzania ilikuwa na viwanda vingi vya nguo. Kiwanda cha Urafiki kilikuwa kimeajiri zaidi ya vijana 3,000, Ufi (Kiwanda cha zana za kilimo) kiliajiri watu 1,000 na Tanita (cha kubangua korosho) kiliajiri wafanyakazi 2,000.
Sasa vyote hivyo akaja mtu akutuambia ohhh kuendeshwa na Serikali haifai, hivi vinatakiwa viende binafsi. Tulivyosema hivyo viendeshwe na watu binafsi, Wahindi wakaja kwanza wakapandisha bei ya korosho. Korosho kilo moja Sh800.
Viwanda vyetu vikakosa korosho kwa hiyo vikasimama na hii imetokea juzi juzi hapa bei ya korosho imeanguka kutoka Sh800 kwa kilo hadi Sh120. Walipoona viwanda vimedorora havifanyi kazi na vyama vya ushirika vimekufa kwa sababu vilikuwa vikiendeshwa na hii biashara ya korosho, wakapunguza bei.
Nenda Morogoro yaani unajua vitu vingine tunasema tu, lakini mimi ambaye niliona viwanda vikifanya kazi leo napita Morogoro unaweza kuona ni mji unaokufa, lakini vilipokuwa vinafanya kazi pita pale saa 10:00 jioni unaona watu wanatoka kule kwenye viwanda sasa wanakuja mjini we mwenyewe unashangaa hivi hii ni Tanzania.
Kwa viwanda tukadanganywa ohh vitu vinavyoendeshwa na serikali haviendi, vibinafsishwe tukasahau kwamba vingine watu wale wanakuja na nia kabisa anakinunua kiwanda palepale anakifunga.
Nenda Mwanza mfano mzuri na huu ndio huwa unanisikitisha kweli kweli, ukiwa unakwenda uwanja wa ndege mkono wako wa kushoto utaona magofu makubwa, yale magofu yalikuwa majengo ya kiwanda kikubwa cha ngozi.
Akaja mtu akabinafsisha akachukua mitambo yote kauza Kenya sasa ukienda pale unalikuta jumba tu tupu.
Swali. Kwa hiyo kwa kifupi ubinasfisishaji haukuwa kitu kizuri?
Malecela: Kwanza binafsi nisingependa kuhukumu kuhusu ubinafsishaji. Mimi ninasema kila kitu mnapokifanya jamani mkifanye hatua kwa hatua. Siku za nyuma tulikuwa hatuna haja ya kuleta hizi juisi kutoka nje ya nchi, tulikuwa na kiwanda cha kutengeneza juisi ya machungwa lakini hata kilivyokufa sijui. Tulikuwa na kiwanda cha betri Matshushita. Unajua Matshushita kilivyokufa? Tajiri mmoja aliingiza betri za matshushita kutoka Indonesia akauza, Matshushita wakaja serikalini wakasema kama hivi tutafunga, wakafunga.
Barabara ya Pugu (Nyerere) ilikuwa mahali ambapo ikifika jioni watu wanatoka kazini unaangalia unajua kweli tuna viwanda, lakini vingi vimefungwa. Pale Dar es Salaam tulikuwa na viwanda vya nguo tulikuwa na Sungura Textile, tulikuwa na Tasini, tulikuwa na kama viwanda vinne vya kutengeneza nguo. Arusha General Tyre, tulikuwa na viwanda viwili vya nguo hiki A-Z kilifikia wakati hadi kinatengeneza nguo za ndani wakiziweka lebo ya mark Spencer, unatoka hapa unakwenda kununua vest Uingereza kumbe inatengenezwa Arusha.
Swali: Kuna wimbi sasa kila mtu anagombea ubunge, maprofesa, madaktari wanaacha kazi zao wanagombea ubunge. Unafikiri ni kwanini?
Malecela: Nadhani hasa kwa wasomi mimi nasema Mungu anisamehe kama ninawasingizia, wengi walifikiri nikiwa mbunge nitakuwa waziri. Kwa huko nyuma maprofesa wachache walipata uwaziri kweli. Walipoanza kuja kwa fujo na kwa wingi ikawa haiwezekani tena, halafu wengine hata ufanisi wao ulikuwa mdogo.
Swali; Pamoja na hapo kuna wimbi hili la watoto wa viongozi nalo linakuja kwa kasi!
Malecela; Mimi nataka kuwaambia kwa kweli hilo la kusema watoto wa wanasiasa mnawaonea. Unamkuta mzee yeye mfua vyuma, anatengeneza visu amekaa na mfuko wake. Mtoto anakaa pembeni anaona baba yake anapopuliza moto, anaona mpaka chuma kinavyokuwa chekundu. Anamwona baba yake anavyokwenda kukigongagonga hadi kinakuwa kisu, ama kama jembe na kadhalika.
Sasa mbona watoto wa walimu wakichukua ualimu hatusemi? Watoto wa madereva wakiwa madereva hatusemi, ila watoto wa viongozi wakiwa wanasiasa mnasema. Sisi tuna msemo kwamba; ukimwangalia ng’ombe mguu wa mbele utakapokanyaga na huu wa nyuma utakuja kukanyaga hapohapo.
Kwa hiyo hawa watoto wa wanasiasa bwana wakati mwingine wanaongozana na baba anapokwenda mahali, mara nyingine haendi kwa sababu anavutiwa na mkutano hapana, yeye anakwenda tu ili apande gari la baba. Kwa hiyo anakwenda pale baba anahutubia pale anaona, sasa watakuwa wajinga sana kama hawajifunzi. Kwa hiyo mimi nasema watoto wa viongozi tuwahukumu kwa utendaji wao.
Kweli kama mtu akianza kutumia jina la baba yake ohh mimi mtoto wa fulaniatashindwa.
Swali: Unatoa ushauri gani kwenye hili wimbi la wasomi maprofesa na madaktari kukimbilia kwenye siasa?
Malecela: Mimi sina ushauri wowote. Ni kama nguo, zilikuja watu wakaanza kulalamika jamani wasichana lakini baadaye ni mtindo ulipita. Hata hivi sasa wengi watakwenda kwenye siasa lakini muda ukifika watagundua kuwa kwenda kwenye siasa ni kupoteza muda.
Swali.Ukiwa Waziri Mkuu, ulikuwa ndio msimamizi wa shughuli zote za Bunge. Kuna kipindi Bunge lilikuwa moto na hasa wakati wa G 55 unaweza kulizungumzia hili?
Malecela: Siwezi kulizungumzia sana kwa sababu kipindi hicho kilipita. Ni kweli kulikuwa na kundi la G 55 ambao walikuwa wanataka Tanganyika. Katika Muungano Tanganyika nayo ionekane iwe Serikali ya Tanganyika ya Zanzibar halafu Muungano. Ilikwenda ilivyokwenda lakini mwisho ikaishia kwenye chama ambacho kilipeleka kwa wanachama basi mambo yakamalizika.
Swali: Ukiwa Waziri Mkuu changamoto uliyoipata unaizungumziaje?
Malecela: Changamoto huwezi kuizungumzia kwa sababu hizi ndizo zinazokujenga kwa wakati huo kwamba ukisikia jina Malecela unalinganisha na hiki na hiki; vizuri na vibaya.
Swali: Ukiwa Waziri Mkuu, uliwahi kujionyesha hadharani kuwa wewe ni mpenzi wa timu ya mpira ya Simba Sports Club, uliwahi kukacha safari yako moja kwa ajili ya kwenda kushuhudia Simba ikifanya vitu vyake uwanjani. Sijui kwa sasa hali yako ikoje kimichezo?
Malecela: Mechi zote ambazo nimewahi kuwa mgeni rasmi Simba inacheza, ilishinda. Ngojeni niwape historia kidogo, mimi wakati nikisoma Shule ya Sekondari Minaki, Dar es Salaam kulikuwa na timu tatu. Kulikuwa na timu ya Wazungu, timu ya Wahindi, Magoha na Waarabu na timu ya Waafrika.
Nendeni kwenye historia mchele walikuwa wanakula Wahindi, Wasomali na wengine Mwafrika ulikuwa huruhusiwi kununua mchele mpaka upate kibali. Sasa hata kama ukiwa mchezaji namna gani, timu ya wazungu ilikuwa ikiitwa Sunderland sasa hata uwe nani ilimradi wewe ni mweusi huwezi kuichezea timu hiyo.
Hii ya wahindi, magoha na waarabu ilikuwa ikiitwa Cosmo Club hata uwe nani huwezi kujiunga na kama sio wa jamii hizo.
Kwa watu weusi ilikuwa Yanga Africans, sasa wewe hata utake kucheza mpira wa namna gani lazima ukawe Yanga. Kwa hiyo hakukuwa na chaguo hivyo mtu ukiwa mpenzi wa mpira lazima tu uwe mwana Yanga.
Kwa hiyo wazungu walipoanza kuondoka ile Sunderland ikaanza kupungukiwa nguvu wakajitahidi kujiunga na Cosmo.
Nao walipoanza kuondoka na kuhama ndio baadaye wakaanza, jamani tuwachukue na wenzetu. Wakawachukua na waafrika na mwenyekiti wa kwanza na ndio akaleta na jina la Simba alikuwa Amon Nsekela. Karume alikuwa Yanga kwa sababu wakati ule hakuwa na chaguo.
Swali: Hadi sasa bado wewe ni shabiki wa Simba?
Malecela: Mimi napenda mpira mzuri tu. Kuna wakati nilikuwa nafikiri hii vita ya Yanga na Simba ilikuwa inadumaza mpira. Nilipokuwa Waziri wa Kilimo kwa kweli nilijitahidi nikaunda timu ikaenda kucheza na hizi timu kubwa zikaenda droo. Baada ya hapo wachezaji wangu wakachukuliwa mmoja mmoja na mtu wa kilimo akafanywa kuwa Mwenyekiti wa Yanga na timu yetu ya Kilimo ikafa.

Swali Kuna jambo ambalo ungependa lifahamike kwa wananchi?
Malecela: Ningependa wananchi wafahamu kwamba maendeleo ni hatua. Mimi nimekwenda Nigeria nimeendesha gari kutoka Abuja kwa barabara mpaka Port Harcourt jamani, umaskini niliouona kule ni wa kupindukia, huwezi kuulinganisha na wetu hata kidogo.
Mimi nilipokwenda kuripoti Tukuyu ilinichukua siku mbili kufika. Siku ya kwanza niliondoka Dodoma na basi nikalala Iringa. Kutoka pale kesho yake nikalala Mbeya ndio nikafika Tukuyu. Lakini sasa ukitoka Dodoma saa 12:00 asubuhi Mbeya saa tisa umeshafika.
Hapa ilikuwa safari ya hapa (Dodoma) hadi Iringa ilikuwa ni maili 240 ilikuwa ni ya kutwa nzima. Unaondoka hapa asubuhi na mabasi haya ya Urafiki unafika kule jioni, lakini sasa hivi unaondoka Iringa saa 12:00 asubuhi saa 4:00 asubuhi uko Dodoma.
Kinyago
Katika sebule ya Mzee Malecela mjini Dodoma ameweka kinyango kikubwa mfano wa mti ambao umebeba watu wakiwa wamebeba vitu mbalimbali.
Malecela anakizungumzia kinyago hicho kilimgharimu sh 300,000 wakati akiwa Waziri Mkuu miaka ya tisini na kilichongwa kwa muda wa miezi miwili.
Kama hiyo haitoshi anasema mchongaji wa kinyago hicho ambaye sasa ni marehemu alikuwa akiifanya kazi hiyo tu kwa kipindi cha miezi miwili ambapo ilimlazimu kumuwekea wafanyakazi kwa ajili ya kumfulia, kumpikia na kumfanyia vitu vingine ili atumie muda mwingi kuchonga kinyago hicho.
Anasema kinyago hicho kimetengenezwa kwa kutumia shina la mti aina ya mpingo na hata kuingia katika sebule yake ilimlazimu kuvunja moja ya dirisha kutokana na ukubwa wa kinyago hicho ambacho ilishindikana kupita mlangoni.
Twende kwenye elimu, nimekuwa Chancellor (Mkuu wa Chuo) wa Open University (Kikuu Huria) kwa miaka 20 tumekuwa na mikutano ya ‘machancellors’. Bado Tanzania tuna vyuo vikuu vingi kuliko jirani zetu Kenya, Uganda na sasa ukishakuwa kuliko Kenya na Uganda sembuse Rwanda na Burundi. Hata Zambia, hata Msumbiji hawajafika hivyo mimi nasema kuwa hili jambo la Watanzania kunung’unika kila siku kwamba hatuna hiki hatujafanya hivi, ni kana kwamba hatujafanya maendeleo nasikitika sana tunajitukana.
Wengine wanaosema hivyo hawajatoka waende wakaone na mahali pengine palivyo. Nenda Horohoro mpaka wa Tanzania na Kenya, ukija kwetu unaona watu, vijiji na nyumba za bati, palepale unapita mpaka unaenda Kenya, utaona tofauti.
Ukiangalia ukubwa wa nchi ukichukua Kenya na Uganda ukaziweka pamoja bado Tanzania ni kubwa kuliko nchi hizo kwa zaidi ya maili 6,000. Kwa hiyo wenzetu wakijenga barabara ya lami zaidi ya km 150 wameshafika kwenye mpaka wa nchi, lakini sisi kujenga barabara kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma ni zaidi ya Km 1000.
Nafikiri kwa nyinyi watu wa habari ukianza kuzungumzia vitu vizuri ambavyo Serikali imefanya wataanza kutukana huyo amekuwa CCM number two au CCM B .
Swali.Sasa hivi tunaona vyuo vyote vinatoa shahada, hata vyuo vya kutoa vyeti au stashahada vinabadilishwa, unalizungumziaje hili?
Malecela: Na hilo ni kosa kubwa sana unapokuwa na mhandisi lazima huku chini uwe na watu wa kukuunga mkono, sasa hao ndio tulikuwa tunawatoa mafundi, Mbeya, Dar Technical ni kweli ulivyosema.
CBE sasa imekuwa chuo kikuu. Chuo cha Mipango kilijengwa kwa lengo la kusaidia maendeleo vijijini, malengo ya Mwalimu (Nyerere) kila kijiji kiwe na mtu ambaye anaweza akasaidia mipango ya maendeleo sasa ni chuo kikuu.
Mimi nilipokuwa India, nimeona mtu na shahada ya uzamili lakini ni kondakta wa daladala, kwa nini? Kwa sababu Chuo Kikuu cha Bombay kilikuwa kinapokea zaidi ya wanafunzi 60,000 kila mwaka.Ndio nakwambia sasa tuna viwanda vya kutengeneza mabomu.

No comments: