Friday 1 August 2014

Uongozi mbaya wa shule chanzo cha ugonjwa wa watoto kupagawa

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia wasichana wengi hasa wakiwa shuleni wakipata matatizo ya kuweweseka, kupiga kelele na kuchanganyikiwa kiasi cha kushindwa kuendelea na masomo.
Ingawa watu wa jinsia zote, wakubwa kwa wadogo wanaweza kupata tatizo hili, wanaoathirika zaidi ni wanawake hasa wasichana wa umri kati ya miaka 12 na18.
Matukio ya wanafunzi kupagawa, kuweweseka na kupiga kelele yametokea jijini Dar es Salaam katika shule kadhaa za msingi. Agosti 2005, wanafunzi 24 wa Shule ya Msingi ya Uwanja wa Ndege walipata tatizo hilo na Novemba 2006, wanafunzi 15 wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Mbuyuni.
Matukio kama yayo yametokea katika mikoa mingine kama tukio la Machi 2007 kwenye Shule ya Msingi ya Lewa wilayani Korogwe, Tanga, Mei  2008 lilipotokea kwa wanafunzi 50 na mwalimu wao mkoani Dodoma na wanafunzi 30 wa Shule ya Msingi ya Mang’ula mkoani Morogoro mwaka 2009.
Hali hii imekuwa ikipokewa kwa hisia tofauti na watu mbalimbali katika jamii. Wengine huihusisha na imani za kishirikina, kupagawa na pepo au kudhuriwa na mizimu.
Ingawa jamii ina maoni tofauti kuhusu tatizo hili, wanasayansi wanaamini kuwa hali hii inatokana na matatizo ya afya ya akili yanayojulikana kama hysteria.
Kihistoria ugonjwa huu ulianza zamani hata kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Jina la ugonjwa huu lilitokana na mawazo ya madaktari wa zamani wa Kigiriki waliokuwa wanafikiria kwamba chanzo cha ugonjwa huu ni matatizo katika mfuko au mji wa mimba wa mwanamke, ambao kwa Kigiriki unaitwa hystera.
Madaktari wa Kigiriki walidhani kuwa huu ni ugonjwa unaowapata wanawake pekee. Hii ilitokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa tatizo hili kuwa wanawake, na hata pale wanaume walipokuwa na dalili za tatizo la hysteria ilidhaniwa kuwa wana tatizo jingine kwa vile hawakuwa na mfuko au mji wa mimba.
Dhana ya madaktari wa kipindi hicho juu ya ugonjwa huu ilikuwa kwamba mfuko wa kizazi (mji wa mimba) unabana na kukauka kutokana na kutokufanya ngono kwa muda mrefu au kuzidiwa na hamu ya ngono.  Matibabu ya enzi hizo yalihusisha kumtekenya mwanamke katika sehemu zake za siri ili apate kumaliza hamu ya ngono, lakini matibabu hayo yalikuwa hayatoi matokeo ya uponaji yaliyotarajiwa.
Hata hivyo, sayansi ya tiba ya binadamu imethibitisha kuwa hysteria ni ugonjwa wa akili unaotokana na msongo mkali wa mawazo na hisia.
Linaonekana ni tatizo zaidi la afya ya akili na kisaikolojia.
Tatizo hili hutokea pale mtu anapopata msongo wa kihisia maishani zaidi ya vile alivyojiandaa au anavyoweza kukabiliana nao. Mara nyingi msongo huu hutokana na hisia au mgogoro wa fikra, kutokuwa na uhakika wa usalama katika siku za usoni, kutengwa na jamii au kutosikilizwa kwa upendo. Tamaa kali ya kutaka kupendwa kuliko kawaida isipotimizwa, pia huleta tatizo hili.
Wakati mwingine hisia na fikra hutokana na matatizo ya kawaida, lakini akili huyakuza sana na mhusika akajiona hawezi kuyakabili, hafai na hathaminiwi.
Mgonjwa anaweza kujilaumu na kupata hisia za kupoteza ulinzi au kupata kumbukumbu isiyonyamazishwa ya tukio la kinyama alilotendewa kama vile kubakwa, kunyanyaswa au ukatili  wa kijinsia.
Watu wanaopata ugonjwa wa hysteria huwa na matatizo ya kihisia ambayo mara nyingi hawapendi kuyazungumzia na kwa sababu hiyo, matatizo hayo huwaelemea sana.
Katika utafiti uliofanywa na Altamura AC na wenzake nchini Malawi, iligundulika kuwa wanawake wengi, hasa wasichana hupata msongo mkali sana wa mawazo, kujilaumu na kushuka sana moyo pale wasiporidhishwa na hali ya maisha waliyo nayo. 
Mwanasaikolojia Mareesa Dannielle wa New Zealand, katika utafiti wake mwaka 2007, alibaini kuwa uongozi mbaya wa watu unaweza kuchangia kwa namna moja ama nyingine kutokea kwa tatizo hilo.
Kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Ulanga,  Eddy Mjungu anasema: “Hii inaweza kuwa watoto kutolelewa vizuri, uhusiano wao na wazazi, walimu na hata migogoro ya kimapenzi.”
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu mmoja pekee lakini pia unaweza kusambaa kwa wengine katika kundi la watu wanaokabiliwa na msongo wa kisaikolojia unaofanana na wanaokaa au kufanya kazi katika mazingira yanayofanana.
Hysteria inayosambaa huanza na mtu mmoja na anapoonyesha dalili, wengine nao huanza kujenga hofu na hisia za kuathirika baada ya kumwona mwenzao.
Mara nyingi dalili za hysteria inayosambaa hazionyeshi chanzo bayana na hazitafasiriki sawasawa lakini zinaenea kwa haraka miongoni mwa walioona mgonjwa wa kwanza aliyepata tatizo.
Hofu huongezeka zaidi na tatizo husambaa zaidi pale linapoanza kuhusishwa na imani za kishirikina, mambo ya kimizimu na kupagawa na majini au pepo wabaya.
Hofu huzidi pale timu ya wataalamu wa uchunguzi wa vyanzo vya magonjwa wanaposhindwa kubaini chanzo bayana cha tatizo.
Hysteria ingawa ni tatizo la  afya ya akili, pia hudhuru afya ya mwili kwa kiwango kikubwa. Hofu, woga na wasiwasi husababisha mapigo ya moyo wa mgonjwa kwenda haraka, kutapika, kupata kichefuchefu, mwili kuishiwa nguvu na maumivu ya kichwa.
Matatizo mengine ni pamoja na miguu kufa ganzi, kushindwa kutembea, kupiga kelele au kucheka sana bila sababu za msingi na  kupata degedege.
Wagonjwa wengine hupoteza hamu ya chakula, kutokupata choo kabisa au kuharisha na wengine hutokwa jasho jingi, kutetemeka, kupumua kwa shida au kushindwa kupumua vizuri kiasi kwamba hewa chafu ya ukaa haitolewi mwilini kwa kiwango cha kutosha.

No comments: