Ni katika kikao cha maridhiano chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Dar es Salaam. Kete ya mwisho ya
kuamua iwapo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watarejea
katika Bunge la Katiba au la itachezwa leo katika kikao cha maridhiano
baina ya umoja huo na CCM, chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi.
Kikao hicho kinafanyika siku nne kabla Bunge hilo
kuendelea na vikao vyake Jumanne ijayo licha ya msimamo wa Ukawa wa
kuendelea kuvisusia.
Kikao hicho kinachovikutanisha vyama vya
NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na CCM ni cha mwisho baada ya kile cha kwanza
kilichofanyika wiki moja iliyopita kumalizika bila mwafaka wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa na
wenyeviti wenzake, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim
Lipumba (CUF), Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hadi jana
msimamo wao ni kutohudhuria vikao vya Bunge hilo labda ikitokea miujiza
katika kikao cha leo.
Mbowe alisema ni miujiza kwa sababu kwa madai ya
Ukawa, ni lazima mjadala huo ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo
imebeba mapendekezo ya wananchi na kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka
CCM, kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha ambayo si
rahisi wenzao kuyakubali.
Moja ya ajenda ya kikao hicho ambacho leo kitakuwa
na wajumbe 20 kutoka kila chama, ni kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni
ili kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa walisusia vikao vya Bunge la Katiba hilo
Aprili 16 wakipinga kubadilishwa Rasimu ya Katiba na wajumbe wa CCM kwa
maelezo kuwa ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alisema ni jambo la kushangaza kuona Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta
wakitoa kauli za kuwashutumu Ukawa wakati wakijua wazi kuwa kuna
mazungumzo kati ya vyama vya siasa na Jaji Mutungi vinaendelea.
Juzi pia, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata), liliisihi Ukawa kurudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa
kupata Katiba Mpya, lakini likasema mjadala huo uzingatie Rasimu ya
Katiba.
“Hata viongozi wa dini nao wametoa matamko
wakitaka Ukawa turejee bungeni, tunashukuru maoni yao. Ila wanatakiwa
kujua sababu zilizotufanya mpaka tukasusia. Wanatakiwa kuwaonya CCM
wanaokwenda kinyume na mchakato huo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati tupo katika mazungumzo, Sitta anaanzisha
kikao chake na kutoa tamko kuwa Bunge litaendelea wakati akijua Ukawa
wapo katika kikao pamoja na viongozi wa chama chake cha CCM. Kauli hizi
zinazokosa umoja zinaonyesha Serikali na timu nzima haiko tayari
kutafuta mwafaka wa suala hili.”
Profesa Lipumba
Akieleza sababu nyingine za Ukawa kususia vikao
vya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba aliwataka viongozi wa dini kutambua
kuwa CCM ndiyo chanzo cha mchakato huo kuingia dosari, kwamba
wanatakiwa kukionya chama hicho kiheshimu maoni ya wananchi.
“Tuliondoka bungeni kwa sababu Sitta alishindwa
kuwadhibiti wajumbe wa Bunge la Katiba waliokuwa wakizungumza lugha za
matusi, kejeli, uchochezi na ubaguzi, alivunja kanuni za Bunge kwa
kuruhusu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni kabla ya Bunge kusikiliza hotuba
ya ufunguzi ya Rais Jakaya Kikwete.”
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kauli ya Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
kueleza kanisani kuwa nchi itaingia vitani iwapo muundo wa serikali tatu
utapita, kwamba Zanzibar inataka serikali tatu ili kurejesha Waarabu
visiwani humo.
“Lukuvi aliyasema hayo kanisani akimwakilisha
Waziri Mkuu Pinda. Licha ya kutoa maneno ya uchochezi hakuna mamlaka
iliyo juu ya Lukuvi iliyoomba radhi kwa kauli yake,” alisema.
Mbatia
Mbatia alisema rasimu inayotakiwa kujadiliwa ni ile iliyopendekezwa na Tume ya Warioba yenye muundo wa Serikali tatu.
“Hata kuhusu Tunu za Taifa zilizotajwa katika
rasimu; yaani utu, uzalendo, uadilifu, uwazi, umoja, uwajibikaji na
lugha ya taifa wenzetu wa CCM wameyakataa. Sasa sijui wanataka
kulipeleka wapi hili taifa. Tutaendeleaje kujadili?” alihoji.
Hofu ya wajumbe
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa Bunge
hilo wamesema kutorejea bungeni kwa Ukawa kutaathiri upatikanaji wa
Katiba Mpya yenye maridhiano.
Mmoja wa wajumbe hao, Charles Mwijage alipendekeza
kusitishwa kwa mchakato huo kwa kuwa maridhiano ni jambo muhimu katika
kutengeneza Katiba.
“Kukosekana kwa Ukawa bungeni kutaathiri
upatikanaji wa Katiba Mpya kwa sababu suala hili linahitaji zaidi
maridhiano ya pande zinazotofautiana kiitikadi,” alisema Mwijage ambaye
pia ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM).
“Ningekuwa na uwezo, ningeamua mchakato huu wa Katiba usitishwe
na tuendelee kutumia Katiba iliyopo kwa sababu suala hili linahitaji
zaidi maridhiano,” alisema.
Mbunge huyo alisema, “Ukawa wanataka kujenga
mazingira ya kuja kuikataa Katiba itakayopatikana ili watusababishie
vurugu na mapigano.”
Alisema Rais aliona kwamba kundi la wajumbe 629
likikaa pamoja linaweza kutengeneza Katiba Mpya kwa maridhiano, lakini
kama kuna kundi linajitoa ni wazi kwamba kutakuwa na dosari katika
utengenezaji.
Mjumbe mwingine, Ezekiah Oluoch alisema iwapo
wajumbe wa CUF kutoka Zanzibar ambao wanaunda Ukawa hawatarejea bungeni,
Katiba Mpya haiwezi kupatikana kwa sababu theluthi mbili haziwezi
kupatikana.
“Katiba haipatikani kwa ubabe au wengi-wape, bali
inapatikana kwa maridhiano na mwafaka bila kujali idadi ya wingi wa
wajumbe,” alisema Oluoch ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Walimu Tanzania (CWT).
Alisema Bunge hilo litatumia fedha nyingi za
walipa kodi bila kupata Katiba Mpya, hivyo akashauri mchakato huo
usogezwe mbele hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Lackson Mwanjali
alisema kitendo cha Ukawa kukataa kurejea bungeni ni pigo katika
mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu inatengenezwa kwa majadiliano na
kufikia mwafaka.
“Tunapokuwa bungeni watu kutoka vyama na itikadi
tofauti tunajadiliana, tunabishana na baadaye kufikia mwafaka na kufanya
maridhiano, sasa wenzetu hawapo ni tatizo kubwa,” alisema.
Mwanjale alisema ingawa wanakwenda kwenye Bunge Maalumu la Katiba itakuwa vigumu kupata Katiba bora.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Diana
Chilolo alisema wangependa Ukawa warejee bungeni lakini kama hawaendi
watawakilishwa na wenzao.
“Wapo watu kutoka katika vyama vya upinzani pale
ambao watawawakilisha. Yupo Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema na
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo watawawakilisha na
tutapata Katiba bora,” alisema Chilolo.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Saidi Mkumba alisema
Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote hivyo kundi la Ukawa kukataa
kurudi bungeni hakuwezi kusimamisha mchakato huo.
Mambo sita ya kuzingatia
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Khoti
Kamanga amebainisha mambo sita yanayotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya
Bunge hilo kuanza vikao vyake Agosti 5.
Akizungumza katika kilele cha Siku ya Wanawake
Afrika iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo
Barani Afrika (WilDAF), Dk Kamanga alisema:
“Mosi, huu utaratibu wa wengi-wape ni mzuri lakini
tusiung’ang’anie ingawa demokrasia inaruhusu na kinachotakiwa ni kuweka
mbele masilahi ya taifa.”
“Kuna wachache wanakuwa na hoja za kutosha lakini
kutokana na uchache wao demokrasia inawatupa. Katika suala la Katiba
maridhiano ni jambo la muhimu na suala la wengi-wape liwekwe kando.”
Pili, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
inatakiwa kufanyiwa marekebisho hasa Kifungu cha 36 (5) kilichobainisha
kuwa endapo mwafaka hautapatikana Katiba ya mwaka 1977 itaendelea
kutumika.
“Unapoanza safari huwezi kushindwa na ukarudi
nyuma, kwa kuwa kila mmoja amekiri kwamba Katiba ya sasa ina viraka 14
ambavyo ni vingi sana,” alisema.
Jambo la tatu, Dk Kamanga alisema kunahitajika
ujasiri katika kubaini na kukubali ni wapi mchakato wa Katiba
ulipojikwaa. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kuheshimiwa na si
kukiukwa.
Jambo la nne ni kuwa, Bunge linatakiwa kujadili
rasimu na kutokwenda kinyume na sheria ilivyo kama ilivyoandaliwa na
Tume ya Katiba kwa mujibu wa sheria.
“Rasimu iliyopo ya Desemba 2013 iliandaliwa na
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyokusanya maoni ya wananchi, hivyo sheria haitakiwi kuvunjwa, pia
Bunge linatakiwa kuizingatia,” alisema.
“Tano, tunatakiwa kusoma rasimu ili unapochangia
au kuona mtu akichangia uwe unajua anachokisema na jambo la mwisho ni
ngumu kwa vyama kuweka kando masilahi yao lakini kwa jambo hili
wanatakiwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa,” alisema Dk Kamanga.
No comments:
Post a Comment