Saturday 4 October 2014

Wanajeshi, polisi watwangana risasi

Tarime. Watu 12 wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi ya kurushiana risasi baina ya askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi 128 KJ cha Nyandoto na Polisi wa Kituo cha Stendi wilayani Tarime mkoani Mara.
Hatua hiyo imekuja wakati wanajeshi hao walipokuwa wakijaribu kumchukua askari mwenzao aliyekamatwa na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuendesha pikipiki bila kuwa na kofia ngumu.
Mashambulizi hayo ya kurushiana risasi na kutwangana ngumi na mateke yalitokea juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Stendi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Bernard Makonyo alisema amepokea majeruhi 10, kati ya hao wawili ni askari wa JWTZ, polisi saba na raia mmoja. Alisema majeruhi tisa wameruhusiwa na mwingine kupelekwa Hospitali ya Shirati kwa matibabu zaidi.
Dk Makonyo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Aloyce Filbert (24) aliyepigwa risasi mguu wa kulia, Deodatus Dominic (26) aliyejeruhiwa puani na wote ni askari wa JWTZ.
Wengine ni askari polisi saba ambao ni Makoye Katula (26), Sylvester Michael (31), Salum Omary (44), Abdallah Halifa (24), Joel Msabila (25), Ally Juma (27) na Deogratius Tryphon (32) na raia Hamza Jumanne (33) aliyepigwa risasi mguu wa kushoto ambaye alipelekwa Hospitali ya Shitari, Rorya kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Ndalama Salumu anadaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa katika vurumai hizo huku mwananchi mwingine, David Kisaro (20) akijeruhiwa kwa bomu jichoni. Alitibiwa katika Zahanati ya Tarime.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Benedict Mambosasa alisema mwanajeshi aliyekamatwa alifanya makosa kwani baada ya kukamatwa na kuombwa kwenda kituo cha polisi, alikaidi.
Mambosasa alisema mwanajeshi huyo licha ya kukiuka taratibu, aliwatolea lugha za matusi polisi jambo lililowalazimu kumkamata kwa nguvu, ndipo wanajeshi wenzake walipoingilia kati na kusababisha kutokea kwa majibishano ya risasi za moto. Hata hivyo, alisema hakuna aliyejeruhiwa.
Alisema wanajeshi watatu ambao hawakutajwa majina, wamekamatwa na polisi kwa kuvunja utaratibu wa usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amelaani kitendo hicho cha kurushiana risasi za moto hewani akisema ni cha utovu wa nidhamu na maadili ya kazi ya jeshi na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema wananchi Tarime wameshangazwa kwa kitendo kilichofanywa na walinda usalama hao, wakisema si cha kinidhamu huku wakisema kilikwamisha shughuli zao kwa muda kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
 Mkazi wa Tarime, Joseph Samson amesema kitendo hicho kimewashangaza sana wananchi.

KATIBA: Mtifuano wahamia uraiani

Dar es Salaam. Baada ya Bunge la Katiba juzi kufanikiwa kupata theluthi mbili ya wajumbe wa pande zote mbili za Muungano na kupitisha Katiba inayopendekezwa, sasa msuguano kuhusu Katiba unaonekana kuhamia uraiani.
Msuguano kuhusu Katiba hiyo unatarajiwa kuendelea mitaani, ndani ya vyama vya siasa na kwenye majukwaa kutokana na tofauti ya mitizamo iliyoibuka kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopitishwa.
Ingawa matokeo ya kura za ushindi yalipokewa kwa furaha na wajumbe waliokuwapo bungeni kwa kucheza na kurusha vijembe kwa wapinzani, huenda kibarua kitakuwa kigumu kwa CCM itakapolazimika kupambana na wananchi, wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa dini ‘waliojeruhiwa’ na mwenendo wa Bunge.
Bunge hilo liliendeshwa kwa upinzani mkali kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu waliokuwa wakitaka lisimamishwe kwa madai kuwa limechakachua maoni yao kama yalivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
CCM na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar
CCM iliingia doa baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kuzua kizaazaa bungeni Jumatano wiki iliyopita kwa kupiga kura ya hapana katika ibara 22 kwenye Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
Mwanasheria huyo ambaye awali alijiondoa kwenye Kamati ya Uandishi kwa kutoridhishwa na mambo yalivyokuwa yanakwenda, alizomewa na baadhi ya wajumbe na kulazimika kutolewa ukumbini akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Bunge.
Akizungumza na gazeti hili, Othman alisema kuwa alichofanya kilikuwa ni utashi wake kwa kuwa Serikali ilitamka kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kuwa haikuwa na msimamo.
 “Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa maana ya upande, maana yake ni ipi pengine unisadie… nilipiga kura kwa kuzingatia utashi wangu na maoni yangu,” alinukuliwa Othman.
Ingawa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta alimtetea Othmani kwa kusema wajumbe hawakupiga kura kwa kutumia vyeo vyao, kwa namna wajumbe walivyoonyesha jazba imeonyesha kuwa CCM itapaswa kusafishwa taswira iliyochafuka.
Sitta na viongozi wa dini
Kwa upande mwingine, Sitta amejikuta akiingia kwenye ‘vita’ na viongozi wa dini, baada ya kuwataka waumini wa madhehebu mbalimbali kuupuza nyaraka zilizotolewa na viongozi hao kwa kuwa hazina utukufu wowote wa Mwenyezi Mungu.
Sitta alisema baadhi ya viongozi wa dini wanalenga kuliingiza taifa kwenye machafuko na kwamba yeye hatakuwa tayari kuvumilia hali hiyo.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
Huku akiwa na waraka huo mkononi, Sitta alisema kuwa lugha iliyotumika haina staha na haikupaswa kutumiwa na watu wanaohubiri dini duniani.
Akizungumzia kauli ya Sitta, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema kauli ya Sitta inaonyesha kuwa amechoshwa na mwenendo wa Bunge la Katiba.
 “Sikutarajia kiongozi kama huyo kutoa kauli mbaya kama hiyo kwa Taifa zima. Sikutegemea mheshimiwa kama huyo kusema maneno kama hayo… Huenda ana stress (msongo wa mawazo). Hata ikiwa hivyo, hakupaswa kutoa kauli nzito kama hiyo. Anatakiwa kufahamu kuwa waraka huo umetoka kwa Wakristo wote hapa nchini,” alisema Askofu Kilaini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana alisema kitendo cha Sitta na wenzake kushindwa hata kuelewa waraka wa viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”, ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.
Hata hivyo, jana Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Father Raymond Saba, amesema bado wanaendelea kutafakari kauli ya Sitta na kwamba kwa sasa hawajatoa taarifa yoyote.
Akizungumzia kauli ya Sitta, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kauli ya kiongozi huyo imeongeza mpasuko wa dini nchini hasa kuhusu mahakama ya kadhi.
“Viongozi wa dini wameipokea kauli ya Serikali kwa kuwa tu alisema ni kiongozi wa Serikali, lakini itatokea shida kama ahadi yao haitatekelezwa,” alisema Salim.
Sitta na Jaji Warioba
Sitta amejikuta kwenye vita ya maneno na Jaji Warioba huku kila mmoja akisisitiza kuwa anafanya kazi aliyotumwa na wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hivi karibuni, Jaji Warioba alisema ataingia mitaani kuitetea Rasimu ya Katiba iliyokuwa imebeba maoni ya wananchi.
Alisema kuwa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu.
Hata hivyo, akizungumza jana na gazeti hili alisema kuwa Katiba hiyo imeacha maswali mengi kuliko majibu hasa kwa upande wa Zanzibar.
Sitta alalamikia kutukanwa
Sitta atakuwa na kibarua kingine cha kujisafisha mbele ya wananchi ambao alikaririwa akisema kuwa wamekuwa wakimtumia meseji za matusi za ya 50 kila siku.
Kwa nyakati tofauti wananchi wasiojulikana wamekuwa wakiandika meseji za matusi kwenye mitandano na simu kwa kile wanachosema kuwa Sitta amelazimisha maoni ya CCM yatawale Bunge.
Wananchi wasubiri waelezo zaidi
Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu mwenendo wa Bunge hilo, waliwalaumu wajumbe wa Bunge waliokuwa wakisema walipiga kuwa kwa niaba ya wananchi kwenye majimbo yao.
Walihoji ni lini wajumbe hao ambao ni wabunge wao walikwenda kuwauliza iwapo wanataka kupiga kura ya hapana au ndiyo dhidi ya Katiba iliyopendekezwa?
‘Mimi nimesikia tu mbunge wetu (anamtaja) amesema wananchi wake wamechagua kura ya ndiyo. Ni nani alimtuma kwenda kuwa tunataka Katiba hiyo wakati maoni yetu tulitoa tofauti, “ Yohana Change mkazi wa Vwawa, Mbozi.
Mwanaidi Suleiman alisema haelewi nini kilichotokea bungeni, kwa kuwa matarajio aliyokuwa nayo kuhusu Katiba yameyeyuka baada ya kusikia mambo mengi yamekataliwa.
“Nafuu kama wangeondoa mambo mengine, lakini siyo serikali tatu na uraia wa nchi mbili. Mimi hayo niliyaona makubwa sana, kama hayapo sasa Katiba itahusu nini?” alihoji Mwanaidi.
Chadema na wanachama wake.

Hali ya hewa ndani ya Chadema ilichafuka baada ya Sitta kusema kuwa kuna wajumbe wawili wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka Zanzibar walikubali kupiga kura kinyume na msimamo wa vyama vyao.
Sitta alisema kuwa kati ya wajumbe hao, mmoja alikubali kupiga kura na kusema yuko tayari hata kufukuzwa na chama chake.
“Sasa wale wanaotumia mbinu za ovyoovyo ili mchakato huu usikamilike wanapoteza muda, maana ukizuia maji huku, yanaelekea kwenye mkondo mwingine,” alisema Sitta.
Taarifa hizo zilionekana kuwalenga wabunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha na Mwanamrisho Abama ambao kwa nyakati tofauti walithibitishwa kutafutwa ili apige kura.
“Kweli nimesumbuliwa sana na watu ambao siwezi kuwataja na wananitaka nipige kura na wengine walifika mpaka nyumbani lakini mimi siwezi kushiriki maana nikifanya hivyo dhamiri yangu itanishtaki,” alisema Msabaha.
Naye Abama alisema kuwa alikuwa amepewa ilani na viongozi wake kwamba anatafutwa ili akapige kura, hivyo aliamua kukaa ndani kukwepa mtego huo.
Kauli hizo mbili tofauti zinauachia Ukawa maswali magumu yanayohitaji majibu ili kubaini iwapo kuna usaliti wowote umefanyika au la.
Wabunge wengine ambao wanaweza kukukumbana na matatizo ndani ya chama hicho ni Mbunge John Shibuda (Maswa Mashariki), Said Arfi (Mpanda Mjini) ambao walikiuka uamuzi wa Ukawa kutoshiriki Bunge hilo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alisema kuwa suala la wasaliti wa chama linatarajiwa kuzungumzwa kwenye vikao vya ndani.
“Siwezi kulitolea uamuzi suala hilo, baada ya kumaliza uchanguzi sasa litazungumzwa ndani ya vikao vya chama na kutolewa uamuzi,” alisema Dk Slaa.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kuwa Sitta alipaswa kuwataja wajumbe kutoka Ukawa waliokubali kupiga kura, lakini hakufanya hivyo.
“Juzi amechukua kura zao na hawataji ni kina nani wala walipiga kura kwa njia gani. Hata akijiongezea hizo kula mbili feki bado BMK upande wa Zanzibar wanabakiwa na kura 145 tu na siyo 146,” alisema Mtatilo.
Wanananchi waikataa rasimu
Naye Joseph Lyimo kutoka Manyara, amesema kuwa baadhi ya wakazi wa mkoani humo, wamesema Bunge la Katiba limepitisha rasimu ya Katiba bila maridhiano kwa baadhi ya wajumbe hivyo kusababisha hofu ya kupatikana kwa katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi.
Wakizungumza jana na mwandishi wa habari hizi, wananchi hao walidai kuwa rasimu hiyo iliyopitishwa bungeni juzi haikukidhi maoni yaliyotolewa kwenye tume ya Warioba kwani ibara 28 zimefutwa na kuwapo ibara mpya 42.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Abdalah Mtengeti alisema kwenye Tume ya Warioba wananchi walipendekeza mbunge awe na ukomo wa madarakani kwa miaka 15, lakini sasa wabunge hao wameridhia asiwe na mwisho wa utawala.
“Wananchi hawawezi tena kumwajibisha  mbunge waliyemchagua wao wenyewe kama walivyopendekeza awali pia hakuna ukomo wa mbunge tena hivyo atatawala hadi mwenyewe aseme sigombei tena,” alisema Mtengeti.
Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Manyara, Frank Oleleshwa alisema rasimu hiyo ya wabunge haikujali maoni ya wananchi kwani walipendekeza kufutwa kwa vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya lakini, wabunge wameridhia.
“Pia wananchi walipendekeza kuwepo na Serikali tatu ikiwamo kurudisha Tanganyika ili kuwapo na usawa wa nchi, lakini wabunge wamegoma hilo na kuridhia Rais wa Zanzibar awe makamu wa pili wa Rais,” alisema Oleleshwa.
CCM, CUF Zanzibar
 Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai walipozungumza na  gazeti hili kwa nyakati tofauti visiwani humo, Mazrui alisema kwamba mambo yaliyopitishwa na Bunge la Katiba katika rasimu hiyo yanagongana na Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ikiwamo suala la mamlaka ya ugawaji mikoa aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Alisema Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano utekelezaji wake utakuwa mgumu kwa baadhi ya mambo Zanzibar mpaka Katiba ya Zanzibar ifanyiwe tena marekebisho na kabla ya kufanyika hivyo lazima kuitishwe kura ya maoni kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kwamba kama viongozi wote watafanya kazi kwa kuzingatia sheria na katiba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK) haitoyumba kwa sababu hakuna mshindi wala mshindwa baada ya rasimu ya katiba kupitishwa.
“Matokeo ya kura ya rasimu ya katiba, ni ushindi wa wazanzibari wote na watanzania kwa ujumla, na hakuna mshindi wala mshindwa” alisema Vuai ambaye pia alikuwa mjumbe wa bunge maalum la katiba.

Warioba: Katiba bado ina maswali mengi

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Katiba inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba hiyo bado ina maswali mengi kuliko majibu, hasa katika muungano na mgombea binafsi.
Amesema licha ya Zanzibar kuridhia mambo kadhaa kuwekwa katika orodha ya mambo ya muungano, hali inaweza kuwa tofauti ukifikia wakati wa Zanzibar kubadili Katiba yao ili kuwezesha utekelezaji wa mabadiliko hayo.
Juzi Bunge hilo lilipitisha Katiba inayopendekezwa kwa tofauti ya kura mbili na kuhitimisha kwa sasa mchakato wa kuandika Katiba hadi mwaka 2016 ambapo litafanyika zoezi la upigaji wa kura ya maoni.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana, Jaji  Warioba alisema, “Wasiwasi wangu ni juu ya muungano kwa sababu katika masharti ya mpito ni lazima Zanzibar ifanye marekebisho ya Katiba yake. Rasimu inayopendekezwa inasema Tanzania itakuwa nchi moja pamoja na madaraka ya rais kugawa nchi. Kwa maana hiyo lazima Katiba ya Zanzibar ibadilike.”
Alisema katika mambo ya muungano, Katiba inayopendekezwa imeliweka suala la kodi ambalo halikuwamo katika rasimu iliyotolewa na Tume ya Katiba, kusisitiza kuwa kitendo hicho hakitajibu swali la ‘Tanganyika kuvaa koti la Muungano’.
“Wameongeza kodi ya mapato, ushuru wa forodha  na bidhaa katika mambo ya muungano. Maana yake ni kwamba kodi yote inayokusanywa, ikiwamo ya kutoka Zanzibar itaingizwa kwenye mfuko wa muungano,”alisema.
Aliongeza, “Wakati huo huo Zanzibar imepewa uwezo wa kusimamia mambo yake yenyewe na ili iweze kulitekeleza hilo ni lazima iwe na vyanzo vyake vya mapato. Sasa watasimamiaje wakati mapato yote yanaingia kwenye mfuko wa muungano.”
Alisema ili suala hilo liweze kutekelezwa ni lazima Zanzibar ibadili Katiba yake na kusisitiza kuwa utakapofika wakati wa kubadili Katiba ya Zanzibar, jambo hilo linaweza kukwama.
“Sioni kama Wazanzibar watakubali suala hili. Kama mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yatakwama, ni wazi kuwa Katiba inayopendekezwa haitatekelezeka. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yanategemea maridhiano ya Wazanzibari wenyewe na kumbuka kuwa CUF na CCM wanavutana sana,” alisema Jaji Warioba.
Akifafanua hilo, alisema mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar lazima yapate theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kusisitiza kuwa kwa mvutano wa vyama hivyo viwili visiwani Zanzibar, itakuwa kazi ngumu kupitisha jambo hilo.
“Katiba ya Zanzibar isipobadilishwa kero za muungano zinazozungumzwa zitaendelea. Kazi iliyopo sasa ni kufikiria maridhiano kuhusu muungano, lazima tuhakikishe Zanzibar imekubali kubadili katiba yake na kuridhia mapato yake kuingizwa katika mfuko wa muungano,” alisema.
Aliongeza, “Kama ambavyo Tanzania Bara waliitegemea Zanzibar kupitisha Katiba inayopendekezwa, ni lazima pia ihakikishe kuwa Zanzibar inakubali kubadili Katiba yake.”
Kuhusu mgombea huru Jaji Warioba alisema, “Katiba inayopendekezwa imeweka masharti ya mgombea ubunge na kutaja sifa za ziada za mgombea huru ambazo ukizitazama kwa undani utabaini kuwa wanamkataa mgombea huru kistaarabu.”
Alisema sifa hizo za ziada walitakiwa kuwekewa na wagombea wengine, si mgombea huru pekee.
“Mfano ni kutoruhusu mtu kutoka katika chama cha siasa kisha  kugombea kama mgombea huru,” alisema.
Jaji Warioba aliyataja baadhi ya mambo ya msingi yalikuwamo katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingizwa tena katika Katiba inayopendekezwa kuwa ni malengo muhimu ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimazingira.

Ukawa sasa waja na tuhuma nzito kuhusu kura

Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeibua shutuma dhidi ya uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kwamba unawarubuni kwa fedha baadhi ya wajumbe wa umoja huo ili kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.
Kamati ya Ufundi ya Ukawa, ilisema jana kuwa wajumbe wanaorubuniwa wapige kura ya ‘ndiyo’ kwa ahadi ya kupewa zaidi ya Sh500 milioni ni wa CUF na wengine wanne wa Chadema wanaotoka Zanzibar.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Khamis Hamad alikanusha madai hayo, akisema hajasikia kitu kama hicho na ndiyo kwanza alikuwa anasikia hilo kutoka kwa mwandishi wa habari hizi... “Hakuna kitu kama hicho, hilo jambo ndiyo nalisikia kutoka kwako.”
Kutokana na madai hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukawa, John Mnyika alisema kamati hiyo ilianza kikao cha siku mbili kuanzia jana kujadili hali hiyo na kutoa mapendekezo kwa uongozi wa juu wa umoja huo.
Licha ya Mnyika kukataa kutaja majina ya wajumbe waliorubuniwa, wajumbe wa Chadema wanaotokea Zanzibar ni Zeudi Abdallah ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Maryam Msabaha, Mwanamrisho Abama na Raya Ibrahim. “Tumewataka wajumbe wetu wote kukusanya ushahidi na kuuwasilisha kwa viongozi wa Ukawa,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara.
Aliongeza, “Chadema ina wajumbe wanne, watatu ni wabunge wa kawaida na mmoja wa kuteuliwa na Rais (Kundi la 201). Tumepata taarifa kutoka kwa wajumbe hao kwamba wanapigiwa simu na uongozi wa Bunge ukiwataka wasaini karatasi za kupigia kura ili uongozi wa Bunge uchakachue kura.
“Tumeanza kikao kujadili suala hili ila tumeamua kwanza tuueleze umma kupitia vyombo vya habari juu ya ‘uharamia’ unaofanywa na Bunge la Katiba linaloongozwa na Sitta (Samuel) na Makamu wake Samia (Suluhu Hassan).”
Ukiukaji kanuni
Akinukuu Kifungu cha 36 (3) cha Kanuni za Bunge la Katiba, Mnyika alisema si sahihi Sitta kutaka wajumbe waliopiga kura ya ‘hapana’ kuitwa katika Kamati ya Mashauriano na uamuzi huo ni kinyume na kanuni...
“Ni kama kuwatisha tu wajumbe.”
Kanuni hiyo inasema; “Endapo baada ya ibara ya Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa upya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye Kamati ya Mashauriano ili kupata mwafaka.”
Sitta awataje
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Joran Bashange alimtaka Sitta kutaja majina ya wajumbe wa CUF na Chadema waliopiga kura... “Tunamtaka awataje kwa majina maana ujanja wake na wenzake tumeshaujua na tuna ushahidi wote.”
Bashange alisema mpaka sasa hakuna mjumbe wa Bunge hilo ambaye ni mjumbe wa Ukawa aliyepiga kura kupitisha Katiba inayopendekezwa.
“Ndiyo maana walibadili kanuni ili kuruhusu wajumbe kupiga kura kwa faksi na baruapepe ili kufanya ‘uharamia’ wa kuiba kura,” alisema.

Friday 19 September 2014

Mbowe ajisalimisha polisi, Shughuli zasimama

Dar es Salaam. Shughuli za kiserikali katika Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi jirani, jana zilisimama kwa siku nzima kutokana na hekaheka zilizoibuka baina ya polisi na wafuasi wa Chadema pale mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alipojisalimisha polisi.
Hekaheka hizo ziliibuka kuanzia saa 5.10 asubuhi baada ya Mbowe akiongozana na wanasheria wa chama hicho, kufika katika ofisi za Makao Makuu ya Polisi ambako pia zipo ofisi za wizara hiyo kuhojiwa kuhusu kauli yake ya kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya Mbowe kuwasili, alifika Mkurugenzi wa Oganaizesheni ya Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, Benson Kigaira na alipojitambulisha akakataliwa kuingia.
Baadaye waliwasili mawakili, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando ambao waliruhusiwa kuingia, kisha wakafuata Mbowe, John Mnyika na wanasheria wengine akiwamo John Malya na Peter Kibatala.
Wakati huo, Barabara ya Garden inayokatiza mbele ya wizara hiyo ilikuwa imefungwa na wafuasi wa Chadema walikuwa wamezuiliwa kwa mbali. Kila mwananchi aliyefika katika jengo hilo kupatiwa huduma, alijibiwa na askari waliokuwa na mbwa na silaha kuwa, “hakuna shughuli yoyote inayofanyika hadi kesho (leo)”.
Hali hiyo iliendelea hadi saa 9:10 alasiri baada ya Mbowe aliyehojiwa kwa saa mbili kuhusu tuhuma za uchochezi kuachiwa kwa dhamana.
Baada ya kuachiwa, Mbowe alisindikizwa kwa msafara wa magari manne ya polisi akielekea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, ambako alipanda ndege kwenda Afrika Kusini kwa shughuli za kichama.
Ilivyokuwa
Ombi lililotolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika kuwataka wanachama wa Chadema kujitokeza kumsindikiza Mbowe polisi, liliitikiwa kwani zaidi ya wanachama 100 walijitokeza katika ofisi hizo.
Walianza kukusanyika mmoja baada ya mwingine nje ya makao mkuu ya jeshi hilo kuanzia saa 4:30 asubuhi na kujichanganya katika kundi la waandishi wa habari, hali iliyosababisha askari polisi waliokuwa na bunduki na mabomu ya machozi kuwataka wanahabari wajitambulishe kwa kuonyesha vitambulisho ili wawatenge na wafuasi hao.
Licha ya juhudi hizo, hawakufanikiwa kuwatawanya wanachama hao ambao awali, walijieleza kuwa walikuwa wamefuata hati zao za kusafiria katika Ofisi za Uhamiaji zilizopo eneo hilo.
Hali ilibadilika baada ya Mbowe kufika katika ofisi hizo akiwa katika msafara wa magari matano huku ukiongozwa na Mnyika na wanachama hao kuanza kuimba nyimbo za chama hicho na kumsifu kiongozi wao.
Msafara huo ulizuiwa kwenye lango la ofisi hizo na askari wa FFU waliwazuia viongozi wengine, wakisema anayetakiwa kuingia ndani ni Mbowe na wanasheria wake pekee.
Baada ya gari la Mbowe kuingia, viongozi na baadhi ya wafuasi wa chama hicho nao walipenya kwa nguvu getini na kuingia ndani ya uzio huku wakisema ‘people’s power’ (nguvu ya umma). Kitendo hicho kiliwatibua FFU na kuanza kutumia nguvu kuwatoa nje, hali iliyozua vurugu kubwa.
Kutokana na mvutano huo, askari zaidi wa FFU waliokuwa katika Land Rover mbili wakiwa na mbwa waliongezeka na kuanza kuwashushia kipigo wafuasi hao huku wakiwataka kusimama umbali wa mita 100 kutoka lilipo jengo hilo.
Baada ya kutolewa ndani ya uzio baadhi ya wafuasi wa Chadema walikaa chini wakisema hawatafanya vurugu na wako tayari kuingia ndani wakiwa wamenyoosha mikono juu.
Katika kundi la wafuasi hao walikuwamo pia baadhi ya wabunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana).
Wabunge waliofika baadaye na kuruhusiwa kuingia ndani ni Suzan Lyimo (Viti Maalumu) na Halima Mdee (Kawe).
Miongoni mwa walioathirika na hekaheka hizo ni wanahabari ambao pamoja na kuonyesha vitambulisho na kamera, baadhi yao walishushiwa kipigo na askari hao.
Katika kipigo hicho, mwandishi wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima, Josephat Isango na Mwandishi gazeti la Hoja, Shamimu Ausi walijeruhiwa. Isango alijeruhiwa mguuni na Ausi usoni karibu na jicho la kulia.
Wakati Isango alisema alivamiwa na askari wawili wa FFU na kwamba hata alipojitambulisha na kuwaonyesha kitambulisho waliendelea kumpiga, Ausi alisema alipigwa rungu usoni na akashangazwa na nguvu kubwa iliyotumika wakati awali, aliruhusiwa kusimama katika eneo alipokuwa akiendelea na kazi.
Baada ya vurugu hizo waandishi wa habari na wafuasi wa chama hicho walitakiwa kusimama katika makutano ya Barabara ya Ghana na Ohio umbali wa mita 100 kutoka yalipo makao makuu ya jeshi hilo kusubiri mahojiano yaishe.
Ilipofika saa 8.45, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alitoka nje ya ofisi hizo na kuzungumza na waandishi wa habari na wafuasi wa chama hicho.
Alisema mahojiano kati ya Mbowe na Jeshi la Polisi yalikwenda vizuri huku akiongozwa na wanasheria na kwamba polisi wamekubali kumpa dhamana lakini kabla hajaondoka, wafuasi wote wanatakiwa kuondoka eneo hilo bila maandamano.
“Polisi wanaomba mtawanyike, hawataki maandamano, wao watamsindikiza hadi makao makuu ya chama yaliyopo Kinondoni, mkifanya maandamano watatumia nguvu kuyazuia na hilo hawataki litokee. Nawaomba mtawanyike,” alisema Lissu.
Baada ya tangazo hilo, wafuasi hao kwa shingo upande, walikubali ushauri huo na kuondoka katika eneo hilo saa 9.00 alasiri.
Ilipofika saa 9.20 Mbowe alitoka katika ofisi hizo akisindikizwa na magari ya polisi aina ya Land Rover zilizojaa askari na baadaye ilielezwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliyekuwa makao makuu ya chama hicho kuwa mwenyekiti huyo alikwenda moja kwa moja Uwanja wa Ndege kwa safari ya kikazi Afrika Kusini.
Mtikila azua gumzo
Wakati hekaheka zikiendelea, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alifika katika ofisi hizo saa 7.26 akiwa katika Bajaj lakini alizuiwa kuingia ndani na akaondoka.
Akizungumza na wanahabari, Mtikila alisema, “Ni lazima Watanganyika tuidai Tanganyika yetu kwa gharama yoyote, aluta continua.”
Makao Makuu
Baada ya kuondoka eneo hilo, wafuasi wa Chadema walikwenda katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni na kupewa maelekezo na Dk Slaa na Lissu.
Lissu alisema Mbowe anatuhumiwa kwa uchochezi kwa kauli yake kuhusu kufanyika maandamano nchi nzima, huku akisisitiza kuwa tuhuma alizopewa “ni za wizi wa kuku”.
“Mbowe aliposema kufanyika maandamano alikuwa na maana kuwa maandamano hayo yatafanyika baada ya Chadema kutoa taarifa, kauli yake haikuwa ya uchochezi hata kidogo,” alisema Lissu.
Aliongeza, “Kama polisi wakitueleza ni sheria ipi inakataza maandamano, sheria ipi inalazimisha wanaotaka kuandamana lazima wawe na kibali na sheria ipi inakataza watu kugoma, watakuwa na ruksa ya kumfunga Mbowe.”
Kwa upande wake, Dk Slaa alisema, “Mbowe baada ya kutoka polisi ameomba nimwagie kwa wanachama wa Chadema. Amekwenda Afrika Kusini katika mkutano wa chama. Safari yake ilikuwa imepangwa tangu juzi na ingeahirishwa kama angenyimwa dhamana leo.”Dk Slaa alimwagiza Kigaira kuhakikisha kuwa wanachama wawili wa chama hicho waliokamatwa na polisi wanaachiwa kwa dhamana. Zoezi la kufanya maandamano likifanyika kama hivi Taifa hili litabadilika,” alisema.

Saturday 13 September 2014

Uwekezaji ulivyoua Mji wa Mirerani-2

Sheikh Mohammed anasema serikali ndio inawanyanyasa wananchi wake kwa kupitisha sheria ambazo zinawazuia kunufaika na rasilimali za taifa lao ambazo Mungu amewapa.
“Wachimbaji wadogo wamepewa migodi yenye ukubwa wa mita 50 kwa 50 lakini mchimbaji mmoja mkubwa amepewa eneo kubwa zaidi ya eka tano halafu inapitishwa sheria ya kuchimba kwenda chini jambo ambalo haliwezekani huku ni kuwazuia wachimbaji wadogo kupata madini” alisema.
Alisema kwa sasa shughuli nyingi za msikiti huo zimesimama kwani wananchi wa Mirerani hawana fedha za kutoa sadaka tofauti na miaka ya nyuma ambapo sadaka ziliwezesha ujenzi wa msikiti huo, shule na kuwa na miradi.
Padri Aloyce Kitomali wa Kanisa la Katoliki Mirerani, alisema kanisa hilo lilikuwa na uwezo wa kukusanya sadaka katika ibada moja zaidi ya milioni moja lakini sasa hata Sh500, 000 hazipatikani kwani waumini hawana fedha.
Anasema miradi mingi ya kanisa hilo, sasa imezorota kwani wananchi wengi wanategemea madini ya tanzanite ambayo sasa hayapatikani na inasemekana anayepata ni mwekezaji.
“Wananchi hapa wengi wana hali ngumu ya maisha tofauti ya miaka ya nyuma kwani uchumi wao ulitegemea sana madini ya Tanzanite” alisema.
Osca Gunewe ambaye ni Katibu wa Bodi ya shule ya Kanisa la Pentekoste, anasema uchumi wa mji wa Mirerani unategemea madini ya Tanzanite hivyo kwa hali iliyopo sasa ni muhimu Serikali kuwasaidia wakazi wa mji huo.
Gunewe ambaye aliwahi kuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mirerani, anasema ingewezekana kuwasaidia watu wa Mirerani hata kwa kutolewa ajira kwa vijana wa Mirerani katika migodi ya mwekezaji.
Anasema lakini kampuni hiyo, haiajiri vijana wa Mirerani na hivyo sasa wapo mitaani tu kwani hata migodi ya wachimbaji wadogo mingi imesimama na ambayo inaendelea na kazi, inachukua vijana wachache sana.
Omar Awadhi alikuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mirerani miaka 10 iliyopita, anasema, maisha ya Mirerani sasa yamebadilika na hata uchangiaji shughuli za maendeleo umepungua sana. Anasema Mirerani licha ya utajiri wote, haina hata huduma ya maji safi, kwani ndoo moja inauzwa kati ya Sh400 na 500.
Awadhi anasema maji hayo yanatolewa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro kitu ambacho siyo sahihi kulingana na utajiri wa tanzanite ambayo inapatikana Mirerani pekee duniani.
“Tatizo hapa ni mwekezaji kama madini haya yangechimbwa na wachimbaji wadogo pekee hali isingekuwa hivi, kwani watu wengi wangepata madini japo kidogo kidogo lakini yangeendelea kuujenga Mji wa Mirerani na hata mikoa ya jirani,” anasema.
Robo tatu ya migodi ya wachimbaji wadogo imesimama
Mayala Raurenti ni Ofisa Madini, Mirerani. Anakiri uchimbaji wa madini hayo kuzorota kwa wachimbaji wadogo, lakini anasema chanzo ni mahitaji makubwa ya teknolojia.
Raurenti anasema madini katika maeneo ya kitalii B na D vinavyomilikiwa na wachimbaji wadogo tofauti na miaka ya nyuma sasa yapo mbali na hivyo kuhitaji teknolojia za kisasa.
Hivi sasa wachimbaji wadogo, wamepungua kutokana na upatikanaji madini kuwa mgumu na kuanza kutumia mashine badala ya watu katika kupandisha michanga juu ya mgodi na hata kuchimba.
Mihayo Franeis ni Ofisa wa Miamba (jiolojist) katika machimbo ya Tanzanite Mirerani. Anasema kati ya migodi zaidi ya 400 ya wachimbaji wadogo ni migodi 120 tu ndiyo inachimbwa kila siku.
Anasema hali hiyo, ,imesababisha kupungua sana kwa wachimbaji wadogo kwani pia migodi hiyo, ambayo awali ilikuwa inawafanyakazi zaidi ya 4,000 sasa hawafiki 500.
“Mgodi ambao ulikuwa na wachimbaji wadogo 100 sasa wapo 15 hii inatokana na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchimbaji,” anasema.
Anasema hata mamia ya vijana ambao walikuwa wamejiajiri kuchambua michanga na kupata dhahabu sasa hawapo na ndio sababu watu wamepungua sana Mirerani. Anasema kitalu B kina migodi 183 na kitalu D kina migodi 368 lakini ambayo inachimbwa kila siku si zaidi ya migodi 120 hivyo ndio sababu mji kama wa Mirerani uliokuwa unategemea madini hayo umebadilika.
Hata hivyo, anakiri licha ya migodi kuwa michache inayochimbwa bado upatikanaji madini siyo kama zamani kwa kuwa miamba ipo mbali zaidi kwa migodi mingi.
“Ni kweli migodi mingi ya wachimbaji wadogo haipati madini, tatizo ni kuwa maeneo mengi yamechimbwa tayari na sasa madini yapo chini zaidi hivyo gharama za uchimbaji ni kubwa,” anasema.
Akizungumzia malalamiko ya wachimbaji kuwa madini mengi yapo eneo la mwekezaji alisema siyo sahihi kwani madini yote yapo kwenye miamba katika eneo la Mirerani lakini kwa maeneo ya wachimbaji wadogo yapo chini zaidi.
Serikali sasa yalia kukosa kodi Mirerani.
Martha Umbulla ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro. Anakiri hali ngumu ya maisha Mirerani lakini anasema hata kodi kutoka katika madini hayo, wilaya hiyo hainufaiki kwa sasa.
“Wakazi wa Mirerani wanategemea madini, sasa hayapatikani hivyo uchangiaji maendeleo siyo mzuri lakini Serikali tungeweza kupata hata kodi kutoka kwa wachimbaji hasa mwekezaji lakini hatupati,” anasema.
Anafafanua kuwa kodi ya mapato ya madini hayo, wachimbaji wanalipa Arusha kutokana na mji wa Mirerani kutokuwa na ofisi za Mamlaka ya kodi (TRA).
Alisema Serikali inafanyia kazi matatizo ya Mirerani ili kuona wananchi wataishi vipi na kutokwama shughuli mbali mbali za kiuchumi. Huu ndiyo mji wa Mirerani ambao sasa upo hoi na wananchi wanalia kila kona baada ya kushindwa kunufaika na madini ya Tanzanite.

Halima Mdee aibuka kidedea Bawacha

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee amechaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Suzan Lyimo.
Mkutano Mkuu wa Bawacha wa uchaguzi ulifanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini hapa na ulianza juzi asubuhi na kuhitimishwa jana asubuhi.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Arcado Ntagazwa akitangaza matokeo hayo jana alisema, Halima Mdee amepata kura 165 dhidi ya wapinzani wake sita ambao ni, Lilian Wasira kura (11), Chiku Abwao (15), Sophia Mwakagenda (18), Rebeka Magwisha (14) na Janeth Rither(35).
Kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti bara, Ntagazwa alimtangaza Hamida Abdalla aliyepata kura 125 dhidi ya Mariam Msabaha aliyejikusanyia kura 66 katika uchaguzi ulioingia ngwe ya pili baada ya kwanza kukosekana mshindi kutokana na kutofikisha asilimia 50 ya makamu mwenyekiti katika kura zilizopigwa. Naye Hawa Mwaifunga aliibuka mshindi wa nafasi ya makamu mwenyekiti bara kwa kupata kura 136 dhidi ya kura 99 alizopata Victoria Benedict katika uchaguzi uliorudiwa mara ya pili baada ya awali kushindwa kumpata mshindi.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi jana asubuhi alianza kwa kuwashukuru wanawake wote waliompigia kura na hata wale ambao hawakumchagua kwani walitumia demokrasia yao.
“Wanawake tutaweza kusonga mbele kama tukipendana kwani uwezo, nguvu na nia tunazo, siri ya kuingia Ikulu mwaka 2015 ni kuwa na wanawake wengi ndani ya Bawacha lakini watakaokipigania chama,” alisema Mdee na kuongeza:
“Viongozi tuliochaguliwa tunatakiwa kushughulikia matatizo ya wanawake ili waweze kutuamini kwani taifa linatutegemea na tusiruhusu rushwa iwe kwetu.”
Kuhusu malengo ya Bawacha kwa siku za usoni Mdee alisema kwa kipindi cha miezi miwili watafanya operesheni kubwa nchi nzima ya kutoa elimu kwa wanawake waweze kujiunga na chama hicho ili kiweze kuwa na mizizi kuanzia ngazi za chini.
“Operesheni tutakayokwenda kuitangaza kuanza itakuwa kubwa, tutakwenda hadi ngazi za chini kabisa, tutawahamasisha wasichana wadogo ambao wamekuwa wakihofu kujiunga na vyama vya saisa hasa vya upinzani waweze kujiunga,” alisema Mdee.
Juzi viongozi wapya wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) waliochaguliwa ni mwenyekiti, Paschal Patrobas, Makamu mwenyekiti bara, Patrick Ole Sosopi, Makamu mwenyekiti Zanzibar, Zuedi Abdullah.
Katibu Mkuu ni, Julius Mwita, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Omary Othuman Nassor na Naibu Katibu Mkuu Bara ni Getruda Ndebalema na mtunza hazina amekuwa Evelin Meena.

Cheyo awavaa Ukawa bungeni



Dodoma. Mwenyekiti wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo amewavaa viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akieleza kuwa walichokubaliana katika kikao chao na Rais Jakaya Kikwete ni kwamba Bunge liahirishwe Oktoba 4 na si kama wanavyodai wakiwa nje.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma jana, Cheyo alisema hakuna makubaliano ya kutaka Bunge lisitishwe kabla ya kukamilisha kazi zake Oktoba 4, ikiwamo kutoa Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi.
“Mojawapo tulilokubaliana ni Bunge hili lipate Katiba itayopendekezwa kwa wananchi,” alisema Cheyo huku akipigiwa makofi na kelele kutoka kwa baadhi ya wajumbe.
“Pia tulikubaliana kwa hali halisi ya muda tulionao, haiwezekani mchakato mzima ukamalizika na maana ya kumalizika mchakato ni kura ya maoni ya wananchi na ndiyo wenye Katiba.”
“Tukasema kama inabidi tufike mpaka kule (kura ya maoni) inatubidi tuahirishe uchaguzi wa 2015 jambo ambalo sisi wote hatuliafiki na mheshimiwa Rais alisema msinitwishe mzigo huu,” alisisitiza Cheyo.
Cheyo alisema Rais katika mazungumzo hayo alitaka utaratibu wa kufanya uchaguzi kila Oktoba ya mwisho wa kipindi cha miaka mitano uendelee ili wananchi wenyewe watoe ridhaa kupitia uchaguzi wa viongozi.
“Bunge hili haliendeshwi kwa amri ya mtu ambaye yuko barabarani. Bunge hili linaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na sheria tuliyokuwa nayo kwa sasa ni GN 254 (tangazo la Serikali) ambayo inasema uhai wa Bunge ni mpaka Oktoba 4,”alisema Cheyo.
Cheyo alisema haiwezekani Rais akasimama mara baada ya makubaliano na kutangaza kuwa siku inayofuata Bunge lisitishe shughuli zake.
“Watu tumekubaliana na kuna video ambayo kila mmoja aliyekuwa akizungumza alirekodiwa. Kweli mnataka tumuombe sasa mheshimiwa Rais tutengenezewe kipindi maalumu kila mmoja aonekane anasema nini?” alihoji.
“Tuwe waungwana. Itoshe mimi kusema yale niliyotangaza hayo ndiyo makubaliano.

Hii nayo ni sanaa ya kimataifa

Utamaduni wa Mtanzania, katika sekta ya burudani, unaweza ukapotea kama waongeaji tusipotumia majukwaa yetu ya kuongelea na kuliongelea hili angalau kwa uchache.
Uchunguzi wa jarida hili umegundua hili na nachukua wasaa huu kama mshikadau wa burudani hapa nchini kuwaambia wandaaji, tuangalie upya aina za burudani tunazotoa na watu tunaowapelekea.
Kiukweli tunaanguka na kwa kuanguka sisi tutajikuta siku moja tukiangusha maadili ya kijana wa kitanzania pia na burudani ni ajira kwa vijana wetu sasa tukisababisha itumike ndivyo sivyo, kutakuwa na hatari ya kuliletea hasara taifa katika siku za usoni.
...Nina maana yangu kusema hivi.
Katika miezi sita ya nyuma nimeshuhudia matamasha mengi ambayo majina yake hayaendani na kinachofanyika kwenye tamasha hilo, hali inayosababisha watu makini wa tasnia ya burudani kuanza kushindwa kabisa kuwaelewa waandaaji, wamekuwa kama wadanganyifu hivi sifa ambayo si nzuri kwa mfanyabiashara aliyedhamiria kukaa kwenye tasnia kwa muda mrefu.
Tamasha linaitwa la kimataifa, lakini kinachopatikana kwenye tamasha hilo utakuta ni kama tamasha la Dar es Salaam hivi, sasa sijui ni kutokana na bajeti au ni kutokana na ufinyu wa fikra ama ni kutokana na uroho wa kipato au ni kuhisi kwamba wale unaowapelekea burudani hawana akili?
Unapomwambia mtu naleta kitu cha kimataifa, halafu zinaonekana sura za hapahapa unataka kusema kwamba sisi ni wa kimataifa?
...tangu lini?
Basi kuwe na angalau na uwakilishi wa nchi mbili tatu...
Hamna!
Tunamdanganya nani sasa?
Tunajidanganya wenyewe kwa taarifa maana mwisho wa siku Watanzania si wajinga tena, wanajua mambo mazuri na mabaya, ..unaona bwana? Mwisho wa siku wakishajua wewe si mkweli kwenye kazi zako watakukimbia na wakikukimbia utataka kumtafuta mchawi, kumbe umejiloga mwenyewe.
Kuna haja ya kuwa makini katika hili ndugu zangu wadau, kuna watu wana akili zao wamekaa tu wanaangalia haya mambo, wanachambua tu na mwishowe watatoa hoja zao na unaweza kuhisi unaonewa, kumbe ndiyo stahili yako.
Ukisema kitu ni cha kimataifa, kiwe cha kimataifa kweli, kikiwa kitu cha kiasili kiwe cha kiasili kweli na wasanii jamani wapo wengi, siyo kila siku wale wale tu tutoe nafasi kwa kizazi kilichopo mtaani kuonyesha uwezo wake tusiangalie tu walio karibu yetu.

Jaji Warioba: Namshangaa Sitta

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema anashangazwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kung’ang’ania kuendelea na Bunge hilo licha ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia lifikie kikomo Oktoba 4 mwaka huu.
Hivi karibuni, Rais Kikwete alikutana na viongozi wa vyama vya siasa vilivyo chini ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na kukubaliana kusitisha mchakato wa Katiba hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu wiki hii jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema ameshangazwa na uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao wakati uwezekano wa kukamilisha mchakato haupo.
“Hivi kuna haraka gani ya kuwa na rasimu katika Bunge hili? Mimi nilivyoelewa makubaliano ya Rais na TCD ni kama walikuwa wanasema kwa ustaarabu hebu twende polepole. Nimeambiwa kuwa Rais alitoa muda mpaka Oktoba 4, lakini uongozi wa Bunge ukapanga mpaka mwisho wa Oktoba,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Mimi nafikiri makubaliano kati ya Rais na viongozi wa vyama ni kukataa kuongeza muda. Hiyo kwangu ni lugha ya kistaarabu kwa Bunge kwamba hamwezi kumaliza kazi hii kwa kipindi hiki,” alisema Jaji Warioba.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Sitta kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa kuhusu Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume yake, badala ya kujihami.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate maoni ya watu ya kila aina. Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema vibaya. Nilisemwa mengi sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja mmoja,” alisema na kuongeza:
“Sitta asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.”
Aliongeza: “Nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii tena. Ni wakati fulani mtu anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema....”
Alisema hatua ya uongozi wa Bunge kung’ang’ania kuendelea na mchakato ni kupingana na Rais Kikwete.
“Lakini mimi inanishangaza ilikuwaje Rais anatoa nyongeza ya hadi Oktoba 4, uongozi wa Bunge unaongeza hadi mwisho wa mwezi? Rais anasema hivi na Bunge linasema hivi. Mimi naomba uongozi wa Bunge utafakari tena,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanywa na uongozi wa Bunge la Katiba hakina shinikizo la CCM , bali ni uamuzi ambao unatokana na matakwa yao
“Kama ni makubaliano ya viongozi wa vyama vya siasa na CCM walikuwapo, sasa kama chama kimeona hatuwezi kupata Katiba bora kwa nini tena uendelee?”
“Sheria ilisema Bunge lile litapewa siku 70, lisipomaliza litapewa nyingine 20, wakafanya tafsiri zao, kwani hizo siku 90 hazijaisha? Walipofikia wakati wakasema sasa tunakutana na Bunge la Bajeti tuahirishe, wakaahirisha. Kama mara ya kwanza liliwafanya wasitishe, nini kinawazuia kwa sasa?”
Alisema mbali ya tamko hilo, uongozi wa Bunge hilo umetangaza kuendelea na mchakato wakisema kuwa rasimu itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu.
“Nasikia wanaendelea, nasikia wanasema rasimu itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu. Hivi katika hali hii wanaweza?” alihoji Jaji Warioba huku akionyesha sura ya mshangao.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya pili ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema ahadi iliyotolewa na Sitta ya kupatikana kwa rasimu ndani ya Septemba haitekelezeki.
“Sina tatizo na kuahirisha Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuwa waliona haiwezekani kupata Katiba kabla ya uchaguzi, lakini sioni uwezekano wa kumaliza kazi zote kwa wakati huu,” alisema na kuongeza:
“Sioni kama wana muda wa kamati kuandika rasimu mpya ya kupigia kura, kwa sababu suala siyo kupiga kura tu, kuna mambo ambayo lazima kuwe na maridhiano na itachukua muda.”
Akitoa mfano wa suala la Muungano, Warioba alisema ni kati ya mambo yanayohitaji maridhiano badala ya kuishia kwenye kupiga kura tu.
“Kwa mfano suala la muungano halitakwisha hivihivi bila maridhiano. Kuna mengine, nimesikia wanajadili Mahakama ya Kadhi, limejitokeza sana. Litakapofika kwenye uamuzi, lazima kuwe na maridhiano. Wasipokuwa na maridhiano inawezekana wakaleta rasimu ambayo haina Mahakama ya Kadhi. Je, wale wanaoitaka wakikataa una uhakika wa kupata theluthi mbili? Wale wanaopinga wakikubali utapata theluthi mbili?” alihoji.
Kupiga kura
Akizungumzia kauli ya Sitta ya kuwasiliana na balozi za nje ili kuhakikisha wajumbe waliosafiri huko wapige kura hukohuko, Warioba alisema kupiga kura peke yake hakutoshi kutoa uhalali wa Katiba bali maridhiano ndiyo msingi.
Aliongeza: “Mimi sielewi uongozi wa Bunge unafanya nini! Kwa sababu ukipitisha kitu kwa siri, hata kabla ya kufika kwenye kura ya maoni kikakataliwa na wananchi. Ni vizuri kutulia na kushauriana, wasiwe na haraka.”
Amewashauri viongozi wa Bunge hilo kutafakari upya uamuzi wa kuendelea na vikao wakati Rais ameonyesha nia ya kuvisitisha.
Misimamo ya vyama imeharibu
Akieleza sababu za Bunge hilo kuyumba, Jaji Warioba alisema licha ya Tume yake kuwapa viongozi wa vyama vya siasa na wajumbe wengine nyaraka 10, lakini wameingiza misimamo ya vyama vyao:
“Mchakato ulipoanza kwa wale ambao tulikabidhiwa kazi hii, tuliamini tunaelekea kupata Katiba bora itakayotokana na maoni ya wananchi. Sisi kwenye Tume hilo ndilo lilikuwa lengo letu. Tulijipanga tulivyoweza mpaka tukatoa rasimu ambayo kwa kiwango kikubwa ilizingatia maoni ya wananchi,” alisema.
Jaji Warioba alisema mwanzo wa Bunge waliamini kuwa maoni ya wananchi yatazingatiwa, lakini baadaye walishangaa kuona maoni ya vyama ndiyo yanazingatiwa badala ya wananchi.
“Lazima nikiri kwamba mwanzo wa Bunge hilo haukuwa mzuri. Sisi tuliamini kwamba chochote kinachokuja kitaangalia tulichofanya kwa msingi wa kuona wananchi wamesema nini….
“Lakini walivyoanza ikabidilika kabisa ikawa ni kwa msimamo wa vyama. Tukatoka kwenye msingi wa maoni ya wananchi tukaingia kwenye maoni ya vyama.”
Aliendelea kusisitza kuwa misimamo ya vyama ndiyo imeua matumaini ya kupata Katiba Mpya licha ya Tume hiyo kutoa nyaraka 10 za randama zinazoonyesha maoni ya wananchi na sababu ya mapendekezo ya rasimu hiyo.
“Nimewasikiliza kwa kirefu wajumbe wa Bunge la Katiba, inaonekana wengi hawakusoma taarifa tulizowapelekea. Tuliwapelekea nyaraka 10. Tuliwapelekea Rasimu, Randama inayoelezea kila ibara, maoni ya wananchi kisha sababu za mapendekezo,” alisema na kuongeza:
“Baada ya hapo kuna vitabu vikubwa viwili vinavyoeleza maoni ya wananchi. Kuna kitabu kingine cha maoni ya mabaraza. Kuna kile cha takwimu na kitabu cha utafiti. Sasa pamoja na vitabu vyote hivyo, bado watu wanazungumza bila kuzingatia yaliyoandikwa.”
Alisisitiza kuwa wajumbe wengi hawakusoma vitabu hivyo kwa sababu walikwenda bungeni na misimamo ya vyama vyao.
“CCM wana misimamo yao, Chadema yao, CUF na NCCR-Mageuzi nao wana yao.”
Kufutwa kwa vipengele muhimu
Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa mambo muhimu katika rasimu hiyo ya Katiba, Warioba alisema hali hiyo inatishia kupatikana kwa Katiba Mpya kama ilivyokusudiwa.
Alisema baada ya kuondolewa kwa vipengele muhimu katika Rasimu ya Katiba ni wazi kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa tofauti na iliyopo sasa.
“Katiba Mpya siyo kuandika waraka mpya, ni kuona kuna tofauti gani kati ya katiba hiyo na ile ya zamani. Kuna maeneo fulani ambayo ndiyo yaliyofanyiwa mabadiliko. Lakini kutokana na mambo yanavyokwenda yale mabadiliko makubwa hayapo tena,” alisema.
Aliyataja maeneo makubwa yaliyobadilishwa katika rasimu hiyo ni suala la maadili akisema kuwa wananchi walisisitiza kuporomoka kwake na kupendekeza njia za kudhibiti.
“Wananchi walikuwa wanataka lazima tuwe na mwongozo kwenye Katiba utakaowezesha kujenga utamaduni na maadili. Kwa hiyo katika rasimu tukaona kwenye utangulizi unaobeba misingi mikuu ya utaifa. Tukaona lazima kuimarisha misingi mikuu,” alisema.
Alisema katiba ya sasa inasema misingi mikuu ni uhuru, haki, udugu na amani na kwamba wananchi walitaka yaimarishwe hayo.
Jaji Warioba alisema wananchi walisema huwezi kuzungumzia haki bila usawa, huwezi kuzungumzia amani bila umoja na katika umoja lazima kuwe na mshikamano.
“Lakini wakasema msingi wa kwanza ni utu, kwa hiyo Tume ikazingatia misingi yote ya utu na maadili ikafika misingi minane badala ya minne.”
Alisema eneo lingine lililofanyiwa mabadiliko ni tunu ya taifa, akieleza kuwa wananchi walitaka ziwekwe kwenye Katiba kutokana na maelezo kwamba ndizo zinazojenga utamaduni wa Taifa.
Maadili ya Viongozi
Kuhusu maadili kwa viongozi, alisema walipendekeza, madaraka ya viongozi yawe ni dhamana, hivyo yawekewe kanuni, lakini Bunge badala ya kuheshimu maoni ya wananchi yamefanyiwa mabadiliko

Alisema Tume yake iliangalia sheria ya maadili wakaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja.
Jaji Warioba alitoa mfano wa nchi ambazo hazikuwa na maadili ya viongozi madhubuti na kujikuta zipo katika matatizo makubwa kuwa ni Ufilipino.
Alisema katika nchi hiyo maadili ya viongozi yalikuwa yameshuka sana, rushwa imezidi, hivyo walipomwondoa madarakani rais wa nchi hiyo, Ferdnand Marcos, maadili ya viongozi wakayaweka kwenye katiba.
Alitaja nchi nyingine ambazo zimeweka maadili ya viongozi kwenye katiba ni Afrika Kusini, Namibia na Kenya.
Aliendelea kusema kuwa hata zawadi wanazopewa viongozi zinapaswa kuwa za Taifa ili kuepusha kuchanganya masilahi ya Taifa na masilahi yao binafsi hasa pale viongozi wanapopewa zawadi wakati wa kutia saini kwenye mikataba ya Serikali.
“Kwanza wananchi walisema zawadi anayopewa kiongozi inakuwa ni mali ya Taifa. Wakasema viongozi wanaingia mikataba na wanajifikiria wenyewe.
Pili, katika kuimarisha maadili kwa viongozi Tume ilipendekeza kiongozi asiwe na akaunti nje kinyume cha sheria.
Tatu, iwe ni wajibu wa kiongozi kutangaza mali zake, kiongozi lazima atofautishe kati ya masilahi yake na masilahi ya umma, na kiongozi aepuke kutumia mali ya umma kwa masiahi yake.
Hata hivyo, alisema mwelekeo wa Katiba Mpya umebadilika hasa baada ya mambo hayo kuondolewa na kuyafanya kuwa sheria za kawaida.
“Wenzetu yaliwashinda wakayaweka kwenye katiba, sisi tunayaondoa. Nimeshangaa hata waliposema uwazi na uwajibikaji siyo tunu. Lakini katika nchi yoyote lazima uzingatie uwazi na uwajibikaji ili kuepuka ufisadi na wizi,” alisema.
Kuhusu madaraka ya wananchi katika Katiba alifafanua haja ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao wakiwamo wabunge akisema kuwa mamlaka hayo yameporwa na kupewa vyama vya siasa.
“Wananchi walisema sisi ndiyo wenye madaraka ya katiba, sasa tunataka mbunge wetu asiwe waziri. Pili tunataka ubunge uwe na kikomo.
“Uchaguzi siku hizi siyo kitu ni kama mnada tu. Walisema kama mbunge ameshindwa tuwe na madaraka ya kumwondoa hata kama muda haujafika, kwa sasa hawawezi kuwaondoa kwa sababu ya rushwa,” alisema na kuongeza:
“Lakini wamesema haiwezekani kumwondoa mbunge na watu watafanya mbinu za kuwaondoa wabunge. Lakini vyama vya siasa vimepewa mamlaka ya kuwaondoa wabunge na vimefanya hivyo. Wananchi wanaomchagua wanasema italeta matatizo.”
Kuhusu wabunge kutokuwa mawaziri, alisema walifanya utafiti na kuona ugumu wa kutenganisha madaraka ya Serikali na madaraka ya Bunge kwa sababu Serikali iko ndani ya Bunge.
Alisema kwa mabadiliko waliyopendekeza wao rais aondolewe bungeni abaki kuwa mtendaji na amiri jeshi mkuu na mawaziri wake wasiwe wabunge.
Alisema hata hivyo mapendekezo hayo yamekataliwa kwa madai kuwa mfumo wa sasa waliouzoea ni wa kibunge ambao Waziri Mkuu anakuwa mbunge na anakaa bungeni.
“Kuna nchi zenye mfumo huo kama vile Uingereza, Canada, Australia, ni nchi za Jumuiya ya Madola, mkuu wa nchi siyo mtendaji mkuu, bali waziri mkuu ndiyo anakuwa mbunge. Lakini hapa unakuwa na rais katika Bunge ambaye haingii bungeni. Kunakuwa na mkanganyiko,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanyika ni Serikali inalibana Bunge ama Bunge linaingia katika mambo ya Serikali,” alisema.
Muungano
Kuhusu suala la muungano alisema Bunge la Katiba limekuwa likijadili udhaifu wa Serikali tatu badala ya kuangalia udhaifu wa Serikali mbili, huku wakipanga kupunguza mambo ya muungano.
“Sasa hivi nasikia wanataka kuondoa mambo mengi zaidi ya muungano. Sisi tuliyaondoa kwa kuwa na Serikali tatu. Lakini kwa sasa watayaondoa bila kuweka utaratibu,” alisema na kuongeza:
“Serikali ya muungano inashughulikia tu mambo ya Bara. Huoni Waziri wa muungano akivuka maji na kwenda kufanya kazi Zanzibar. Hiyo imeleta matatizo makubwa. Kwa kuwa Serikali ya Muungano inashughulikia zaidi mambo ya Bara,” alisema.
Alitoa mfano wa mikopo akisema kuwa Zanzibar haiwezi kukopa kwa kuwa haitambuliki kama nchi kimataifa bali ni lazima ije bara na ipate dhamana.
Huku akitoa mifano ya dira na mikakati ya maendeleo, Warioba aliendelea kufafanua kasoro za muungano.
“Chukua mfano wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ni ya Bara maana Zanzibar wao wana Dira ya Maendeleo ya 2020. Mikakati ya maendeleo kama Mkukuta ni wa Bara, Zanzibar kuna Mkuza. Kama ni hivyo, Wazanzibari wanakuja Bara kufanya nini? Kwa nini wanakuja kushiriki katika maamuzi ya bara? Hilo limekuwa ni tatizo la kisiasa na yamekuwapo malalamiko ya muda mrefu.”
Aliongeza suala la kuwapo kwa migongano ya Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar huku moja ikisema nchi ni moja na nyingine ikisema nchi mbili zilizoungana.
Jaji Warioba alisema kutokana na mabadiliko muhimu yaliyopendekezwa na Tume yao kuondolewa, huenda kukawa na Katiba yenye mabadiliko kidogo.
“Wamechukulia yale mambo ya uongozi tu, uwe na muundo mpya wa Tume ya uchaguzi, uchaguzi wa rais, Rais achaguliwe kwa asilimia 50 na zaidi, uchaguzi wa rais unaweza kuhojiwa mahakamani. Lakini yale ya wananchi yameachwa.
Haki za binadamu
Kuhusu haki za binadamu, Warioba alisema kuwa wananchi walitaka vikwazo vilivyokuwapo viondolewe, hivyo tume ilifanya marekebisho ikiwamo kuweka mgombea binafsi.
Baada ya uchaguzi Katiba itapatikana?
Kuhusu suala la kuahirisha mchakato hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Jaji Warioba alisema rais ajaye atalazimika kufuata sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kumalizia mchakato huo.
“Sheria ipo, sidhani kwamba akija atapingana nayo. Tumekusanya maoni, tumekwenda bungeni na tunangoja kura za maoni, kwa nini avunje sheria? Labda kwa kuwa sheria inasema wajumbe wa Bunge la Katiba ni pamoja na wabunge wa muungano, sasa kama hawakurudi sijui atafanyaje? Je, waendelee hao hao au wateuliwe wengine?” Alihoji.
Ardhi na Maliasili
Jaji Warioba pia ameshangazwa na Bunge hilo kuingiza masuala ya ardhi, maliasili na Serikali za Mitaa kwa siri akisema huko ni kuvuruga mchakato.
Alisema mambo hayo si ya Muungano na yanahitaji na yalipaswa kutolewa hadharani ili wananchi waone kwanza.
“Kuna mambo ambayo Bunge limeyafanya kwa siri. Wameingiza sura mpya kwenye rasimu, kuhusu ardhi na maliasili na Serikali za Mitaa,” alisema .
Alisema kuziingiza kwenye rasimu lazima muwe na uhakika kwamba yatatumika pande zote, na kwamba bara wana utaratibu wao wa Serikali za Mitaa na Zanzibar wana utaratibu wao wa ardhi na maliasili ambao ni tofauti kabisa na ule wa Bara.
Alisema kuweka kwenye Katiba ya Muungano mambo hayo ni kuvuruga. Huku akitoa angalizo kuhusu umiliki wa ardhi na rasilimali zake, Warioba alisema kuwa hilo ni suala linalopaswa kujadiliwa na kila upande wa muungano:
“Sisi tuliliona suala la ardhi na maliasili, lakini kwa kuwa siyo suala la muungano tukaliacha. Wananchi walisema Serikali haithamini ardhi yao, mtu anahamishwa kwa lengo zuri tu la kujenga shule au barabara, lakini fidia anayopewa hailingani na thamani ya ardhi yake. Wanahesabu miti tu, hatuwezi kumletea maisha mtu huyu,” alisema na kuongeza:
“Wanasema kama Serikali inapendelea wawekezaji wa nje na wa ndani. Hata hapa mjini matatizo yanatokea, watu wanahamishwa mtu mwenye uwezo akishatokea. Kwa mfano, mahali kuna madini wanaondolewa anapewa mwekezaji, mwananchi anaendelea kuwa masikini. Ilitakiwa kuwe na utaratibu ambao mwananchi mwenye ardhi awe anapewa asilimia tano, Serikali za Mitaa asilimia 10 na Serikali Kuu asilimia 25, wanataka wafaidi. Ndiyo siri ya mambo ya Mtwara.”
Jaji Warioba ambaye amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza rushwa ya mwaka 1996, alisema kuwa anafarijika kuona kuwa anaaminiwa na Serikali na matokeo ya kazi zake yanafanyiwa kazi ndani na nje ya nchi.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa katika kazi zake.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate mrejesho wa kila aina. Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema na nilisemwa mengi sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja mmoja.
“Alivyosema Sitta nakubaliana naye, kazi ya binadamu haikosi kasoro na sisi hatukuamini kwamba kazi yetu haikuwa na kasoro. Ilikuwa nazo, kulikuwa na mambo labda tulipitiwa. Ningefikiri, hayo anayosema angeyatumia na kwake, asifanye mambo kama hivi anavyofanya… Asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.
Lakini mimi nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii… ni kweli.
“Ni wakati fulani fulani mtu anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema. Bado nina matumaini, wananchi hawa wametoa mawazo ya msingi, tukiyazingatia tutapata Katiba bora, tusipoyazingatia tutapata Katiba itakayoanzisha mgogoro,” alisema Jaji Warioba.
.