Dar es Salaam. Kwa nini siasa imegeuka kimbilio la wengi, wakiwamo wasomi Tanzania?
Ni swali aliloulizwa Spika mstaafu, Pius Msekwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni.
Akijibu swali hilo, Msekwa alieleza kwa ufupi
sababu za wasomi kuacha taaluma zao na kuwekeza nguvu na akili zao
katika siasa akisema inalipa kwa haraka na kwa njia nyingi zikiwamo
mishahara minono, posho na marupurupu kuliko zilivyo taaluma nyingine.
Msekwa ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, akitokea kwenye Chama cha Tanu na baadaye
kurejea kwenye siasa, alisema malipo manono yamewafanya wasomi wengi,
wakiwamo maprofesa, madaktari na wengineo kuifanya kimbilio.
Alisema pia uhuru wa watu kuchagua kazi nyepesi za
kufanya katika maisha yao umefanya waione siasa kama kimbilio rahisi
kuliko kutoka jasho kwenye taaluma, zikiwamo za utafiti, tiba, upasuaji,
ualimu na nyinginezo. “Siasa imegeuka kimbilio kwa kuwa ina posho na
marupurupu mengi zaidi,” alisema Msekwa na kuongeza kuwa wanasiasa
wanajipitishia posho ambazo haziwezi kutolewa kwingineko.
“Mpe mtu choice (chaguo), acha aende kokote hata
katika siasa, lakini ni vyema taaluma pia ikaheshimika,” alisema na
kuongeza kuwa jambo hilo lilianzia kwenye awamu zilizopita ambako
wasomi, ama walioteuliwa au kuchaguliwa waliamua kushiriki siasa na
hivyo kuziacha taaluma zao. Msekwa alimtaja msomi mmoja, Profesa Mazengo
ambaye aligombea ubunge baadaye akautelekeza baada ya kushindwa
kutimiza dhamira yake.
“Kulikuwa na mtu anaitwa Profesa Mazengo, yeye
alikimbilia kwenye siasa akilenga kupata uwaziri. Ubunge alishinda
lakini alipokosa uwaziri akautelekeza ubunge wake, hata jimboni
hakwenda, hakuwakilisha wananchi na wapigakura wake, hivyo hakurudi
baada ya miaka mitano,” alisema.
Kwa siku za karibuni, siasa na hasa ubunge,
unaonekana kuwa na masilahi na fursa zaidi kuliko nafasi nyingine katika
jamii na ndiyo maana wasomi wamekimbilia huko kwa matarajio ya kupata
fursa za kupitisha mambo yao. Baadhi yao (wasomi), ubunge siyo tija,
wamejikita zaidi kwenye nafasi katika serikali, zikiwamo za mitaa ili
kufanikisha biashara zao au kuwa karibu wananchi wa ngazi ya chini.
Kwa mfano, orodha ya wabunge kwenye Bunge la sasa,
inaonyesha wasomi wengi wakiwamo maprofesa, madaktari wa falsafa,
madaktari wa tiba au wahandisi.
Msekwa alipoulizwa anadhani ni kwa nini Serikali
haiboreshi masilahi ya wasomi katika taaluma zao, alicheka kisha akasema
uwezo wa nchi ni mdogo, haiwezi kuboresha masilahi ya watumishi wote
lakini inaweza tu kwa wabunge.