Tanzania imekumbwa na kashfa nyingi kubwa tangu ipate uhuru wake.
Kashfa hizi mbali ya kulitikisa taifa zimeliachia
taifa maumivu makali ya upotevu wa fedha na kusababisha baadhi ya
mawaziri na viongozi wa juu wa Serikali kung’olewa.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere
aliyeiongoza nchi tangu mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali
Hassan Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais
Jakaya Kikwete (2005-hadi sasa), kashfa zilizoitikisa nchini ni pamoja
na Operesheni Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji
Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS) na Kashfa ya
Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya Epa, Kashfa ya
Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na hii ya sasa ya uchotaji
mabilioni katika Akaunti ya Escrow.
Kwa hakika, kashfa hizi ni nyingi mno, ambazo zinatakiwa kutupa funzo la kudhibiti mianya ya kutokea kashfa nyingine.
Hata hivyo, inavyoonekana hatujajifunza kitu mbali
ya kutokea kashfa hizo. Hii inadhihirishwa na jinsi kashfa ya escrow
ilivyoshughulikiwa na Bunge letu.
Kama kuna kitendo cha aibu ambacho Bunge letu
linakifanya mjini Dodoma ni kile kilichofanyika Ijumaa usiku cha baadhi
ya wabunge na kiti cha Spika kuonyesha kuwalinda watuhumiwa wa kashfa ya
Akaunti ya Tegeta Escrow.
Ilikuwa inashangaza kuona baadhi ya wabunge ambao
wananchi wamewapa dhamana ya kuwawakilisha katika chombo hicho kikuu cha
uamuzi, wakijadili kashfa hiyo kwa itikadi za vyama.
Pia, lilichefua zaidi watu wengi waliokuwa
wakishuhudia Bunge hilo kupitia redio na televisheni, baada ya baadhi ya
wabunge kupendekeza adhabu nyepesi kwa watuhumiwa.
Ilikuwa kama mchezo wa kuingiza kuona mbunge
akisema; “Mheshimiwa Spika mtuhumiwa huyu ni mtu mzuri hana ubaya
wowote, hivyo naona asichukuliwe hatua.”
Wengine walilazimika kupotosha ukweli ilimradi
kuwalinda watuhumiwa kwa madai kwamba fedha zilizochotwa kwenye Akaunti
ya Tegeta Escrow, siyo fedha za umma.
Wabunge wengine wakaenda mbali zaidi ya kueleza
kuwa tuhuma za kuwapo wizi wa fedha hizo umeibuliwa na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe na wapinzani wenzake una lengo baya na Serikali.
Hata, wengine wakafikia mahali pa kusema kuwa wabunge wa CCM
ambao watapitisha au kuunga mkono kuchukuliwa hatua kwa Waziri wa
Nishati na Madini na watuhumiwa wengine basi siyo wana CCM.
Pia, jambo lingine la kushangaza ni kuona Spika
Anne Makinda akimchagua kupendekeza adhabu anayostahili kuchukuliwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi baada ya
kubainika kuwa alishindwa kuzuia au alizembea kuishauri Serikali kuhusu
kuchotwa kwa fedha za escrow, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge
ambaye naye ni mmoja wa watuhumiwa wa sakata hilo.
Kwa ujumla mambo hayo yote yalivuruga mjadala mzima na kufikia mahali hata Spika Makinda kushindwa kufanya maamuzi yanayotakiwa.
Wabunge wa upinzani waliona wazi kuwa wabunge wa
CCM walikuwa wakijaribu kuwalinda watuhumiwa kitu ambacho walikiona
hakina tija kwa taifa.
Hali hiyo ndiyo iliyofanya baadhi ya wabunge wa
upinzani kusimama na kuimba, kupinga kiti cha Spika kujaribu kuwalinda
watuhumiwa.
Nini kimetufikisha hapo? Matukio ya ufisadi
yanaongezeka nchini kutokana na Serikali kushindwa kuweka bayana hatua
zinazopaswa kuchukuliwa watu wanapatikana na makosa hayo, ili iwe
fundisho kwa wengine.
Kila mara wizi wa fedha za umma unapotokea,
Serikali hupata kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya
watu wengi kuamini kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza azma
zao.
Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani,
kuna kulindana sana, lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi
pengine ufisadi usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii.
Nadhani kinachotakiwa kufanyika ni wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa, wanatakiwa kujitathmini upya.
Nasema wajitathimini upya kwa sababu haiwezekani kila mara nchi iingie katika kashfa ambazo tunaweza kuzizuia.
Kama hatua madhubuti zingeweza kuchukuliwa basi hakuna mtu ambaye angeweza kuingiza nchi katika aibu hii.
Kwa mfano kama waziri fulani angekuwa ameshafungwa
miaka kumi jela kwa kuiibia serikali, naamini hakuna kiongozi wa
serikali angekuwa na hamu ya kujiingiza katika ubadhirifu wa mali za
umma. Kutokana na tabia ya kulindana ambayo ipo hivi sasa kila kiongozi anajua
kuwa hata kama atapora mali ya umma sana sana akichukuliwa hatua
itakuwa ni kuondolewa madarakani na yeye kubakia akiponda mali aliyoiba.









