Friday, 31 October 2014

JK: Watendaji wakuu wananikwamisha

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amewatuhumu baadhi ya watendaji wa serikali yake kuwa ni kikwazo katika kufanikisha masuala mbalimbali ya maendeleo kutokana na urasimu usiokuwa wa lazima katika kutoa huduma kwa wananchi.
Akifungua kongamano la miaka 10 ya Tume ya Utumishi wa Umma Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alikemea na kulaumu tabia ya baadhi ya watendaji hao wa Serikali ambao wamekuwa wakikwamisha kwa makusudi kasi ya viongozi wa kisiasa ya kuleta maendeleo.
“Katika utendaji wa baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali limekuwa ni tatizo na wamekuwa wakikwamisha sana kasi ya utekelezaji wa haraka wa malengo ya kisiasa,” alisema.
“Mara nyingine, viongozi wa kisiasa wamekuwa mbele kimtazamo kuliko watumishi wa umma, hili limekuwa tatizo sana katika utekelezaji wa malengo kwa haraka,” alisema Kikwete.
Alisema kumekuwa na malalamiko kwa makatibu wakuu wa wizara kutoka kwa wawekezaji ambao huwachelewesha kwa makusudi kwa visingizio vya kufuata utaratibu.
Alisema katika kufuatilia, amekuwa akilazimika kuingilia utendaji wa baadhi ya wizara ili kuhakikisha mambo yanakwenda na mara nyingine urasimu huo umekuwa ukifanywa kwa makusudi ili kuwachosha wawekezaji na ‘kuwatoa upepo’ kwa manufaa binafsi.
“Haya ni malalamiko makubwa sana na yanatoa picha mbaya kwa nchi yetu…watendaji wa namna hii ni lazima wabadilike, ninahitaji kuona mabadiliko makubwa kwa kupitia Tume ya Utumishi ambayo inatakiwa kukaa na hawa watumishi na kuwapa mafunzo ya kiutendaji yanayoendana na mahitaji ya sasa,” alisema.
Abeza zawadi ya uprofesa
Akizungumzia utaratibu wa upandishwaji vyeo, Rais Kikwete alisema ni muhimu weledi ukazingatiwa na utaratibu uliowekwa ukaheshimiwa, kwamba lazima wafanyakazi wapandishwe vyeo na madaraja ndani ya kipindi kilichowekwa, ambacho ni miaka mitatu.
Alisema kumekuwa na malalamiko kwa wafanyakazi wengi wa Serikali kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na hata wanapopandishwa vyeo mabadiliko ya mishahara kuendana na vyeo na madaraja mapya hayafanyiki kwa wakati.
Alieleza kwamba utaratibu unaotumika katika vyuo vikuu wa namna ya kuwapata wahadhiri wasaidizi, wahadhiri, maprofesa ni wa wazi na ni mfano wa kuigwa kutokana na namna unavyofanyika, kwa kutoa mafunzo kisha kuyathibitisha na kumpandisha mhusika daraja.
“Vyuo vikuu wana ngazi wanazotakiwa kuzipitia na mafunzo maalumu hadi mtu anakuwa profesa. Siyo honorary professor (uprofesa wa heshima) niliopewa mimi nilipokwenda China…walinishtukiza. Nilifika pale wakanipiga na uprofesa, nikasema haya sasa makubwa! (kicheko),” alisema.
Alisema matatizo ya upandishwaji vyeo yasipotatuliwa kwa wakati ni tatizo kubwa kwa Serikali hasa unapokutana na vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu kama Chama cha Walimu na wanapofikia hatua ya kusema wanagoma, unalazimika kuwaangukia.
Alisema suala la mtumishi kupandishwa cheo ni haki yake ya msingi kazini hivyo hatarajii kusikia matatizo ya malalamiko ya watumishi kutopanda vyeo kwa wakati.

No comments: