Friday, 31 October 2014

Ukawa na dhana ya nguvu ya mnyonge au ‘zamu yetu kula’

Dar es Salaam. Kwa jumla, kuungana ni jambo jema kwani muungano huongeza nguvu. Muungano ni silaha ya mnyonge dhidi ya mwenye nguvu.
Ni kwa sababu hii, tumekuwa tukipigania umoja wa Afrika ili kujenga nguvu ya pamoja dhidi ya mabeberu wa mataifa ya Magharibi tukiamini kwamba bila nguvu moja mataifa ya Afrika hayataweza kuukabili ubeberu wa mataifa haya.
Tunao msemo maarufu usemao nguvu ya mnyonge ni umoja na hivi ndivyo waasisi wa mataifa ya Afrika walivyofanya katika kumfukuza mkoloni.
Bila kujali tofauti zao za kikabila na vinginevyo, wananchi wa Afrika waliunganisha nguvu na hatimaye pamoja na silaha zao duni, wakafanikiwa kumfukuza mkoloni katika ardhi ya Afrika.
Katika uwanja wa siasa, vyama vya siasa huungana kwa sababu mbalimbali lakini sababu tatu ni za msingi zaidi. Mosi, huungana pale ambako hakuna chama kinaibuka na ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi ulio na ushindani mkali.
Katika mazingira haya, inakuwa hakuna chama kinachoweza kuunda serikali imara peke yake bila kushirikisha kingine kwa sababu hakitaweza kupitisha sera au sheria yoyote bungeni.
Hivi ndivyo vyama vya Conservatives na Liberal Democrats vilivyoungana huko Uingereza baada ya vyama vikuu nchini humo vya Labour na Conservatives kushindwa kupata ushindi ambao ungekiwezesha chama kimojawapo kuunda serikali na kupitisha sera bungeni bila msukosuko mkubwa.
Hivi ni vyama ambavyo vina itikadi na msimamo tofauti kabisa kifalsafa na ilibidi viongozi wake wakae saa nyingi kukubaliana programu ya kutekeleza kabla hawajakubaliana kugawana nafasi za uongozi.
Kiongozi wa Liberal Democrats, Nick Cleggy alimshinikiza David Cameroon akubaliane na masharti ya kulegeza misimamo mikali ya chama chake kuhusu sera ya uhamiaji na hifadhi ya jamii kabla hajakubali kuingia naye ubia kuunda serikali.
Cameron amekiri mara kadhaa kwamba alilazimika kulegeza msimamo kuhusu sera mama za Conservatives ili kufanikisha kuwashawishi Liberal Democrats kuunda nao serikali vinginevyo Nick Cleggy angeunda serikali na Gordon Brown wa chama cha Labour.
Ni katika mazingira ya chama kimoja kushindwa kupata ushindi wa wazi ambayo yalivilazimisha vyama hasimu vya CUF na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar.
Pamoja na kwamba SUK iliundwa kama njia sahihi ya kuepusha shari na vita visiwani, msingi wa serikali hiyo ni ukweli kwamba hakuna chama chochote kati ya hivi viwili chenye uwezo wa kuunda serikali imara kwa sababu ushindi wa chama chochote huwa ni mwembamba. Hata hivyo, hatujui ni kwa kiwango gani vyama vya CUF na CCM huko Zanzibar vilikubaliana kutekeleza programu ya pamoja inayotokana na sera za vyama hivyo viwili.
Sababu ya pili ya vyama kuungana ni kuunganisha nguvu katika jitihada za kumwondoa adui anayefanana.
Kwa mfano, huko Zanzibar kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964, vyama kadhaa viliungana katika jitihada za kuuondoa utawala wa Sultani uliokuwa unaendeshwa kibaguzi. Kwa hiyo, adui hapa alikuwa Sultani na ubaguzi wake wa rangi.
Sababu ya tatu ni pale vyama vinapounganisha nguvu ili kushinda uchaguzi kwa kutambua kwamba vikiingia kwenye uchaguzi kimoja, kimoja havitaweza kushinda kutokana na nguvu kubwa aliyonayo mshindani wao.
Hata hivyo, kushinda uchaguzi hakuwezi kutokana na kuunganisha nguvu ya kiuongozi pekee. Ni lazima kuunganisha pia nguvu ya kiitikadi, kifalsafa na kisera ili kuweza kujipambanua kwa wananchi.
Muungano wa kisera ni muhimu ili kuweza kutabirika tabia za wagombea watakapokuwa madarakani. Aidha, ni programu ya kisera inayoweza kuongoza kuchagua mgombea anayefaa zaidi kushika usukani wa utekelezaji wake baadaye.
Muungano wa vyama vinavyounda Ukawa umepokewa kwa shangwe kubwa. Furaha hii inatokana na msingi nilioueleza hapo awali kwamba wanyonge wakiungana hupata nguvu ya ajabu hata ya kuweza kuangusha milima.
Kwa hiyo, watu ambao wamekuwa wakisubiri utawala wa CCM kuanguka wanaamini kwamba kwa muungano huu angalau vyama vya upinzani vitafuta unyonge.
Nami naungana na Watanzania wengine kuwapongeza viongozi wa vyama ya Chadema, CUF, NCCR na NLD kwa ujasiri na uthubutu waliouchukua katika kujaribu kushirikiana katika chaguzi mbalimbali zijazo.
Lakini tunapowapongeza Ukawa, ni vizuri kutambua kwamba kuunganisha nguvu kama walivyofanya ni hatua moja tu inayopaswa kuanzisha hatua nyingi huko mbele. Hatua muhimu inayofuata sasa ni kujipambanua kwa wananchi kiitikadi, kifalsafa na kisera.
Kwa bahati viongozi wa sasa wa vyama vilivyoungana siyo watu wanaoamini katika mambo ya itikadi na falsafa.
Hawa ni viongozi ambao huitwa ‘wayakinifu’ (pragamatists). Myakinifu ni kiongozi anayeamini katika kinachowezekana leo na haongozwi na falsafa bayana ya kisiasa.
Kwa hiyo kiongozi yakinifu atambeba yeyote anayeona anafaa na huwezi kumuweka katika mrengo wowote kiitikadi. Kimsingi, hii ndiyo aina ya viongozi tulionao sasa tangu Mwalimu Julius Nyerere alipoondoka.
Ndiyo maana tumekuwa Taifa ambalo si la kijamaa, wala kiliberali wala kibepari. Tupotupo tu maadamu siku zinakwenda.
Pamoja na uyakinifu wao, bado naamini kwamba Ukawa watahitaji programu ya pamoja ya kisera. Hii ni hatua muhimu ili kutoa nafasi kwa wananchi kupima aina ya serikali watakayounda kama watashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Bila msimamo yakinifu wa kisera, ni rahisi kutofautiana kwa sababu ya kukosa msingi wa kugawana madaraka. Bila sera yakinifu, utakapofika wakati wa kugawana nafasi za kugombea na hatimaye katika kuunda Serikali watalazimika kuzingatia sifa za kuchagulika na umaarufu badala ya sifa za kiuwezo.
Nakumbuka mwaka 2005 palipokuwa na jitihada za kuunda ushirikiano kama huu wa sasa, nilipewa jukumu la kufanya utafiti kujua nani alikuwa anakubalika zaidi katika Jimbo la Ubungo kati ya mgombea wa Chadema (John Mnyika) na mgombea wa CUF (marehemu mama Minja).
Niliandaa hojaji na nikaligawa katika kata zote za Jimbo la Ubungo kwa kutumia sampuli iliyopatikana kwa njia ya bahati nasibu. Matokeo yalionyesha kwamba Mnyika alikuwa anakubalika kwa mbali dhidi ya wagombea wengine wa upinzani.
Hata hivyo, katika kikao cha kujadili matokeo hayo, wawakilishi wa CUF waliyakataa na kunituhumu kwamba nilikuwa napendelea chama changu na huo ndiyo ukawa mwanzo wa ushirikiano kusuasua na hatimaye kusambaratika kabisa kabla ya kampeni kuanza.
Yote hii ni kwa sababu tuliwekeza zaidi kwenye kugawana wagombea lakini hatukuwekeza kabisa katika ushirikiano wa kisera.
Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba, muungano wowote endelevu wa vyama vya siasa Tanzania, lazima uwe wa kuunganisha nguvu za wanyonge dhidi ya mabavu ya chama dola cha CCM.
Muungano wa namna hii lazima uwaunganishe kisera Watanzania na ndiyo unaopaswa kuwa msingi wa kugawana vyeo.

No comments: