Friday, 27 March 2015

SHERIA: Sheria gharama za uchaguzi kung’ata zaidi

Dar es Salaam. Serikali inakusanya nguvu kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, inang’ata wagombea wote watakaojihusisha na rushwa katika harakati zao za kusaka uongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watendaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamesema, utekelezaji wa sheria hiyo ulikuwa na changamoto nyingi katika uchaguzi uliopita mwaka 2010.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ofisi yake ilikumbana na  changamoto nyingi zilizofanya ishindwe kuisimamia sheria hiyo ipasavyo.
“Mwaka 2010 changamoto zilikuwa nyingi lakini tumejifunza. Uchaguzi wa mwaka huu tumeshajipanga, tunajua jinsi gani ya kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, tunajua tunahitaji ushirikiano wa karibu wa wadau ili kuweza kufanikisha jambo hilo,” alisema Nyahoza.
Nyahoza alitaja wadau ambao ofisi hiyo inatarajia kushirikiana nao katika kuisimamia sheria hiyo kuwa ni pamoja na vyama vyote vya siasa, asasi za kijamii, waandishi wa habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ushirikiano huu unaanza kuimarishwa kabla ya uchaguzi. tumebaini kwamba wadau hawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya namna wanavyoweza kushiriki kufanikisha utekelezaji wa sheria hii, pia kutakuwa na simu maalumu za kuripoti matukio yatakayokuwa kinyume,” alisema. 
Kauli ya Takukuru 
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alikiri kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha nguvu hizo, licha ya kukabiliwa na changamoto ya rasilimaliwatu.
“Ni kweli hata sisi tumeona kuna umuhimu wa kushirikiana katika kufanikisha jambo hili, ingawa kuna changamoto ya rasilimali watu, tunaamini kazi zitafanyika kwa namna ambayo itadhihirisha dhana ya kuwapo kwa Takukuru,” alisema Dk Hoseah.
Dk Hoseah pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuepuka kuuza haki zao za kuchagua viongozi bora kwa kudanganywa na zawadi za kanga, fulana, kofia na fedha. 
Sheria ikoje?
Ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari 2010. Sheria hiyo  imeweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato, matumizi  na gharama za kampeni na uchaguzi wa vyama vya  siasa na wagombea.
Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Machi 17, 2010 ili iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kwa lengo la   kukuza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.
Madhumuni ya kuwekwa Sheria hii ya Gharama za Uchaguzi ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hii imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo ni jina, tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hii katika Tanzania Bara na Zanzibar  na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.
Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa  na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.
Sehemu ya  tatu inahusu masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi, uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama  ambazo vyama vya siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti  kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama kwa vyama na taasisi za kiserikali  wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu masharti yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu  gharama kwa vitendo vinavyozuiwa  au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sehemu ya sita ya sheria hii inapendekeza makosa ya  ujumla  pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya Sheria hii.
Sehemu ya saba inaweka masharti  kuhusu haki ya mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari, wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia  haki  hiyo.
Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa kutumia  vyombo vya ulinzi  na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya Siasa, wagombea wao na  wapiga kampeni wanafikia wapigakura bila ubaguzi wala  kupewa vitisho.
Sehemu ya nane ya sheria inafanya marekebisho katika Sheria ya vyama  vya siasa ili kuoanisha masharti  ya sheria hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza  kifungu cha 13A katika Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii wakati wa kampeni za uchaguzi.

No comments: