Dar es Salaam. Tanzania imeomba msaada kwa
taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery – ICAR (Kituo
cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano
zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha
nchini humo.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la
mabilioni hayo ya Uswisi, Serikali iliunda kikosi kazi chini ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kulifanyia kazi.
Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na
kubaini kuanza kwa uchunguzi huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba
zinatokana na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi
hivi karibuni, Mtafiti wa Sheria wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema:
“Tuna makubaliano na Serikali ya Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), tunachunguza kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji
wa fedha, hivyo tuko katika ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano
ya moja kwa moja kwa sababu bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa
katika utoaji wa taarifa.”
Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.
“Ni kweli tumeombwa na Serikali ya Tanzania
kusaidia kuchunguza baadhi ya kesi… zilikuwa zimeshachunguzwa lakini
kutokana na uwezo wao mdogo tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema
tunazo kesi tano hivi… ni kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu
masuala ya fedha. Hatuwezi kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa
na mkataba wetu na taasisi tunazofanya nazo kazi.”
Licha ya kutotaja majina, Zinkernagel alisema
wanaochunguzwa katika kesi hizo wanahusishwa na kampuni hewa
zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota fedha kisha kwenda kuzificha nje ya
nchi.
“Kuna watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa
wakipokea rushwa au wamekuwa wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni
kivuli na ushirika mwingine wa kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda
kwenye kampuni fulani kwa lengo la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na
wafanyabiashara kuhamisha fedha haramu na mwisho hujisafisha,” alisema.
Jaji Werema
Jaji Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya
uchunguzi huo lakini akakataa katakata kutaja watu wala kampuni
zinazofanyiwa uchunguzi.
“Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa
kesi kwa sababu kwanza tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pili,
tunaweza kuwataja lakini baadaye ikabainika kuwa si kweli, bali ni
tuhuma tu na wakaja kutushtaki na tatu, tutakapowataja watu hao
tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi wetu.
“Katika kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu
kwa utaratibu ili tusiharibu upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani
tumekaa kimya hatufuatilii lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika
mtaona na mtasikia.”
Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema watu au taasisi
zilizoweka fedha nchini humo hawawezi kutajwa kwani ulinzi wa faragha za
watu ni suala la kimataifa... “Sizungumzii tu akaunti za Tanzania,
suala la kulinda faragha za watu ni la kimataifa. Ukiwa raia wa
Uingereza, Ufaransa au Tanzania, huwezi kupata taarifa za maisha ya mtu
binafsi. Kwa sababu wewe kama ni raia mwema, una haki ya kuwa na faragha
yako.”
Taarifa za 2011 kutoka Uswisi zilionyesha kuwa
kuna kiasi cha Sh327.9 bilioni zilizofichwa kwenye benki za nchi hiyo,
lakini Ripoti mpya ya mwaka 2012 ya Benki za Uswisi inaonyesha kuwa
fedha hizo zimepungua hadi Sh291.96 bilioni.
Akizungumzia kupungua kwa fedha hizo, Balozi Chave
alisema: “Inawezekana ni kutokana na kelele za vyombo vya habari hasa
Mwananchi, pengine wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye benki za
nchi nyingine.”
Taarifa ya Global Financial Integrity ya 2013
inaonyesha kuwa utoroshaji haramu wa fedha kutoka Tanzania kati ya 2008
na 2011 umefikia jumla ya Dola za Marekani 2.935 bilioni (Sh4.2
trilioni) na inakadiriwa kuwa Watanzania wanamiliki utajiri wa Dola za
Marekani 750 milioni (Sh1.23 trilioni) katika Visiwa vya Jersey.
Muda wa uchunguzi
Wakati Tanzania ikiwa imepeleka kesi hizo mbele ya
taasisi hizo ndani ya mwaka mmoja, Zinkernagel alisema zinaweza
kuchukua miaka mitano hadi 10 ili kufanikisha kurejesha fedha
zilizofichwa.
“Tangu uchunguzi unaanza hadi fedha zirudishwe kwa
nchi husika inaweza kuchukua hadi miaka 10. Sisi hatuna muda mrefu
tangu tuanzishe taasisi hii, lakini tunafahamu baadhi ya kesi zimechukua
hadi miaka 20. Hizi ni kesi za kimataifa, hivyo unaanza kufuatilia
akaunti na mifumo ya taasisi nyingine… hiyo tu inaweza kuchukua hata
miezi sita. Bado mtuhumiwa anaweza kukata rufaa. Ni kweli unataka mambo
yaende haraka lakini pia huwezi kukiuka utawala wa sheria.”
Mbali na Tanzania, Zinkernagel alisema taasisi
yake pia inashughulikia kesi za nchi nyingine 12 duniani na kwamba
wamefanikiwa kukamata baadhi ya fedha na mali zilizoibwa katika baadhi
ya nchi.
Alisema kazi hizo hufanywa bila malipo yoyote kwa kuwa taasisi hiyo hupata fedha kutoka serikali za Uswisi na Uingereza.
Changamoto
Akieleza changamoto zilizopo katika kupambana na
uhalifu wa fedha haramu, Zinkernagel alisema ni ushirikiano hafifu kati
ya nchi zinazoibiwa fedha na zile zinazoficha.
“Mamlaka za Uswisi zikigundua kuwapo kwa mali
labda kama za Tanzania, wanaweza kuanzisha uchunguzi wao lakini ili
kuhusisha uchunguzi na nchi husika watahitaji msaada kutoka nchi husika.
Mamlaka ya Uswisi haiwezi kuendeleza kesi bila ushirikiano na mamlaka
za Tanzania, kwa mfano. Hapo ndipo tunapokumbana na siasa nyingi pale
tunaposhughulikia kesi kama hizo. Inakuwa vigumu kupata ushirikiano wa
wanasiasa tunapouhitaji, hiyo ni changamoto kubwa.
“Changamoto nyingine, ni uwezo mdogo wa vyombo vya usalama vya
Tanzania wa kushughulikia kesi za rushwa, matumizi mabaya ya fedha na
madaraka. Ni kazi ngumu kufuatilia kesi kama hizo kwani unahitaji
kuhusisha sekta mbalimbali. Changamoto hiyo ya utaalamu pia inaigusa
Tanzania ndiyo maana haina uwezo wa kuchunguza kesi kama hizo.”
Kwa upande wa nchi zinazoficha fedha, Zinkernagel
alisema kuna tatizo la kutoweka vikwazo kwa taasisi za fedha
zinazotuhumiwa kuhifadhi fedha haramu.
Tanzania imetajwa kuwa nchi ya 13 kati 20 duniani kwa utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika mitandao
mbalimbali ikiwamo Global Financial Integrity, Carl Smith, One Dola
Bilioni na Taarifa ya Swiss,” zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza
mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na biashara haramu ya uhamishaji
wa fedha na misamaha ya kodi na mikataba mibovu.

No comments:
Post a Comment