Thursday, 19 June 2014

Tuliteleza mikataba ya madini, sasa tusonge mbele-2

Madini na maisha ya wananchi
Haiingii akilini kuona kampuni za kigeni zinazochimba madini Tanzania zinawekeza nchi za nje, huku wananchi wa Tanzania wakiendelea kuwa maskini.
Nafahamu kuwa mimi siyo mwandishi wa kwanza kuandika suala la madini Tanzania, lakini haimaanishi kwamba tufunge mdomo au tutupe kalamu zetu.
Madini ni miongoni mwa rasilimali zenye thamani kubwa, hivyo kama zitawekewa sheria na usimamizi mzuri, taifa linaweza kunufaika sana kimaendeleo.
Tanzania tunazalisha madini ya aina nyingi kama dhahabu, almasi, rubi, tanzanite, ulanga nk.
Katika uzalishaji huo, kuna baadhi ya migodi inamilikiwa na wachimbaji wadogo wazalendo na mingine inamilikiwa na wachimbaji wakubwa hususani kampuni za kigeni na mingine inamilikiwa kwa ubia baina ya wageni na wazawa au mengine ya wazawa.
Ulinzi wa madini yetu
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 27 ibara ndogo ya 1 inaeleza kuwa kila mwanachi ana jukumu la kulinda mali ya nchi ikiwa ni pamoja na madini. Hii ndiyo kusema kwamba kwa kuacha madini kuchimbwa kiholela, wananchi na Serikali yenyewe haijitendei haki. Madini ni mali ya yote inapaswa kuwanufaisha wote.
Madini katika pato la taifa
Hivi karibuni kuna michango mbalimbali inaendelea bungeni kuijadili bajeti, hatujaelezwa kwa kina mapato yanayotokana na madini, miaka yote tumeendelea kuwa tegemezi.
Wasomi wanaongezeka, ajira haziongezeki, deni la taifa nalo linazidi kupanda. Tuna rasilimali nyingi zikiwamo madini, lakini ni kama yametushinda kujinufaisha, sasa tunakimbilia sekta ya gesi. Rais wa Botswana, Festus Mogae tarehe 7, Juni, 2006 alisema: “Kwa watu wetu, kila almasi inayouzwa inawakilisha chakula mezani, mazingira mazuri ya kuishi, afya bora, maji safi, barabara kuunganisha jamii zetu na vingi zaidi.”
Kasoro za sheria za madini Tanzania
Sheria inayosimamia madini Tanzania ni Sheria ya Madini ya mwaka 2010 Na.14 pamoja na kanuni zake mbalimbali zinazohusu mazingira zilitolewa na gazeti la Serikali Na. 403 la tarehe 5/11/2010 inayohusu kanuni za mazingira.
Sheria hizo zinahitaji kupitiwa upya kwa sababu ya kasoro zake kadhaa zinazoonekana.
Moja ya kasoro hizo ni kwamba katika maombi ya kupewa leseni za uchimbaji madini kama watu wana sifa sawa za kupewa, wanaangalia nani wa kwanza kuomba, kama wameomba siku moja wataangalia mazingira husika.
Tunahitaji kufanya mabadiliko na sheria hiyo kutamka kuwa utaifa ndiyo kitu cha msingi cha kuangalia.
Tumeona wiki iliyopita mjini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alikuwa akizindua kampeni ya Uzalendo, mambo haya ya uzalendo yasambae katika sekta zote mpaka za madini.
Mbili, waziri ana mamlaka makubwa sana kwenye sheria hii ya madini, anasaini mikataba kwa niaba ya Watanzania; kifungu cha 15 cha sheria ya madini ya mwaka 2010 kinamruhusu waziri husika kuamua kugawa maeneo ya uchimbaji kwa zabuni au kawaida.
Madaraka ni makubwa sana ukizingatia na unyeti wa sekta. Kumpa mtu madaraka makubwa kiasi hicho ni kuweka mwanya wa rushwa. Tatu, kamishna wa madini kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha sheria no. 14 ya mwaka 2010 ya madini huteuliwa na Rais tu. Hii ni nafasi nyeti inatakiwa kuwa ya wazi na ya kiushindani, Watanzania waombe nafasi hiyo, mwenye uwezo mkubwa ndiyo apewe nafasi.
Kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kinakataza mtu yeyote zaidi ya mmiliki halali wa leseni ya madini, kumiliki, kusafirisha au kuuza madini, jambo kama hili pia linapaswa kuangaliwa, kwa sababu kwa namna moja ama nyingine kinazuia watu wengine kujiingiza kwenye biashara hii.
Kifungu cha 18 (3) kinakataza mtu yeyote kusafirisha nje ya nchi madini au sampuli za madini bila kuwa na leseni ya madini, kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi na uthibitisho wa malipo ya mrabaha. Sheria kama hii inapaswa kuangaliwa, kwani angeweza kuruhusiwa tu yeyote ili mradi awe anafuata taratibu nyingine za biashara.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 18 (4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, mtu yeyote atakayekiuka sheria kuhusiana na umiliki na biashara ya madini akipatikana na hatia atatozwa faini ya kiasi kisichozidi Sh10 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu, au adhabu zote mbili.
Kwa kampuni, adhabu iliyopo kwa mujibu wa sheria kwa kosa hilo ni kulipa faini isiyozidi Sh50 milioni. Wataalamu wa madini wanabainisha kuwa faini iliyowekwa na sheria na adhabu yake ni ndogo sana ukilinganisha na thamani ya madini.
Kifungu cha 6 (4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kinampa mamlaka kamishna wa madini kutaifisha madini yaliyopatikana kinyume cha sheria, pamoja na vifaa vilivyotumika kuzalisha madini hayo. Sheria ilipaswa kueleza zaidi juu ya uhifadhi na uuzaji wa madini hayo.
Tano, sheria ya madini kifungu cha 25 (1) inaeleza kuwa ripoti inayotolewa na wamiliki wa haki miliki za migodi ni siri, kwa nini ripoti iwe siri? Kwa nini isiwekwe wazi mfano kwenye tovuti ya wizara na kufanya kila mwananchi ajionee kinachoendelea kwenye rasilimali ya nchi yao. Mikataba ni siri, ripoti kutoka kwa wamiliki nayo ni siri. Waswahili wanasema “halali haina siri, haramu ndiyo ina siri.”
Hizi ni baadhi ya kasoro kwenye sheria ya madini. Haya mambo yawekwe wazi kila mmoja ajue kinachoendelea.
Maeneo ya migodi yatangazwe wazi, kila mtu agombanie kwa ushindani ulio sawa. Maeneo ya madini yaianishwe na yatangazwe, watu wagombanie kwa usawa, kipaumbele wapewe wazawa wenye sifa na uwezo, tusiwabeze Watanzania juu ya hili.
Kwa mfano kwa sasa tunataka kujikita kwenye kuchimba urani, lakini imefahamika kuwa madini hayo ya urani yana hatari kubwa kwa binadamu kutokana na kuwa na mionzi yenye madhara. Lazima tujifunze kutoka kwenye uchimbaji wa madini mengine kama dhahabu, almasi, Tanzanite na chokaa, ambao ulisababisha wananchi kupata magonjwa ya ngozi, saratani, uchafuzi wa maji na vifo vya mifugo na wanyama wengine wa porini na majini.
Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na 403 la tarehe 5/11/2010 kanuni ya 7 na 8 zinakataza uchafuzi wa mazingira, lakini kanuni ya tisa inasema ukifanya kosa la uchafuzi faini haitazidi milioni moja au kifungo kisichozidi miezi sita, najiuliza hiyo adhabu kweli inaonyesha nia ya dhati ya kulinda mazingira kweli?
Jibu jepesi, hapana, tutunze mazingira yetu, madini yana thamani sana lakini hata mazingira yetu yana thamani kubwa sana.
Kwa kifupi, baada ya mikataba hiyo kutomnufaisha mwananchi, Serikali haina budi kuangalia mapungufu hayo katika sheria na kuyafanyia kazi ili madini na rasilimali nyingine ziwe na usimamizi thabiti na wenye manufaa kwa kila Mtanzania.

No comments: