Thursday, 19 June 2014

Bajeti ya elimu 2014/15: Serikali imesikiliza kilio cha wananchi?

Pamoja na changamoto za viwango duni vya ubora, ufaulu hafifu, uhaba wa miundombinu, mazingira yasiyoridhisha ya kujifunza na kufundishia; sekta ya elimu imeendelea kukumbwa na matatizo ya miongozo duni inayosababisha ikose mwelekeo.
Matatizo haya ni kama vile kuanzishwa kwa utaratibu wa kuweka kivuli (OMR) kwa shule za msingi, kupanga upya viwango vya alama za ufaulu elimu ya sekondari (angalia matokeo ya kidato cha nne 2012).
Mengine ni kufutwa kwa daraja sifuri na kuanzishwa kwa daraja la tano (dalili ya kuficha aibu ya ongezeko la daraja sifuri), kurejeshwa na kubatilishwa tena kwa sharti la ufaulu kidato cha pili na kuanza kutumika kwa viwango vipya vya ufaulu vilivyokataliwa na Bunge mwaka 2013.
Kimsingi matatizo haya sehemu tu ya matukio yanayotoa picha ya mkanganyiko uliopo katika mfumo unaoongoza elimu.
Taswira inayojitokeza hapa ni kuwa serikali inatumia nguvu nyingi kuipamba sura ya elimu kwa kurekebisha matokeo na kurahisisha ufaulu huku kwa ndani imeficha udhaifu mkubwa katika ufundishaji, ujifunzaji, usimamizi wa shule, uwajibikaji na ubovu wa elimu inayotolewa.
Hakuna haja ya kulumbana, kila Mtanzania anaguswa na hali ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini. Umefika wakati Serikali ichukue hadhari na kuachana na tabia ya kupuuza ushauri unaotolewa na wadau wa elimu wanaosisitiza mambo ya msingi ya kufanyia kazi ili kuboresha elimu.
Kwa mfano, kufaulisha wanafunzi ambao hawakufundishwa kikamilifu ni kutengeneza kansa nyingine ambayo italitafuna taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Huu si uzalendo.
Tukemee tabia ya serikali kufanya amuzi wa mzaha katika elimu na kuitaka isikilize vilio vya wananchi na kuwataka watendaji kutanguliza mbele maslahi ya taifa.
Tunaitaka serikali na wabunge kuzingatia mambo muhimu yafuatayo katika bajeti ya elimu ya mwaka 2014/15.
Masilahi ya walimu
Kwa mujibu wa Takwimu za Chama cha Walimu (CWT), hadi kufikia Desemba 2013 madai ya walimu ambayo hayakulipwa yalifikia Sh 61bilioni. Ombi la CWT kwa serikali kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 50 limekataliwa na walimu wameendelea kupuuzwa.
Wakati huohuo serikali inatumia asilimia 43 tu ya fedha za mishahara ya watumishi wa umma kuwalipa walimu ambao idadi yao ni asilimia 67 ya wafanyakazi wote wa umma. Lakini serikali ilitumia asilimia 57 ya fungu la mishahara ya umma kuwalipa wafanyakazi wa sekta nyingine ambao ni asilimia 33 tu ya watumishi wote wa umma.
Serikali kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, imeahidi kuwa italipa madai haya ya walimu katika mwaka wa fedha 2014/15.
Hata hivyo, tunakumbusha kuwa haya ni madai ya muda mrefu na ahadi kama hizi zimekuwa zikitolewa mara kwa mara pasina utekelezaji.
Serikali itambue msemo usemao; “Uzuri wa mfumo wa elimu unategemea ubora wa walimu wake”. Kwa mantiki hii haina budi kuwathamini walimu kama kweli inakusudia kuboresha elimu.
Walimu wamekata tamaa na tusipokuwa makini hali hii itaambukizwa kwa watoto wetu, familia zao na hatimaye sehemu kubwa ya jamii pia itakata tamaa.
Uwekezaji katika elimu
Katika makubaliano ya mpango wa Elimu Kwa Wote (EFA - 1990), ambayo Tanzania imeridhia, iliazimiwa kuwa uwekezaji katika elimu katika kila nchi mwanachama ufikie walau asilimia 20 ya bajeti nzima au asilimia sita ya pato la nchi husika.
Hata hivyo, hali imekuwa tofauti katika nchi yetu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita uwekezaji umekuwa ukishuka badala ya kuongezeka.
Kwa mfano, mwaka 2008/09 bajeti ya sekta ilifikia asilimia 20, lakini ikashuka mpaka asilimiua 18 mwaka 2010/11. Na baadaye mwaka 2013/14 ikashuka hadi asilimia 17.3.
Tunazidi kuikumbusha serikali katika kipindi hiki wanachoelekea kupanga na kupitisha bajeti, izingatie makubaliano haya ambayo kwa hiyari ilitia saini na kuridhia kuwa itajitahidi kupanga walau asilimia 20 ya bajeti yake kuu katika sekta ya elimu.
Upungufu wa ruzuku shuleni
Tanzania iliporidhia kutekeleza mipango ya maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari, lengo lilikuwa kuziwezesha shule za umma kuwa na uwezo wa kujiendesha na kusimamia utoaji wa elimu katika kiwango kinachostahili.
Utoaji wa ruzuku (Sh 10,000 kwa wanafunzi wa msingi na 25,000 kwa sekondari) ulikuwa sehemu ya maazimio ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
Jambo la ajabu ni kuwa, taarifa za utekelezaji wa mpango na azimio hili la utoaji ruzuku zinaonyesha kuwa kiasi ambacho kimekuwa kikifika shuleni ni pungufu ya kilichopangwa.
Mathalani, katika awamu ya kwanza ya mpango wa elimu ya msingi, wastani wa Sh 6,497 tu ndizo zilizofika shuleni badala ya Sh10,000, huku wastani wa Sh 5,500 tu ndio ukifika shuleni wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili.
Hali hii inaendelea hata katika utekelezaji wa awamu ya tatu. Wastani wa kiwango kilichofika shuleni mwaka 2012/13 ni Sh 3,580 badala ya Sh 10,000.
Hali hii inazikumba pia shule za sekondari ambazo nazo zinapokea wastani wa Sh 16,384 badala ya 25, 000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Ikumbukwe tu hapa kuwa viwango hivi ni wastani tu wa hali ya utoaji ruzuku shuleni, lakini katika hali halisi ziko shule nyingi ambazo hupata chini ya wastani wa 1,500 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Bajeti ya elimu ya awali
Kwa kutambua umuhimu wa elimu ya awali katika makuzi na maendeleo ya mtoto kitaaluma na kijamii, serikali imeazimia katika mipango yake mbalimbali kufanya uwekezaji stahili katika eneo hili.
Sera ya Elimu ya 1995, mtaalaa wa elimu ya awali wa 2007, Dira ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM), Mkukuta ni miongoni mwa mipango ambayo inaakisi azimio la serikali kukuza elimu ya awali.
Pamoja na maazimio haya serikali imeshindwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano haya. Mathalani uwiano kati ya wanafunzi wa awali na darasa umebaki kuwa 1:115 badala ya 1:25, uwiano kati ya mwanafunzi kwa mwalimu pia ni 1:124 badala ya 1:25. (BEST 2013).
Tutakumbuka kuwa elimu ya awali haikugusiwa kabisa katika mpango wa ruzuku katika awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM ). Na hata ilipogusiwa katika awamu ya pili, fedha kwa ajili ya ruzuku elimu ya awali hazikutoka kabisa.
Katika awamu ya tatu, elimu ya awali imejumuishwa katika bajeti ya ruzuku kwa shule za msingi. Hata hivyo, taarifa za utekelezaji mipango zinaonyesha fedha kwa ajili ya elimu ya awali hazijumuishwi katika fedha ya ruzuku inayokwenda shuleni.
Kuimarisha ukaguzi 
Hali ya ukaguzi bado ni mbaya, uwezo wa serikali kukagua shule hauridhishi. Takribani asilimia 19.1 tu ya shule zote za msingi ndizo zinazokaguliwa kwa mwaka na asilimia 21.4 kwa shule za sekondari.
Wizara husika ijitahidi kuongeza bajeti ya ukaguzi wa shule angalau idara iweze kukagua asilimia 50 ya shule zote za msingi na sekondari kwa mwaka.
Kama bajeti ya ukaguzi itaongezwa tuna imani shule zetu zitakaguliwa. Hivyo viwango vya ubora vitafahamika, upungufu utafanyiwa kazi ili hatimaye tuweze kuwa na elimu bora.
Wakati tukiitaka serikali kuongeza bajeti ya ukaguzi, tunasisitiza pia umuhimu wa kuwa na Wakala ya Ukaguzi wa Elimu kama zilivyo sekta nyingine. Hii ndio njia pekee na sahihi ya kuboresha ufanisi katika suala la ukaguzi.
Mazungumzo ya mchakato huu yamekuwepo kwa taribani miaka mitatu sasa lakini mafanikio yake hayaonekani. Itaendelea wiki ijayo

No comments: